Riwaya: Msako wa Hayawani

Riwaya: Msako wa Hayawani

SEHEMU YA ISHIRINI NA NANE



Bessy akakijaza kikombe cha chai, akauliza, "Ilikuwaje usiwe na msichana hadi makamo hayo?" Dennis akakipokea kikombe akasema, "Huko ninakoishi wasichana ni bidhaa adimu sana. Mno ni manyani tu."
Bessy, akakijaza kikombe chake. Akatabasamu na kuketi akauliza, "Ulitarajia kuishi porini huko hadi lini?"


"Sijui." Denny alijibu. "Jana nilipoirudisha jeep na kuomba likizo ya dharura, Kanali aliniambia nakaribia kupewa Ukapteni na kuhamishiwa kitengo kingine."
"Kitengo gani?"
"Hakusema waziwazi ni kitengo gani. Lakini nashuku kitakuwa kitengo cha Busara - yaani Intelligence - Makao Makuu."
"Itakuwa safi sana. Tutakuwa tukionana mara kwa mara."
"Lakini patakuwa na mafunzo kwanza bila shaka. Pengine ng'ambo."
Denny akanywa funda la chai. Akauliza, "Wewe je?"
"Mimi kitu gani?"
"Imekuwaje usiwe na mvulana?"
"Ooh, nimeshafanya urafiki na wavulana wawili watatu. Mara mbili nilikaribia kufunga ndoa, lakini mara zote nikaghairi dakika za mwisho."
"Kwa nini."
"Kila mtu humwona ana walakini - maneno mengi, ahadi tele, mbwembwe, mikogo... aah, unafiki mtupu!"
"Wasichana wengi huvutiwa na hayo." Alisema Denny.
"Nao pia ni wanafiki." Alijibu Bessy
"Au ni mazumbukuku."
"Mimi je? Ni mnafiki pia?"


"Ooh, wewe uko tofauti. Kwani mwenyewe hujioni ulivyo?"
"Kuna mtu anajiona alivyo kikweli kweli?"
"Wapo." Alijibu Bessy. Kisha akaminya uso. "Lakini hapana. Nadhani ni kweli. Hakuna mtu anayeweza kujiona alivyo. Hao wanaodhani wanajijua walivyo wanajihadaa. Kila mtu hujiona mwema, mzuri. Hata Hitler, Amin na Mobutu walijona kama malaika."
Denny akakubali kwa kichwa akasema, "Hebu niambie. Umesema niko tofauti nikoje?"
"Ooh, uko kama nyani."


Wote kwa mara ya kwanza tangu wakutane wakacheka, kicheko cha dhati. Bessy akasema, "Hebu niambie, ni kitu gani kilichokuvutia kwangu?"
"Sijui." Alijibu Denny. "Labda kwa vile wewe ndiye mrembo wa kwanza na wa pekee kukutana naye tangu niachane na manyani wenzangu. Lakini nadhani hasa ni kwa sababu ya jeuri yako. Msichana mrembo kama wewe hupaswi kuwa jeuri hivyo."
"Mimi jeuri?"
"Mwenyewe hujijui?" Wakacheka tena. Baada ya kimya kifupi Bessy akasema. "Kwa hiyo tumekubaliana?"
"Ndiyo." Denny alijibu haraka.
"Chagua siku uipendayo. Mimi niko tayari kabisa. Nna hakika."
Bessy akaminya uso akauliza, "Unazungumzia nini wewe?"
"Harusi yetu."
"Idiot! Sijakwambia nakupenda. Sijakwambia niko tayari kuolewa na wewe?"
Denny naye akakunja uso. "Kumbe unazungumzia nini? Tumekubalina kitu gani?"
"Kwenda kupambana na Chiko>"
"Aah! Hilo mbona tumeshalimaliza."
"Denny, huwezi kwenda peke yako."

"Sikiliza. Ngoja nikwambie mambo mawili. La kwanza, ninapotoa ahadi, iwe kwa Musa au kwa Firauni sirudi nyuma. Na pili Chiko akiona tupo wengi atakimbia. Tutakuwa hatukufanya lolote."
"Sikiliza. Acha nichukue watu wawili au watatu tu. Watajibanza garini. Nitachagua watu wa uhakika."
Denny akatikisa kichwa. "No way, baby."
Bssy akakibamiza kikombe mezani na kufoka, "Laanakum wewe! Laanakum wewe! Mbishi kama - laanakum."


****************************************


Chiko aliipunguza mwendo pikipiki, akaiacha barabara kuu na kupinda kulia. Akaongeza mwendo na kutimua vumbi, akiukumbatia mkoba wa ngozi uliokuwa mbele yake kwenye tanki la petroli.
Kiwanda cha zamani cha sukari kilikuwa kilometa nne kutoka barabara kuu. Kikiwa kimekufa miaka kadhaa nyuma. Kilichobakia ni magofu tu yaliyotelekezwa na kushambuliwa na wezi wa mabati, mbao, milango, madirisha na chochote kile chenye manufaa.

Sasa yalikuwa magofu uchi, yapigayo miayo, yaliyonyukwa na mvua kadhaa za masika na jua kali la viangazi na kuzungukwa mbudu na ukoka. Upande wa pili palikuwa na masalia ya majengo ya ofisi, na kushoto masalia ya korona na ghala, na katikati palikuwa na uwanja.
Ilimchukua Chiko dakika chake tu kufika hapo, wakati jua likianza kuwa jekundu upande wa Magharibi. Akaiona pikipiki ya Fensy iliyoegeshwa mbele ya jengo la korona.


Akaisimamisha pikipiki yake kando ya pikipiki ya Fensy. Akaizima na kuteremka, akiuchukua mkoba wake wa ngozi. Fensy akachomoza kwenye kona ya lango la korona. Chiko akamwuliza, "Mambo?"
"Poa kama jahannam,"Alijibu Fensy.
"Hakuna chochote kilichotokea?"
"Si mtu, si jini. Upepo tu ukipiga miluzi kwenye haya magofu ya kichawi. Unaonaje, inawezekana asije?"


Chiko akaitazama saa yake. Akasema, Tutaonana baada ya robo saa. Kama ana chembe ya busara hatakuja." Akaufungua mkoba na kutoa SMG iliyokatwa kitako. "Au atakuja na kikosi. Nyuma kuko wazi?"
"Wazi kama jahannam - hakuna kikwazo ." Alijibu Fensy. Akaongeza, "Lakini nisingependa kuiacha pikipiki yangu, ingawa imechakaa."
"Hata mimi . Naamini hatutaziacha."


*************************************


Dennis aliitizama saa yake, akasema, 'wakati' na kuinuka. Bessy akainuka pia, macho yamemuwiva. Akasema, "Denny, uwe mwangalifu tafadhali."
"Ndiyo, nitakuwa mwangalifu." Alisema Dennis. "Sikiliza, usitoke hapa. Kuwa karibu na simu. Ukiona kimya hadi saa kumi na moja na nusu, chukua kikosi mje kiwanda cha zamani cha sukari. Niahidi utafanya hivyo, na si lolote jingingine."


Dennis akawasili kwa kasi kiwanda cha zamani cha sukari, akitimua vumbi. Akaziona pikipiki zilizoegeshwa mkono wa kushoto, akalisereresha gari mkono wa kulia. Likaenda kutulia mbele ya gofu la mwisho, mabaki ya ofisi ya meneja wa kiwanda hapo zamani.
Akaufungua mlango wa gari, akachupa na kujibiringisha, akifuatiwa na mvua ya risasi za SMG iliyokuwa ikichakarika kwenye lango la korona.


Alipopenya tu ndani ya gofu hilo, Denny akainuka, akaichomoa bastola na kuangaza haraka humo ndani. Uwazi wa mahali lilipokuwa dirisha la nyuma ukamkenulia. Akaruka na kusimama nyuma ya gofu, akisikiliza kwa makini.
Kwa nukta kadhaa kote kulikuwa kimya isipokuwa kuvuma kwa upepo. Kisha akaisikia sauti ya Chiko ikiita kwa mbali. "Hey! School Boy! Niko hapa." Dennya akatambaa kinyoka kwenye majani yaliyozunguka gofu hilo akachomoza kichwa na kuliona gofu la korona. Akamuona Chiko akizungumza na kumfanyia ishara mwenzake. Kisha akaachia risasi za mfululizo, akilishambulia gofu la ofisi.


Wakati huohuo Fensy akatoka mbio, bastola mkononi akilifuta gari. Akachungulia ndani, akitazama kama mlikuwa na watu waliojifcha. Kisha akanyata, akajibanza na kuchungulia ndani ya gofu. Alipohakikisha liko tupu akapenya ndani kwa tahadhari, bastola ikilenga mbele.
Denny akajikunja na kumfuata. Akamkuta akivhungulia kwenye uwazi wa dirisha. Ingekua rahisi sana kumrukia hata kama Denny asingekuwa na Bastola mkononi. Lakini badala yake, akamwamuru, "Ganda."


Fensy hakuganda. Alishtuka, akageuka kwa kasi, akiachia risasi ovyo. Zote zilipita juu, Kwani Denny alikuwa amechutama. Akaachia risasi mbili. Zikamsomba Fensy mzimamzima na kumrusha nje ya uwazi wa dirisha na kudondoka chini kwa kishindo.
Denny akageuka na kuchungulia nje, kwenye gofu la korona. Kote kulikuwa kimya, kumetulia tuli, isipokuwa upepo ukipeperusha vumbi. Akatambaa hadi nyuma ya gari na kujibanza. Akaukinza mdomo wake kwa viganja na kuita, "Chiko!"


Chiko akachomoza uso kwenye lango la korona na kuita "Fensy? Vipi?" Denny akalitambua kosa la Chiko. Alimdhania mwenzake,Denny akaamua kubahatisha. Akaukinza tena mdomo wake na kusema, "Tayari mshenzi kaniumiza mguu."
Chiko akasita kidogo, kisha, akachomoza, SMG madhubuti mkononi. Akaanza kutembea kwa tahadhari, macho yake na mdomo wa mtutu kwenye mlango wa mabaki ya ofis ya meneja wa kiwanda.


Alipofika katikati ya uwanja, Denny akainuka ghafla nyuma gari, mdomo wa bastola ukikilenga kichwa cha mkora huyo. Akamwamuru, "Dondosha."
Chiko akaganda, akageuza kichwa, akatoa kichwa kwa mshangao wa dhati. Akanong'ona kama anayeota, "School Boy!"
"Ndiyo." Dennya alimjibu. "Ni School Boy yuko darasani. Dondosha hiyo Bunduki."


************************************


Bessy aliposema angevuja jasho kila nukta ya dakika hizo zote hakuwa akidhihaki. Kwa sababu kama - kama hapakuwa na sababu yoyote nyingine ya maana - kwa sababu kama Dennis angefikwa na balaa lolote huko kiwanda cha zamani cha sukari, hata kujeruhiwa tu, yeye Bessy angewajibika.
Akiwa afisa wa polisi hakupaswa kumwacha mtu ahatarishe maisha yake kwa kupambana na magaidi hatari. Hata kama mtu huyo alikuwa ni komandoo wa Jeshi la Ulinzi. Hii ilikuwa ni kazi ya polisi. Hivyo sasa Bessy alikuwa anajuta.


Muda wote huo akitokwa jasho. Na hakuweza kutulia. Mara aketi, mara ainuke na kutembea tembea hapo sebuleni. Na wakati wote mara aiangalie saa yake, mara aiangalie simu, huku akihimiza, "Come on boy! Come on boy! Come on boy!"
Hivyo, simu ilipolia, jinsi alivyoruka ni kama aliyegusa umeme. Haishangazi. Akaunyakua mkono wa simu na kusema, "Hallo Denny!"
"Bessy?"
Haikuwa sauti ya Denny bali ya Kamishna Msaidizi wa polisi. "Bessy . Mbona hujaripoti mpaka saa hizi?"
Bessy akakumbwa na fazaa. Akababaika, "Mzee, Mzee, nna - nnamsubiri Denny."
"Kwa nini?"
"Amekwenda - amekwenda kiwanda cha zamani cha sukari."
"Kufanya nini?"
"Kukutana na Chiko."


"Mbona sikuelewewi, Bessy!" Alisema Kamishna Msaidizi. "Unazungumza kitu gani?"
"Ooh, samahani sana kwa kukuficha Mzee. Ukweli ni kwamba Denny anakichwa kigumu sana. Amepatana na Chiko kukabiliana huko kiwanda cha sukari, na amekataa kufuatana na mtu yoyote."
"Mungu wangu, Bessy! Umeruhusu kitu kama hicho?"
"Ningefanya nini, Mzee? Amesema hakuna njia nyingine. Vinginevyo tutamkosa Chiko, na yeye ni Komandoo."
"Hata angekuwa nani!" Kamishna Msaidizi alifoka. "Yeye si polisi. Ni afadhali kumkosa huyo mlaaniwa kuliko kuhatarisha maisha yake. Akiumia sisi wote tutaonekana wazembe wakubwa! Sasa sikiliza. Jitayarishe. Natuma watu watatu wakupitie."
"Lakini Mzee, nimemwahidi sitafanya lolote hadi saa kumi na moja na nusu."
"Sitaki kusikia upuuzi wowote. Gari litakuwa hapo baada ya dakika mbili au tatu."


Simu ikakatwa. Bessy akapumua. Kwa upande alifurahi. Kwani alikuwa akitii amri ya mkuu wake, hakuwa akivunja ahadi kusudi.
Alipomaliza kufunga milango tu akasikia king'ora cha gari la polisi likija kwa kasi


Itaendelea
 
idawa naona umeskia kilio cha wananchi, Thanks ila endeleza hata sehemu moja tu
 
Last edited by a moderator:
Asee idawa usione pako kimya humu ukadhani hatupo! Mamia wanapita kimya kimya tu.
 
Last edited by a moderator:
SEHEMU YA ISHIRINI NA TISA




Chiko akasita, macho yake yakizungumza waziwazi mawazo yake. Alikuwa akikadiria ingemchukua sehemu gani ya sekunde kuugeuza mdomo wa bunduki mzunguko wa nyuzi kama ishirini au thelathini,na ingemchukua Denny sehemu gani ya nukta kukivuta kilimi cha bastola yake iliyokuwa imemlenga.
Kisha akaona macho ya Denny yanavyowaka. Akasisimka mwili mzima na kuibwaga SMG. Ulikuwa mtego. Denny naye akaidondoasha bastola na kuanza kumfuata kwa hatua za polepole, macho yao yameumana.


Alipobakiza hatua tano, Chiko kwa kasi ya chui akaichupia SMG. Vidole vyake vilikwishagusa chuma alipofumuliwa teke la kifuani lililompindua chali.
"Inuka." Denny alimwamuru.
Chiko akakurupuka kama nyati aliyejeruhiwa. Akakutana na teke la mzunguko lililombwaga kifudifudi. Denny akamkwida ukosi na kumwinua. Akamzungusha na kumnyuka ngumi nne za mfululizo.


Chiko akapepesuka. Akakung'uta kichwa kuondosha ulevi na nyota zilizomzonga. Akajizatiti na kukumbuka yeye ni nani. Akakurupuka tena! Akarusha ngumi, akarusha teke. Vyote viliambulia patupu. Akajirekebisha na kujaribu kujiweka sawa. Akarusha ngumi, akarusha teke. Akajikuta anakata tena hewa na kuzidi kujichosha. Denny akajizungusha na kumfumua teke la juu kwa juu. Chiko akapepesua. Akafumuliwa teke la usoni. Akadondoka 'puu' kama gunia la mchanga. Alipotaka kuinuka Denny akamkanyaga kwa nguvu kwenye uti wa mgongo. Mfupa ukalia 'ko', Chiko akapiga yowe na kurudi chini kifudifudi.


"Huo," Denny akamwambia, "Ni mfupa wa kiuno. Ili kuhakikisha huinuki tena katika maisha yako yote. Wala huketi. Wala huchutami. Wala hutambai. Sasa wewe ni mtu wa kubebwa na kugeuzwa tu kama maiti. Na huo ni mwanzo tu." Denny alimfahamisha. Akamuuliza kwa ukali. " Wapi anaishi Kassim Hashir?"
"Go to hell."
"Hajahamia huko bado." Denny akamnyuka teke la mdomoni. Chiko akatema damu na meno mawili.
"Wapi nitampata Kassim Hashir?"
"Nakwambia simjui jamaa huyo." Chiko aliloloma.
"Namtaka mtu aliyemgonga babangu. Na utaniambia tu alipo, pamoja na ubabe wako. Ikibidi nitakung'oa meno yote. Na kisha niivunjevunje mifupa yako yote."
"Nakwambia aliyemgonga babako haitwi hivyo."
"Potelea mbali anaitwaje. Nataka kujua anakoishi."


"Sikujui anakoishi."
"Sikuamini."
"Shauri yako."
Chiko akala teke jingine na kutema jino jingine. Akaloloma, "Nakwambia kweli. Sijui anakoishi. Nilikwenda kwake mara moja tu, tena usiku. Huko Buffalo Hill."
"Ulifikaje?"
"Nilipelekwa na...na..."
"Na nani?"
Chiko akabaki kimya. Denny akainua mguu, lakini Chiko akamzuia. "Subiri! Nilipelekwa na Kembo. Sam Kembo."
"Ndiye nani huyo?"
"Rafiki yake huyo aliyemgonga babako."
"Yaani ndie mtu wa kati baini yenu na huyo Kassim Hashir?"
"Ndiyo."
"Nitampata wapi?"
"Sijui"
Denny akaanza kulitayarisha teke.

"Subiri!" Chiko akasema kwa haraka. "Anatusuburi Flamingo Guest House, chumba Namba 202."
"Kama unanidanganya, ole wako. Nitakurudia. Na ujue nitakukuta hapa hapa, hivyo hivyo ulivyo."
"Kwa nini nidanganye? Mimi nimekwisha, kwa nini wao wapone?"
Denny akaifuata bastola. Alipoinama aiokote akasikia king'ora cha polisi. Akaiokota, akageuka na kuitazama barabara.


Golf ilikuwa ikija kasi, ikitimua vumbi. Ikaserereka na kusimama. Bessy akatoka mbio, akaita "Denny!" Akajitupa kwenye kifua cha Denny, huku akicheka na akilia wakati huo huo.
Denny akampigapiga mgongoni, akimwambia, "It's okay baby. It's okay." Akawatazama askari watatu wakitoka garini, kila mmoja kakumbatia SMG. Akawaambia, "Naona mmechelewa kidogo mabwana. Mchezo umekwisha. Majeruhi huyo hapo, na mzoga uko nyuma ya gofu lile."


"Ni wao wawili tu?" Askari mmoja aliuliza.
"Ni wao tu."
Askari mmoja akamwendea Chiko na kumtekenya kwa kiatu. Hey, wewe! Inuka twende."
"Siwezi." Chiko alilalama. "Mwanakharamu kanivunja kiuno."
Bessy akamtazama Denny, macho yake yakimshutumu.
"Kaniita School Boy."
"Hilo ni tusi kubwa?"
"Akha, shika!" Akamkabidhi bastola yake. "Twende zetu. Kuna kazi ya kufanya."
"Wapi?" Bessy aliuliza, wakielekea kwenye gari.


"Flamingo Guest House. Kukanyaga ngazi ya mwisho. Mtu mmoja aitwaye Sam Kembo. " Denny akaliwasha gari na kuling'oa. Akasema, Kwa hiyo hukuweza kusubiri hadi saa kumi na moja na nusu?"
Hapana, Nimelazimishwa na Kamishna Msaidizi nikufuate pamoja na wale askari watatu. Lakini nilifurahi. Jinsi nilivyokuwa nikitokwa na jasho ningerukwa akili."
"Ndiyo maana unanukia vizuri zaidi. Nitakufanya utokwe jasho kila siku."
"Shetani mkubwa we."


Baada ya kimya kifupi Bessy akasema, "Nasikitika kufanya kile kitendo cha kipimbavu mbele ya wenzangu."
"Kitendo gani?" Denny aliuliza.
"Kule kukuvamia nilipoona uko salama."
"Hakikuwa kitendo cha kipumbavu. Ulionyesha jinsi unavyonipenda. Ulinifurahisha sana."
"Sikukuvamia kwa sababu nakupenda, you idiot. Nilifurahi kukuona uko salama. Ungeumia ningefukuzwa kazi."


********************************


Punde akalisimamisha gari nje ya Flamingo, picha ya ndege huyo, korongo mweupe aliyesimama kwa mguu mmoja, akipatangaza mahali hapo.
Wakazipanda ngazi hadi ghorofa ya pili. Mbele ya mlango wenye nambari 202 Denny akamfanyia ishara Bessy abishe. Akaugonga mlango.
Sauti nzito ikauliza, "Nani?"
"Ni mimi." Bessy alisema kwa sauti laini ajabu. "Nifungulie."


Mlango ukafunguliwa kidogo. Denny akaupiga kikumbo na kuingia nao ndani. Huku akipepesuka kwa hicho kikumbo, Kembo akaupeleka mkono wake ndani ya koti.
Denny akamkwida na kumbamiza ukutani. Akamnyang'anya bastola aliyokuwa ikiitoa. Akamzungusha na kumsukumia mlangoni. "Twende."
"Wapi?" Kembo aliuliza, akijifuta damu mdomoni. "Nyie ni nani?"
"Ni Inspekta Bessy na Dennis Makete. Tupeleke kwa rafiki yako, Kassim Hashir."
"Simjui mtu huyo." Denny akamnyuka Kofi la kelbu. "Usimwige Petro."
"Ndiye nani huyo Petro?"
"Jesus Christ! Hata Petro humjui! Ni Mkristo kweli wewe?"


"Sikiliza," Kembo alihema kwa nguvu. "Sikilizeni. Mimi si mtu wa ghasia."
"Alaa! Ndio maana ukawatuma akina Chiko wakufanyie ghasia zako?"
"Chiko!" Kembo aliguna kizembezembe. "Yuko wapi Chiko?"
"Nilidhani utasema naye pia humfahamu!" Denny alisema, akiufungua mlango na kumsukumia Kembo nje. "Chiko na Fensy wa wanakostahili kuweko - Jehanamu."


Wakaziteremka ngazi. Chini Denny akamrushia Bessy funguo za gari. "Endesha wewe." Alimwambia. "Sisi tutastarehe kwenye siti ya nyuma na huyu rafiki yangu."
Wakaingia garini. Bessy akalitia moto. Akauliza, "Buffalo Hill?"
"Buffalo Hill." Denny alimjibu. Akamtekenya Kembo kwa mdomo wa bastola yake mwenyewe. "Mtaa gani?"
"Kitosi." Kembo alijibu bila ya kusita.
"Namba?"
"Ishirini na moja."




Itaendelea
 
Kiongozi safi kabisa tena kwa kasi hii tunaumaliza msako huu, na hayawani lazima apatikane
 
Asante sana idawa, endelea kumwaga vitu mkuu. Natumia simu hakuna kitufe cha like nikiingia kwenye computer nitakupa like za kutosha.
 
Back
Top Bottom