Riwaya: "Hujuma Nzito"

RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 34


Leo nina huzuni kuliko kawaida, mwili wangu ni dhaifu na roho yangu imekuwa nyepesi sana. Nimempoteza kijana wangu mpambanaji Nathanieli ambaye alikuwa anafanya kazi kwa ukaribu zaidi na Bosi wako Newton Temba" alifungua mazungumzo Profesa akiwa anamhadithia Kachero Manu bila kufahamu huyo anajua kila kitu na ndio mhusika wa kifo cha Nathanieli kupitia pacha wake Yasmine.


Kisha Profesa akaendelea, machungu ninayoyapata ni kama siku kijana wangu Hamza Bendelladji wa Algeria alipokamatwa". Alipofikia hapo kwenye maelezo yake ya kumtaja Hamza, Kachero Manu alipigwa na butwaa na kuachwa mdomo wazi kwa sekunde kadhaa akiwa haamini kumbe Hamza, mhalifu nguli alipikwa kiuhalifu na Profesa.


Huyu Hamza Bendelladji ni mhalifu aliyefanikiwa kuiba pesa nyingi zaidi za mabenki kwa njia ya mtandao. Alikuwa ni kijana mdogo sana (25) raia wa Algeria, ambapo miaka kadhaa iliyopita alihukumiwa kifungo cha miaka 15 gerezani kwa uhalifu wa kuiba zaidi ya Bilioni 500 (Tsh) kutoka kwenye benki 217 za Ulaya na Marekani. Mashirika yote ya habari duniani kuanzia televisheni mpaka redio yaliripoti taarifa zake kijana huyo.


Kachero Manu akaanza kuomba kimoyomoyo Mwenyezi Mungu aweke baraka zake wamtie mbaroni Profesa ili dunia nzima iweze kujua kuwa Tanzania ina mashushushu bobezi kama wale waliopo katika mashirika makubwa kama CIA, FBI, MOSSAD, KGB na mengineyo yenye heshima ya kutukuka duniani.


"Hongera sana Profesa na sisi tunatakiwa tujue mbinu ulizompika nazo Hamza tukazitumie Tanzania" alijitia kupongeza kinafiki Kachero Manu huku akimtia shemere azidi kufunguka.


"Ha.. ha... ha...! Ahsante umenifurahisha sana kwa sifa unazonipa, mimi Tanzania kwa uwezo wangu wa kiakili wakati nafundisha Chuo Kikuu ilitakiwa niwe na eskoti ya ving'ora kunipeleka Chuoni na kunirudisha nyumbani, lakini hata heshima tulikuwa hatupewi.

Afadhali kidogo sasa hivi wasomi wenzangu wanakumbukwa na wanasiasa wanapewa vyeo vya kuteuliwa" alicheka kwa majigambo na majivuno bila kujua kuwa Kachero Manu ni popo, yupo nao kimagazigazi tu kuwapekenyua taarifa zao nyeti.


"Yule Hamza alikuwa na akili za kuzaliwa, kwanza alikuwa anaitambuka mashine husika ya ATM, kisha kwa kutumia "boot CD" ama "boot flash" anaathiri mfumo mzima wa mashine, hii ni diski maalumu yenye uwezo wa kutunza mafaili makubwa sana kwa kufanya mashine isinzie kwa muda. Baada ya hapo kirusi kiitwacho 'Tyupkin' kinaingizwa kwenye mfumo huo wa ATM, kazi ya kirusi hiki ni kukata mawasiliano ya kimtandao kati ya mashine ya ATM na seva za benki.


Baada ya hapo mfumo wa mashine unaanza kufuata masharti ambayo mtumiaji anaamuru na si maelekezo ya benki tena. Mpaka Hapo sasa unaweza kuingiza namba za siri ambazo zimetegeshwa tangu awali na kukupa uwezo wa kupakua kiasi chochote cha pesa kilichopo katika mashine. Njia hii huiba pesa zilizopo kwenye ATM mashine bila kuathiri akaunti za benki za mtu mmoja mmoja.

Na pia ni njia inayoitaji ujuzi wa juu sana wa Kompyuta. Njia nyingine aliyokuwa anaitumia kuwaliza wazungu wa Ulaya ni kuvamia ulinzi wa Kompyuta za benki za wale wa madirisha ya wateja na maofisa wao, kisha akawa anarusha kirusi cha 'Spying software'.


Kirusi hiki kinaunganisha taarifa zote za maafisa wa benki na wewe mvamizi ikiwemo namba za siri kadhaa, hivyo kumpa uwezo wa kuendesha mifumo ya benki kama afisa wa benki husika. Baada ya hapo sasa mvamizi anaweza kuhamisha pesa kutoka kwenye akaunti za watu wengine na kuweka kwenye akaunti yake binafsi. Na hii njia ya pili ndio tumeitumia sana kwa hizi pesa zilizopo hapa nchini Afrika ya Kusini". Alizidi kufunguka Profesa akiwa sasa ameanza kupata uchangamfu tofauti na mwanzoni walivyoanza maongezi yao.

Baada ya maongezi hayo Kachero Manu akakabidhiwa rasmi nywira za siri za kuwasiliana nae pindi atakapokwama akiwa kazini. Huku akiahidi kuwa watakutana Tanzania siku chache zijazo mara pesa zitakapokuwa zimefika. Pia usiku aliahidiwa kuwa atasaini mkataba rasmi wa kuhakikisha Dola ya Nyasa inasimamishwa na akifanikisha malengo yake aliyopewa atapewa nyadhifa gani kwenye hiyo serikali mpya.

Pia alipewa jukumu la kutafuta wataalamu wa kufoji nyaraka 'Cobbler' watakaowatumia sana wakati wa kuhamisha pesa taslimu kuirudisha Benki kwenye akaunti za VICOBA na SACCOS. Wakaagana Kachero Manu akarudi chumbani kwake kupumzika.
Wakati amejipumzisha chumbani kwake, akaamua kuingia kwenye barua pepe yake akakutana na taarifa za kupendeza kutoka kwa rafiki yake Dr.Edson Nkube.


Vipimo vya DNA vya mama mzazi wa mwendawazimu, marehemu Van-Dubbe vilishatolewa huku vikithibitisha pasina kuacha mashaka kuwa Van-Dubbe ndio aliyezikwa Tanzania na ndio mtoto wake. Hivyo akataarifiwa kuwa tayari leo mchana Mama yake Van-Dubbe anasafirishwa kwa ndege kuelekea nchini Tanzania tayari kwa ajili ya kutoa ushahidi mahakamani pindi mambo yakikamilika.


Akafurahishwa na kazi nzuri na ya kutukuka iliyofanywa na Dr.Edson Nkube, Afisa Usalama wao wa siri ambaye hata ndani ya usalama wenyewe wengi wao hawamjui "Deep Cover". Hasa akikumbukia namna alivyomuokoa kwenye hatari alipotegewa mtego kwenye nyumba ya kulala wageni siku ya kwanza kukanyaga nchini Afrika ya Kusini.

Kachero Manu baada ya kuperuzi jumbe mbalimbali alizotumia, akaanza kupanga namna ya kuwatumia kwenye sakata hili raia wa Tanzania wanaoishi Jijini Johanesburg na kulipwa na kitengo cha Usalama Tanzania, hasa kuchunguza nyendo za namna hizo pesa zitakavyosafirishwa kwa njia ya barabara.


Taarifa alizopata ni kuwa Jijini Johanesburg pekee kulikuwa na Maafisa Usalama Waliolala "Sleeper Agents" zaidi ya 20, wanaolipwa mshahara na serikali. Ambao wengi wao kati ya hao 20 walikuwa wanakula shushu hawajawahi kupewa kazi yoyote toka waajiriwe.

Hawa mashushushu walikuwa wanajichanganya mitaani hawajulikani na watu shughuli zao halisi. Wengine walikuwa wanafanyakazi saluni za kiume za kunyoa nywele, wengine wakiuza matunda mitaani, na shughuli kedekede zilizokuwa zinatumika kuwapoteza maboya watu wasiwajue kazi zao.


Walikuwa wamewekwa kama akiba ya kutumika siku wakihitajika. Na sasa wakati ulifika wa kutumika ambapo jukumu lao litakuwa ni kuchukua ushahidi wa kutosha uwe na video au picha wakati pesa zinatolewa mlundi kwa mlundi na kupakizwa kwenye magari.


Mawasiliano yake yote wakati yupo kwenye jumba hilo la Profesa gwiji wa Kompyuta alikuwa anayafanya kwa kutumia simu yake yenye programu maalumu ya kuzuia udukuzi. Hakutaka kabisa kugusa Kompyuta za ndani ya jumba lile, akiogopea 'Carnivore Computer', ambazo ni kompyuta maalumu zinategeshwa kwa ajili ya kufukua taarifa za mtumiaji.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji125][emoji125][emoji125]

Majonzi na huzuni vilitawala msibani, nyumbani kwa Nathanieli. Ndugu, jamaa wa karibu na majirani walikuwa wamefurika kwenye kilinge cha nyumba hiyo. Askari polisi tayari walishaiondosha maiti ya Nathanieli. Wafanyakazi wenzake wa Benki Kuu nao hawakujivunga, walikuwa mstari wa mbele pale msibani kuhakikisha mambo yanaenda sawia bila kuharibika. Kila mtu alikuwa anasema lake pale msibani.

Penyenye za nguvu zilizoenea ni kuwa amevamiwa na majambazi usiku wa manane akauliwa. Wengine wakavumisha ni kifo kinachotokana na kisasi cha ugoni. Wakanyetisha kuwa alikutwa chumbani na mke wa mtu ndio mwenye mke akajichukulia sheria mkononi. Wakatilia nguvu nadharia yao kwa kuwa marehemu kakutwa yupo na chupi tu mwilini mwake, huku boksi kadhaa za kondomu zikifumwa chumbani mwake.


Hizi habari za uzushi zilikuwa zinaenezwa kwa kasi pale msibani na mitaani na vidinga popo na wale habari kuuzwa. Bila wenyewe kufahamu kuwa hizo habari zote ni propaganda zilizopikwa na kusambazwa na watu wa kitengo, mashushushu ili mradi kuwapoteza maboya mahasimu wao na pia ndugu, jamii na marafiki ili wasije kuharibu ushahidi wakati muda umekwenda matiti.

Maneno hayo ya ndarire yalizaa matunda chanya yaliyokusudiwa hasa ile dhana ya pili ya kushikwa na ugoni ndio ilishika kasi na kuaminiwa na wengi pale msibani. Huku dhana hiyo ikichagizwa na maisha binafsi ya Nathanieli ya kuishi bila mke wala kuwa na mtoto hata wa kusaga mkungu.


Vikundi mbalimbali vya kwaya vilikuwa vinatumbuiza nyimbo za maombolezo pale msibani. Kachero Yasmine nae alikuwa yupo pale msibani sako kwa bako na shoga yake kipenzi wa kazini Flora Tarimo. Alikuwa anawachora tu, huku akikumbukia vuta n'kuvute, patashika nguo kuchanika ya usiku wake alipokuwa anapambana na marehemu Nathanieli.
ITAENDELEA

Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 35


Vikundi mbalimbali vya kwaya vilikuwa vinatumbuiza nyimbo za maombolezo pale msibani. Kachero Yasmine nae alikuwa yupo pale msibani sako kwa bako na shoga yake kipenzi wa kazini Flora Tarimo. Alikuwa anawachora tu, huku akikumbukia vuta n'kuvute, patashika nguo kuchanika ya usiku wake alipokuwa anapambana na marehemu Nathanieli.


Shoga yake Flora alikuwa hajiwezi kwa kilio cha Bosi wake, huku Yasmine akifanya kazi kubwa kumliwaza. Ushoga wao ulikuwa wa kinafiki hasa kwa upande wa Yasmine. Kuna kitu Yasmine alikuwa akikitafuta kwa Flora bila yeye mwenyewe kufahamu.


"Shosti Shemeji yangu anasafiri kwenda Afrika ya Kusini leo, hivyo nataka nichomoke nimuwahishe Uwanja wa Ndege halafu nitarudi..!" Flora alimnong'oneza rafiki yake Yasmine sikioni. "Twende wote na mie sibaki hapa nitakuja baadae maana hata ratiba bado, wanasubiriwa ndugu wa marehemu toka Mkoani Ruvuma waje ndio kila kitu kitaeleweka". Kachero Yasmine alisema huku akijionyesha kubwa ni mtu aliyekabwa na huzuni kuu.


Flora kwa shingo upande akakubaliana na ombi la Yasmine kuwa waende wote, wakanyanyuka kwa pamoja huku wakiwaomba udhuru Wafanyakazi wenzao wa Benki Kuu na kwenda kwenye maegesho ya magari kisha kila mtu akaondoka ene lile na gari lake, Flora mbele, Yasmine nyuma yake linafuata.


Flora alikuwa anaishi Mbezi Tangibovu kwenye nyumba yake ya roshani mbili, jirani kabisa na shule ya msingi Mwalimu Nyerere. Kwa mtazamo tu wa jumba la Flora kwa nje lilikuwa linakuonyesha ukwasi wa mmiliki wake. Lilikuwa limetiwa nakshi za gharama zenye asili ya Asia na Mashariki ya Kati. Yasmine akilini mwake alikataa katakata kuwa hili kajenga kwa ngwenje zake mwenyewe Flora.

"Hapa kuna mkono wa danga, umenyooshwa kusimamisha huu mjengo" aliwaza Yasmine wakati anakaribishwa ndani ya nyumba hiyo wakiwa tayari wameyaacha magari yao kwenye eneo la maegesho. Alithubutu kuwaza hivyo kwa sababu alikuwa anajua dhahiri shahiri kiasi cha mshahara anaoupata sahibu wake Flora.

"Karibu sana Shosti jisikie upo nyumbani, nimefurahi sana ujio wako, maana kila siku kukutaniana kwenye Mahoteli marafiki kama sisi haipendezi. Nimekufahamu muda mfupi tu lakini nakuchukulia ni kama ndugu kwangu sio rafiki tena.." alizidi kujibaraguza Flora bila kufahamu anamkaribisha shushushu 'Birdwatcher' hatari sana.

Mtu aliyekuja hapo kwa malengo maalumu ya kuhakikisha uwepo wa marehemu Dr.Pius Chilembwa ndani ya nyumba hiyo. Hasa akikariri maneno ya marehemu Nathanieli aliyowahi kumpasha Yasmine kuwa Flora alikuwa ana mahusiano ya kimapenzi na Dr.Pius.

"Ahsante sana Shosti, nimejaa kama pishi la mchele, huu ni mwanzo tu, nitakuja mpaka utanichoka" akajibu Yasmine mpaka wote wakaangua kicheko huku wanagongesha viganja vya mkono na kuingia ndani ya nyumba. "Tena mjengo kama huu unanitia hasira na wivu wa maendeleo, uliwezaje kujenga jengo la watu tabaka a'ali kama hili? Nimegee siri kidogo" alianza kumfukunyua undani huku usoni mwake ameunda tabasamu la uongo na kweli.


"Mhh...nilipunguza anasa zote, nikilipwa masurufu ya safari zote zinakuja saiti, marupurupu yangu yote nilikuwa nayaleta huku bila kusahau kibubu cha nyumbani nilikuwa naweka fedha akiba nikivunja mwisho wa mwaka sikosi milioni 10 mpaka 15" alijifaragua Flora majibu yenye ushobo ndani yake, majibu ambayo uso wake ulikuwa unaonyesha fika kuwa anaongopa mchana kweupe.

"Daah...hongera sana, Shosti hivi ndio tunataka, Wanawake tufanye mambo ya maendeleo tumiliki uchumi, kuondoa dhana ya kwamba hatuwezi mpaka tuwezeshwe na Madanga" alimpaka mafuta kwa mgongo wa chupa wakati mawazoni mwake alikuwa anamng'ong'a kuwa thubutu yako, kibubu kwio gani hicho cha ajabu kwa mtumishi wa umma cha kuweza kuweka akiba mpaka milioni 10-15, wakati wananuka madeni mpaka ya sembe huko mitaani kwenye vigenge.


Wakapiga soga mbili tatu kisha wakaelekea mesini kutia riziki kinywani maana walikuwa bado hawajaiona asubuhi yao kutokana na hekaheka na taharuki za msiba huo wa ghafla. "Sasa Shosti huyo Shemeji yako, mbona unamficha, muweke hadharani huenda na mie nikampenda nikaopoa mchumba, tukaolewa wote kwa mkubwa na mdogo!" Kachero Yasmine alichomekea akiwa na hamu ya kumuona huyo anayesemwa ni shemeji ili ahakikishe kama sio kweli Dr.Pius.

"Mmhhh...Shosti nawe una vibweka, haya twende ukamuone maana tayari yupo kwenye gari akinisubiri mimi tu nipate staftahi nimkimbize Uwanja wa ndege" aliongea huku akiwa na wasiwasi mkubwa usoni mwake akijitahidi kuuficha kwa tabasamu. Wakaanza kushuka toka roshani ya pili wanaelekea maegesho ya magari huku tayari Yasmine akivaa miwani yake maalumu aina ya "Kestrel 1080p HD Camera Eye Glasses".

"Shosti mbona miwani tena una matatizo ya macho?" aliongea Flora akimshangaa rafiki yake kuvaa miwani ghafla maana hajawahi kumshuhudia amevaa miwani tokea wamefahamiana.
"Aaaah....macho yangu kwa sasa hayapatani kabisa na jua pia nipo kamili kumtega Shemeji yako anione ni mrembo!" alitoa jibu la uongo na kuchomekea utani ndani yake ili kumzubaisha, wote wakafa kicheko huku wamekamatana viganja vyao wanaelekea kwenye maegesho ya magari.

"Shem...kutana na rafiki yangu tupo nae ofisi moja anatokea Zanzibar anaitwa Yasmine, amenisumbua sana anataka walau akuone tu....! " Flora alifanya utambulisho mfupi huku Yasmine akichezea mkono wa upande wa kushoto wa hiyo miwani akijifanya kuiweka sawa, kumbe anafanya vitu vyake bila wao kung'amua.

"Ahaaa...vizuri nashukuru kukufahamu nadhani tutazidi kufahamiana zaidi nikirudi safari yangu maana sasa nina haraka, poleni sana na msiba uliokufikeni" aliongea yule jamaa aliyejifanya Shemeji wa Flora baada ya kusalimiana huku machozi yakimlenga mpaka akashindwa kabisa kuyazuia machozi yake, yakaanza kumdondoka. Akatoa hanchifu yake kutoka kwenye mfuko wa suruali yake na kuanza kujifuta.

"Tumepoa, nashukuru pia kukufahamu, mbona unalia sasa kumbe unamjua Bosi Nathanieli...?" Yasmine akashukuru na kuchomekea swali baada ya kuona hali sio ya kawaida katika uso wa Shemeji.

"Aah..Aah...OK.. OK....I'm fine usiwe na wasiwasi simjui ila kanisimulia Shem Flora jinsi alivyokuwa mwema kazini kwenu, nimejikuta nimeshindwa kujizuia kabisa, ama kweli wema hawadumu" alijing'ata, huku anajikany'aga katika kujieleza akijua fika tayari ameshaharibu kwa kuruhusu machozi yale. Lilikuwa ni swali lililomtia kitumbo uchungu, hakulipenda kabisa. Jambo lilizidi kumtia mashaka Kachero Yasmine kuwa huyu mtu anaficha uhalisia wake.

Baada ya hapo Yasmine wakaagana na Flora huku Flora nae akipakia kwenye gari la anayejidanganyia ni shemeji yake, akimpa ahadi rafiki yake kuwa hatochelewa kurudi nyumbani ili mradi waweze kurudi tena msibani. "Usichelewe basi mie nakungojea twende wote" alijifaragua Yasmine kujifanya ana haraka sana wakati kiuhalisia alikuwa anatamani achelewe ili aweze kuyasoma mazingira yote ya pale nyumbani.

"Sichelewi kuwa na subira, si unajua waswahili tusipoonekana tunaweza zushiwa tukio tumekula njama Bosi afe ili tupate Cheo chake ndio maana hatuonekani msibani, hatuna uchungu" alitilia msisitizo Flora mazungumzo yao wakati tayari ameshaanza kulitoa gari eneo lile. Shemeji mtu akiwa amekaa kiti cha mbele cha abiria akawa anampungia mkono Yasmine kisha akamkonyeza. Yasmine nae akapunga mkono kurudisha maagano hayo huku anatabasamu. Hivyo Yasmine akaachwa, solemba peke yake pale nyumbani.

Mungu ampe nini Yasmine!, upele ajikune? Kwake kuachiwa jumba analohisiwa kuishi adui yake ilikuwa ni kama mbuzi kufia mlangoni kwa muuza supu usiku wa manane au ngedere aliyesusiwa shamba la mahindi ajipocholee atakavyo. Kabla hajaingia ndani akaingia kwenye gari yake na kuitoa kompyuta yake ya kazi pamoja na mkoba wake maalumu wa vifaa vya kazi, wenye dhana zote anazohitaji, akaingia navyo ndani ya nyumba.
ITAENDELEA
Marehemu feki DR.PIUS kaonana uso kwa uso na KACHERO YASMINE

Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 36




Mungu ampe nini Yasmine!, upele ajikune? Kwake kuachiwa jumba analohisiwa kuishi adui yake ilikuwa ni kama mbuzi kufia mlangoni kwa muuza supu usiku wa manane au ngedere aliyesusiwa shamba la mahindi ajipocholee atakavyo. Kabla hajaingia ndani akaingia kwenye gari yake na kuitoa kompyuta yake ya kazi pamoja na mkoba wake maalumu wa vifaa vya kazi, wenye dhana zote anazohitaji, akaingia navyo ndani ya nyumba.



Ile miwani yake aina ya 'Kestrel' haikuwa ni miwani ya kawaida kama udhaniavyo zile miwani za jua halisi. Ilikuwa ni miwani maalumu ya kijasusi yenye uwezo wa kurekodi video mpaka masaa 8 ikiwa na uwezo wa kuhifadhi wa '64GB'. Wakati anaongea na yule anayejifanya Shemeji wa Flora alisugua upande wa kushoto wa mshikio wa miwani, lengo ilikuwa ni kuiweka tayari kumrekodi mshukiwa wake.


Alipoingia sebuleni na kutulizana, akaichomoa chipu ya kuhifadhi video toka kwenye miwani na kuichomeka kwenye kompyuta yake na kuanza kuangalia video hiyo huku akiisimamisha mara kwa mara wakati ametingwa na zoezi la uchoraji picha hiyo kwa kutumia kalamu ya risasi na karatasi nyeupe.


Baada ya nusu saa alikuwa tayari ameshamchora yule Shemeji wa Flora. Akaifungua toka kwenye Kompyuta yake picha halisi ya Dr.Pius Chilembwa aliyoidukua kazini kule Benki Kuu na kuilinganisha na picha ya yule Shemeji wa Flora. Akaanza kulinganisha picha hizo kwa kuondoa zile ndevu, sharubu na masharafa ya kwenye picha aliyoichora toka kwenye video. Kadri alivyokuwa anapunguza vitu kwenye ile picha ya kuchora ndivyo alivyokuwa anaanza kufurahi mpaka tahamaki zikawa picha mbili za watu wanaorandana.


Shabaashi..! Nimekushika Dr.Pius Chilembwa, hatimaye mbio zako za sakafuni zimekaribia kuishia ukingoni. Kitanzi kinakuita kwa uhaini uliouandaa. Ni aibu kubwa mtu kama wewe uliyetopea na kutabahari katika elimu, kushiriki ujinga kama huu. Kumbe machozi yako kwa kifo cha Nathanieli ni machozi halisi ya kufiwa na kijana wako wa kazi!.


Sasa napata picha nzima kuwa unasafiri kwenda nchini Afrika ya Kusini kama nilivyosoma dondoo za moja ya mikutano yenu nyumbani kwa Nathanieli. Huko unakokwenda unaenda kukutana na pacha wangu hatari sana katika kazi, Kachero Manu nina imani utarudishwa maiti au atafanya kitu ambacho kitazidi kukuacha uchi zaidi ewe Marehemu mtarajiwa uliyejichuria kifo kabla ya siku zako..!" Yasmine alikuwa anaongea na Dr.Pius Chilembwa pale kwenye picha huku anamsoza na kidole cha shahada utasema anamsemesha mtu halisi mbele yake kumbe picha tu.


Kazi aliyobakiza kwenye nyumba ile ikawa ni kupandikiza vifaa mbalimbali vya kunasa mazungumzo na video, kitaalamu walikuwa wanaita Black Bag Operation (BBO). Kwa kutumia vifaa hivyo vya maalumu akafanikiwa kufungua mlango wa chumbani kwa Flora. Akafunga vifaa vyake chini ya kitanda na vingine bafuni. Alipokuwa bafuni ndipo alipogundua kuna njia nyingine ya kutokea bafuni kushuka chini ya jengo. Kati ya makutano ya kuta mbili kushotoni kwa choo cha kukaa aligundua kuna uwazi uliofungwa kitaalamu sana, sio rahisi kwa mtu wa kawaida kugundua. Kwa utundu wake wa kishushushu akafanikiwa kufungua uwazi huo na kushuka chini kwa chini mpaka alipokutana na chumba kingine.


Alipofanikiwa kukifungua akakuta ni chumba ambacho ni kama kipande cha chumba cha Hoteli, chenye hadhi ya nyota tano kikiwa na kila kitu kwa mahitaji ya mwanadamu. Hakutaka kukaa sana huko zaidi ya kupandikiza vitu vyake anavyotaka kisha akafunga chumba hicho na kurudi juu. Akafanikiwa kukamilisha zoezi hilo kwa umakini mkubwa.


Punde si punde sahibu wake Flora akarejea toka Uwanja wa ndege alipomsindikiza marehemu Dr.Pius Chilembwa. Wakakaa sebuleni wakaendelea mazungumzo yao mengine, kisha wakakata shauri kurejea msibani huku moyoni Kachero Yasmine ana furaha sheshe ya kukamilisha bila purukushani lile alilolikusudia kulifanya nyumbani kwa Flora.
[emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586][emoji3586]

SURA YA KUMI NA TANO

Majira ya adhuhuri wakati Kachero Manu anajiandaa kwenda mesini kupata maakuli kabla hajatoka chumbani kwake akachungulia nje ya dirisha la chumba chake. Moyo wake ghafla ikampiga paaah..! akiwa haamini ambacho macho yake yanacho mshuhudisha.

Alistaajabishwa na kuona ulinzi maradufu ukiimarishwa katika jumba lile huku walinzi hao wakiwa na silaha nzito za kijeshi.
Pia kulikuwa na helikopta ndogo si chini ya tatu zikiwa nazo zimekaa mkao wa kupaa wakati wowote. Kwa ujumla kuuvuka ulinzi ule bila ruksa yao ilihitajika nguvu za Mungu tu na si vinginevyo.

Ghafla bin vuu akiwa bado yupo pale pale dirishani hajachomoka, akaanza kusikia sauti ya ving'ora kuashiria punde tu msafara mzito unaingia eneo lile nyumbani kwa Professor Potchefstroom, au ukipenda muite Profesa 'Asante-Rabbi' mwenye Mji wake.


Akashikwa na wahaka na tashiwishi ya kushuhudia mchezo mzima unaoendelea pale nyumbani kwa Profesa mubashara kupitia dirishani. Yalikuwa magari yasiyopungua 10 ya kifahari yenye rangi nyeusi yanayofanana kila moja kimuonekano, yanaingia eneo lile. Yaliposimama tu wakashuka mabausa zaidi ya 50 kwenye magari yale yote, wakiwa wamevalia sare mithili za kijeshi. Mabaunsa hao hawakukaa sambejambe, bali walijipanga kiutaratibu maalumu kuonyesha wamefunzwa wakafunzika.

Kisha kwenye gari ya katikati akashuka mtu mmoja ana mwili mdogodogo mrefu wa wastani amefuga ndevu za kutosha na masharubu hali iliyomfanya aonekane umri wake umekimbia. Alikuwa amevaa pensi ya kaki na sendo nyeupe miguuni huku juu akivalia sweta la kumuwezesha kuhimili baridi ya nchini Afrika ya Kusini.

"Hatimaye hayati Dr Pius Chilembwa amefufuka toka kaburini kwake na kutua nchini, karibu sana kama kweli wewe ni mvuvi wa pweza tukutane mwambani" alijikuta anaropoka Kachero Manu bila kutarajia baada ya kumuona Dr Chilembwa anasaidiwa mizigo na mmoja wa watumishi wa nyumbani pale ili aingie ndani.

Kachero Manu akatoka zake nje ya chumba, akakifunga na kuelekea mesini kwa ajili ya chakula. Huko mesini alikutana na baadhi ya mabaunsa aliowaona chini ya jengo, wameingia kula kwa zamu zamu huku wenzao wakikaa ange kama washika doria. Hakuwajali, akaketi kitini na kuanza kufakamia maakuli ipasavyo mchana huo ili kuupa mwili virutubisho vyote muhimu.

Alipomaliza kula akawa anarejea chumbani kwake kusubiria wito wa kikao tena cha baadae. Alikuwa anapenda safari yake ya kurejea Tanzania iwe ya haraka alishachoka kukaa kitawa kwenye jumba lile. Alitamani waungane tena na pacha wake Yasmine kwanza ampongeze kwa kazi nzuri aliyoifanya, pili walianzishe varangati la pamoja la kuwatia mbaroni wahalifu. Maana siku zote Yasmine alikuwa anaishi katika kivuli cha Kachero Manu, hata afanye uhodari gani sifa zilikuwa zinammiminikia kwake Kachero Manu.


Alipokanyaga tu korido ya kuelekea chumbani kwake, chumba cha pili kushoto kwake akamuona Dr Pius Chilembwa anatokeza kwenye hiko chumba huku anaongea na mtu kwenye simu. "Hellow...yeah! sasa naenda kupata mlo wa mchana baada ya hapo nitaenda chumba cha kujisomea kuweka mambo sawa kisha baadae ndio nitakuwa na mkutano na Professor Potchefstroom..!" alikuwa anaongea na simu huku amerudishia tu mlango wake hajaufunga vilivyo. Akapishana na Kachero Manu kwenye korido wakasalimiana kwa kupeana ishara ya kupungiana mikono tu.


Kachero Manu alishashtukia mchezo mzima kuwa Dr Chilembwa kasahau kubana mlango na anatokomea zake kwenda mesini. Akawa anamsindikiza kwa macho mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yake. Jasiri haachi asili yake hata akiwa ugenini, Kachero Manu alijikuta ameshageuka na tayari na yupo mlangoni mwa chumba cha Dr Pius Chilembwa. Salama yake ni kuwa korido zote hazikufungwa kamera za usalama kutokana na Profesa kuamini sana ulinzi wa nje ya nyumba yake.


Kachero Manu alikadiria kuwa kasi ya kula kwa mtu mzito kama Dr. Pius Chilembwa haitokuwa si chini nusu, hivyo muda huo unamtosha sana kufanya vitu vyake. Akafungua mlango na kutoma ndani ya chumba hicho. Kilikuwa ni chumba kikubwa chenye kitanda, kabati kubwa la kuhifadhia nguo na mizigo. Pia kulikuwa na seti la runinga pamoja na birika la kuchemshia maji ya moto kwa ajili ya chai. Pia kulikuwa na choo cha ndani kwa ndani cha kisasa. Akaurudishia mlango kwa kuubana vizuri, haraka haraka akakimbilia kwenye mizigo ya Dr.Chilembwa kwa ajili ya kufanya speksheni.
ITAENDELEA


Sent from my TECNO CC6 using JamiiForums mobile app
 
Daaah kazi nzuri Sana.

Ila kachero Manu sidhani Kama atatoka salama Kama oacha wake jasmine
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…