MAUAJI YA KASISI
MTUNZI: richard MWAMBE
“Soldier!!!” Askari, sergeant Maria aliita kwa sauti na askari wote wakaja eneo hilo na kumbeba mwenzao wakimpakia kwenye gari, wengine wakabaki kufanya utaratibu wa kumuondoa Gichui ambaye alikuwa hana maisha tena na kichwa chake kikiwa kimevurugika kwa risasi ya Kariithi, moja kwa moja walimfikisha katika hospitali ya taifa ya Nairobi.
SEEMU YA 11
6
MADAM S alisimama kwenye mlango maalum wa kioo akimtazama Kamanda Amata aliyekuwa amelala kitandani akiwa ndani ya mitambotiba, sasa alikuwa ameamka baada ya kazi kubwa ya daktari wa muhimbili ya kumtoa sumu mwilini, alifumbua macho, aliweza kuongea japo kwa shida, alikutana macho na bosi wake, akamtazama, “Karibu Nairobi Madam,” Kamanda alimkaribisha madam S.
“Aliyekwambia hapa Nairobi ni nani?” Madam alimuuliza Kamanda.
“What?” akajiinua na kuketi, “Niko wapi?” akauliza.
“Upo Muhimbili, karibu sana Dar es salaam, Kamanda umefanya mambo ya kijinga sana Kamanda, siwezi kukuvumilia hata kidogo, tumekaa kikao na kuona kukutoa wewe katika cheo chako cha TSA 1 na kumpa mtu mwingine,” Madam S akameza mate, “Kila mara nakuonya na wanawake wako hutaki kunisikia, kwa nini? Sasa wlitaka kukuua, mshukuru bwana Shikuku na kijana wake Ndege, ulikuwa marehemu tayari, na sasa tungekuwa tunautafuta mwili wako. Kamanda huna maana tena kwetu na kwa serikali kwa ujumla, tunaandaa utaratibu wa kukustahafisha hasa kwa uzembe unaouonesha, unajua wewe ni kama roho ya serikali, wakikubana wewe watakuwa wamepata kila kitu, kila siri, na sumu waliyokupa si ajabu imekufanya utoe siri nyingi bila kujijua.” Madam akageuka na kuondoka zake na kufunga milango nyuma yake, Kamanda Amata akabaki kajiinamia kisha akajitupa kitandani kwa hasira, “Biiiiiillllllllllllllll !!!!!!!” alipiga ukelele wa nguvu kisha akapoteza fahamu. Ilikuwa ni zamu ya madaktari na wauguzi kuhakikisha wanaokoa maisha ya Kamanda Amata katika dakika hizo, haikuwa rahisi maana ilionekana mapigo ya moyo yakishuka zaidi, walijaribu mbinu zote za kitaalamu lakini bado hali ilikuwa tete, baada ya kuhangaika kwa muda refu, kidogo hali yake ilianza kurudi na mapigo ya moyo yalirejea kwenye hali ya kawaida ingawaje bado alikuwa katika usingizi mzito uliogubikwa na taswira ya Bill kama mtu wa kutisha na hatari, aliyetaka kuyakatisha maisha ya Kamanda kwa mtindo ambao hakuutegemea, wauguzi na madaktari walishusha pumzi wakiwa wamekizunguka kitanda cha Amata, walifarijika zaidi walipomshuhudia akiwa amefumbua macho akiwaangalia mmoja baada ya mwingine, “Kuna nini?” aliuliza, “Mbona mmenizunguka hivyo?”
“Kamanda! Ulikuwa katika hali mbaya sana, kiasi kwamba bila jitihada za hawa wote tungekukosa,” Daktari alimueleza akiwa amemuinamia. Ilikuwa kama hali ya mshangao kwa Amata, alijitazama kama mtu aliyerukwa na akili, “Yuko wapi Bill?” aliuliza. “Bill?! Bill ni nani?” aliulizwa na daktari, Amata alizungusha shingo yake na kuona wauguzi tu na madaktari, akajilaza kitandani kwa mara nyingine. “Ok, tumuache apumzike sasa,” ilikuwa ni kauli ya daktari akiwaambia wale wauguzi pamoja na wasaidizi wake, wote wakakiacha kile chumba na kurudi katika idara zao. Akili ya Kamanda Amata haikutulia, muda wote ilimuwaza Bill, hasira zikaanza kuuteka moyo wake, maneno ya Madam S yakamvunja nguvu, ‘Bill anataka kunisababishia kushushwa cheo na kustahafishwa kabisa,’ alijiwazia; ‘Haiwezekani,’ alinyanyuka katika kile kitanda alichokilalia, akajichomoa drip iliyokuwa ikiendelea kuingia mwilini mwake, akatazama huku na kule hakuona nguo yake yoyote zaidi ya yale mavazi aliyovaa, mavazi ya hospitalini, hakujali, akauendea mlango na kutoka, huku na kule, hakuna mtu, akatoka mlango wa pili na mpaka ule wa nje, akiwa pale nje alikutana na watu mbalimbali hakujali wala kushangaa, alipita eneo la walinzi na kufikia maegesho ya tax, akajichagulia moja, “Wapi mzee?” dereva Tax alimuuliza, “Kinondoni, mkabala na Leaders Club,” akampa maelekezo, wakatokomea kutoka hapo.
“Una simu hapo?” Amata alimuuliza yule dereva tax.
“Ndiyo braza,” akajibiwa.
“Niazime nipige mahali, pia niambie ni shilingi ngapi,”
“Haina shida, hapa utanipa shilingi elfu thelethini,” lilikuwa ni jibu lingine la dereva tax.
Kamanda Amata alichukua simu na kubofya namba Fulani, kisha kuweka sikioni, “Baada tu ya kukata simu hii, naomba uingize shilingi elfu hamsini katika namba hii, (…) niangalizie kama kuna ndege inayoondoka mida hii kupitia Nairobi, iwe inaelekea hapo au inapita hapo, niandalie safari tafadhari, nina dharula, call aborted” Akakata simu na kumrudishia, dedreva tax, akamuamuru kusimama, akashuka na kuagana nae baada ya kumpa maelekezo kuwa hela yake itaingia kwa simu.
§§§§§
“Pamoja na maumivu ulonayo, nitakupa malipo yako ya mwisho, umenifanyia kazi kubwa sana Cheetah,” Bill Van Getgand alikua akimuangalia Cheetah kwa jicho la uchungu sana hasa pale kijana huyo alipokuwa akiugulia kwa maumivu ya jeraha lake, hakuweza kwenda hospitali kwa kuhofia polisi, hivyo alijificha katika moja ya magheto yake katika mji mdogo wa Kinangop ya kaskazini. Bill akatoa bunda la noti na kumpatia, “Ugawane na Mellina, lakini usisahau kumnunulia sanda Gichui,” akanyanyuka na kulitwaa lile begi la ngozi na kumpa Wambugu kisha kwa kutumia ile fimbo yake akaujongelea mlango wa kutokea nje ya ghto hilo, akasimama na kugeuka nyuma, akawa akitazamana na Cheetah. “Asante braza, nitafanya hilo, wewe ni mwema sana, maana mwingine angeshapata mzigo wake na kutoroka hata asingekumbuka kazi kubwa aliyofanyiwa na swahiba zake,” Cheetah aliongea kwa tabu kidogo, akionekana wazi ni mwenye maumivu makali katika jeraha lake. “Nami na shukuru kwa kazi njema mliyonifanyia, nasikitika sana juu ya Gichui lakini naamini Mellina mtaonana usiku huu, lazima akufuate. Kwa kuwa mimi sijakudhulumu haki yako basi naomba na wewe usimdhulumu Mellina haki yake. Cheetah lazima ujue hata waovu wana aina ya wema uliobaki mioyoni mwao,” Bill akanyanyua ile fimbo yake ya kutembelea, akaongea huku akiwa ameiyooshea kwa Cheetah pale kitandani, akitoa maneno ya faraja na kumshukuru, mkono wake wa kulia ulioishika ile fimbo ukafyatua kibati Fulani karibu kabisa na kwa kushikia, ukakibonyeza tena ka namna nyingine, mara kitu kama msumari kikachomoka kwa kasi kutoka katika ncha ya fimbo ile na kuzama moyoni mwa Cheetah, macho yakamtoka Cheetah, akabaki akimtazama Bill, damu ilitiririka na kuichafua fulana yake, akalegea na kudondokea kifuani, “Asta la Vista baby,” Bill alitamka maneno hayo na kuchukua tena lile bunda la noti akaligawanya nusu, nusu akaiacha pale kitandani na nusu akatoka nayo.
“Kuna watu ninaohitajia pumzi zao leo kabla sijaondoka,” Bill alimwambia Wambugu wakiwa ndani ya gari yao.
“Mi nilijua ushamaliza kazi kaka,” Wambugu aliijibu kauli ya Bill
“Hapana, lazima tusafishe makandokando yanayoweza kutuletea shida wakati wa kula bata,” Bill aliendelea.
“Kwa hiyo unasemaje?”
“Nina muda mchache sana wa kupotea hapa mjini, najua natafutwa, nimeshawaona, FBI ninaowafahamu, watu wa MOSSAD wapo mjini, ukiachana na wana usalama wa hapa Kenya, nafurahi tu kuwa Kamnda Amata popote alipo lazima apoteze uhai, sumu niliyompa ni mbaya sana,” akakohoa, “Wambugu!” akaita na kumtazama kijana huyu wa Kikuyu, “nataka roho ya Mellina na Kahaba Rose ndani ya masaa machache yajayo.”
Ilikuwa ni kauli iliyotaka kumfanya Wambugu ashindwe kuendesha gari lakini alijikaza kisabuni nyuma ya usukani na kumeza mate maana alihisi koo limekauka kau.
“Mi nilifikiri hao hawana maana,” Wambugu aliongea kwa upole.
“Wakishakufa niulize kwa nini nimewaua nitakwambia sababu ambayo hata wewe ungewaua, cheetah tayri nimeshamuua,” Bill alisema huku akiwasha sigara yake kuvuta akizitupia nywele zake ndefu mgongoni.
“Simamisha gari pale karibu na ile Subaru,” Bill aliamuru na Wambugu akasimamsiha kama alivyoagizwa, Bill akashuka na kulichukua lile begi, akasimama na kumwangalia Wambugu, “Sikia, kama unataka maisha yako basi ufunge mdomo, hakuna ajuaye undani wa sakata hili zaidi zaidi yaw ewe, Mellina na kahaba Rose. Naomba uchunge mdomo wako, ila kazi moja ukanifanyie, hakikisha unamuua Rose na Mellina kabla hujajiua mwenyewe,” Bill aliongea huku akimrushia kile kibunda cha pesa Wambugu kupitia dirisha la ile gari, akakidaka na kukiweka kitini. “Nitakupigia simu baada ya masaa matatu ili nijue kazi yangu imefikia wapi, elewa kuwa hauko peke yako,” akageuka na kuliendea lile gari aina ya Subaru na kulitupia lile begi kiti cha nyuma kisha yeye akakaa nyuma ya usukani wa gari ile na kutokomea akiifuata barabara ya Uganda.
§§§§§
Haikuwa rahisi kwa Madam S kuelewa kile anachoambiwa na dakatari kuwa Kamnda Amata ametoroka hospitalini, alibaki kimya huku akiwa anashindwa kuchanganyikiwa, akizunguka kutoka upande mmoja kwenda mwingine wa ofisi ile, akasimama katikati na kumtazama daktari kwa makini, “Hebu nambie, katoroka au katekwa?”
“Kweli Madam katika hilo siwezi kujibu, mi nimerudi sikumkuta kila niliyemuuliza anadai hakumuona,” alimjibu.
Madam S alitoka kwa daktari bila kuaga na kuielekea gari yake, akaketi ndani na kuitia ufunguo, switch on, kisha akabonya bonya mahali Fulani. Skrini ndogo ikachomoza na kujifungua katia ile dashboard ya gari, akaminya mahali Fulani katika skrini hio mara ramani kubwa ikatokea, akaingiza namba Fulani ambazo hutumia kumpata Kamanda Amata, kwa kujua mahali alipo lakini haikuwa rahisi kupatikana, alijishika kichwa hajui la kufanya, akawasha gari na kurudi ofisini.
Mawazo yalimtawala hakujua la kufanya, alishika hiki mara kile, alijaribu mbinu zote za kitaalam kupata Kamanda, haikuwa rahisi. Akapata wazo, akampa kazi Chiba amsake mpka amtie mkononi.
Gina aliegesha gari yake katika maegesho ya uwanja wa ndege wa Dar es salaam,
“Mtu awaye yote akikuuliza juu yangu mwambie nipo katika majukumu ya kiserikali, najua Madam S atakutafuta jioneshe kuwa hata hujui wapi nilipo zaidi ya Nairobi, kwa heri mpenzi tutaonana tena,” Kamanda Amata alimkumbatia Gina kumuaga, Gina alikuwa akitokwa na machozi ya upendo.
“Kamanda, najua hauko sawa sana, lakini nakuombea urudi salama, mambo yakiwa magumu basi nipe taarifa nije kukusaidia kwa lolote,” Gina aliongea sikioni mwa Amata wakiwa bado wamekumbatiana, kisha wakaachana na Kamanda akaelekea katika chumba cha wasafiri, huko haikumchukua muda, akaondoka zake na ndege ya shirika la ndege la Kenya na kurudi katika jiji la Nairobi, sasa akiwa binafsi zaidi, hakuna aliyejua kama yupo huko zaidi ya Gina, katibu muhtasi wake.
Masaa machache yalimchukua hewani na baadae kuikanyaga tena ardhi ya Kenya, moja kwa moja alirudi palepale katika hoteli ya Intercontinental maana alijua wazi kuwa si pengine pa kuanzia kazi zaidi ya hapo. Ni masaa ishirini na nne na kidogo alikuwa mahali hapa, aliingia chumbani kwake na kukagua harakaharaka kwa macho, akaona jinsi chumba kilivyopekuliwa kitaalamu lakini zile alama ndogondogo alizoziweka alikuta haziko vile kutokana na upekuzi huo, alijaribu kuangalia kama kuna kitu chochote chenye hatari kwake, lakini hakukuwako, alipojiridhisha akaweka vitu vyake sawa na kuketi kitini akiwa tayari na bastola yake mkononi, alijuwa wazi kwa vyovyote lazima wapo wanaojua juu ya ujio wake hivyo kuna uwezekano wa kuja usiku huo, alizima taa na kuketi macho kodo katika kiti kilichopo kwenye moja ya kona ya chumba hicho.
Kamanda Amata hakukosea, katikati ya usiku alihisi mlango ukifunguliwa, akajiweka sawa tayari bastola yake iliyofungwa kiwambo cha sauti ikiwa mkononi mwake. Taratibuuuuu mlango ukasukumiwa ndani, na huyo mtu akajaribu kuwasha taa ya ndani lakini haikuwakam akachezesha mara kadhaaa ile switch lakini bado taa haikuwaka. Akavuta hatua chache ndani na kuingia kisha akarudisha mlango nyuma yake, kabla hajafanya lolote alijikuta akimulikwa na mwanga mdogo mwekundu katika kifua chake, akachangayikiwa hajui la kufanya, mara taa ya mezani ikawaka kwa mwanga hafifu.
“Tulia hivyo hivyo,” sauti ya Kamanda Amata alitua katika masikio ya mtu Yule, kama alikuwa hajawahi kukutana na mtu huyu sasa ilikuwa zamu yake, miguu ilimchezacheza, alitamani kukimbia lakini haikuwa hivyo.
“WE nani?” Yule mtu aliuliza.
“Kwani we umekuja kumfuata nani?” Amata alijibu kwa swali. Risasi ya kwanza ikavunja mguu wa mtu Yule kabla hajajiweka vizuri pale chini alipokuwa akiugulia kwa maumivu tayari Kamanda Amata alikuwa amemfikia na kumkanyaga kwenye jeraha hilo lililokuwa likivuja damu mbichi.
“Jibu maswali yangu, nikuache hai,” Kamanda alianza namna hiyo, “Nani amekutuma?” akaanza namna hiyo.
“Mimetumwa na boss kaka,”
“Sawa, nitajie jina lake,”
“Mi simjui kaka, simjui kabisa,” alijibu huku akilia kwa maumivu.
“Sikiliza wewe bwege, ukilia utasumbua watu kwenye vyumba vingine, jibu maswali kwa ufasaha, sawa?!” Kamanda aliuliza kwa ukali huku bado akikandamiza lile jeraha la Yule mtu.
“Basi kaka nasema, nasema, usiniumize nasema,” akameza mate, kisha akaendelea, “Tumetumwa na mtu mmoja anaitwa Wambugu”
“Kawatuma nini?” lilikuwa swali lingine kutoka kwa Amata.
“Begi na nyaraka nyingine za muhimu kama zipo,”
“Ok, nay eye yuko wapi?”
“Kuna kazi nyingine anafanya huko mjini,” alipojibu hayo mara simu yake ya mkononi ikaita kutoka katika mfuko wa jeans, Amata akainyakuwa na kusoma jina lililopo hapo juu ‘Moriyo’, “Moriyo ndo nani?” Amata aliuliza tena.
“Ni mwenzangu yuko hapo chini ananisubiri, tumeambiwa tupeleke haraka hilo begi,” Kamanda Amata hakupenda kupoteza muda, alimuwekea ile bastola katika sikio lake la kuume, “Usiniue kaka, nina watoto mimi watalelewa na nani?” alilia kwa uchungu.
“Ungekuwa na watoto unaowajali, ungefanya kazi za kishetani kama hizi, sikuui lakini lazima uwe mlemavu ili siku zote za maisha yako umkumbuke Kamanda Amata,” alipotamka jina hilo, akamuona Yule jamaa akishituka na kuguna kama aliyekutana na jinamizi.
“Umesema we nani?” aliliza hata akawa amesahau kama ana jeraha baya la risasi katika goti lake, “Amata, Kamanda Amata, na siyo mzimu ni mimi mwenyewe halisi, namtaka huyo Wambugu na mwenzake Bill,” Yule jamaa bado aliduwaa akimkodolea macho Amata, “WE umeshakufa kaka,” Yule jamaa aliongea kwa unyonge.
“Ni sawa, na sasa nimefufuka kutoa wafu kama nilivyosema,” kabla hajaendelea na lolote, Kamanda Amata alimshuhudia Yule jamaa akitapatapa akirusha miguu huku na kule, alipomtazama vizuri, aligundua tundu la risasi kifuani mwake, risasi imepigwa wakati gani, kitendawili. Alichosikia yeye ni mvumo hafifu wa kitu kama nyigu kumbe tayari chuma hicho kilishatumwa kutoa uhai wa mtu. Amata alitazama huku na kule bado ukimya ulitawala, mara akasikia nyayo za mtu zikitembea harakaharaka kwenye korido, akatoka haraka na kuufungua mlango , akashuhudia mtu akiishia kwenye lifti ya jingo hilo, haraka akakimbia na kuziwahi ngazi za kushukia chini na kuteremka nazo. Kamanda Amata alfika chini na kushsudia Yule mtu akiwahi kuingia katika gari Fulani, lakini kabla hajaisjia garini, tayari shabaha isiyo na chembe ya uongo kutoka katika mikono makini ya Kamanda Amata, Tanzania Secret Agency ilikuwa imeshafumua ubongo wa kiumbe huyo na kumfanya alalie kiti cha dereva bila uhai huku miguu ake bado ikiwa nje ya gari hiyo, kazi imeanza. Hakumjali marehemu wa ndani wala nje, aliichukua ile simu aliyokuwa ameichukua kwa Yule jamaa wa kule ndani na kuifungua, haikuwa na namba hata moja, akenda kwenye meseji pale mwili ulimsisimka hata nywele alihisi zina simama baada ya kukutana na ujumbe uliondikwa,
‘Hakikisha kahaba Rose anauawa kabla ya jua la asubuhi, kisha nitakupa kazi ingine,’
‘Kahaba Rose,’ Kamanda Amata alilirudia jina hilo akilini mwake mara kwa mara, akiwa amesimama kwenye kiambaza cha ukuta aliendelea kusukuti juu ya kahaba huyo kamanahusika na lolote katika sakata hili, lakini muunganiko wa matukio haukuwa sawa kwake, alimfikiria Yule mwanamke aliyepewa kumstarehesha kama ndiye lakini haikuwa hivyo, nwuisho alimua la kuamua, kumsaka kahaba ni kazi ndogo sana, aliweka bastola yake mfukoni na kuiendea simu iliyokuwa jirani, ‘simu ya jamii’ akukwanyua mkono kutoka katika kikalio chake na kubofya namba yenye tarakimu tatu na kusikiliza upande wa pili.
“Yes hallo tukusaidie nini?” ilikuwa ni sauti ya polisi wa kikenya, ambayo ilitaka kumfanya Amata kucheka lakini hakufanya hivyo.
ITAENDELEA.....