SEHEMU YA 33
Fausta alivyofika nje alishtushwa sana kumuona mgongaji, alijikuta akisema kwa taharuki,
"Maiko!!!"
Maiko alikodoa macho kwani hakudhani kama angekutana na Fausta mahali hapo, na hakujua kuwa Fausta anayetafutwa na Mashaka ndio yuleyule anayemjua yeye.
FAUSTA: Ona ulivyokodoa macho kama fundi saa, katika wanaume ninao wachukia hapa duniani wewe unaongoza Maiko.
MAIKO: Ni haki yako kusema hayo yote uyasemayo, najua unavyoumia Fausta.
FAUSTA: Unajua maumivu ya mtoto wewe Maiko? Unajua mtoto anavyouma wakati wa kujifungua? Sikufikiria kama wewe ni gaidi kiasi kile na sikudhani kama ungenifanyia unyama ule Maiko.
MAIKO: Yote nakubali Fausta ila huu si muda muafaka wa kuzungumza hayo, napenda kukuokoa sasa.
FAUSTA: Kwenda zako huko, sipendi hata kukuona nahisi kichefuchefu. Na kama umepanga kuniua, nimalize tu sikuogopi wala nini.
Maiko akaanza kuondoka akiwa amenywea sana. Fausta aliendelea kubwabwaja maneno kama vile amemeza kanda, aliongea bila kumeza mate tena aliongea kwa hisia na hasira.
FAUSTA: Wewe Maiko sio binadamu kabisa, wewe ni mnyama tena shetani wa mashetani, narudia tena sikuogopi ukitaka kunimaliza njoo tu unimalize, wewe si gaidi bhana, njoo unimalize. Siwezi kusahau unyama uliofanya kwa mwanangu, Maiko sitakusahau wala kukusamehe hadi naingia kaburini najua ni Mungu tu ndiye atakayenilipia, mabaya uliyoyafanya kwangu hayatasahaulika kamwe. Shetani mkubwa wewe, hata sijui umetokea wapi leo.
Ingawa Maiko alikuwa ameshaondoka, Fausta hakuacha kuongea, aliongea sana na mwisho wa siku alijikuta akikaa chini na kuanza kulia, alikuwa akilia na kuomboleza.
Maiko aliondoka na Yuda, huku akiwa na mawazo mengi sana.
YUDA: Bosi, mbona siwaelewi jamani? Nilipokuja na Mashaka nae akakutana na mtu anayemfahau, leo tena na wewe, vipi tena kwani yule ni nani yako?
MAIKO: Kwakweli nilikuwa shetani sana si uongo wala utani, hata mimi maneno yake yameniingia sana. Ushetani wa Mashaka sasa ulikuwa ndani yangu, nimetesa watu wengi sana, nimeua sana, hadi sasa sina mtoto kabisa. Fausta aliwahi kuwa mwanamke wangu, ila nilimtenda vibaya sana sidhani kama anastahili adhabu ya Mashaka.
YUDA: Inamaana wakati Mashaka anakwambia kuwa anataka kumuua Fausta, wewe hukujua kama ni Fausta yule?
MAIKO: Kwakweli sikujua, na wala sikutambua kama leo ningekutana na yule mwanamke. Yuda, wewe ni mgeni kwenye kazi hizi, tukirudi Arusha nitakupeleka kwenye chumba changu maalum ukaone, hapo utaelewa kwanini yule mwanamke amesema vile.
YUDA: Sawa, na Mashaka je utamwambiaje?
MAIKO: Kuhusu Mashaka usijari, najua jinsi ya kufanya hawezi nisumbua kitu. Ila leo dah, nilikosa cha kusema mbele ya Fausta, sikujipanga kukutana nae, sikupanga kumuona dah!! Nimejikuta roho ikiniuma sana leo sijui kwanini jamani!! Siku zote huwa sijihisi kuwa na hatia, ila leo mmh!!
Maiko alionekana kuguswa sana na maneno aliyoongea Fausta.
Pamela naye alitafakari sana mambo aliyomfanyia mwenzie, alijiona kuwa na makosa makubwa sana.
PAMELA: Debo, nakubali makosa ila naomba unieleweshe kitu kimoja.
DEBORAH: Kitu gani?
PAMELA: Patrick umezaa na nani?
DEBORAH: Hayakuhusu.
PAMELA: Nauliza nikiwa na maana Debo, kama Patrick ni mtoto wa Jumanne basi Tusa atakuwa dada yake.
DEBORAH: Jumanne nilizaa nae mtoto mmoja tu ambaye ni yule Jasmine wangu aliyefanana kila kitu na Tusa, (akainama kidogo kufuta machozi), haya ya Patrick hayakuhusu, niachie mwenyewe na moyo wangu.
PAMELA: Mmh!! Kwani ulibakwa?
DEBORAH: Pamela usitake kuniudhi tafadhari, nishakwambia hayakuhusu sasa chokochoko za nini?
PAMELA: Nisamehe tafadhari, sitarudia tena.
DEBORAH: Sina sababu ya kutokukusamehe mtu kama wewe usiyejielewa, ila kumbuka kuwa chochote ulichomtendea mwingine, utarudishiwa kwa namna tofauti. Wengine husema, what goes around comes around. Mimi sikuhukumu wala nini, ila niliongea kwa hasira tu ukizingatia mapito niliyopitia ni mengi. Sina baya na wewe na wala sina sababu kubwa ya kukuchukia.
PAMELA: Asante Debo kwa msamaha wako.
DEBORAH: Ila kikubwa, nitapenda Jumanne aje kwa miguu yake mwenyewe huku Mwanza kukufata.
PAMELA: Hilo halina tatizo Debo, cha muhimu ni kuishi kwa amani.
Ingawa Deborah aliongea mengi ila kidonda chake moyoni bado kilimuuma sana.
Pamela nae hakumshangaa sana Deborah kuhusu Patrick kwani hata dada yake Fausta hakumjua mtu aliyezaa nae mtoto wake Tina.
Tina aliyekuwa ametoka kidogo, aliporudi pale kwa Adamu, akamshangaa mama yake aliyekuwa chini akilia sana, Tina akamsogelea na kumuita "mama"
Fausta aliinua macho yake na kumtazama Tina, akamkumbatia kwa nguvu huku akiendelea kububujikwa na machozi.
TINA: Una nini mama yangu?
FAUSTA: Tina mwanangu, dunia ni duara na binadamu wote hukutana humo. Leo nimetembelewa na shetani.
TINA: (Aliuliza kwa mshangao), shetani!!
FAUSTA: Ndio, shetani alikuja leo.
Tina alihisi mama yake ameanza kuchanganyikiwa kwani hakufikiria kama mtu unaweza kumuona shetani kwa macho ya kawaida.
TINA: Mama, mbona sikuelewi?
FAUSTA: Nimetembelewa na baba yako Tina, alimuua pacha wako mbele ya macho yangu. Unajua alimfanyaje?
TINA: Mmh!! Alimfanyaje mama?
FAUSTA: Alimuua, alimchukua akam....
Aliangusha kilio kikubwa kabla ya kumalizia kauli yake, alikuwa akilia sana, "mwanangu mimi, mwanangu jamani"
Tina alijikuta akilia na mama yake, alimuonea huruma sana.
Tusa alikuwa bado hajauelewa vizuri uhusiano wa mama yake na Deborah, alipokuwa akitafakari alifatwa na Sele.
SELE: Tusa, hapa ni swala moja tu.
TUSA: Swala gani?
SELE: Inatakiwa tutoroke hapa, sidhani kama hapa ni mahali sahihi pa kuishi.
TUSA: Na mama yangu je?
SELE: Mama yako hakuna tatizo Tusa, yeye yuko salama na mamdogo ila wewe hauko salama Tusa, sidhani kama Patrick ni mtu sahihi kwako.
TUSA: Kwanza futa hiyo kauli kuwa Patrick ni mtu, Patrick si mtu kabisa, Patrick hata sijui nimfananishe na mdudu gani hapa duniani. Amenifanyia mambo mabaya sana sijawahi kufikiria kama ningefanyiwa vile.
Tusa akainama na kuanza kulia, Sele akamsogelea karibu na kuanza kumbembeleza.
Patrick akarudi na kumkuta Sele akimbembeleza Tusa, Patrick akapatwa na hasira za ajabu.
Akaingia ndani bila kuwasemesha, wote wawili hawakujua ni kipi kingewapata Patrick atakapo toka nje, walichofanya ni Sele kuondoka na Tusa kwenda alipo Deborah kwani ndio mtu pekee anayesikilizwa na Patrick.
Walipofika Arusha, Maiko kama alivyomuahidi Yuda, akampatia funguo zake za chumba cha siri aende akatazame.
Yeye alienda kuzungumza na Mashaka ili aweze kuweka mambo sawa kabla Mashaka hajaamua kumdhuru Fausta.
Wakiwa katika maongezi mara Maiko alimuona Yuda akija na ghadhabu nyingi usoni.
Moja kwa moja Yuda alienda kumkaba Maiko huku akiwa na hasira kali.