SEHEMU YA KUMI NA MOJA.
Kwa Shangazi Suzy palikuwa na mambo. Mojawapo lilikuwa ni lile la watu kutengwa kufuatana na daraja. Wateja wa daraja la kwanza - 'maofisa' waliwekwa chumbani, ambamo mlikuwa na kitanda maridadi, seti ya sofa, viti na meza. Labda waliwekwa humo kwa vile hawakuwa wengi. Na walikuwa wasafi. Na hawakupendelea sana mapuya. Zaidi walikunywa bia na konyagi.
Wateja wa daraja la pili - 'waungwana,' waliwekwa ukumbini kwenye mabenchi. Hakuna alieweza kukisia sababu ya wao kuwekwa hapo. Wengi wao walikuwa wa umri mkubwa. Mno walikunywa mapuya. Waliagiza konyagi kwa nadra. Bia - mwaka mara moja. Sikukuu hadi sikukuu.
Wateja wa daraja la tatu na la mwisho - vichwa vya panzi - waliwekwa uani, ambako walikalia chochote kile, kuanzia matofali hadi chini aridhini.
Sababu za wao kuwekwa huko zilikuwa wazi. Kwanza walikuwa wengi, na wengi wao walioga na kufua kauka nikuvae, Jumapili hadi jumapili. Pili walikuwa hususani watu wa mapuya. Tatu, walikuwa wadoezi na wagandaji - yaani nusu lita ilimfanya mtu agande hapo tangu asubuhi mpaka usiku wa manane. Na nne walilipata jina lao 'vichwa vya panzi' - kwa sababu walikuwa hawakawii kulewa . Na hapo huwa wenye kelele, wagomvi, waimbaji na wachezaji.
Lakini ajabu ni kwamba hakuna hata mmoja, hata siku moja, alielalamikia ubaguzi huo. Kila mmoja alipajua mahali pake na aliridhika napo.
Lakini kwa Kikoti alikuwa tofauti kidogo. Yeye alijipandisha ngazi moja moja. Alianzia kwa 'vichwa vya panzi' alipokuwa hana kazi maalum, ndiyo kwanza aingie jijini.
Akahamia kwa 'waungwana' alipopata kibarua katika kampuni moja ya ujenzi. Akahamia kwa 'maofisa' alipota kazi ya kuhudumu huko Buffalo Hill.
Hata huvyo, kwa kuwa hakuwa mgeni mahali popote, na alikuwa 'memba' kila siku,ilikuwa juu yake mwenyewe kuchagua pa kuketi - aghalabu kutokana na mfuko wake au mwaliko.
Siku hiyo, mfuko wa karatasi mkononi, alipitiliza moja kwa moja hadi chumbani akawakuta 'maofisa' wawili wa kudumu, Bob na Butu, wamekwisha fika,walikuwa wakinywa konyagi.Bob, kwa sababu ya kitambi chake, katika nguo za kawaida alionekana kama meneja wa benki.
Bila ya kusema neno, Kikoti aliitoa chupa ya wiski na kuikita mezani. Bob akaitazama kwa makini. Akainua uso na kuuliza. "Umeipata wapi wiski hii, Kikoti? Ni ya thamani sana!"
"Kanipa tajiri yangu." Kikoti aliongopa, macho makavu. "Huyo ndie tajiri wa kumtumikia. Nikichoka kufokeana na madereva wakorofi, nitakwambia unipeleke na mimi nikaombe kazi."
"Shangazi yupo wapi utupe glasi?" Kikoti akauliza. "Atakuwa wapi kama sio kwa vichwa vya panzi?" Butu alimwuliza.
**********************
"Karibuni." Mzee Maliki aliwakaribisha. Alikuwa mtu wa makamo alietazamia kustaafu muda wowote. Sare yake ya Ukamishna Msaidizi ilimpendeza sana. Ofisi yake ilikuwa pana na nadhifu.
"Ketini." Wakaketi. "Ni nani mwenzako Bessy?"
"Luteni Dennis Makete. Baba yake, Dk.Raymond Makete, aligongwa na gari leo asubuhi nyuma ya Benki ya Wakulima. Aliemgonga hakusimama na hakuna mtu aliwahi kuzisoma namba za gari. Tunaamini mtu huyo ni Kassim Hashir na alimgonga Mzee Makete kusudi."
"Simkumbuki..."
"Ulimfungulia faili hili mwaka 1969 na kulifunga mwaka 1974, ukiamini amekufa."
Mzee Maliki akalipokea lile faili na kulifungua. Baada ya kuupitisha macho ukurasa uliokuwemo, akasema, "Ndiyo, nakumbuka sana. Nilipokea telegram kutoka Polisi ya Kenya ikieleza Kassim Hashir alifikwa na ajali mbaya ya gari na kufariki papo hapo. Sijui kwa nini telegram hiyo haimo humu! Ukweli ni kwamba kesi yake ilikuwa dhaifu sana. Kila mtu aliidharau, pamoja na kuhusiana na mamilioni ya pesa za kigeni. Kwa nini mnadhani yuko hai na ndiye aliemgonga Dk.Makete?"
"Mzee Makete alizinduka kwa nukta chache alipokuwa thieta na kulitaja jina lake."
"Hawezi kuwa amekosea?"
"Hatujui. Lakini kwa vile hatuna fununu yoyote nyingine..."
"Ikoje hali ya babako, Denny?"
"Niliarifiwa amejeruhiwa vibaya. Lakini Dk.Beka anaamini hayuko katika hali ya kutisha." Alijibu Denny. "Huwezi kufanya chochote kile kuhusu mtu huyo?"
" Hatujui chochote kile zaidi ya kulijua jina lake na kuiona picha iliyomo humo, ambayo sidhani kama itatusaidia sana,ni ya zamani mno - tuko gizani kabisa."
"Mmmh, labda nianze toka mwanzo." Alisema Mzee Maliki, akiwaza. "Kama unavyofahamu, nchi hii ilipata uhuru mwaka 1960. Bwana Nelson Benjamin Nseloa akawa Rais wa kwanza. Watu wote walifurahi jinsi alivyopigani uhuru, wote tulimpenda Nselo.
"Lakini kadri miaka ilivyozidi kupita bila ya yeye kutimiza kile ambacho wananchi wengi walitamazamia angetenda, mapenzi yakaanza kupungua. Wananchi wengi walitazamia kuwa baada ya uhuru, Nselo angewafukuza wageni wote - wazungu na waasia na mali zao kugawiwa kwa wazawa. Yeye hakufanya hivyo. Kinyume chake, aliwatetea na kuwalinda. Kwa vile tangu mwanzo walikuwa ndio wafanyabiashara wakubwa na wenye kumiliki mashamba makubwa na mazuri, wakazidi kutajirika. Wananchi wakaishiwa furaha."
Mzee Maliki alitoa mtemba akaanza kuujaza tumbaku kabla hajauwasha na kuukoleza.
"Mkuu wa majeshi wakati huo, Meja Jenerali Ibrahim Mbelwa,akaamua kuutumia mwanya huo. Akaipindua serikali ya Nelson Benjamin Nselo,ambaye alikuwa ng'ambo, na kutwaa madaraka."
Baada ya kuuwasha mtemba kwa kutumia njiti tatu,akaendelea, "Hiyo bila shaka, ni historia mnayoifahamu vizuri. Inasikitishwa vile watu wanavyofurahishwa na kitendo cha Mbelwa, hasa alipowafukuza wageni na kugawa mali zao kwa wananchi. Lakini haukupita muda mrefu kabla ya hulka ya kweli ya Mbelwa kudhihirika. Kwa vile hakuwa na elimu, aliwachukia wasomi, kwa vile alikuwa Mwislam ,aliwachukia wakristo. Kwa vile alikuwa Mshongwe, aliwachukia watu wa makabila mengine,hasa kabila la Nelson Nselo. Si tu aliuteketeza uchumi wa nchi, bali aliteketeza watu karibu milioni. Kwa vile wakati huo tulikuwa miloni chache tu, idadi hiyo ilikuwa kubwa ya kutisha. Watu wakaanza kujuta."
Mtemba ulikuwa umezimika. Akauwasha tena kabla ya kuendelea. "Kwa sababu moja au nyingine, maelfu ya wananchi wakaihama nchi na kuomba hifadhi katika nchi jirani. Nelson Nselo akaweza kuwaunganisha na kuwapa mafunzo ya kijeshi. Wakati ulipowadia wakaingia nchini. Wakashinda kirahisi askari wa Ibrahim, ambao hawakuwa na moyo hata na moyo wa kupigana. Yeye mwenyewe aliuliwa wakati akijaribu kutoroka nchi. Risasi zangu zilikuwa miongoni mwa risasi zilizomtoa roho."
Kikapita kimya cha muda, Dennis akajikuta anamtazama Mzee Maliki kwa matazamo mpya. Mzee huyo akaendelea, "Sasa kuhusu Kassim Hashir. Yeye na Ibrahim walikuwa marafiki, licha ya kutokuwa rika moja. Akampa Kassim pasipoti ya kibalozi na kumtumia kutorosha mali. Katika kipindi cha utawala wa miaka mnne ya utawala wake, Kassim alitorosha mamilioni kwa mamilioni. Alikwenda Ulaya karibu kila wiki kupeleka pesa za kigeni na chochote kile ambacho kilikuwa mali. Kazi hiyo inasemekana aliimudu vizuri. Pia inasemekana alikuwa na kichwa cha biashara. Hakuyaacha mamiloni hayo yalale benki, aliyazalisha katika vitega uchumi mbalimbali.
"Alipoona mambo yanaanza kuharibika hapa nyumbani, akayeyuka. Kwanza alikimbilia Ulaya, baadaye akawa hatulii mahali pamoja. Akawa mfanyabiashara wa kimataifa. Bila ya shaka aliposikia Ibrahim amekufa aliinua mikono mbinguni. Hakuwa na mtu wa kumghasi na wala kugawana nae tena. Na kama ni kweli angali hai atakuwa tajiri mkubwa sana - tajiri wa kuweza kushindana na serikali yoyote ya nchi ya Kiafrika."
Bessy akashusha pumzi. "Sioni kitendo chake cha kurosha mali kinaweza kuhusiana na Dk.Makete."
"Hata mimi sioni." Alikubali Mzee Maliki. Dennis akauliza, "Kwa nini ulisema kesi yake ilikuwa dhaifu - hamkujali sana?"
"Mara tu baada ya Ibrahim kung'olewa, niliteuliwa kuongoza skwadi ya kuwasaka, kuwakamata na kuwapeleka mahakamani wote waliotenda makosa wakati wa utawala wa fasishisti huyo. Walikuwa wengi, zaidi ya elfu. Wengine walikuwa wamefanya makosa madogo tu, lakini wengi walikuwa wametenda unyama kweli kweli. Kwa wengine palikuwa na ushaidi, na kwa wengine hapakuwa na ushaidi wa kutosha. Ilikuwa kazi kubwa kupata majina yao na makosa yao kuwafungulia mafaili, kuwasaka, kuwakamata, kutafuta ushaidi na hatimae kuwapeleka mahakamani. Kadhaa tuliwanasa na walihukumiwa kunyongwa au kufungwa. Lakini wengi pia ilibidi waachiwe na makama kwa uhaba wa ushaidi."
" Wote tuliona Kassim angekuwa mmojawapo wa kuachiwa. Kwanza, kwa vile alikuwa na pesa, angeweka mawakili kabambe. Pili, hatukuwa na ushahidi madhubuti kumtia hatiani. Mashahidi tuliowapata ni maafisa wa forodha na uhamiaji, ambao walikiri kuwa hawakuwa wakimpekua Kassim aendapo ng'ambo kwa sababu ya pasi yake ya kibalozi, ingawa walishuku mizigo yake. Huo sio ushahidi kitu mahakamani. Walishindwa hata kusema kwa hakika ni vitu gani alivitorosha.
"Ushahidi mwingine ulikuwa wa minong'ono tu, wa watu waliokuwa wakimtafutia bidhaa,ambao hatimae akawadhulumu. Unadhani wangekubali kusimama mahakamani na kutoa ushaidi? Wao na wao walikuwa wanavunja sheria. Hata kama wangekubali ili kumkomoa Kassim,wakili yoyote yule angewachakaza vibaya sana."
"Bessy akauliza, "Kwa hiyo hakuna juhudi zozote zilizofanywa za kutaka akamatwe huko Ulaya na kumrudisha nyumbani?"