MARA BAADA YA CHAZ SIGA kukata simu, sulle Kiganja akaipiga simu ile
akirudiarudia mara tatu zaidi bila mafanikio mwishowe akakata tamaa kabisa baada
ya kuhisi kuwa ile simu ya Chaz Siga ingekuwa imezimwa upande wa pili. Kisha
taratibu akageuka na kuwatazama maafisa usalama wenzake waliokuwa wakiyafuatilia
maongezi yale kwa makini wakiwemo Fulgency Kassy,Pweza na Kombe waliokuwa
wamekuja kumletea ripoti juu ya kutoweka kwa yule dada aliyesemekana kuhusika na
kifo cha meneja wa benki ya Zanzibar Marine ndugu Aden Mawala.
“CID Dan Maro bado mzima na lazima tufanye namna ya kumuokoa” Sulle
Kiganja akavunja ukimya huku akivigongesha vidole vyake mezani katika namna ya
kufikiri zaidi na hatimaye akayatembeza tena macho yake kuwatazama wale maafisa
usalama wengine mle ndani.
“Ningeshauri tusubiri kwanza hadi hiyo saa mbili usiku Chaz Siga atakapokupigia
simu na kuzungumza na wewe”.Tiblus Lupogo,mwanausalama kutoka kitengo
maalum cha upelelezi cha ofisi ya mashtaka DPP akatoa ushauri.
“Tunahitaji vijana wetu wataalam wa masuala ya mawasiliano watakaoweza
kufuatilia na kujua huyu Chaz Siga alikuwa akizungumza kutoka eneo gani halafu
baada ya hapo tutaanda mtego mzuri wa kumnasa” afisa usalama na mwanakamati
ya kudumu ya ulinzi na usalama ya jijini Dar es Salaam,Siraju Chenga akashauri kwa
utulivu huku ameyatuliza macho yake kufikiria jambo.
“Mimi siamini kuwa muuaji mkubwa kama huyu Chaz Siga anaweza kukosa
umakini kiasi cha kufanya mawasiliano yatakayopelekea kukamatwa kwake kirahisi
namna hiyo. Ngoja tusubiri hadi hiyo saa mbili usiku tukiwa na vijana wetu wa
mawasiliano na kama wataweza kutambua kuwa simu hii imepigwa kutokea wapi basi
tutakuwa na nafasi nzuri ya kumnasa” mkuu wa kamati ya dharura ya usalama na itikadi
za jeshi la wananchi Luteni Kanali Davis Mwamba akafafanua kabla ya wachangiaji
wengine kuendelea huku kila mmoja akionekana kuridhishwa na mchakato mzima wa
mikakati ya kumnasa Chaz Siga.
Kwa kuwa ripoti kutoka kwa Fulgency Kassy,Pweza na Kombe ilikuwa imejaa
viashiria vyote kuwa yule dada muuaji wa meneja wa benki ya Zanzibar Marine
alikuwa ameelekea kisiwani Zanzibar hivyo Sulle Kiganja hakuona sababu ya
kuendelea kupoteza muda badala yake akawataka Fulgency Kassy,Pweza na Kombe
haraka waondoke usiku ule na kuelekea kisiwani Zanzibar na kuhakikisha yule dada
anakamatwa kabla hajafika mbali.
Mara baada ya Fulgency Kassy,Pweza na Kombe kuondoka mle ndani majadiliano
ya kina yakaendelea zaidi baina ya wale makachero wa usalama katika mkutano ule
mfupi wa dharura.
“Uchunguzi nilioufanya kupitia vijana wangu umeanza kunipa uelekeo mzuri
kuwa huyu Chaz Siga na huyu mwanamke anayesemekana kuhusika na kifo cha
meneja wa benki ya Zanzibar Marine hawana mahusiano na pengine hawajuani kabisa.
Lakini vilevile taarifa za uchaguzi kutoka kwa vijana wangu zinaonesha kuwa bastola
iliyokuwa ikimilikiwa na meneja wa benki ya Zanzibar Marine haikuwa ikimilikiwa
kihalali na mmiliki wake anaonekana kuwa ni raia wa kisiwani Zanzibar mwenye jina
la Khalid Makame ingawa uchunguzi wa zaidi bado unaendelea” Sulle Kiganja akatoa
ufafanuzi wa kina.
“Mimi nina wazo jipya kidogo” Tiblus Lupogo akavunja tena ukimya na hapo
wote wakageuka na kumtazama kwa shauku kabla ya kuendelea.
“Kwa muda mrefu tangu kutokea kwa haya mauaji ya wanausalama wenzetu
nimekuwa nikifanya uchunguzi na kugundua kuwa wanausalama wote hawa
waliouwawa walikuwa katika tume ya udhibiti na upambanaji wa biashara haramu
ya dawa za kulevya iliyoteuliwa na mheshimiwa rais hapa nchini. Sasa hamuoni kuwa
huwenda hawa wanausalama wenzetu wanaweza kuwa wanauwawa kama sehemu ya
kuwafumba midomo na kupoteza ushahidi juu ya kile wanachokifahamu kuhusiana
na uchunguzi unaofanywa na tume yao?” hoja ya Tiblus Lupogo ikaonekana
kuwaingia vizuri wale wanausalama na hivyo kuibua minong’ono mingi huku kila
mmoja akizumza kwa mtazamo wake kuhusiana na hoja ile. Hatimaye Siraju Chenga
akuvunja ukimya.
“Nadhani hata mimi nimeanza kukubaliana na hoja hii lakini swali ni kwamba
mnadhani ni nani anayeweza kuwa nyuma ya mpango huu wa kuwafumba midomo
wanausalama wenzetu?”
“Anayeweza kufanya hivyo ni dhahiri anapaswa kuwa ni mtu mwenye madaraka
ya juu zaidi kama siyo wafanyabiashara wenye nguvu kubwa ya pesa” Tiblus Lupogo
akafafanua.
“Mimi ningependekeza kuwa mmiliki wa benki ya Zanzibar Marine naye
achunguzwe” Sulle Kiganja akapendekeza huku akiwatazama wanausalama wenzake
walioketi kwenye meza ya umbo duara yenye nane vilivyokaliwa na wanausalama wa
idara tofauti.
“Hilo nadhani halina mjadala na baada ya hapa nitatoa warrant ya kufanyika kwa
uchunguzi dhidi ya benki ya Zanzibar Marine” M.D Kunzugala mkurungenzi mkuu
wa idara ya usalama taifa akatanabaisha. Majadiliano machache yakaendelea kabla
ya kikao kile cha dharura kufika ukomo na wanausalama wale kuaga na kuondoka
wakikubaliana kukutana tena.
Mara baada ya maafisa usalama wale kuondoka mle ofisini wakabaki M.D
Kunzugala na Sulle Kiganja wakifanya majadiliano mengine ya kina zaidi kabla ya
kufikia hitimisho huku wakiwa wamekubaliana kuweka mfumo wa siri wa mawasiliano
kwa maafisa wote wa usalama waliokuwa kwenye kikao kile kama mkakati wa
upelelezi katika kutaka kufahamu kama kungekuwa na kuvuja kwa taarifa. Hatimaye
Sulle Kiganja na M.D Kunzugala wakaagana kila mmoja akishika majukumu yake.
_____
BOTI ALIYOIPANDA Koplo Tsega ilitia nanga kwenye bandari ya kisiwani
Zanzibar huku tayari usiku ukiwa umeshaingia. Kama ilivyo miji mingine ya pwani hali
ya hewa ya Zanzibar ilikuwa imetawaliwa na joto lenye upepo wa wastani. Mwanga
kutoka kwenye meli kubwa za mizigo za safari za masafa marefu zilizotia nanga katika
nanga bandarini pale kwa mbali mwanga wa taa kutoka katika majumba ya kale ya
ghorofa yaliyopakana na ufukwe wa bahari ya Hindi ulipelekea ziada nyingine katika
kuongeza uzuri wa mandhari ile.
Safari haikuwa ndefu sana lakini haikuwa imemzuia Koplo Tsega kutongoa walau
lepe moja la usingizi na sasa alikuwa ameshtuka kutoka usingizini baada ya sauti kali
ya honi ya meli kusikika wakati boti ile ilipokuwa ikitia nanga bandarini. Koplo Tsega
haraka akageuka na kuyatembeza macho yake kuwatazama abiria waliokuwa eneo
lile na kitendo cha kumuona kila mtu akisimama na kuanza kuchukua mzigo wake
ikawa ni ishara tosha kuwa safari ile ilikuwa imefika tamati. Hivyo haraka na yeye
akachukua begi lake na kulivaa mgongoni kisha akasimama na kuunga msafara wa
abiria waliokuwa wameanza kushuka kwenye boti ile huku mawazo juu ya yule mtu
aliyekuwa akifahamika kama White Sugar yakianza kuumbika tena kichwani mwake.
Akiwa anaendelea kushuka kwenye ile boti Koplo Tsega akajikuta akiwakumbuka
Fulgency Kassy,Pweza na Kombe huku hisia za kuwa huwenda wangefanya maamuzi
ya kuja kisiwani Zanzibar kumtafuta zikitengeneza ushawishi katika mawazo yake.
Hata hivyo alijipa matumaini kuwa jina la Shamsa Hafidhi alilolitumia kuiabiri boti ile
lisingekuwa na maana yoyote kwao hivyo akajipa moyo kuwa bado alikuwa salama.
Mara tu Koplo Tsega alipomaliza kushuka na kutoka kwenye bandari ile ya
Zanzibar akatembea kwa utulivu kuelekea kwenye maegesho ya teksi yaliyokuwa
nje kidogo ya eneo lile. Kijana mmoja dereva wa teksi aliyekuwa amejitega kusubiri
abiria akawa wa kwanza kumuona na kumkaribisha kwenye teksi yake kwa bashasha
zote. Koplo Tsega akatabasamu kidogo na alipoifikia ile teksi kwenye maegesho yale
akafungua mlango wa nyuma na kuingia huku akigeuka nyuma na kutazama kama
kungekuwa na mtu yeyote akimfuatilia. Hakumuona mtu yeyote na hali ile ikampa
faraja kuwa bado alikuwa salama. Yule dereva wa teksi alipofungua mlango na kuingia
mle ndani akageuka na kumuuliza Koplo Tsega kwa utulivu.
“Unaelekea wapi dada?”
“Nipeleke eneo la Changa,unapajua?” Koplo Tsega akauliza huku kumbukumbu
ya kisiwa cha Zanzibar ikiwa bado imehifadhika vyema kichwani mwake.
“Ondoa shaka napafahamu vizuri sana Changa,ndiyo wewe unapoishi?” yule
dereva akauliza huku akiitoa ile teksi kwenye maegesho yale hata hivyo Koplo Tsega
hakumjibu badala yake akatumbukiza swali kwenye maongezi yale.
“Utanitoza pesa kiasi gani?”
“Utanipa elfu kumi na tano tu dada yangu,bei ya mafuta imeongezeka sana” yule
dereva wa teksi akajitetea kabla hajaombwa kupunguza hali iliyompelekea Koplo
Tsega ajikute akitabasamu.
“Endesha gari” Koplo Tsega akaongea kwa utulivu na hapo safari ikaanza huku
ile teksi ikiacha maegesho yale na kushika uelekeo wa upande wa kulia kuifuata
barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha kandokando ya bahari ile na hapo Koplo Tsega
akajiegemeza taratibu kwenye siti ya nyuma ya ile teksi.
Tangu utawala wa kwanza wa Sultan Majid bin Said hadi utawala wa mwisho wa
Sultan Jamshid bin Abdallah kabla ya kupatikana kwa uhuru wa mtu mweusi kisiwa
cha Zanzibar kimekuwa ni mji wa kale uliozungukwa na magofu ya zamani mazuri
yaliyokuwa makazi ya watawala na walowezi kutoka uajemi.
Muda huu wa usiku kandokando ya barabara ile kuelekea mji wa Stone Town
wachuuzi wa samaki walikuwa wameweka meza zao na kuendelea kuuza bidhaa
mbalimbali pamoja na samaki. Wenyeji kwa wageni watalii kutoka mataifa mbalimbali
duniani walionekana kutembea kwa miguu na kufanya manunuzi katika mtindo wa
maisha unaowafurahisha. Hoteli mbalimbali za kitalii zilionekana kupandwa katika
baadhiya maeneo ya pwani ya bahari ya Hindi na hivyo kuongeza uzuri wa mandhari
ya usiku ya kisiwa kile.
Baada ya safari ndefu kidogo hatimaye ile teksi ikaingia barabara ya Mizingani
iliyokuwa ikipakana na ufukwe wa bahari ya Hindi upande wa kulia. Safari ikaendelea
huku teksi ile ikilipita eneo la Old Customs House halafu mbele kidogo ikalipita eneo
la Palace Museum. Hata hivyo kabla ya kulifikia eneo la Forodhani Garden dereva
wa teksi ile akakunja kona kuingia upande wa kushoto akikatisha katikati ya barabara
ya mtaa wa Nyumba ya Moto iliyokuwa ikipakana na magofu mengi ya kale. Safari
ile ikaendelea hadi pale walipoifikia barabara ya Jamatin ambapo yule dereva aliingia
upande wa kulia akiifuata barabara iliyokuwa ikitokezea kwenye Msikiti wa Jamat
Khana. Dereva wa ile teksi alipoupita ule msikiti mbele kidogo akaingia upande wa
kulia akiifuata barabara ya kuelekea Changa.
“Nishushe hapo mbele ya huo mgahawa wa Café Laaziz” Koplo Tsega
akamwambia yule dereva wa teksi baada ya kuuona mgahawa ule maarufu ambao
mbele yake kulikuwa na meza nyingi zilizokuwa na vitafunwa vya kila aina kama
chapati, vipande vya pweza, vitumbua, kalimati, kachori, kababu, kashata, maandazi,
tambi, bagia na vingine vingi vyenye majina ya asili.
Ile teksi iliposimama Koplo Tsega akafungua pochi na kumlipa yule dereva wa teksi
pesa yake kisha akafyatua kabari ya mlango na kushuka akielekea kwenye ule mgahawa
huku akifahamu fika kuwa macho ya yule dereva wa teksi yalikuwa yakimsindikiza
nyuma yake. Akiwa mle ndani yule dereva wa teksi akaendelea kumtazama Koplo
Tsega kwa utulivu hadi pale alipoingia kwenye ule mgahawa na hapo ndiyo akawasha
gari na kugeuza akirudi kule kwenye kijiwe chake alipotoka.
Lengo la Koplo Tsega likiwa ni kuondoa ushahidi juu ya wapi alipokuwa akielekea
mara tu alipohakikisha kuwa ile teksi iliyombeba ilikuwa imegeuza na kuondoka nje
ya ule mgahawa haraka na yeye akatoka nje ya ule mgahawa na kukodi bajaji moja kati
ya bajaji nyingi zilizokuwa eneo lile akimtaka dereva ampeleke eneo la soko la zamani
la watumwa ama Old Slave Market. Dereva wa bajaji ile kijana machachari akaanza
safari haraka akiifuata barabara ya Mtaa wa Kajificheni iliyokuwa ikikatisha katikati ya
makazi ya watu. Baada ya safari ndefu hatimaye dereva yule akakunja kona na kuingia
upande wa kushoto akiifuata barabara ya New Mkunazini na baada ya kitambo kifupi
cha safari ile bajaji hatimaye ikasimama eneo la Old Slave Market. Koplo Tsega
haraka akamlipa yule dereva pesa yake na ile bajaji ilipogeuza na kurudi ilipotoka
akaanza kutembea kwa miguu akielekea mbele ya ile barabara hadi pale alipoyafikia
makutano ya barabara ya Benjamin Mkapa na barabara ya Karume. Alipofika pale
akavuka makutano yale ya barabara na kukodi tena pikipiki ya Vespa akimtaka dereva
ampeleke mahali lilipokuwa duka kubwa la Zanzibar Stone City Bazaar. Dereva wa
pikipiki ile alikuwa kijana wa mjini aliyeujua vizuri mji na vichochoro vyake hivyo
haraka akashika uelekeo wa upande wa kulia akiifuata barabara ya Benjamini Mkapa
kisha akaipita shule ya Haile Selassie upande wa kulia hadi pale alipoyafikia makutano
mengine ya barabara ya Benjamini Mkapa,barabara ya Mapinduzi na barabara ya
Kawawa ambapo aliingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Kawawa.
Safari ikaendelea huku ile pikipiki ikilipita eneo la The State University of Zanzibar
kwa upande wa kulia na mbele kidogo akilipita jumba kubwa la Majestic Cinema. Hatua
chache mara baada ya ile pikipiki kulipita lile jengo la Majestic Cinema yule dereva
akaingia upande wa kulia eneo la Kibokoni ambapo alipofika mbele akashika uelekeo
wa barabara ya Sokomuhogo na baada ya safari fupi hatimaye ile pikipiki ikaenda
kusimama nje ya duka kubwa la kisasa lenye maandishi makubwa yanayosomeka juu
yake Zanzibar Stone City Bazaar. Kuona vile Koplo Tsega akatabasamu kidogo kisha
akushuka na kufungua pochi yake akitoa pesa na kumlipa yule dereva wa pikipiki.
Yule dereva wa pikipiki akaipokea ile pesa na kuitia mfukoni kisha akawasha pikipiki
yake na kutokomea mitaani.
Kwa sekunde kadhaa Koplo Tsega akasimama ng’ambo ya barabara ile
akilichunguza kwa makini lile jengo la Zanzibar Stone City Bazaar huku akishangazwa
sana na uwekezaji mkubwa wa biashara wa namna ile. Hapakuwa na shaka yeyote
kuwa duka lile lilikuwa ndiyo duka kubwa na la kisasa katika eneo lote la Stone Town.
Kupitia kuta safi za vioo za duka lile la kisasa bidhaa za kila namna zilionekana ndani
yake.
Nje ya jengo lile kwenye eneo la maegesho kulikuwa na magari machache
yaliyoegeshwa labda kwa vile muda ulikuwa umeanza kuyoyoma kwani maduka
mengi ya kisiwani Zanzibar yalikuwa tayari yamefungwa. Kadiri Koplo Tsega
alivyokuwa akilitazama lile jengo la Zanzibar Stone City Bazaar ndivyo taswira ya
yule mtu aliyekuwa akifahamika kama White Sugar ilivyokuw a ikijengeka upya katika
fikra zake. Hatimaye akavuka barabara ile kuelekea upande wa pili na kisha kuanza
kutembea akielekea kwenye mlango mkubwa wa lile duka la Zanzibar Stone City
Bazaar na muda mfupi baadaye alikuwa mle ndani.
Kama yalivyokuwa maduka mengi makubwa ya mijini ya kisasa duka la Zanzibar
Stone City Bazaar halikuwa tofauti sana kwani mle ndani kulikuwa bidhaa za kila
namna zilizopangwa vizuri katika maeneo tofauti kutegemeana na aina ya bidhaa
yenyewe. Mle ndani kulikuwa na raia wengi wa kigeni waliofika kufanya manunuzi
huku wakizunguka korido moja ya bidhaa kwenda nyingine na vitoroli vidogo vya
kusukuma kwa mikono vyenye magurudumu madogo na vitenga cha kubebea bidhaa
nyingi kwa pamoja.
Upande wa kushoto wa lile duka kulikuwa na rafu nzuri za mbao zenye bidhaa
zilizopangwa katika mtindo unaovutia. Mara baada ya kuingia mle ndani upande wa
mbele kulikuwa na sehemu zenye mashine za kusoma thamani ya bidhaa kando yake
wakiwa wameketi wafanyakazi wa duka lile. Upande wa kulia kulikuwa na maduka ya
simu na vifaa vya umeme.
Koplo Tsega taratibu akapiga hatua zake hafifu kuelekea kwenye yale maduka
ya simu na wakati akifanya vile macho ya watu waliokuwa mle ndani yakamtazama
kwa utulivu huku yakionekana kuvutiwa na namna ya uvaaji wake. Ndani ya duka la
kwanza la simu aliketi msichana mweupe mlimbwende mwenye asili ya bara la Asia
aliyevaa Baibui.
“Habari za kazi?”
“Salama karibu sana” yule dada akaongea kwa utulivu huku akimtazama
KoploTiglis Tsega
“Ahsante” Koplo Tsega akaitikia huku akijitia kutazama simu zilizokuwa
zimepangwa katika rafu za vioo za lile duka na wakati akifanya vile pia akawa
akiyachunguza vizuri mandhari ya mle ndani. Kutoka pale kwenye lile duka la simu
za mkononi upande wa kushoto kulikuwa na ngazi za kuelekea sehemu ya juu ya
lile jengo kulipokuwa na ofisi za utawala za lile duka. Hivyo kwa namna moja au
nyingine Koplo Tsega alijikuta akiwaza kuwa White Sugar angeweza kuwa ndani ya
ofisi mojawapo kati ya zile. Baada ya muda mfupi wateja wengine wakawa wameingia
mle ndani na kufika pale kwenye duka la simu na hivyo kuongeza idadi ya watu eneo
lile hali iliyompelekea Koplo Tsega kuweza kufanya uchunguzi wake kwa uhuru zaidi.
Koplo Tsega akiwa bado anaendelea kununua muda pale kwenye lile duka la simu
ghafla mlango mmoja kati ya milango mingi ya vyumba vya utawala vilivyokuwa juu
ya lile jengo ukafunguliwa. Koplo Tsega haraka akageuka na kutazama kule juu. Mara
baada ya mlango ule kufunguliwa wakatoka wanaume watatu wote wakiwa katika
mavazi nadhifu ya suti na kuanza kutembea kwa haraka wakazifuata zile ngazi za
kushukia sehemu ya chini ya lile duka katika korido pana iliyozuiliwa na ukuta mfupi
wa mabomba ya vyuma.
Mara moja moyo wa Koplo Tsega ukapoteza utulivu,damu ikamchemka
mwilini,nywele zikamcheza na jasho jepesi likaanza kumtoka. Miongoni mwa wale
wanaume watatu mmoja wao alikuwa ni yule aliyefahamika kwa jina la White Sugar
ambaye Koplo Tsega alikuwa amemkumbuka vizuri kuwa ndiye yule aliyepishananaye
mlangoni kule kwenye lile duka jingine la Zanzibar Stone City Bazaar lilioko Mlimani
City Shopping Mall jijini Dar es Salaam. White Sugar alikuwa katika muonekano wake
uleule wa awali pasipo kubadili mavazi. Upande wake wa kushoto na kulia kulikuwa
na vijana wawili waliokuwa wakitembeanaye sambamba kama walinzi wake huku
mmoja akiwa amebeba Briefcase nyeusi ambayo Koplo Tsega aliikumbuka vyema
kuwa ilikuwa ni ileile aliyomuonanayo White Sugar kule jijini Dar es Salaam.
Wakati White Sugar akishuka ngazi na wale wapambe wake kuelekea lile eneo
la chini kwenye lile duka kubwa la Zanzibar Stone City Bazaar njiani akapishana na
wafanyakazi wawili wa lile duka wakiwa katika sare zao za kazi ambapo walimsalimia
kwa heshima zote huku yeye akiitikia salamu zao kwa kupunga mkono kivivuvivu
kama mtu asiye na muda. Koplo Tsega akaendelea kumtazama vizuri White Sugar na
wapambe wake namna alivyokuwa akizishuka ngazi zile kwa madaha kama mfalme
katika utukufu wake na kupitia mwanga mkali wa taa zilizokuwa ndani ya jengo lile
Koplo Tsega akajiridhisha vizuri kuwa White Sugar alikuwa mwanaume mweusi sana
kuwahi kuonekana duniani angawaje afya na rangi yake ya ngozi viliusanifu vizuri
mwenekano wake wa hali ya ukwasi.
Mara tu alipomaliza kushuka zile ngazi White Sugar na wapambe wake wakashika
uelekeo wa upande wa kulia wakiufuata mlango mdogo uliokuwa kwenye kona moja
ya lile jengo. Wafanyakazi wa lile duka kuona vile wakawa ni kama vile waliotekwa
umakini huku wakijisogeza karibu na kumsalimia kwa bashasha zote za kirafiki ambapo
aliwaitikia kwa kuwapungia mkono kivivuvivu kama kawaida yake kisha White Sugar
akamuita mtu mmoja aliyekuwa eneo lile amevaa suti nyeusi na kumnong’oneza
jambo. Yule mtu akawa ni kama anayepokea maelekezo fulani yaliyompelekea ageuke
na kutazama kwenye lile duka la simu jambo ambalo Koplo Tsega hakulielewa maana
yake.
White Sugar alipoufikia ule mlango uliokuwa kwenye kona ya lile duka mpambe
wake mmoja kati ya wale vijana wawili akawahi mbele na kuufungua ule mlango na
hapo White Sugar akapita kisha wale vijana wapambe wakafuatia nyuma yake kabla
ya mlango ule kufungwa. Koplo Tsega alipotazama juu ya ule mlango akaona kibao
cha rangi nyeusi chenye maandishi makubwa meupe yakisomeka EXIT DOOR-For
Administration use only.
Kuona vile Koplo Tsega hakutaka kuendelea kusubiri hivyo taratibu akalitoroka
lile kundi la watu waliokuwa wamesimama nje ya lile duka la simu na kushika uelekeo
wa upande wa kushoto ulipokuwa mlango wa kutoka nje ya lile duka la Zanzibar Stone
City Bazaar. Mara tu alipotoka kule nje akaambaa na ukuta akielekea kwenye kona lile
jengo.Hata hivyo kabla hajafika mara akajikuta akisita na kujibanza baada ya kusikia
muungurumo wa injini ya gari likiacha maegesho ya magari ya lile jengo. Haukupita
muda mrefu mara gari kubwa aina ya Ford jeusi likayaacha maegesho yale na kuingia
kwenye ile barabara ya lami iliyokuwa ikikatisha mbele ya lile jengo la Zanzibar Stone
City Bazaar likishika uelekeo wa upande wa kushoto kuifuata barabara ya mtaa wa
Sokomuhogo eneo la Kibokoni kuelekea kwenye ile kona ya Majestic Cinema.
Lilikuwa tukio la kushtukiza ambalo Koplo Tsega hakuwa amelitarajia kwani White
Sugar na wapambe wake walikuwa wakiondoka eneo lile na kuelekea kusikojulikana.
Kuona vile Koplo Tsega akaiacha ile kona na kuanza kutafuta usafiri wa haraka eneo
lile hata hivyo hakufanikiwa kwani lile eneo halikuwa na kituo cha usafiri wa namna
yoyote hivyo akajikuta akianza kutimua mbio kulifukuza lile gari kwa nyuma kama
mwehu na lile gari likaendelea kutimua mbio likitokomea. Koplo Tsega akaendea
kukimbia akilifukuza lile gari lakini mwendo wake haukufua dafu kwani baada ya
muda mfupi tu lile gari likawa limetokomea kabisa mbele yake na hivyo kwa mara
nyingine White Sugar akawa ameponea kwenye tundu la sindano kitendo ambacho
Koplo Tsega alikilaani sana.
Hapakuwa na tumaini jingine la kumfikia White Sugar usiku ule hivyo Koplo
Tsega akaamua kuchepuka na kuifuata barabara nyingine iliyokuwa upande wa kulia
wa ikikatisha katikati ya majengo marefu ya ghorofa ya kale katika mtaa uliokuwa na
utulivu na ukimya wa aina yake huku mawazo mengi yakipita kichwani mwake.
Ile barabara ilikuwa tulivu mno na isiyokuwa na pilika zozote za binadamu
huku ikiangazwa kwa taa hafifu kutoka katika nguzo za taa zilizokuwa kando yake.
Wakati Koplo Tsega akiendelea kutembea katika barabara ile akajikuta akiyakumbuka
matukio yote yaliyojili tangu siku ya kwanza alipoingia jijini Dar es Salaam akitokea
eneo la Kivu ya kaskazini,jamhuri ya kidemokrasia ya nchi ya Kongo.
Ilikuwa ni wakati alipokuwa mbioni kufika mwisho wa barabara ile ili aingie
upande wa kushoto kwenye barabara nyingine pale alipokumbuka kutazama nyuma
nyake. Kwa kufanya vile mara moja baridi nyepesi ya ghafla ikasambaa mgongoni
mwake huku moyo wake ukipiga kite kwa nguvu.
Kulikuwa na wanaume wawili waliokuwa wakija kwa haraka nyuma yake kwenye
barabara ile. Mwanaume mmoja alikuwa akitembea upande wa kushoto na mwingine
akitembea upande wa kulia na mwendo wao wa haraka ulitia mashaka. Koplo Tsega
kuona vile akaongeza mwendo huku akiendelea kugeuka nyuma na kuwatazama
wale watu mara kwa mara huku hofu ikiwa imeanza kumuingia na alipoifikia ile kona
ya barabara kuingia upande wa kushoto sehemu kulipokuwa na barabara nyingine
iliyokuwa ikikatisha katikati ya majengo ya kale ya ghorofa makazi ya watu akaanza
kutimua mbio. Koplo Tsega akaendelea kutimua mbio hadi pale alipofika mwisho wa
ile barabara ambapo haraka akachepuka upande wa kulia na kwenda kujibanza kwenye
kona moja ya jumba bovu la kale lililotelekezwa miaka mingi iliyopita ambalo sasa
lilikuwa halitumiki kama makazi ya binadamu kisha akageuka nyuma na kuchungulia
kule alipotoka.
Koplo Tsega akiwa bado amejibanza kwenye ile kona haukupita muda mrefu
mara akawaona wale wanaume wawili wakichomoza kwenye kona ya ile barabara na
kuanza kutimua mbio wakija upande ule wa ile barabara kwenye ile kona ya jumba
bovu alipokuwa bado amejibanza. Koplo Tsega alipowachunguza kwa makini wale
watu akagundua kuwa walikuwa wameshika bastola mikononi mwao hali iliyopelekea
hofu ya kukabiliana na hatari ianze kuchipua taratibu moyoni mwake. Wale watu
wakaendelea kutimua mbio na walipofika pale kwenye ile kona wakapunguza mwendo
na hatimaye kusimama huku wakishauriana kuwa washike uelekeo upi kwa vile ile
barabara ilikuwa imegawanyika katika barabara kuu mbili. Barabara moja ikinyoosha
mbele na nyingine ikiingia upande wa kulia mbele ya lile jumba bovu.
“Atakuwa ameelekea wapi?” mmoja akasikika akimuuliza mwenzake kwa sauti ya
chini.
“Nahisi ni kwenye barabara hii hii kwani kama angekuwa amenyoosha kule mbele
kwa vyovyote tungekuwa tumemuona tu” mwenzake akasikika akitengeneza hoja
kisha kitambo kifupi cha ukimya kikafuatia huku wale watu wakiwa bado wamesimama
eneo lile kabla ya kushaurina jambo na kuanza kusogea taratibu kwenye kona ya lile
jengo bovu la kale. Koplo Tsega kuona vile taratibu akaicha ile kona aliyojibanza na
kuingia ndani kabisa ya lile jumba bovu huku akienda kujibanza kwenye kona moja
iliyokuwa na giza zaidi.
Haukupita muda mrefu mara wale watu nao wakaingia mle ndani ya lile jumba
bovu huku wakinyata kwa tahadhari na bastola zao mikononi. Walipofika katikati
ya lile jumba wakashauriana kitu kisha mmoja akaanza kupanda ngazi na kuelekea
sehemu ya juu ya lile jengo kwa mwendo wa kunyata. Yule mtu mwingine aliyesalia
pale chini akaanza taratibu kuzunguka kwenye kona za vyumba vya lile jengo
lisilokuwa na madirisha wala milango. Kuona vile Koplo Tsega akaichomoa bastola
yake yenye kiwambo maalum cha kuzuia sauti kutoka mafichoni na kuikamata vyema
mkononi. Yule mtu aliyebaki chini ya lile jengo akavikagua vyumba vyote vya chini
ya lile jengo na alipoona kuwa hakuna kitu cha maana akarudi mle ndani na kuanza
kuzikagua kona za eneo lile.
Koplo Tglis Tsega akiwa bado amajibanza gizani kwenye ile kona akamsubiri yule
mtu amfikie usawa wake kisha akatupa pigo moja la kareti lililoipokonya mkononi
bastola ya yule mtu na kuitupa kando. Yule mtu alipotaka kugeuka akajikuta akikabiliana
na mapigo mengine mawili ya kareti shingoni mwake yaliyolipasua vibaya koo lake
na kabla hajapiga mayowe ya kuomba msaada Koplo Tsega akawahi kumtundika
kabari matata shingoni isiyoruhusu hewa kupenya. Yule mtu akafurukuta akitupa
miguu yake huku na kule na kujitahidi kujinasua lakini ilishindika hivyo mwishowe
akaishiwa pumzi na kutulia uhai ukiwa mbali na nafsi yake. Kuona vile Koplo Tsega
akamburuta taratibu yule mtu hadi kwenye chumba kimoja cha lile jengo na kuanza
kumpekua mifukoni. Hakupata kitu chochote na wakati akimalizia kumpekua mtu
yule mifukoni mara akamsikia yule mwenzake akishuka zile ngazi za lile jengo bovu
kuja kule chini hivyo haraka akachepuka na kwenda kujibanza nyuma ya zile ngazi.
Yule mtu akawa ni kama aliyehisi jambo fulani kwani mara tu alipomaliza kushuka zile
ngazi akasimama kwa utulivu na kuanza kumuita yule mwenzake kwa sauti ya chini
“Tino…Tino…!” na yule mtu alipoona kuwa hakuna dalili zozote za kuitikiwa
akawasha kurunzi yake na kuanza kumulikamulika mle ndani na kwa kufanya vile
akawa ni kama aliyeziona zile alama za mburuto wa yule mwenzake aliyeuwawa hivyo
haraka akaikamata vyema bastola yake mkononi na kuanza kuifuatilia ile alama ya
mburuto kwa tahadhari. Koplo Tsega kuona vile haraka akatoka kwenye yale maficho
na kumvamia yule mtu kwa nyuma hali iliyowapelekea wote kwa pamoja waanguke
na kujibwa chini kama mizigo huku bastola zao zikiwaponyoka mikononi. Hata hivyo
yule mtu aliwahi kusimama haraka na kurusha teke la nyuma lililomtandika vibaya
Koplo Tsega kifuani na kumtupa tena chini. Pigo jingine la teke lilipomfikia Koplo
Tsega akawahi kuinama kidogo na hivyo kulipelekea pigo lile likate upepo bila majibu
kisha akaikita mikono yake chini kwa nyuma akijibetua vizuri na kusimama.
Kuona vile yule mtu akaruka hewani na kutupa mapigo mawili mengine ya mateke.
Pigo moja likamzaba Koplo Tsega kichwani na lile pigo la pili Koplo Tsega akawahi
kulipangua kwa mikono yake miwili kisha akajitupa chini akijiviringisha na kumfuata
yule mtu kwa kasi ya ajabu na aliponyanyuka akamchapa yule mtu ngumi mbili kavu
za korodani,mapigo matatu makini ya kareti tumboni na kisha nyumi moja ya nguvu
ya shingoni iliyompelekea yule mtu apige yowe kali la maumivu huku akipepesuka.
Kisha Koplo Tsega akajirusha upande wa pili huku akitupa teke la nyuma lililojikita
vizuri kwenye mgongo wa yule mtu na kumfanya agune kabla ya kuanguka chini. Hata
hivyo Koplo Tsega akawahi haraka kumrudia yule mtu pale chini kabla hajasimama na
hapo akaikamata miguu yake na kuanza kumburuta kwa kasi hadi kwenye nguzo moja
iliyokuwa katikati ya lile jumba bovu ambapo aliigongesha vibaya pacha ya miguu ya
yule mtu na kumsababishia maumivu makali ya korodani hali iliyompelekea yule mtu
apige yowe kali la maumivu. Yule mtu alipotaka kufurukuta kajikuta akitazamana na
mdomo wa bastola ya Koplo Tsega mkononi.
“Wewe ni nani?”
“Go to hell…!” yule mtu akajibu kwa jeuri huku akilalama kwa maumivu makali ya
korodani zake na hapo Koplo Tsega akamshindilia ngumi moja kwenye mwamba wa
pua yake iliyomsababishia maumivu makali yule mtu.
“Nakuuliza,wewe ni nani?”
“Farouk…!” yule mtu akalalama kwa maumivu makali
“Mnataka nini kwangu?”
“Tumetumwa tukufuatilie”
“Nani aliyewatuma?” Koplo Tsega akamuuliza yule mtu huku akishtushwa na
maelezo yale
“Bosi wetu…”
“Bosi wenu nani?” Koplo Tsega akamuuliza yule mtu kwa udadisi na alipomuona
akisita kunyoosha maelezo akamzaba kofi la uso.
“White Sugar…” jibu lile likampelekea Koplo Tsega kwa sekunde kadhaa ashikwe
na mduwao huku akimtazama yule mtu kwa makini. Maelezo ya yule mtu yakawa
yamempelekea amkumbuke White Sugar wakati alipokuwa akimnong’oneza mtu
mmoja muda mfupi kabla ya kutoka na wapambe wake kwenye lile duka Zanzibar
Stone City Bazaar muda mfupi uliopita.
“White Sugar anaishi wapi hapa Zanzibar?”
“Sifahamu” yule mtu akajitetea hata hivyo Koplo Tsega hakukubaliananaye
hivyo akamzaba tena makofi mawili ya nguvu usoni yaliyompelekea yule mtu aanze
kunyoosha vizuri maelezo yake.
“Mimi sijawahi kufika nyumbani kwake ila niliwahi kusikia kuwa anaishi eneo
linaloitwa Bumbwini karibu na Slave Chambers” yule mtu akafafanua na Koplo Tsega
hakuona sababu ya kuendeleza tena mjadala ule hivyo akaielekeza bastola yake kwa
yule mtu na kufyatua risasi mbili zilizomlaza yule mtu chali.