RIWAYA: Mifupa 206

RIWAYA: Mifupa 206

Sioni sababu ya kumramba miguu kisa hadithi yake hiyo..Yeye ndio kaanza kuniita Gay. Akitaka hata leo asiposti Akiposti nitasoma.🙂
Daah mondray tuwe wastaarabu nimejisikia vibaya mno kuna maisha nje ya jf lazima watu tujue ukiona mtu hajaingia kuleta story amekosa mda mkuu the banker tusamehe sisi
 
Nimekuja niko hapa mnaweza kuniambi kinachoendelea humu ndani?
 
The banker jifunzi kujizuia hasira.Humu kuna watu wa kaliba tofauti.Kwenye hadhira kunakuwa na watu wa aina tofauti.Take easy na tupia hapa muendelezo wa riwaya.Tunakusubiri!
 
MARA BAADA YA CHAZ SIGA kukata simu, sulle Kiganja akaipiga simu ile
akirudiarudia mara tatu zaidi bila mafanikio mwishowe akakata tamaa kabisa baada
ya kuhisi kuwa ile simu ya Chaz Siga ingekuwa imezimwa upande wa pili. Kisha
taratibu akageuka na kuwatazama maafisa usalama wenzake waliokuwa wakiyafuatilia
maongezi yale kwa makini wakiwemo Fulgency Kassy,Pweza na Kombe waliokuwa
wamekuja kumletea ripoti juu ya kutoweka kwa yule dada aliyesemekana kuhusika na
kifo cha meneja wa benki ya Zanzibar Marine ndugu Aden Mawala.
“CID Dan Maro bado mzima na lazima tufanye namna ya kumuokoa” Sulle
Kiganja akavunja ukimya huku akivigongesha vidole vyake mezani katika namna ya
kufikiri zaidi na hatimaye akayatembeza tena macho yake kuwatazama wale maafisa
usalama wengine mle ndani.
“Ningeshauri tusubiri kwanza hadi hiyo saa mbili usiku Chaz Siga atakapokupigia
simu na kuzungumza na wewe”.Tiblus Lupogo,mwanausalama kutoka kitengo
maalum cha upelelezi cha ofisi ya mashtaka DPP akatoa ushauri.
“Tunahitaji vijana wetu wataalam wa masuala ya mawasiliano watakaoweza
kufuatilia na kujua huyu Chaz Siga alikuwa akizungumza kutoka eneo gani halafu
baada ya hapo tutaanda mtego mzuri wa kumnasa” afisa usalama na mwanakamati
ya kudumu ya ulinzi na usalama ya jijini Dar es Salaam,Siraju Chenga akashauri kwa
utulivu huku ameyatuliza macho yake kufikiria jambo.
“Mimi siamini kuwa muuaji mkubwa kama huyu Chaz Siga anaweza kukosa
umakini kiasi cha kufanya mawasiliano yatakayopelekea kukamatwa kwake kirahisi
namna hiyo. Ngoja tusubiri hadi hiyo saa mbili usiku tukiwa na vijana wetu wa
mawasiliano na kama wataweza kutambua kuwa simu hii imepigwa kutokea wapi basi
tutakuwa na nafasi nzuri ya kumnasa” mkuu wa kamati ya dharura ya usalama na itikadi
za jeshi la wananchi Luteni Kanali Davis Mwamba akafafanua kabla ya wachangiaji
wengine kuendelea huku kila mmoja akionekana kuridhishwa na mchakato mzima wa
mikakati ya kumnasa Chaz Siga.
Kwa kuwa ripoti kutoka kwa Fulgency Kassy,Pweza na Kombe ilikuwa imejaa
viashiria vyote kuwa yule dada muuaji wa meneja wa benki ya Zanzibar Marine
alikuwa ameelekea kisiwani Zanzibar hivyo Sulle Kiganja hakuona sababu ya
kuendelea kupoteza muda badala yake akawataka Fulgency Kassy,Pweza na Kombe
haraka waondoke usiku ule na kuelekea kisiwani Zanzibar na kuhakikisha yule dada
anakamatwa kabla hajafika mbali.
Mara baada ya Fulgency Kassy,Pweza na Kombe kuondoka mle ndani majadiliano
ya kina yakaendelea zaidi baina ya wale makachero wa usalama katika mkutano ule
mfupi wa dharura.
“Uchunguzi nilioufanya kupitia vijana wangu umeanza kunipa uelekeo mzuri
kuwa huyu Chaz Siga na huyu mwanamke anayesemekana kuhusika na kifo cha
meneja wa benki ya Zanzibar Marine hawana mahusiano na pengine hawajuani kabisa.
Lakini vilevile taarifa za uchaguzi kutoka kwa vijana wangu zinaonesha kuwa bastola
iliyokuwa ikimilikiwa na meneja wa benki ya Zanzibar Marine haikuwa ikimilikiwa
kihalali na mmiliki wake anaonekana kuwa ni raia wa kisiwani Zanzibar mwenye jina
la Khalid Makame ingawa uchunguzi wa zaidi bado unaendelea” Sulle Kiganja akatoa
ufafanuzi wa kina.
“Mimi nina wazo jipya kidogo” Tiblus Lupogo akavunja tena ukimya na hapo
wote wakageuka na kumtazama kwa shauku kabla ya kuendelea.
“Kwa muda mrefu tangu kutokea kwa haya mauaji ya wanausalama wenzetu
nimekuwa nikifanya uchunguzi na kugundua kuwa wanausalama wote hawa
waliouwawa walikuwa katika tume ya udhibiti na upambanaji wa biashara haramu
ya dawa za kulevya iliyoteuliwa na mheshimiwa rais hapa nchini. Sasa hamuoni kuwa
huwenda hawa wanausalama wenzetu wanaweza kuwa wanauwawa kama sehemu ya
kuwafumba midomo na kupoteza ushahidi juu ya kile wanachokifahamu kuhusiana
na uchunguzi unaofanywa na tume yao?” hoja ya Tiblus Lupogo ikaonekana
kuwaingia vizuri wale wanausalama na hivyo kuibua minong’ono mingi huku kila
mmoja akizumza kwa mtazamo wake kuhusiana na hoja ile. Hatimaye Siraju Chenga
akuvunja ukimya.
“Nadhani hata mimi nimeanza kukubaliana na hoja hii lakini swali ni kwamba
mnadhani ni nani anayeweza kuwa nyuma ya mpango huu wa kuwafumba midomo
wanausalama wenzetu?”
“Anayeweza kufanya hivyo ni dhahiri anapaswa kuwa ni mtu mwenye madaraka
ya juu zaidi kama siyo wafanyabiashara wenye nguvu kubwa ya pesa” Tiblus Lupogo
akafafanua.
“Mimi ningependekeza kuwa mmiliki wa benki ya Zanzibar Marine naye
achunguzwe” Sulle Kiganja akapendekeza huku akiwatazama wanausalama wenzake
walioketi kwenye meza ya umbo duara yenye nane vilivyokaliwa na wanausalama wa
idara tofauti.
“Hilo nadhani halina mjadala na baada ya hapa nitatoa warrant ya kufanyika kwa
uchunguzi dhidi ya benki ya Zanzibar Marine” M.D Kunzugala mkurungenzi mkuu
wa idara ya usalama taifa akatanabaisha. Majadiliano machache yakaendelea kabla
ya kikao kile cha dharura kufika ukomo na wanausalama wale kuaga na kuondoka
wakikubaliana kukutana tena.
Mara baada ya maafisa usalama wale kuondoka mle ofisini wakabaki M.D
Kunzugala na Sulle Kiganja wakifanya majadiliano mengine ya kina zaidi kabla ya
kufikia hitimisho huku wakiwa wamekubaliana kuweka mfumo wa siri wa mawasiliano
kwa maafisa wote wa usalama waliokuwa kwenye kikao kile kama mkakati wa
upelelezi katika kutaka kufahamu kama kungekuwa na kuvuja kwa taarifa. Hatimaye
Sulle Kiganja na M.D Kunzugala wakaagana kila mmoja akishika majukumu yake.
_____
BOTI ALIYOIPANDA Koplo Tsega ilitia nanga kwenye bandari ya kisiwani
Zanzibar huku tayari usiku ukiwa umeshaingia. Kama ilivyo miji mingine ya pwani hali
ya hewa ya Zanzibar ilikuwa imetawaliwa na joto lenye upepo wa wastani. Mwanga
kutoka kwenye meli kubwa za mizigo za safari za masafa marefu zilizotia nanga katika
nanga bandarini pale kwa mbali mwanga wa taa kutoka katika majumba ya kale ya
ghorofa yaliyopakana na ufukwe wa bahari ya Hindi ulipelekea ziada nyingine katika
kuongeza uzuri wa mandhari ile.
Safari haikuwa ndefu sana lakini haikuwa imemzuia Koplo Tsega kutongoa walau
lepe moja la usingizi na sasa alikuwa ameshtuka kutoka usingizini baada ya sauti kali
ya honi ya meli kusikika wakati boti ile ilipokuwa ikitia nanga bandarini. Koplo Tsega
haraka akageuka na kuyatembeza macho yake kuwatazama abiria waliokuwa eneo
lile na kitendo cha kumuona kila mtu akisimama na kuanza kuchukua mzigo wake
ikawa ni ishara tosha kuwa safari ile ilikuwa imefika tamati. Hivyo haraka na yeye
akachukua begi lake na kulivaa mgongoni kisha akasimama na kuunga msafara wa
abiria waliokuwa wameanza kushuka kwenye boti ile huku mawazo juu ya yule mtu
aliyekuwa akifahamika kama White Sugar yakianza kuumbika tena kichwani mwake.
Akiwa anaendelea kushuka kwenye ile boti Koplo Tsega akajikuta akiwakumbuka
Fulgency Kassy,Pweza na Kombe huku hisia za kuwa huwenda wangefanya maamuzi
ya kuja kisiwani Zanzibar kumtafuta zikitengeneza ushawishi katika mawazo yake.
Hata hivyo alijipa matumaini kuwa jina la Shamsa Hafidhi alilolitumia kuiabiri boti ile
lisingekuwa na maana yoyote kwao hivyo akajipa moyo kuwa bado alikuwa salama.
Mara tu Koplo Tsega alipomaliza kushuka na kutoka kwenye bandari ile ya
Zanzibar akatembea kwa utulivu kuelekea kwenye maegesho ya teksi yaliyokuwa
nje kidogo ya eneo lile. Kijana mmoja dereva wa teksi aliyekuwa amejitega kusubiri
abiria akawa wa kwanza kumuona na kumkaribisha kwenye teksi yake kwa bashasha
zote. Koplo Tsega akatabasamu kidogo na alipoifikia ile teksi kwenye maegesho yale
akafungua mlango wa nyuma na kuingia huku akigeuka nyuma na kutazama kama
kungekuwa na mtu yeyote akimfuatilia. Hakumuona mtu yeyote na hali ile ikampa
faraja kuwa bado alikuwa salama. Yule dereva wa teksi alipofungua mlango na kuingia
mle ndani akageuka na kumuuliza Koplo Tsega kwa utulivu.
“Unaelekea wapi dada?”
“Nipeleke eneo la Changa,unapajua?” Koplo Tsega akauliza huku kumbukumbu
ya kisiwa cha Zanzibar ikiwa bado imehifadhika vyema kichwani mwake.
“Ondoa shaka napafahamu vizuri sana Changa,ndiyo wewe unapoishi?” yule
dereva akauliza huku akiitoa ile teksi kwenye maegesho yale hata hivyo Koplo Tsega
hakumjibu badala yake akatumbukiza swali kwenye maongezi yale.
“Utanitoza pesa kiasi gani?”
“Utanipa elfu kumi na tano tu dada yangu,bei ya mafuta imeongezeka sana” yule
dereva wa teksi akajitetea kabla hajaombwa kupunguza hali iliyompelekea Koplo
Tsega ajikute akitabasamu.
“Endesha gari” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu na hapo safari ikaanza huku
ile teksi ikiacha maegesho yale na kushika uelekeo wa upande wa kulia kuifuata
barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha kandokando ya bahari ile na hapo Koplo Tsega
akajiegemeza taratibu kwenye siti ya nyuma ya ile teksi.
Tangu utawala wa kwanza wa Sultan Majid bin Said hadi utawala wa mwisho wa
Sultan Jamshid bin Abdallah kabla ya kupatikana kwa uhuru wa mtu mweusi kisiwa
cha Zanzibar kimekuwa ni mji wa kale uliozungukwa na magofu ya zamani mazuri
yaliyokuwa makazi ya watawala na walowezi kutoka uajemi.
Muda huu wa usiku kandokando ya barabara ile kuelekea mji wa Stone Town
wachuuzi wa samaki walikuwa wameweka meza zao na kuendelea kuuza bidhaa
mbalimbali pamoja na samaki. Wenyeji kwa wageni watalii kutoka mataifa mbalimbali
duniani walionekana kutembea kwa miguu na kufanya manunuzi katika mtindo wa
maisha unaowafurahisha. Hoteli mbalimbali za kitalii zilionekana kupandwa katika
baadhiya maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi na hivyo kuongeza uzuri wa mandhari
ya usiku ya kisiwa kile.
Baada ya safari ndefu kidogo hatimaye ile teksi ikaingia barabara ya Mizingani
iliyokuwa ikipakana na ufukwe wa bahari ya Hindi upande wa kulia. Safari ikaendelea
huku teksi ile ikilipita eneo la Old Customs House halafu mbele kidogo ikalipita eneo
la Palace Museum. Hata hivyo kabla ya kulifikia eneo la Forodhani Garden dereva
wa teksi ile akakunja kona kuingia upande wa kushoto akikatisha katikati ya barabara
ya mtaa wa Nyumba ya Moto iliyokuwa ikipakana na magofu mengi ya kale. Safari
ile ikaendelea hadi pale walipoifikia barabara ya Jamatin ambapo yule dereva aliingia
upande wa kulia akiifuata barabara iliyokuwa ikitokezea kwenye Msikiti wa Jamat
Khana. Dereva wa ile teksi alipoupita ule msikiti mbele kidogo akaingia upande wa
kulia akiifuata barabara ya kuelekea Changa.
“Nishushe hapo mbele ya huo mgahawa wa Café Laaziz” Koplo Tsega
akamwambia yule dereva wa teksi baada ya kuuona mgahawa ule maarufu ambao
mbele yake kulikuwa na meza nyingi zilizokuwa na vitafunwa vya kila aina kama
chapati, vipande vya pweza, vitumbua, kalimati, kachori, kababu, kashata, maandazi,
tambi, bagia na vingine vingi vyenye majina ya asili.
Ile teksi iliposimama Koplo Tsega akafungua pochi na kumlipa yule dereva wa teksi
pesa yake kisha akafyatua kabari ya mlango na kushuka akielekea kwenye ule mgahawa
huku akifahamu fika kuwa macho ya yule dereva wa teksi yalikuwa yakimsindikiza
nyuma yake. Akiwa mle ndani yule dereva wa teksi akaendelea kumtazama Koplo
Tsega kwa utulivu hadi pale alipoingia kwenye ule mgahawa na hapo ndiyo akawasha
gari na kugeuza akirudi kule kwenye kijiwe chake alipotoka.
Lengo la Koplo Tsega likiwa ni kuondoa ushahidi juu ya wapi alipokuwa akielekea
mara tu alipohakikisha kuwa ile teksi iliyombeba ilikuwa imegeuza na kuondoka nje
ya ule mgahawa haraka na yeye akatoka nje ya ule mgahawa na kukodi bajaji moja kati
ya bajaji nyingi zilizokuwa eneo lile akimtaka dereva ampeleke eneo la soko la zamani
la watumwa ama Old Slave Market. Dereva wa bajaji ile kijana machachari akaanza
safari haraka akiifuata barabara ya Mtaa wa Kajificheni iliyokuwa ikikatisha katikati ya
makazi ya watu. Baada ya safari ndefu hatimaye dereva yule akakunja kona na kuingia
upande wa kushoto akiifuata barabara ya New Mkunazini na baada ya kitambo kifupi
cha safari ile bajaji hatimaye ikasimama eneo la Old Slave Market. Koplo Tsega
haraka akamlipa yule dereva pesa yake na ile bajaji ilipogeuza na kurudi ilipotoka
akaanza kutembea kwa miguu akielekea mbele ya ile barabara hadi pale alipoyafikia
makutano ya barabara ya Benjamin Mkapa na barabara ya Karume. Alipofika pale
akavuka makutano yale ya barabara na kukodi tena pikipiki ya Vespa akimtaka dereva
ampeleke mahali lilipokuwa duka kubwa la Zanzibar Stone City Bazaar. Dereva wa
pikipiki ile alikuwa kijana wa mjini aliyeujua vizuri mji na vichochoro vyake hivyo
haraka akashika uelekeo wa upande wa kulia akiifuata barabara ya Benjamini Mkapa
kisha akaipita shule ya Haile Selassie upande wa kulia hadi pale alipoyafikia makutano
mengine ya barabara ya Benjamini Mkapa,barabara ya Mapinduzi na barabara ya
Kawawa ambapo aliingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Kawawa.
Safari ikaendelea huku ile pikipiki ikilipita eneo la The State University of Zanzibar
kwa upande wa kulia na mbele kidogo akilipita jumba kubwa la Majestic Cinema. Hatua
chache mara baada ya ile pikipiki kulipita lile jengo la Majestic Cinema yule dereva
akaingia upande wa kulia eneo la Kibokoni ambapo alipofika mbele akashika uelekeo
wa barabara ya Sokomuhogo na baada ya safari fupi hatimaye ile pikipiki ikaenda
kusimama nje ya duka kubwa la kisasa lenye maandishi makubwa yanayosomeka juu
yake Zanzibar Stone City Bazaar. Kuona vile Koplo Tsega akatabasamu kidogo kisha
akushuka na kufungua pochi yake akitoa pesa na kumlipa yule dereva wa pikipiki.
Yule dereva wa pikipiki akaipokea ile pesa na kuitia mfukoni kisha akawasha pikipiki
yake na kutokomea mitaani.
Kwa sekunde kadhaa Koplo Tsega akasimama ng’ambo ya barabara ile
akilichunguza kwa makini lile jengo la Zanzibar Stone City Bazaar huku akishangazwa
sana na uwekezaji mkubwa wa biashara wa namna ile. Hapakuwa na shaka yeyote
kuwa duka lile lilikuwa ndiyo duka kubwa na la kisasa katika eneo lote la Stone Town.
Kupitia kuta safi za vioo za duka lile la kisasa bidhaa za kila namna zilionekana ndani
yake.
Nje ya jengo lile kwenye eneo la maegesho kulikuwa na magari machache
yaliyoegeshwa labda kwa vile muda ulikuwa umeanza kuyoyoma kwani maduka
mengi ya kisiwani Zanzibar yalikuwa tayari yamefungwa. Kadiri Koplo Tsega
alivyokuwa akilitazama lile jengo la Zanzibar Stone City Bazaar ndivyo taswira ya
yule mtu aliyekuwa akifahamika kama White Sugar ilivyokuw a ikijengeka upya katika
fikra zake. Hatimaye akavuka barabara ile kuelekea upande wa pili na kisha kuanza
kutembea akielekea kwenye mlango mkubwa wa lile duka la Zanzibar Stone City
Bazaar na muda mfupi baadaye alikuwa mle ndani.
Kama yalivyokuwa maduka mengi makubwa ya mijini ya kisasa duka la Zanzibar
Stone City Bazaar halikuwa tofauti sana kwani mle ndani kulikuwa bidhaa za kila
namna zilizopangwa vizuri katika maeneo tofauti kutegemeana na aina ya bidhaa
yenyewe. Mle ndani kulikuwa na raia wengi wa kigeni waliofika kufanya manunuzi
huku wakizunguka korido moja ya bidhaa kwenda nyingine na vitoroli vidogo vya
kusukuma kwa mikono vyenye magurudumu madogo na vitenga cha kubebea bidhaa
nyingi kwa pamoja.
Upande wa kushoto wa lile duka kulikuwa na rafu nzuri za mbao zenye bidhaa
zilizopangwa katika mtindo unaovutia. Mara baada ya kuingia mle ndani upande wa
mbele kulikuwa na sehemu zenye mashine za kusoma thamani ya bidhaa kando yake
wakiwa wameketi wafanyakazi wa duka lile. Upande wa kulia kulikuwa na maduka ya
simu na vifaa vya umeme.
Koplo Tsega taratibu akapiga hatua zake hafifu kuelekea kwenye yale maduka
ya simu na wakati akifanya vile macho ya watu waliokuwa mle ndani yakamtazama
kwa utulivu huku yakionekana kuvutiwa na namna ya uvaaji wake. Ndani ya duka la
kwanza la simu aliketi msichana mweupe mlimbwende mwenye asili ya bara la Asia
aliyevaa Baibui.
“Habari za kazi?”
“Salama karibu sana” yule dada akaongea kwa utulivu huku akimtazama
KoploTiglis Tsega
“Ahsante” Koplo Tsega akaitikia huku akijitia kutazama simu zilizokuwa
zimepangwa katika rafu za vioo za lile duka na wakati akifanya vile pia akawa
akiyachunguza vizuri mandhari ya mle ndani. Kutoka pale kwenye lile duka la simu
za mkononi upande wa kushoto kulikuwa na ngazi za kuelekea sehemu ya juu ya
lile jengo kulipokuwa na ofisi za utawala za lile duka. Hivyo kwa namna moja au
nyingine Koplo Tsega alijikuta akiwaza kuwa White Sugar angeweza kuwa ndani ya
ofisi mojawapo kati ya zile. Baada ya muda mfupi wateja wengine wakawa wameingia
mle ndani na kufika pale kwenye duka la simu na hivyo kuongeza idadi ya watu eneo
lile hali iliyompelekea Koplo Tsega kuweza kufanya uchunguzi wake kwa uhuru zaidi.
Koplo Tsega akiwa bado anaendelea kununua muda pale kwenye lile duka la simu
ghafla mlango mmoja kati ya milango mingi ya vyumba vya utawala vilivyokuwa juu
ya lile jengo ukafunguliwa. Koplo Tsega haraka akageuka na kutazama kule juu. Mara
baada ya mlango ule kufunguliwa wakatoka wanaume watatu wote wakiwa katika
mavazi nadhifu ya suti na kuanza kutembea kwa haraka wakazifuata zile ngazi za
kushukia sehemu ya chini ya lile duka katika korido pana iliyozuiliwa na ukuta mfupi
wa mabomba ya vyuma.
Mara moja moyo wa Koplo Tsega ukapoteza utulivu,damu ikamchemka
mwilini,nywele zikamcheza na jasho jepesi likaanza kumtoka. Miongoni mwa wale
wanaume watatu mmoja wao alikuwa ni yule aliyefahamika kwa jina la White Sugar
ambaye Koplo Tsega alikuwa amemkumbuka vizuri kuwa ndiye yule aliyepishananaye
mlangoni kule kwenye lile duka jingine la Zanzibar Stone City Bazaar lilioko Mlimani
City Shopping Mall jijini Dar es Salaam. White Sugar alikuwa katika muonekano wake
uleule wa awali pasipo kubadili mavazi. Upande wake wa kushoto na kulia kulikuwa
na vijana wawili waliokuwa wakitembeanaye sambamba kama walinzi wake huku
mmoja akiwa amebeba Briefcase nyeusi ambayo Koplo Tsega aliikumbuka vyema
kuwa ilikuwa ni ileile aliyomuonanayo White Sugar kule jijini Dar es Salaam.
Wakati White Sugar akishuka ngazi na wale wapambe wake kuelekea lile eneo
la chini kwenye lile duka kubwa la Zanzibar Stone City Bazaar njiani akapishana na
wafanyakazi wawili wa lile duka wakiwa katika sare zao za kazi ambapo walimsalimia
kwa heshima zote huku yeye akiitikia salamu zao kwa kupunga mkono kivivuvivu
kama mtu asiye na muda. Koplo Tsega akaendelea kumtazama vizuri White Sugar na
wapambe wake namna alivyokuwa akizishuka ngazi zile kwa madaha kama mfalme
katika utukufu wake na kupitia mwanga mkali wa taa zilizokuwa ndani ya jengo lile
Koplo Tsega akajiridhisha vizuri kuwa White Sugar alikuwa mwanaume mweusi sana
kuwahi kuonekana duniani angawaje afya na rangi yake ya ngozi viliusanifu vizuri
mwenekano wake wa hali ya ukwasi.
Mara tu alipomaliza kushuka zile ngazi White Sugar na wapambe wake wakashika
uelekeo wa upande wa kulia wakiufuata mlango mdogo uliokuwa kwenye kona moja
ya lile jengo. Wafanyakazi wa lile duka kuona vile wakawa ni kama vile waliotekwa
umakini huku wakijisogeza karibu na kumsalimia kwa bashasha zote za kirafiki ambapo
aliwaitikia kwa kuwapungia mkono kivivuvivu kama kawaida yake kisha White Sugar
akamuita mtu mmoja aliyekuwa eneo lile amevaa suti nyeusi na kumnong’oneza
jambo. Yule mtu akawa ni kama anayepokea maelekezo fulani yaliyompelekea ageuke
na kutazama kwenye lile duka la simu jambo ambalo Koplo Tsega hakulielewa maana
yake.
White Sugar alipoufikia ule mlango uliokuwa kwenye kona ya lile duka mpambe
wake mmoja kati ya wale vijana wawili akawahi mbele na kuufungua ule mlango na
hapo White Sugar akapita kisha wale vijana wapambe wakafuatia nyuma yake kabla
ya mlango ule kufungwa. Koplo Tsega alipotazama juu ya ule mlango akaona kibao
cha rangi nyeusi chenye maandishi makubwa meupe yakisomeka EXIT DOOR-For
Administration use only.
Kuona vile Koplo Tsega hakutaka kuendelea kusubiri hivyo taratibu akalitoroka
lile kundi la watu waliokuwa wamesimama nje ya lile duka la simu na kushika uelekeo
wa upande wa kushoto ulipokuwa mlango wa kutoka nje ya lile duka la Zanzibar Stone
City Bazaar. Mara tu alipotoka kule nje akaambaa na ukuta akielekea kwenye kona lile
jengo.Hata hivyo kabla hajafika mara akajikuta akisita na kujibanza baada ya kusikia
muungurumo wa injini ya gari likiacha maegesho ya magari ya lile jengo. Haukupita
muda mrefu mara gari kubwa aina ya Ford jeusi likayaacha maegesho yale na kuingia
kwenye ile barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha mbele ya lile jengo la Zanzibar Stone
City Bazaar likishika uelekeo wa upande wa kushoto kuifuata barabara ya mtaa wa
Sokomuhogo eneo la Kibokoni kuelekea kwenye ile kona ya Majestic Cinema.
Lilikuwa tukio la kushtukiza ambalo Koplo Tsega hakuwa amelitarajia kwani White
Sugar na wapambe wake walikuwa wakiondoka eneo lile na kuelekea kusikojulikana.
Kuona vile Koplo Tsega akaiacha ile kona na kuanza kutafuta usafiri wa haraka eneo
lile hata hivyo hakufanikiwa kwani lile eneo halikuwa na kituo cha usafiri wa namna
yoyote hivyo akajikuta akianza kutimua mbio kulifukuza lile gari kwa nyuma kama
mwehu na lile gari likaendelea kutimua mbio likitokomea. Koplo Tsega akaendea
kukimbia akilifukuza lile gari lakini mwendo wake haukufua dafu kwani baada ya
muda mfupi tu lile gari likawa limetokomea kabisa mbele yake na hivyo kwa mara
nyingine White Sugar akawa ameponea kwenye tundu la sindano kitendo ambacho
Koplo Tsega alikilaani sana.
Hapakuwa na tumaini jingine la kumfikia White Sugar usiku ule hivyo Koplo
Tsega akaamua kuchepuka na kuifuata barabara nyingine iliyokuwa upande wa kulia
wa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa ya kale katika mtaa uliokuwa na
utulivu na ukimya wa aina yake huku mawazo mengi yakipita kichwani mwake.
Ile barabara ilikuwa tulivu mno na isiyokuwa na pilika zozote za binadamu
huku ikiangazwa kwa taa hafifu kutoka katika nguzo za taa zilizokuwa kando yake.
Wakati Koplo Tsega akiendelea kutembea katika barabara ile akajikuta akiyakumbuka
matukio yote yaliyojili tangu siku ya kwanza alipoingia jijini Dar es Salaam akitokea
eneo la Kivu ya kaskazini,jamhuri ya kidemokrasia ya nchi ya Kongo.
Ilikuwa ni wakati alipokuwa mbioni kufika mwisho wa barabara ile ili aingie
upande wa kushoto kwenye barabara nyingine pale alipokumbuka kutazama nyuma
nyake. Kwa kufanya vile mara moja baridi nyepesi ya ghafla ikasambaa mgongoni
mwake huku moyo wake ukipiga kite kwa nguvu.
Kulikuwa na wanaume wawili waliokuwa wakija kwa haraka nyuma yake kwenye
barabara ile. Mwanaume mmoja alikuwa akitembea upande wa kushoto na mwingine
akitembea upande wa kulia na mwendo wao wa haraka ulitia mashaka. Koplo Tsega
kuona vile akaongeza mwendo huku akiendelea kugeuka nyuma na kuwatazama
wale watu mara kwa mara huku hofu ikiwa imeanza kumuingia na alipoifikia ile kona
ya barabara kuingia upande wa kushoto sehemu kulipokuwa na barabara nyingine
iliyokuwa ikikatisha katikati ya majengo ya kale ya ghorofa makazi ya watu akaanza
kutimua mbio. Koplo Tsega akaendelea kutimua mbio hadi pale alipofika mwisho wa
ile barabara ambapo haraka akachepuka upande wa kulia na kwenda kujibanza kwenye
kona moja ya jumba bovu la kale lililotelekezwa miaka mingi iliyopita ambalo sasa
lilikuwa halitumiki kama makazi ya binadamu kisha akageuka nyuma na kuchungulia
kule alipotoka.
Koplo Tsega akiwa bado amejibanza kwenye ile kona haukupita muda mrefu
mara akawaona wale wanaume wawili wakichomoza kwenye kona ya ile barabara na
kuanza kutimua mbio wakija upande ule wa ile barabara kwenye ile kona ya jumba
bovu alipokuwa bado amejibanza. Koplo Tsega alipowachunguza kwa makini wale
watu akagundua kuwa walikuwa wameshika bastola mikononi mwao hali iliyopelekea
hofu ya kukabiliana na hatari ianze kuchipua taratibu moyoni mwake. Wale watu
wakaendelea kutimua mbio na walipofika pale kwenye ile kona wakapunguza mwendo
na hatimaye kusimama huku wakishauriana kuwa washike uelekeo upi kwa vile ile
barabara ilikuwa imegawanyika katika barabara kuu mbili. Barabara moja ikinyoosha
mbele na nyingine ikiingia upande wa kulia mbele ya lile jumba bovu.
“Atakuwa ameelekea wapi?” mmoja akasikika akimuuliza mwenzake kwa sauti ya
chini.
“Nahisi ni kwenye barabara hii hii kwani kama angekuwa amenyoosha kule mbele
kwa vyovyote tungekuwa tumemuona tu” mwenzake akasikika akitengeneza hoja
kisha kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia huku wale watu wakiwa bado wamesimama
eneo lile kabla ya kushaurina jambo na kuanza kusogea taratibu kwenye kona ya lile
jengo bovu la kale. Koplo Tsega kuona vile taratibu akaicha ile kona aliyojibanza na
kuingia ndani kabisa ya lile jumba bovu huku akienda kujibanza kwenye kona moja
iliyokuwa na giza zaidi.
Haukupita muda mrefu mara wale watu nao wakaingia mle ndani ya lile jumba
bovu huku wakinyata kwa tahadhari na bastola zao mikononi. Walipofika katikati
ya lile jumba wakashauriana kitu kisha mmoja akaanza kupanda ngazi na kuelekea
sehemu ya juu ya lile jengo kwa mwendo wa kunyata. Yule mtu mwingine aliyesalia
pale chini akaanza taratibu kuzunguka kwenye kona za vyumba vya lile jengo
lisilokuwa na madirisha wala milango. Kuona vile Koplo Tsega akaichomoa bastola
yake yenye kiwambo maalum cha kuzuia sauti kutoka mafichoni na kuikamata vyema
mkononi. Yule mtu aliyebaki chini ya lile jengo akavikagua vyumba vyote vya chini
ya lile jengo na alipoona kuwa hakuna kitu cha maana akarudi mle ndani na kuanza
kuzikagua kona za eneo lile.
Koplo Tglis Tsega akiwa bado amajibanza gizani kwenye ile kona akamsubiri yule
mtu amfikie usawa wake kisha akatupa pigo moja la kareti lililoipokonya mkononi
bastola ya yule mtu na kuitupa kando. Yule mtu alipotaka kugeuka akajikuta akikabiliana
na mapigo mengine mawili ya kareti shingoni mwake yaliyolipasua vibaya koo lake
na kabla hajapiga mayowe ya kuomba msaada Koplo Tsega akawahi kumtundika
kabari matata shingoni isiyoruhusu hewa kupenya. Yule mtu akafurukuta akitupa
miguu yake huku na kule na kujitahidi kujinasua lakini ilishindika hivyo mwishowe
akaishiwa pumzi na kutulia uhai ukiwa mbali na nafsi yake. Kuona vile Koplo Tsega
akamburuta taratibu yule mtu hadi kwenye chumba kimoja cha lile jengo na kuanza
kumpekua mifukoni. Hakupata kitu chochote na wakati akimalizia kumpekua mtu
yule mifukoni mara akamsikia yule mwenzake akishuka zile ngazi za lile jengo bovu
kuja kule chini hivyo haraka akachepuka na kwenda kujibanza nyuma ya zile ngazi.
Yule mtu akawa ni kama aliyehisi jambo fulani kwani mara tu alipomaliza kushuka zile
ngazi akasimama kwa utulivu na kuanza kumuita yule mwenzake kwa sauti ya chini
“Tino…Tino…!” na yule mtu alipoona kuwa hakuna dalili zozote za kuitikiwa
akawasha kurunzi yake na kuanza kumulikamulika mle ndani na kwa kufanya vile
akawa ni kama aliyeziona zile alama za mburuto wa yule mwenzake aliyeuwawa hivyo
haraka akaikamata vyema bastola yake mkononi na kuanza kuifuatilia ile alama ya
mburuto kwa tahadhari. Koplo Tsega kuona vile haraka akatoka kwenye yale maficho
na kumvamia yule mtu kwa nyuma hali iliyowapelekea wote kwa pamoja waanguke
na kujibwa chini kama mizigo huku bastola zao zikiwaponyoka mikononi. Hata hivyo
yule mtu aliwahi kusimama haraka na kurusha teke la nyuma lililomtandika vibaya
Koplo Tsega kifuani na kumtupa tena chini. Pigo jingine la teke lilipomfikia Koplo
Tsega akawahi kuinama kidogo na hivyo kulipelekea pigo lile likate upepo bila majibu
kisha akaikita mikono yake chini kwa nyuma akijibetua vizuri na kusimama.
Kuona vile yule mtu akaruka hewani na kutupa mapigo mawili mengine ya mateke.
Pigo moja likamzaba Koplo Tsega kichwani na lile pigo la pili Koplo Tsega akawahi
kulipangua kwa mikono yake miwili kisha akajitupa chini akijiviringisha na kumfuata
yule mtu kwa kasi ya ajabu na aliponyanyuka akamchapa yule mtu ngumi mbili kavu
za korodani,mapigo matatu makini ya kareti tumboni na kisha nyumi moja ya nguvu
ya shingoni iliyompelekea yule mtu apige yowe kali la maumivu huku akipepesuka.
Kisha Koplo Tsega akajirusha upande wa pili huku akitupa teke la nyuma lililojikita
vizuri kwenye mgongo wa yule mtu na kumfanya agune kabla ya kuanguka chini. Hata
hivyo Koplo Tsega akawahi haraka kumrudia yule mtu pale chini kabla hajasimama na
hapo akaikamata miguu yake na kuanza kumburuta kwa kasi hadi kwenye nguzo moja
iliyokuwa katikati ya lile jumba bovu ambapo aliigongesha vibaya pacha ya miguu ya
yule mtu na kumsababishia maumivu makali ya korodani hali iliyompelekea yule mtu
apige yowe kali la maumivu. Yule mtu alipotaka kufurukuta kajikuta akitazamana na
mdomo wa bastola ya Koplo Tsega mkononi.
“Wewe ni nani?”
“Go to hell…!” yule mtu akajibu kwa jeuri huku akilalama kwa maumivu makali ya
korodani zake na hapo Koplo Tsega akamshindilia ngumi moja kwenye mwamba wa
pua yake iliyomsababishia maumivu makali yule mtu.
“Nakuuliza,wewe ni nani?”
“Farouk…!” yule mtu akalalama kwa maumivu makali
“Mnataka nini kwangu?”
“Tumetumwa tukufuatilie”
“Nani aliyewatuma?” Koplo Tsega akamuuliza yule mtu huku akishtushwa na
maelezo yale
“Bosi wetu…”
“Bosi wenu nani?” Koplo Tsega akamuuliza yule mtu kwa udadisi na alipomuona
akisita kunyoosha maelezo akamzaba kofi la uso.
“White Sugar…” jibu lile likampelekea Koplo Tsega kwa sekunde kadhaa ashikwe
na mduwao huku akimtazama yule mtu kwa makini. Maelezo ya yule mtu yakawa
yamempelekea amkumbuke White Sugar wakati alipokuwa akimnong’oneza mtu
mmoja muda mfupi kabla ya kutoka na wapambe wake kwenye lile duka Zanzibar
Stone City Bazaar muda mfupi uliopita.
“White Sugar anaishi wapi hapa Zanzibar?”
“Sifahamu” yule mtu akajitetea hata hivyo Koplo Tsega hakukubaliananaye
hivyo akamzaba tena makofi mawili ya nguvu usoni yaliyompelekea yule mtu aanze
kunyoosha vizuri maelezo yake.
“Mimi sijawahi kufika nyumbani kwake ila niliwahi kusikia kuwa anaishi eneo
linaloitwa Bumbwini karibu na Slave Chambers” yule mtu akafafanua na Koplo Tsega
hakuona sababu ya kuendeleza tena mjadala ule hivyo akaielekeza bastola yake kwa
yule mtu na kufyatua risasi mbili zilizomlaza yule mtu chali.
 
SAA MBILI KAMILI USIKU ILIPOTIMIA ilinikuta nikiwa mwisho wa korido
ya ghorofa ya nne ya jengo la Millenium Architectures eneo la Kigamboni jijini Dar es
Salaam. Kisha nikaichukua simu yangu ya mkononi kutoka mfukoni na bila kupoteza
muda nikaanza kupekuwa hadi pale nilipoifikia namba ya simu ya mkuu wa idara
ya intelijensia ya kijasusi ya usalama wa taifa,Sulle Kiganja ambapo haraka nikaipiga
namba ile na kuiweka simu sikioni.
Mojawapo ya vitu nilivyokuwa na uaminifu navyo ni katika suala zima la kuzingatia
muda. Ombi langu likionekana kuzingatiwa vizuri mwito mmoja tu simu yangu
ikapokelewa upande wa pili na sauti ya mtu aliyepokea simu ile nikaikumbuka haraka
kuwa ilikuwa ni ya Sulle Kiganja.
Nikiwa na hakika kuwa mawasiliano ya simu yangu sasa yalikuwa yakichunguzwa
na sauti yangu kunaswa na vifaa maalum vya kijasusi upande wa pili nikapanga
kutokupoteza muda katika maongezi na hivyo kukimbilia kwenye hoja yangu ya
msingi.
“Haloo Chaz Siga habari za usiku?”
“Mpe simu Mwasu nahitaji kuzungumzanaye sasa hivi”
“Chaz nahitaji kwanza kuonana na wewe,niambie sehemu ulipo nitakuja sasa hivi”
Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu.
“Sitaki hadithi nimekwambia mpe simu Mwasu sasa hivi na kama haiwezekani
nakata na usije kunilaumu” nikasisitiza
“Unadhani unaweza kuikimbia serikali?” Sulle kiganja akaniuliza kwa dharau.
“Ndani ya dakika kumi kuanzia sasa maiti ya afisa wako CID Dan Maro utaikuta
kwenye buti ya gari Mark II pembeni ya njia panda ya Kawe. Usiku mwema…”
nikaongea kwa hasira na kabla sijakata ile simu nikasikia.
“Mwasu huyu hapa zungumza naye” kitambo kifupi cha ukimya kikapita baada ya
sauti ya Sulle Kiganja kutoweka na hapo nikasikia sauti nyepesi ya kike ikiita upande
wa pili wa simu ile.
“Chaz…!”
“Mwasu…!”
“Bhee…!”
“Mwasu unaendeleaje?” nikamuuliza Mwasu kwa shauku
“Naendelea vizuri” Mwasu akanijibu hata hivyo nilipoitathmini vizuri sauti yake
nikagundua kuwa ilikuwa tulivu kupita kiasi na kile alichokiongea kilipingana kabisa
na hali yake.
“Upo wapi Mwasu?”
“Sipafahamu mahali hapa”
“Kuna watu wangapi hapo ulipo?” nikamuuliza Mwasu kwa utulivu na baada ya
kitambo kifupi cha ukimya nikamsikia akinijibu.
“Tupo watu nane humu ndani”
“Wamekutesa?”
“Hapana” Mwasu akaitikia kinyonge hata hivyo niligundua haraka kuwa alikuwa
akinidanganya kutokana na kushinikizwa kusema vile na watu waliomzunguka.
“Pole sana Mwasu muda siyo mrefu tutakuwa pamoja”
“Sitaki kufa Chaz nahitaji msaada wako” Mwasu akaongea kwa huzuni.
“Ondoa shaka Mwasu muda siyo mrefu watakuachia kwani hauna makosa
yoyote” nikaongea kwa utulivu nikijitahidi kumtia Mwasu moyo ingawa hadi kufikia
muda ule sikuona dalili zozote za kuweza kumuokoa kutoka katika mikono ya watu
wale na kabla Mwasu hajasema neno ile simu ikapokonywa haraka kutoka mikononi
mwake na hapo sauti ya Sulle Kiganja ikarudi tena hewani.
“Mwasu anaendelea vizuri kama ulivyomsikia”
“Hakuna haja ya kunieleza nimekwishazungumza naye tayari” nikawahi
kumkatisha Sulle Kiganja
“Afisa wangu Dan Maro anaendeleaje?”
“Amelala kwa sasa na daktari amesema asisumbuliwe” nikaongea kwa hila
“Usithubutu kumdhuru vinginevyo urafikiwetu utakwisha” Sulle Kiganja
akaongea kwa msisitizo
“Mimi na wewe hatuna urafiki Sulle usijidanganye”
“Unaweza kusema hivyo Chaz kwa vile unanichukia lakini mimi ni rafiki mwema
kwako” Sulle Kiganja akaongea kwa utulivu akiununua muda hata hivyo nilikuwa na
kila hakika kuwa vijana wake walikuwa kazini kuhakikisha wanainasa sauti yangu na
kuchunguza kuwa nilikuwa eneo gani kwa wakati ule ili waweze kunikamata na hilo
sikuwa na mashaka nalo kabisa. Nikiwa bado naendelea kufikiria mara sauti ya Sulle
Kiganja ikarudi tena hewani.
“Chaz…”
“Zungumza”
“Nimeona kuwa sihitaji kuendelea kumshikilia Mwasu hivyo kama utakubaliana
na mimi tunaweza kubadilishana. Wewe ukamchukua Mwasu wako na mimi
ukanikabidhi afisa wangu usalama,Dan Maro” nilimsikiliza vizuri Sulle Kiganja na
kugundua kuwa lile lilikuwa ni wazo la hila lenye lengo la kuandaa mapango mzuri
wa kunikamata. Hata hivyo niliishilia kutabasamu kwani sikuwa mbumbumbu kama
vile alivyokuwa akinifikiria huku mpango mpya ukianza kujengeka kichwani mwangu.
“Lini na wapi?” nikamuuliza
“Eneo la Mnazi mmoja saa nne kesho asubuhi”
“Saa sita mchana juu ya alama eneo la makutano ya barabara Uhuru Kariakoo”
nikaongea kwa hakika
“Mnazi mmoja ni sehemu nzuri isiyokuwa na msongamano…” Sulle Kiganja
akatetea hoja yake ya hila
“Nimesema saa sita mchana eneo la makutano ya barabara Uhuru Kariakoo nje ya
duka la simu za mkononi la Al-Mustaphar bila hila yoyote” nikasisitiza
“Okay!,okay!…usijali Chaz hakuna hila yoyote” hatimaye Sulle Kiganja
akakubaliana na hoja yangu na kabla hajatia neno jingine nikawahi kuikata simu
yangu na kuizima nikiitia mfukoni. Kisha nikaelekea mwisho wa korido ile na kuanza
kushuka ngazi na muda mfupi baadaye nilikuwa mbali na jengo lile la ghorofa laMillenium Architectures Dar es Salaam.
 
MARA BAADA YA CHAZ SIGA kukata simu Sulle kiganja akajizungusha
taratibu kwenye kiti chake cha ofisini akibembea kwa utulivu kutoka upande mmoja
na kwenda upande mwingine huku akiwatazama vijana wake wa kazi kwenye meza
ile ya ofisini namna walivyokuwa makini kuinasa sauti ya Chaz Siga na kuchunguza
kuwa muda ule mfupi alipokuwa akizungumza kwenye simu alikuwa eneo gani jijini
Dar es Salaam.
“Mmegundua nini?” Sulle Kiganja hatimaye akawauliza wale vijana huku wakiwa
bado wameziinamia kompyuta zao maalum na vifaa vyao vya kunasa sauti vikiwa
masikioni.
“This guy is very clever” mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya ujasusi cha usalama
wa taifa Micky Sengo akageuka taratibu kwenye kiti chake na kumtazama Sulle Kiganja
huku akionesha kukata tamaa.
“Nani?” Sulle Kiganja akauliza kwa shauku kabla ya kuwaamuru vijana wake
wengine wamchukue Mwasu na kwenda kumfungia kwenye kile chumba mle ndani.
“Chaz Siga”
“Kwa vipi?” Sulle Kiganja akauliza.
“Jana inaonekana alifanya mawasiliano na simu hii akiwa eneo fulani kando
ya ufukwe wa bahari ya hindi kati ya Osterbay,Msasani au Mbezi beach na sasa
inaonekana amepiga hii simu akiwa jengo la ghorofa la Millenium Architectures
eneo la Kigamboni. Inaovyoonekana ni kama ameshtukia kuwa tunaanda mtego wa
kumnasa hivyo anarukaruka kama ndama kutupotezea timing.
“Ondoa shaka!,bado kuna njia nyingine ya kumnasa Chaz Siga” Sulle Kiganja
akaongea kwa kujitapa.
“Njia ipi?”
“Kesho saa sita mchana makutano ya barabara ya uhuru kariakoo” maelezo ya
Sulle Kiganja yakampeleka Micky Sengo amtazame kwa utulivu bila kusema neno
kisha akawasha sigara na kuitia mdomoni.
_____
NIKIWA NDANI YA PANTONI wakati nikivuka bahari kutoka eneo la
Kigamboni na kuelekea Posta usiku huu nikajikuta nikishawishika kuwasha simu na
kutazama muda kwa vile saa yangu ya mkononi nilikuwa nimeisahau kule kwenye
chumba changu cha siri nilipokuwa na mateka wangu kachero CID Dan Maro. Hata
hivyo nikiwa katika harakati za kutazama muda baada ya ile simu yangu kuwaka mara
nikaiona namba ya simu ya mzee James Risasi ikianza kuita. Mshtuko ukanipata
kidogo kwa vile nilikuwa sijatarajia simu yoyote kutoka kwa mzee James Risasi
hususani muda ule hata hivyo baada ya kuyatembeza macho yangu na kuridhishwa na sura za watu waliokuwa eneo lile na hapo nikaipokea ile simu.
 
“Chaz…” sauti ya mzee James Risasi ikaunguruma upande wa pili.
“Shikamoo mzee,habari za kazi?”
“Naomba tuonane saa tatu usiku huu kwenye mgahawa wa Black Coffee eneo la
Namanga”
“Kuna shida gani mzee?” nikamuuliza kwa wasiwasi
“Fanya haraka” mzee James Risasi akamaliza kuongea na kukata simu na kwa
kweli alikuwa ameniacha njia panda huku nikishindwa kuelewa nini kilichokuwa
kikiendelea nami nikaizima simu yangu na kuitia mfukoni.
Muda mfupi baadaye lile Pantoni likatia nanga ukingoni upande wa pili wa Kivuko
kile huku nikiwa wa kwanza kushuka baada ya kulipangua kundi kubwa la abiria
waliokuwa wakijitahidi kushuka kwa pupa. Nilipofika nje ya kituo kile cha usafiri wa
Pantoni kwenye barabara ya Kivukoni nikakodi teksi na kumtaka dereva anipeleke
eneo la Namanga.
Yule dereva wa teksi haraka akaingia barabarani akiifuata barabara ya Balack
Obama Drive kandokando ya ufukwe wa bahari ya Hindi. Muda wa nusu saa baadaye
teksi niliyoikodi ikasimama nje ya mgahawa wa Black Coffee eneo la Namanga kisha
nikamlipa dereva pesa yake na ile teksi ilipoondoka nikavuka barabara nikielekea
ndani ya ule mgahawa na wakati nikifanya vile nikayatembeza macho yangu eneo lile
na kuiona gari nyeusi Toyota Prado ya mzee James Risasi ikiwa imeegeshwa katika
maegesho ya magari ya mgahawa ule.
Black Coffee ulikuwa mgahawa wa kisasa na wenye ubora stahiki. Ndani yake
kukiwa na meza nzuri za umbo duara zilizozungukwa na viti imara vya mbao za mti wa
Jakaranda,kuta zake zilipakwa rangi tulivu na safi zinazovutia. Madirisha yake mapana
ya mbao na vioo yalifunikwa kwa mapazia mepesi marefu yenye rangi rafiki kwa
macho ya binadamu. Kulikuwa na runinga mbili kubwa zilizofungwa mle ndani,moja
upande wa kushoto na nyingine upande wa kulia huku harufu nzuri ya vitafunwa
ikisambaa mle ndani. Wahudumu wake wasichana warembo walikuwa katika sare zao
safi za kazi na sura za kupendeza. Sehemu ambayo mtu yeyote angeweza kukaa muda
mrefu zaidi ya malengo aliyojiwekea. Mle ndani kulikuwa na watu wachache baadhi
yao wakiwa ni wazungu waliokuwa wamezama kwenye kusoma English novels huku
taratibu wakijipatia kahawa.
Nilimkuta mzee James Risasi akiwa ameketi kwenye meza moja iliyokuwa kwenye
kona ya upande wa kulia mle ndani ya mgahawa huku akijipatia kikombe cha kahawa
chukuchuku bila kitafunwa. Uso wake haukuwa mchangamfu kama nilivyozoea
kumuona hapo siku za nyuma. Alikuwa amevaa kofia nyeusi ya Pama,koti la suti refu
jeusi la kijivu lililoishia magotini,shati jeupe na tai nyeusi huku miwani yake kubwa ya
macho ikiwa imetuama vyema machoni mwake. Nilipofika kwenye ile meza nikavuta
kiti na kukaa,mhudumu alipokuja nikaagiza kikombe cha maziwa moto.
“Pole na kazi kijana wangu”
“Ahsante!,pole na wewe mzee”
“Nimesaliwa na mwaka mmoja tu wa kustaafu na sasa naona ni mbali sana
nimechoka na hii kazi” mzee James Risasi akaongea kwa utulivu huku akivuta funda
la kahawa na sikutaka kuamini kuwa yale yangekuwa ndiyo maongezi aliyoniitia.
“Ukistaafu utaelekea wapi?” nikamuuliza baada ya yule mhudumu kuniletea
kikombe cha maziwa na kuvuta funda moja.
“Kijijini kwangu Mwisenge,Musoma”
“Umekuwa mzee sasa,unawajukuu wangapi sasa?”
“Sina mke,mtoto wala mjukuu,nitajizika mwenyewe na pesa zangu za kiinua
mgongo” mzee James Risasi akaongea kwa utulivu na nilipomtazama usoni sikuona
chembe ya mzaha na jambo lile likanisikitisha sana.
“Pole sana!”
“Nimeugua kisukari kwa muda wa miaka mingi sana tangu ujana wangu,kisukari
sugu kikanipelekea nikose uwezo wa kuzalisha,wanawake wakawa wananikimbia
baada ya kushindwa kuwatimizia mahitaji yao ya kimwili. Hivyo sikuona sababu ya
kuoa na suala la watoto na wajukuu kwangu limekuwa ni ndoto ya mchana kweupe”
mzee James Risasi akaongea kwa utulivu kisha akavuta funda moja la kahawa na
kunitazama kwa makini kabla ya kuniuliza.
“Umefikia wapi na kazi yangu?” swali la mzee James Risasi likanipelekea nianze
kueleza kwa kifupi sana juu ya nilipofikia katika upelelezi wangu huku maeneo
muhimu nikimuahidi kuwa angekutana nayo kwenye ripoti nzima baada ya kukamilika.
Nilipomaliza kusimulia mzee James Risasi akavuta tena funda la kahawa na kuvunja
ukimya.
“Nataka kufahamu kama Mwasu amekamatwa akiwa na taarifa zozote zinazohusu
huu mkasa wa Mifupa 206”
“Ondoa shaka External hard disc yenye mafaili yote ya kiofisi ninayo mimi”
“Nataka uwe makini kwani sasa hivi unatafutwa kila kona ya jiji la Dar es Salaam
kwa gharama yeyote ile” mzee James Risasi akaongea kwa utulivu huku akinitazama
kwa makini na hapo nikavuta funda moja la maziwa na kuyatuliza vizuri macho yangu
nikimtazama.
“Ondoa shaka,hawawezi kunipata mpaka nitakapoikamilisha kazi yangu”
“Utafanya nini kuhusu Mwasu?” mzee James Risasi akaniuliza kwa udadisi
“Mpaka sasa bado sijafahamu nini cha kufanya ila kwa kuwa muda upo chochote
kinaweza kutokea”
“Taarifa nilizozisikia ofisini zinakutuhumu wewe kama muuaji wa maafisa
usalama,Guzbert Kojo,Pierre Kwizera,P.J Toddo,Masam na Remmy”
“Siwafahamu hao watu”
“Una hakika?” mzee James Risasi akaniuliza akionekana kutaka kupata hakika ya
jibu langu.
“Sina sababu ya kuwaua na hadi sasa bado sijawathibitisha kuhusika na kile
ninachokipeleleza”
“Unadhani nani atakuwa anahusika na vifo vyao?” mzee James Risasi akaniuliza
huku akiiondoa miwani yake machoni na kufikicha macho kabla ya kuirudishia.
“Hiyo ni kazi nyingine yenye malipo yanayojitegemea” nikaongea kwa utulivu na
kumpelekea mzee James Risasi atabasamu kidogo huku mawazo yangu yakihamia
kwa yule mwanamke hatari aliyeniokoa mikononi mwa wale wanausalama chini ya lile
jengo la ghorofa kule Posta. Kitambo kifupi cha ukimya kikafuata huku kila mmoja
akionekana kushughulika na kinywaji chake kabla ya kukumbuka jambo na kumuuliza
mzee James Risasi.
“Sulle Kiganja anawadhifa gani katika ofisi yenu?”
“Mkuu wa idara ya intelijensia ya ujasusi ya usalama wa taifa na kabla ya kupewa
wadhifa huo cheo hicho kilikuwa chini ya Abdulkadir Badru” mzee James Risasi
akafafanua na hapo nikamtazama kwa makini huku hoja mpya zikichipuka kichwani
mwangu.
“Kwanini Abdulkadir Badru aliondolewa kwenye wadhifa wake na kupewa huyo
Sulle Kiganja?”
“Baada ya kutokea kwa mauaji ya wanausalama hao unaoshukiwa kuwauwa kamati
ikamtuhumu Abdulkadir Badru kuwa ni mzembe” mzee James Risasi akafafanua.
“Sasa hivi Abdulkadir Badru ana wadhifa gani?”
“Ni afisa usalama wa taifa wa kawaida kabisa asiyekuwa na kazi maalum”
“Anaisha wapi hapa Dar es Salaam?” nikauliza kwa shauku huku nikimtazama
mzee James Risasi kwa makini.
“Block H,jengo la ghorofa la shirika la nyumba la taifa NHC,nyumba namba
14,mtaa wa Lugalo eneo la Upanga. Abdulkadir Badru ni rafiki yangu wa siku nyingi
kama una shida naye yoyote kupitia mimi hatoshindwa kukusaidia” jibu la mzee James
Risasi likanipelekea niupishe utulivu tena kichwani mwangu.
“Ukitoka hapa unaelekea wapi?” mzee James Risasi akaniuliza kwa utulivu baada
ya kitambo kifupi cha ukimya.
“Kanisa la The Last Day Gospel Ministry,nahitaji kuonana na Pastor Romanus
ana taarifa muhimu juu ya huu upelelezi wa mkasa wa Mifupa 206”
“Kuwa mwangalifu sana na nyendo zako huku ukitambua kuwa roho yako
inawindwa”
“Ondoa shaka”
Maongezi ya hapa na pale yakafuatia hadi pale tulipoonekana kutosheka na
vinywaji na hapo tukasogeza viti nyuma na kusimama kisha nikalipia vile vinywaji na
kuongozana na mzee James Risasi tukielekea nje ya ule mgahawa. Mara tu tulipotoka
nje ya ule mgahawa tukaagana huku tukikubaliana kuwasiliana tena katika kujulishana
hali ya mambo itakavyokuwa inaendelea.
Ilikuw a ni mara tu baada ya kuachana na mzee James Risasi nje ya mgahawa
ule huku yeye akielekea sehemu alipoegesha gari lake na mimi nikitembea taratibu
kuelekea kwenye kituo cha teksi kilichokuwa jirani na eneo lile pale nilipoliona gari
moja aina ya Landcruiser jeupe likichomoza na kuja mbele yangu. Kuliona gari lile
hisia mbaya zikaniingia akilini na nilipogeuka nyuma kumtazama mzee James Risasi
nikamuona kuwa alikuwa amebakiwa na hatua chache kulifikia gari lake kwenye
yale maegesho ya magari. Nilipoyarudisha macho yangu kulitazama lile gari jeupe
Landcruiser lililokuwa likija mbele yangu likawa tayari limenifikia na hapo nikaona
kioo kimoja cha dirisha la ubavuni kikishushwa haraka kisha ukachungulia mkono
wa mtu ulioshika bastola. Sikutaka kusubiri zaidi hivyo nikawahi kujirusha na kujitupa
mtaroni huku mvua ya risasi ikifuatia nyuma yangu. Hata hivyo mlengaji yule alikuwa
amechelewa kwani mara tu nilipoingia kwenye ule mtaro wa kando ya ile barabara
nikaingia chini ya daraja dogo la mfereji ule kujikinga na risasi zile. Ile Landcruiser
haikusimama badala yake mara tu iliponipita kule mbele nikasikia milio miwili ya risasi
na kisha nikaisikia injini ya ile gari ikiyoyoma na kutokomea zake.
Niliendelea kujibanza ndani ya lile daraja dogo kwa dakika kadhaa nikijihakikishia
usalama wangu kisha nikaichomoa bastola yangu kutoka mafichoni na kutoka sehemu
ile nikielekea kwenye yale maegesho ya gari la mzee James Risasi. Wakati nikifika eneo
lile moyo wangu ukaingiwa na baridi ya ghafla kabla ya simanzi kuziteka fikra zangu.
Nilimkuta mzeeJames Risasi akiwa amelala chini kwenye maegesho yale hatua
chache kabla ya kulifikia gari lake. Kifuani alikuwa na matundu mawili ya risasi
yaliyokuwa yakivuja damu nyingi. Alikuwa ametulia kimya huku mdomo na macho
yake vikiwa wazi kama mtu anayetazama mbingu ingawa nilipomsogelea na kumshika
shingoni sikuona mjongeo wowote wa damu. Mwili wake ulikuw a ukipoa taratibu
huku uhai ukiwa mbali na nafsi yake. Mzee James Risasi tayari alikuwa amekata
roho. Niliendelea kumtazama mzee James Risasi huku machozi yakinilengalenga
hata hivyo sikuwa na namna ya kufanya. Nilipogeuka na kuyatembeza macho yangu
eneo lile nikaona kuwa watu walishaanza kukusanyika hivyo sikutaka kupoteza muda
badala yake haraka nikampekua mzee James Risasi mifukoni na kuchukua vitu vyote
alivyokuwanavyo na hatimye kutoweka haraka eneo lile.
 
MAONGEZI YA SIMU KATI YA mzee James Risasi na Chaz Siga yalikuwa
yamenaswa vizuri na mkuu wa idara ya mawasiliano ya kijasusi ya usalama wa taifa
Micky Sengo huku akishirikiana na vijana wake wa kazi baada ya namba za simu zote
za wanausalama kuwa zimeunganishwa katika mfumo wa kitaalam unaomuwezesha
opareta kuweza kusikia kila kitu pale namba ya simu ya afisa usalama mmoja
inapopigiwa au kumpigia mtu mwingine.
Taarifa zile zilipomfikia Sulle Kiganja haraka akawatuma vijana wake kuelekea
eneo la Namanga sehemu kulipokuwa mgahawa wa Black Coffee huku kwa mara
ya kwanza akijiridhisha kuwa mwanausalama mwenzao mzee James Risasi ndiye
aliyekuwa akivujisha nje taarifa za kijasusi za idara ya usalama wa taifa. Lakini bado
akishindwa kuelewa kuwa mzee James Risasi alikuwa na mahusiano gani na Chaz
Siga,mtu hatari waliyekuwa wakimsaka kila kona kama shilingi ya mkoloni.
_____
MWILI WANGU ULIKUWA MLE NDANI lakini fikra zangu zilikuwa nje
kabisa ya eneo lile kwenye ulimwengu wa sayari nyingine kabisa ya masafa marefu.
Kifo cha mzee James Risasi kilikuwa kimenihuzunisha sana na kuacha kovu kubwa
lisilofutika kamwe moyoni mwangu. Kila nilipotulia na kuupisha utulivu nafsini
mwangu zile sauti za milio ya risasi zilizohitimisha safari ya uhai wa mzee James Risasi
hapa duniani zikaendelea kuchukua nafasi kubwa katika mawazo yangu na kunipelekea
niugue maradhi ya fedheha na unyonge kwenye mtima wangu. Ni dhahiri kuwa wauaji
wale hawakuwa na sababu za kutosha za kuukatisha uhai wa mzee James Risasi ingawa
kwa upande mwingine taratibu zake za kazi zingetosha kabisa kumshtaki kwa kitendo
cha kuvujisha siri za usalama kwa mtu asiyehusika ambaye sikuwa na shaka yoyote
kuwa mtu huyo ni mimi.
Nikiwa bado nimezama kwenye fikra zile swali moja likaibuka katikati ya
fikra zangu kuwa wale wauaji ambao sikuwa na shakanao kuwa walikuwa ni
wanausalama,waliwezaje kufahamu kuwa mimi na mzee James Risasi tulikuwa
ndani ya ule mgahawa wa Black Coffee kule Namanga?. Jibu sikulipata hata hivyo
nilipozidi kufikiri wazo fulani likachipua kichwani mwangu na kunipa faraja kiasi cha
kushawishika kuuchomoa mche mmoja wa sigara kutoka kwenye pakiti niliyoinunua
kando ya duka moja lililokuwa karibu na kituo cha teksi kule Namanga na kuibana
kwenye pembe moja ya mdomo wangu kabla ya kuilipua kwa kiberiti changu cha gesi
huku taratibu nikijiegemeza kwenye siti moja ya nyuma ya ile teksi.
Mwanga wa kile kiberiti ukawa umemshtua kidogo yule dereva wa teksi na
kumpelekea ageuke haraka na kunitazama kupitia kwenye kioo cha mbele cha mle
ndani kilichokuwa chini ya paa ya ile teksi. Hata hivyo dereva yule akaishilia kunitazama
pasipo kusema chochote huku akigeuka na kuingiza gia kabla ya kukanyaga mafuta
katika ile barabara ya Balack Obama Drive iliyokuwa ikikatisha kandokando ya
ufukwe wa bahari ya Hindi,nikielekea eneo la Posta sehemu lilipokuwa kanisa la The
Last Days Gospel Ministry. Nilikuwa nimekodi teksi ile muda mfupi baada ya lile
tukio la kuuwawa kwa mzee James Risasi kule eneo Namanga nje ya mgahawa wa
Black Coffee.
Wazo moja lilikuwa limenijia akilini. Miongoni mwa vitu nilivyokuwa nimevipata
muda ule baada ya kumaliza kuipekua maiti ya mzee James Risasi mifukoni ilikuwa ni
simu yake ya mkononi,kitambulisho cha kazi,kadi mbli za ATM za benki tofauti na
bastola moja ndogo iliyojazwa risasi. Hivyo haraka nikaichukua ile simu ya mzee James
Risasi na kuanza kuichunguza kwa makini. Sikuona chochote hadi pale nilipouondoa
mfuniko wa betri ya simu ile na kuuchunguza ndani yake.
Kidude kidogo mfano wa kifungo chembamba sana cheusi. Kinasa sauti
kinachoweza kusafirisha mawimbi ya sauti kwa umbali wa maelfu ya maili nyingi
kilikuwa kimepandikizwa kwa hila katika mfuniko wa betri wa simu ile ili kunasa
maongezi ya namna yoyote ambayo simu ile ingetumika kuyafanya. Sasa nilikuwa na
hakika kuwa wakati ule mzee James Risasi alipokuwa akinipigia simu nikiwa kwenye
Pantoni kutokea jengo la ghorofa la Millenium Architectures eneo la Kigamboni
nilipoenda kuwasiliana na Sulle Kiganja kwa simu kama mkakati wangu wa kumzuia
kutekeleza mipango yake ya kunikamata kwa urahisi basi maongezi yetu yalikuwa
yakisikika moja kwa moja na watu wale hatari. Hali iliyowapelekea waweze kufahamu
kwa urahisi mahali tulipokuwa na hatimaye kutufikia.
Bila kusita nikawa nimeiwasha ile simu na ilipowaka mara nikaiona ikianza kuita
na nilipochunguza kwa makini kuwa mpigaji wa simu ile angekuwa nani nikaliona jina
la Sulle Kiganja. Pasipo kujiuliza nikaipokea ile simu na kuiweka sikioni bila kusema
neno lolote na kwa kufanya vile nikaisikia sauti ya Sulle Kiganja ikianza kuita upande
wa pili. Sikuwa na neno lolote la kuzungumza badala yake nikajikuta nikimlaani Sulle
Kiganja moyoni mwangu kwa kufanya kitendo cha kihuni cha namna ile cha kumpigia
simu marehemu. Hatimaye nikaikata ile simu na kuizima kisha nikaitia mfukoni.
Muda mfupi baadaye ile teksi ikasimama barabara ya mtaa wa pili nyuma ya ule
mtaa wenye lile kanisa la The Last Days Gospel Ministry huku lengo langu likiwa ni
kuhakikisha hali ya usalama wangu kwanza kabla ya kulifikia kanisa lile. Nikamlipa
dereva wa ile teksi pesa yake na kushuka. Ile teksi ilipoondoka tu eneo lile nikavuka
barabara na kuanza kutembea taratibu na kwa tahadhari kuelekea nyuma ya mtaa ule
huku mkono wangu ukiwa ndani ya mfuko wa koti langu umeikamata bastola tayari
kwa kumdhibiti mtu yeyote ambaye angejitokeza mbele yangu na kuniwekea kizingiti.
Sikupata upinzani wa namna yoyote na baada ya safari ndefu kidogo ya miguu
hatimaye nikapita getini na kuufikia mlango wa mbele wa kanisa la The Last Days
Gospel Ministry na hatimaye kuusukuma. Mara tu nilipoingia mle ndani nikagundua
kuwa lile kanisa lilikuwa limemezwa na ukimya wa aina yake. Mapazia meupe marefu
na mepesi yalikuwa yakipepea taratibu kufuatia upepo mwanana wa usiku uliokuwa
ukipenya kupitia kwenye madirisha makubwa ya kanisa lile.
Mle ndani mbele ya kanisa sehemu ya madhabahu kulikuwa na mishumaa
mikubwa mitatu iliyokuwa juu ya meza moja ndefu yenye umbo mstatili iliyofunikwa
kwa kitambaa cheupe chenye msalaba mkubwa mwekundu uliyodariziwa kwa ustadi.
Mishumaa ile ikiteketea taratibu na kuangaza mle ndani. Nikapiga hatua chache
na kusimama katikati ya kanisa lile huku nikiyatembeza macho yangu mle ndani.
Sikumuona mtu yeyote na jambo lile likanipa wasiwasi na kujiuliza kama muda ule
Pastor Romanus angekuwa ndani ya lile kanisa au lah!.
Hata hivyo sikukata tamaa badala yake nikazidi kujongea taratibu nikielekea
sehemu ya mbele ya lile kanisa na kwa kufanya vile nikagundua kuwa nyuma ya
ile meza ya madhabahu mbele ya kanisa lile kulikuwa na mtu aliyeketi kwenye kiti
huku akiwa katika mavazi ya utukufu kama yale niliyokuwa nimemuona nayo Pastor
Romanus siku ile nilipofika mle ndani kwa mara ya kwanza japokuwa sikuweza kuiona
vizuri sura ya mtu yule kwa vile alivyokuwa ameketi kwa utulivu na kuiinamia meza ile
akionekana kusoma maelezo kwenye kitabu fulani. Hata hivyo kitendo cha yule mtu
kuinua macho yake na kunitazama haraka na kisha kuendelea kusoma kile kitabu pale
mezani pasipo kunikaribisha wala kutia neno lolote kikawa kimenishangaza sana huku
nikijipa moyo kuwa huenda Pastor Romanus alikuwa tayari amenisahau.
Nilitaka kusogea karibu zaidi ya ile meza ya pale madhabahuni mle ndani kanisani
ili niweze kumsalimia kwa karibu zaidi yule mtu aliyeketi kwenye kile kiti huku
nikiamini kuwa angekuwa ndiye Pastor Romanus na hivyo salamu yangu ya karibu
ingempelekea anitazame vizuri na kunikumbuka. Hata hivyo hilo halikutokea kwani
wakati nilipokuwa nikikaribia ile meza haraka nikagundua kuwa yule mtu aliyeketi
kwenye kile kiti nyuma ya meza ile hakuwa mzee kama alivyokuwa Pastor Romanus
ingawa pia alikuwa amevaa vizuri yale mavazi ya utukufu.
Kile kitabu alichokuwa akikisoma yule mtu pale mezani nikakitambua haraka
kuwa ilikuwa ni Biblia ingawa nilipoichunguza kwa makini ile Biblia haraka nikashtuka
baada ya kuuona mdomo wa bastola ukichungulia chini yake. Yule mtu hakuinua tena
macho yake kunitazama badala yake akawa amezama katika kusoma maelezo fulani
yaliyokuwa kwenye kurasa ile.
Wasiwasi ukiwa tayari umeanza kuniingia haraka nikayapeleka macho yangu na
kuyatembeza jirani na eneo lile na kwa kufanya vile mara nikaiona michirizi ya damu
nyingi ya kitu kilichoburutwa na kupelekwa kwenye uchochoro mmoja uliokuwa
upande wa kushoto wa ile madhabahu. Nywele zikanicheza,moyo wangu ukapiga kite
kwa nguvu,koo likanikauka ghafla na hapo utulivu ukahama kabisa kichwani mwangu.
Hatimaye uvumilivu ukanishinda hivyo haraka nikaupeleka mkono wangu mafichoni
kuichukua bastola. Lakini tayari nilikuwa nimechelewa kwani muda uleule nikasikia
sauti ya kiume ikinionya nyuma yangu huku mdomo baridi wa bastola ukikitekenya
kisogo changu.
“Tupa bastola yako chini Chaz Siga na usithubutu kufanya hila yoyote”
Kwa kweli nilijihisi kuchanganyikiwa nikataka kugeuka nyuma na kumtazama yule
mtu kuwa angekuwa nani. Lakini wakati nikiwa katika harakati zile mara nikajikuta
nikikatizwa na yule mtu aliyekuwa ameketi nyuma ya ile meza pale madhabahuni kwa
namna alivyoupenyeza mkono wake haraka chini ya ile Biblia na kuichomoa bastola
yake mafichoni. Kisha akaikamata vyema bastola ile mkononi kabla ya kusimama kwa
utulivu huku akiielekezea kifuani kwangu.
Muda uleule wakachomoza watu wengine wawili kutoka kwenye vichochoro
vilivyokuwa upande wa kulia na kushoto wa lile kanisa pale madhabahuni kutokea
kwenye vyumba vya maandalizi ya neno huku wakiwa na bastola zao mkononi katika
mavazi nadhifu ya suti. Nilipogeuka kutazama nyuma yangu nikamuona mwanaume
mmoja makini aliyeikamata vyema bastola yake mkononi na kuielekeza kwangu na
nilipotazama kule kwenye mlango wa kanisa nikawaona wanaume wengine wawili
wakiwa wamesimama mlangoni. Nilijua kuwa nisingeweza kufurukuta tena dhidi
ya watu wale hatari waliojidhatiti kikamilifu hivyo baridi nyepesi ya hofu ikapenya
taratibu moyoni mwangu na kunipelekea nijione mzembe kwa kutokuwa makini.
“Nahitaji kuonana na Pastor Romanus tafadhali!” nikajiongelesha kwa sauti huku
nikihisi kuchanganyikiwa.
“Nani aliyekwambia kuwa huu ni muda wa ibada?” yule mtu mbele yangu
akaniuliza swali la kipuuzi lililowapelekea wale wenzake waangue kicheko cha mahoka
mle ndani. Sikuwa na namna nyingine ya kufanya hivyo nikaitoa bastola yangu taratibu
na kuiweka chini sakafuni.
“Pastor Romanus yuko wapi?” nikauliza huku nikijidai sielewi mada
“Rafiki yako amekufa” yule mtu mbele yagu akaongea kwa utulivu kisha akasogea
pale niliposimama na kunichapa ngumi mbili za tumbo zilizonipelekea nihisi kutaka
kutapika.
“Mmemuua Pastor Romanus…?” nikauliza kwa hasira huku nikiugulia maumivu
ya tumbo.
“Haikuwa kazi rahisi hata hivyo tulilazimika kufanya hivyo” yule mtu akajitapa
“You bastard you killed God’s servant…?” nikauliza kwa mshangao na hapo nikajikuta
nikitandikwa ngumi nyingine mbili kavu za mgongoni zilizonipelekea nianze kuhisi
kichomi.
“Chaz Siga!...umetusumbua kwa muda mrefu lakini hatimaye tumekutia mikononi.
Usijaribu kuleta hila za kutoroka kwani bahati huwa haijitokezi mara mbili na mimi
nitakuwa mtu wa kwanza kukushindilia risasi za kutosha ukafie mbali” yule mtu
akajitapa huku akinizunguka taratibu na kunitazama kwa dhihaka.
“Mnashida gani na mimi?” nikawauliza wale watu na nilipowatazama vizuri
nikajiridhisha kuwa sura zao zilikuwa ngeni kabisa machoni mwangu ingawa
nilifahamu fika kuwa wale wangekuwa makachero waliotumwa na Sulle Kiganja
kunikamata.
“Hatuna muda mrefu wa majadiliano na wewe. Tuambie, CID Dan Maro yuko
wapi?” yule mtu aliyekuwa akinizunguka akaniuliza huku akinipekua mifukoni. Hata
hivyo hakuambulia kitu chochote kwa vile vitu vyagu nilikuwa nimeviweka mafichoni
kwenye mfuko wa siri wa lile koti sehemu isiyofikika kirahisi na mtu asiye makini.
“Kachero wenu CID Dan Maro yupo sehemu salama kabisa ondoeni shaka”
nikaongea kwa utulivu.
“Sehemu salama wapi?” yule mtu aliyekuwa akinipekua akaniuliza hata hivyo
nikalipuuza swali lake na kutumbukiza langu.
“Kwanini mmemuua Pastor Romanus kama kweli shida yenu hasa ilikuwa ni
mimi?”
“Alijitia mkaidi vinginevyo tusingekuwa na bahari naye” yule mtu akanijibu na
baada ya kukohoa kidogo akaendelea.
“Unaweza kujiuliza ni kwa namna gani tumeweza kuigundua sehemu yako hii
ya tambiko kirahisi namna hii. Jibu ni kuwa kazi ilikuwa rahisi tu kwani mara tu
ulipofanikiwa kututoroka siku ile kwenye lile eneo la Botanical Garden huku ukipitia
eneo la chini kwenye mifereji ya maji machafu tulianza kufanya uchunguzi wa kina
na makini tukiwauliza watu na kuchunguza maeneo tuliyoyashuku. Hatimaye turufu
yetu ikaangukia hapa na majibu ya kiongozi wako wa kiroho baada ya kumbana vizuri
akatueleza kuwa ulikuwa hapa. Siri moja tu rafiki yako aliyokufa nayo moyoni ni kuwa
hakutueleza kuwa ulifika hapa kufanya nini.
Hatutaki kuamini kabisa kuwa ulifika hapa kwa sababu za kiimani kwa vile
mikono yako imetapakaa damu za watu wasio na hatia. Hivyo tunaamini kuwa
kuna sababu nyingine zaidi ya hiyo ambayo hatuna wasiwasi wowote kuwa muda
utakapofika utazungumza kila kitu. Safari ya kwanza baada ya kutoka hapa tunaelekea
moja kwa moja sehemu ulipomficha CID Dan Maro na baada ya hapa Sulle Kiganja
atakuwa anakusubiri kwa hamu sana ofisini kwake” yule mtu aliyeonekana kuwa ndiye
kiongozi wao akajitapa kwangu na muda uleule akanisogelea mbele na kunivisha pingu
mikononi na wakati akifanya vile macho yangu yakawa yameweka kituo na kuitazama
vizuri ile michirizi ya damu iliyoelekea upande wa kushoto kwenye uchochoro hafifu.
Michirizi ile ya damu ikanifanya nianze kuvuta picha namna risasi za wauaji wale
zilivyotumika kuukatisha uhai wa Pastor Romanus. Hasira zikanipanda kichwani hata
hivyo sikuwa na namna ya kufanya badala yake nikameza funda kubwa la mate na
kupiga moyo konde. Mara tu yule mtu alipomaliza kunifunga ile pingu tukaanza safari
ya kutoka mle ndani huku mawazo mengi yakipita kichwani mwangu.
Nilifahamu fika kuwa namna yoyote ya kujiokoa kutoka mikononi mwa wale watu
nilipaswa kuwa makini kwa vile ulinzi niliyokuwa nimewekewa ulikuwa mkubwa tena
wa watu walionekana kuwa makini na nyendo zangu. Hata hivyo nilifahamu kuwa
endapo ningekubali kuchukuliwa na wale makachero basi ile ndiyo ingekuwa hatua
ya kwanza ya kuelekea kwenye kifo cha kinyama chenye mateso makali ya jasho la
damu kwani ni dhahiri kuwa ukweli wowote ambao ningejitetea nao kuwa mimi siyo
niliyehusika na mauaji ya makachero wenzao usingenisaidia kitu.
Sasa nilikuwa nikitembea kwa tahadhari ya hali ya juu katikati ya korido pana
iliyopakana na mabenchi katikati ya kanisa lile kuelekea nje huku nikiwa chini ya
ulinzi mkali. Nyuma yangu walikuwa watu watatu,mmoja akiwa ni yule kiongozi
wao,wawili wakiwa ni wale vijana waliokuwa wamejificha kule kwenye vichochoro
vya madhabahuni kuelekea kwenye vyumba vya kuandaa neno. Mbele yangu alikuwa
amenitangulia mtu mmoja tu ambaye ndiye yule aliyekuwa ameielekezea bastola yake
kisogoni kwangu. Nilipotazama kule mbele kwenye ule mlango wa kanisa nikawaona
wale wanaume wengine wawili wakinisubiri kwa protokali zote za ulinzi huku mmoja
akiwa amesimama upande wa kushto wa ule mlango wa kanisa na mwingine akiwa
amesimama upande wa kulia,wote wakiwa na bastola zao mikononi.
Tuliendelea kutembea kwa utulivu na tulipofika katikati ya lile kanisa kumbukumbu
ya lile tukio la kuuwawa kwa mzee James Risasi na taswira ya ile michirizi ya damu
isiyokuwa na hatia ya Pastor Romanus kule madhabahuni ikavuka kiwango cha
mwisho cha uvumilivu wangu. Sikuona sababu ya kuendelea kusubiri hivyo kwa
kasi ya upepo nikasafiri kwa hatua moja zaidi mbele yangu kisha nikatupa teke moja
makini nikiupiga ule mkono ulioshika bastola wa yule mtu mbele yangu. Ile bastola
ikamponyoka mkononi na kuruka hewani tukio ambalo lililowashangaza sana wale
wenzake na kuwapelekea washindwe kufanya maamuzi ya haraka.
Wale makachero wakiwa bado wanashangaa shangaa nikajitupa hewani kama
kivuli na kumtandika yule mtu mbele yangu mateke mawili matata ya mgongoni
yaliyomtupa vibaya kwenye mabenchi yaliyokuwa upande wa kushoto eneo lile.
Kisha nilipotua chini ile bastola ya yule kachero ikawa imeangukia mikononi mwangu
huku nikiserereka sakafuni na kupotelea kwenye uvungu wa mabenchi yaliyokuwa
jirani na eneo lile nyuma yangu nikikoswakoswa na risasi kadhaa za wale makachero.
Mapigano ndani ya hekalu la Mungu ilikuwa ni zaidi ya laana kwa wanadamu lakini
kwa kuwa uhai wangu ulikuwa mbioni kununuliwa kwa gharama ya risasi sikuwa na
namna nyingine ya kujihami.
Risasi nyingi zikawa zikirindima na kunifuata nyuma yangu kwenye yale mabenchi
ya kanisa hata hivyo kutokana na giza hafifu la mle ndani wale makachero wakapoteza
malengo ya shabaha na kuishia kuvunja mbao za mabenchi yale kwa risasi huku
mimi nikitambaa chini kwa chini. Wale makachero walipoona kuwa nilikuwa mbioni
kuwatoroka wale wenzao waliokuwa wamesimama kule mlangoni haraka wakawahi
kuja mle ndani kuongea nguvu. Kachero mmoja akashika uelekeo wa upande wa
kushoto kwenye uchochoro mdogo uliokuwa kati ya yale mabenchi ya kanisa na ukuta
huku yule kachero mwingine akianza kaparamia yale mabenchi moja baada ya jingine
na bastola yake mkononi akitazama chini kunitafuta. Hata hivyo hakufanikiwa kafika
mbalimbali kwani nilijibanza na kumsubiri hadi pale aliponikaribia kisha nikaikamata
vyema bastola yangu. Risasi mbili nilizozifyatua moja ikakilenga kiganja cha ule
mkono wake uliyoshika bastola na kukikata vibaya kidole chake tukio lililopelekea ile
bastola aliyoishika ianguke chini. Risasi nyingine ikapasua vibaya mifupa ya goti lake
na hapo akapiga yowe kali na kuanguka chini akiparanganya vibaya na yale mabenchi
na kulia kama mtoto.
Nikiwa chini ya yale mabenchi haraka nikayatembeza tena macho yangu na kuiona
miguu ya yule mwenzie akinikaribia kwa jazba. Tabasamu jepesi likapita usoni mwangu
na hapo nikajiviringisha vizuri na kuvuta kilimi cha bastola yangu mkononi. Risasi
moja ikapasua kifundo cha mguu wake na kumpelekea apige yowe kali la maumivu
na alipotua chini kwenye ile sakafu macho yetu yakakutana na hapo nikamuona yule
kachero akanisihi sana kwa ishara na kuniomba msamaha kuwa nisiukatishe uhai
wake na kwa kujenga uaminifu akinitupia ile bastola yake katika namna ya kunionesha
kuwa alikuwa hataki tena upinzani na mimi. Sikumuacha badala yake nikamlegeza
kwa risasi mbili za kiuno ambazo zingempelekea atembelee kiti cha walemavu kwa
sehemu yake ya maisha iliyosalia hapa duniani.
Muda uleule mvua kubwa ya risasi ikaanza tena kurindima mle ndani ya lile kanisa
huku risasi zile zikinifuata pale chini ya benchi nilipojibanza. Mbao za mabenchi ya
eneo lile zikaanza kipukutika ovyo na vibanzi vyake kuniangukia. Zile risasi sasa zikawa
zikinikosakosa na kunifanya nianze kuhisi hatari ya kifo ikinikaribia. Nilitaka kuanza
tena hila yangu ya kutambaa chini ya yale mabenchi ili kuikwepa mvua ile ya risasi
lakini mara moja nafsi yangu ilinionya kuwa mjongeo wowote ambao ningeufanya wa
kuhama eneo lile ningekuwa nimetoa mwanya mzuri wa shambulio la hakika la risasi
dhidi yangu na hali ile ingekuwa hatari zaidi. Hivyo nikiwa nimejibanza pale chini ya
benchi nikaanza kupiga akili nyingine ya haraka ya kujinasua.
Mle ndani ya kanisa sasa nilikuwa nikishambuliwa na makachero wanne baada ya
wale wawili kuwa nimefanikiwa kuwapunguza nguvu kama siyo kuwatuliza kabisa.
Nilipochungulia na kuwatazama wale makachero waliokuwa wakinishambulia
nikagundua kuwa wawili kati yao walikuwa nyuma yangu wakinishambulia kutoka
nyuma ya nguzo moja ya kanisa na makachero wengine wawili waliosalia walikuwa
kwenye korido pana ya katikati ya kanisa.
Wazo fulani likawa limenijia akilini. Kutoka pale uvunguni mwa lile benchi
nilikojificha nisingeweza kuwashambulia kwa urahisi wale makachero waliokuwa
kwenye ile korido ya katikati ya kanisa lakini juu yao kwenye dari ya lile kanisa
kulikuwa na feni nyingi kubwa za pangaboi zilizotundikwa kupunguza joto la mle
ndani wakati wa ibada. Hivyo bila kupoteza muda nikaikamata tena vyema bastola
yangu mkononi na kufanya mashambulizi matatu makini kuelekea kwenye vishikizo
vya zile feni kwenye dari ya lile kanisa.
Muda uleule nikaziona feni tatu zikianguka chini kwa kasi ya ajabu usawa wa wale
makachero wawili pale walipokuwa. Wale makachero kwenye ile korido hawakuwa
wameelewa vizuri ni maana ya shambulio lile hivyo wakawa wanashangaa shangaa
na muda uleule feni mbili kati ya zile tatu zikawaangukia vichwani na kuwaangusha
chini. Ile feni moja iliyosalia ikatua kwenye mabenchi ya jirani na eneo lile na kuanza
kurukaruka ovyo huku mapangaboi yake yakitishia usalama. Wale makachero
walioangukiwa na zile feni hawakufurukuta wala kusimama pale chini na hapo nikajua
kuwa walikuwa kwenye hali mbaya sana huku damu ikiwatoka kwenye majeraha ya
miili yao yaliyotokana na kukatwa vibaya na mapangaboi ya zile feni.
Sasa mle ndani kukawa kumesaliwa na makachero wawili tu ambao nao kwa
wakati ule walikuwa wameacha kufyatua risasi na hivyo kupelekea mle ndani ya kanisa
kutawaliwa na ukimya wa aina yake. Zile kelele za milio ya risasi zilikuwa zimewashtua
njiwa waliokuwa wamejenga viota vyao kwenye paa la lile kanisa na sasa njiwa wale
walikuwa wakipukutisha mbawa zao na kukimbia eneo lile.
Niliendelea kujibanza chini ya lile benchi huku nikiupima utulivu wa mle ndani na
nilipoona kuwa hakukuwa na rabsha nyingine taratibu nikaanza kutambaa chini ya yale
mabenchi kuelekea mbele ya lile kanisa. Baada ya muda mfupi nikawa nimefika kule
mbele hivyo nikatoka kwenye yale mabenchi na kwenda kujibanza kwenye kona moja
ya lile kanisa nikisikilizia kama kungekuwa rabsha zozote huku bastola yangu ikiwa
mkononi. Bado sikusikia kitu chochote ingawa nilikumbuka kuwa yale mashambulizi
ya risasi yaliyokuwa yakitokea nyuma yangu wakati ule yalikuwa yakitokea kwenye
nguzo moja kubwa ya kanisa lile ambayo haikuwa mbali sana kutoka pale nilipojibanza.
Mle ndani ya kanisa hali bado ilikuwa tulivu hivyo nikaanza kunyata taratibu
nikielekea kwenye ile nguzo kubwa ya kanisa na kwa kufanya vile mara nikamuona
kachero mmoja akichomoka kutoka kwenye ile nguzo na kuanza kukimbia akielekea
kule kwenye ule mlango mkubwa wa kanisa huku akigeuka na kuanza kunishambulia
kwa risasi. Kuona vile haraka nikawahi kujitupa chini na kujikinga mbele ya benchi
moja lililokuwa jirani na eneo lile na kwa kuwa sikutaka yule mtu anitoroke mle ndani
hivyo haraka nikajiviringisha sakafuni kuelekea kwenye ile korido ya katikati ya
ya kanisa
na nilipofika nikatafuta mhimili mzuri na kufyatua risasi moja kumlenga yule kachero
aliyekuwa mbioni kuufikia ule mlango wa kanisa ili atoke nje.
Muda uleule mara nikamsikia yule mtu aliyekuwa akikimbia akipiga yowe kali la
maumivu huku akisombwa na kutupwa hewani kabla ya kuanguka chini. Ile risasi yangu
moja ilikuwa imempata kwenye paja la mguu wake wa kushoto. Hata hivyo yule mtu
alikuwa na roho ngumu kama ya paka kwani haukupita muda mrefu mara nikamuona
akisimama tena na kuchechemea huku mkono wake wa kushoto ukijitahidi kuusaidia
kuukokota ule mguu wake wenye jeraha na hivyo kukaza mwendo tena akikimbia kwa
taabu kuufuata ule mlango wa kanisa ili atoke nje.
Sikutaka kumpa yule mtu nafasi ya kunitoroka hivyo nikavuta tena kilimi cha
bastola yangu kuisukuma risasi nyingine. Shabaha yangu makini ikapelekea risasi ile
nyingine kupenya kwenye paja la mguu wake mwingine wa kulia na hapo nikamsikia
yule kachero akipiga yowe jingine kali la maumivu kabla ya kutupwa mbele na kuanguka
chini kwenye ile korido katika mtindo wa kupiga magoti kama mtu anayeungama
dhambi zake kanisani. Huku akiutazama ule mlango wa kanisa hatua chache mbele
yake.
Yule kachero mmoja aliyesalia mle ndani kuona vile akawa ameshikwa na kihoro
hivyo kufumba na kufumbua akakurupuka kutoka kwenye maficho yake gizani na
kuanza kuparamia dirisha moja jembamba lililokuwa karibu na ile madhabahu ya
kanisa na hatimaye kujirusha nje kabla ya kusikia kishindo kikubwa cha mwanguko
wake chini ya lile dirisha huku risasi zangu mbili zikimkosakosa na kumpunyua begani.
Muda mfupi uliyofuata mara nikasikia sauti za vishindo vya hatua za yule kachero
akitimua mbio na kuyoyomea mbali na lile kanisa. Yule kachero akawa amefanikiwa
kunitoroka.
Bila kupoteza muda zaidi mle ndani haraka nikatafuta funguo za ile pingu
niliyofungwa mikononi kutoka katika mfuko wa koti la suti la yule kachero kiongozi
aliyeangukiwa na feni mojawapo la mle ndani kisha nikajifungua ile pingu na kuitupa
kando. Muda mfupi uliyofuata nikarudi tena kule madhabahuni na kuanza kuifuatilia
ile michirizi ya damu iliyokuwa imeelekea kwenye ule uchochoro wa upande wa
kushoto wa ile madhabahu.
Nilimkuta Pastor Romanus akiwa amaketi chini kwenye kona moja ya kichochoro
cha upande wa kushoto wa madhabahu ile huku akiwa katika mavazi yake ya kiraia
ya shati jeupe,suruali nyeusi ya kitambaa na viatu vya ngozi vya rangi ya udongo
miguuni. Nilimposogelea na kumshika shingoni sikuona dalili zozote za uhai na mwili
wake tayari ulikuwa wa baridi roho yake tayari ikiwa imefika kwenye sayari nyingine.
Nilipozidi kumchunguza vizuri Pastor Romanus nikagundua kuwa tumboni alikuwa
na majeraha mengi ya risasi yaliyokuwa ukingoni kuvuja damu. Macho yake alikuwa
ameyafumba ingawa mdomo wake ulikuwa wazi. Mikononi alikuwa ameikumbatia
Biblia ndogo iliyotapakaa damu. Huzuni ikanishika hata hivyo sikuwa na namna badala
yake nikainama pale chini na kumfumba vizuri mdomo wake kisha nikaichukua ile
Biblia ndogo kutoka mikononi mwake huku nikiwa nimekata tamaa kabisa ya kupata
taarifa zozote za kunisaidia kwenye harakati zangu
Niliendelea kumtazama mzee yule rafiki yangu mwenye ufahamu wa elimu ya juu
ya mambo mengi ya ulimwengu huu kisha nikageuka na kuanza kuondoka taratibu
eneo lile huku mkononi nikiwa nimeichukua ile Biblia yake iliyotapakaa damu.
Nilipofika katikati ya ile madhabahu ya kanisa sikuona haja tena ya kuondoka
na ile Biblia kwa kuwa ilikuwa imetapakaa damu nyingi ya Pastor Romanus. Hivyo
nikaelekea kwenye ile meza ya kanisa yenye mishumaa nikipanga kuitelekeza ile Biblia
juu yake. Lakini wakati nikiwa katika harakati zile nafsi yangu ikajikuta ikishawishika
kuifunua ile Biblia na kwa kuwa sikuona sababu yoyote ya kupingana na msukumo ule
moyoni mwangu nikaamua kusimama na kisha kuifunua ile Biblia. Hatimaye macho
yangu yakatua juu ya kurasa ya kwanza nyeupe ya kitabu kile iliyoandikwa kwa hati
inayosomeka vizuri.
Gabbi Masebo & Milliam Casian
Wishing you all the best in your wedding day
Revelation 13;17-18
Welcome to heaven night club
Dar es Salaam
Saturday 6th,July-2005
Oga & White Sugar
Nilipozidi kupekuwa kwenye kurasa za ile Biblia katikati nikakuta picha moja ya
zamani ya wanandoa wakiwa katika mavazi yao ya kupendeza ya harusi na nyuma yao
walikuwa wamesimama wasimamizi wa ndoa ile mwanamke na mwanaume. Yule
mwanamke msimamizi wa ile ndoa haraka nilimfahamu kuwa alikuwa ndiye yule
dada niliyepambana naye ndani ya lile jengo la ghorofa la waabudu shetani lililoko
maeneo ya Posta Dar es Salaam siku ile akifahamika kwa jina la Oga. Yule mwanaume
kwenye ile picha sikuwahi kumuona hata siku moja katika harakazi zangu na kutoka
pale nikiwa nimeanza kupata muunganiko mzuri wa matukio ya nyuma ingawa picha
bado ilikuwa haijakamilika.
Ingawa nilikuwa siifahamu vizuri Biblia na maandiko yake lakini kwa namna
moja au nyingine hisia za kuwa Pastor Romanus alikuwa ameniachia ujumbe fulani
kupitia kitabu kile zikawa zimeanza kujengeka kichwani. Hivyo bila kupoteza muda
nikaichukua ile Biblia na kuifuta ile damu iliyotapakaa nikitumia kile kitambaa
kilichokuwa juu ya ile meza ya madhabahu na kuitia mfukoni. Kisha haraka nikaanza
kuondoka eneo lile nikikatisha katikati ya lile kanisa kuelekea nje huku mawazo mengi
yakipita kichwani mwangu. Usikuwa bado ulikuwa unamengi ya kuzungumza.
 
Back
Top Bottom