RIWAYA : KIJIJINI KWA BIBI.
MTUNZI : ALEX KILEO.
SEHEMU YA AROBAINI.
__________________
ILIPOISHIA....
-----------------------------
Kona ya kwanza aliikata vizuri huku akiwa katika mwendo ule ule wa kasi, kwenye kona ya pili ndo kulikuwa na shughuli, gari ya polisi ambayo alikuwemo Babu wa monchwari na askari nayo ilikua katika spidi ya juu, ndio ya mwisho, nao walibakia mita chache waifikie nyumba ya mama kayoza, ile kukata kona tu, ili gari lishike barabara ya nyumba ya wakina kayoza, na Sajenti Minja nae ndio alikuwa anaingia katika hiyo hiyo barabara inayoelekea kwa dada yake, basi kikasikika kishindo kikubwa sana ambacho hakikuwai kutokea pale mtaani, ni gari ya polisi iliivaa gari ya Sajenti Minja kwa ubavuni, ilikuwa ni ajali ya kutisha sana.
Ni damu pekee ndizo zilionekana vizuri katika eneo lile na gari ya Sajenti Minja ilibondeka vibaya sana, haswa upande wa dereva. Hakuna mtu aliyeweza kuiangalia Mara mbili gari ya Sajenti Minja na hakuna mtu aliyekuwa na akili timamu aliyedhani katika ile ajali kuna mtu yupo hai....
*********ENDELEA**********
..eneo lote liligubikwa na harufu ya damu, watu wakaanza kujisogeza mmoja mmoja, dakika mbili tu zilitosha kujaza watu eneo la tukio.
Wasamalia wema wakatoa taharifa polisi baada ya kugundua kuwa gari moja lilikuwa na polisi.
Kwa jinsi hali ilivyoonekana, ilikuwa vigumu kujua kama watu waliohusika katika ajali ni wazima, ilionesha wote wamekufa. Kwenye gari ndogo ambayo ndani alikuwepo Sajenti Minja peke yake, yeye aliganda pale pale huku damu zikimtoka puani na mdomoni, wakati katika gari ya polisi, dereva, babu wa mochwari na askari mmoja aliekuwepo mbele, wote walitokea kupitia kioo cha mbele na kuangukia juu ya gari la Sajenti Minja, wote watatu walikuwa wamepoteza maisha, na nyuma ya gari, hakukuwa na dalili yoyote iliyoonesha bado kuna mtu ana hati miliki ya pumzi yake, wote walikuwa wamepoteza uhai.
Baada ya dakika kadhaa, gari ya polisi ilifika huku ikiongozana na ambulance ya hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
Mkuu wa polisi alishtuka sana baada ya kugundua kuwa lile gari dogo ni la Sajenti Minja, aliakikisha kila jambo linafanyika haraka.
Madaktari waliofika pale waligundua kuwa yule aliyekuwepo katika gari dogo ni mzima, baada ya kumpima na kugundua kuwa mapigo yake ya moyo yanapiga kwa mbali sana.
Wakamwekea mashine ya kusukuma hewa safi (oxygen) puani kwake, pamoja na dripu, kisha gari ya hospitali ikaondoka kwa kasi sana, huku ikipiga king'ora kumuwahisha hospitali majeruhi.
Kisha gari ya polisi nayo iliubeba mwili wa Babu wa monchwari na wale askari waliopoteza maisha na kuwapeleka monchwari kuwahifadhi.
Masikini Babu wa monchwari, toka kulinda maiti mpaka kulindwa kama maiti.
Ndivyo dunia ilivyo, kifo chake kilifanya aukose utajiri aliokuwa anaenda kuupata Siku chache zijazo. Kifo chake kimeacha majonzi kwa ndugu, marafiki na familia yake. Na zaidi kifo chake kimeacha tabu sana kwa watu waliokuwa wanamtegemea.
Alazwe pema peponi babu wa monchwari.
*****************
Mama kayoza na wanae walikuwa wanaongea maongezi yao ya kawaida pale nyumbani, ghafla wakasikia kishindo kikubwa sana,
"mh!, na huku kuna kambi ya jeshi karibu nini?", Kayoza alimuuliza mama yake,
"hakuna, ila iko kishindo inaweza kuwa tairi la gari limepasuka", mama Kayoza alijibu,
"Sio tairi ya gari hilo mama, mlio wa tairi naujua" Omary alimbishia Mama Kayoza na kisha Omari peke yake ndio aliamua kwenda nje kuangalia kilichotea.
Baada ya kusikia kelele za watu, nae alitoka tu mlangoni akamuuliza mtu mmoja aliekuwa anapita pale nje, akamjibu kuwa kuna ajali, baada ya kuridhika na jibu, Omari akarudi ndani.
"vipi, umeshaangalia?",Kayoza akamuuliza Omari,
"yah, ni ajali imetokea pale kwenye kona", Omari akamjibu,
"mtu kagongwa nini?", Kayoza akaendelea kudadisi,
"mimi sijafika, ila kwa kile kishindo, itakuwa gari imeikuta gari pale", Omari alijibu,
"madereva wa siku hizi hovyo kabisa, enzi zetu hizi ajali zilikuwa ni nadra sana", mama Kayoza aliongea kwa manung'uniko,
"mama ile kona mbaya sana", Kayoza aliongea kuwatetea madereva wa siku hizi,
"hata kama", mama Kayoza alishikilia msimamo wake,
"Wewe mama hushangai Sikh hizi magari yapo chungu mzima lakini ajali ni chache sana?" Kayoza aliendelea kuwatetea madereva wa kisasa,
"Zamani magari yalikuwa machache ndio, ila miundombinu ilikuwa mibovu na ajali zilikuwa chache pia" Mama Kayoza aliongea,
"Mimi nafikiri madereva wa Siku hizi ndio chanzo cha ajali nyingi, kwanza hata leseni zenyewe hawasomei, ila wanazipata kiujanja ujanja tu kwa kununua kwa rushwa" Omary aliongea kwa kumuunga mkono Mama Kayoza,
"Bora wewe mwanangu umeongea, hili likayoza bishi sana, kama marehemu Baba yake vile" Mama Kayoza aliongea,
"Basi yaishe, maana mmeamua kunichangia sasa" Kayoza aliamua kumaliza mada,
"Sio yaishe tu, kwanza kubali madereva wa sasa si madereva ila washika usukani tu" Mama Kayoza aliongea kwa utani,
"Sawa, kwa hiyo hata Mjomba Minja ni mshika usukani tu?" Kayoza aliuliza huku akicheka,
"Sasa yule udereva ni Nazi yake?, yule ni polisi bwana" Mama Kayoza alimjibu mwanaye,
"Tunapozungumzia madereva tunajumuisha wote, wanaobeba abiria na wanaoendesha magari yako binafsi" Kayoza aliamua kuipa nguvu point yake,
"Haya sawa umeshinda, maana unachotaka ni kubishana tu na mimi sitaki" Mama Kayoza aliongea,
Na katika kipindi hicho hicho kuna mtu alikuwa akigonga hodi mlangoni, kwa hiyo hodi iliyokuwa inapigwa ndio iliwakatisha maongezi yao,
"pita, mlango uko wazi", Mama Kayoza aliongea kwa sauti ili mgonga hodi amsikie,
"hodi tena, jamani salama hapa?", Kijana mmoja ambae anakaa nyumba ya pili kutoka pale, aliwasalimia huku akionekana mwenye wasiwasi,
"kumbe ni wewe Tino, sisi wazima, we hujambo?", mama Kayoza akamuuliza yule kijana,
"jambo ninalo mama yangu", yule kijana alijibu,
"haya tuambie hilo jambo sasa", mama Kayoza aliongea kwa sauti ya ucheshi,
"yule bro polisi, white white hivi, anaekujaga hapa amepata ajali pale kona", Yule kijana alitoa taharifa iliyowapa mshtuko wote waliopo pale,
"ah!, kagonga mtu", Omari aliuliza huku akisahau kuwa yeye ndiye aliyesema kile kishindo sio cha kugongwa mtu, ila ni magari yamegongana,
"gari yake imegongana uso kwa uso na gari ya polisi", Yule kijana aliendelea kuelezea alichokiona,
"ile gari ya polisi wote wamekufa, ila yule bro kabebwa hajielewi, sijui hata kama atafika hospitali", Yule kijana alipigilia msumari wa mwisho katika maumivu ya mama kayoza na wanae, kisha akawaaga, ila hakujibiwa kutokana na hali iliyokuwepo.
"Mama sasa tunafanyaje?" Kayoza aliuliza kwa sauti tulivu,
"Twendeni tu hospitali, hatuna muda wa kupoteza" Omary alijibu na kipindi chote mama Kayoza alikuwa amefumba macho anasali, hali aliyokuwa nayo ni dhahiri alikuwa amechanganyikiwa.
"Haya twendeni" Mama Kayoza aliongea huku akisimama,
"Sasa mama tunaenda hospitali gani?, au unajua hospitali aliyopelekwa?" Kayoza alimuuliza mama yake huku akimshangaa,
"Acha kuuliza maswali ya kijinga, wewe unadhani atapelekwa hospitali gani zaidi ya hospitali juu ya mkoa?" Mama Kayoza aliuliza huku akijitanda khanga,
"Mama tunapoteza muda bure, twendeni tuwahi" Omary aliongea huku akiwa amesimama mlangoni,
"Si huyu mpumbavu anauliza uliza vitu visivyokuwa na maana" Mama Kayoza aliongea kwa hasira huku akiuelekea mlango wa kutokea.
***********************
Majira ya saa sita mchana, mama Kayoza na wanae walikuwa wameshafika hospitali, moja kwa moja wakaenda kujitambulisha kwa madaktari, kisha wakaambiwa mgonjwa wao alipowekwa,
wakatoka tena hadi katika chumba cha wagonjawa mahututi(I.C.U), walizuiliwa mlangoni na manesi, wakaambiwa bado madaktari wako ndani wanapigania uhai wa mgonjwa.
Wakarudi kukaa katika benchi lililo jirani na kile chumba na wote wakakaa kimya huku kila mtu akiwaza jambo lake.
Mama Kayoza ndiye aliyeonekana amechanganyikiwa zaidi kuhusu hali aliyokuwa nayo Sajenti Minja.
Baada ya nusu saa, Daktari alitoka kutoka katika kile chumba alichokuwa amelazwa Sajenti Minja.
Mama kayoza na wanae wakamkimbilia, kisha wakajitambulisha, yule Daktari akawaangalia sekunde kadhaa, kisha akatingisha kichwa,
"Aya baba tuambie hali ya mgonjwa wetu ikoje?" Mama Kayoza aliuliza huku machozi yakianza kumtoka,
"Sasa mama unalilia nini, usilie bwana unakuwa unaleta uchuro" Kayoza alimwambia mama yake,
"Ebu ngojeni kwanza, wewe mama ni nani yake?" Daktari alimuuliza Mama Kayoza,
"Mimi ni dada yake, tumezaliwa baba mmoja na mama mmoja, baada ya kuzaliwa mimi ndio akafuata yeye" Mama Kayoza alijibu na kumfanya Daktari akili kuwa Mama Kayoza hayupo katika akili zake za kawaida,
"Na nyie vijana ni zake?" Daktari aliuliza huku akiwageukia Kayoza na Omary,
"Awa ni wanangu kabisa, yule ni mjomba wao" Mama Kayoza aliamua kuwajibia, maana aliona kama watachelewa vile kutoa jibu,
"Basi kama ni hivyo, mama nakuomba utusubiri nje, acha niongee na awa watoto wa kiume" Daktari aliongea huku akimtazama Mama Kayoza,
"Sasa utawaeleza nini awa watoto? Nieleze mimi mama yao, awa watoto wenyewe wananitegemea mimi" Mama Kayoza aliongea kwa hasira huku akianza kulia,
"Mama msikilize daktari, unapopayuka unakuwa unakosea mama" Kayoza alimwambia Mama Yake,
"Kaa kimya, tena funga mdomo wako, hujui uchungu ninaousikia hapa" Mama Kayoza alimkaripia mwanae huku akilia,
"Basi usilie, unalilia nini sasa?" Omary aliuliza baada ya kuona hakuna maelewano kutokana na kilio cha Mama kayoza,
"Muache alie, anastahili kulia kwa maana hata nyinyi mtalia muda mchache ujao" Daktari alimjibu Omary na kisha akawaambia habari mbaya ambayo ilipelekea mama Kayoza kupiga mueleka wa nguvu na kupoteza fahamu palepale...
**********ITAENDELEA**********
the Legend☆