SEHEMU YA NNE
Kassimu aliliangalia Benzi likitoka nje ya geti kisha akageuza kichwa na kumtazama mtunza bustani. Alikuwa kama hatua arobaini mbali naye,akimwagilia miwaridi. Akajiuliza kama ameweza kusikia kuyasikia mazungumzo yao. Alizungumza kwa sauti ndogo kwa ajili yake. Akaamua asingeweza kumsikia. Akageuka na kuingia ndani.
Vyumba vyote vya kulala vya jumba hilo vilikuwa ghorofani. Sehemu kubwa ya chini ilikuwa ukumbi mkubwa uliopambwa vilivyo. Sakafu yote ilifunikwa na zulia. Upande mmoja ulitawaliwa na meza iliyozungukwa na viti kumi na viwili. Upande mwingine ulikuwa na TV na rafu za vitabu,mapambo na vinywaji, hasa vikali na aina kadhaa za mvinyo aghali toka ng'ambo. Hapa na pale palikuwa na seti za sofa na vimeza vifupi. Ngazi za kwenda ghorofani zilikuwa mkabala na mlango wa mbele.
Kassim alikwenda moja kwa moja kwenye rafu ya vinyaji. Akatoa chupa ya kinywaji kikali na kjitilia robo glasi. Akaimeza kwa mkupuo.
Kisha akaenda kwenye simu iliyokuwa pembeni. Baada ya kubonyeza namba atakazo na kujibiwa, akasema "Nipatie Bwana Kembo." Punde sauti upande wa pili akasema, " Kembo hapa." Kassim akatamka neno moja tu, "Vipi?"
"Ohh, Bwana Kessy! Nahitaji kukuona. Tuna tatizo."
"Na mimi pia nina tatizo."
"Tatizo gani?" Kembo aliuliza kwa mashakamashaka.
"Tuna watu karibu sehemu zote mhimu."
"Vizuri. Kuna mtu alifikwa na ajali ya gari nyuma ya Benki ya Wakulima muda mfupi uliopita. Nataka kujua ni nani mtu huyo na hali yake ikoje. Unaweza kufanya hivyo?"
"Hakuna lisilowezekana, Bwana Kessy. Hakuna lisilowezekana."
"Fanya hivyo halafu njoo unione,"
***********************
Bessy hakua mgeni na Dk. Beka, Daktari Mkuu wa hospitali kuu ya serikali. Tangu avishwe uinspekta mwaka mmoja na nusu nyuma, alikwisha kutana nae mara kadhaa,kuhusiana na kesi mbalimbali.
Kwa hiyo alipofika hapo hospitalini alikwenda moja kwa moja ofisini kwake. Akabisha na alipoambiwa aingie, akaufungua mlango na kuingia.
"Ohh, ni wewe Inspekta." Alisema Dk. Beka kwa suti yake tulivu na ya chini. Leo Bessy aliona,ilikuwa ya chini zaidi - ya huzuni.
Akasema, "Ni kuhusu Dk. Makete." Naye pia alitumia sauti ndogo. Dk.Beka akaitikia kwa kichwa. akaivua miwani yake na kuyafikicha macho yake machovu.
"Ikoje hali yake?" Bessy aliuliza,akiketi na kukitoa kijitabu chake.
"Nasikitika kusema si nzuri. Bado yuko thieta anashughulikiwa na wataalamu wa hali ya juu."
"Uko uwezekano wake wa kuishi?"
"Kitu kama hamsini kwa hamsini,"
Bessy alikwishaizoea kauli hiyo. Dk. Beka hakupenda kumkatisha mtu tamaa,hata kama alijua kuwa mgonjwa huyo asingetoka thieta akiwa hai.
Akauliza, "Aliwai kurudiwa na fahamu?"
"Alizinduka thieta kwa nukta chache tu kabla ya ganzi kumkolea sawasawa."
"Aliwai kusema lolote lile katika nukta hizo chache?" Bessy aliuliza kwa matumaini kalamu ikisubiri mdomoni.
"Alisema maneno machache. Lakini hakusikika vizuri. Alikuwa kama anaeota - anaeweweseka. Sauti yake ilikuwa ya chini sana, na maneno hayakuwa ya kuleta maana. Nilichoweza kukidaka ni maneno mawili tu - kama tutayaita maneno - 'kassi hashi.' Aliyarudia maneno hayo mara mbili tatu."
Baada ya kuyaandika maneno hayo,Bessy akasema kwa sauti ya mkazo , "Dk. Beka, lazima nizungumze na Dk. Maketemapema iwezekanavyo - kabla....kabla mambo hayajawa mabaya zaidi. Dk. Makete aligongwa kusudi. Na kwa bahati mbaya hakuna aliewai kuzisoma namba za gari."
"Una maana haikuwa ajali ya kawaida?" Dk. Beka aliuliza kwa mshangao wa kutoamini.
"Hapana! Lilikuwa jaribio la kuua!" Sauti ya Bessy ilikuwa imepanda. Akavuta pumzi na kuendelea kwa sauti ya kawaida. "Nadhani Dk. Makete anamfahamu mtu aliemgonga. Na sababu yake. Huwezi kumgonga mtu kusudi bila sababu."
" Una uhakika haikuwa ajali? Madereva wengi wanapomgonga mtu...."
"Najua. Hukimbia. Hukimbilia polisi kujisalimisha. Lakini huyu hakufanya hivyo. Zaidi ya masaa mawili sasa yameshapita. Nina hakika hata jisalimisha. Isitoshe, uchochoro aliogongewa Dk. Makete hautumiwi na magari, na kama kuna gari litapita, basi si kwa kasi ya kuweza kusababisha ajali.
Dk. Beka akatikisa kichwa kwa majonzi.
Inspekta Bessy akaendelea, "Isitoshe tuna ushahidi. Ingawa kichochoro kile - kichochoro cha Benki ya Wakulima - hakina pilika za watu. Tumebahatika kupata watu wawili walioshuhudia tukio hilo. Wote wanaelekea kuwa watu wa kuaminika. Wote wapo tayari kuapa kuwa Dk.Makete aligongwa kusudi."
Dk. Beka alifumbua mdomo ili aseme neno lakini akabadili mawazo na kuufumba
Bessy akaendelea, "Mashahidi hao wanatoa sababu mbili. Kwanza. Dk Makete hakuwa katikati ya njia. Alikuwa pembeni. Alifuatwa. Pili, gari lililomgonga lilimnyemelea. Liliongezwa mwendo ghafla lilipomkaribia. Mmoja kati ya mashahidi hao aliwai hata kuguta. Hakumbuki alisema kitu gani. Bila ya shaka kitu kama 'Hey...! au 'Wewee...!' Hajui kama alikuwa anamkemea yule dereva au anamtahadharisha Dk. Makete. Anasema alikuwa katika mshituko wa kuruka akili. Ndiyo maana hakuweza kuzisoma namba za gari."
Dk.Beka akatikisa tena kichwa. Akasema, "Nashindwa kuamini."
"Amini usiamini, hivyo ndivyo mambo yalivyo. Dk. Makete amegongwa kusudi."
"Hukunielewa. Nina maana....." Beka alitafuta maneno ya kumalizia sentesi yake lakini hakuyapata. Akasema, "Namfahamu Dk. Makete vizuri sana. Nimefanya nae kazi kwa zaidi ya miaka ishirini. Miaka kumi nikiwa msaidizi wake mkuu. Ni rafiki yangu mkubwa. Tumekuwa kama ndugu. Siri yake ni yangu. Mkewe ananiita shemeji, na mwanae ananiita mjomba. Hata siku moja sijaona wala kusikia Raymond akikorofishana na mtu. Nakuhakikishia yeye si mtu wa kuweza kuwa na adui hata mmoja hapa duniani."
"Na mimi nakuhakikishia kuwa anao. Angalau mmoja. Na ni wajibu wangu kumtia mbaroni. Nina imani Dk. Makete anamfahamu mtu huyo. Kwa hiyo lazima nizungumze nae kabla hali yake haijawa mbaya zaidi."
Dk. Beka aliinua uso akauliza, "Unamaana iwapo hata .... hatarudiwa na kauli, mtu huyo hataweza kupatikana?"
Badala ya kujibu swali hilo Inspekta Bessy alisema kwa sauti kavu, "Dk. Beka tafadhali usinifiche niambie ukweli. Dk. Makete atatoka thieta akiwa hai au maiti?"
"Mimi siyo mtabiri! Wala siyo Mungu!" Ingawa maneno hayo yalitamukwa kwa sauti ndogo lakini ilikuwa sauti ya ukali. Iliyojaa uchungu na ghadhabu. Dk. Beka akapumua na kusema kwa sauti yake ya kawaida, "Bessy, hatuwezi kufanya miujiza, kufanya lisilowezekana. Hatuwezi kufufua maiti. Hakuna anaeweza kufanya hivyo zaidi ya Yesu."
"Ndiyo kusema Dk. Makete hana tumaini?"
"Sijasema hivyo. Raymond hajawa maiti. Hivi tunavyozungumza anashughulikiwana mabingwa. Wanaweza wakafaulu kuyaponya maisha yake, wanaweza wasifaulu. Ikishindikana, hakuna yeyote wa kuweza kufanya lolote."
Bessy alikunja uso na kusema. " Kuna sindano ya kuua ganzi na kumzindua mtu na kumfanya aweze kijibu swali moja au mawili kabla ya kukata roho.Kama Dk. Makete hana tumaini lazima sindano hiyo itumiwe ili atutajie mtu alie mgonga."
"Dk.Beka akamtazama Bessy kwa mshangao. Akamwuliza, "Umeisikia wapi hiyo sindano?"
"Katika kitabu."
"usiamini kila unachosoma kwenye vitabu vya hadithi."
"Hakikuwa kitabu cha hadithi."
Kimya kizito kikazagaa humo ndani kwa nukta kadhaa. Hatimaye Bessy akauliza "Sindano hiyo ipo au haipo?"
"Ndiyo - ipo."Dk. Beka alijibu kwa karaha. "Lakini haitumiwi ovyo. Kwa sababu humumaliza kabisa mgonjwa. Hata kama alikuwa asife atakufa."
"Kwa mtu asie na matumaini ....?"
"Ni nani wa kuamua kuwa hana matumaini? Si mimi. Ninavyoamini mimi, mtu anaepumua ni mzima, Hata kama tumaini la kupona ni moja katika milioni. Oh, tunapoteza bure wakati kuizungumzia sindano hiyo. Kwanza hatuwezi kuitumia bila amri toka juu. Ni nani wa kwenda ikulu? Wewe?
Na hata kama nitalazimishwa kuitumia sitaitumia. Nitajiuzulu. Kwa sababu moja tu. Siwezi kukubali kuua - kumwua mtu yeyote yule, achilia mbali mtu huyo kuwa rafiki yangu mkubwa."
Bessy alishusha pumzi ndefu akasema. "Nimekuelewa, Dk. Samahani."
Dk. Beka akapumua pia. Akasema, "Kuhusu swali langu?"
itaendelea.