RIWAYA:MIFUPA 206
MTUNZI:KELVIN e MPONDA
0688058669
3
WAKATI NIKILITOA GARI LANGU kwenye maegesho chini ya jengo
lile la ghorofa ilipokuwa ofisi yangu wazo la kuwa ni wapi nilipaswa
kuelekea likazichukua fikra zangu hivyo nikaipa akili yangu utulivu. Utulivu
ulipokuja jina la msichana mrembo aitwaye Milla likachukua nafasi na hapo hisia
zangu zikaniambia kuwa sikuwa na sehemu nyingine ya kuendeleza upelelezi wangu
isipokuwa kwa kumtafuta msichana yule aliyekuwa na yule mwanaume kwenye ile
nyumba jana usiku ambaye hapo awali nilimdhania kuwa alikuwa dalali wa nyumba
ya Gabbi Masebo.
Nilijikuta nikilikumbuka jina la msichana yule aitwaye Milla baada ya kumsikia yule
mwanaume akimuita wakati ule tulipokuwa tukipambana kwenye ile nyumba. Milla
alikuwa msichana mzuri sana miongoni mwa wasichana wazuri niliowahi kuwaona
jijini Dar es Salaam. Uzuri wa asili ambao mama yeyote angeweza kujivunia kuwa
na binti mrembo kama yule lakini kulikuwa na kasoro moja tu kwa msichana yule.
Kasoro ambayo pindi nilipoyakumbuka macho yake wakati tulipotazamana usiku
ule wa jana yaliacha ujumbe moyoni mwangu. Milla alifaa kufananishwa au kuitwa
changudoa au kahaba professional wa jiji la Dar es Salaam. Uso wake haukuwa na haya
hata kidogo kama walivyo wasichana wa umri wake wakati macho yangu yalipokuwa
yakiteseka na muonekano wa umbo lake la kipekee katika sayari hii. Hatimaye hisia
zangu zikaniambia kuwa isingekuwa vigumu kumtafuta Milla katika jiji la Dar es
Salaam. Swali likabaki je ni wapi ambapo ningempata?,kwa kweli sikufahamu.
Maeneo yanayotumiwa na wanawake makahaba wa jiji la Dar es Salaam katika
kuuza miili yao ili kujiingizia vipato vya kuendeshea maisha ama ajira binafsi kama
wenyewe wanavyosema yamegawanyika katika sehemu kuu tatu kwa kutegemeana
na aina za vipato vya wateja wao na hali za afya za wachuuzi wa biashara hiyo.Wale
makahaba ambao huuza miili yao kwa bei ya chini hufanya biashara hiyo katika maeneo yenye wateja wenye hali dhaifu za kiuchumi kama maeneo ya Uwanja wa FisiManzese,Chama,Mabibo mwisho,Buguruni hususani kwenye baa maarufu ya Kimboka by
Night,Keko Machungwa,Mwananyamala Hospitali,Kigamboni Sokoni na kwengineko.
Makahaba ambao huuza miili yao kwa wateja wa kipato cha kati hufanya
biashara yao katika maeneo ya Afrika Sana,Maisha Club eneo la Msasani,Barabara ya
Morocco kuelekea Posta kituo cha Mbuyuni,Club Billicanas,Sansiro Club eneo la Sinza na
kwengineko.
Wale makahaba ambao huuza miili yao kwa wanaume wenye vipato vya juu zaidi
maeneo yao ya biashara huwa ni katika hoteli kubwa za jiji la Dar es Salaam ingawa
wakati mwingine hufanya biashara hiyo bila wamiliki wa hoteli hizo kufahamu kile
kinachoendelea.
Zile hoteli zenye hadhi ya nyota tatu,nne,tano na kundelea kama Sunrise Beach
Resort iliyopo Kigamboni Dar es Salaam. ShaMool Hotel ya Sinza,Tanzania Executive
Suites ya mtaa wa Mali. Blue Pearl Hotel and Apartments – Ubongo Plaza,Kunduchi Beach
Hotel and Resort,Peacook Hotels -barabara ya Bibi Titi Mohamed,New African Hotel –mtaa
wa Azikiwe. Sea Cliff Hotel – Toure Drive. Msaki Peninsula,Dar es salaam Serena Hotel
mtaa wa Ohio,Mikadi Beach Lodge. Marble Arch Hotel ya Mikocheni B na nyinginezo
nyingi. Vilevile makahaba hao hufanya biashara zao kwenye kwenye casino kubwa
kama Kilimanjaro Casino iliyopo mtaa wa Azikiwe,Le Grande Casino eneo la Samora
Evenue. New Africa Casino mtaa wa Azikiwe,Las Vegas Casino barabara ya Ali Hassan
Mwinyi,Princes Casino Tanzania na casino nyinginezo zilizokuwa zikifunguliwa kila
kukicha jijini Dar es Salaam.
Lakini kwa mtu yeyote aliyemfahamu msichana Milla angekubaliana na mimi
kuwa msichana mzuri namna ile asingekubali kuuza mwili wake kwa watu wenye
vipato vya chini au kati. Hivyo sehemu pekee ya kumpata Milla bado ingekuwa ni
kwenye hoteli za hadhi ya juu na kwenye casino za jiji la Dar es Salaam.
_____
NILIUACHA MTAA WA KISUTU ilipokuwa ofisi yangu na nilipofika mbele
kidogo upande wa kulia nikaingia mtaa wa Mrima. Barabara ya mtaa ule ikanichukua
hadi barabara ya mtaa wa Jamhuri lakini kabla ya kufika mwisho wa barabara ile
nikachepuka upande wa kulia nikiifuata barabara ya mtaa wa Mkwepu ambayo
mwisho wake ingenikutanisha na ile barabara ya Samora Avenue.
Nilipofikia kwenye barabara ile nikachepuka na kuingia barabara ya upande wa
kushoto. Sasa nikawa nikiendelea na safari yangu kwenye ile barabara ya Samora
Avenue huku nyuma yangu nikiiacha barabara ya Morogoro. Niliendelea na safari
yangu na nilipofika mbele nikaingia barabara ya upande wa kulia na baada ya kuupita
mzunguko wa barabara wa Askari Monument mbele kidogo nikaegesha gari langu nje
ya New Africa Hotel.
Kulikuwa na watu wachache ndani ya ukumbi wa hoteli ile na kama zilivyokuwa
hoteli nyingi za kisasa zenye hadhi ya juu utulivu ulizingatiwa mle ndani. Wakati nikiingia mle ukumbini wahudumu wa ile hoteli walinipokea kwa nyuso za kirafiki
na tukio lile likanifurahisha. Mara tu nilipoingia mle ndani nikaelekea moja kwa moja
eneo la mapokezi ambapo nilimkuta kijana mhudumu wa eneo lile akiwa amevaa sare
zake za kazi.
“Karibu kaka” kijana yule alinikaribisha huku akinitazama kwa shauku.
“Babari za kazi?”
“Nzuri” kijana yule akanikaribisha huku akinitazama kwa udadisi na bila ya
kuchelewa nikatoa kitambulisho changu cha kazi na kukiweka juu ya dawati la
mapokezi karibu na yule kijana. Yule kijana akakichukua kile kitambulisho na
kukitazama kisha akakirudisha pale juu mezani na kunitazama kama anayefikiri jambo
na kabla hajasema neno nikavunja ukimya.
“Namuulizia msichana anayeitwa Milla” yule kijana akanitazama kwa udadisi kisha
akatikisha kichwa akionesha kutomfahamu.
“Simfahamu!” hatimaye akaongea kwa utulivu.
“Hujawahi kumsikia msichana yeyote mwenye jina la Milla hapa hotelini?”
nilimuuliza yule huku nikitaka kuyatathmini maelezo yale.
“Unadhani kazi yangu hapa ni kukariri nyuso za watu?” yule kijana aliongea kwa
dharau huku kionesha kuchoshwa na maswali yangu.
Sikupenda yule kijana anidharau hivyo nikakishika kidole chake kimoja cha
mkononi kisha nikakipinda kwa nyuma hadi pale sauti ya mvunjiko iliposikika na
hapo yule kijana akapiga yote la kistarabu akikwepa kuwashtua wageni waliokuwa pale
ukumbini. Jasho likamtoka huku akihema ovyo.
“Pumbavu! wakati mwingine ujifunze kuongea vizuri na wateja!” nilifoka kwa hasira
na kumuacha yule kijana pale mapokezi akigugumia kwa maumivu. Nikachukua
kitambulisho changu pale juu ya meza na kuelekea nje huku nikiwa nimeanza kukata
tamaa.
_____
NILIKUWA NIKIFAHAMU WAPI ILIPOKUWA Kilimanjaro Casino hivyo
mara baada ya kutoka pale New Afrika Hotel niliingia kwenye gari langu na kuanza
safari nikawa kama ninayeifuata barabara ya Kivukoni lakini kabla ya kuifikia barabara
ile nikakunja kona nikiingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Sokoine Drive.
Niliendesha gari langu nikilipita jengo la Hyatt Regency kwa upande wa kulia halafu
mbele kidogo nikaingia upande wa kulia nikiifuata barabara ya Mirambo. Niliendelea
na safari yangu nikiipita barabara ya mtaa wa Madaraka upande wa kushoto na
nilipoipita tu barabara ile mbele kidogo upande wa kulia nikaenda na kuegesha gari
kwenye maegesho ya magari ya Kilimanjaro Casino.
Kulikuwa na magari machache yaliyoegeshwa mbele ya jengo la Kilimanjaro Casino
hivyo haikuniwa vigumu kutafuta maegesho ya gari langu eneo lile kisha nikashuka
na kuelekea kwenye mlango wa mbele wa kuingilia wa Casino ile. Kulikuwa na mlinzi
ambaye alinisimamisha mlangoni hata hivyo baada ya mazungumzo ya kifupi na kumuonesha kitambulisho changu akaniruhusu kuingia mle ndani.
Nilipoingia mle ndani mandhari ya casino ile yakanieleza kuwa ile haikuwa casino
ya kubabaisha kwani mle ndani kulikuwa na vitu vyote muhimu kama sehemu ya
mazoezi ya viungo ama Fitness center,Pool,Shopping galler,mashine za kisasa za kuchezea
kamari,casino na mazingira ya kisasa ya kuvutia. Niliyatembeza macho yangu na sura
nyingi nilizoziona mle ndani zilikuwa ni za kutoka nje ya bara la Afrika. Hatimaye
nikaelekea eneo la mapokezi ambapo niliwakuta wasichana wawili warembo waliovaa
sare za kazi. Uzuri wao ukanifanya nijisikie faraja kuwakaribia.
“Poleni na kazi warembo,” niliwasalimia wasichana wale.
“Ahsante! kaka karibu”
“Nishakaribia”
“Naomba nikusikilize kaka” mmoja wa wale wasichana akawahi kuniuliza.
“Nimuulizia msichana anayeitwa Milla”
“Anaitwa Milla?...” yule mwenzake akadakia na kuniuliza huku akinitazama kwa
shauku.
“Ndiyo! anaitwa Milla na aliniambia kuwa ningempata hapa kwa jina hilo”
niliwaambia wale wasichana na hapo wakageuka na kunitazama kwa mshangao
kidogo na tukio lile likapeleka ujumbe fulani kichwani mwangu.
“Kahaba professional wa jiji la Dar es Salaam,Miriam Cash au ukipenda muite Milla
Cash,ndiye huyo unayemuulizia?” yule dada akaniuliza kwa hakika na hapo tumaini
likaanza kuchipua moyoni mwangu.
“Vipi kaka na wewe umelizwa nini?” mwenzake akadakia akiniuliza kwa kicheko
hafifu.
“Hapana!,nina miadi naye tu” niliongea kwa utulivu kisha nikageuka kuwatazama
tena wale wasichana kwa udadisi.
“Mbona kila mwanaume anamuulizia Milla Cash kwani ana ziada gani jamani?”
mwenzake akaongea huku akiibetua midomo yake.
“Wanaume gani tena mbona mnataka kunitia wivu!” nikaongea huku nikitabasamu.
“Sasa wewe unadhani uko peke yako?” mwenzake akadakia huku akicheka.
“Mimi mbona kaniambia niko peke yangu!” niliwaambia wale wasichana na hapo
wakaanza kucheka kiasi cha kuwashitua baadhi ya watu waliokuwa karibu na eneo lile.
“Pole sana kaka”
“Nishapoa” niliitikia huku nikiangua kicheko hafifu cha kuwazuga wale wasichana
wahudumu.
“Vipi nimemkuta?” hatimaye nikawauliza huku tabasamu langu likiziroga hisia
zao.
“Poleni sana kwa kudanganywa”
“Tumedanganywa! mimi na nani?” nikawauliza wale wasichana kwa shauku.
“Mwenzako aliyeondoka hapa muda mfupi uliyopita” yule msichana aliyewahi
kuniongelesha wakati nikiingia akaongea kwa hakika huku akinionea huruma.
“Milla Cash kwa sasa hayupo hapa"
“Nitampata wapi?” nikauliza huku nikionesha kukata tamaa
“Kwa kweli hakuna anayemfahamu mahali alipo ingawa wakati mwingine inaweza
kutokea bahati tu ukamuona hapa”
“Mnaweza kunisaidia namba zake zake za simu?”
“Kaka mbona unakuwa mshamba wa mambo?,kahaba tangu lini akatumia namba
moja ya simu. Biashara ikimalizika line ya simu inakunjwa na kutupwa chooni. Hakuna
kuwekeana inzi na ukitana tena huduma yake anakuelekeza wapi pa kumpata na
ikitokea umechelewa kufika usimlaumu kwani mwenzako hana muda wa kupoteza”
yule msichana aliendelea kunieleza na mimi sikuwa na budi kumsikiliza.
“Na huyo mwenzangu aliyefika hapa ni nani?”
“Mwanaume kama wewe”
“Yupoje?”
“Mwembamba na mrefu amevaa suti nyeusi nadhifu,shati la kijivu na tai ya rangi
ya damu ya mzee”
“Handsome kama wewe” mwenzake akadakia huku akiangua kicheko hafifu cha
kibiashara na hapo nikafanya fadhila kidogo kwa kutabasamu huku nikianza kuhisi
kuwa juhudi zangu zilikuwa mbioni kugonga mwamba.
Niliitazama saa yangu na hapo nikaona kuwa nilikuwa nikipoteza muda wangu
hivyo hatimaye nikawaaga wale wasichana na kuondoka huku nikiwashukuru kwa
ushirikiano wao.
Kuzunguka kwenye hoteli zote na casino za jiji la Dar es Salaam ingekuwa kazi
ngumu sana ambayo pia sikuwa na hakika sana na majibu yake. Hivyo nikaanza
kufikiria namna ya kuchagua sehemu za kwenda kasha nikapanga kuwa endapo
nisingefanikiwa kumpata Milla Cash kwenye maeneo hayo basi ningeamua namna
nyingine ya kufanya.
Mara baada ya kutoka nje ya Kilimanjaro Casino niliingia kwenye gari langu na
kuyaacha maegesho yale nikirudi na ile barabara ya mtaa wa Mirambo. Nilipofika
mbele kwenye makutano ya barabara nikaingia upande wa kulia nikiifuata barabara
ya Sokoine Drive. Niliendesha gari langu kwa utulivu hadi nilipoyafikia makutano ya
barabara ya Sokoine Drive na ile ya barabara ya mtaa wa Shaaban Robert.
Nikayapita makutano yale na kuendelea na safari yangu nikiifuata barabara ya
Sokoine Drive hadi pale nilipokutana na makutano mengine ya barabara na hapo
nikakunja kona upande wa kushoto nikiifuata barabara ya Luthuli. Mbele kidogo
upande wa kushoto nikaicha barabara ya Sokoine Drive kasha na ile barabara ya Samora
Avenue. Nilipoyafikia makutano ya barabara ya Luthuli na ile ya Garden Avenue nikaingia
upande wa kulia nikiifuata barabara ya mtaa wa Chimara. Nilipofika mwisho wa ile
barabara ya mtaa wa Chimara nikaingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya
Barack Obama Drive na upande wa kulia kwangu nikawa nikipepewa upepo mwanana
wa bahari ya Hindi.
Niliyatazama mandhari ya bahari ya Hindi huku nikiendelea kufarijika na upepo
wa bahari hiyo na wakati nikiendelea na safari fikra zangu zikaanza kutumbukia kwenye mjadala mwingine. Niliyakumbuka maelezo ya wasichana wale wafanyakazi
wa Kilimanjaro Casino wakati nilipokuwa nikumuuliza Milla Cash juu ya mwanaume
mwingine aliyefika pale Casino kumuulizia Milla Cash. Kwa kweli Sikufahamu hasa
ni kitu gani kilichonipelekea kuanza kuunda hoja juu ya mtu yule lakini hisia fulani
zilikuwa zikinivuta kutaka kumfahamu mwanaume huyo mwembamba na mrefu
aliyevaa suti nadhifu nyeusi,shati la kijivu na tai ya rangi ya damu ya mzee Handsome
kama mimi. Mojawapo ya tabia ninazozipenda ni kuvutiwa na watu wapya wanaoingia
katikati ya harakati zangu.
Mawazo yangu yaliporudi mle ndani ya gari nilikuwa tayari nimekwishafika
makutano ya barabara ya Sea View,Barack Obama Drive na barabara ya Ufukoni.
Nilipofika kwenye makutano yale nikakunja kona kuingia upande wa kushoto
nikiifuata barabara ya Ufukoni.
Jua kali lilikuwa likiwaka pamoja na kuwa nilikuwa bado nipo kwenye eneo la
mwambao wa bahari lakini niliweza kuhisi hali ya joto kali la jiji la Dar es Salaam.
Hakukuwa na foleni kubwa kwenye barabara ile hivyo sikupata usumbufu mkubwa
katika kuzifikia sehemu nilizozihitaji.
Nyumba za kifahari,hoteli zenye hadhi ya juu na supermarket za kisasa,mandhari
yale yakanifanya kwa muda kidogo nijisahau kuwa nilikuwa kwenye jiji la Dar es
Salaam.
Niliyafikia makutano ya barabara ya Ufukoni na ile barabara ya Ali Hassan Mwinyi
hapo nikaingia ile barabara ya Ali Hassan Mwinyi halafu mbele kidogo nikaingia
upande wa kushoto ilipokuwa Las Vegas Casino. Hii ilikuwa ni Casino ya tatu kuifikia
tangu asubuhi kulipopambuzuka nikimtafuta Milla Cash.
Nilitafuta maegesho mazuri nje ya Las Vegas Casino kisha nikaegesha gari langu.
Kulikuwa na magari machache yaliyokuwa kwenye eneo lile la maegesho hivyo kwa
vyovyote gari langu lingekuwa rahisi kuonwa wakati nilipokuwa nikitafuta maegesho
eneo lile lakini hali ile haikunipa changamoto yoyote.
Kabla ya kushuka kwenye gari nilitulia kidogo nikitathmini mazingira ya nje ya
casino ile na hapo nikashtushwa na aina ya uwekezaji ule. Ilikuwa casino ya kisasa
na yenye vionjo vya hadhi ya juu vya kimatifa kama eneo kubwa la maegesho na
mazingira mazuri ya bustani ya kuvutia.
Niliwachunguza walinzi wa casino ile na kuridhishwa na utendaji wao. Wote
walikuwa wamevaa sare maalum za kazi na silaha zao mikononi. Baada ya kuyazoea
vizuri mazingira yale na kuilewa mienendo ya wenyeji wa eneo lile nilifungua mlango wa
gari na kushuka nikielekea mlango wa mbele wa ile casino. Wakati nikitembea kuelekea
kwenye ule mlango wa mbele ya kuingilia kwenye ile casino wafanyakazi wachache wa
nje ya casino ile waliacha shughuli zao kwa muda wakinitazama. Tukio lile halikunipa
shida kwani niliendelea kuzitupa hatua zangu makini nikiyapuuza macho yao.
Wakati nikiusukuma mlango wa kioo wa casino ile ili niingie mle ndani
nikashtushwa na mlio wa alamu iliyoanza kupiga kelele na hapo nikakumbuka kuwa
nilikuwa nimeingia na bastola yangu mle ndani. Kabla sijaamua nini cha kufanya mara mwanaume mrefu mwenye mwili uliojengeka vizuri kwa mazoezi huku akiwa
amenyoa upara katika sare zake za kazi akaja na kusimama mbele yangu akinizuia
nisiingie mle ndani.
“Toa vitu vyako vyote vya chuma ulivyonavyo na uviweke pale” yule mtu aliniambia
huku akizifuatilia nyendo zangu kwa makini. Sikutaka kuanzisha purukushani za
namna yoyote hivyo niliingiza mkono kwenye koti langu kuichukua bastola yangu
kisha nikaiweka kwenye kibeseni maalum cha wavu kilichokuwa pembeni ya meza ya
mapokezi kwenye mashine ya Metal ditector.
“Sheria ya humu ndani hairuhusu mtu yeyote kuingia na silaha ndugu, mbona
unataka kuleta ukorofi usiyo na maana?” yule mtu akaniambia kwa kufoka.
“Samahani ndugu yangu nilipitiwa kidogo” nikamwambia yule huku nikiyatembeza
macho yangu mle ndani.
“Naomba kitambulisho chako!” yule mtu akaniuliza na hapo nikajua kuwa alihitaji
kitambulisho cha uanachama wa ile casino. Hata hivyo nikajidai kuwa sijamuelewa
vizuri na badala yake nikaingiza mkono mfukoni na kutoa kitambulisho changu
batili cha kazi. Yule mtu akakipokea kile kitambulisho na kuanza kusoma maelezo
yaliyokuwa kwenye kitambulisho kile. Alipomaliza kuyasoma yale maelezo akageuka
na kunitazama kwa udadisi zaidi.
“Wewe ni kachero?” akaniuliza kwa utulivu.
“Ndiyo! lakini hilo siyo lililonileta hapa” nilimjibu.
“Sasa ni kipi kilichokuleta hapa?” yule mtu akaniuliza.
“Umewauliza swali hili wateja wote walioingia humu ndani?” nilimuuliza yule mtu
huku hali ya uvumilivu ikianza kuyeyuka nafsini mwangu. Kabla yule mtu hajanijibu
mara simu yake ikaanza kuita na hapo akaitoa simu yake kutoka mfukoni na kuipokea
huku macho yake yakiwa kwangu. Wakati yule mtu akiongea na simu mimi nikautumia
tena ule muda kuyapeleleza maeneo ya mle ndani kwa macho. Mara nikaiona kamera
moja ya CCTV iliyokuwa imetegwa juu ya ule mlango mkubwa wa kuingilia. Kuiona
ile kamera nikajua kuwa tulikua tukitazamwa kupitia kamera ile.
Wakati nikiendelea kutafakari mara yule mtu mbele yangu akakata simu kisha
akageuka kunitazama.
“Pole sana ndugu yangu” yule mtu akaniambia huku akitabasamu.
“Pole ya nini?”
“Uongozi wa casino haupendi wateja wa aina yako. Chukua bastola yako na urudi
ulipotoka” yule mtu akaniambia kwa dharau. Nikaduwaa kidogo nikimtazama kama
ambaye sikumsikia vizuri kisha nikaichukua bastoa yangu na kuishindilia mafichoni
huku nikihisi jaribio langu jingine kukwaa kisiki.
“Kazi njema” nilimuaga yule mtu.
“Jaribu polisi mesi Oysterbay watakukubali” yule mtu akaniambia kwa kejeli huku
akiangua kicheko hafifu. Sikuweza kuvumila hivyo nikageuka kwa kasi ambayo
hakuitarajia kisha nikakishika kichwa chake na kukigongesha kwa nguvu kwenye ile
meza ya mapokezi. Mwamba wa pua yake ukapasuka na hapo akapiga yowe kali la maumivu huku damu ikianza kumtoka puani. Bila kuongea neno lolote nikajitengeneza
vizuri na kuelekea nje ya casino ile nikiwa nimeishapandwa na ghadhabu. Nilipofika
eneo lile la maegesho nikaingia kwenye gari langu na kuondoka.
_____
SIMU ILIPOANZA KUITA Fred Bagunda alisitisha shughuli aliyokuwa
akiifanya na kuitazama simu ile. Wakati alipokuwa akijiandaa kuipokea simu ile mara
ikakata na hali ile ikampelekea aitelekeze pembeni na kuendelea na shughuli zake.
Hata hivyo kabla hajafika mbali ile simu ikaanza kuita tena na hapo akaichukua kwa
haraka na kubonyeza kitufe cha kupokelea huku tayari simu hiyo ikiwa sambamba na
sikio na mdomo wake.
“Haloo Njama…!” Fred Bagunda akawahi kuita huku akiisikiliza sauti ya upande
wa pili kwenye simu.
“Vipi bado upo ofisini?”
“Nipo ofisini Njama nipe ripoti!”
“Kazi nzuri”
“Safi sana,imekuwaje?”
“Nahisi tayari nimefanikiwa”
“Umempata huyo msichana?”
“Msichana aliyekuwa na Alba Gaumo jana usiku ni Milla Cash” Njama aliongea
kwa utulivu upande wa pili wa simu.
Maelezo ya Idris Njama yakampelekea Fred Bagunda aupishe kidogo ukimya
huku akitafakari kisha akauliza.
“Sasa hivi po wapi?”
“Barabara ya mtaa wa Kibasila naelekea ilipo Vampire Casino kuonana na Milla
Cash”
“Nilikuwa nikifikiri kitu kama hicho kuwa Alba Gaumo alikuwa na Milla Cash”
“Nimeanza kupata wasiwasi” Njama akaongea kwa utulivu.
“Wasiwasi gani?”
“Mtu aliyemshambulia Alba Gaumo huenda alikuwa akichunguza jambo fulani”
“Kwa nini unafikiri hivyo?”
“Kama Alba Gaumo angekuwa amehisi hatari yoyote hapo kabla angeniambia”
maelezo ya Njama yakapelekea kitambo kifupi cha ukimya huku kila mmoja akitafakari
kisha Fred Bagunda akavunja tena ukimya.
“Okay! mtafute huyo Milla Cash akueleze huyo mtu aliyemvamia Alba Gaumo ni
nani na alikuwa na shida gani halafu baada ya hapo tutajua nini cha kufanya”
“Bila shaka!”
“Okay! kazi njema”
_____
NILIKUWA NA HISIA KUWA sikuwa nimepiga hatua yoyote katika harakati zangu. Katika casino zote nilizozifikia kumtafuta Milla Cash nilikuwa nimeambulia
majibu mabovu yaliyoishilia kunipandisha hasira na sasa njaa ilikuwa imeanza kuniuma
huku kwa mbali nikisikia mikaromo hafifu tumboni.
Mara baada ya kutoka Las Vegas Casino nilikuwa nimeamua kuelekea kwanza
ofisini kwangu huku nikiwa na hisia kuwa nikiwa huko huenda ningepata wazo jipya
la kubadilisha mfumo wa harakati zangu. Hivyo nilivuka ile barabara ya Ali Hassan
Mwinyi nikaingia barbara ya Nkomo. Nilipofika mwisho wa barabara ya Nkomo
nikakutana na barabara ya Aly Khan ambapo niliifuata barabara ile kwa upande wa
kulia,safari iliyonichukua dakika chache kabla ya kuifikia barabara ya Malik iliyokuwa
upande kushoto.
Nilikuwa nimeazimia kurudi ofisini kwangu Kisutu na wakati huu sikupenda kurudi
na ile njia ya awali hivyo ile barabara ya Malik ingekuja kuniunganisha na ile barabara
ya United Nations ambayo baadaye ingeniunganisha na ile barabara ya Morogoro na
kutoka hapo ikawa rahisikufika eneo la Kisutu ilipo ofisi yangu. Niliendelea na safari
yangu nikaipita barabara ya mtaa wa Magore na nilipofika mbele nikaingia upande wa
kushoto nikiifuata barabara ya United Nations. Nikiwa kwenye barabara ile wazo la
kupata mlo likanijia baada ya kuuona mgahawa
Niliendelea na safari yangu nikapita barabara ya mtaa wa Magore na nilipofika
mbele nikaingia upande wa kushoto nikiifuata barabara ya United Nations. Nikiwa
kwenye barabara ile wazo la kupata mlo likanijia akilini baada ya kuuona mgahawa wa
kisasa kando ya barabara ile. Hivyo nikakunja kona upande wa kushoto nikiuendea
mgahawa ule na wakati nikifanya vile ikawa kama bahati mara nikakiona kibao cha
barabarani kinachoelekeza eneo ilipokuwa Vampire Casino.
Nilikitazama kibao kile cha barabarani kama niliyekiona kibao kinachoelekeza eneo
lililonitoka siku nyingi katika fikra zangu. Nilijaribu kuvuta kumbukumbu kichwani
mwangu hata hivyo jina la Vampire Casino lilishindwa kujisajili upya kichwani mwangu
na hapo nikahisi huenda casino ile ilikuwa mpya masikioni mwangu. Hata hivyo kwa
kuwa casino ile haikuwa mbali na pale nilipokuwa sikuona sababu ya kuiipuuza.
Nilimaliza kupata mlo wangu katika mgahawa ule uliyopo kandokando ya barabara
ya United Nations na hapo nikaingia kwenye gari na kuufuata ule uelekeo wa kile kibao
cha barabarani kinachoelekeza mahali ilipokuwa Vampire Casino. Nilikuwa nimepoteza
muda mwingi katika mgahawa ule nikisubiri usiku uingie ili niweze kufanya upelelezi
wangu kwa uhuru zaidi.
Niliifuata barabara ile iliyoelekezwa na kile kibao cha barabarani na hapo nikawa
nikipita katikati ya majengo marefu ya ghorofa na nyumba za watu walioridhika na
hali zao za miasha. Ilikuwa barabara tulivu isiyokuwa na watu wala msongamano wa
magari. Niliitazama saa yangu ya mkononi na hapo nikagundua kuwa dakika chache
zilikuwa zimesalia kabla ya kutimia saa tatu usiku. Muda wa kuanza harakati zangu.
Magari machache yalinipita wakati nikiendelea na safari lakini macho yangu
yalikuwa makini kutazama kiashiria chochote cha sehemu ilipokuwa Vampire Casino.
Hatimaye nikaiona casino ile upande wa kulia kwangu ikitazamana na ofisi za kampuni moja ya utalii na hapo tabasamu jepesi likanawiri usoni mwangu.
Mwekezaji wa Vampire Casino bila shaka alikuwa amefanya utafiti mzuri wa
masoko kabla ya kuanzisha casino ile kwani siyo tu Vampire Casino ilikuwa ipo kwenye
sehemu nzuri lakini vilevile ilikuwa kwenye eneo tulivu la biashara.
Nililitazama bango kubwa linalowaka taa za rangi tofauti za kuvutia lililokuwa na
maandishi makubwa ya neno Vampire Casino chini yake kukiwa na maandishi madogo
Our world in Dar es Salaam lililokuwa nje ya jengo lile na hapo nikaridhika kuwa sikuwa
nimepotea njia.
Idadi kubwa ya magari ya kifahari yaliyoegeshwa nje casino ile ilitosha kunieleza
kuwa Vampire Casino haikuwa casino tu ila casino ya kimataifa yenye kila aina ya starehe
za dunia hii.
Nilijisikia mfadhaiko wakati nilipokuwa nikiegesha gari langu Peugeot 504 kando ya
gari la kifahari BMW V6 nyeusi upande wangu wa kulia lakini nilipoangalia upande
wa kushoto kwangu na kuiona gari ndogo aina ya Corolla Limited nyeupe nikafurahi
kuwa mwenye gari la kichovu sikuwa peke yangu. Wakati huu sikuwa mwepesi wa
kushuka kwenye gari kwani nilihitaji kwanza kuyazoe mandhari yale ile nijue wapi
pa kuanzia. Hivyo niliziacha dakika kadhaa zikiteketea taratibu huku macho yangu
yakifanya utafiti.
Kulikuwa na magari mawili yaliyoingia na kuegeshwa katika eneo la maegesho
la Vampire Casino. Tayota Avalon nyeusi na Nissan Altima ya rangi ya kijivu. Magari
hayo yaliongozana wakati yakiingia na kwenda kusimama kwenye maegesho kisha
wakashuka wanaume wanne waliovaa suti nadhifu nyeusi na kuelekea kwenye ule
mlango wa casino na hapo nikawaona wakionesha vitambulisho vyao pale mlangoni
ambapo waliruhusiwa kuingia mle ndani na walinzi wawili waliokuwa pale mlangoni.
Tukio lile likanifanya nikumbuke kuwa sikuwa na kitambulisho cha mwanachama wa
casino ile hivyo suala la kuingia mle ndani bado lingekuwa kitendawili.
Nilichukua sigara moja kutoka kwenye pakiti iliyokuwa mfukoni na nilipoiweka
mdomoni nikajiwashia na kuivuta taratibu huku nikiipa akili yangu utulivu. Niliiacha
sigara ile ikiteketea taratibu mdomoni huku nikifikiria nini cha kufanya. Nikiwa katika
hali ile mara ghafla macho yangu yakajikuta yakivutiwa na gari lingine lililokuwa
likiingia eneo lile. Nililitazama gari lile na kushtuka sana. Nimewahi kutembelea miji
mingi mikubwa barani Afrika lakini sikumbuki kama niliwahi kuliona gari la namna ile.
Lilikuwa gari refu na jeusi aina ya Van. Niligeuka vizuri na kulitazama gari lile na hapo
nikagundua kuwa lilikuwa ni gari aina ya Texas Longhorn Tailgate Van ya rangi nyeusi
na yenye urefu unaokaribiana na urefu wa minbus yenye vioo vyembamba madirishani
vinavyoruhusu sura ya mtu kuchungulia kwa shida.
Tofauti na magari mengine yote yaliyotangulia kuingia eneo lile na kuegesha katika
maegesho ya Vampire Casino gari lile lililoingia halikufanya hivyo badala yake gari lile
lilipita moja kwa moja hadi mbele ya ule mlango wa kuingilia casino kisha likasimama.
Wakati huu nilikuwa nimesahau kabisa sigara yangu mdomoni kwani macho na
ubongo wangu vilikuwa vikikazana kushirikiana kikamilifu katika kutafsiri vizuri ile taswira iliyokuwa mbele yangu.
Nikiwa naendelea kulitazama lile gari muda mfupi uliyofuata mara nikamuona
mwanaume fulani akitembea taratibu kutoka kwenye gari moja lililokuwa katika eneo
lile la maegesho akielekea sehemu liliposimama lile gari van. Nilimtazama yule mtu
na kwa haraka nikatambua kuwa mtu yule alikuwa akiongea na simu na alipolikaribia
lile gari refu na jeusi nilimuona akiikata ile simu na kuitia mfukoni. Muda uleule mara
nikauona mlango wa nyuma wa ile van ukifunguliwa. Mlango ule ulipofunguliwa
wakashuka wanaume wawili warefu waliovaa suti nadhifu nyeusi na kofia za pama
ingawaje suti zao bado hazikuweza kuificha miili yao imara iliyojengeka vizuri.
Wanaume wale waliposhuka wakasimama kando ya ule mlango wa nyuma wa ile
van mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia huku wakiwa wamekunja
mikono yao vifuani kwa ustaarabu. Yule mtu aliyekuwa akiongea na simu sasa alikuwa
amefika nyuma ya ile van na kusimama kisha akasalimiana na wale wanaume wawili
na kusogea akitazama nyuma ya ile van. Haukupita muda mrefu mara nikamuona
mtu fulani akishuka kutoka nyuma ya ile van. Mtu yule alikuwa mwanamke aliyevaa
kofia aina ya Sombrero ama zile kofia zinazovaliwa na watu wa kusini mwa bara la
Marekani. Sehemu nyingine ya mwili wake ilikuwa imesitiriwa na gauni fupi sana jeusi
lililoyaweka wazi mapaja yake. Nilijitahidi kwa kila hali ili niweze kuziona sura za watu
wale lakini giza hafifu lililokuwa eneo la nje ya casino ile halikunipa nafasi hiyo.
Yule mwanamke akashuka na kasalimiana na yule mwanaume aliyekuwa akiongea
na simu muda mfupi uliopita kwa kubusiana mashavuni na hapo nikasikia sauti
nyepesi ya kicheko cha mahaba kutoka kwa yule mwanamke.
Wakati nilipokuwa nikijiandaa kushuka kwenye gari ili nielekee kwenye ule mlango
wa casino kitu kingine kikanivutia na kunifanya nisitishe kwa muda kile nilichokuwa
nikitaka kukifanya. Miale mitatu ya mwanga mkali wa flash ya kamera ilitoka kwenye
kioo cha mbele cha lile gari jeupe aina ya Corolla limited lililokuwa jirani yangu na hapo
nikamwona mtu fulani ndani ya lile gari akimaliza kupiga picha na kuificha kamera
yake.
Akili yangu ikapumbazwa kidogo huku nikishindwa kuelewa nini kilichokuwa
kikiendelea eneo lile. Nilipoyarudisha macho yangu kutazama kwenye ule mlango wa
ile casino sikuliona tena lile gari jeusi aina ya van wala wale watu waliokuwa wamesimama
na hapo akili yangu ikawa kama iliyopigwa na ugonjwa wa kiharusi. Sikuwa na muda
wa kusubiri zaidi hivyo nikafungua mlango wa gari langu na kushuka kisha nikaanza
kutembea nikielekea kwenye ule mlango wa casino.
Wanaume wawili mabaunsa wa mlangoni wakiwa katika mavazi yao ya suruali
nyeusi na fulana nyepesi zilizoishika vizuri miili yao imara walinikabili na kusimama
mbele yangu wakitengeneza ukuta makini usiopitika kirahisi.
“Onesha kadi yako ya mwanachama ndugu!” mmoja wa wale mabaunsa aliniambia
kwa utulivu.
“Hii ni mara yangu ya kwanza”
“Njoo kesho kuanzia saa nne asubuhi utapewa utaratibu wa namna ya kujiunga” mwenzake akadakia.
“Nahitaji kuonana na meneja wa casino nina shida ya dharura” niliongea huku
nikijitafutia uhalali wa kuingia mle ndani lakini hali ilikuwa tofati kwani sikupata
ushirikiano wowote badala yake wale mabaunsa walinipuuza na kumsikiliza mteja
mwingine aliyefika eneo lile. Sikuwa na ujanja tena hivyo nikasimama huku nikifiria nini
cha kufanya na wakati nikiwa katika hali ile nikashtushwa na kelele za muungurumo
wa gari lililokuwa likiondoka kwenye lile eneo la maegesho ya magari la casino.
Niliyahamisha macho yangu na kutazama ule upande muungurumo ule wa gari
ulipokuwa ukisikika na hapo nikaliona lile gari dogo jeupe aina ya Corolla limited
likiacha eneo lile la maegesho taratibu na kuelekea nje ya lile eneo la casino. Nikageuka
tena kuwatazama wale mabaunsa wa mlangoni na hapo nikagundua kuwa walikuwa
wakiendelea na hamsini zao. Sikuwa na muda zaidi wa kupoteza hivyo nikaanza
kuharakisha nikielekea sehemu lilipokuwa gari langu kwenye yale maegesho ya casino
na nilipofika nikafungua mlango na kuingia. Muda mfupi baadaye nikaanza safari ya
kuifuatilia ile gari Corolla limited nyeupe iliyoondoka kwenye eneo la maegesho ya casino
muda mfupi uliopita.
Kumfuatilia mtu pasipo kumpa nafasi yoyote ya kunitilia mashaka ilikuwa
taaluma yangu ninayoimudu vizuri hivyo nililiacha lile gari Corolla limited litangulie
mbele yangu kwa umbali fulani na hapo nikaanza kazi yangu. Lile gari mbele yangu
likaingia barabara ya United Nations halafu baada ya safari fupi nikaliona tena lile gari
likichepuka na kuingia upande wa kushoto ilipokuwa barabara ya mtaa wa Mindu.
Baada ya kitambo kirefu kidogo cha safari ile mara nikaliona tena lile gari likikunja
kona na kuingia upande wa kulia kuifuata barabara ya Mazengo.
Nikiwa nimeridhika kuwa mwenye lile gari mbele yangu hakuwa ameshtukia
chochote kuwa nilikuwa nikimfuatilia kwa nyuma,nilijitahidi vizuri kuidhibiti miguu
yangu kwenye pedeli za breki na mafuta,nikipunguza mwendo na kuongeza kila pale
nilipohitajika kufanya hivyo. Hatimaye nikaliona lile gari likikunja kona tena upande
wa kushoto kuingia barabara kuu ya Morogoro. Foleni ya magari iliyokuwa kwenye
barabara ile ya Morogoro ikaninyima uhuru wa kulifanya zoezi langu kwa starehe na
hapo nikavunja sheria kadhaa za barabarani katika kuhakikisha kuwa lile gari Corolla
limited nyeupe mbele yangu halinipotei machoni mwangu.
Lile gari likaendelea na safari na lilipofika mbele baada ya kulipita eneo la Fire
likakunja kona kuingia kwenye barabara ya kumbukumbu ya Patrice Lumumba. Safari
yetu ikaendelea. Tulisafiri kwenye barabara ile hadi pale tulipoyafikia makutano ya
barabara ya Patrice Lumumba,barabara ya mtaa wa Kisarawe,ile ya Bibi Titi Mohamed na ile
barabara ya mtaa wa Nkurumah. Tulipofika pale kulikuwa na foleni kubwa ya magari
hivyo sote tulisimama tukisuburi foleni ile ipungue.
Foleni ilipopungua nikaliona lile gari likiingia upande wa kushoto kuifuata
barabara ya mtaa wa Nkurumah. Hatukwenda mbali sana mara nikaliona tena lile
gari likichepuka na kuingia upande wa kulia likipotelea kwenye barabara inayokatisha
katikati ya majengo marefu ya ghorofa ya shirika la nyumba la taifa. Nami nikaendelea kulifungia mkia.
Kuingia kwenye barabara ile kukatufanya tuwe wawili tu,yaani mimi na yule mtu
kwenye lile gari mbele yangu niliyekuwa nikimfuatilia na hali ile sikuipenda kwani yule
mtu angeweza kuishtukia kwa wepesi dhamira yangu. Hivyo hatimaye nilipunguza
mwendo. Tuliingia kwenye barabara ya mtaa wa kwanza kisha barabara ya mtaa wa
pili na hatimaye barabara ya mtaa wa tatu tukikatisha katikati ya majengo marefu ya
ghorofa.
Tulipofika kwenye barabara ya mtaa wa nne mara nikaliona lile gari Corolla Limited
nyeupe mbele yangu likichepuka upande wa kushoto na kwenda kusimama nje ya
jengo moja la ghorofa. Niligeuka kulitazama lile gari wakati likisimama eneo lile kisha
nikaongeza mwendo na kuendelea mbele na safari kama mtu niliyekuwa kwenye
hamsini zangu na nilipofika mbele kidogo nikasimama kando ya barabara na kushuka
nikiharakisha kurudi kule lile gari Corolla Limited nyeupe liliposimama.
Yule mtu sasa alikuwa ameshuka kwenye lile gari na sasa alikuwa ameshika ile
kamera mkononi mwake huku akitembea taratibu na kwa utulivu kuelekea kwenye
jengo la ghorofa lililokuwa mbele yake. Hakuonekana kuwa na mashaka yoyote kwani
macho yangu makali yalikuwa yakizikagua vizuri nyendo zake. Nilifanya jitihada
kidogo za kumkaribia na mara hii nikashikwa na mshangao. Tofauti na hisia zangu za
hapo awali mtu yule hakuwa mwanaume kama nilivyodhani.
Alikuwa mwanamke au pengine niseme msichana wa umri wa kati ya miaka
ishirini na sita hadi ishirini na tisa kwa tathmini yangu ya haraka. Umbo lake la kike
maridhawa lilitengeneza mitetemo imara pindi alipokuwa akizitupa hatua zake kwa
utulivu. Alikuwa amevaa Pullneck nyeusi,suruali ya jeans iliyolikamata vyema umbo lake
na buti ngumu za ngozi miguuni aina ya Travolta.
Niliitazama ile kamera aliyoishika mkononi na hapo nikaongeza ziada nyingine
katika fikra zangu. Ile kamera aliyoishika yule msichana ilikuwa ni kamera aina ya
Toymaster. Kamera ambayo mara nyingi hutumiwa na waandishi wa habari katika
ukanda wa mapigano ya kivita. Niliwahi kuiona kamera kama ile katika maeneo tofauti
wakati nilipokuwa katika harakati zangu. Hivyo kuiona kamera ile mikononi mwa
yule msichana kukaniletea taharuki nyingine katika harakati zangu huku nijiuliza kuwa
huwenda alikuwa mwandishi wa habari.
Yule msichana aliendelea kutembea kwa utulivu huku akipotelea kwenye sehemu
ya mbele ya lile jengo la ghorofa mahali kulipokuwa na baraza iliyofunikwa kwa kofia
ya zege na hivyo kufanya giza hafifu sehemu ile. Nilizitupa hatua zangu nikimkaribia
yule msichana na hapo nikamsikia akianza kuzipanda ngazi za jengo lile kuelekea
sehemu ya juu ya lile jengo la ghorofa. Sauti ya mgongano wa soli za viatu vyake na ile
sakafu ya ngazi za lile jengo ilinieleza kuwa hakuwa msichana mvivu.
Sikutaka yule msichana aniache hivyo mara alipomaliza kuzipanda zile ngazi
za ghorofa ya kwanza mimi nilikuwa nimebakisha nusu ya umbali kumfikia. Na
kila alipokuwa akiutua mguu wake chini ulienda sambamba na mguu wangu katika
kuhakikisha kuwa hatua zangu hazisikiki.Zoezi lile liliendelea hadi tulipofika ghorofa ya nne ya lile jengo na hapo nikamuona
yule msichana akiingia kwenye korido ya ghorofa ile hivyo nikajibanza kwenye kona
ya ukuta nikimtazama. Korido ile ilikuwa ikitazamana na milango nane na katika
milango ile ni vyumba vitatu tu ndivyo vilivyokuwa vikiwaka taa.
Yule msichana aliendelea kutembea bila shaka yoyote hadi pale alipofika kwenye
mlango wa chumba cha mwisho cha ile korido hapo akasimama na kugeuka akitazama
nyuma yake alipotoka kama ambaye anataka kuhakikisha kuwa hapakuwa na mtu
yeyote aliyekuwa akimfuatilia.
Baada ya kitambo kifupi kupita mara nikamuona tena yule msichana akipachika
funguo kwenye kitasa cha ule mlango na muda mfupi uliyofuata akausukuma
ule mlango na kuingia ndani. Taa ya mle ndani ya kile chumba aliwashwa wakati
nilipokuwa kwenye harakati ya kuufikia ule mlango wa kile chumba yule msichana
alichoingia hata hivyo kabla sijaufikia ule mlango ile taa ya mle ndani ikazimwa na
kunifanya nisite kuendelea na safari yangu.
Nikasimama huku nikijishauri kuwa niendelee na harakati zangu au niachane
na mpango ule ili nije siku nyingine. Hatimaye nikajiambia kuwa nilipaswa kuwa
mvumilivu endapo ningetaka mambo yangu yafanikiwe. Hivyo nilisimama kidogo
huku nikiyatembeza macho yangu eneo lile katika namna ya kuisajili vizuri taswira
ya mandhari yale kichwani mwangu ili pindi nitakaporudi kwa mara nyingine nisiwe
mgeni. Nilipojitosheleza na kumbukumbu nzuri iliyojengeka kichwani mwangu
nikageuka na kuanza kuondoka taratibu eneo lile.
_____
AKIWA AMERIDHIKA KUWA YULE mtu aliyekuwa akimfuatilia tangu
alipokuwa akitoka kule Vampire Casino sasa alikuwa ameondoka baada ya kuzisikia
hatua za mtu huyo zikiyoyoma kwenye ile korido ya mbele ya chumba kile alichoingia
na baadaye kupitia dirishani akimuona mtu yule chini ya ghorofa akiondoka kuliendea
gari lake aliloliegesha barabara ya mtaa wa pili. Koplo Tsega aliliruhusu tabasamu
lake la asili kuchanua vizuri usoni mwake halafu kumbukumbu fulani za matukio
huko nyuma zilipoanza tena kuusimanga mtima wake tabasamu hilo likafifia haraka
na hatimaye kutoweka na hapo sura yake ikavaa uso wa kazi. Uso usiokuwa na mzaha
na mtu yoyote ambaye angejichanganya katika anga zake.
Hata hivyo wasiwasi haukwenda mbali na nafsi yake. Ukweli ni kwamba hakupenda
mtu yeyote atambue uwepo wake tangu alipoingia jijini Dar es Salaam kwa sababu
alizokuwa akizifahamu yeye mwenyewe. Hivyo kumuona mtu yule akimfuatilia tangu
alipokuwa akitoka kule Vampire Casino,tukio lile lilikuwa limemuacha na maswali
mengi sana kichwani.
Koplo Tsega akiwa amesimama pale dirishani aliisubiri taswira ya mwanaume
yule aliyekuwa akimfuatilia itoweke machoni mwake chini ya jengo lile la ghorofa
kisha maswali mengi yakaanza kupita kichwani mwake huku akijiuliza kuwa mtu yule
angekuwa nani. Hatimaye akajikuta akinong’ona
“Hakuna mtu yeyote anayemfahamu Lady butterfly hapa jijini Dar es salaam labda huwenda
wewe ukawa ni mtu wa kwanza lakini ni afadhali nisikufahamu”. Wakati akinong’ona akahisi
kama maneno yale yalikuwa yakimfikia yule mtu kule chini ya ghorofa lakini kitendo
cha kumuona mtu yule akitokomea bila kugeuka nyuma kumfanya akumbuke kuwa
alikuwa akijiongelesha mwenyewe.
Halafu akiwa katika tafakari ile nafsi yake ikaanza kusumbuliwa tena na
kumbukumbu za matukio ya nyuma huku akikumbuka mwendo wa safari ndefu
yenye umbali usiopungua kilometa 1628. Safari iliyomchukua muda wa siku nne kabla
ya kulifikia jiji la Dar es Salaam akitokea eneo la Kivu ya kaskazini nchini D.R Congo
mahali ulipo mlima mkubwa wa Govender.
Koplo Tsega akiwa bado amesimama pale dirishani fikra zake zikaendelea
kukusanya kumbukumbu za matukio na misukosuko yote aliyoipitia tangu siku ya
kwanza alipoingia katika misitu mizito na minene ya nchini D.R Congo iliyopo eneo
la Bunagana. Safari ya kutoka eneo la Bunagana ulipo msitu wa Govender ilikuwa
ngumu,ya kificho na iliyohitaji ujasiri wa hali ya juu huku akitumia njia zisizo rasmi
katika kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote anayemfahamu kama siyo kumtilia
mashaka.
Safari hiyo ikianzia usiku wa manane katikati ya msitu mzito wa Govender eneo la
Bunagana hadi eneo la Kisoro nchini D.R Congo. Kisha akavuka eneo la mpaka wa
nchi ya D.R Congo na nchi ya Rwanda liitwalo Cyahati. Koplo Tsega alipofanikiwa
kuuvuka mpaka huo kwa kificho akaingia mji wa Butaro nchini Rwanda halafu
akaendelea na safari yake akiingia mji wa Nyamugali,Shyorongi hadi Kigali,mji mkuu
wa nchi ya Rwanda. Koplo Tsega alipofika jijini Kigali akaweka kituo na kulala kwenye
gesti moja ya kichochoroni kabla ya kuanza tena safari yake asubuhi ya siku iliyofuata
akiingia mji wa Bicumbi,Rwamagana,Kigarama,Kibauya,Kirehe na baadaye kuuvuka
mpaka wa nchi hiyo na Tanzania eneo la Rusumo.
Asubuhi kulipopambazuka Koplo Tsega akaanza tena safari ya kutoka eneo la
Rusumo kisha akaingia mji wa Nyakasanza, Nyabugombe, Muzani, Ushirombo,
Marongwe, Kahama, Nzega, Ziba, Shelui, Igugumo, Singida, Puma, Manyoni,
Kilimatinde, Kintiku na hatimaye kuingia mji wa Dodoma wakati wa usiku huku
akiweka kituo na kulala. Siku ya nne alfajiri kulipopambazuka akaanza tena safari ya
kutoka mjini Dodoma na kuelekea jijini Dar es Salaam akipitia mkoani Morogoro.
Ingawa alifika jijini Dar es Salaam mapema lakini kwamwe hakupenda uwepo
wake ufahamike. Hivyo akatafuta hoteli moja iliyopo nyuma ya stendi kuu ya mabasi
yaendayo kasi eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam na kulala huku akisubiri siku
inayofuata kupambazuke ili aanze kazi iliyomleta jijini Dar es Salaam.
Ingekuwa rahisi sana kwake kufikia eneo la Kimara Suka alikokuwa amepanga rafiki
yake aitwaye Salma lakini hilo hakulipenda sababu ikiwa ni ileile ya kutopenda uwepo
wake katika jiji la Dar es Salaam ufahamike hadi hapo atakapokuwa amekamilisha
kazi yake.
Hivyo akiwa kwenye kile chumba cha hoteli aliyofikia Koplo Tsega akaamua kumpigia simu Momba ama dereva wa teksi na dalali aliyemsaidia kupata nyumba
ya kupanga huko siku za nyuma wakati alipokuwa akiishi jijini Dar es Salaam. Huku
akimtaka dalali huyo aliyejenga naye urafiki kuwa amkodishe gari lake kwa kipindi
chote atakachokuwa jijini Dar es Salaam.
Saa nane mchana ilipotimia Koplo Tsega akakutana na Momba nje ya mashine
za ATM za benki ya CRDB eneo la posta kuu jijini Dar es Salaam. Halafu akamlipa
Momba kiasi cha pesa kwa ajili ya kulikodi gari lake kwa muda wote ambao angekuwa
na mizunguko yake jijini Dar es Salaam. Muda mfupi baadaye baada ya kuagana na
Momba Koplo Tsega akaanza safari ya kuelekea mahali ilipo Vampire Casino ili kuanza
harakati zake.
Koplo Tsega aliwasili kwenye viunga vya maegesho ya Vampire Casino giza likiwa
tayari limeanza kuingia. Hivyo akatafuta sehemu nzuri na kuegesha gari lake ambapo
alitulia ndani ya gari hilo bila kushuka huku akimtazama kila mtu anayetoka na kuingia
kwenye casino ile.
Baada ya masaa machache ya kusubiri huku Koplo Tsega akiwa ndani ya gari lake
mara akaliona gari jeusi aina ya van likiingia na kwenda kusimama mbele ya mlango
wa casino ile. Macho yake yakiwa makini Koplo Tsega hakutaka tukio lile limpite hivyo
akaichukua kamera yake na kuanza kuchukua picha za kile alichokuwa akikihisi kwa
muda mrefu huko nyuma kabla ya kuliona gari lile jeusi likitoweka mbele yake.
Wakati akitoka Vampire Casino Koplo Tsega alikuwa ameazimia kurudi chumbani
kwake kwenye ile hoteli aliyofikia iliyopo nyuma ya stendi kuu ya mabasi yaendayo
kasi eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam. Lakini kitendo cha kuliona gari dogo aina ya
Peugeot 504 likimfungia mkia nyuma yake mara baada ya kutoka kwenye yale maegesho
ya Vampire Casino kukamfanya abadili dhamira yake ya kurudi kule hotelini alikofikia
na badala yake akaona kuwa aelekee moja kwa moja hadi mtaa wa Nkurumah kwenye
jengo la ghorofa la shirika la nyumba taifa yalipokuwa maskani ya muda ya Meja
Khalid Makame ambaye alikuwa humo tangu alipoitwa kwenye tume ya upambanaji
na udhibiti wa biashara haramu ya dawa za kulevya jijini Dar es Salaam. Huku
akiamini kuwa akiwa huko angeweza kumtambua vizuri mtu aliyekuwa akimfungia
mkia nyuma yake na hapo angeweza kumshughulikia kikamilifu.
Koplo Tsega aliamini kuwa kumlengesha yule mtu aliyekuwa akimfuatilia kwenye
nyumba hii kungempelekea kupata nafasi nzuri ya kumnasa na hatimaye kumalizana
naye kimyakimya bila ya mtu yeyote kufahamu. Lakini sasa mpango huo ulikuwa
umeharibika baada ya mtu yule aliyekuwa akimfuatilia tangu kule Vampire Casino
kugeuza na kurudi alipotoka. Mawazo yake yakaanza kusumbuka katika kutaka kujua
kuwa mtu yule alikuwa na nani na kwa nini alikuwa akimfuatilia. Hisia za kuwa uwepo
wake jijini Dar es Salaam ulikwishaanza kufahamika zikaanza kumtafuna taratibu
moyoni hata hivyo akaapa kuwa yoyote atakayeonesha kumfahamu kwenye harakati
zake atajuta kuzaliwa.
Koplo Tsega akiwa amejiridhisha kuwa yule mtu aliyekuwa akimfuatilia sasa
alikwisha toweka machoni pake akauacha muda uendelee kusogea mbele huku akiupisha utulivu akilini mwake kisha akaondoka pale dirishani na kuanza uchunguzi
wake.
Kwa kitambo kifupi kilichofuata Koplo Tsega alisimama kwa utulivu huku
akiyatembeza macho yake taratibu katika sebule ile mbele yake huku akijaribu
kurudisha kumbukumbu zake dhidi ya mandhari yale tangu mara ya mwisho alipofika
kwenye nyumba hii kuonana na Meja Khalid Makame wakati walipokuwa wakifanya
kazi pamoja kwenye tume ya kupambana na kudhibiti biashara haramu ya dawa za
kulevya jijini Dar es Salaam.
Kumbukumbu zake zikamtanabaisha kuwa hakuwa amekosea nyumba kama
alivyodhani hapo awali baada ya kuikumbuka namba 88 iliyokuwa juu ya mlango wa
nyumba ile wakati alipokuwa akiingia. Mara baada ya Meja Khalid Makame kupokea
wito wa kujumuishwa kwenye tume maalum ya kudhibiti na kupambana na biashara
haramu ya dawa za kulevya jijini Dar es Salaam akitokea kambi ya kijeshi ya 521
Chukwani kisiwani Zanzibar. Tume hiyo ilikuwa imemuandalia nyumba hii kama
makazi yake kwa kipindi chote ambacho angekuwa jijini Dar es Salaam akifanya
kazi na tume hiyo. Koplo Tsega aliendelea kusimama akitathmini madhari yale huku
akikumbuka siku alizokuwa akifika katika nyumba hii kuitikia wito wa Meja Khalid
Makame ambaye haraka alimshtukia kuwa alikuwa akimtaka kimapenzi.
Tathmini yake ikamueleza kuwa mandhari ya sebule ile yalikuwa bado
hayajabadilika kwani kila kitu kilikuwa vilevile. Sebule ilikuwa na makochi manne ya
mbao yenye mito ya rangi ya Samawati. Katikati ya sebule ile kulikuwa na meza fupi ya
mbao juu ya kipande kidogo cha zulia lenye mchirizi ya rangi ya ngozi ya Pundamilia.
Chini ya meza ile kulikuwa na magazeti machache ya siku za nyuma yaliyopangwa
vizuri. Upande wa kulia wa subule ile kulikuwa na kabati moja kuukuu lenye mafaili
yaliyoshika vumbi ambayo kwa haraka Koplo Tsega aliyakumbuka kuwa yalikuwa
yamebeba karatasi za nakala zenye maelezo tofauti juu ya matukio mbalimbali ya tume
ile huko siku za nyuma.
Pembeni ya kabati lile kulikuwa na meza fupi ya mbao ya Mahogany na juu ya meza
ile kulikuwa na picha ya Meja Khalid Makame akiwa katika uso wa furaha na sare
zake za kijeshi mwilini,picha hiyo ikiwa kwenye flemu pana ya kioo. Koplo Tsega
akapiga hatua zake taratibu kuisogelea picha ile ya Meja Khalid Makame ambaye kwa
sasa hakustahili tena kupewa heshima ya kuitwa mpiganaji mzalendo wa taifa hili bali
alistahili kuitwa majina yote mabaya ya dunia hii kama vile fisadi, baradhuli, nduli,
ndumilakuwili, dhalimu, mshenzi, muuaji, hayawani, mtu mwenye tamaa ya pesa,
msaliti na majina yote mengine ambayo yangeweza kuutambulisha ubaya wake.
Koplo Tsega akaichukua picha ile iliyoshika vumbi na kuitazama kidogo kisha
akaipigiza chini na kuivunja. Redio na seti moja ya runinga iliyokuwa kwenye meza
fupi nyeusi kwenye kona ya sebule ile vilikuwa vimeshika vumbi kila mahali. Koplo
Tsega akayatembeza macho yake akivitazama vitu vile kabla ya kuhamia kwenye
lile kabati kuukuu lililokuwa pale sebuleni. Alipofungua sehemu ya juu ya kabati lile
vumbi jepesi likatimka sambamba na kelele za Mende wengi waliokuwa wakitafuta maficho kwenye mafaili mengi yaliyoshika vumbi.
Vumbi lile lilipotulia Koplo Tsega akaanza upekuzi akipekuwa mkaratasi
yaliyokuwa ndani ya mafaili yale moja baada ya jingine. Kazi ilikuwa ngumu na
inayohitaji umakini wa hali ya juu na hata alipoimaliza hakuambulia kitu chochote cha
maana zaidi ya chafya zisizo na idadi. Sehemu ya chini ya kabati lile ilikuwa imefungwa
kwa funguo. Ngumi moja ya nguvu ikazipasua mbao za sehemu ile na kuacha tundu
pana lililomruhusu Koplo Tsega kuingiza mkono na kufyatua kabari yake. Sehemu
ile ilipofunguka Koplo Tsega akajikuta akitazamana na mlima wa makabrasha
yaliyopangwa vizuri pamoja na vitabu vichache vya mafunzo ya kijeshi. Koplo Tsega
akaweka macho yake kituo akiyatazama makabrasha yale kama anayefikiri jambo
fulani kisha akaanza upekuzi.
Vumbi lilikuwa kali mno kwani makabrasha yale yalikuwa hayajashikwa na
kufanyiwa usafi kwa muda mrefu lakini hakukuwa na namna. Koplo Tsega alianza
kwa kupekua kabrasha moja baada ya jingine huku mara kwa mara akiweka kituo
kuyapitia maelezo fulani ambayo yalimvutia. Lakini akajikuta akiachana nayo baada ya
kuhisi kuwa maelezo yale hayakuwa na umuhimu wowote kwake na vilevile hayakuwa
yakihusiana na kile alichokuwa akikitafuta. Mwishowe akamariza upekuzi wake pasipo
kupata kitu chochote cha maana.
Upande wa kushoto wa sebule ile kama zilivyokuwa nyumba zote katika jengo lile
la ghorofa kulikuwa na mlango na mara baaya ya kuufungua mlango ule ungekutana
na korido pana kiasi upande wa kushoto. Mwisho wa korido ile kulikuwa na milango
miwili. Mlango mmoja ulikuwa upande wa kulia kuelekea chumba cha kikuu cha
kulala ama Master bedroom na mlango mwingine ulikuwa mwisho wa korido ile kuelekea
sehemu ya maliwato na bafu la kuogea. Upande wa kulia kulikuwa na korido fupi
iliyopakana na milango ya kuelekea jikoni,kwenye ukumbi mdogo wa kulia chakula
wenye meza na viti na chumba kidogo cha stoo,mlango wake ukitazamana na ile
korido.
Koplo Tsega akasimama na kuelekea kwenye korido ile huku bastola yake
ikiwa mkononi. Alipoifikia ile korido akaelekea upande wa kushoto kulipokuwa na
ile milango miwili. Mlango wa ile sehemu ya maliwato na bafu ulikuwa wazi hivyo
aliusukuma kidogo na kuyatembeza macho yake mle ndani ambapo hakuona kitu
chochote cha maana. Nyumba yote ilikuwa imemezwa na ukimya kama iliyokuwa na
hakika kuwa isingemuona tena mwenyeji wake. Koplo Tsega aliuacha mlango ule na
kuusogela ule mlango uliokuwa upande wa kulia. Mapigo ya moyo wake yakiwa katika
utulivu wa kawaida akakijaribu kitasa cha mlango wa chumba kile. Mlango ulikuwa
umefungwa na hapakuwa na matumaini yoyote ya kuufungua hata hivyo kwa msaada
wa funguo zake malaya mlango ule ukafunguka kwa usumbufu kidogo
Chumba kilikuwa kipana chenye kitanda kikubwa cha mbao kilichofunikwa kwa
shuka safi za rangi nyekundu zenye maua yaliyodariziwa kwa ufundi wa namna yake.
Juu ya kitanda kile kuliku kulikuwa na mito miwili ya kuegemea. Pembeni ya kitanda
kile kulikuwa na meza fupi na juu ya meza ile kulikuwa na taa ndogo ya mwanga hafifu ya chumbani ama Lampshade na vocha za simu zilizotumika. Koplo Tsega alitembea
taratibu akikizunguka kitanda kile kwa utulivu. Mandhari yale mle ndani yalikuwa
tulivu na ya kisomi na kila kitu kilikuwa kimepangwa katika namna ya kuvutia kama
zilivyokuwa tabia za kijeshi.
Kabati la mbao la ukutani la chumba kile lilikuwa limejaa nguo za Meja Khalid
Makame,baadhi zikiwa ni sare zake za jeshi na nyingine nguo za uraiani. Koplo Tsega
akazipekuwa nguo zile bila kupata chochote cha maana.
Upande wa kushoto wa chumba kile kulikuwa na sanduku moja la nguo hata hivyo
ndani ya sanduku lile hakukuwa na kitu chochote hivyo Koplo Tsega akaendeleza
uchunguzi wake akiinama na kutazama chini ya kitanda kile. Kisha akafunua lile
godoro pale kitandani hata hivyo bado hakuona kitu chochote cha maana.
Alipokuwa mbioni kukata tamaa mara macho yake yakajikuta yakivutiwa na droo
moja ya kitanda kile iliyokuwa imefungwa. Koplo Tsega akaisogelea droo ile taratibu
na mara hii hisia fulani zikamjia akilini hivyo akaishika ile droo na kuifungua.
Ile droo ilikuwa imefungwa hata hivyo kwa msaada wa funguo zake malaya mlango
wa droo ile ukafunguka. Koplo Tsega akasogea karibu kuichunguza droo ile na mara
hii akaona kuwa ndani yake kulikuwa na bahasha ndogo ya kaki iliyotuna na kufungwa
kwa gundi kali. Akaichukua bahasha ile na kuichunguza na hapo akagundua kuwa juu
ya bahasha ile hapakuwa na maelezo yoyote,hali ile ikamshangaza sana.
Akiwa na shauku kubwa ya kutaka kufahamu nini kilichokuwa ndani ya bahasha
ile Koplo Tsega akaichukua ile bahasha na kuichana na hapo macho yake yakajikuta
yakitazamana na karatasi fupi zenye ukubwa unaolingana. Karatasi hizo zilikuwa
zimefungwa vizuri kwa utepe maalum mweupe. Alipoukata utepe ule na kuzichunguza
vizuri zile karatasi akagundua kuwa karatasi zile fupi zilikuwa ni hundi za benki fulani
maarufu iliyopo jijini Dar es Salaam huku zikiwa na majina tofauti ya watu.
Baada ya kuyapitia majina yaliyokuwa kwenye hundi zile Koplo Tsega akajikuta
akishikwa na mshangao. Majina yale yalikuwa ya watu aliokuwa akiwafahamu ambao
wengi wao walikuwa wajumbe wa tume maalum ya kudhibiti na kupambana na
biashara haramu ya dawa za kulevya nchini. Kitu cha kushangaza ni kuwa katika
hundi zile ni majina ya watu mawili tu ndiyo yaliyokuwa yamekosekana ili kukamilisha
orodha ya watu waliokuwa kwenye tume ile hapo awali. Majina hayo yaliyokosekana
likiwa ni jina lake yaani yeye Koplo Tiglis na Sajenti Chacha Marwa ambaye kwa
pamoja mchango wao ndiyo uliyokuwa mkubwa sana katika mafanikio yaliyofikiwa
na tume hiyo.
Koplo Tsega alirudia kuyasoma majina yaliyokuwa kwenye hundi zile katika
namna ya kuhakikisha kile alichokuwa akikidhania na alipomaliza zoezi lile akawa
na hakika kuwa hakuwa amekosea kwani ni kweli kuwa ni wao wawili tu majina yao
ndiyo hayakuwepo kwenye hundi zile. Hali ile ikapelekea uhalali wa hisia zake dhidi ya
kile alichokuwa akikiamini hapo awali uzidi kujengeka kichwani mwake. Kiwango cha
pesa kilichokuwa kimeandikwa kwenye hundi zile kilikuwa kimoja hata hivyo pesa zile
zilikuwa nyingi sana kiasi kwamba tawi la benki yoyote lisingeweza kuruhusu utoaji wa kiasi kile cha fedha kwa wakati mmoja. Swali likabaki kuwa kiasi kile kikubwa cha fedha
kilikuwa kinatoka kwa nani? Koplo Tsega akajiuliza bila kupata majibu.
Chini ya hundi zile kulikuwa na sahihi iliyoandikwa kwa hati safi na sahihi ile
ilikuwa ni ya mtu mmoja kutokana na namna ilivyofanana. Koplo Tsega aliitazama
sahihi ile kwa umakini hata hivyo aligundua kuwa ilikuwa mpya kabisa machoni
mwake. Hatimaye akazirudisha zile hundi kwenye ile bahasha na kuitia ile bahasha
mfukoni mwake.
Upekuzi aliomaliza kuufanya ndani ya chumba kile haukumletea majibu ya ziada
hivyo hatimaye akatoka nje ya chumba kile na kufunga mlango. Katika sehemu
nyingine zilizosalia za nyumba ile hapakuwa na kitu kingine cha maana hivyo hatimaye
alifungua mlango na kutoka nje ya ile nyumba.
Wakati huu ni nyumba moja tu ndiyo iliyokuwa ikiwaka taa katika korido ile
mbele ya ile nyumba na hivyo kulifanya eneo kubwa la korido ya jengo lile la ghorofa
litawaliwe na giza. Koplo Tsega aliitazama hali ile na kufurahishwa nayo kwani uwepo
wa giza lile ungeweza kumruhusu kuyatoroka mazingira yale pasipo kuonwa na
macho ya mtu yoyote ambaye angekuwa eneo lile.
Mara baada ya kutoka kwenye nyumba ya Meja Khalid Makame na kufunga
mlango Koplo Tsega alitembea kwa makini akikatisha mbele ya nyumba zile kuelekea
mwisho wa ile korido sehemu kulipokuwa na ngazi za kushukia chini ya jengo lile la
ghorofa. Muda mfupi baadaye alikuwa chini ya jengo lile la ghorofa akielekea sehemu
alipokuwa ameegesha gari lake kisha akafungua mlango na kuingia ndani. Dakika
chache zilizofuata Koplo Tsega alikuwa barabarani akivipangua vichochoro vya jiji
la Dar es Salaam.
Hata hivyo kabla ya kwenda mbali zaidi Koplo Tsega alikuwa ameamua
kujizungusha hapa na pale huku akichunguza kama kulikuwa mtu yoyote aliyekuwa
akimfuatilia. Alipoona kuwa hali ilikuwa shwari akaingia barabarani akiifuata barabara
ya Nkurumah,kisha akaendelea na safari yake hadi pale alipokutana na barabara ya
Morogoro. Halafu alipovuka barabara ya Morogoro akaingia barabara ya mtaa wa India
ambapo alisafiri kwenye barabara hiyo kwa kitambo kifupi kabla ya kuchepuka
upande wa kulia akiifuata barabara ya mtaa wa Makunganya.
Mtaa wa Makunganya haukuwa na pilika nyingi wakati huu wa usiku. Kulikuwa na
magari machache yaliyoegeshwa kando ya barabara ile na kwa kuzingatia kuwa wakati
huu yalikuwa majira ya mvua za masika hivyo idadi ya watembea kwa miguu nayo
ilikuwa imepungua sana. Koplo Tsega alipoingia kwenye barabara ya mtaa ule mbele
kidogo akatafuta mahali pazuri na kuegesha gari lake kando ya barabara. Ingawa
kipindi kirefu kilikuwa kimepita tangu mara ya mwisho alipofika katika mtaa ule wa
Makunganya lakini hali hiyo haikupunguza hata chembe ya kumbukumbu zake juu ya
mandhari yale.
Kumbukumbu alizokawanazo Koplo Tsega juu ya mtaa ule ni kuwa Guzbert
Kojo alikuwa akiishi nyumba namba 46 katika ghorofa ya nne ya jengo moja la
ghorofa lililokuwa miongoni mwa majengo mengi ya ghorofa yaliyokuwa kando ya barabara ya mtaa ule.Alipoegesha gari lake akatulia kwa muda akijaribu tena kuyakumbuka vizuri
mandhari yake kisha akafungua mlango wa gari na kushuka. Jengo la ghorofa alilokuwa
akiishi Guzbert Kojo lilikuwa upande uleule alikoegesha gari lake hivyo Koplo Tsega
hakuwa na sababu ya kuvuka barabara na badala yake alitembea taratibu akiliendea
jengo lile yalipokuwa maskani ya Guzbert Kojo. Na wakati akitembea kuelekea
kwenye jengo lile la ghorofa Koplo Tsega akajikuta akiomba kimoyomoyo kuwa
ingefaa amkute Guzbert Kojo akiwa ndani ya nyumba yake kesharudi kutoka kwenye
mizunguko yake kwani tofauti na hapo kungekuwa na kiasi fulani cha upotezaji wa
muda wakati akimsubiri ambapo hakuipenda kabisa hali hiyo itokee.
Muda mfupi baadaye akawa amelifikia jengo lile na wakati akipanda ngazi kuelekea
juu kwenye ghorofa ya nne alikokuwa akiishi Guzbert,Kojo Koplo Tsega akapishana
na mwanamke mmoja mwenye asili ya kihindi aliyejitanda baibui mwili mzima. Hata
hivyo hakusalimiana naye badala yake akazichomoa glovu zake nyeusi kutoka mfukoni
na kuzivaa viganjani kisha akaupeleka mkono wake kiunoni kuipapasa bastola yake
aina ya Fort 12 Silent. Uwepo wa bastola ile mahala pake ukamfanya atabasamu.
Katika jengo lile la ghorofa alilokuwa akiishi Guzbert Kojo idadi kubwa ya wakazi
wake walikuwa raia wa kitanzania wenye asili ya bara la Asia au niseme walowezi
wa kihindi na kiarabu walionogewa na mtindo wa maisha ya kitanzania. Guzbert
Kojo huwenda alikuwa na sababu ya kujificha katikati ya jamii hii,Koplo Tsega aliwaza na
huwenda sababu hiyo ilikuwa ni kujitengenezea maficho salama yasiyofikirika kwa
urahisi na maadui zake. Lakini sasa Koplo Tsega alikuwa mbioni kuyafikia maficho
hayo baada ya kitambo kirefu cha utunzaji wa kumbukumbu zake juu ya maskani yale.
Koplo Tsega aliendelea kupanda ngazi zile kwa utulivu huku akiendelea kuvuta
picha namna ugeni wake utakavyomshangaza Guzbert Kojo kama utakavyo kuwa
ujio wa pili wa masihi hapa duniani. Surprise! ya aina yake.
Ngazi za mwisho zilimkaribisha Koplo Tsega katika korido pana yenye uzio mfupi
upande wa kushoto na pia inayotazamana na milango ya nyumba zinayofuatana. Koplo
Tsega alipoifikia korido ile alisimama kidogo huku akijaribu kuyakumbuka mandhari
yale kupitia uwepo wa vitu fulani katika eneo lile ambavyo alikuwa akivikumbuka
tangu mara ya mwisho alipofika.
Hatimaye akajikuta akitabasamu baada ya kukumbuka vizuri kuwa alikuwa
amefika sehemu sahihi. Hivyo akaendelea tena na safari yake huku akitembea taratibu
na kwa utulivu kama mtu anayeogopa kukanyaga ardhini. Wakati akitembea kwenye
korido ile akawa akiyatembeza macho yake taratibu kutazama namba zilizokuwa juu
kwenye ile milango iliyokuwa ikitazamana na ile korido.
Kulikuwa na vyumba vitatu vilivyokuwa vikiwaka taa. Chumba cha kwanza
kulisikika sauti za maongezi ya wenyeji wake sebuleni. Chumba kilichofuata kilikuwa
kimya huku taa zake zikiangaza mle ndani na sauti pekee iliyokuwa ikisikika ilikuwa
ni sauti ya runinga ambayo mwanga wake ulijitahidi kupenya kupitia pazia jepesi
lililokuwa dirishani.Chumba kilichofuata kilikuwa na namba 46 mlangoni. Mara alipoina namba ile
Koplo Tsega alisita na kusimama kidogo akiitazama namba ile juu ya ule mlango wa
huku akihisi baridi nyepesi ikipenya moyoni mwake. Sasa alikuwa na hakika kuwa
mlango ule aliokuwa akiutazama mbele yake ulikuwa ni mlango wa nyumba aliyokuwa
akiishi Guzbert Kojo ama mtu aliyekuwa akimtafuta kwa udi na uvumba.
Taa ya sebuleni ya nyumba ile ilikuwa ikiwaka na hivyo kufanya idadi ya nyumba
zilizokuwa zikiwaka taa kwenye korido ile kufikia tatu. Koplo Tsega alisimama
nje ya mlango ule huku akiupima utulivu wa mle ndani na hapo akagundua kuwa
kulikuwa na kila dalili za uwepo wa watu au mtu mle ndani na hali ile ikamfurahisha.
Yeyote ambaye alikuwa mle ndani alipaswa awe ni Guzbert Kojo kwani tofauti na
hapo mtu huyo angejikuta akiijutia vibaya nafsi yake.
Kupitia uwazi mdogo uliyoachwa baina ya pazia la sebule ile na dirisha Koplo
Tsega aliweza kuiona vizuri mandhari ya sebule ile pasipo na uwepo wa mtu yeyote
mle ndani na hapo akajaribu kufungua kitasa cha mlango ule pasipo mafanikio. Ule
mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani na alipochungulia kwenye tundu la kitasa kile
akaona kulikuwa na ufunguo kwa ndani. Hali ile ikamfanya aliachie tabasamu lake
hafifu kisha akachukua kitambaa chake cha leso kutoka mfukoni na kukipitisha chini
ya ule mlango usawa wa lile tundu la funguo kwenye kile kitasa.
Zoezi lile lilipokamilika akachukua ufunguo wake wa gari na kuanza kuusukuma
ule ufunguo kwa ndani kupitia lile tundu la funguo kwenye kile kitasa. Muda mfupi
baadaye jitihada zake zikazaa matunda kwani ule ufunguo uliangukia juu ya kile
kitambaa cha leso chini ya ule mlango kwa ndani katika namna ya kutokutoa sauti kubwa
ambayo ingeweza kumshtua mtu yeyote ambaye angekuwa mle ndani ya ile nyumba.
Hivyo kazi iliyosalia ikawa rahisi tu. Koplo Tsega akainama na kukivuta taratibu kile
kitambaa hadi pale kitambaa kile kilipotoka nje kisha akauchukua ule ufunguo na
kuupachika kwenye lile tundu la kitasa. Jitihada kidogo alizozifanya kuuzungusha ule
ufunguo kwa uangalifu sambamba na kuzimudu vizuri kelele zilizotokana na zoezi lile
hatimaye kabari ya ule mlango ikafyatuka na hapo akausukuma ule mlango taratibu
akiingia mle ndani.
Sebule ilikuwa kubwa kiasi lakini yenye samani za kisasa kama makochi makubwa
ya sofa za kifahari,seti ya runinga moja kubwa ya inchi arobaini na mbili,sistimu kubwa
ya muziki aina ya JVC,jokofu la kisasa lenye milango pande mbili,zulia maridadi
sakafuni na meza fupi ya kioo iliyokuwa katikati ya sebule ile.
Koplo Tsega alisimama mle ndani huku akiyatembeza macho yake taratibu
kuipeleleza sebule ile na masikio yake yalipopata utulivu akagundua kuwa ile redio
ya mle ndani ilikuwa ikipiga muziki fulani kwa sauti ya chini. Na hapo akahisi kuwa
mwenyeji wa mle ndani hakuwa mbali sana na eneo lile.
Nyuma ya sebule ile kulikuwa na mlango mpana wa kutokea kwenye korido,mlango
ule uliyokuwa wazi ulikuwa umefunikwa kwa pazia la kifahari na jepesi. Koplo Tsega
alipolisogeza pazia lile macho yake yakajikuta yakitazamana na korido pana iliyopakana
na milango ya vyumba viwili kwa upande wa kushoto. Mlango mmoja ukitazamana na ile korido mwishoni na mlango mwingine upande wa kulia. Katika ule mlango
uliyokuwa mwishoni mwa ile korido mwanga hafifu wa taa iliyokuwa imewashwa
mle ndani ya kile chumba ulipenya kupitia uwazi mdogo uliyokuwa chini yake. Hali
ile ikamfanya Koplo Tsega atembee taratibu na kwa tahadhari kuusogelea ule mlango
katika namna ya kupeleleza zaidi.
Kulikuwa na kelele za maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka kwenye bomba la maji
lililokuwa mle ndani sambamba na kelele nyingine za mtu aliyekuwa akijiimbia wimbo
fulani usioeleweka.’Bila shaka Guzbert Kojo alikuwa bafuni akioga!’,Koplo Tsega aliwaza
huku bastola yake tayari ikiwa mkononi kumkabili. Utulivu uliyokuwa mle ndani
ilikuwa ni ishara tosha kuwa hakukuwa na dalili za uwepo wa mtu mwingine yeyote
mle ndani. Badala yake sauti pekee zilizosikika ni ile ya mtiririsho wa maji kule bafuni
na ile sauti ya muziki uliokuwa ukipiga kwa utulivu kwenye ile redio kule sebuleni.
Koplo Tsega akatuliza fikra za kukumbuka kuwa Guzbert Kojo alikuwa akiishi
peke yake mle ndani. Pamoja na kuwa alikuwa msomi mzuri na mtu mwenye kazi ya
kipato kikubwa lakini alikuwa hajaoa kwa kigezo kuwa hakuwa amempata mwenza
wa kueleweka.
Katika kipindi chote alichofanya kazi na tume ya udhibiti na upambanaji wa
biashara haramu ya dawa za kulevya nchini,Koplo Tsega alimfahamu Guzbert Kojo
kama kijana mchapa kazi na mwenye mtazamo wa kizalendo na maendeleo ya taifa.
Huwenda aliyemchagua katika tume ile alikuwa amefanya utafiti wa kutosha juu ya
tabia zake kwani hakuwa mtu wa kupumzika hadi pale suluhisho la jambo fulani
lililokuwa likimtatiza lilipopatikana. Mtu msiri na asiyekuwa na maneno mengi,makini
na anayejua kuishi vizuri na watu wenye tabia zilizoshindikana.
Kulikuwa na kasoro moja kubwa kwa Guzbert Kojo. Tabia yake ya usiri ilikuwa
imemfanya siku zote aonekane kuwa ni mtu asiyetabirika. Tabia yake hii ilikuwa
imempelekea kufanya kazi kwenye kitengo nyeti cha usalama wa nchi ingawa hakuna
mtu yeyote aliyekuwa akiifahamu vizuri kazi yake. Umri wake wa miaka thelathini
na sita,umbo lake kubwa,kakamavu na refu lakini lenye uwiano mzuri. Sura yake
nyembamba kiasi yenye mvuto wa aina yake kwa watu. Kifua chake kipana cha wastani
na tabia yake ya ucheshi vilikuwa vimeongeza chachu nyingine katika kuwanasa
wasichana warembo aliyowahitaji. Koplo Tglis Tsega hakuwa miongoni mwao!
Baada ya kitambo kifupi cha kusubiri huku akiwa amejificha hatimaye Koplo Tsega
akauona ule mlango wa bafuni ukifunguliwa kisha mwanaume mrefu na mweusi kiasi
mwenye kitambi kidogo cha wastani alichokibana vema kwa pindo la taulo lake jeupe
akatoka huku akionekana mwingi wa furaha na sauti ya mruzi mwepesi mdomoni.
Mara mtu yule alipotoka bafuni akaelekea kwenye ule mlango wa kile chumba kingine
kilichokuwa upande wa kulia wa ile korido lakini kabla hajakishika kitasa cha ule
mlango akawa ni kama aliyekumbuka kitu fulani. Hivyo akakiachia kile kitasa cha ule
mlango na kuelekea sebuleni na wakati akitembea Koplo Tsega aliweza kumuona
vizuri mtu yule kuwa alikuwa ni Guzbert Kojo.
Guzbert Kojo alipofika sebuleni akausogeza mto wa kuegemea uliyokuwa kwenye kochi moja la pale sebuleni na kuichukua simu yake iliyokuwa kwenye lile kochi. Kisha
taratibu akaanza kuipekuwa simu ile hadi pale alipoifikia namba fulani ambapo aliipiga
na kuanza kuongea na mtu wa upande wa pili ambaye bila shaka alikuwa mwanamke
kutokana na aina ya maongezi yale.
Wakati Guzbert Kojo akimalizia yale maongezi na kukata simu mara akahisi kitu
cha baridi kikikigusa kisogo chake. Hali ile ikapelekea kwa sekunde kadhaa mapigo
ya moyo wake yasimame kabla ya kuanza kwenda mbio. Koplo Tsega tayari alikuwa
nyuma yake.
“Tulia hivyo hivyo na usijaribu kuleta hila” Koplo Tsega alinong’ona
“Wewe ni nani?” Guzbert Kojo akauliza kwa mshangao.
“Weka simu yako chini Kojo na nakuonya tena kuwa usithubutu kuleta ujanja
wowote” Koplo Tsega alifoka na mara hii Guzbert Kojo akaikumbuka vizuri sauti ile
nyuma yake kuwa haikuwa ngeni masikioni mwake.
“Ah! Koplo…!” Guzbert Kojo akaita kwa wasiwasi pasipo kuwa na hakika.
“Ndiyo mimi,vipi mlidhani kazi imekwisha?” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu
huku mtutu wa bastola yake ukikigusagusa kichwa cha Guzbert Kojo kisogoni.
“Koplo!,kumbe bado upo hai na umeingiaje humu ndani?” Guzbert Kojo
akauliza kwa mshangao huku akigeuka nyuma taratibu. Hakufanikiwa kwani muda
uleule alijikuta akikabiliana na maumivu ya kichapo cha ngumi mbili kavu za mgongo
zilizosambaza maumivu makali mwilini mwake.
“Ukifuata kile ninachokueleza nothing bad will happen to you Kojo!”
“Koplo!,nini hivi unavyonifanyia,mbona sikuelewi?” Guzbert Kojo akalalama.
“Muda siyo mrefu utanielewa tu”
“What…!” Guzbert Kojo akafoka na kugeuka kwa kasi lakini Koplo Tsega
alikuwa mwepesi wa kuishtukia hila ile. Pigo la ngumi matata aliyoitupa Guzbert Kojo
lilikata hewa bila shabaha huku Koplo Tsega akiinama chini kidogo kulikwepa pigo
lile kisha akazituma ngumi zake kavu tatu za chapuchapu mbavuni mwa Guzbert
Kojo ambazo zilimpelekea Guzbert Kojo abweke mara moja kama mbwa kabla ya
kuachama mdomo wake wazi huku maumivu makali yakisambaa mwilini mwake.
Alipotaka kufurukuta zaidi akatandikwa kiwiko cha nguvu usoni kilichompelekea
ahisi kizunguzungu huku lile taulo kiunoni likimuamguka chini. Alipotaka kuliokota
lile taulo Koplo Tsega akalipiga teke na kulirushia pembeni. Guzbert Kojo alipotaka
kwenda kulichukua lile taulo mdomo wa bastola ya Koplo Tsega ukamuonya kuwa
asithubutu kufanya vile na hapo akatulia huku uso wake umesawajika.
“Hebu keti kwenye kochi Kojo nahitaji kuzungumza vizuri na wewe” Koplo
Tsega akaongea kwa sauti tulivu lakini isiyokuwa na mzaha. Guzbert Kojo hakuwa
na namna ya kufanya zaidi ya kutii amri ile hivyo akasogea kwenye kochi lililokuwa
pale kando yake na kuketi huku akiwa uchi. Kitendo kile kikamfanya na Koplo Tsega
naye azunguke na kwenda kuketi kwenye kochi jingine la upande wa pili lililokuwa
pale sebuleni. Hivyo wakawa wakitazamana huku kila mtu akitafakari jambo fulani
kichwani mwake. Guzbert Kojo akabaki akimtazama Koplo Tsega huku akiwa haamini kile
kilichokuwa kikitokea mbele yake huku mshangao umemshika kama aliyeona mzimu.
Koplo Tsega hakuwa msichana wa kumletea mchezo kama alivyozoea kumuona
hapo awali wakati walipokuwa wakifanya kazi pamoja. Guzbert Kojo akaanza
kujiuliza kuwa Koplo Tsega alikuwa msichana wa namna gani mwenye mbinu kali
za mapambano na nguvu za ajabu kiasi kile. Hatimaye akahitimisha kuwa alikuwa
amekivaa kisiki cha mpingo chenye umbo la kike na sura nzuri ya mapenzi lakini
chenye nguvu za umeme na roho ya paka.
“Habari za siku nyingi Kojo?” hatimaye Koplo Tsega akavunja ukimya ukimya
huku mguu wake mmoja akiupandisha juu ya mwingine pale kwenye kochi.
“Nzuri!” Guzbert Kojo akaitikia huku idadi ya matusi mengi ya kumlaani msichana
yule mbele yake yakipita kichwani mwake.
“Okay! kidogo utanisamehe kwa uvamizi huu lakini tambua sikuwa na namna
nyingine ya kufanya” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akimtazama Guzbert
Kojo sambamba na bastola yake iliyokuwa mkononi. Hata hivyo Guzbert Kojo
hakuzungumza neno badala yake alitazama pembeni huku akionekana kuzama
kwenye tafakari nzito.
“Nani aliyekwambia kuwa mimi nimekufa?” Koplo Tsega akavunja ukimya huku
akimtazama Guzbert Kojo mbele yake. Guzbert Kojo akashikwa na hofu hata hivyo
alijimudu na kuongea kwa sauti dhaifu iliyopoteza ushujaa.
“Kila mtu anafahamu kuwa umekufa Koplo usinilaumu mimi” Guzbert Kojo
akaongea kwa woga pasipo kuitilia maanani hali yake yauchi.
“Hujajibu swali langu bado,nimekuuliza ni nani aliyekwambia siyo akina nani
wanafahamu”
“Nimesikia kwenye vyombo vya habari” Guzbert Kojo akaongea kwa kujiamini.
“Umesikia nini?”
“Kati ya wanajeshi watatu wa kutoka Tanzania waliouwawa na waasi wa M23
Kivu ya kaskazini nchini D.R Congo,wewe ni muongoni mwao na jina lako limetajwa”
Guzbert Kojo akaongea huku sauti yake ikitawaliwa na kitetemeshi cha hofu.
“Na hao wanajeshi wengine ni akina nani?” Koplo Tsega akauliza kwa makini
huku akionesha kuvutiwa na taarifa zile.
“Meja Khalid Makame kutoka kambi ya kijeshi 521 ya Chukwani kisiwani
Zanzibar na Sajenti Chacha Marwa kutoka kikosi 36 cha kambi ya jeshi Msangani
mkoani Pwani”
Taarifa zile zikampelekea Koplo Tsega atabasamu kidogo kabla ya tabasamu hilo
kuyeyuka muda mfupi baadaye kisha akauliza kwa sauti ya utulivu huku macho yake
yakiweka kituo kumtazama Guzbert Kojo mbele yake.
“Miili yetu italetwa lini hapa Dar es Salaam?”
“Wametangaza kuwa itapokelewa na amiri jeshi mkuu kesho kutwa jioni” Guzbert
Kojo akaongea kwa waoga huku habari zile zikizidi kumshangaza na kumfurahisha
Koplo Tsega
“Una hakika na hicho unachokizungumza?” Koplo Tsega akauliza huku
akionekana kuzama kwenye tafakari lakini muda huo huo vidole vyake vikiipapasa
bastola yake mkononi.
“Ndiyo!”
“Basi nafurahi sana kusikia kuwa nimekufa”
“Koplo..!” Guzbet Kojo akaita kwa sauti ya woga huku macho yake yakiutazama
mdomo wa ile bastola ya Koplo Tsega.
“Zungumza nakusikia” Koplo Tsega akaitika huku akiinua macho yake yenye
chuki kumtazama Guzbert Kojo mbele yake.
“Mbona habari hizi zinatuchanganya sana!. Sasa inakuwaje wakutangaze kuwa
umekufa wakati wewe bado ni mzima?”
“Zimewachanganya wewe na nani?” Koplo Tsega akauliza kwa hasira huku
akilipuuza lile swali la Guzbert Kojo.
“Agh! watu wengi tu ambao huwenda wakawa na maswali kama yangu baada ya
kukuona”
“Kwa nini uzungumzie mtazamo wa watu wakati humu ndani tuko wawili tu?”
“Na kwa nini univamie usiku huu na kuniaziri hivi?” Guzbert Kojo akaendelea
kuuliza huku akili yake ikianza kufanya kazi.
“Nimekuja kukuletea taarifa za kifo changu,bahati mbaya tu ni kuwa kumbe
taarifa zenyewe tayari unazo”
“Mbona sikuelewi!,tangu lini marehemu akasambaza taarifa za msiba wake
mwenyewe?” Guzbert Kojo akauliza huku ameshikwa na taharuki ya aina yake.
“Nilipenda nije mwenyewe ili muweze kuniamini’’ Koplo Tsega akaongea kwa
utulivu huku sauti yake ikionekana kuwa mbali na mzaha.
“Mbona sielewi,tukuamini mimi na nani?”
“Wenzako unaoshirikiana nao na usidhani kuwa mimi ni mwendawazimu au
mzimu,nafahamu vizuri ninachokizungumza” Koplo Tsega akaongea kwa hasira.
“Wenzangu ninaoshirikiana nao kufanya nini?...“ kabla Guzbert Kojo hajamaliza
kuongea akakatishwa.
“Tafadhali! nieleze nini kinachoendelea” Koplo Tsega akaongea akiweka mzaha
kando huku akimtazama Guzbert Kojo kwa makini.
“Kuhusu nini?” Guzbert Kojo akauliza kwa mshangao.
“Meja Khalid Makame!”
“Meja Khalid Makame amefanya nini?” Guzbert Kojo akauliza huku hofu ikianza
kumuingia.
“Nahitaji kufahamu utaratibu uliotumika katika kujumuishwa kwake kwenye
mpango wa amani D.R Congo”
“Sasa kitu cha ajabu ni kipi,yeye si mwanajeshi kama wewe na hiyo si ndiyo kazi
yenu?. Kwanini ushangazwe na uwepo wa Meja Khalid Makame nchini D.R. Congo
ilhali unajua kuwa na yeye pia ni mwanajeshi tena mwenye cheo kikubwa zaidi yako?”
“Sijashangazwa na kumuona Meja Khalid Makame nchini D.R. Congo ila ninachotaka kufahamu ni utaratibu gani uliotumika katika kujumuishwa kwake”
Koplo Tsega akaongea kwa utulivu hata hivyo alichokiona usoni kwa Guzbert Kojo
ni tabasamu jepesi lenye hila ndani yake. Kisha Guzbert Kojo akatikisa kichwa chake
taratibu kama mtu asiyekubaliana na hoja ile lakini wakati huo huo akionekana kufikiri
jambo halafu akavunja ukimya.
“Utaratibu uliotumika kwake ni kama ule uliotumika kwako na kwa Sajenti
Chacha Marwa”
“Unapokuwa muongo jitahidi usiwe msahaulifu Kojo!. Wakati ulipokuwa
unatukabidhi barua za kutakiwa kuachana na hii tume na kwenda kujiunga na
askari wenzetu kwenye mpango wa amani nchini D.R Congo mimi na Sajenti
Chacha Marwa,tulikuuliza juu ya Meja Khalid Makame kama tungeambatana naye.
Ukatuambia kuwa hilo lisingewezekana kwa yeye kwenda D.R Congo kwani kwa
kufanya hivyo tume hii isingekuwa na mwakilishi hata mmoja wa jeshi,kitu ambacho
kingekuwa si sahihi.
Ndiyo maana nataka kufahamu utaratibu uliyokuja kutumika hapo baadaye katika
kumleta Meja Khalid Makame nchini D.R Congo huku sisi tukiwa tumeshangulia”
Koplo Tsega alimaliza kuongea huku akimtazama Guzbert Kojo usoni.
“Sasa huoni kuwa hilo swali lipo nje ya uwezo wangu Koplo?. Hizo ni taratibu za
kijeshi na viongozi wako wa kijeshi ndiyo wenaoweza kulitolea hoja”
“Majibu unayo wewe Kojo unapoteza muda tu kunibabaisha. Uongozi wa kijeshi
pia una taratibu zake lakini taratibu zake zinaeleweka na zipo wazi. Uongozi huo
usingeweza kukupa barua za kutujumuisha kwenye mpango wa amani D.R Congo
pasipo kukupa sababu za msingi kwani sisi tulikuwa ni wanatume tena kwenye
sehemu nyeti na kazi yetu ilikuwa bado haijakamilika.
Ina maana kati ya wanajeshi wote katika nchi hii ni sisi tu ndiyo tunafanya kazi
kwa bidii?”
“Mimi sifahamu chochote. Kama mwenyekiti wa tume mimi kazi yangu ilikuwa ni
kupokea barua na kuwakabidhi kama taratibu zinavyotakiwa”
“Hukupewa sababu ya kuenguliwa kwetu?”
“Sikupewa” Guzbert Kojo akajibu baada ya kitambo kifupi cha ukimya kupita
kisha Koplo Tsega akauliza tena.
“Kuna mgao wowote wa pesa uliokuwa ukiutaraji kutoka kwa Meja Khalid
Makame?”
Swali la Koplo Tsega likazidi kumchanganya Guzbert Kojo na hapo ukimya
kidogo ukapita huku Guzbert Kojo akionekana kutafakari halafu akakohoa kidogo
kusafisha koo lake kabla ya kujibu kwa kujiamini.
“Hapana!”
Koplo Tsega akamtazama Guzbert Kojo kwa udadisi na hapo akagundua kuwa
hakukuwa na uhalisia kati ya kile alichokuwa akikizungumza na mwonekano wake.
Kisha akaingiza mkono wake mfukoni na kuichukua ile bahasha ya kaki yenye
hundi aliyoipata kule kwenye nyumba ya Meja Khalid Makame mtaa wa Nkurumah.Alipoitoa ile bahasha akaifungua na kuanza kupekuwa zile hundi hadi pale alipoipata
hundi yenye jina la Guzbert Kojo na hapo akaichomoa na kuitupia pale mezani karibu
na Guzbert Kojo.
“Nahitaji sahihi yako” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu wakati Guzbert Kojo
alipokuwa akiisogelea ile hundi pale mezani na kuanza kuisoma. Alichokiona usoni
kwa Guzbert Kojo ni mshangao wa aina yake.
“Nani aliyekupa hii hundi?” Guzbert Kojo akauliza kwa taharuki huku jasho
jepesi likimtoka.
“Ulikuwa ukitarajia pesa ya namna hii kukufikia?”
“Hapana!,lakini…”
“Basi tia sahihi” Koplo Tsega akasisitiza huku sauti yake ikimezwa na hasira.
Guzbert Kojo alipoinua macho yake kumtazama akajikuta akikabidhiwa kalamu.
Hakuwa na namna ikabidi aipokee ile kalamu kinyongenyonge lakini akasita kusaini
huku akimkodolea macho ya mshangao Koplo Tsega.
“Kuna ugumu gani katika kutia sahihi?” Koplo Tsega hatimaye akauliza baada
ya kumuona Guzbert Kojo akisita huku akiikamata vyema bastola yake mkononi.
Guzbert Kojo kuona vile akasaini ile hundi na hapo Koplo Tsega akaichukua ile
hundi na kuitia kwenye ile bahasha kisha ile bahasha akaitia mfukoni na kumuacha
Guzbert Kojo akishikwa na mshangao usioelezeka.
“Mbona unaichukuwa hundi yangu?”
“Hundi yako kutoka kwa nani?”
“Agh! lakini si imeandikwa jina langu?”
“Nahitaji kwanza kufahamu pesa hizi zinatoka kwa nani halafu baada ya hapo
nitakupa mgao wako” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu huku akimalizia kuiweka
vizuri mfukoni ile bahasha na kumuacha Guzbert Kojo njia panda.
“Nani aliyekupa hizo hundi?” Guzbert Kojo hatimaye akauliza huku sauti yake
ikipwaya.
“Mtu wenu mliyemtuma kutuua”
“Mbona sikuelewi Koplo?”
“Umewezaje kuelewa kuwa hii hundi ni yako halafu ukashindwa kuelewa
ninachozungumza?” maneno ya Koplo Tsega yakamfanya Guzbert Kojo ashindwe
cha kuongea kisha Koplo Tsega akavunja ukimya tena.
“Nimefuata faili langu mlilonipokonya,nahitaji kuendelea na kazi yangu
mlioniachisha njiani”
“Mambo hayaendi hivyo Koplo. Kila kitu kina utaratibu wake!”
“Huu ndiyo utaratibu wangu“ Koplo Tsega akaongea kwa utulivu.
“Tume ndiyo iliyokupokonya faili lako Koplo siyo mimi na ukweli ni kwamba
hukupokonywa faili ila ulibadilishiwa majukumu”
“Kwanini nibadilishiwe majukumu wakati kazi ya mwanzo sijaimaliza?”
“Mbona unaongea utadhani wewe siyo askari!,amri inapotoka kwa mkubwa wako
sharti kuitikia wito Koplo na siyo kubishana .Hivi kila askari angetaka kubishana tungekuwa na jeshi la namna gani?” Guzbert Kojo akaongea katika jitihada za kuzidi
kuununua muda.
“Mkubwa wangu ni nani?”
“Viongozi wako wa kijeshi waliopendekeza wewe na askari wenzako kuwa
mjumuishwe kwenye mpango wa amani nchini D.R Congo”
“Faili la kazi yangu linahusika vipi na wao?”
“Sasa kama umefuata faili lako si ungekuja kesho ofisini tena katika masaa ya
kiungwana kuliko kunifanyia uvamizi na kuniadhiri namna hii?” Guzbert Kojo
akaongea huku ametahayari.
“I need your backup,afisa mkubwa na msomi kama wewe huwezi kuitegemea ofisi
tu ikutunzie mafaili yako?”
“Kompyuta yangu nimeisahau ofisini” Guzbert Kojo akaongea huku akianza
kuhisi hali ya amani ya mle ndani ilikuwa mbioni kubadilika.”Lakini mimi nakushauri
ungeachana na hilo faili lako kwani tume imeshawateua watu wengine kuchukua
nafasi zenu. Hivyo kujiingiza kwako tena kwenye harakati za tume hii ni kinyume na
taratibu na ni jambo linaloweza kukuletea matatizo”
“Unadhani hilo ndiyo linaloweza kuniogopesha?” Koplo Tsega akauliza huku
akiangua kicheko hafifu.
“Mimi sikuogopeshi ila najaribu kukuonya kwani huelekei kufahamu uzito wa
matokeo ya hicho unachotaka kukifanya”
“Wewe ni muoga Kojo,wewe na wenzako wote ni waoga. Unadhani unaweza
kunishawishi na kunihadaa ili na mimi niwe kama nyinyi?. Kama ulidhani hivyo basi
umekosea sana na tambueni kuwa mmefanya vibaya sana kumjeruhi nyoka mwenye
sumu kali baada ya jaribio lenu la kumuua kushindikana kwani kisasi chake ni kibaya
zaidi”
“Kwa hiyo unadhani mimi ni muoga?. Anyway pengne upo sahihi lakini tambua
kuwa siku zote waoga huwazika mashujaa. Na kama unadhani kuwa unapambana na
mimi au kikundi cha watu wachache basi umefanya kosa kumbwa sana ku-underestimate
nguvu iliyoko mbele yako. Huu ni mtandao wenye nguvu ya pesa na mamluki kwenye
kila idara hivyo siyo jambo rahisi kama unavyodhani.
Unaweza kunilaumu mimi au wenzangu lakini sisi ni watu wadogo sana katika
huo mtandao na tunafanya hivi ili vitumbua vyetu visitiliwe mchanga”.Guzbert Kojo
akaongea kwa msisitizo huku akijitahidi kuunda hoja yenye ushawishi mkubwa.
“Kwa hiyo ndiyo maana mkaamua kumtuma Meja Khalid Makame atuue eti
kwa vile tu hamtaki vitumbua vyenu visitiwe mchanga?” Koplo Tsega akauliza huku
akitabasamu.
“Mimi sijui chochote kuhusu Meja Khalid Makame”
“Nimemuua mtu wenu mliyemtuma,nimemuua Meja Khalid Makame kwa risasi
zangu mwenyewe na laiti ningeufahamu mpango wenu mchafu mapema bila shaka
ndiyo mnenifahamu vizuri kwanini wananiita Lady butterfly”
“Kwa hiyo wewe ndiye uliyemuua Meja Khalid Makame?” Guzbert Kojo akauliza kwa mshangao.
“Muda wa maswali na nasaha umeisha Kojo!,nimefuata faili langu” Koplo Tsega
akaongea kwa utulivu baada ya kuitazama saa yake ya mkononi kisha akasimama.
“Nimeshakuambia Koplo kuwa faili lako halipo hapa. Kwanini usije kesho masaa
ya kazi ofisini?” Guzbert Kojo akazidi kusisitiza.
“Unayo back up!,nina hakika kabisa kuwa unayo humu ndani and don’t waste my
time” Koplo Tsega akafoka kwa hasira na hapo Guzbert Kojo akainamisha kichwa
chake chini kama anayetafakari jambo baada ya kuhisi kuwa hila zake zilikuwa mbioni
kugonga mwamba na alipoinua kichwa akawa ameinuka na hila mpya. Akajidai
kuyatembeza macho yake kuitazama saa iliyokuwa imetundikwa ukutani pale sebuleni.
Tukio lile likamfanya Koplo Tsega naye ageuke kutazama kule alipokuwa akitazama
na hilo likawa kosa.
Guzbert Kojo alikuwa mwepesi kuisukuma meza fupi ya kioo iliyokuwa pale
sebuleni kuelekea upande ule alipokuwa Koplo Tsega . Lilikuwa ni tukio la kushtukiza
na Koplo Tsega hakuwa amejiandaa kwani ile meza ilimgonga miguuni na kumtupa
nyuma na ile bastola yake mkononi ikamponyoka na kuanguka ikitelezea chini ya ile
meza. Koplo Tsega alipotaka kusimama alikuwa amechelewa kwani Guzbert Kojo
akamuwahi pale chini na kumtandika teke la mgongo lililompelekea Koplo Tsega
apige yowe la maumivu. Kisha Guzbert Kojo akaishika miguu ya Koplo Tsega na
kuanza kumburuta pale sebuleni katika namna ya kuzidi kumchanganya akili yake.
Koplo Tsega akapiga mayowe huku akijitahidi kujitetea bila mafanikio. Zoezi lile
likaendelea hadi pale walipofika kwenye kona ya ule mlango wa kuingia kwenye ile
korido na hapo Koplo Tsega akapata mhimili mzuri. Akaishika kona ya ukuta ule
na kujizungusha kwa kasi ya ajabu. Guzbert Kojo hakuwa na namna ya kufanya ila
kuiachia ile miguu ya Koplo Tsega aliyoishika,na hilo likawa kosa kubwa.
Koplo Tsega akajipinda na kujifyatua kwa sarakasi matata na kumrukia Guzbert
Kojo,tukio ambalo liliwapelekea wote waanguke na kujibwaga sakafuni kwa kishindo.
Hata hivyo Koplo Tsega alikuwa mwepesi kuinuka kisha akarusha pigo la teke la
kiufundi lililolitawanya vibaya korodani za Guzbert Kojo na kumfanya apige yowe
kali la maumivu huku akirudi pale chini bila ya kupenda.
“Hutafanikiwa chochote Koplo,soon wataifahamu hila yako” Guzbert Kojo
akalalamika kwa maumivu makali.
“Tulia wewe bwege!” Koplo Tsega akafoka kwa hasira huku akiifuata bastola yake
kule chini ya meza lakini kabla hajaifika Guzbert Kojo akawa ameishtukia dhamira
yake hivyo akakusanya nguvu na kulivuta kwa kasi zulia lililokuwa pale sebuleni.
Tukio lile likampelekea Koplo Tsega apige mwereka wa aina yake huku akirushwa
juu hewani. Lakini alikuwa mpiganaji mahiri kwani alitua pale chini kama Paka kisha
akaiokota ile bastola yake pale chini ya meza tayari kumkabili Guzbert Kojo aliyekuwa
tayari amemfikia pale chini.
Pigo la teke la kwanza alilorusha Gizbert Kojo likampangusa Koplo Tsega kidogo
kichwani. Teke la pili lilipokuja akalidaka hewani kisha akamchota Guzbert Kojo kwa mtama wa kiufundi. Hivyo ikawa ni zamu ya Guzbert Kojo kurushwa hewani bila
ya kupenda na hapo tusi zito likamponyoka mdomoni. Alipotua chini akaangukia
matako kwa kishindo na hapo yale maumivu ya korodani yakamrejea tena na
kumpelekea aachame mdomo wazi na huku neno alilokusudia kulitamka likishindwa
kutoka mdomoni. Mkono wake mmoja ulikuwa tayari umevunjika.
“Usijaribu kuleta hila Kojo kwani hila hazitakufikisha mahali popote. Nahitaji faili
langu kwani ni kazi niliyoifanya mwenyewe tena katika mazingira magumu. Kama
mlikuwa hamna haja na sisi kwanini mlituita?“ Koplo Tsega akafoka kwa hasira huku
mtutu wa bastola yake mkononi ukikikodolea kichwa cha Guzbert Kojo.
“Go on you bastard! si umedhamiria kuniua?“Guzbert Kojo akalalama.
“Mbona unakwepa hoja ya msingi kwa visingizio visivyo na maana!. Nimesema
nahitaji faili langu” Koplo Tsega akafoka huku macho yamemtoka kwa gadhabu.
“Nimekuambia sina faili hapa nyumbani sasa unataka nifanyaje ili uniamini?”
“Na huo mtandao unaouzungumzia ni wa akina nani na una lengo gani?” Koplo
Tsega akamuuliza Guzbert Kojo kwa hasira huku akimkodolea macho ya chuki pale
chini.
“Go on Koplo kwani utapoteza muda wako bure kunishawishi”
“Kumbe unawafahamu sasa kwanini usiwataje?”
“Nayapenda maisha yangu’’ Guzbert Kojo akaongea kwa utulivu.
“Pumbavu!,sasa waoga kama nyinyi mnadhani mnaweza kuifikisha hii nchi mahali
salama?” Koplo Tsega akaongea kwa hasira lakini Guzbert Kojo hakuongea kitu
badala yake alimkodolea macho Koplo Tsega kama mtu asiyekuwa na ujanja tena.
Lakini akili yake ilikuwa ikifanyakazi haraka sana.
“Nakuuliza huo mtandao ni wa akina nani na lipi lengo lake?” Koplo Tsega
akauliza tena lakini hakujibiwa badala yake kitambo kifupi cha ukimya kikapita huku
wakitazamana. Hatimaye Koplo Tsega akavunja ukimya huku akizungumza kwa sauti
ya chini lakini inayosikika vizuri.
“Nimekuja kukuua ingawa sasa nimebadili dhamira yangu baada ya kufahamu
kuwa una taarifa muhimu nizozihitaji. Ninachohitaji kutoka kwako ni ushirikiano wa
hali ya juu. Nipe faili langu na baada ya hapo utanieleza vizuri kuhusu huo mtandao”
Koplo Tsega akaongea huku akiiruhusu risasi moja kuingia kwenye chamber ya bastola
yake tayari kufanya kazi. Lakini kabla hajakamilisha dhamira yake Guzbert Kojo
ambaye muda wote alikuwa akiuvuta kwa hila waya wa pasi iliyokuwa karibu yake pale
chini sebuleni akamrukia Koplo Tsega na kuuviringisha ule waya wa pasi shingoni
mwake.
Lilikuwa tukio la kushtukiza lakini lenye shabaha makini. Ule waya uliikaba vizuri
shingo ya Koplo Tsega na hapo Guzbert Kojo akaanza kuuvuta kwa kuukaza kwa
mikono yake ingawa ule mkono wake mwingine ulikuwa tayari umeshavunjika.
Koplo Tsega akataharuki huku macho yakimtoka kadiri Guzbert Kojo alivyokuwa
akizidi kuukaza ule waya shingoni mwake. Koplo Tsega akaanza kujitupa huku na kule
huku akirusha miguu na mikono yake katika harakati za kujitahidi kujinasua kwenye kabari ile bila dalili zozote za mafanikio kwani Guzbert Kojo aliendelea kuukaza ule
waya bila kikomo. Sasa zikawa vurumai za aina yake pale sebuleni huku wakivutana
na kupelekana huku na kule na katika kukurukakara zile ile bastola ya Koplo Tsega
ikaanguka tena sakafuni.
Akiwa ameanza kukata tama Koplo Tsega alijaribu kufurukuta kwa mbinu zake
zote lakini hakuna hata mbinu moja iliyofua dafu na hali ile ikazidi kumuogopesha.
Guzbet Kojo alikuwa nyuma yake akizidi kuukaza ule waya wa pasi shingoni
mwake. Matumaini yakiwa mbioni kutoweka mara Koplo Tsega akakumbuka kuwa
mfukoni alikuwa na kalamu na kitabu kidogo alichokuwa akikitumia katika kuandika
mambo yake. Kumbukumbu hiyo ikamfanya aupeleke mkono wake mfukoni
kujipapasa. Mara bahati ikawa yake kwani akakipata kile alichokuwa akikitafuta.
Kwa kasi ya ajabu akaichukuwa ile kalamu kutoka mfukoni na kuishindilia kwenye
jicho la Guzbert Kojo nyuma yake na hapo damu nyingi ikaruka hewani huku Guzbert
Kojo akiuachia ule waya na kupiga yowe kali la maumivu. Ile kalamu ilikuwa imezama
kwenye jicho la Guzbert Kojo ikisalia kwa sehemu ndogo tu kupotelea ndani. Guzbert
Kojo akaanza kulia kama mtoto huku akilishika jicho lake.
Kelele za Guzbert Kojo zikawa zimewashtua majirani hivyo wakaanza kufungua
milango ya majumbani mwao wakitaka kushuhudia nini kilichokuwa kikitokea mle
ndani. Koplo Tsega akiwa ameshtukia hali ile akawahi kuiokota ile bastola yake
pale chini sakafuni halafu muda uleule ule mlango wa sebuleni ukaanza kugongwa.
Koplo Tsega akausogelea ule mlango na kuufungua na hapo macho yake yakajikuta
yakitazamana na mwanaume mmoja mwenye asili ya kihindi aliyevaa kanzu na
makubadhi miguuni,mfupi kiasi,mwenye kitambi na kipara chenye nywele chache
kukizunguka kichwa chake. Kabla mwanaume yule hajaongea akajikuta akishikwa na
mshtuko wa aina yake baada ya kuiona bastola mkononi mwa KoploTiglis Tsega.
“Veve…!” yule mhindi akaongea katika sauti ilyopwaya baada ya kuiona bastola
mkononi mwa Koplo Tsega.
“Nenda ukalale na mkeo huku mkifikiria mbinu mpya za kuzidi kutunyonya,
Sipendi kuua mtu asiye na hatia” Koplo Tsega akafoka na yule mhindi kuona vile
hakutaka kuendeleza mjadala badala yake akageuza na kurudi ndani kwake. Halafu
zikafuatia kelele za milango mingine ya jirani kila mtu akijitahidi kujifungia vizuri
ndani kwake.
Ilikuwa zamu ya Koplo Tsega kushikwa na mshangao kwani wakati alipomaliza
kuufunga ule mlango na kurudi pale sebuleni Guzbert Kojo hakuwepo na hapo
paridi nyepesi ikaanza kuutafuna mtima wake. Kulikuwa na michirizi ya damu kutoka
sehemu ile sebuleni kuelekea kwenye ile korido iliyopakana na vile vyumba.’Guzbert
Kojo alikuwa ametoweka wakati yeye alipokuwa akiongea na yule mhindi’ Koplo Tsega
aliwaza kisha akaikamata vema bastola yake mkononi na kuanza kuifuatilia taratibu
ile michirizi ya damu iliyokuwa ikichuruzika bila shaka kutoka kwenye lile jeraha la
kalamu jichoni mwake.
Alipotoka pale sebuleni ile michirizi ya damu ikaelekea kwenye ile korido. Koplo Tsega aliitazama kwa makini michirizi ile na sehemu fulani ukutani kulikuwa na
alama za viganja vya mikono ya mtu vilivyotapakaa damu. Koplo Tsega akatambua
kuwa alama zile za damu zilitokana na viganja vya Guzbert Kojo wakati alipoiondoa
mikono yake kwenye lile jeraha na kushika kwenye zile kuta wakati akitafuta mhimili
mzuri wa kutembea. Ile michirizi ya damu iliendelea mbele na kupotelea kwenye
mlango mmoja wa chumba. Chumba hicho kilikuwa ni kile kilichokuwa karibu na
kile chumba cha bafu.
Koplo Tsega alipofika kwenye mlango wa kile chumba alisimama kidogo na
kutega masikio yake kuupima utulivu uliokuwa mle ndani. Chumba kilikuwa kimya
kama kilichokufa na hali ile ilimshangaza sana. Baada ya kujiridhisha na tathmini yake
Koplo Tsega akakishika kitasa cha ule mlango na kukusanya nguvu za kutosha kisha
akaupiga kumbo ule mlango kwa nguvu zake zote. Ule mlango ukafunguka kwa kasi
na hapo akazama ndani huku bastola yake ikiwa tayari kufanya kazi mkononi. Koplo
Tsega alitulia kidogo akiyatembeza macho yake mle ndani hata hivyo hakukuwa na
dalili zozote za uwepo wa Guzbert Kojo mle ndani.
Hali ile ikazidi kumchanganya zaidi Koplo Tsega na hapo akatafuta swichi ya taa
ya mle chumbani na kuiwasha. Macho yake yakapumbazika kidogo na chumba kizuri
chenye samani za kifahari;kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita na pembeni ya kitanda
kile kulikuwa na meza fupi na juu ya meza ile kulikuwa na redio ndogo. Kwenye kona
moja ya chumba kile kulikuwa na jokofu dogo ambalo lilikuwa likitoa muungurumo
hafifu mle ndani. Runinga kubwa iliyounganishwa na sistimu nzuri ya muziki wa
Home theatre ilikuwa pembeni ya Dressing table ya kisasa yenye lukuki ya vipodozi
vya kiume juu yake ilitokuwa ikitazamana na kitanda cha mle ndani. Ukutuani kulikuwa
na picha nzuri za kuchorwa zilizotundikwa katika namna ya kupendeza sana. Guzbert
Kojo hakuwepo mle ndani.
Pazia jepesi lililokuwa likipepea taratibu kwenye dirisha la kile chumba bila
kikwazo chochote lilitosha kumjulisha Koplo Tsega kuwa dirisha lile lilikuwa wazi.
Hivyo akashawishika na kuanza kuzitupa hatua zake taratibu kulisogelea lile dirisha.
Alipofika pale dirishani akalisogeza lile pazia kando na kutazama. Dirisha lile kubwa
la vioo lilikuwa wazi na Koplo Tsega alipolisogelea vizuri na kutazama chini nje ya
dirisha lile mara akaona kitu mfano wa kifurushi kisichoeleweka kikiwa kule chini ya
ghorofa usawa wa lile dirisha. Baada ya kutulia na kutazama kule chini kwa makini
kifurushi kile kisichoeleweka hatimaye taswira yenye hakika ikaumbika machoni pake.
Guzbert Kojo alikuwa amejiuwa kwa kujirusha chini ya jengo lile ghorofa kupitia lile
dirisha.
Koplo Tsega aliendelea kuyatuliza macho akitazama kule chini huku akishindwa
kuamini kama Guzbert Kojo angeweza kuchukua uamuzi wa namna ile.’Guzbert
Kojo alikuwa akificha siri gani hadi akadiliki kuyakatisha maisha yake kinyama namna ile
pasipo kutoa ushirikiano?’ Koplo Tsega akajikuta akijiuliza mwenywewe pasipo kupata
maajibu. Kisha akaanza kuvuta picha namna ambavyo taarifa za kifo cha Guzbert
Kojo kitakavyowavuta watu fulani mara baada ya taarifa hizo kuwafikia watu hao.ITAENDELEA
********
Sasa leo nitaendeleza kidogo. Lakini pia nitaanzisha adithi ya TAI KWENYE MZOGA. Inatakiwa mjue lengo la mwandishi kuleta kazi yake kwetu ni kujalibu kujitanga mjie kazi zake na hatimaye yeye kujulikana na hatimaye tena yeye kuweza kuuza zaidi kwani soko lake litakuwa limetanuka. Anashukuru kuna wadau wanampigia simu za kumpongeza na kuomba nakala. Naomba tuendelee namna hii kumtia moyo. kwani kadri mnavyompigia simu ndio kadri anavyoniruhusu kuachia kazi zaidi.