Pombe ikampalia Kikoti. Radio ilikuwa inasema, "Dk. Makete aligongwa kusudi nyuma ya Benki ya Wakulima. Gari lililomgonga ni Benzi jeupe, likiendeshwa na mtu alievaa koti au jaketi la kunguru. Zawadi ya milioni moja iliyochangwa na wafanyakazi wa hospitali itatolewa kwa yoyote atakaesababisha mtu huyo kukamatwa."
Kikoti akaanza kutetemeka. Kila kitu kilikuwa waziwazi. Yule bwana kulitazama gari lake upande wa mbele, kumuonyesha Isidori,kumpa koti lake la kunguru .....kila kitu.
Hata yale maneno aliyoyadaka - 'ajali ...faini..heshima.' yalidhibitisha kitu kimoja tu. Tajiri yake ndie aliyetaka kumwua Dk. Makete. Sasa afanyeje? Alijiuliza. Lazima apate ushauri. Akawatazama wenzake. Akasema, "Bob! Butu! Mmesikia ajali iliyotangazwa?"
"Kikoti!" Alisema Bob kwa sauti yake ya kisajini, "Unasema kweli au umelewa? Maana wisk hii si......"
"Naapa. Nasema kweli. Mtu huyo ndiye tajiri yangu. Ana Benzi jeupe. Alirudi nyumbani boneti na bampa vikiwa vimeharibika. Alivaa koti la kunguru. Akaligawa haraka sana."
Bob na Butu wakatazamana. Kisha Butu akamwambia Kikoti, "Unataka tukusaidie kuipata hiyo milioni? Utatumegea?
"Ndiyo."
"Subirini." Bob akainua mkono. Si ulisema tajiri yako ni kizito?"
"Ni kizito kwelikweli."
"Basi hii nafasi ambayo mtu hawezi kuipata mara mbili katika maisha yake."
"Bob, unazungumza nini?" Butu aliuliza.
"Huyo Makete anatuhusu nini sisi?"
"Bob, mbona sikuelewi!"
"Hii ni nafasi ya kuokota mamilioni, na sio kimilioni kimoja, tena cha kugawana watu watatu." Butu akatikisa kichwa. Akasema, "Naona unakuja na mawazo ya hatari Bob."
"Hatari gani. Toka lini kuukacha umaskini, ulofa, ikawa hatari? Eti Kikoti, huyo tajiri yako hawezi kutupa milioni tatu ili tufumbe mdomo?"
"Anaweza kutoa hata zaidi."
"Unaona?" Bob aliumuuliza Butu.
"Hapana, Bob, mimi simo.Tumefanya mengi ya kipuuzi, lakini hili litakuwa la kichizi." "Butu, utakuja juta. Utakufa bila kushika milioni mkononi mwako."
"Potelea mbali."
"Lakini....lakini...utatufichia siri yetu?"
"Sina ninachokijua. Na hivi naondoka. Nakuacheni mwendelee na mipango yenu."
*************************************
"Mama, Kassim Hashir ndiye nani?"
Walikuwa katika chumba cha mgonjwa. Bi mkubwa aliketi kwenye sofa, Bessy na Denny vitini. Bi mkubwa akashusha pumzi. Akasema "Denny, pengine babako amekosea."
"Umeshamwona akisema neno au akitenda jambo bila ya kuwa na uhakika nalo?"
"Basi tusubiri apate fahamu atakueleza mwenyewe ni nani huyo Kassim Hashir - iwapo ataamua kukueleza."
"Mama, hatuna muda. Huyo hayawani anaweza kuihama tena nchi na kutoweka."
"Yaani umeshapata habari zake!"
"Ndiyo, za kijuujuu. Polisi wana faili lake, na mwandishi mmoja aliwekwa kizuizini kwa kufuatilia kifo cha babake. Inasemekana alimwua. Huyo mwandishi amesema wewe na baba mnakijua kisa hicho. Ni kweli?"
Mama Denny akasita.
"Mama, ni kweli au si kweli?"
"Ni kweli."
"Ndicho kilichomfanya atake kumwua baba?"
"Sikioni kinahusika vipi." Bessy akaingilia, "Tueleze kisa hicho. Sisi tutaamua kama kina uhusiano na tukio la leo."
Baada ya kusita tena, mama Denny akawasimulia kisa hicho......
Wakati huo, zaidi ya robo karne iliyopita, hospitali hiyo ilikuwa ndogo tu. Dk. Makete na mama Denny walikuwa ndio kwanza waoane.
Siku hiyo kama kawaida yao, walikuwa sehemu ya wagonjwa wapya,machela ilipoletwa, ikifuatiwa na msichana wa miaka kumi na mbili, aliyekuwa analia. Wakati mama Denny anamfariji msichana huyo, Dk. Makete alilifunua blanketi akaitazama maiti. Ilikuwa ya mzee wa kati ya miaka hamsini na sitini. Shingo yake ilikuwa imevunjika.
Akaifunika tena na kusema, "Hakuna cha kufanya. Amesha kufa. Amevunjika shingo. Apelekwe chumba cha maiti."
Mama Denny akasema, Rey, unamfahamu marehemu?"
"Hapana. Ni nani?"
"Othman Hashir."
Dk. Makete akaifunua tena maiti na kuitizama sura. Akasema, "Oh, my God! Ndiye. Imekuwaje?"
Msichana akasema huku akiendelea kulia, "Amesukuma."
"Ni nani aliyemsukuma?"
"Kaka Kassim, alimsukuma ghorofani, akabiringika kwenye ngazi."
"My God! Lazima turipoti polisi."
Dk. Makete alipofika Kituo cha Kati, akawekwa benchi asuburi karibu saa nzima. Hatimaye akapelekwa kwenye ofisi ya afisa mmoja wa cheo cha juu.
"Ndiyo, Dk. Makete?" Hakuambiwa aketi. Akasema, "Nimekuja kutoa taarifa ya kifo cha Mzee Othman Hashir. Binti yake anasema kaka yake Kassim Hashir alimsukuma kusudi kwenye ngazi. Kifo kimesababishwa na kuvunjika shingo."
"Dk. Makete," Alisema afisa huyo wa polisi, "Unataka kuyatia maanani maneno ya mtoto mdogo? Nimeambiwa hafiki hata miaka minane."
"Ana zaidi ya miaka kumi."
"Oh, sawa. Tutafanya uchunguzi. Ila ningekushauri uzingatie zaidi kazi yako kuliko kujihusisha na mambo mengine, mambo yasiyokuhusu."
"Ni wajibu wangu kuripoti mauaji." Dk. Makete alisema.
"Sawa. Umesharipoti. Ni juu yetu kuamua kama ilikuwa ajali au mauaji kama unavyodai. Kwisha."
"Usiwe na wasiwasi." Kembo alimwambia Kassim. "Nimepata kijana jasiri wa kuifanya ile kazi. Ataifanya usiku huu. Ametaka milioni saba."
"Sawa."
Wakikuwa sebuleni, wakinywa mvinyo kabla ya chakula cha jioni. Simu ikaita. Kembo akaenda kuisikiliza.
"Hallo."
"Bwana Kessy?" Ilikuwa sauti nzito.
"Hapana."
"Nataka kuzungumza naye."
"Nimwambie nani anayetaka kuzungumza naye?"
"Bob."
Kembo akauziba mdomo wa simu na kusema, "Mtu aitwaye Bob anataka kuzungumza nawe." Kassim akainua nyusi. "Bob nani?"
Kembo akasema simuni, "Bob nani?"
"Bob tu inatosha. Mwambie ni mhimu sana aje simuni. Ni kwa manufaa yake."
Kembo akamwambia Kassim, "Anasema Bob tu inatosha. Anasema ni mhimu sana."
Kassim akainuka na kuupokea mkono wa simu. Akasema, "Yes?"
"Bwana Kessy?"
"We ni nani? Kwa kawaida sizungumzi na watu nisiowajua."
"Hiyo ni kawaida mbovu. Ungekula hasara kubwa kweli kweli."
"Una maana gani?"
""Hukuisikiliza taarifa ya habari?"
Akibana pumzi, Kassim akauliza, "Inanihusu nini?"
"Looh! Inakuhusu sana. Tena sana. Unajua, kuna daktari mmoja aliyegongwa na gari leo asubuhi, nyuma ya Benk ya Wakulima. Wameitangaza habari hiyo. Wamesema kuna zawadi milioni...."
"Unataka kiasi gani?"
"Saba tu Bwana Kessy."
"Laki saba?"
"Laki saba ni kitu gani siku hizi ndugu yangu? Hata banda la kuku hujengi. Nazungumzia milioni saba."
"Unazitaka lini?" Kassim akauliza kwa sauti kavu.
"Biashara sampuli hii bwana Kessy huwa hailazwi,"
"Hujui habari kuwa benki hufungwa usiku? Au unadhani naweka nyumbani kiasi kikubwa kama hicho? Ni wapumbavu tu wafanyavyo hivyo."
"Ah, we ni mtu mkubwa bwana Kessy. Huwezi kukosa ndugu, jamaa na marafiki wa kukuazima kiasi kidogo kama hicho."
"Milioni saba ni kiasi kidogo?"
"Oh, kwa mtu kama mimi ni hela nyingi sana. Lakini kwa mtu kama wewe......"
"Nipigie simu baada ya masaa mawili."
"Maneno si hayo bwana!"
Kassim akaurudisha mkono wa simu kwa nguvu. "Vipi?" Kembo aliuliza.
"Balaa jingine. Anafahamu. Ni Mungu ajuaye ni nani mtu huyo na amejuaje. Anataka milioni saba."
"Nazo ndiyo huna hapa nyumbani?"
"Nina zaidi ya milioni ishirini ndani ya sefu." Kassim alifoka. Akajizatiti na kuzungumza kwa sauti ya kawaida, "Nimetaka muda wa kufikiri."
"Pana cha kufikiri? Nilikwambia kitendo ulichotenda ni cha kipumbavu sana."
"Mbona unanitia wasiwasi Kembo?"
"Nakutia wasi wasi?"
"Ndiyo. Yaelekea unapendelea nililipe hilo baradhuli."
"Sioni kama njia nyingine."
"Unajuaje kama hatakuja kudai tena? Anaweza kunigema hadi shilingi yangu ya mwisho." Kembo akabaki mdomo wazi.
"Kinachonitia wasiwasi zaidi ni kule kufichuka siri hii. Ninavyoamini, mnaifahamu watu wawili tu. Wewe na Isidori."
"Bwana Kessy," Kembo akasema kwa mshangao,"Unataka kunitilia mashaka mimi!"
"Kwa vyovyote msaliti hawezi kuwa Isidori. Kwanza, kama unavyofahamu, tuko nae hapa hapa nyumbani. Hajatoka na hana mawasiliano yoyote ya simu. Pili, ananihusudu vibaya vibaya sana. Yuko tayari kufa kwa ajili yangu."
Kembo akatikisa kichwa akasema, "Nitakwamia jambo moja. Ili kukutoa kabisa mashaka , mimi mwenyewe nitamkomoa mtu huyo na kukuonyesha maiti yake."
**************************************
"Mama, hiyo inaweza kuwa ndio sababu ya kumfanya Kassim atake Kumwua baba?"
"Mlisema nikikuelezeni, mtaamua wenyewe."
Denny akamtazama Bessy, ambaye alitikisa kichwa. Denny akamwuliza mamake. "Kwa nini baba aliendelea kumfuata fuata Kassim?"
"Hakuendelea." Alijibu Bi mkubwa. "Alichofanya ni kumfahamisha Harold, huyo mwandishi."
Denny naye akatikisa kichwa. Akasema, "Mama, kuna kisa kingine." Mama Denny akabaki kimya. "Mama, nakuomba utueleze."
Badala ya kujibu, Bi mkubwa huyoo akadondosha tone la chozi.
"Oh, Mungu wangu!" Dwnny akainuka haraka na kupiga magoti mbele ya mamake. Akaufumbata mkono wake. "Niwie radhi mama."
Bessy akasema, "Denny, umefika wakati wa kumpeleka nyumbani mama."
"Utaweza kuilinda ngome peke yako?" Denny alimwuliza Bessy akimtazama kwa macho makali.
"Kama unadhani nimepewa Uinspekta kwa sababu ya sura yangu, umekosea."
"Twende nikupeleke nyumbani mama."
Bi mkubwa akainuka kwa kujizoazoa polepole akisaidiwa na Denny. "Sitakawia kurudi." Alimwambia Bessy.
"Oh, usiwe na wasi wasi. Kula, oga, badili. Utanikuta hapahapa." Bessy alisema akiokota gazeti.
Denny akaufungua mlango na kumtanguliza mamake. Ukumbini akamshika mkono na kumwongoza kwa hatua za kizee.
Ngazini, wakiteremuka kwa hadhari, wakapishana na kijana anayepanda kwa hima. Denny hakumtazama mara mbili. Hadi walipokuwa kwenye ngazi za ghorofa ya kwanza ndipo kengele ya hatari ilipogonga kichwani mwa Dennis.
"Mama!" Dennis akauachia mkono wa mamake. "Yule kijana haonyeshi kuwa daktari! Nisubiri hapa hapa!"
Akaanza kuzipanda ngazi mbili mbili.
Macho yake kwenye gazeti, masikio yake yakanasa kitu kama hatua zilizokoma ghafla. Bessy akainua kichwa na kuutazama mlango.Kitasa kilikuwa kinazunguka pole pole.
Kufumba na kufumbua, Bessy akawa nyuma ya sofa, mgongo wa kiti hicho umemziba kabisa, ameshaufungua mkoba wake, ameshaitoa bastola, iko imara mkononi, tayari imeshakokiwa.
Akachungulia kwa chini ya mgongo wa sofa, siyo kwa juu. Akauona mlango ukifunguliwa taratibu.
Cha kwanza kupenya ndani kilikuwa ni sailensa. Kisha bastola yenyewe na mkono. Na mwisho nusu ya kiwiliwili cha mtu.
Alikuwa Hoza. Akayazungusha haraka macho yake mekundu humo ndani. Akaamini hamkuwa na mtu mwingine humo ndani zaidi ya mgonjwa aliyelala kitandani.
Hayo yote yalitendeka katika nusu nukta.
Bessy akimwona Hoza wazi wazi, akaamuru. "Dondosha chini bastola yako. " Sauti yake ikavuma humo ndani.
Hoza akashtuka. Akayaondosha macho yake kitandani na kuyazungusha tena humo ndani. Asione mtu.
Akamlenga Dk. Makete .
Bessy akabana pumzi na kukivuta kilimi cha bastola yake. Ikalipuka kwa kishindo cha kumtia mtu uziwi wa muda.
Risasi akakita katikati ya paji la uso na kuwa kama ndonya ya Kigogo. Nguvu zake zilimsomba Hoza, zikamrusha kinyumenyume, na kumbwaga kwenye korido, kando ya miguu ya Dennis aliyewasili nukta hiyo hiyo.
Dennis akautazama mwili wa Hoza na kuiona ndonya. Akauliza kwa ukali, "Ilikuwa lazima?" Bessy akiwa ameshainuka, na yuko katikati ya chumba, akafoka, "Una maana gani 'ilikuwa lazima'?"
"Ilikuwa lazima umwue? Angekuwa hai tungemhoji."
"Na mzee angekuwa amekufa." Bessy alijibu.
"Au unataka kuniambia hiyo bastola yake ni ya bandia?"
Dennis akaitupia jicho bastola yenye sailensa iliyokuwa kwenye korido,hatua kadhaa mbali na maiti. Haikuonyesha mzaha hata chembe.
Denny akainua mikono na kusema, "Yamekwisha."
"Bora yaishe." Akasema Bessy kwa sauti yake tulivu ya kawaida. "Watu wanaanza kusogea sogea."
"Ilete ndani bastola yake." Dennis alimwambia, akiinama na kuishika miguu ya maiti.
Bessy akaguna, "Denny!"
"Kitu gani?"
"Hatupaswi kitu chochote. Inapasa kupiga simu kituoni na kuwaarifu wenzangu. Watakuja...."
"Achana nao. Utawaarifu baadaye. Ilete bastola yake." Dennis akasema akiiburutia maiti chumbani.
Bessy alisita kidogo, kisha akabetua mabega na kuokota bastola ya Hoza. "Iweke mezani." Dennis akamwambia. "Nenda kwenye ngazi za ghorofa ya kwanza, mchukue mama umtafutie usafiri."
Bessy akakubali kwa kichwa na kutoka . Denny alipokuwa anaufunga mlango, mwuguzi msimamizi wa wodi hiyo akataka kuingia. Denny akamzuia.
"Pametokea nini?" Aliuliza mwuguzi huyo, akijaribu kuchungulia ndani, macho yamemtoka pima.
"Tatizo dogo tu." Denny akamjibu. "Kaendelee na shughuli zako."
"Nimesikia mshindo. Kama .... kama bunduki."
"Ilikuwa ni bastola ya Inspekta Bessy. Usiwe na wasi wasi . Taarifa kamili utaipata baada ya muda mfupi tu.
Mwuguzi akasita, akiona vigumu kuondoka bila ya kuingia ndani na kuchunguza kama wajibu wake ulivyo. Lakini hapakuwa na nafasi ya kupenya ndani bila kutiana mieleka na kijana huyu. Na hilo halikuwa katika ajenda yake ya wakati huo.
Hatimeye akauliza. "Mzee Makete yupo salama?"
"Kama hazina ya taifa." Dennis akamhakikishia. "Usiwe na wasiwasi hata chembe. Nakuzuia kwa sababu kuna kazi ndogo ya kipolisi. Inspekta Bessy ameua jambazi lililoingia na bastola. Lakini hakuna madhara yoyote kwa babangu."
Mwuguzi akaonyesha kuridhika. Dennis akaufunga mlango. Akaichukua bastola yenye sailensa na kuichunguza. Akashangaa wapi watu hawa wanapata silaha za hatari kama hiyo!
Akairudisha bastola mezani na kuigeukia maiti. Baada ya kuitizama kwa nukta moja au mbili akaanza kushughulika.
Aliivua nguo zote, hata chupi. Kisha akazipekua kwa uangalifu, akitoa kitu kimoja kimoja, akakiangalia kwa makini kabla ya kukiweka mezani.
Bessy aliporejea, alikuta akiigeuza maiti na kuichunguza. Mwana mama akalalama. "Mtume! Dennis unafanya nini? Hiyo si kazi yetu! Kuna watalaamu...."
"Ambao huchukua siku kadhaa kuichunguza maiti, wakiringia utalaamu wao, kisha wakueleze jambo ambalo ungefahamu katika dakika mbili tu!"
Bessy akashusha pumzi na kujibwaga kwenye sofa. "Denny, wakuu wangu wakigundua nimekuacha ufanye hivyo...."
"Hukuniacha. Hukuwepo. Ulikwenda kumtafutia mama usafiri. Je, umempatia?"
"Ndiyo. Nimemchukulia teksi."
"Hakukudadisi?"
"Alitaka kujua ule mshindo ulikuwa wa nini."
"Ukamwambiaje?"
"Tanki la maji limepasuka."
Dennis akakubali kwa kichwa, akiwa ameridhika. Akasema. "Sawa kabisa."
Bessy akauliza, "Denny, kitu gani kilichokurudisha? Yaani ulipotoka na mama?"
"Huyu nyani. Nilipishana naye ngazini. Lakini sikumtanabahi hadi nilipokuwa kwenye ngazi za ghorofa ya kwanza."
"Kitu gani kilichokufanya umshuku?"
"Macho yake na nywele zake." Dennis alijibu, akiendelea kuikagua maiti.
Bessy akasema, "Denny kadri ninavyochelewa kupiga simu kituoni, ndivyo unavyozidi kunitia matatani."
Watu wanne waliketi wakinywa na wakisubiri kwenye sebule ya nyumba Namba 21 mtaa wa kitosi, eneo la Buffalo Hill. Kessy au Kassim Hashir na Kembo waliketi upande mmoja wakinywa kimya, nyuso kavu. Chiko na Fensy waliketi upande mwingine wakinywa huku wakizungumza na kucheka.
Baada ya muda Kassim akaitazama saa yake ya dhahabu na kusema. "Kwa nini huyu mwanaharamu hapigi simu? Tulikubaliana masaa mawili, yanakaribia masaa matatu sasa!!"
"Anataka uvuje jasho kidogo." Kembo alimwambia. "Anataka utaharuki. Katika hali hiyo unakuwa fal@ zaidi, unafanya chochote anachosema, tena mbio mbio."
"Mwana wa mbwa koko."
"Sikiliza Bwana Kessy, atakapopiga simu ni mimi nitakayezungumza naye, siyo wewe. Na nyote pamoja na nyinyi Chiko na Fensy - mtanyamaza kimya kabisa. Akijua tuko wengi anaweza kugutuka. Tumeelewana?"
"Ndiyo."
"Nitajaribu kuiga sauti yako."
Kembo aliendelea akimtazama Kassim.
"Pengine ni mtu anayekufahamu."
"Sidhani." Akasema Kassim. "Sauti yake ilikuwa ngeni kabisa."
"Anaweza kuwa ameibadili, simuni kitu kama hicho ni rahisi sana." Kengele ya simu ikalia. Akasema. "Hapana hata kukohoa kwa sauti."
Kila mmoja akakubali kwa kichwa, kama vile kipindi cha ukimya kimeshaingia.
Kembo akainuka akaenda kwenye simu, akauinua mkono wa kusikilizia na kuuweka sikioni. Akiigiza sauti nzito ya Kassim akasema, "Yes?"
"Bob."
Kikapita kimya cha nukta mbili au tatu kisha. "Je, mwenzangu ni Bwana Kessy?"
"Ndiyo."
Kimya kingine kifupi kisha, "Je, umefanikiwa?"
"Ndiyo." Kembo alijibu.
"Zote saba?"
"Ndiyo."
"Very good. Sasa sikiliza kwa makini. Saa sita kamili uendeshe gari lako kwenye barabara ya Kaskazini. Ukilivuka tu daraja la Singisa utaona kibanda cha simu mkono wa kushoto."
"Nakifahamu."
"Good. Ufikapo hapo punguza mwendo, rusha mkoba wenye fedha na uendelee na safari yako.
"Umenipata?"
"Vizuri kabisa."
"Very good. Usiku mwema."
"Subiri." Kembo akasema haraka.
"Nini tena?"
"Najuaje hii itakuwa ndiyo alfa na omega?"
"Una maana gani?"
"Najuaje hurudi tena kutaka fedha zingine?"
"Bwana Kessy mimi si fisi. Hivyo sina tamaa ya fisi."
"Kudai milioni saba siyo tamaa ya fisi?"
"Unataka nikachukue milioni iliyotangazwa? Sikiliza we fal@. Mimi nakufanyia hisani kubwa sana. Dk.Makete yu mahututi. Ulimgonga kusudi. Lilikuwa jaribio la kuua. Hata akipona, unaweza kufungwa maisha."
Kikapita kimya cha zaidi ya nukta kumi, kila pande ikipumua kwa nguvu. Hatimaye Bob akauliza.
"Umenipata vizuri?"
Kembo akasema, "Wewe ni mwanaharamu, mtoto wa mbwa koko, mjaa mavi uliyelaaniwa."
"Umemaliza?"
Kembo hakujibu
"Bob akaendelea. "Itasaidia nini? Hata ukinitwisha kontena zima la matusi, itasaidia nini? Wewe umeshaimeza ndoano na mshipi wake. Hufurukuti. Utafanya uambiwacho."
"Usiwe mpumbavu kiasi hicho. Mimi nina pesa. Naweza kuyeyuka sasa hivi."
Bob akapumua kwa nguvu, kama aliyepigwa ngumi ya tumbo. Pumzi zilipomrudia akasema, "Polisi watakusaka. Watajua ni wewe uliyemgonga Makete. Habari zitazagaa magazetini. Heshima yako kwisha. Pamoja na mamilioni yako, utaishi kama panya ndani ya shimo."
Kimya cha safari hii kilichukua karibu dakika nzima.
Hatimye Bob akasema, "Sema fyoko!"
Kembo hakusema
Bob akaunguruma kwa sauti yake ya kisajenti. "Saa sita kamili."
Simu ikafa. Taratibu Kembo akaurudisha chini mkono wa simu.
Kassim akasema, "Kembo, palikuwa na haja ya kubishana naye vile?"
"Alinijazibisha, mwana hizaya." Alijibu Kembo. "Mambo yakienda kombo ataleta ushenzi." Alisema akiwakazia macho Chiko na Fensy na kuongeza, "Kwa sababu hiyo sitaki yaende kombo. Mmesikia, sitaki mboronge."
"Amesema saa sita kamili." Kembo akasema akirudi mahali pake. Akaitazama saa yake. "Tuna muda wa kutosha."
Akajitilia kinywaji, akakimeza na kuendelea.
"Pesa zikadondoshwe kwenye kibanda cha simu cha karibu na daraja la Singisa saa sita kamili. Amejua kuchagua mahali pazuri, kwake na kwetu. Mahali hapo saa sita kamili ni sawa na makaburini.
Akajiwashia sigara na kuendelea, akiwaambia Chiko na Fensy. "Mahali hapo pana sehemu nyigi za kujibana, mojawapo ikiwa ni chini ya hilo daraja."
"Tunapafahamu." Alisema Fensy.
"Kumsubiri huyo Bob. Lakini msifanye lolote mpaka mmwone akiuufuata mkoba wa fedha na akiinama kuuchukua. Msije mkamdhuru mtu mwingine, ingawa uwezekano huo ni mdogo sana kwa mahali hapo saa hizo. Sawa?"
"Sawa." Vijana hao walijibu wakimalizia vinywaji vyao.
"Itakuwa ni vizuri zaidi kama mtamshika akiwa angali hai, ili tumhoji kwanza. Tujue siri hii ameijuaje, na kama kuna mtu mwingine anaijua."
"Sawa. Tunajua nini cha kufanya." Alisema Chiko.
"Mimi nitakuja na fedha saa sita kamili. Nitaudondosha mkoba na kuendelea na safari kama alivyoagiza."
"Sawa."
Kembo akamtazama Kassim na kumwambia, "Bwana Kessy, kajaze magazeti ya zamani kwenye mkoba."
*****************************
"Huyu nguruwe ni Hoza Kamkimbile, kama kitambulisho chake ni cha kweli." Alisema Dennis akikitumbukiza mfukoni kitambulisho hicho.
Bessy akamkuta, "Denny! Unafanya nini?"
"Enh?"
"Huruhusiwa kuchukua chochote."
"Ooh, ninakiazima kwa muda mfupi tu. Nitawarudishia kesho. Pamoja na huu ufunguo. Ni ufunguo wa chumba Namba 408 cha Tupetupe Hotel."
Bessy akatikisa kichwa kwa masikitiko. "Denny, ikigundulika......."
"Nitabeba lawama zote."
Dennis akaanza kuivika maiti. "Ana makovu kadhaa ya visu. Mawili mabaya. Moja ni la zamani sana, zaidi ya miaka kumi iliyopita. Ndiyo kusema ukora aliuanza utotoni."
"Ni hilo ulilogundua?"
"Nimegundua pia alikuwa mtu wa madawa ya kulevya. Aliyauza na kuyatumia. Mtu wa aina yake hawezi kuwa mgeni kwenu. Lazima mtakuwa na faili lake. Pengine amewai hata kufungwa."
"Sawa nitakwenda kupekua." Alisema Bessy na kuongeza, "Ni wazi ametumwa na huyo Kassim Hashir."
"Ni wazi." Alijibu Denny. "Ni madawa ya kulevya yanayowafanya wawe na shida kali ya pesa. Ni ghali mno na wanapoyatumia huwapa ujasiri wa bandia, huwafanya watende lolote lile bila woga."
Bessy akakubali kwa kichwa. "Ndiyo maaana katika nchi zingine kama Arabuni na Indonesi, adhabu yake ni kifo."
Baada ya kimya kifupi, Dennis akasema, "Unaweza kwenda kuwapigia simu wenzako. Mimi hawatanikuta. Nakwenda nyumbani. Na wewe pia nenda nyumbani ukapumzike. Weka mtu mwingine wa kulinda, ingawa sidhani kama patatoke lolote jingine usiku huu."
"Denny utakwenda Tupetupe?" Denny akasita kabla ya kujibu. "Labda usiku wa manane, baada ya usingi wa masaa mawili au matatu."
"Lazima twende sote."
"Hapana Hoteli hiyo hawaendi wanawake wenye heshima zao."
***************************************
Naam, palikuwa mahali pazuri kwa mahepe, ngoma ya wanga. Palikuwa kimya na patupu. Hapakuwa na wapita njia, na magari yalipita kwa nadra sana.
Taa za barabarani zilikuwa pande zote mbili za daraja. Lilikuwa daraja refu lakini haukuwa mto mkubwa. Na kwa vile ilikuwa kiangazi, ulijaa zaidi mchanga kuliko maji.
Wakiwa wamevaa nguo nyeusi, chini ya daraja, Chiko na Fensy walikuwa kama vivuli. Walijibnza sehemu nzuri, wakikiona wazi wazi kibanda cha simu. Fensy akasema, "Nina kiu ya sigara."
"No." Akamaka Chiko. "Hakuna kuvuta. Hakuana kubananga."
"God! Sikujua kama patakuwa na baridi kiasi hiki! Kwa ninitukaja mapema kiasi hiki.... kabla hata ya saa tano!"
"Ulitaka tuje saa sita kamili?" Aliuliza Chiko. Unajua vizuri sana ilibidi tuje mapema. Huyo mwanaharamu anaweza kuwa hapahapa anatuangalia."
"Kama atakuwa eneo hili ana digrii ya kazi hii. Nimelikagua eneo lote na sikuona hata mzoga wa panya."
"Kama hayupo basi ni chizi, amevamia kazi asiyo na ujuzi nayo. Laiti ningekuwa mimi ningeitumia simu ile pale, na kisha nisingeondoka mahali hapa mpaka hizo pesa zimeletwa. Na nisingezichukua mpaka nimehakikisha hakuna unyayo wowote. Nisingeacha nitumbukie katika mtego wa kipumbavu hivi!"
"Wewe ungechukua tahadhari hizo kwa sababu kwanza, hii ni kazi yako, na pili unafahamu kuwa Bwana Kessy ana watu kama Kembo na sisi. Nina hakika huyo Bob hafahamu hivyo. Anadhani kuwa Bwana Kessy yuko peke yake. Ndiyo maana Kembo alitutaka tuwe kimya kabisa wakati anazungumza naye simuni. Hakutaka kumgutusha. Alitaka abaki na uzumbukuku wake."
"Na kweli ni zumbukuku kweli kweli. Bila ya kuchukua tahadhari yoyote mbele ya milioni saba, kama vile zinatingishwa mtini
"Ooh, karibu watu wote wanaodaipesa za kifumba mdomo ni wapumbavu." Alisema Fensy. "Hugundua siri ya mtu kwa bahati tu, kisha huingiwa na tamaa na kuanza kudai, bila kufikiri wala kupanga. Wakati mwingine matokeo yake huwa ndio haya - kumdai kifumba mdomo mtu kama Kessy."
Wakasikia mvumo wa gari, wakaona VW [kobe] kuukuu likivuka daraja na kuegsha pembeni, mkono wa kulia, kama hatua thelathini kutoka kwenye kibanda cha simu.
"Wako wawili." Alisema Chiko akiitazama saa yake. "Saa sita kasoro tano. Ni wehu. Siyo wapumbavu."
"Utakuwaje na hakika kuwa ndio wao?" Fensy aliuliza.
"Unataka tuwekeane dau? Hamsini kwa laki."
"Sina pesa ya kuchezea."
"Sikiza." Chiko akasema kikazi. "Ni mmoja tu atakayeshuka kuufuata mkoba wa fedha. Huyo atakuwa ndiye wako. Atakaye baki garini ndiye wangu. Wako usimcheleweshe. Tutamhoji atakayebaki garini."
"Sawa."
"Sasa tumsubiri Kembo alete hiyo fedha." Alisema Chiko na kuitizama saa yake tena. "Bado dakika mbili."
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.