RIWAYA-HUJUMA NZITO-PART 4
Kachero Yasmine alikuwa tayari ameshatinga Hotelini yupo upande wa maeneo ya chooni anafanya usafi. Lakini akili yake yote ilikuwa inawaza na kuwazua namna gani atafanikiwa kuingia ukumbi wa mkutano, ambao kwa bahati ulikuwa kama meta 25 kutoka eneo la vyoo analofanyia usafi. Kingine kilichokuwa kinampa mawazo ni kujua je Kachero Manu kafanikiwa kuingia ukumbini? Ni moja ya maswali yaliyokuwa yanamsumbua sana kichwani mwake.
Ghafla bin vuu wakati bado anapiga deki kwenye korido nje kidogo ya vyoo akamuona Kachero Manu anakokotwa kidari wazi huku damu zinamvuja mwilini wakiwa wanatokea chini ya jengo wakimpandisha roshani ya juu. Alikuwa anasindikizwa na walinzi wa kike watatu huku mmoja wao akionekana kama ndio kiongozi wao akiwa yupo nyuma amefuatana na Chew Master wanabonga simulizi mbili tatu. Akawaangalia kwa makini mpaka wanatokomea ndani ya jengo lile.
Kachero Yasmine alishikwa na uchungu usiomithilika hasa baada ya kumuona Bosi wake yupo kwenye dhahama na nakama isiyoelezeka. Sasa alijua jukumu lote la kubutua kombolela lipo mikono mwake. Akiwa bado amepigwa na tahayuri anawaza jambo la kufanya ili apindue upande wa pili wa shilingi.
Akiwa kwenye hali hiyo akamuona yule mkuu wao wale walinzi wa kike kutoka nchini Ethiopia, 'Black Guards" akiwa anakuja kwa kasi upande wa chooni alipo Kachero Yasmine na sare zake za watumishi wa usafi wa Hoteli ile ya "The Pride of Indian Ocean". Tayari akili ya kuzaliwa ya Kachero Yasmine ikafanya kazi haraka sana, akajua kitu cha kumfanyia yule Afisa Mkuu, pindi akiingia kwenye anga zake.
Yule Afisa akampita na kumsalimu kwa tabasamu jepesi huku akimpungia mkono halafu akaharakisha kufungua mlango wa kuelekea chooni, akionyesha fika amebanwa na haja. Alimpa sekunde zisizozidi 35 akamfuata upande wa chooni kwa mwendo wa kunyata usiotengeneza michakato ya sauti za nyayo.
Kwanza akaufunga mlango mkuu wa kuingilia vyoo vile maalumu kwa watu VIP huku nje ya mlango akaweka kibao cha kuonyesha kuwa havitumiki kwa sasa kutokana na usafi unaoendelea. Alipotupa jicho lake kule ndani ya choo akaona kuna choo kimoja mlango wake umefungwa kuonyesha kuna mtu anakitumia. Akakipita choo hicho na kujibanza nyuma ya mlango wa choo kinachofuata.
Punde si punde akasikia sauti ya maji yanatoka kwenye flashi ya chooni kuashiria kuwa ameshamaliza kushughulika kule chooni hivyo anajiandaa kutoka. Alipofungua tu mlango, yule Mkuu akachomoa simu yake mfukoni na kuanza kuiperuzi bila kuangalia usalama wake. Akawa amempa mgongo Kachero Yasmine.
Likawa kosa kubwa kwake, Kachero Yasmine akamfuata taratibu na kisha akarusha karate ya shingo ili ammalize pale pale bila kupata muda wa kuomba maji wala kutoa sala ya toba. Kumbe yule dada hakuwa Afisa machejo, kazi yake alikuwa anaziweza haswa.
Kwa kutumia hisia tu akainamisha shingo yake chini bila kuangalia nyuma jambo ambalo lilimsabisha Kachero Yasmine ayumbe kidogo kutokana na nguvu alizokusanya za kurusha karate ile.
Yule Afisa hakumchelewesha Kachero Yasmine, akageuka kama umeme na kumtwanga konde la juu ya jicho la kushoto na kumsababisha Yasmine alambe sakafu bila kupenda.
Alikuwa ni komandoo wa kundi la Oromo Empire Supporters (OES), kundi ambalo walikuwa na malengo pacha yanayofanana na Nyasa Empire Supporters (NES) ya kujitenga kutoka nchi ya Ethiopia. Walikuwa wanataka kuunda nchi mpya ya kabila la Oromo wanaoishi kaskazini mwa nchi ya Ethiopia.
Kachero Yasmine akajizoazoa sakafuni, aliposimama na kugusa jicho lake akalikuta linachuruzika damu. Yule Afisa Mkuu hakuwa na papara akawa anamsubiria Kachero Yasmine aamke, wafirigisane kiukweli.
Kitendo cha kuona damu yake mzalendo wa nchi inamwagika tena imemwagwa na watu mamluki hasira zake zikachemka. Alimfuata kwa kasi na kuanza kumrushia mateke na mangumi mfululizo katika mitindo mipya kabisa ya sanaa za mapigano ambayo yule komandoo toka Oromo alikuwa hajawahi kuishuhudia.
Baada ya dakika kama 3 tu yule Afisa Mkuu alikuwa amechakazwa vibaya sana hatamaniki, amekula dafrao sakafuni.
Haraka haraka akamvua nguo zake na kumsachi mifukoni akamkuta ana ufunguo wa pingu pamoja na bastola moja ya kisasa. Akamburuta mpaka chooni kisha hima hima akazivaa yeye nguo zake kisha akamfungia mule chooni. Akaenda kwenye sanduku la huduma la kwanza lililomo chooni mule mule, na kutoa dhana za kitabibu anazohitaji. Akasogelea kwenye kioo na kuanza kujishona jeraha la juu ya jicho lake la kushoto. Baada ya muda mfupi tu akawa ameshamaliza kujishona, akafunika jeraha lake kwa kutumia plasta ndogo.
Akajiangalia kwenye kioo na kutabasamu baada ya kujiona amefanana vilivyo na yule Afisa Mkuu, hasa kutokana na rangi yake ya Kipemba alionekana mithili ya wadada toka nchini Ethiopia. Akafungua mlango wa kutokea kwenye korido akaishushia kofia yake upande wa kushoto kidogo kuficha plasta iliyofunika jeraha lake.
"General General....you are needed urgently General..!" mmoja wa walinzi alikuwa anakuja kwa kasi uelekeo wa chooni kumuita Afisa Mkuu akidhania Kachero Yasmine ndio Afisa wao Mkuu.
Yasmine hakujibu kitu zaidi ya kuitikia kwa kichwa kuonyesha amekubaliana na maelezo aliyopewa. Akachomoa simu yake toka mfukoni na akaanza kupiga simu mbili tatu za haraka kisha akakata simu na kuiweka mfukoni mwake na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba cha mkutano kuitikia wito.
Kabla hajafungua mlango, akasita kuingia kama vile kuna kitu amekumbuka. Akamuita mmoja wa wafanya usafi wa kiume aliyekuwa ana hanjahanja na kumnong'oneza kitu. Walipokelewa na maagizo aliyompa, akachomoka mbio mbio kama mwehu, mpaka Kachero Yasmine akaachia tabasamu pana. Akakamata kitasa na kuingia ukumbini, tayari kwa mapambano.
Alipoingia na kutupa macho yake pembeni, akamuona Kachero Manu kwa mbali kawekwa pembezoni mwa meza kuu. Machozi ya hasira yakiwa yanamtiririka Kachero Manu akitamani muujiza utokee awashughulikie wabaya wake. Kachero Yasmine bila kusema chochote moja kwa moja akaenda mpaka alipo Kachero Manu na kuanza kumfungua pingu zake, halafu akaziegesha huku akimnong'oneza kuwa yeye ndio Kachero Yasmine. Aliwazuga kama anahakikisha amefungwa zile pingu kisawasawa.
Wana kikao walikuwa wanaendelea na mkutano wao huku wakimsubiria Profesa aingie wamuadabishe Kachero Manu. Kachero Yasmine akaona moja ya siti ipo tupu, akaenda kukaa kwenye kiti nyuma ya Chew-Master huku akijinuiza nafsini mwake kuwa wa kwanza kumtia adabu atakuwa huyu Chew-Master. ambaye ndio mzizi wa ulinzi wao mahasimu zake.
Punde si punde ghafla wote wakasimama ukumbi mzima wakati Profesa akiingia ukumbini akiwa katika sura yake halisi bila kujificha uso. Walikuwa wanapiga makofi ya pongezi kwa kishindo kuonyesha kufurahishwa na ujio wake mkutanoni. Wengi wao macho yaliwatumbuka kumshangaa Profesa Asante-Rabbi ikiwa ni mara yao ya kwanza kwao sura yake kudhihiri mbele yao. Walikuwa wanamsikia tu simulizi zake za kustaajabisha ila leo wamefanikiwa kumuona mubashara.
Alipoketi kitini, mara moja mipango mbalimbali ya namna pesa zitakavyowafikia huko Mikoani za kuhonga wapiga kura kwa ajili ya kukichagua chama cha 'National Movement Party' (NMP) ikaanza kupangwa. Malengo yao yalikuwa ni kupata kura milioni 8 tu za kununua huku wakijumlisha na wale wafuasi kindakindaki walikuwa na uhakika wa kupata kura milioni 10. Kura ambazo zingewatosha kuingia Ikulu na kuunda serikali.
Ajenda yao ya mwisho ikaanza kumjadili Kachero Manu, huku ikiamrishwa asogezwe mbele ya meza kuu. Kachero Yasmine alitoa amri mmoja wa askari wake wa kike ndio akae jirani na Kachero Manu ili awe chambo cha kupokonywa silaha kirahisi na Kachero Manu ili wakilianzisha wote waanzishe vagi kwa pamoja wakiwa na silaha.
Profesa sasa ukawa uwanja wake wa kujimwayamwaya kwa kujifunga kibwebwe uwanjani dhidi ya adui yake Kachero Manu.
"Nitakuchinja mbele ya umati huu wa watu iwe fundisho kwa wasaliti wengine" alizungumza Profesa huku akiwa anafoka kwa hasira.
"Umenidanganya kuwa umetumwa na kijana wangu Man-Temba kumbe wewe ndio umempoteza, na kijana wangu Nathanieli pia mmemuua. Umekaa nyumbani kwangu nimekupa mbinu zote za medani za udukuzi kumbe unanidhihaki ukinifanya zuzu tu eeh...sasa nitakuonyesha kilichomtoa kanga manyoya..!". Akaanza kumkaribia Kachero Manu huku ameshachomoa bisu kubwa lenye makali toka kiunoni amekaa nyuma ya shingo la Kachero Manu.
Kachero Manu hakusubiri kugeuzwa kuwa mbuzi wa kafara, fujaa bila kutarajiwa, alijirusha hewani toka kitini na kufanikiwa kumpokonya silaha yule mlinzi mwanamke kisha akiwa bado hewani akafanikiwa kumbana Profesa roba ya miguu kwenye shingo. Wote kwa pamoja wakaanguka chini kwa kishindo cha tii!.
Kachero Yasmine nae hakulaza damu akaanza kuchakaza meza kuu kwa risasi akianzia na Chew Master.
Kishindo kikubwa cha mlango kuvunjwa na bomu kikasikia huku wakiingia makomandoo 5 wa jeshi la wananchi, JWTZ. Walipata wito wa Kachero Yasmine waje kuongeza nguvu wakawasili kwa kutumia nyambizi.
Ndio hao makomandoo alimtuma yule mtumishi wa usafi ahakikishe anawaelekeza mkutano ulipo kwa haraka. Makomandoo wengine walipigiwa simu na Yasmine wakati anatoka chooni wakawa wameshaizunguka nyumba ya Flora Tarimo.
Papatu papatu ya mapigano ilirindima vilivyo. Washirika zaidi ya 20 walishapoteza maisha, huku wengine wote wakijisalimisha na kutiwa mbaroni.
Profesa Asante Rabbi na Chew Master walikuwa wapo hoi kwa mkong'oto kabambe wa paka mwizi walioupokea siku hiyo. Walinzi wa kike karibia wote walikuwa wameuliwa. Tayari zilishaitishwa boti za kutosha za kuwapakiza washirika wote wa NES tayari kwa ajili ya kuwafikisha katika vituo mbalimbali vya polisi.
Kachero Manu na Kachero Yasmine wakakumbatiana kwa furaha, wakipongezana. "Ahsante Yasmine, kazi imekwisha!" alisema Kachero Manu. "Bosi bado kazi mbichi, pesa bado hatujazikomboa na marehemu Dr.Pius Chilembwa bado hatujamtia mbaroni. Anatakiwa akafufuliwe alipojizika aje kusimama mbele ya vyombo vya dola kujibu mashitaka yake" Kachero Yasmine alimgutusha Bosi wake wajibu wake uliobakia. Wakati makomandoo wale wakiwaswaga washirika wale kuwaingiza kwenye boti, Kachero Manu na Kachero Yasmine walitoweka kimaajabu Hotelini pale bila kujulikana wanapoelekea.
ITAENDELEA
Sent from my TECNO CC6 using
JamiiForums mobile app