SURA YA SABA
WIKI ILIYOFUATIA SIKU ya Jumapili Ray aliambatana na mke wake hadi kituo cha Agape kama walivyokuwa wamekubaliana na Padre Kiko wiki moja kabla. Jumapili hiyo ilikuwa ni ya jua kali siyo kama ile iliyotangulia. Kama ilivyokuwa wiki moja kabla safari hii tena walifika wakati ambapo ibada ya misa ilikuwa imeisha na tayari watu walikuwa wameshakula na kwenda kwenye mapumziko ya mchana. Sofia alikataa kushiriki ibada ya Kikatoliki japo alilelewa utotoni katika ukatoliki hadi alipoamua kuanza kwenda kwenye makanisa ya Kilokole.
Waumini wanaokaa maeneo ya jirani na pale Agape walikuwa tayari wametawanyika na pale kituoni palikuwa panaelekea katika hali ya ukimya. Ray alikuwa amevaa suruali ya jeans na shati la rangi nyekundu lililokuwa na miraba miraba ya rangi nyeusi. Shati lile jepesi liliweza kuonesha vesti nyeupe aliyokuwa ameivaa chini na hivyo kuonesha ni jinsi gani Ray alikuwa ni kijana wa miraba mine. Walipofika walipokelewa kwa ukarimu wote kama ilivyokuwa kawaida ya Agape na kwa vile walikuwa wanatarajiwa basi walielekezwa moja kwa moja ofisini kwa Padre Kiko ambaye alikuwa anawasubiria kwa hamu.
Pd. Kiko kwa upande wake alikuwa amevaa kanzu yake nyeupe ya kichungaji ikiwa na mkanda wake mweusi ambao unajulikama kama
fascia ambao huwa unaning’inizwa upande wa kushoto pembeni kidogo tu ya usawa wa paja la kushoto. Kama kawaida yake alikuwa kihuduma zaidi. Ilikuwa ni nadra sana kumkuta Kiko akiwa hajavaa aina yoyote ya mavazi ya kichungaji.
“Karibuni sana” Fr. Kiko aliwakaribisha huku Ray akimtambulishe mkewe kwa Padre Kiko.
“Asante sana Father, Tumsifu Yesu Kristu” Ray alimsalimia Padre Kiko.
“Milele Amina”
“Mke wangu Sofia, Sofia huyu ni Padre Kiko mwalimu wangu nikiwa seminari” Ray aliwatambulisha huku akitumia mkono wake kuwaashiria.
“Shikamoo Padre, nashukuru kukufahamu” Sofia aliitikia utambulisho lakini hakutaka kutumia salamu ya kikatoliki.
“Mimi vile vile, karibu sana” Padre Kiko alimpa mkono Sofia na kuwakaribisha.
Sofia hakuweza kusema tu lakini ukweli ni kuwa hakutaka kuwepo pale na ni kwa vile mumewe alimlazimisha tu ndio maana alikubali. Kilichomtibua zaidi ni wazo la kwenda kwa Padre wa Kikatoliki kutafuta ushauri wa ndoa kwa mtu ambaye hajawahi kuoa. Hilo lilimtibua zaidi kuliko kuliko hata matatizo aliyokuwa nayo na mumewe.
Haikuchukua muda mrefu baada ya kupata vinywaji vya soda na biskuti kabla hawajaanza kuingia kwenye mazungumzo yaliyowaleta pale. Aliyeanzisha mjadala alikuwa ni Padre Kiko mwenyewe aliyemkaribisha Sofia kwa kuelezea kwa ufupi mkutano wake na Ray wiki iliyotangulia. Alielezea manung’uniko na hofu ya Ray juu ya kile kinachoendelea hasa masuala ya imani ambayo inaonekana kama Sofia alikuwa ameyapeleka katika ngazi nyingine kabisa. Kwa kadiri Fr. Kiko alivyokuwa akizungumza alizidi kuona jinsi gani uso wa Sofia uliokuwa ukikunja ndita. Lakini Fr. Kiko aliendelea kwa utulivu na kwa kuchagua maneno taratibu.
“Sofia, wewe unaonaje kuhusu aliyoyasema mwenzako” Fr. Kiko alimuuliza Sofia huku akimkazia macho.
Sofia bado alikuwa ameinamisha kichwa chake kama kwa aibu fulani hivi ya mtoto wa kike anayezungumza na babake. Taratibu kama asiyetaka lakini aliyelazimika alijiinua na kukaa huku akiegemea kiti kwa upande kidogo kama anayegoma. Alivuta pumzi ndani kwa sauti kidogo kidogo halafu na kuishusha taratibu. Aliiuma midomo yake kidogo na kuguna kama mtu ambaye alikuwa na hasira lakini asiye tayari kusema kitu. Mikono yake alikuwa ameituliza kwenye magoti yake huku vidole vikiwa vimeshikana. Kwa sekunde kadhaa hivi alikuwa anaiminyaminya mikono yake taratibu; alimuangalia kwanza Ray kwa jicho la pembeni halafu akayarudisha macho kwenye mikono yake.
“Mimi kwa kweli sina la kusema; sijaelewa tu kwanini matatizo yetu ya nyumbani ameyaleta kwako” alisema Sofia kwa sauti ya kiburi kidogo na yenye kutoa shutuma ndani yake. Sauti yake ikitetemeka.
“Kwani kuna ubaya gani?” Ray aliunguruma na yeye hakuficha hasira yake. Sauti yake ilitoka kwa nguvu kidogo na kumshtua hata Fr. Kiko pale. Kiko alijua mara moja nini kinaweza kutokea kama hatodhibiti mazungumzo hayo.
“Taratibu Ray, taratibu!” Fr. Kiko aliingilia kati akimuashiria kwa mkono wake wa kulia. “Ngoja tumsikilize mwenzako halafu kila mmoja atatoa maoni yake, lengo ni kuelewena na kujua mtazamo wa kila mmoja. Hakuna sababu ya kugombana au kubishana” aliendelea Fr. Kiko kwa sauti iliyokuwa imetulia isiyoonesha hisia zake. Miaka karibu arobaini ya uchungaji ilimuandaa kwa mambo mengi na aliyasikia mengi katika maisha yake yale ya kichungaji na katika chumba cha maungamo. Hili la Ray na Sofia lilikuwa ni moja tu. Tofauti ni kuwa Ray alikuwa ni kama mtoto wake wa kumzaa mwenyewe. Fr. Kiko alikuwa akijiambia mara nyingi kuwa kama angekuwa amezaa mtoto wa kiume basi angeona fahari sana angekuwa kama Ray.
“Ehe endelea Sofia” Kiko alimuashiria Sofia kuendelea.
“Padre, kusema ukweli mimi sijafurahia. Kila mtu kwenye ndoa ana matatizo yake ya aina mbalimbali na watu huzungumza huko na kujaribu kuyatatua” Sofia aliendelea pale alipoishia kabla Ray hajaingilia sauti. “Sasa nimeshangaa mwenzangu kaja huku wakati miye nimemuomba mara kadhaa twende kwa Askofu Ndondo lakini amekataa kabisa” alisema huku akimrudishia tuhuma mmewe.
“Siwezi kwenda kwa tapeli Father!” Ray alirukia baada ya kushindwa kujizuia. Hasira na dharau zake zikiwa wazi kabisa. Hakusema kwa sauti bali alikuwa ameamua kuchomekea tu, akirusha mkono pembeni kama kupuuzia.
“Yeye ni mtumishi wa Mungu, unajua watu wangapi wamebarikiwa kwa huduma yake? Unajua kina mama wangapi wamejaliwa kupata watoto na mafanikio ya kila namna kwa kuombewa naye? Askofu Ndondo ni kama T.B. Joshua kabisa wa Tanzania” Sofia alimtetea Askofu Ndondo kama mtu aliyekuwa analipwa kumtetea.
“Kwa hiyo sababu kubwa ya kwenda huko ni kwa ajili ya kutaka kuombewa?” aliuliza Fr. Kiko.
“Ni zaidi ya kuombewa, miye ninabarikiwa sana kule! Siyo kama huku kwa Wakatoliki! Kule, tunamuabudu Mungu kwa uhuru, na Mungu anafanya miujiza mikubwa kila siku” Sofia aliamua kuwatolea uvivu; aliamua kuwapiga gombo. Aliendelea kuwahubiria “na kule kwa Mtumishi wa Mungu Ndondo watu wanaishi kwa Neno kweli kweli” Sofia alirusha mishale yake kama kutoka kwenye podo la mwindaji mahiri. Hakujali nani inamgusa au nani anaumia. Alitumia mikono yake kujieleza kama mwalimu wa shule ya msingi.
“Na unaona kuwa kule kwa Ndondo kuna chakula kizuri zaidi cha kiroho” alisema tena Fr. Kiko kama kumfanya Sofia aendelee kutiririka.
“Kweli kabisa!” alidakia Sofia na kuendele akiombea moyoni labda Padre Kiko anaweza kukubali hoja zake. Alifafanua kuhusu manufaa anayoyapata kinamna akilinganisha na yale yanayopatikana kwenye Kanisa Katoliki “chakula cha kiroho ni kipya kila siku. Kuna mafundisho ya kila namna na yanamjenga mtu kiroho. Jumatatu wanakutana vijana, Jumanne ni huduma ya kuombea wagonjwa na wenye matatizo mbalimbali” hakusimama kupumzika maana alikuwa anazungumza kama hotuba ya mshindi wa tuzo ya Oscar. “Jumatano ni masomo ya Biblia, Alhamisi kina mama tunakutana na kufanya
intercession na Ijumaa ni kufunga. Jumamosi wanakwaya wanakutana na Jumapili ni siku ya ibada” aliendelea kuzungumza bila kuvuta pumzi. Hoja yake ni kuwa maisha ya kiroho yalikuwa yanalelewa vizuri zaidi kwa Ndondo kuliko kwa Wakatoliki.
Alipofika mwisho hapo alimeza fundo kubwa la mate na kushusha pumzi. Alichukua glasi ya maji na kupiga mafundo mawili. Ingekuwa kwenye umati mkubwa wa watu wangesimama kumpigia makofi. Ray na Fr. Kiko walikuwa wanamsikiliza kwa makini kabisa. Fr. Kiko alijua Ray amepata mshindani kwenye masuala ya kujenga hoja. Ray mwenyewe kwa namna aliona fahari kwa jinsi mke wake alivyokuwa anajiamini. Ingekuwa mazingira mengine Ray angempongeza mkewe.
“Na unaona Ray hashiriki katika mambo hayo ya kiroho?” Kiko alimgongelea kwa swali jingine kama mwendesha mashtaka akimuongoza shahidi muhimu kizimbani.
“Siyo tu hashiriki, ananipinga kwa kila kitu” Sofia alijibu kwa sauti ya juu kidogo. Aliposema maneno hayo alikaa viizuri na kumuelekea mumewe moja kwa moja. “Tuna miaka mingapi hii hatujajaliwa mtoto; tumeenda kwa kila daktari hapa nchini lakini hakuna mafanikio, mwenzangu yeye ameweka mkazo wake huko kazini sijui anataka kuwa nani katika nchi hii. Na mimi umri ndio unaenda hivyo” alisema huku sauti yake ikipanda kufichua hasira iliyojificha ndani yake. Macho yake yalianza kutengeneza madimbwi. Alivyomeza fundo lile la mate na machozi yakamdondoka. Fr. Kiko alimpa tishu nyepesi ya kujipangusia machozi.
“Ray unasemaje kuhusu aliyoyasema Sofia hapo?” Fr. Kiko alimuuliza Ray ambaye alikuwa anamuangalia mke wake kama mtu aliyekuwa anashuhudia mwigizaji aliyebobea. Upande mmoja hata hivyo alijikuta anaona huruma lakini upande mwingine akijua kabisa ni nini kilicho kwenye matatizo baina yao. Fr. Kiko alijiinua kidogo kujikalisha vizuri kwenye kochi lake kumsikiliza kijana wake.
“Fr. Kiko, tatizo langu na mke wangu siyo mtoto -
at least not from where I stand” alianza kujieleza kuwa yeye alivyoona tatizo halikuwa kupata mtoto. “Tatizo letu ni mahusiano na kutosikilizana. Mtoto kwa kadiri ninavyofahamu mimi siyo haki ambayo unaweza kumdai mwenzako kana kwamba naye ana uamuzi wa mwisho wa kumtoa mtoto” alijieleza kwa sauti kavu, iliyochagua maneno herufi kwa herufi, kituo kwa kituo. “Tumekuwa tukijaribu miaka yote lakini hatujajaliwa, sote tumeenda kwa madaktari na hawaoni matatizo yoyote; miye simlaumu yeye na sijilaumu mwenyewe maana kama kujaribu tunajaribu
sana!” Alisema na kuweka msisitizo kwenye neno
sana na kumfanya Kiko aelewe amemaanisha nini.
Baada ya kumeza fundo la mate aliendelea “Sasa kama njia za kisayansi zote zimeshindikana huku kwingine tunaenda kutafuta mambo ya kishirikina tu na baadaye kujiletea matatizo”
“Kwani kuombewa ni ushirikina?” alidakia Sofia akionesha hakuwa tayari kuburuzwa. “Nilikuwa naenda kwa waganga wa kienyeji wa kila sehemu na wengine niliwaleta hadi nyumbani, mwenzangu akagoma kabisa na kuwafukuza, sasa nimeamua kujaribu kwa mambo ya sala bado yeye anaona ni ushirikina!” alisema kwa sauti ya juu kidogo akiona kama amekata tamaa.
Ray naye hakuwa tayari kusalimu amri; “Ni aina ya ushirikina hasa kwa hawa wahubiri uchwara ambao unaenda kwao, watu wanataka utoe sadaka sijui za kila namna gani ili ati mtu abarikiwe; sasa wana tofauti gani na waganga wa kienyeji wanaotaka watu wapeleke mbuzi, kuku na bata” alisema sauti yake ikizidi kuonesha hasira. Midomo yake ilikuwa imeanza kumkauka, akachukua na yeye glasi yake ya maji na kupiga fundo moja na kujilamba kidogo.
“Siyo ushirikina ni imani na…” Sofia alijibu mapigo kutetea imani yake.
“Ushirikina ni imani vile vile” Ray alimkatiza bila kufikiria.
“Twende taratibu” Fr. Kiko aliamua kuingilia kati kwani aliona sauti zinazidi kupandiana juu kama ngazi. “Sasa hili suala la fedha na viwanja ni vipi Sofia maana inaonekana hapa ndipo hasa mwenzako anaona kama ndio msingi wa hofu yake kwamba unaweza kuleta umaskini kwenye nyumba hasa unapofanya maamuzi kama haya bila kumshirikisha au kukubaliana na mwenzako?”
“Kwa mtu alivyo hivi ningemwambia natakiwa kutoa sadaka unadhani angekubali?” Sofia alijaribu kuelezea kwa sauti ya kejeli kidogo. Aliamini ametoa sababu ambayo ilikuwa ina mantiki ya aina fulani hivi. “Inawezekana nilikosea na hapo naomba msamaha lakini tayari imefanyika siwezi kwenda kwa Askofu na kumdai tena” alisema huku sauti yake ikiwa imebeba aina fulani ya kutokuaminika na yeye mwenyewe akigeuza macho yake kuangalia dirishani.
“Lakini vipi kuhusu kuachana na hilo kanisa?” Kiko alimuuliza moja kwa moja bila kuzungusha maneno.
“Ah, sasa mambo ya imani Father ni imani ya mtu, kama yeye anaamini katika ukatoliki na kaja hapa kwako na mimi nina haki ya kuamini ninavyoamini” alisema Sofia. Wote wawili Fr. Kiko na Ray walikosa majibu ya moja kwa moja kwani kweli Sofia alikuwa na hoja hapo. Kiko alijua kuwa kwa kuzungumza tu Sofia alikuwa na kipaji kwani ni miongoni mwa vitu vilivyomvutia Ray hata kufikia kumtongoza, kuchumbia na hatimaye kumuoa. Sofia alikuwa na shahada ya pili katika uandishi wa habari na wakati anakutana na Ray alikuwa ameanza kazi Televisheni ya Taifa kama Mhariri Mwandamizi Msaidizi.
Kama fahari wawili waliokuwa wameshikana mapembe wakigomeana ushindi, Ray na Sofia walikuwa wamekamatana. Hawakuwa na mengine ya kusema isipokuwa kwa siku ile waliamua kukubaliana kutokukubaliana na kupingana bila kupigana. Jioni ilikuwa imeanza kuingia na Fr. Kiko alikuwa ana kikao cha kupanga wiki ya waombeaji ambayo Agape walikuwa wanaiandaa kwa wale wenye huduma ya kuombea wengine. Ni huduma kama ya kanisa la Ndondo ambapo watu wenye karama ya kuombea walikuwa wanakutanika kufanya maombezi. Makanisa mengi ya Kipentekoste yana vikundi vya waombeaji na Wakarismatiki wa Kikatoliki nao walikuwa na vikundi kama hivyo hivyo.
Waliagana na Fr. Kiko aliwasihi kuwa itakuwa vyema wakitafuta muda mwingine mzuri zaidi waje tena kuzungumza naye. Aliwapa maongozi mengine ya kiroho na kimaisha kama baba kwa watoto wake. Ray aliyashika moyoni lakini Sofia yaliingia sikio moja na kutokea kwingine, tena yakitoka mkuku.
Walipoondoka pale Agape hawakuzungumza kabisa. Sofia alikuwa anaangalia nje ya dirisha la gari. Majaribio yote ya Ray kumsemesha yalikuwa kama kujaribu kukinga mikono kusubiria mvua jangwani. Moyoni Sofia alikuwa amekasirishwa sana lakini pia aliamini kabisa kuwa mume wake alikuwa na mapepo na hakuwa tayari kumpa shetani nafasi kwani aliamini shetani alikuwa hataki afanikiwe. Alikuwa ametulia moyoni anakemea mapepo yale na alidhamiria kabisa kuwa akipata nafasi tu atafanya mpango akazungumze na Askofu wake kumueleza matatizo yake.
Kutokana na sadaka zake na kujitolea kwake kwenye shughuli mbalimbali za kina mama pale kanisani Sofia alikuwa anajulikana na Askofu Ndondo na viongozi wengine wa kanisa. Hata hivyo, hajawahi kuwa na muda hasa wa kuzungumza na Askofu matatizo yake au mambo yake au hata kuweza kukaribishwa katika ofisi za Askofu ukiondoa zile zilizopo ndani ya jengo la kanisa. Askofu alijua tu kuwa Sofia alikuwa ni mke wa afisa wa polisi, hapo hakujua undani wa cheo na shughuli za ofisa yule.
Ray hakuwa anaelewa kwanini mke wake ambaye mwanzoni alikuwa anamsikiliza, na wanazungumza vizuri tu na kushauriana mambo mbalimbali alikuwa kama mwenye mapembe yaliyochongoka kama mbilimbi. Kila walipokuwa wakijaribu kuzungumza ilikuwa ni kama kondoo wanagonganisha vichwa. Walipofika nyumbani hata chumbani hawakulala pamoja; haikuwa mara ya kwanza Ray kujikuta anajilaza kwenye makochi kwani mkewe aliingia chumbani na kufunga mlango. Aliamua tu kumwacha aendelee na mambo yake na yeye aendelee na kazi zake. Kutokana na majukumu yake asingeweza kuachilia matatizo ya nyumbani yamtawale mawazo kiasi cha kushindwa kufanya majukumu yake ya kiusalama kwani Taifa na jamii ilikuwa inamtegemea.