MAUAJI YA KASISI
MTUNZI: richard MWAMBE
+255 766 974 865
Sehemu ya 19 & 20
“Ooh, karibu sana, tulikuwa tunakusubiri wewe tu, watu wote wako tayari kwenye ndege,” alizungumza Yule mwanadada aliyevalia nadhifu kabisa alimkaribisha Madam S na kuingia nae ndani moja kwa moja kwenye ndege hiyo ya kisasa kabisa, alimuonesha siti yake na Madam akaketi tayari kwa safari, baada tu ya yeye kuwa ameingia, ndege ile ilijitoa katika vizuiz vyake ikisukumwa na gari kubwa kuipeleka barabarni.
§§§§§
NDEGE na Kamanda Amata walikuwa wameegesha gari yao pembezoni mwa jengo la Posta katika mji wa Nairobi, wakijadiliana hili na lile jinsi ya kumnasa Wambugu. Kamanda Amata alichukua simu ya Wambugu, simu ya kisasa kabisa akaigeuzageuza na kumtazama Wambugu, “Unamjua Wambugu kwa sura?” akamuuliza.
“Hapana, sijawahi hata kumuona, hata hilo jina ni geni sana kwangu,” Ndege alijibu. Kamanda Amata akaichukua namba ya Wambugu na kuiingiza katika simu hiyo, akaiunga kwenye mtandao wa internet, kisha akaingiza nambari Fulani Fulani na kufungu mtandao wa usalama wa Tanzania, akaingiza ile namba pamoja na jina Wambugu katika na kujaribu kufananisha vitu hivyo. Haikumchukua muda mrefu simu hiyo ilimpa majibu, namba, jina na picha vyote vitatu vilionekana kwa wakati mmoja na maelezo mengine kedekede.
“Ndege!” Amata aliita na kumpa ile simu, “Unahisi huyu anaweza kuwa ndiye?” akamuuliza, Nege akaitazama ile picha kwa makini sana akatikisa kichwa.
“Naijua sura hii vizuri, ni moja kati ya wahalifu wanaoisumbua serikali,” Ndege alijibu huku akiirudhisha ile simu kwa Kamanda, kamanda Amata akaihifadhi ile picha katika sehemu maalumu kwa kazi hiyo ndani ya simu ile. Kisha akafunga ule mtandao na kurudisha simu katika hali ya kawaida, hakuishia hapo, “Ndege, piga simu kwa jamaa yako wa kampuni ya simu, atuambie simu tatu za mwisho za Wambugu zinasemaje tunaweza kupata majibu ya shaka letu.” Ndege akaichukua ile simu na kufanya hivyo kisha wakasubiri jibu watakaloletewa. Haikuchukua muda ukatumwa ujumbe wa sauti katika simu hiyo, Ndege akaufungua na kusikiliza, hawakukosea, ilikuwa sauti ya Bill ikimtaka Wambugu aende Iryamurahi akajifiche huko.
“… najua kuwa una mahangaiko makuu, najua kuwa Mellina amekamatwa, sasa sikiliza, na husijibu simu hii bali tekeleza unaloambiwa, ondoka haraka Nairobi kwa njia za siri unazozijua wewe, njoo Iryamurahi utanikuta hapa, kisha tupange mpango kabambe wa kuondoka katika nchi hii, nakusubiri, ukifika hapa mjini nitakupigia…”
Ilikuwa ni mwisho wa ujumbe ule wa sauti.
“Ina maana Bill yupo Iryamurahi?” Ndge aliuliza kwa mashaka, huku akiwasha gari na kuliingiza barabarani kuchukua barabar ya kueleka Embu.
“Ndege, Bill ni jasusi la kimataifa, hawezi kukaa nchini kwako wakati kazi aliyopewa imekwisha,” Amata alimjibu Ndege, akaichukua tena simu ya Ndege nakuanza kufanya utundu mwingine wa kupata uelekeo ambao Wambugu atakuwepo kwa wakati huo.
“Unafanya nini?” Ndege akauliza.
“Natafuta uelekeo wa Wambugu atakuwa wapi, kama katoka Nairobi au bado hajatoka tusije tukapoteza muda,” Kamanda Amata alijibu.
“Hiyo kazi ndogo Kamanda, piga simu kwa huyo jamaa atatuambia point gani alipigia simu mara ya mwisho na sasa atakuwa maeneo gani kadiri ya signal inavoonesha,” Ndege alimuelekeza Kamanda.
“Ndege acha kutumia njia za kianalogia hizo, sasa hivi namtafuta kwa GPS na nitakwambia alipo,” Kamanda Amata akaiweka simu katika program ya GPS akajaribu kuingiza namba za Wambugu na kuitafuta simu anayoitumia, jibu likaja, ikatumwa namba ya IMEI ya simu ambayo kwa wakati ule ilikuwa imebeba sim card ile, akaendelea na utundu wake mpaka akaweza kuunganisha mtandao huo, taraytibu ramani ya Nairobi na vitongoji vyake ikaonekana katika kioo cha simu hiyo, kidoti chekundu kikatua katika maeneo ya Juja. Kamanda Amata alicheka kwa ushindi huo.
“Wambugu hayupo mbali sana,” Amata alimwambia Ndege, akamtajia na vpimo vya ardhini kabla hajamaliza Ndege akamwambia hilo ni eneo gani. Gari ikaongeza moto kuelekea barabar ya Embu kumuwahi Wambugu, “Tusifanye lolote, twende nae mpaka Iryamurai tukaone kuna nini,” Kamanda Amata alimwambia Ndege aliyekuwa katika usukani akiendesha gari hiyo kwa kasi ya ajabu.
“Kamanda, kimpata Bill utamfanyan nini?” Ndge aliuliza swali la kizushi.
“Sijui, ila shetani anajua maana nina hasira nae, na nitamfuata popote alipo katika dunia hii, mpaka nimtie mkononi,” Amata alijibu. Wakati huo walipita maeneo ya Kasarani na kuendelea kuikanyaga lami kusonga mbele.
§§§§§
Saa sita usiku, ndege ya Swiss ilikanyaga ardhi ya Nairobi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta. Madam S alikuwa ni mtu pekee aliyeshuka katika ndege hiyo, aliwashukuru wafanyakazi kwa ukarimu wao na kuzishuka ngazi hizo kwa fujo. Alipomaliza itifaki zote, alitoka nje lutafuta usafiri wa kwenda mjini.
“Karibu Madam, karibu sana Nairobi,” ilikuwa ni sauti ya kiume iliyotokea kwa nyuma yake, madam alisita kwa kuwa hakutegemea kupata ukaribisho wa aina yoyote hapo Nairobi, mkono mmoja ukiwa ndani ya jacket aliloliva muda mfupi uliopita katika kukabiliana na baridi ya Nairobi, aligeuka nyuma na kumuona kijana huyo mwembamba mrefu, sura yake haikuwa ngeni sana machoni, alimtazama tena na tena kisha akamkubuka, “Mashaka?” alimuuliza.
“Ndiyo, Mashaka, kutoka ubalozi wa Tanzania,” alijibu Yule kijana ambaye jina lake ni Mashaka, alietumwa miaka kadhaa nyuma kufanya kazi za idara ya usalama katika ofisi za ubalozi wa Tanzania huko Kenya.
“Kwangu?” Madam aliuliza.
“Ndiyo,” Yule kijana akajibu, kisha madam akaondoka eneo lile na kuelekea kunakoegeshwa tax, akaingia na kuketi ndani, Yule kijana akarudi na kuingia kwenye gari binafsi nyingine. Dereva wa tax hiyo akageuka nyuma na kumtazama Madam S, kabla hajaongea chochote Madam S alimwambia, “Safari Park Hotel,” kisha akampa noti tatu za shilingi elfu moja moja za Kenya, safari ikaanza.
Kwa kuwa ni usiku haikuwa tabu na wala haikuchukua muda kwao kufika katika hotel hiyo. Akiwa ameketi katika gari hiyo mara alihisi mfinyo katika mkono wake wa kushoto, akauinua na kuitazama saa yake kisha akabofya kitufe Fulani, mara mkanda mwembamba ukatoka kwa chini ukiwa na maadishi Fulani, akausoma na kuukata kisha akautia kwenye mfuko wa suruali.
‘…Kamanda Amata yupo Nairobi, kwa sasa yupo barabara iendayo Embu akielekea upande wa kaskazini, nimemnasa pindi alipotumia mtandao wetu wa usalama kwa kupitia nywila yako. Chiba…’
Ulikuwa ni ujumbe uliokuwa katika kijimkanda hicho. Madam S alikunja sura, ‘mshenzi kabisa Amata, kaipata wapi password yangu?’ alijiuliza.
Ilimbidi Kamanda Amata kutumia password ya Madam S baada ya kugundua kuwa ile yak wake ilikuwa imefungwa hivyo hakuweza kuingia kwenye mtandao wa usalama wa Tanzania, alijaribu kuibuni password ya Madam S mara mbili, mara mbili ya tatu akaipata na kuingia kwa kutumia jina hilo, baada ya kumaliza kazi hiyo ndipo Chiba alipojua kuwa kamanda Amata yupo Nairobi kwa jinsi alivyokuwa akichukua data ambazo zinaendana na kazi aliyotumwa tangu mwanzo huko Nairobi. Ubalozi wa Tanzania huko Kenya kupitia mtaalamu wa mawasiliano aliyepelekwa kwa ajili ya kublock password zilizoibwa na Bill, Frank Masai aligundua kuwa muingiliano huo uliotokea Nairobi kwa vyovyote madam S alikuwapo hapo, alipowapa taarifa hiyo wengine wakafanya uchunguzi wa haraka na kugundua kuwa Madam S yupo njiani kuja hapo Nairobi, hivyo wakamtuma Mashaka kumuwekea ulinzi kutokana na hali halisi ilivyo katika jiji hilo.
Madam S aliweka kambi katika hotel ya Safari park, alihakikisha kila kitu kipo salama, na kupanga jinsi ya kumsaka Kamanda Amata kwa udi na uvumba. Aliifungua laptop yake ndogo na kuingia kwenye mtandao wa idara ya usalama, kwanza akaangalia ni nini Kamanda Amata alikuwa akifanya katika mtandao huo, akasoma maelezo ya Wambugu na kuitazama picha yake, akaangalia na maelekezo mengine mengi, akaichukua namba ya simu iliyojitokeza hapo ambayo Amata aliitumia kuchukua maelezo hayo, akatabasamu na kumsifu Amata kimoyomoyo kwa jinsi alivyokuwa mtundu wa kufikiri pindi anapohitaji maelezo Fulani. Alikumbuka jinsi anavyoweza kuiga sauti na saini za watu pindi anapohitaji kufanya hivyo, hakushangaa kusikia kuwa ameweza kupenya mtandaoni kwa kutumia password yake. Alijiuliza mwenyewe, nani anaweza kukaa katika cheo cha Kamanda Amata na akatosha katika kila idara, mapambano ya mikono, utumiaji wa silaha za aina na aina, lugha za kutumia, utundu wa kuendesha vyombo vya ardhini, majini na angani, utundu wa kuiga sauti za watu, saini za watu, vyote hivi nani angeweza, kama isingehitajika watu wawili au zidi kufanya kazi ya mtu mmoja. Jambo moja tu lililomuuzi ni wanawake, Kamanda Amata alikuwa mdhaifu sana mbele ya mwanamke, na adui zake wengi walimuweza kwa hilo tu, walimkamata kwa hilo tu. Lakini bado walipokuja kuona jinsi na njia aliyotumia kutoroka walibaki hoi. ‘Kamanda atabaki kuwa Kamanda tu,’ Madam S alijisemea huku akiifunga laptop ile ndogo na kuirudisha mahala pake.
EMBU – KENYA
EMBU, mji uliopo kilomita takribani 120 kutoka Nairobi, upande wa Kaskazini mashariki kuelekea mlima Kenya. Ukifika miezi ya kumi na kumi na moja utafurahi kuona barabara na viunga vyake vilivyopambwa kwa maua ya rangi ya zambarau kutoka katika miti ya Jacaranda.
SAA 4:15 USIKU
MAINA HIGHWAY HOTEL
KWA KUTUMIA mwendo wa miguu, Wambugu alivuta hatu kuelekea katika hoteli hiyo iliyopo katikati ya mji katika mtaa ya Haille Selasie, moyoni mwake alikuwa na amani sana kuwa sasa kafanikiwa kulitoka jiji la Nairobi. Akitegemea kukutana na mtu wake, Bill siku inayofuata huko Iryamurai, kabla hajaifikia kaunta ya hotel hiyo simu yake ikatikisika mfukoni mwake, akaitoa na kuitazama, private call, ilijiandika, hakuipokea akaenda kaunta na kuchukua chumba.
Akiwa ndani ya chumba chake Wambugu aliiona tena simu yake ikiita, akainyakua na kupoke,
“Wambugu, nikipiga simu upokee mara moja, unafuatwa, hapo mahali si salama, ondoka mara moja, nenda utafute sehemu salama,”
Ile simu ikakatika, Wambugu akabaki ameduwaa, hajui la kuamua, ‘Nani ananifuata?’ alijiuliza, ‘Bill amejuaje?’, ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Wambugu kufanya uamuzi, kwa kuwa alikuwa akijiandaa kuoga, ilibidi aahirishe zoezi hilo na kujipanga kutoka katika hoteli hiyo, alirudi kaunta akiwa kaweka mkono wake mfukoni, kashikilia bastola tayari kwa lolote ambalo litatokea. Alikabidha funguo na kuaga kuwa atarudi muda si mrefu. Alitoka na kuzishuka ngazi kadhaa za mlango huo na kupotelea kwenye kichochoro Fulani ambacho kilimleta katika maduka na mchanganyiko wa watu, ‘niende wapi?’ akajiuliza, hakupata jibu, usiku ulizidi kuwa mnene, kichwa kikimuuma, mawazo yake yakivurugika, mipango ikigoma kupangika, ulikuwa wakati mgumu. Wambugu alivuta hatua ndogo ndogo kuelekea kituo cha tax, pale alizikuta tax chache zinazongoja abiria wa usiku, akiwa kutahamaki hivyo mara gari moja aina ya Jeep Cherokee ilisimama ghafla miguuni mwake, mlango ukafunguliwa kwa haraka na Kamanda Amata akatoka bastola mkononi, Wambugu akajua hapo kazi nzito, alipiga risasi moja kwenye kioo cha dereva, wakati Kamanda Amata anazunguka gari kiufundi ili kumfiikia Wambugu, kumbe mwenzake alishaliona hilo, akalala chini na kupita uvungu wa gari akatokea upande wa pili kisha risasi mbili zilifumua matairi nay a tatu ikalenga tank la mafuta. Kamanda Amata alipogeuka nyuma alishuhudia ile gari ikipaishwa juu kwa mlipuko huo, akajishika kichwa kwa sekunde kadhaa kisha akaikimbilia ile gari na bila kujali, alifungua kwa taabu mlango wa dereva, na kumtoa Ndege ambaye alipigwa risasi begani na Wambugu, akamvuta na kumtoa nje, hali ya Ndege haikuwa nzuri kwani jeraha la risasi na ule moto almanusura vimmalize. Haikuwa na aja ya kumtafuta Wambugu aliomba msaada wa wananchi na kumkimbiza hospitali ya Agha Khan.
Wambugu baada ya kuona kafanikisha hilo, alikimbilia kwenye viunga vya mji na kutokomea mbali kidogo na mji. Alitembea polepole na kutafuta mahali pa kujihifadhi usiku huo maana aliona sasa hakuna sehemu yanye usalama kwake.
Polisi wa Embu, walifika katika hospitali hiyo na kukutana na Kamanda Amata aliyekuwa pembeni mwa kitanda cha Ndege wakati mwenyewe akiwa katika chumba cha upasuaji.
“Tunataka tujue ni nani jambazi na nina mwanausalama?” askari mmoja alieonekana kuwa ndio mwenye sauti aliuliza. Kamanda Amata alimtazama kwa tuo askari huyu aliyeonekana anajua sana kuongea. Akamuonesha kitambulisho chake, lo, Yule askari alilowa ghafla na kutoa salamu ya kiaskari kwa ukakamavu wa hali ya juu.
“Sasa sikia, kuna jambazi hili hapa,” akachukua simu ya Ndege na kumuonesha ile picha, Yule polisi akashtuka kidogo na kushangaa akiwa kakunja ndita si kitoto, “Huyu, kafika hapa, ni mtu hatari sana tunamtafuta nchi nzima mpaka nje ya mipaka, ok sasa kama unaruhusu nianze doria usiku huu,” Yule polisi alimueleza Kamanda Amata, baada ya kufikiri kidogo, akaona hiyo ni njia nzuri ya kujua ni wapi huyo mtu anaweza kuwapo. “Ok, hakikisheni mnampata akiwa hai maana kuna maelezo nayataka kutoka kwake,” Yule askari alipopokea hiyo amri, akapiga saluti na kuondoka.
Usiku huo mchakamchaka ulianza, kila kona kila mtaa ni gari za polisi kumsaka Wambugu. Kila nyumba ya wageni ilipekuliwa usiku huo na akila aliyefanana alibebwa na kupekwa kituoni.
Melchior Ndege alirudishwa wodini baada ya lisaa limoja kwa oparesheni iliyofanikiwa sana ya kuitoa risasi iliyokwama katika mifupa ya bega lake la kulia, majeraha ya moto hayakuwa mabaya sana, aliweza kuongea kama kawaida japo chupa ya damu ilikuwa ikiendelea kuingia mwilini mwake.
“Kamanda! Siwezi tena,” alimwambia kamanda Amata kwa sauti ya chini kidogo, wakati huo Kamanda Amata alikuwa ameketi kwenye kiti jirani kabisa ya kitanda kile, “Kwa nini kaka? Tupo pamoja usijali,” Amata alijibu. “Sikia, nina hasira sana na Wambugu kama wewe ulivyo na hasira na Bill, nenda kamsake popote alipo, nitapona tu nikisikia kuwa umempata na umemtoa roho, nenda Kamanda kamalize kazi kabla hawajajua kuwa tuko pamoja,” Ndege alimueleza maneno hayo Amata. Wakapeana mikono, Kamanda Amata akatoka pale hospitali na mlangoni wakakutana na Yule polisi, “Vipi?” alimuuliza, lakini Yule polisi hakujibu kitu, nyuma yake kulikuwa na polisi wengine watatu, “Kamanda Amata, upo chini ya ulinzi kwa kuwa unaifanya kazi hii kinyume cha sheria,” Yule polisi mkubwa akasema hayo, “Nani aliyekwambia?” Kamanda Amata akauliza, “Tumepata taarifa kutoka makao makuu ya polisi Nairobi kwa uthibitisho kutoka katika ofisi yako huko Tanzania, twende kituoni,” Yule askari alimuamuru Kamanda. Kamanda Amata hakuwa na ubishi, alitii sheria bila shuruti, akapakiwa katika gari na kuondolea hospitalini hapo.
Wambugu alipoona hali si nzuri, polisi kila upande alijua kuwa sasa mambo yameharibika, alichomoka kutoka maficho yake na kutega barabara kuu kuona kama kuna gari litakalotokea. Mara akaona pikipiki ikija upande wa kulia kwake akaokota jiwe na kumpiga nalo Yule mwendesha pikipiki, kisha akajitokeza barabarani na kuokota ile pikipiki, akakaa juu yake na kuitia moto, akaondoka kwa kasi kubwa. Gari iliyokuwa imemchukua Kamanda Amata ilikuwa ikipita barabara hiyo na mara wakaiona ile pikipiki ikija kwa kasi sana, dereva akapunguza mwendo kuona ni nani huyo, “Msimamishe tafadhali,” Yule mkuu akamwambia polisi mwingine, ambaye kwa haraka aliruka chini na kutua barabarni kisha akasimama katikati ya barabar kumsimamisha jamaa huyo, lakini akiwa katika hali hiyo, mlio wa risasi ukasikika na mara Yule polisi akawa chali barabarani, Kamanda Amata akatzama huku na huku akishuhudia Yule dereva akishuka kumsaidia mwenzake, akaruka upande wa mbele kwa dereva na kuigeuza gari kwa fujo kuifuata ile pikipiki, mwendo uliokuwa ikiendeshwa hiyo land cruiser haikuwa ya kitoto, Kamanda Amata alikanyaga mafuta kwa ustadi wa hali ya juu, akaiona ile pikipiki ikikata kushoto na kuingia barabara nyingine nae alipofika pale vivyo hivyo akakunja kuelekea kushoto akiendelea kuifuata ile pikipiki.
§§§§§
Usiku wa manane, Madam S alipata taarifa ya kukamatwa kwa Kamanda Amata, taarifa zilitoka katika ofisi za ubalozi usiku huo, likaandaliwa gari kwa ajili ya kwenda Embu kutoka ubalozini kwa minajiri ya kumchukua Kamanda na kumrudisha Tanzania. Aliamka kwa kusuasua, na kujiandaa, alipokuwa tayari aliteremka kwa lifti mpaka chini ambako aliikuta gari hiyo ikimsubiri, akaketi kiti cha mbele na kuanza safari na watu wengine wawiliyaani dereva na Mashaka, Yule kijana waliekutana pale uwanja wa ndege.
Upande mwingine bwana Shikuku alishtushwa na taarifa za kijana wake Ndege kupigwa risasi na Wambugu pia kupata ajali ya moto uliosababishwa na mtu huyo huyo, moyo ulimchafuka na usiku huo akapanga safari yake ya kwenda Embu kujua nini kinaendelea. Akiwa njiani alikuwa akijaribu kuwasiliana na watu wa usalama upande huo kujua hali kwa ujumla ikoje, na kama ni chuki basi hakuna mtu aliyemchukia wakati huo kama Wambugu, aliapa moyoni lazima amtie nguvuni na atumikie kifungo chake kwa mateso makali.
Kwa ujumla usiku huo kila mtu alikuwa akiwaza yake juu ya Wambugu. Madam S alikuwa ametulia kitini haongei chochote, aliwaacha dereva na Mashaka waongee.
Haikuwachukua muda mrefu usiku huo, masaa mawili na nusu tu tayari walikuwa Embu na moja kwa moja walienda katika kituo kikuu cha polisi na kukutana na mkuu wa polisi wa kituo hicho. Madam S alijitambulisha kwao na kuonesha kitambulisho chake.
“Tunasikitika kuwa kijana wako ametoroka,” ilikuwa kauli ya mkuu Yule. Mashaka akamtazama Madam S ambaye alikuwa ameketi bila kuongea neno lolote, “Na isitoshe ametoroka na gari ya polisi,” akaongeza tena Yule mkuu wa polisi. Madam S alikuwa akitikisa kichwa tu kuashiria kuwa ameelewa anachoambiwa.
“Atarudi tu, msiwe na shaka,” madam S akajibu kwa kifupi, kisha akanyanyuka na kumuamuru dereva waelekee hospitali ya Agha Khan ili akamuone bwana Ndege aliyejeruhiwa katika sakata hilo. Alipofika tu pale hospitali alikutana na Bwana Shikuku, kila mmoja alimkumbuka mwenzie, waksalimiana kwa bashasha kwa kuwa ni miaka mingi hawajaonana. Baada ya hapo wote wawili wakaelekea ndani ya hospitali hiyo kumuona Ndege aliyekuwa amelala usingizi.
“Kwa nini usimrudishe Nairobi kwa matibabu?” Madam S akauliza.
“Amesema hatotoka hapa mpaka amuone Kamanda Amata,” Shikuku alijibu.
“Ok, wameivana hawa. Ulikuwa unajua kama AmaTa yuko hapa?” madam S aliuliza tena.
“Ndio kwanza nafahamu sasa kuwa yuko hapa siku nzote sikuwa najua,” Shikuku alidanganya, wakati Ndege alishamwambia kuwa kamanda Amata yupo Nairobi kwa shughuli hiyo ila si kiofisi.
Madam S alitulia kimya akitafakari jambo Fulani, alionekana wazi kukosa raha usiku huo, aliitazama saa yake ilikuwa tayari ni saa kumi alfajiri.
§§§§§
Kamanda Amata alikunja kona kali kuingia ile barabara ambayo ile pikipiki iliingia, alipoenda kama mwendo wa mita mia hivi hakuiona ile pikipiki wala dalili zake, akajua kwa vyovyote huyu jamaa atakuwa mitaa, akasimamisha gari na kushuka bastola yake mkononi, akawa anashangaa akitafuta huku na kule akizungukazunguka kwa hadhari kubwa sana, alipokuwa tayari kukata tama alisikia mnguruno wa pikipiki kwenye vichaka, akawahi na kuiona ikitokomea porini, akainu bastola yake na kufyatua risasi ya kwanza haikua na shabaha ila ya pili alipiga tairi na kulitoa upepo, ile pikipiki ikaanguka, na Wambugu akawa chini, Kamanda Amata akafika eneo lile na kumkuta Wambugu amekwishasimama na amejiandaa kwa mapigano, Kamanda Amata alitaka kufyatua risasi lakini akakuta zimemuishia, aliirusha ile bastola kumpiga nayo Wambugu, Wambugu aliruka hewani kama ninja na kuipiga tik tak ile bastola ikapotelea kwenye vichaka, wakati huo tayari Amata alifika pale kabla hajajiweka sawa, mguu wa nguvu ulimshukia Amata begani, akayumba upande na Wambugu akasimama kwa mguu mmoja kisha akaushusha ule mwingine taratibu kwa madaha, “Siku zote mnajua kuwa kila mtu ni bwege, kama ulikuwa hujui basi mimi ni Sempai,” Wambugu alijisifu huku akisimama katika pozi la kungfu, Kamanda Amata akaona hapo ndo penyewe, “Huwa sijibishani na wahalifu kabla sijawafundisha adabu,” Kamanda Amata alizungumza kwa gadhabu, akaruka hewani kiufundi na kuimshia mapigo makali Wambugu, lakini mapigo yote aliyapangua vizuri sana, kisha akaanza yeye kupeleka mashambulizi ya mikono kwa Kamanda Amata, ambaye naye alikuwa akiyapangua kiufundi sana mpaka Wambugu akamaliza mapigo yote, Kamanda Amata alipomuona sasa hana ujanja mwingine ndipo alipombadilishia staili kutoka kungfu kwenda kick boxing. Teke la kwanza lilitua mbavuni kabla hajakaa sawa lapili likatu shingoni kisha zikafuata ngumi mfululiozo kama ishirini na tano zilizomuacha Wambugu hoi akigalagala, “Nyanyuka juu Sempai, upambane na mwanaume wa shoka, hayo mapigo niliyokupa niliagizwa na Melchior Ndege sasa naanza ya kwangu,” Kamanda Amata alipomaliza maneno hayo, alijivuta kwa hatua ndefu amgfikie Wambugu, lo, Wambugu akamzidi ujanja, alijirusha kutoka pale alipolala akasimama kisha akajibinua na miguu yake yote miwili ikatua tumboni mwa Amata na kumfanya ateme damu, hasira za Amata zikawaka ghafla, aligeuka nyuma kwa kasi na kumchota ngwala Wambugu lakini jamaa akaruka na ule mguu ukapita chini kisha Wambugu akashusha pigo moja la karate lililotua sawia kwenya shingo ya Amata na kumpeleka chini mzima mzima. Kamanda Amata alitambaa kama motto, damu zikimvuja puani na mdomoni, akaona wazi asipofanya makeke anaweza akazimishwa na watu wasiione maiti yake.
“Ha ha ha ha Tanzania Secret Agency namba 1 ndio wewe!!? Unatambaa kama motto, nyanyuka upambane na jabali la chuma linalotisha kama kifo, Kenya yote wananijua na hapa kila goti linapigwa,” Wambugu akasema hayo kwa kujitamba akijipigapiga kifuani. Maneno hayo yalimuuma sana Amata, akanyanyuka kwa kasi na kugeuka akitazamana na Wambugu ambaye mkononi mwake alikuwa ameokota gongo, akaliinu na kumpiga nalo Kamanda lakini Kamanda akalidaka kwa mkono mmoja, akatazamana na macho mabaya ya Wambugu.
Taswira za mauaji ya kikatili ya kahaba Rose ikamjia na kumtia hasira, taswira ya Ndege akiungua moto ikamjia na kumuongezea hasira, kauli ya kushushwa cheo ikamaliza kila kitu akilini mwake.
Kamanda Amata akiwa kalishika lile gongo kwa mkono mmoja alinyanyua mguu wake na kulikanyaga kwa juu akalivunja kwa mtindo huo kisha akabaki na kipande, kwa hasira na visasi akamchoma nacho Wambugu tumboni, yowe la uchungu lilimtoka akaanguka chini, Amata akamuendea palepale alipo na kumvua kibegi chake kisha akakivaa yeye mgongoni, akamnyang’anya simu yake na kuitia mfukoni kisha akamkamata ukosi wa jacket lake na kumburuza mpaka kwenye kibarabara, akampigiza sura yake chini kwa nguvu, “Bill yuko wapi?” akamuuliza kabla hajajibu akampigiza tena kwa nguvu na kuvunja mfupa wa pua. “Sasa ukiniua ndio ntasema?” Wambugu alijibu kwa uchungu. “Nambie haraka, Bill yuko wapi?” Kamanda aliuliza kwa kelele maana hasira ilikuwa bado imetawala kichwa chake. Wambugu alinyanyua uso wake na kutema mabonge ya damu, “Kuna binadamu ambao hamtakiwi kuzaliwa kabisa, kama wewe na Bill, nakuuliza mara ya mwisho kabla sijakutenganisha na roho yako, Bill yuko wapi?” Kamanda aliendelea kuhoji, “Mi si si si sssjui,” Wambugu alijibu kwa tabu sana. Kamanda Amata akamburuza mpaka aliposimamisha gari na kumuinua akamsimamisha wima akimuegemezea katika bodi la gari. “Wambugu! Nakuua,” Amata alimwambia, “Niue braza, kwa maana ukiniacha hai nitateseka sana na mkono wa sheria,” Wambugu akajibu. “Niambie Bill yuko wapi?” akauliza tena, “Braza utanitesa utaniua lakini mimi sijui Bill yuko wapi alishatoroka hapa muda mrefu,” kamanda Amata alishikwa na hasira akampiga kichwa kimoja maridadi na kumuachia akianguka chini kama mzigo.
Mara taa za gari mbili zikawamulika kutoka barabara kuu, na zile gari zikaja mpaka pale, walikuwa ni polisi, wakateremka haraka na kumuweka Kamanda Amata chini ya ulinzi. Kamanda Amata akanyosha mikono juu, wale polisi wakaja na kumtia pingu, nyuma yao akaja mtu mnene kiasi aliyeonekana kuwa na sura ya kikatili isiyo na chembe ya huruma, akamuendea Kamanda Amata, akamtazama usoni, juu mpaka chini, “Hey, askari!” akaita, “Mfungue pingu Kamanda, mpe na begi lake,” wale askari wakafanya hivyo, kamanda Amata akapokea lile begin a kulitupia mgongoni. “Mzima au amekufa?” Yule bwana akamuuliza Kamanda. “Mzima huyo hawezi kufa kirahisi,” Amata akajibu. Yule bwana akatoa amri ya kupakiwa Wambugu garini kisha yeye na Kamanda Amata wakaingia katika gari ndogo ya polisi na kurudi mjini.
“Kamanda Amata, umetusaidia kazi moja ngumu sana ambayo jeshi la polisi la Kenya na vyombo vingine vya usalama imetusumbua kwa miaka takribani kumi kumpata huyu mtu, asante sana kijana” akamshukuru Kamanda na safari ikaendelea mpaka kituo cha polisi cha Embu.
Madam S na Mashaka walikuwa hapo kituoni pia wakimsubiri Kamanda Amata, walimuona alipokuwa akishuka katika ile gari na waziwazi alikuwa ameumia sana kwa jinsi alivyokuwa akitembea, wakakutana uso kwa uso na Amata, wakatazamana. “Madam, kijana wako huyo wapo, sisi hatuna deni nae!” alisema Yule bwana mwenye mwili mnene, kisha akapita kwenda ndani ya kituo hicho, ijapokuwa ilikuwa alfajiri lakini watu walijazana kutaka kuhakikisha kama kweli jambazi sugu Wambugu limekamatwa, jambazi lililowanyima usingizi Wakenya wengi kwa miaka mingi.
Kamanda Amata, Madam S na Mashaka waliingia kwenye gari yao na kuondopka eneo lile, moja kwa moja mpaka hospitali ya Agha Khan ili kwanza apate huduma ya kwanza. Ndani ya nusu saa alikuwa tayari amefanyiwa check up ya nguvu na kutibiwa palipohusika, Mashaka akamuendea Amata katika chumba alichokuwapo kisha akamkabidhi begi jeusi mpano wa briefcase, alkipofungua ndani akakuta suti mpya, saa ya kisasa kwa kazi yake na bastola ndogo.
“Umerudi katika hali yako Kamanda,” Madam S alimwambia walipokutana mara tu Kamanda alipotoka kule ndani, “Yeah, lakini bado kitu kimoja,” kamanda alisema, “Nini?”
“Nataka kumuona Ndege,” akajibu. Wote watatu wakaingia wodini alikolazwa Ndege na kumkuta tayari amewekwa katika kitanda cha magurudumu, amefungwa mikanda sawia na chupa ya majiiliyowekwa baada ya ile ya damu ikiendelea kwenda, “Melchior Ndege,” Kamanda alimwita huku akwa amemuinamia pale kitandani, “Amekufa au amekimbia?” Ndege aliuliza kwa shauku, “Hali yake ilivyo hawezi kuiona jioni, yuko katika mikono ya polisi,” Amata alimwambia Ndege ambaye alionekana wazi kuifurahia habari hiyo. “Asante Kamanda,” Ndege alishukuru, “Asante na wewe” Kamanda akamalizia.
§§§§§
Kama kuna habari iliyomfurahisha Sargeant Maria, basi ni hii ya kupatikana kwa Wambugu, kwa sababu baada ya kumbana sana Mellina kwa kipigo na mateso makali alitaja washirika wote akiwamo Wambugu. Sargeant Maria na wenzake waliishiwa nguvu kusikia kuwa Wambugu anahusika na mauaji ya Kasisi, swali lilikuwa, tutampataje? Lakini ghafla alfajiri hiyo wanaambiwa kuwa Wambugu kapatikana huko Embu karibu na msitu wa Njukiri baada ya vyombo vya usalama kupambana nae vilivyo, baada ya kutaka kujua zaidi ndipo Sargeant Maria aliposikia juu ya Kamanda Amata ambaye yeye siku zote alijua ni mtu wa kwenye riwaya tu, hakujua kuwa ni burudani ya waandishi kuandika visa vyake kila amalizapo kimoja na kuanza kingine. Ulikuwa ni ushindi mkubwa, mkubwa sana, Maria alijiuliza, Mellina tumemkamata, Cheetah, kauawa, Wambui kauawa, Wambugu ndio huyu hapa, sasa ile Mostrance ambayo ndicho chanzi cha kazi nzima haijapatikana, bado kuna kazi mbele.
ITAENDELEA....