RIWAYA: Mume Gaidi

RIWAYA: Mume Gaidi

SEHEMU YA 90


Kila mmoja alianza kupiga kelele mule ndani na kuogopa.
Maiko hakuwa na wasiwasi wowote na kile kichwa mkononi na hiyo ikawathibitishia na kufanya waamini kuwa kweli Maiko ni muuaji.
Patrick hakushangazwa sana kumuona Maiko ameua ila kitu kilichomshangaza ni kuwa Maiko amempata wapi Mashaka.
Patrick akainuka na kuanza kumsogelea Maiko.
PATRICK: Umempata wapi Mashaka?
MAIKO: Tafadhari usinisogelee.
Deborah kusikia vile akainuka na kuanza kumvuta Patrick kwani alihofia nae kupatwa na matatizo kama yale. Ila Patrick alikuwa mbishi, bado alihitaji kujua Maiko kamtoa wapi Mashaka.
PATRICK: Nataka uniambie ulipomtoa Mashaka.
MAIKO: Yote nitasema ila usinisogelee.
Deborah akazidi kumvuta mwanae na kumuomba warudi kukaa. Ndio Patrick akarudi kwani hata yeye hakujua hatma yake ni nini.
Mwita pale nje hakutaka kujiuliza mara mbili mbili akachukua simu yake na kuwapigia maaskari kisha akawaelekeza eneo la tukio ili waje kumkamata muharifu yule halafu akaingia ndani, alitamani hata muujiza utokee kuwa muongeaji wa yale maneno asiwe baba yake, alitamani hata awe ni mtu mwingine.
Mwita alipoingia tu ndani, Maiko aliweza kumsikia na kumuona.
Maiko akatoa bastola na kumuwahi nayo Mwita kuwa akae chini, Maiko hakuwa kama binadamu wa kawaida. Wote walibaki kushangazwa na ile hali.
Mwita aliamua kukaa huku akivizia namna ya kumnyang'anyanya silaha hiyo baba yake kwani alijua wazi kuwa kitendo cha kumsogelea ni kuhatarisha maisha yake.
Maiko akawaelezea tena vile anavyojielewa yeye.
"Sikufikiria kama ninachokifanya ni kitu kibaya na kuwa ipo siku itanigharimu, kuhusu kukamatwa na polisi sikuwa na shaka nao haswa kwa vijana wanaopenda rushwa kama Taifa letu.
Sitaki mtu anisogelee kwavile nataka kueleza niliyonayo jambo kwa ufupi na kwa kuruka ruka ili wote mpate kunielewa.
Mtoto wa Deborah huyo Jasmine ni mimi kweli niliyetoa oda kwa vijana wakammalize mtoto huyo, sio kwamba nilikuwa na ugomvi na mume wa Deborah au Deborah mwenyewe hapana!! Ila nilifanya kwa kuifurahisha nafsi yangu, ila mwanzoni sikujua kama mtoto huyo ni wa Deborah, nilitoa sifa za mtoto na badae nikaletewa. Nilikuja kugundua wakati mtoto mwenyewe tushamteka ila nikaamua kuipotezea tu, Laiti kama ningejua kuwa Jumanne ni ndugu yangu nisingethubutu kufanya vile.
Vijana wangu walinipa taarifa juu ya kukamatwa kwa yule binti aliyetuletea mtoto, nikafanya mpango hadi yule binti akawa huru kabisa hakuwa na kesi tena hapo pesa yangu ndio iliyoongea.
Nilipomkuta Deborah tena na mtoto nilishangaa sana nikajua labda kipindi tunamteketeza mwanae alikuwa mjamzito. Sikuhisi hata kidogo kama Patrick si mtoto wa Deborah.
Huyu mwanamke ana moyo wa kijasiri sana anahitaji kuigwa.
Ni kweli mimi ni mume gaidi, Deborah hajakosea kuniita hivyo sikuwa na huruma kwa mke wala mtoto.
Nilimtenda vibaya Fausta tena bila hata ya kujua ni dada yangu. Halafu kibaya zaidi ni kitendo cha kumbaka mwanangu Tina.
Sifai kuigwa na yeyote, nilipandikizwa roho mbaya na ya kikatili moyoni mwangu ila hadi nitakapoingia kaburini nitakuwa namlaumu huyu mwenye kichwa hiki.
Msimuhukumu Patrick kwa chochote, najua vyote alivyofanya mimi ndiye chanzo. Nimemuharibu sana Patrick kimawazo na kitabia.
Ni mimi niliyempa mbinu za kumpata Tusa kwa urahisi na kumfanya atakavyo.
Patrick si mtu mbaya kwani kuna kipindi huwa anajirudi.
Patrick alimteka Mashaka, mimi nilikuwa nikimfatilia.
Patrick alimfunga Mashaka huko porini nami nimeitumia nafasi hiyo kummaliza Mashaka kwani tushamaliza watu wengi sana ila Mashaka hakuacha kutamani kuendelea kumaliza watu wasio na hatia.
Mashaka hafai tena hafai kabisa, najua hapa hakuna wa kumsamehe Mashaka wala mimi.
Narudia tena msimuhukumu Patrick, akili yake ilivurugwa.
Deborah ni mwanamke mwema, yani mateso yote yale hakuthubutu kumtupa Patrick.
Laiti kama ningerudi ujanani basi ningemfanya Deborah kufurahia maisha yake duniani.
Kifo cha baba yangu mzazi kimeniumiza sana, ni mengi nimeyafanya bila huruma. Kwangu mimi mwanamke hakuwa na thamani yoyote.
Pole mama yangu bi.Rehema najua hukutarajia kitu cha namna hii ila ndio hivyo mwanao sio mtu wa kawaida kabisa.
Mkienda Arusha mtaweza kuona uajabu wangu humo ndani.
Pole na wewe Deborah kwani uliponitoroka niliitumia nafasi hiyo kummaliza baba yako mdogo. Mimi ndiye niliyemuua.
Wote niliowaumiza nawaambia pole, poleni sana kwa kuumizwa na Maiko.
Sitaki kufungwa na siko tayari kwenda jera.
Najua hakuna wa kunisamehe, ila nawaomba kitu kimoja.
Patrick anakujua nyumbani kwangu Arusha.
Mwende huko, mkateketeze kila kitu cha ndani haswa viungo vya binadamu na mali zangu zote nawaachia nyie mtajua cha kufanya ila nawaomba myasikilize mawazo ya Deborah.
Najua kuna maswali bado mnayo ya kuniuliza ila hiyo barua itawajibu kila kitu. Nimemaliza ila sitaki mtu wa kunisogelea"
Akachukua bastola yake, mara gafla mule ndani mkavamiwa na kundi la maaskari ambao Mwita aliwapigia simu.
Wakataka kumsogelea Maiko, akawanyoonyea bastora.
MAIKO: Atakayenifata nakwenda nae na maji, siko tayari kwenda jela. Kweli nimeamini, mwisho wa ubaya ni aibu.
Wale mapolisi wakikazana kutafuta mbinu ya kumkamata Maiko hakupoteza muda, akaweka ile bastora kichwani mwake na kusema neno moja tu.
MAIKO: Kwaheri mama.
Kisha akajifyatua kwenye ubongo na kuanguka chini huku kichwa cha Mashaka kikiwa mkononi.
Ilikuwa ni tukio la kushtua sana mule ndani.
Polisi wale wakamfata Maiko pale chini aliyeonyesha kuwa bado hajakata roho vizuri,
Polisi mmoja akainama ili amsikilizie akashangaa akivutwa kwa chini.
Itaendelea kesho....!!!
 
SEHEMU YA 91

Polisi mmoja akainama ili amsikilizie akashangaa akivutwa kwa chini.
Yule askari alizidi kuvutwa pale chini na Maiko, wote ndani ya nyumba wakastaajabu na wote wakaogopa kumsogelea.
Askari alianza kuhangaika pale chini kwani alishikwa kwa nguvu sana na Maiko, alihangaika hadi alitia huruma ila waliogopa kumsogelea. Baada ya muda roho ya Maiko ikaachana na mwili na kumuachia yule askari ambaye alikuwa amelowa damu ya Maiko na kuumia pia.
Yule askari alivyoweza kuinuka pale alijikuta akikimbia na kuwaacha maaskari wenzie mule ndani, hakutaka kurudi tena kwani aliona kuwa ni kitu cha kushangaza.
Mvua kubwa ikanyesha, hadi ikawashangaza wote mule ndani, wakajikunyata ili ikatike na haikuchukua muda mrefu ikakatika.
Mule ndani wakawa wanashauriana jinsi ya kubeba mwili wa Maiko na kichwa cha Mashaka kwenda kuzika.
Ilikuwa ngumu kwa kila mmoja kumsogelea Maiko pale chini, maaskari waliokuwepo wakaamuru mwili wa Maiko uachwe pale kwa muda kwaajili ya uchunguzi na upelelezi, na sababu zingine za kiusalama.
Wanausalama zaidi wakapigiwa simu na kufika eneo la tukio, muda huo familia nzima ilikuwa nje wakingoja kutolewa kwa mwili wa Maiko, na walioutoa walilalamika kuwa ule mwili wa Maiko ulikuwa ni mzito sana kuliko marehemu wote waliowahi kuwabeba.
Nyumba ya Deborah ikawa inatisha sana, wakajipanga namna ya kumzika Maiko.
Deborah akawa anaongea na dada yake kuhusu kifo cha Maiko.
DEBORAH: Kifo cha Maiko hakijanisikitisha hata kidogo, amekufa kirahisi sana ukiangalia na makosa aliyoyafanya.
MARIUM: Ila bora amekufa, kwani angeendelea kuwa hai angezidi kutuumiza wengine hapa.
Deborah alifurahia kwa Maiko kuamua kujiua mwenyewe na mabaya yake kudhihirika.
Kama familia wakaamua kupanga mahali ambako patafaa kumzika Maiko baada ya uchunguzi kukamilika.
REHEMA: Nadhani itakuwa vyema kama mwanangu akienda kuzikiwa alipokuwa anaishi, yani huko huko Arusha.
ADAMU: Hapana mama, itabidi tukamzike Morogoro karibu na kaburi la baba.
DEBORAH: Nawahurumia sana, kuacha kuongelea mambo ya msingi na kukazana pa kumzika Maiko. Yani jinsi Maiko alivyokuwa, bado mnapata nguvu za kumsafirisha sijui Arusha sijui Morogoro, ingekuwa amri yangu ningemtupa kwenye mto wa mamba ili mamba wamtafune na mwili wake usibaki hata chembe.
MARIUM: Kweli kabisa mdogo wangu.
Wengine wote walikuwa kimya kwani hawakujua hata waseme nini ila wakaona kuwa kumzika Morogoro itakuwa vizuri zaidi, ukizingatia Maiko alikuwa na pesa kwahiyo wakaona kuwa watatumia pesa yake hiyo na kumsafirisha kwa ndege.
Pamela alipigiwa simu na wifi yake wa Morogoro Amina, alikuwa anamtaarifu wifi yake huyo kuwa na yeye yupo Mwanza.
AMINA: Wifi dada, mimi niko Mwanza. Kwani nyie bado hamjarudi Dar?
PAMELA: Bado ila tumepatwa na matatizo, wewe umefata nini Mwanza?
TULO: Mwanangu kanipigia simu kuwa yupo huku kashikiriwa na polisi, ndio nimekuja kumuona.
Pamela hakuelewa ni mtoto yupi wa Amina, ikabidi ampe maelekezo Amina ya kufika walipo ili pia akamueleze kuhusu Maiko na undugu wao.
Nyumba ya Deborah ilikuwa inatisha sana, kama vile kulikuwa na maruweruwe ndani ya nyumba.
Tusa na Tina ndio waliogopa kabisa kukaa ndani ukizingatia wakikumbuka jinsi Maiko alivyokibeba kichwa cha Mashaka.
Rehema na Adamu wakamuomba Patrick awapeleke mahali alipomuacha Mashaka ili kuangalia mwili wake ikiwezekana kuuzika.
Waliondoka na maaskari kwenda eneo la tukio, waliukuta mwili wa Mashaka ukiwa umenyofolewa nyofolewa na ndege na kunguru pamoja na mmbwa.
Wale maaskari wakabeba viungo vilivyobaki na kupiga picha kwa uchunguzi zaidi.
Ile kesi hata haikujulikana itaendeshwa vipi ila maaskari walihitaji kupata uchunguzi wa kutosha tu.
Amina alifika hadi alipoelekezwa na Pamela, halafu akaenda nae nyumbani kwa Deborah.
Amina alishangaa sana kumuona Deborah aliyekuwa wifi yake mwanzoni, akamfata na kumkumbatia kisha kusalimiana nae.
AMINA: Deborah!! Hata sijui ulipoteaje jamani, nilishangaa tu kaka kutuletea wifi dada.
Wakaongea ya hapa na pale na kukumbuka mambo mengi yaliyopita.
Pamela akamueleza Amina juu ya tukio lililotokea na kifo cha Maiko.
AMINA: Alikuwa anaitwa nani?
PAMELA: Maiko ndio jina lake, alikuwa anaishi Arusha.
AMINA: Mungu wangu, umesema ni ndugu yetu?
PAMELA: Ndio, hata sisi wenyewe tumemjua tulivyofika Mwanza. Kwani unamjua?
Amina alikaa muda kwa kimya, kisha akaanza kutoa maelekezo ya Maiko anayemjua yeye.
PAMELA: Ndio huyohuyo, hata hujakosea.
AMINA: Yule Maiko kajiua mwenyewe? Halafu mnapanga mipango ya kumsafirisha? Hata kama ni ndugu yangu, siko tayari kumsafirisha yule shetani. Nadhani hamumjui vizuri nyie, yule Maiko si mtu wa kawaida kabisa. Mkimsafirisha mnajitafutia matatizo tu.
PAMELA: Sasa tutafanyaje?
AMINA: Hakuacha maelekezo yoyote juu ya kuzikwa kwake?
PAMELA: Kuna barua alitukabidhi ila bado hatujaisoma.
AMINA: Maiko hakuwa mtu wa kawaida, kwa ushauri wa bure tu. Someni hiyo barua yake ndipo mkamzike. Maiko hakuwa kama binadamu wengine, mi sikujua kama ni ndugu yangu ila kumbuka mimi ni daktari nishaonana na Maiko mara nyingi sana, hakuwa binadamu wa kawaida kabisa yule.
Pale nyumbani wakaafikiana kuisoma barua ya Maiko kwanza.
Amina akawapa taarifa kuwa kilichomleta Mwanza ni juu ya mtoto wake kwani amesikia kuwa amekamatwa, walipomdadisi vizuri wakagundua kuwa Tulo ni mtoto wa Amina, wote wakashangaa.
Hadi Mwita akajikuta akiuliza kwa mshangao.
MWITA: Inamaana Tulo nae ni ndugu yangu!!
ANNA: Ndio, atakuwa nduguyo.
MWITA: Sasa nimeamini maneno ya Patrick, kweli huu ukoo una laana. Kesi ya Tulo nimeishikilia mimi.
Amina akauliza kwa mshangao kuwa ni kesi gani kwani hakujua kuwa mtoto wake alikuwa na mambo ya ajabu.
Ukoo haukueleweka na kila mmoja alibaki kushangaa tu.
Nyumbani kwa Deborah ilikuwa ni gumzo tu, hakuna kulala wala nini muda mwingi walijikuta wakizungumza na kutafuta chakula tu.
Patrick aliporudi kuonyesha mwili wa Mashaka, alienda moja kwa moja na kumfata mama yake Deborah.
Alimuita na kwenda kuongea nae.
PATRICK: Mama, mimi si mtoto mzuri tena. Mama sidhani kama nastahili kuwepo kwa maisha ya sasa, najua ukishajua maovu niliyotenda utanichukia pia.
DEBORAH: Siwezi kukuchukia Patrick hata mara moja, ondoa kabisa fikra za kuchukiwa na mimi mwanangu. Ngoja tumalize haya mambo ya kina Maiko na tuanze kujenga familia yetu upya kabisa mwanangu.
Patrick alishukuru kwa kauli ya Deborah kwani hakuwa na raha wala na amani moyoni mwake.
Tusa hakuwa na raha kabisa kwani hakujua hatma yake na Patrick ni nini, Patrick nae hakuwa na raha kabisa na bado aliendelea kujishangaa kuwa kwanini aliangukia kimapenzi kwa dada yake. Kwakweli wote walikuwa na mawazo sana ndani ya familia na hawakuelewa cha kufanya.
Mwita hakuelewa afanyeje na Tulo kwani kesi ile alikuwa ameishikilia yeye na sasa anagundua kuwa Tulo ni ndugu yake anajikuta hana la kufanya.
Waliamua kusoma zile barua kama familia, ila walikuta barua mbili moja ikiwa na maelezo mengi sana na nyingine iliandikwa kwa kifupi tu.
"Nitakapokufa, naomba mwili wangu uchomwe na kuzikwa pamoja na viungo vyote vya binadamu ambavyo vipo kwenye nyumba yangu"
Familia iliangaliana na kukubali kuwa kweli Maiko hakuwa mtu wa kawaida, alikuwa ni zaidi hata ya gaidi.
Wakasafiri wote na kwenda Arusha ili kujishuhudia kila kitu kuhusu Maiko.
Kufika nyumbani kwa Maiko walikuta ukuta wa upande mmoja wa nyumba yake umeanguka, walipojaribu kuuliza mambo hayo yametokea lini, wakatajiwa siku na saa aliyokufa Maiko.
Ni familia ile nzima ndiyo iliyokuwepo hapo kustaajabu mambo ya Maiko.
Wakiwa wanashangaa, ukatokea upepo mkali sana na kuwapuliza pale nje.
Mara kuna kitu kikatoka nje ya nyumba ya Maiko.
 
SEHEMU YA 92


Mara kuna kitu kikatokea nje ya nyumba ya Maiko.
Upepo mkali nao ukazidi kuvuma nje ya ile nyumba, watu wote wakaanza kuogopa hofu ikawatanda kwenye mioyo yao.
Wakatazamana bila hata kuelewa nini kinaendelea, kile kitu cha ajabu kiliwazunguka na kwenda kuishia nyuma ya ile nyuma na upepo nao ukakatika gafla.
Wakasogea pembeni na kuanza kujadiliana ile hali iliyowatokea na waliyoiona.
FAUSTA: Ndiomana mimi sikutaka kabisa kuja huku, niliyajua yote haya. Bora hata ya Tusa na Tina waliobaki nyumbani.
DEBORAH: Huu sio wakati wa kulaumiana jamani kama jambo limeshatokea hakuna jinsi zaidi ya kukubaliana na hali halisi.
REHEMA: Tuzungumzie ya kufanya jamani tusipeane lawama za bure.
AMINA: Kwa kiasi kidogo namfahamu Maiko, hakuwa binadamu wa kawaida kama mnavyodhani. Inabidi ifanyike namna nyingine ya ziada ili kukabiliana na hii hali, hata kilichotokea wakati anakata roho sio kawaida ila kama.
DEBORAH: Basi utuambie unavyomfahamu huyo Maiko, pengine inaweza kutusaidie.
Basa Amina akaanza kuwaeleza vile anavyomfahamu maiko.
"Mimi ni daktari, nilifahamiana na Maiko kipindi nipo hospitali kwenye ofisi yangu mjini Dodoma, alikuja na mgonjwa wake moja kwa moja ofisini na kuniomba nimfanyie operesheni ndogo. Nikamuuliza mgonjwa anaumwa nini, bila kificho aliniambia kuwa mgonjwa yule ana madawa ya kulevya tumboni na alitaka niyatoe.
Kwanza kabisa nikakataa, Maiko akatishia kuniua ikabidi nikubali na kumfanyia yule mgonwa operesheni ila yule mgonjwa alikuwa kachoka sana ilionyesha kuwa amekaa na madawa kwa muda mrefu tumboni na hali yake kiafya haikuwa nzuri ila Maiko hakutaka yule mgonjwa ahudumiwe zaidi badala yake alisema nimmalize kwa sindano kwakweli nilipinga kabisa swala hilo nikamwambia aondoke tu na mgonjwa wake.
Kesho yake nikiwa ofisini nikasikia kuna binti amekutwa kauwawa na kutupwa kwenye mtaro, tulipoenda kumuona alikuwa ni yule yule binti aliyeletwa na Maiko jana yake. Dah nilisikitika sana kwani sikutarajia kabisa tena aliuwawa kwa kuchinjwa.
Baada ya miezi kadhaa nilikuwa mjamzito na Maiko alinitembelea tena pale hospitali, akasema ameutamani sana ujauzito wangu, kwanza nilimshangaa pili nilimuogopa kutokana na yule binti na tatu niliogopa kuwaambia watu kuwa yule jamaa ndiye muuaji wa yule binti.
maiko aliendelea na hoja yake ya kutamani ujauzito wangu, nikaona ni kitu cha ajabu kwa mwanaume kutamani ujauzito inamaana anatamani awe yeye mjamzito au ni nini.
Akaingia nesi fulini mule ofisini, alipomuona Maiko alishtuka sana na kutoka mule ofisini, badae nikamfata na kumuuliza kwanini alishtuka akaniambia kuwa Maiko si mtu mzuri, mi nikahisi kuwa labda nae anamjua Maiko kuwa anahusika na kile kifo cha yule mdada. Halafu akanipa onyo kuwa nisipende kuwa karibu na Maiko.
Siku nyingine Maiko alikuja ofisini na kuniletea pesa nyingi sana za asante, nikashangaa ni za nini ila sikuziacha nikazipokea na siku iliyofuata mimba yangu ilitoka, kwakweli nilihudhunika sana kwani yule angekuwa mwanangu wa pili baada ya Tulo ila bado sikuelewa.
Kuna siku Maikom alikuja na kunikuta na mwanangu Tulo ofisini aliniambia kuwa amempenda sana mwanangu na atafurahi siku akifanya nae kazi moja, nikapatw na uoga na mashaka ndipo nilipoamua kumsafirisha mwanangu Tulo na kumpeleka Dar es salaam akaishi na shangazi yake.
Yule nesi alinifata tena na kuniambia kuwa Maiko si mtu mzuri, anafuga majini nyumbani kwake hata mimba yangu iliyotoka yeye ndio chanzo na hawezi kuacha kunifatilia sababu nimeshaonja utamu wa pesa yake.
Hapo ndipo nilipoamua moja, niliacha kazi na kurudi kwetu Morogoro ili niepukane na balaa la Maiko.
Nadhani hata huyo askari aliyekabwa itakuwa ni hayo majini ya Maiko yalitaka msindikizaji, na hali ya hapa kwake nadhani ni hayo majini"
Rehema aliumia sana kama mzazi wa Maiko alijihisi kuwa na mkosi kama mama wa Maiko hakujua cha kufanya kuweza kuvumiliana na ile hali halisi iliyokuwepo.
DEBORAH: Jamani hii ni khatari sana, tutafanyaje sasa?
REHEMA: Tufanye kama alichosema kwenye barua yake tu.
Adamu na Pamela walishindwa hata kuelewa cha kufanya.
MARIUM: Tusikawie jamani, hali ya huku si shwari kabisa.
Kwa waliokuwepo pale mwenye nguvu ya kufanya chochote alikuwa ni Yuda tu.
Tina na Tusa hawakwenda Arusha, Tusa hakutaka kabisa kukanyaga mji wa Arusha na pia hawakuweza kukaa nyumbani kwa Deborah kwa kuogopa kutokew na Maiko. Wao waliondoka na Sele na kwenda kukaa nyumbani kwa Marium.
TUSA: Sidhani kama mama yangu ana roho mbaya kiasi hiko cha kutupa mtoto.
TINA: Hata mimi sifikirii kama mama yangu anaweza kufanya hivyo.
TUSA: Sasa Patrick ni mtoto wa nani?
TINA: Mimi nadhani mama yake Patrick amesahau tu ila mama zetu hawawezi bhana kutupa mtoto. Hawana roho mbaya kiasi hiko.
TUSA: Na mbona walikuwa wanalia sasa?
Sele akaingilia mazungumzo yao.
SELE: Jamani yote yanawezekana ngoja tuwasubiri warudi waje kutuambia ukweli wote.
Sele alitulia sana tangu amesikia stori nzima kuhusu Patrick. Alikuwa anangoja kujua hatma ya Patrick na Tusa itakuwa ni nini.
Patrick nae hakwenda Arusha alijifungia ndani tu, hakutaka kufanya chochote ingawa mama yake alimsihi sana aende nao.
Patrick akaenda dukani na kuchukua sumu ili ajimalize, kabla hajafanya hivyo mzimu wa mzee Ayubu ukamtokea Patrick na kumsihi asifanye vile.
Mwita nae mawazo yalimjaa sana kwani hakujua cha kufanya, stori ya Maiko ilimpelekea kuamini kuwa Patrick anahusika na vifo vya wale wajeshi kwani aina ya uuaji ilifanana na aina ya uuaji aliokuwa akiufanya Maiko.
Akimfikiria Tulo nae ambaye pia ni ndugu yake alikosa jibu kabisa ya nini cha kufany ukizingatia yeye ni usalama wa Taifa. kauli ya Maiko nayo ilimrudia mara kwa mara kuwa wasimuhukumu Patrick.
Deborah aliwaambia kuwa wanatakiwa kuharakisha kwani wameacha watu wengi muhimu huko nyumbani.
Wakaamua mwili wa Maiko na Mashaka wauingize ndani ya ile nyumba na waichome moto nyumba yote.
Wakasaidiana na baadhi ya watu kufanya hivyo, hakuna aliyetaka chochote toka kwenye nyumba ya Maiko.
Viungo vya binadamu viliwatisha sana mule ndani na hapo wakaamini wote kuwa Maiko alikuwa gaidi.
Walitoa begi moja ndogo yenye mafaili toka kwenye ile nyumba kisha wakaimwagia petroli na kuichima, kwavile ilikuwa mbakli kidogo na maeneo ya watu haikuwapa shida sana kuichoma.
Wakati wanaichoma walisimama mbali kabisa, mara gafla ukasikika mlio mkubwa kama bomu.
 
SEHEMU YA 93


Wakati wanaichoma ile nyumba ya Maiko, walisimama mbali kabisa. Mara gafla ukasikika mlio mkubwa kama bomu.
Wote wakaogopa na kutetemeka kwa hofu, moshi mzito ukawa unatoka pale kwenye ile nyumba na gafla mvua ikaanza kunyesha na kuwafanya wakimbie hovyohovyo kutafuta sehemu ya kujificha.
Ubaya wa eneo lenyewe lilikuwa mbali na maeneo ya watu wengine.
Mvua ilikuwa ni kubwa sana, wakabahatika kupata usafiri uliowasogeza kwenye nyumba kidogo ya jirani na pale.
Pale kwenye ile nyumba walikutana na majirani wa Maiko, ambao walishangaa sana kuelezewa kuwa Maiko amekufa tena kwa kujiua. Hawakuelewa kwanini tajiri mkubwa kama Maiko kujiua.
Na walivyoambiwa kuwa ile sauti ya bomu ilitokea nyumbani kwa Maiko napo walishangaa sana na kujiuliza je ni kitu gani, wengine wakajaribu kueleza kuwa kwavile wamechoma ile nyumba na miili ya watu ikiwa mule ndani kwahiyo huenda ile sauti ya kama bomu ni kupasuka kwa kichwa, ikabidi waamini vile wanavyoambiwa.
Mvua nayo ilizidi kunyesha eneo lile bila hata ya kukatika.
Hali ya Patrick haikuwa nzuri bado, Patrick alikuwa anaumizwa sana kwa kuujua ukweli kuwa Deborah si mama yake mzazi, hakutaka kabisa kuamini na kukubaliana na ukweli huo.
Alitamani hata ukweli huo ugeuzwe, hakutamani kuujua ukweli wa namna ile maishani mwake, mzimu wa mzee Ayubu nao haukuacha kuwa karibu yake.
Ulikuwa ukimtazama tu na kuendelea kumsihi kuwa asijidhuru.
"usijiumize Patrick wala usijidhuru, ukweli humuweka mtu huru. Kubaliana na ukweli na usijipe mawazo sana kwa yaliyopita, yaache yapite na mengine mapya yaje. Mimi ni babu yako Patrick"
Sauti ile ya mtu asiyeonekana ilizidi kumliza Patrick, uelekeo wote wa Patrick ulipotea kwani hakuwa kama vile alivyotegemea.
Mvua ilipokatika, bi.Rehema alitoa wazo la kwenda kutazama lile eneo la tukio ila Deborah alipinga na kuwaambia kuwa warudi tu Mwanza kwani hata yeye hakutaka tena kuendelea kuwepo kule Arusha.
AMINA: Nakubaliana na wazo la Deborah, bora turudi Mwanza kuliko kwenda kutazama nyumba ya Maiko huwezi jua ni kitu gani kitatupata tena huko ukizingatia nyumba yenyewe ilikuwa na majini.
FAUSTA: Hata mimi sioni umuhimu wa kwenda kuitazama, tuondokeni tu.
Wakakubaliana kuondoka ila bi.Rehema hakuafikiana nao kabisa.
Alitamani kuona yaliyojiri kwenye nyumba ya mtoto wake, ila hakuwa na la kufanya zaidi ya kufatilizana na wakina Deborah kuwa waende stendi na kuondoka kurudi Mwanza.
Walipokuwa stendi kwaajili ya kuondoka bado roho ya bi.Rehema haikukubali kabisa, alitamani kuona hata majivu yaliyobaki kwenye nyumba ya mwanae, akawaomba na kuwasihi sana. Ikabidi Adamu akubali kumpeleka tena mama yake kupaona nyumbani kwa Maiko na kwavile Yuda ndio anayepajua vizuri ilibidi yeye akubali kuwasindikiza ila Deborah na wenzie wakagoma kurudi na kuamua kwenda zao Mwanza.
Wakati wao wakisafiri kwenda Mwanza, bi.Rehema, Adamu na Yuda walipanga kwenda kwa Maiko kesho yake.
Nia kubwa ya bi.Rehema ni kuona tu jinsi nyumba ya mwanae ilivyoteketea na jinsi mwanae alivyoangamia.
Walipotua Mwanza, Deborah hakutaka kupoteza muda aliwaomba wote na kuamua kwenda moja kwa moja nyumbani kwake kumuangalia Patrick.
Walipofika Patrick alikuwa chumbani ikabidi Deborah amfate na alimkuta Patrick akiwa na hali mbaya sana, hali ya kutokujielewa kabisa.
Deborah alimfata mwanae na kumkumbatia sana.
DEBORAH: Haijalishi mambo yote yaliyotokea, wewe Patrick utaendelea kuwa mtoto wangu mpendwa na wa pekee.
PATRICK: (Akiongea kwa uchungu), kwanini mama? Kwanini mimi nisiwe mwanao wa kiukweli? Nakupenda mama na siwezi kumpenda mama yeyote kama ninavyokupenda wewe.
DEBORAH: Naelewa mwanangu Patrick ila una haki ya kujua ukweli kuhusu wazazi wako. Ni kweli mimi nimekulea na kukunyonyesha ila si mimi niliyekubeba miezi tisa Patrick.
PATRICK: Na kwanini nilitupwa?
DEBORAH: Tulia mwanangu, ukweli wote utaujua.
Wakiwa pale nyumbani kwa Deborah, Fausta na Pamela walijikuta wakikumbuka tena yaliyopita na kuanza tena kulia.
Deborah alitoka na kuwafata,
DEBORAH: Kulia hakuta wasaidia cha muhimu muwe wazi, Patrick ni mtoto wa nani kati yenu ili naye apate kuwajua ndugu zake.
Walikuwa wakitazamana na kushindwa hata kusema.
Tusa na Tina waliposikia wazazi wao wamerudi, nao wakajipanga kwenda nyumbani kwa Deborah lengo lao ni kuujua ukweli na kutambua hatma ya Tusa na Patrick itakuwa ni nini ukizingatia na ndoa ambayo walishafunga.
Mwita alienda polisi kuzungumza na Tulo, na kumtolea dhamana ya kutoka huku kesi ikiendelea.
Tulo hakuelewa kuwa kwanini amepewa dhamana ya kutoka pale polisi tena dhamana hiyo kutolewa na Mwita, wakati ni mtu aliyemgeuka na kumkamata na kumpeleka polisi, hakujua ni kitu gani kilibadilisha moyo wa Mwita.
Kesho yake Mwita na Tulo walienda nyumbani kwa Deborah na Tulo alifurahi sana kumuona mama yake, hata Amina nae alifurahi kumuona mtoto wake.
Wakamueleza Tulo kila kitu kilichotokea, ila walipomwambia kuwa kuna watu wamerudi kuitazama nyumba ya Maiko alishtuka sana na kusema wapigiwe simu na kuzuiliwa, wote wakashangaa ni kwanini.
Bi.Rehema, Adamu na Yuda wakaenda kutazama nyumba iliyoungua, kufika pale wote wakapigwa na mshangao kuona ile nyumba ikiwa nzima kabisa.
Haikuungua hata nyasi, hakuna aliyeamini kati yao wakati waliiona ikiungua.
 
SEHEMU YA 94


Hakuna aliyeamini kati yao wakati waliiona ikiungua.
Kila mmoja alikuwa akishangaa na kubaki wanatazamana tu.
REHEMA: Jamani, hiyo nyumba si tumeiacha inaungua?
ADAMU: Ndio, na moshi mkali ulitoka na kusababisha mvua kubwa.
YUDA: Haya ni mauzauza jamani, tuondokeni tu.
REHEMA: Hapana tusiondoke, tunatakiwa kwenda kushuhudia humo ndani kuna vitu gani kwa sasa.
ADAMU: Hapana mama, hiyo nyuma ni ya maajabu.
REHEMA: Hapana huwezi jua bhana, labda ile mvua iliuzima ule moto sidhani kama kuna miujiza ya namna hii.
YUDA: Kama nyie mnaenda kuingia nendeni ila mimi hapana kabisa, siwezi kuingia nyumba ya maajabu kama hiyo.
Yuda alipinga kabisa, hakutaka kwenda kuingia kwenye nyumba ya Maiko ila bi.Rehema aliendelea kusisitiza kuwa anataka kwenda kuangalia ndani kama kuna vile vitu walivyoviacha mwanzoni, walimpinga sana ila aling'ang'ania ikabidi Adamu aamue kumsindikiza mama yake ndani ya nyumba ya Maiko.
Wakaondoka pale na kumuacha Yuda akiwa amesimama pale pale akiwatizama.
Wakati wanakaribia kuingia kwenye ile nyumba mara simu ya Adamu ikaanza kuita na kumfanya Adamu asimame na kuisikiliza, mwanzoni aliongea na Pamela ila badae alipewa Tulo ili kuwaeleza vizuri.
TULO: Nasikia mnataka kwenda kuitazama nyumba ya Maiko mliyoichoma. Tafadhari msiende.
ADAMU: Umeshachelewa tayari, ndio tupo huku.
TULO: (Akashtuka), mmepakutaje?
ADAMU: Tumeikuta nyumba ya Maiko ipo vile vile hata haijaungua.
TULO: Basi rudini tafadhari.
ADAMU: Tunataka kwenda kuona ndani kuna nini.
TULO: Msithubutu tafadhari, hayo ni mauzauza jamani. Rudini tu tafadhari. Hiyo sio nyumba ni mauzauza tu.
Ile simu ikakatika, Adamu akamtazama mama yake kwa makini aliyekuwa anajiandaa kuingia ndani.
Akamfata na kumshika mkono kisha akamvuta,
ADAMU: Tafadhari mama tuondoke mahali hapa.
REHEMA: Kwanini Adamu, hutaki kuona mwenzio anapatwa na nini humo ndani?
ADAMU: Mama kumbuka kuwa Maiko ni marehemu tayari hatuko nae tena. Hiyo si nyumba mama ni mauzauza tu.
REHEMA: Msinichanganye jamani, mi sioni kama ni mauza uza wala nini. Kama hutaki kwenda niache niende mwenyewe.
Adamu hakumuachia mama yake kwani alijua akimuachia lazima ataenda tu.
Bi.Rehema nae alizidi kung'ang'ania kwenda ila Adamu akazidi kumzuia huku akimvuta waondoke, Yuda kuona vile ikabidi nae asogee ili kusaidiana na Adamu katika kumvuta bi.Rehema.
Alipofika pale, mara gafla ukatokea mlipuko mkubwa sana toka kwenye nyumba ya Maiko na kuwafanya wale watatu wote kutupiwa mbali kabisa.
Nyumbani kwa Deborah bado walitaka kujua kuwa Tulo kwanini ameshtuka sana kusikia habari ya kwa Maiko haswa swala la wakina Adamu kurudi kuangalia ile nyumba.
AMINA: Kwanza mwanangu, huyo Maiko alikupatia wapi na ulimjulia wapi?
DEBORAH: Na pia alijuaje kama nyumba ile ina mambo ya ajabu?
TULO: Si mimi tu ninaejua hili nadhani hata Patrick analijua hili. Ila mimi nimekuwa msiri wa Maiko kwa kipindi kirefu sana, hata anapoondoka pale kwake ni mimi ndiye aliyekuwa ananiacha.
AMINA: Ndio useme huyo Maiko anakujuaje wewe? Kwakweli bado napigwa na mshangao sana tena sana.
TULO: Lazima mshangae ila Maiko huwa akidhamiria kitu lazima afanikiwe. Nitawaeleza mahusiano yangu na Maiko yalikuwaje na kwanini nimewakataza wale kwenda kule.
Muda huo na wakina Tusa nao wakawasili na kuwakumbatia wazazi wote ila wote walisikitika kwa yale waliyoambiwa kuwa kule Arusha wamewaacha ndugu zao wengine ambao hawajulikani kama watafika salama.
Yuda ndiye aliyekuwa wa kwanza kushtuka, kuangalia pembeni anamuona bi.Rehema na Adamu wakiwa hawajitambui kabisa, alisogea na kumshtua Adamu ambaye hakukawia kushtuka.
Na kuanza kumshtua bi.Rehema ila ilikuwa ngumu sana kushtuka kwani alikuwa hoi zaidi, wakaamua kumbeba na kuanza kujikongoja ili wafike japo barabarani kupata usafiri wa kurudi.
Tulo aliwakalisha wote ili kuwaeleza alivyofahamiana na Maiko na jinsi gani alikuwa mtu wake wa karibu.
TULO: Sikutakiwa kutoa siri hii ila nitaitoa kuyakomboa maisha ya ndugu zangu waliopo huko Arusha.
PAMELA: Inamaana wamepatwa na matatizo?
TULO: Inawezekana, kwajinsi walivyonieleza inawezekana kabisa wamepatwa na matatizo ila siri hii itaweza kuwakomboa.
DEBORAH: Tueleze basi hiyo siri.
Tulo akaanza kwa kuwaelezea namna alivyofahamiana na Maiko.
"Ilikuwa ni Dar es salaam, kwa mara ya kwanza nilionana na Maiko nikiwa ufukweni, eneo maharufu kabisa lijulikanalo kama Coco beach, kwa mimi nilijua kuwa ile ndio mara yangu ya kwanza kufahamiana nae ila yeye aliniambia kuwa ile ni mara ya pili kwa mimi na yeye kuonana na kusema kuwa amenifahamu mimi tangia mdogo na amewahi kumwambia mama yangu kuwa anatamani siku moja afanye kazi na mimi.
Nilimshangaa sana, ila sikupinga alinikaribisha kufanya nae kazi ambayo alisema itakuwa na kipato kikubwa sana.
Nilijiuliza sana aina ya kazi ila sikujari sana kwavile nilisikia kuwa ina kipato kikubwa.
Nikazoeana sana na Maiko na kuamua kumuaga shangazi kisha nikatokomea Arusha, kazi za Maiko lazima ule kiapo na kiapo anachokulisha anakuwa na maana kubwa sana, kwavile nilitaka pesa sikuwa na maswali mengi.
Maiko akaniweka kama msiri wake namba moja na hapo ndipo nilipogundua siri kubwa sana iliyojificha kwa Maiko"
Wakati Tulo akielezea hayo, Yuda na Adamu huku wakiwa wamembeba bi.Rehema walifanikiwa kufika kwenye barabara, wakaona gara likija na wakalisimamisha ili wafike mjini.
Gari likasimama na wakapanda, ile kumtazama dereva wakapambana na sura ya Maiko.
 
SEHEMU YA 95


Gari likasimama na wakapanda, ile kumtazama dereva wakapambana na sura ya Maiko.
Wakapatwa na mshtuko mkubwa sana huku ile sura ikiwachekea, walitamani kuteremka ila walishindwa kwakuwa gari lilikuwa kwenye mwenye.
Adamu na Yuda hawakutambua kabisa cha kufanya, bora bi.Rehema aliyekuwa bado amezimia.
Wakiwa ndani ya lile gari, likafika mahari na kusimama na gafla lile gari likapotea na kujikuta wote wakiwa nje bila hata ya kushuka. Walikuwa mbele ya nyumba ya Maiko.
Hakuna aliyeamini lile tukio kati yao, mara gafla bi.Rehema nae akazinduka na kuwaona Yuda na Adamu wakiwa kwenye mshangao na mshtuko wa hali ya juu. Akabaki akiwashangaa, kuangalia mbele anamuona mtu kasimama mbele yao, bi.Rehema hakuamini macho yake akayafikicha sana na kutazama tena akamuona ni mwanae Maiko tena Maiko yule yule aliyejiua mbele yao na kukaa monchwari karibia wiki nzima kwa uchunguzi leo hii yupo mbele yao tena akiwa mzima kabisa.
Bi.Rehema alijikuta akiropoka,
"Hivi naota au ni kweli jamani?"
Wote wakakaa kimya kuona atakachofanya Maiko pale mbele yao.
Ndani ya nyumba ya Deborah waliendelea kusikiliza maelezo ya Tulo kuhusu Maiko.
DEBORAH: Ndio useme hiyo siri basi maana hatujui huko wapo kwenye hali gani ili kama kuna uwezo wa kuwasaidia tuwasaidie.
PAMELA: Kweli kabisa Tulo, endelea kutueleza ili tujue la kufanya.
Tulo akaendelea kuwaeleza habari za Maiko.
"Ukianza kazi kwa Maiko lazima ule kiapo, kiapo cha kutokutoa siri wala kukiuka malengo ya kazi yake. Kiapo ambacho unalishwa na Maiko kinakufanya uwe mtumwa wake na mara nyingi unafanya kitu anachotaka yeye na sio unachotaka wewe.
Mimi pia nililishwa hicho kiapo na nikawa mfanyakazi wake hodari na shupavu, nimefanya kazi nyingi kwa Maiko kama vile kusambaza madawa ya kulevya na viungo vya watu.
Katika hali ya kawaida ya ubinadamu lazima mtu utaogopa kusambaza vitu kama viungo vya binadamu ila kiapo cha Maiko kinakupa ujasiri na kukuondoa uoga kabisa.
Mashaka alikuwa mtu wa karibu sana na Maiko, yeye alikuwa akichukua viungo vya binadamu na kupeleka nje ya nchi na akirudi huko anakuja na pesa nyingi sana na kuchukua mzigo mwingine, kwakweli hadi leo sijui huwa wanafanyia nini viungo vya binadamu ingawa nimefanya nao kazi kwa muda wa kutosha tu.
Mara nyingi Mashaka ndio alikuwa anatoa oda ya kuua watu wa aina flani na kuchukua viungo vyao ila Maiko akienda kuua mtu ujue ana kisasi nae na atabeba kichwa na kukitunza ndani ya nyumba yake.
Unaweza ukamuona mtu anamuonekano ambao si wa kawaida na wengine labda ana macho makubwa sana au madogo sana, kama umeongozana na Mashaka basi atakupa oda muda huohuo kuwa anayataka macho ya yule mtu, tunachofanya ni kuwaambia vijana wakatekeleze kazi hiyo. Ndiomana Mashaka alipomuona Tusa alitoa oda mapema ya kuhitaji vitu vya mwilini mwake maana alikuwa tofauti kidogo na wengine.
Siri kubwa ya Maiko ni majini aliyoyahifadhi ndani ya nyumba yake, siri hii ni mimi pekee ndiye aliyenieleza na kunitaka niitunze nami nikamuahidi kufanya hivyo.
Maiko aliniambia kuwa aliyapata majini hayo alipokuwa Mombasa kule ufukweni ndipo alikutana nayo na yakamuahidi kumtajirisha atakavyo na kumfanyia chochote atakacho ila tu anatakiwa kuwasikiliza wanachotaka.
Maiko alianza kutajirika taratibu huku Mashaka akisaidiana nae.
Mashaka alimsaidia Maiko kutoka Mombasa na wakaanza kusafiri wote ila yale majini hayakupenda Maiko asafiri safiri mara kwa mara nje ya nchi ndipo yakamtafutia sehemu ya kuishi kule Arusha, ukiangalia ile nyumba ya Maiko ilivyokubwa na muda ambao Maiko ametumia kuijenga huwezi kufikiria hata kidogo kama inawezekana ila aliwezeshwa na yale majini.
Wakati Maiko akiishi Arusha, yale majini yalipendelea sana damu kitu kilichomfanya Maiko kuchinja ng'ombe mkubwa kila baada ya miezi mitatu kama kafara yake kwa majini hayo, haikuwa kazi kubwa kwavile Maiko ni mtu mwenye pesa tofauti na watu wengine ambao hawana pesa.
Kulikuwa na chumba maalum kwaajili ya kuchinjia ng'ombe hao.
Kiukweli wakati ananieleza kuwa ile nyumba ina majini niliogopa sana, hata kulala niliogopa ila badae nikazoea.
Majini yale yalimpa Maiko sharti moja kubwa sana kwa Maiko ila ni dogo kulingana na hali ya kawaida tena ni sharti zuri sana.
Maiko alipewa sharti la kutokuthubutu kumdhuru baba yake mzazi.
Aliponiambia hilo sharti nilimwambia ni sharti dogo sana ukizingatia babake anaishi nae vizuri hapo nilijua Mashaka ndiye mzazi wake.
Maiko akaniambia kuwa Mashaka si baba yake mzazi ila nisimwambie Mashaka na kwa kifupi alikuwa hamjui baba yake mzazi si kwa jina wala sura, aliniambia anamjua mama yake tu ambaye alimuona zamani sana hata hivyo mamake huyo amekwisha kufa.
Maiko aliona lile sharti kuwa gumu sana kwake, hivyo basi alitoa oda kuwa tukimuona mtu kafanana nae tumpe taarifa huenda akawa baba yake ili awe huru na kazi yake.
Viungo vya binadamu ambavyo Maiko alikuwa anahifadhi ndani kwake alikuwa anayahifadhia majini yake.
Majini yale yalimwambia kuwa akikiuka hilo sharti atajiharibia sana kwani mambo yake mengi yataharibika na mtu asiyemtarajia atamgeuka na nguvu zake zitapungua hataweza kumdhibiti mtu yeyote yule tena na atakosa mwelekeo wa maisha, biashara zake zitayumba, siri zake zitafichuka na maisha yake kudolola hata kuisha kabisa.
Hapo hata mimi nikajifikiria sana na kugundua kuwa mali za majini ni za mikataba ndomana wanakupa sharti ambalo wanajua siku moja utaligeuka tu na kufanya wao wakufilisi kila kitu na kukuacha patupu.
Maiko aliwahi kuniambia kuwa hata atakapokufa lazima apate wafuasi wa kwenda nao na maji.
Mambo ya Maiko yameharibika kwa kifo cha baba yake mzazi, alikuja Mwanza kumsaka Patrick ndipo alipogundua kuwa walimuua baba yake.
Maiko aliporudi Arusha alienda kuyaomba majini yake yamrejeshee nguvu zake kama zamani, Maiko alilia sana na kusema anazidiwa na Patrick. Yale majini yalimwambia kitu kimoja kuwa anatakiwa kwenda na Patrick kule Arusha kwavile yeye na Mashaka walishindwa kumpeleka Patrick kule Arusha ndiomana mimi nikajitoa kuja kumfata Patrick nimpeleke Arusha.
Mashaka alishukuru sana kwani mambo yao mengi yaliharibia ukizingatia Mashaka alimfanya Maiko kama chambo chake kwahiyo akiyumba Maiko na yeye anayumba.
Maiko alipewa onyo la mwisho kuwa hatakiwi kuguswa mwilini mwake na kitu chochote chenye asili ya moto hadi pale atakapompeleka Patrick kule Arusha kwenye majini yake, na kama akiguswa na kitu cha moto ataharibu kila kitu.
Wakati mimi niko Mwanza, nilikutana na Patrick ambaye alipogundua dhamira yangu akanipiga sana hadi nikapoteza fahamu.
Patrick ana nguvu za ajabu ambazo zinanifanya nihisi kuwa kuna kitu amepandikizwa.
Nilipopata nafuu niliwasiliana na Maiko aliyeniambia kuwa amemwagiwa maji ya moto na bi.Deborah, hamu yote ya kurudi Arusha ikaniishia hapo niliogopa kuwa huenda yale majini yakanibadilikia mimi kwani sharti limeshavunjwa tayari na Maiko alikuwa akiuguza tu kidonda chake.
Nilijua mambo yameshaharibika ila nilijikaza kiume, ndipo nilipoanza kumtokea Tina ili nipate mwanamke wa kurudi nae kule kwani majini ya Maiko yalijua sana kuwahurumia wanawake ingawa Maiko alikuwa akimchukia mwanamke kuliko mtu yeyote duniani huku akimpachika sifa kuwa mwanamke ni mtu muongo, mlaghai, mwizi, tapeli na hafai kwenye jamii.
Mliponiambia kuwa mmefata maneno aliyoacha Maiko kuwa msimzike bali mkamchome kwenye nyumba yake nikaona si mbaya sana ila ingekuwa vyema kama mngemzika tu.
Mliponiambia kuwa kuna watu wamerudi kutazama nyumba ya Maiko iliyoungua, hapo ndipo pabaya tena nilipowapigia simu na kusema wameshaenda na nyumba haijaungua kabisa hapo ndipo pabaya zaidi.
Nadhani watakuwa na matatizo na tatizo lao linaweza kutatuliwa na kitabu kidogo cha Maiko kilikuwa kwenye begi lake dogo"
Ndipo Deborah akakumbuka kuwa kuna kibegi kidogo chenye mafaili walitoka nacho kwenye nyumba ya Maiko ikabidi aende kuangalia kama kweli lile begi wamefika nalo Mwanza.
Kila mmoja aliombea hilo begi liwepo ili Tulo awaambie cha kufanya na hicho kitabu kuweza kukomboa maisha ya ndugu zao.
Hali iliendelea kuwa mbaya pale nje walipowekwa kwenye nyumba ya Maiko, wakashangaa Maiko akitangulia na wao wakimfata vilevile wakiwa chini kama wanavutwa na sumaku.
Yuda alijilaumu sana kwa kuwasindikiza, alikumbuka maneno ya mama yake kuwa warudi wote Mwanza.
Adamu nae alizidi kumlaumu mama yao kwani walikuwa katika hali mbaya ya bila kutarajia.
Wakiendelea kuvutwa kama sumaku, mara gafla yule mtu aliyekuwa Maiko akageuka kuwa mti mkubwa wa mbuyu.
Kila mmoja alibaki kutaharuki, mara ule mti ukaanza kusogea.
 
SEHEMU YA 96


Kila mmoja akaanza kutaharuki, mara ule mti ukaanza kusogea.
Hofu ikazidi kuwatanda, wakashindwa cha kufanya, wakatamani kupiga kelele ila sauti zao hazikutoka.
Kufika mahali ule mti nao ukayeyuka, woga ukawatanda na wakatamani kunyanyuka na kukimbia ila walijikuta wakiwa wazito sana kuinuka, hakuna aliyeweza kunyanyuka walikuwa kama wamegandishwa pale chini.
Mara kuna kuna majimaji yenye asili ya damu yakawa yanawamwagikia pale walipokuwa.
Deborah aliendelea kusaka lile begi, Tulo aliendelea kuzungumza pale haswa na mama yake.
AMINA: Kwakweli huyu Maiko ni mtu mbaya sana, yani mimi kukuhamisha kote kule bado akakupata mmh!
TULO: Hukutakiwa kunihamisha mama, ulitakiwa uwe nami karibu kunikinga nae na hata kunipa onyo. Ila Maiko ni mtu mwenye vishawishi vingi sana, hutumia njia mbadala kumpata mtu yeyote amtakaye.
Deborah alifanikiwa kukipata kile kibegi na kukipeleka kwa Tulo ambaye alichukua na kumwaga vitu vyote kuangalia kama atakiona hicho kitabu, na kwa bahati nzuri alifanikiwa kukiona.
Kilikuwa ni kitabu kidogo sana chenye karatasi kumi tu na kimeandikwa kwa lugha ya ajabu ambayo huwezi kuisoma kama sio mmoja wao.
Tulo alikishika kile kitabu na kupitia kurasa zake za ndani huku akikisoma kwa lugha ya ajabu na wote wakabaki kumshangaa tu, kadri alivyokisoma kikawa kinabadilika rangi na kuwa nyekundu. Alipokimaliza chote kikawa na rangi ya damu ambayo ilienea hadi kwenye mikono ya Tulo.
Kisha Tulo akawatazama wote pale sebleni na kuwaambia,
"Jamani, hiki ambacho mimi nafanya ni khatari sana kwahiyo msishangae kwa chochote kile ambacho kitanipata.
Ni kheri apotee mtu mmoja kuliko kundi la watu wasiokuwa na hatia, najua yale majini hayawezi kuacha hadi siri hii imetoka.
Nimeua watu wengi kwa kushinikizwa na Maiko pamoja na majini yake, nisingependa Patrick awepo katika mlolongo wa watakao angamia.
Maiko alikiuka masharti na ndiomana hajamuweza tena Patrick ambaye amekuwa na nguvu za ajabu, napenda Patrick awe mtu wa kawaida sitapenda aangamie kama wengine."
Tulo akamuangalia Patrick kisha akamuita kuwa amsogelee.
Patrick akamsogelea Tulo na kumsikiliza.
TULO: Ulitumia kitabu hiki kula kiapo mbele ya Maiko, sasa nakuomba utumie tena kitabu hiki kuvunja kiapo ulichokula kwa Maiko.
Patrick akachukua kile kitabu na kukishika huku akivunja kiapo kwa kufatiliza maneno anayoambiwa na Tulo, baada ya hapo Tulo akamfanyia kitu ambacho Patrick alifanyiwa mwanzoni wakati wa kula kiapo.
TULO: Swala la kiapo limeisha kwako Patrick, ila kuna kitu cha ziada utakachofanya. Hiki kitabu kitachomwa na wewe ndio utahusika kufukia majivu ya kitabu hiki.
Patrick akaitikia kwa ishara kuwa ameelewa kinachoongelewa.
Tulo akaendelea kuzungumza.
"Jamani, swala kubwa la kuwakomboa wale ni kukichoma hiki kitabu.
Ila katika kukichoma hiki kitabu, kuna mambo ambayo lazima yatokee moja wapo ni mimi kuangamizwa. Napenda kusema tena kuwa ni kheri aangamie mtu mmoja na wengi wapone.
Nimeshamaliza watu wengi sana kwa kusaidiwa na Maiko kwa nguvu za majini yake.
Hiki kitabu kinamaana kubwa sana kwa Maiko na Majini yake ndiomana amekuwa akikitumia hiki kitabu katika kulisha watu kiapo na kuangamiza watu mbalimbali.
Siri ya hiki kitabu ndio ambayo itaniangamiza mimi"
Amina uoga na hofu vikamtanda kuwa huenda mtoto wake nae anataka kufa.
AMINA: Unanitisha Tulo, unamaana gani kusema utaangamia? Inamaana na wewe unataka kufa?
TULO: Mama, kufa ni kawaida ya mwanadamu. Wanadamu kifo tumeumbiwa kwahiyo usiwe na shaka.
AMINA: Nisiwe na shaka kivipi wakati maneno yako yananikosesha amani?
Ikabidi Tulo ampe mama yake maneno ya kumtuliza kisha akaendelea kuwaeleza kuhusu kile kitabu.
"Hiki kitabu ndio kina mambo yote ya majini ya Maiko, tusipokiteketeza hiki kitabu basi tutakuwa na tatizo kubwa sana. Hata Maiko alipopewa hiki kitabu alikula kiapo, na mimi nilipopewa siri za hiki kitabu nililishwa kiapo cha kutokusema siri hiyo ila leo nimeisema na pia naenda kukiteketeza hiki kitabu.
Naomba mniletee kisu, kibiriti na mfuko wa plastiki niweze kufanya hii kazi kiufasaha. Na Patrick ataenda kufukia jivu kwakuwa yeye ni shupavu na ana nguvu sana"
Wakamletea vitu alivyohitaji na kumkabidhi ili afanye ile kazi ya kukiteketeza kitabu.
Upande wa wakina bi.Rehema hali ilikuwa mbaya sana.
Uoga nao ulizidi kuwatawala kwani walikuwa wamelowa damu mwili mzima huku wakitetemeka sana.
Yule mtu wa kufanana na Maiko akawatokea tena mbele yao, safari hii alikuwa amebeba panga linalong'aa sana. Wote wakaogopa, ikabidi bi.Rehema ajaribu kujitetea,
REHEMA: Maiko mwanangu, mimi ni mama yako mzazi na hawa ni ndugu zako tuhurumie tafadhari.
Yule mtu akacheka sana kisha akaongea kwa kejeli tena kwa kutumia sauti ya Maiko.
"Mama mzazi! Huoni fahari kuwa sehemu ambayo mwanao yupo?"
Halafu akanyoosha mkono, kisha ikatua maiti ya Maiko mbele yao tena akiwa vilevile kama alivyojiua nyumbani kwa Deborah.
Wote wakaogopa, kumtazama Maiko maiti na Maiko aliyesimama.
Yule mtu alilishikilia lile panga vizuri kama vile anajiandaa kuwachinja.
Tulo alichukua kisu na kujikata kwenye kiganja na mkono wake huku damu nyingi zikimwagika zikiungana na zile damu za kwenye kijitabu.
Halafu akachukua kiberiti na kuchoma karatasi moja moja za kile kitabu na kumalizia na ganda la nje.
Kisha akakusanya jivu lote na kuliweka kwenye ule mfuko wa Plastiki, akaufunga vizuri na kumpa Patrick akafukie huku akimpa maelekezo ya namna ya kufukia lile jivu ambapo alitakiwa aende pekeyake kufukia.
Wakati Patrick analifukia lile jivu, hali kwakina bi.Rehema ilikuwa mbaya sana mara mvua mara jua, mara mwanga unakuwa na rangi nyekundu mara wa kawaida, mara ile maiti ya Maiko na yule mtu vinatoweka mara vinakuja tena mbele yao.
Hali ilikuwa mbaya sana, upepo mkali ukavuma na kuwafanya wapatwe na kizunguzungu pale chini.
Mara gafla wakainuliwa juu kabisa wote watatu yani bi.Rehema, Adamu na Yuda kisha wakabwagwa chini kama mzigo wa kuni halafu wote wakapoteza fahamu.
Patrick alitumia ujasiri wa hali ya juu katika kufukia lile jivu kwani alipolitua pale chini lilikuwa zito kama vile kitu kikubwa ila kwakuwa Patrick alikuwa na nguvu sana, aliweza kulifanikisha lile zoezi halafu akarudi ndani.
Kufika ndani akawapa taarifa kuwa ameshafanikiwa kufukia lile jivu na hapo hapo Tulo akaanguka chini na povu kumtoka mdomoni.
 
SEHEMU YA 97


Tulo akaanguka chini na povu kumtoka mdomoni.
Tulo alitapatapa kama vile mtu aliyekunywa sumu tena sumu kali.
Wote wakamsogelea na kujaribu kumpa huduma ya kwanza kisha kumuwahisha hospitali.
Amina alikuwa akiyakumbuka maneno ya mwanae tu kuwa lazima aangamie, alikosa imani kuwa Tulo atarudi tena katika hali ya kawaida.
Pale hospitali kila mmoja alikuwa na wasiwasi, hakuna aliyekuwa na amani kabisa.
Bi.Rehema na wenzie walizinduka na kujikuta wote wapo hospitali, kumbe wasamalia wema waliwasaidia na kuwapeleka hospitali.
Yuda ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzinduka baada ya kupata unafuu kiasi, kisha akafatiwa na Adamu na badae bi.Rehema.
Walikuwa wamechoka sana kama vile wamefanya kazi ngumu.
Baadhi ya wasamalia wema waliowasaidia walikuwepo pale hospitali kuwaangalia hali zao zinavyoenda.
Kwakweli waliwashukuru sana na kuwauliza walipowatoa.
Mmoja wao akawaambia ilivyokuwa,
"Kwakweli tulishtuka sana kuwaona pale kando kando ya barabara tena wote mkiwa hamna fahamu, ikabidi tuwabebe na kuwawahisha hapa hospitali. Sijui mlipatwa na nini jamani!!"
Ikabidi wajifanye wamesahau kitu ambacho kiliwatokea hapo kabla.
Hawakuwa na kitu chochote si pesa wala simu, vyote vilibebwa na ndivyo ilivyo upatapo tatizo mwingine anakusaidia na mwingine anashukuru kupata nafasi ya kukuibia kwa urahisi.
Hali ya Tulo ilikuwa mbaya sana na mwisho wa siku akapoteza maisha.
Ikawa uchungu na simanzi kubwa ndani ya familia, kilio kikatawala sana uchungu na masononeko ya kumkosa Tulo.
Kila mmoja alikuwa akiilaumu kazi ya Maiko kwani ndio iliyopoteza watu wengi waliowapenda.
Wakapanga safari na kuamua kwenda kumfanyia Tulo mazishi mkoani Morogoro ili wakamzike karibu na kaburi la babu yake.
Walifika Morogoro na kupokelewa kwa kilio na mazishi ya Tulo kufanyika.
Tulo alikufa kishujaa kwani alikubali kutoa siri ya kuangamiza maisha yake ili kuwakomboa watu wengine.
Ilikuwa ni huzuni sana kwani hakuna aliyetarajia kitu cha namna ile.
Taratibu zote za mazishi zilifanyika na Tulo akazikwa pembezoni mwa kaburi la mzee Ayubu.
Patrick alipiga magoti kwenye kaburi lile, alilia sana tena sana akakumbuka jinsi alivyomzoea mzee Ayubu tena kwa muda mfupi kabisa. Akakumbuka jinsi alivyomlaghai kwa stori za hapa na pale na jinsi alivyomdanganya kwa pombe.
Akakumbuka na siku waliyommaliza kabisa mzee Ayubu, mzee ambaye hakuwa na hatia. Walimkata viganja vya mikono na kumchuna kipara chake, uchungu ulimshika sana Patrick na machozi mfululizo yalimtoka, ndipo mama yake bi.Deborah alipomsogelea na kumshika huku akimbembeleza atulie, hadi pale walipotoka makaburini.
Tusa nae alilia kwa mengi sana, alimlilia babu yake kwa uchungu uliopitilize alitamani siku zirudishwe nyuma apate kumuona tena akiongea na kutabasamu kwa ucheshi wake ila haikuwezekana kwani mzee Ayubu alishaoza mule kaburini.
Walipopata unafuu wakina bi.Rehema walihitaji kurudi Mwanza ila hawakuwa na chochote kile, wakaamua kutafuta mawasiliano ya ndugu zao na uzuri ni kuwa Yuda alikuwa anakumbukumbu ya namba nyingi kichwani.
Yuda akakumbuka moja wapo ya namba alizokuwa nazo kisha wakaazima simu na kujaribu kupiga, Deborah alipokea simu ile na kuongea nao.
Kwakweli alishukuru kusikia kuwa wamepona, ikabidi afanye mpango wa kuwatumia nauli ili wakakutane nao moja kwa moja Dar es salaam kwani nao walishapanga mipango ya kuondoka kule Morogoro na kwenda Dar es salaam ili kumaliza swala zima linalohusu wazazi wa Patrick.
Familia nzima ilifika Dar es salaam, ndugu wa Deborah hawakuacha kuambatana nae ili kujua vyote na mipango yote itakapoelekea kwani bado familia nzima iligubikwa na wasiwasi na mashaka ukizingatia mambo yaliyopita mbele yao ni makubwa sana.
Patrick hakutaka kwenda Dar es salaam ila alikubali kwenda kwa heshima ya mama yake aliyempenda kuliko kitu chochote.
Pamela aliwakaribisha vizuri ambapo Deborah alikuwa anangoja wale waliotokomea Arusha warudi pale na wapate kuondoka na Yuda kurudi nae Mwanza ili kama mipango mingine ifanywe badae.
Wakina bi.Rehema nao wakawasili na kupokelewa vizuri sana ingawa walichoka mno kutokana na hali halisi ilivyokuwa.
Wakaeleza mambo yaliyowapata. Adamu akaelezea ilivyokuwa na mambo waliyokumbana nayo.
"Kwakweli sikufikiria kama tungepona, hii itakuwa fundisho kwetu katika maisha yetu yote. Maana tusingeng'ang'ania kurudi kule yote haya yasingetupa."
Bi.Rehema aliongea kwa uchungu mno,
"Sikutegemea kabisa kama mtoto wangu wa kumzaa mwenyewe anaweza kufanana na jini kiasi kile. Sasa nakubaliana na wewe Deborah kuwa mwanangu Maiko alikuwa ni mume gaidi. Nashindwa kuamini na kuelewa hadi sasa kwa mambo yaliyotukuta"
DEBORAH: Msijari sana, katika maisha kila kitu hutokea kwasababu maalum kwahiyo yote yaliyotokea yalikuwa na maana yake na mafunzo yake ili tusirudie tena kosa lililotendeka.
Deborah alionekana sasa kuwa mtu makini sana katika kushauri kwani aliweza kuwaweka wote kwenye mstari.
Yuda hakuwa na hamu kabisa na ukoo wa Maiko ila bado aliendelea kumpenda Tina. Sele nae alikuwa anaendelea kusikilizia tu hatma ya Tusa na Patrick.
Zilipita siku mbili bila kuwepo kwa dalili yoyote ya Fausta wala Pamela kutaka kusema ukweli, ilionyesha bado hawakuwa wazi kueleza mambo ambayo yamepita nyuma katika maisha yao.
Ikabidi Deborah aamue kufanya kikao cha lazima kwani yeye na familia yake walihitaji kurudi kwao Mwanza.
DEBORAH: Jamani, ukweli humuweka mtu huru. Patrick ni kijana mkubwa sasa anatakiwa kujua ukweli kuhusu wazazi wake, nani mama yake na nani baba yake. Naona kimya kimezidi, tafadhari Fausta na Pamela fungukeni maana mimi nina hakika kuwa Patrick ni mtoto wa mmoja wenu.
PATRICK: Ila mama, mimi sihitaji kuwajua tena hao wazazi wangu. Wewe tu unanitosha.
DEBORAH: Kuna ulazima wa kuwajua Patrick, angalia hapo Tusa ni mke wako na muda huo huo ni dada yako. Ni bora ukweli ujulikane ujue hatma yako na Tusa sio kazi ya kufanya kukutenganisha na Tusa kisiri bila kujua ukweli.
Deborah aliongea hayo kwani alimuona Pamela akifanya kazi ya kumkwepesha Tusa kwa Patrick.
REHEMA: Ni kweli usemayo Deborah, mengi yamepita sasa ni wakati wa kuweka mambo yote wazi.
Pamela akainama chini kisha akapiga magoti na kumfata Patrick kwa kilio,
"Nisamehe baba, mimi ndio mama yako mzazi"
Patrick alishtuka na kushangaa kwani hakuhisi kabisa kama mama yake atakuwa Pamela, Tusa nae machozi yakawa yanamtoka.
Kila mmoja alimtazama Pamela kwa makini.
 
SEHEMU YA 98


Kila mmoja alimtazama Pamela kwa umakini.
Pamela alikuwa anamwaga machozi na kugundua kuwa alichofanya nyuma ndio kimemuumbua sasa.
Patrick aliendelea kuangalia kwa mshangao.
PATRICK: Inamaana Tusa ni dada yangu?
PAMELA: (Huku akiendelea kulia) ndio ni dada yako.
PATRICK: Acha unafki wa kulia kizembe, wakati unanitupa je ulilia au mbwembwe tu.
Pamela hakuwa hata na la kujitetea na kuishia kulia tu.
Ikabidi wakina Deborah waingilie kati na kuanza kujaribu kumtuliza Patrick aliyeonyesha kuwa amepandwa na jazba.
PATRICK: Kwakweli huyu mama nitamchukia maisha yangu yote, mama aliyenilea ndiye mama yangu.
DEBORAH: Hata Pamela pia ni mama yako mwanangu.
PATRICK: Siwezi kumkubali mama alinitupa kweli, je nisingeokotwa leo hii angemuomba msamaha nani?
DEBORAH: Yote ni mapito jamani, ni mapito ya maisha ila na wewe Pamela ilikuwaje hadi ukadiriki kumtupa mtoto wako mwenyewe?
Pamela akawa analia na kujaribu kujieleza.
"Si kwamba nilitaka kumtupa mtoto wangu, hapana kabisa ni maisha tu na mimba yenyewe iliingia bahati mbaya.
Kipindi naonaoka Dar es salaam na kukimbilia Morogoro nilikuwa ni mjamzito kipindi hiko na ubaya zaidi Deborah alishanigundua kuwa nina ujauzito, nilipomueleza muhusika akanishauri niitoe ili tuendelee kufaidi maisha mengine.
Kwa hapa Dar nilijaribu mara mbili kunywa dawa za kutoa mimba ila ilishindikana, mimba haikutoka zaidi ya damu kutoka kidogo na kukata.
Ndipo nilipoamua kwenda Morogoro kwa Fausta ambaye ni dada yangu, nilipomweleza akanishauri kuwa ni bora kuitoa ila kuepukana na matatizo yasiyo ya lazima.
Fausta akaenda kuniletea dawa toka kwa daktari wake, dawa ambazo hata yeye amewahi kutumia.
Basi na mimi nikatumia zile dawa ila ikawa ola kama mwanzo ile mimba haikutoka wala nini na ikaendelea kukua, dada akanishauri niitoe kwa njia ya kujifungua mwanzoni nilikataa kabisa na mimba nayo ikaendelea kukua. Sijui ni kwa nini ilishindikana kutoa kwa njia ya kunywa dawa.
Ile mimba ilipoendelea kukua ikawa inanisumbua sana nikashindwa kufanya kitu chochote, dada akaniambia kwavile tumejaribu kuitoa mara kwa mara ndiomana imeanza kunisumbua.
Hadi pale Adamu alipofika Morogoro, akanikuta niko hoi kabisa sitamaniki kutokana na ile mimba sikuweza kufanya kitu chochote.
Adamu akatoa ushauri kuwa nikafanyie hata operesheni kuweza kukitoa kiumbe hicho na tukashauriana kama huyo mtoto tumlee au la ila Fausta akasema yule mtoto atakuwa tahira kwani atakuwa ameshaathirika na yale madawa ya kutolea mimba, na mimi sikuwa tayari kulea tahira tukashauriana kuwa tukimtoa tumtupe kwani hatokuwa mwanadamu wa kawaida.
Tukaenda hospitali moja kule Morogoro na kumuomba daktari anifungulishe naye akanipima na kukuta mimba imekaa vibaya hapo uoga na wasiwasi mwingi vikanishika.
Adamu akaamua kusafiri na kurudi Dar na kutuambia kuwa tujitahidi kukamilisha mambo kabla hayajaharibika.
Ni hapo kesho yake mimi na Fausta tukakubaliana turudi Dar kushughulikia hili swala kwani dada alikuwa anajuana na madaktari wengi, tulipofika kwa daktari tukamueleza kila kitu naye akasema ni kweli kuna uwezekano mkubwa sana wa mtoto atakayezaliwa kuwa ameathirika na madawa niliyokunywa kabla, lazima atakuwa na kasoro na kutofautiana na binadamu wa kawaida na hatoweza kuchukua muda mrefu wa kuishi.
Nilimuomba anitoe tu hivyo hivyo ili nipate kupumua.
Nikiwa mimi na dada pale hospitali, niliingizwa chumba cha kufanyia operesheni na huko nilikuwa nusu kaputi hata mtoto gani aliyezaliwa sikubahatika kumuona alivyokuwa.
Nilipozinduka jambo la kwanza niliulizia kuwa mtoto mwenyewe yuko wapi, daktari akaniambia kuwa dada yangu amemchukua nikachukia sana kwani nilihitaji kwanza kumuona mwanangu.
Daktari aliniambia mtoto niliyejifungua alikuwa wa kiume ila afya yake imedhoofika sana kutokana na madawa niliyokunywa kuitoa mimba ile.
Roho iliniuma sana kumuhusu huyu mtoto na sikujua kwanini dada amechukua maamuzi ya gafla ya kwenda kumtupa mwenyewe bila kuningoja mwenye mtoto nishtuke na nitoe maamuzi yangu.
Sikutamani hata kulala tena, nilikuwa namngoja tu dada arudi ili anipeleke alipokwenda kumtupa mwanangu laiti kama kungekuwa na simu kama sasa basi ningempigia na kumsihi asimtupe mwanangu.
Nilimngoja na hatimaye akarudi, niligombana nae sana kwa maamuzi yake ya haraka kwenda kumtupa mtoto, nikamwambia kuwa namtaka mwanangu akasema atakuwa ameshakufa nikamwambia hata kama namtaka hivyo hivyo nikamzike mwenyewe kuliko kumtupa.
Kuteseka nayo ile mimba na aibu yake ndio vilivyonifanya niwaze kuitoa na kujaribu kufanya hivyo ila alipotolewa mtoto uchungu ulinishika sana juu ya huyo mtoto, nilikuwa tayari kwa lolote juu ya mtoto huyo ila ndio hivyo alikuwa ameshatupwa.
Ilikuwa usiku hata sikutaka kusubiri pakuche kwani nilihofia kukuta mwanangu ameliwa na mbwa.
Nilimlazimisha dada anipeleke tukamchukue mwanangu, ingawa nilikuwa na maumivu ya operesheni ambako sikutakiwa kulia wala kuhangaika sana ili kuepusha nyuzi kukatika.
Niliondoka na dada pale hospitali hadi eneo alilotupa mtoto, tulitafuta sana ila hatukumuona na mawazo machafu yakanijua kuwa mwanangu atakuwa ameliwa na mbwa tu.
Nililia sana na kujikuta nikiampa lawama zote dada yangu Fausta, nililia hadi mshono ukafumuka.
Maumivu makali ya kidonda na ubaridi wa hapo sikuweza kusogea kwani nilikuwa hoi kabisa kabisa, dada akatafuta gari na kuniwahisha tena hospitali.
Nikashonwa tena, ila kila nikishtuka na kuwaza kuhusu mwanangu kuliwa na mbwa machozi yalinitiririka sikuwa na wazo kabisa kama mtoto yule ameokotwa na mtu.
Nilipopona kiasi eneo lile ndio lilikuwa mahali pa kupumzikia, nilikuwa nikimkumbuka mwanangu basi naenda kulekule ambako dada alimtupa mtoto wangu. Nalia sana na kurudi nyumbani.
Ndipo nilipoamua na dada yangu turudi pale Dar tulipokuwa tukiishi mwanzo na badae yeye kwenda Morogoro na kuniacha mimi pale, niliamua kurudi ili nikaongee na Deborah nilitaka kwenda kumueleza ukweli na kumuomba msamaha kwani niliona kama ile ni laana tu.
Kufika pale mtaani nikakutana na habari nyingi sana kuhusu mtoto wa Deborah, roho iliniuma sana kwani Jasmini nilimchukulia kama mwanangu wa kumzaa.
Ndipo nikapata habari kuwa Deborah aliacha skendo na asingeweza kurudi tena, hapo tumaini la kuonana na Deborah likaisha.
Nikaonyeshwa msichana aliyekatwa miguu na Deborah ambaye alikuwa ni mtoto wa mama mwenye nyumba yake, kwanza nilishindwa kuelewa kwanini Deborah kachukua uamuzi ule.
Yule binti alikaa hospitali mwezi mzima na aliporudi alikuwa anatembelea baskeli za walemavu kwani miguu yote miwili hakuwa nayo tena.
Na habari nyingine ni kuwa nilikuja kusikia kuwa yule binti alipata ajari na kufa.
Adamu aliporudi kwake alikutana na maskendo hayo na alitakiwa asaidie upelelezi ambapo walifika hadi Mwanza kumsaka Deborah ila hawakumpata na hakuna aliyejua alipo.
Ikabidi mahusiano yangu na Adamu yaanze upya na ni hapo tulipoamua kuhama mtaa na alipoamua kubadili jina toka Jumanne hadi Adamu ili kusahau yaliyopita na kufanya kuwa yamepita, ingawa tulipokwenda kwa mzee Ayubu akatuambia kuwa sisi ni ndugu haitakiwi tuwe mume na mke tukampuuzia na kumwambia kuwa sisi tumeshapendana hatuwezi kuachana.
Akatusihi sana ila hatukumsikiliza na sasa ndio tunaelewa laana tuliyojijengea sisi wenyewe.
Siku Deborah anaelezea historia kuhusu maisha yake na Patrick iliniuma sana kujua kuwa Patrick ni mwanangu tena kamuoa Tusa mwanangu. (Pamela akainama na kulia tena).
Roho inaniuma sana hata sijui kwanini imekuwa hivi, najua Patrick huwezi kunisamehe, najua Tusa mwanangu nimekusababishia kidonda kikubwa ambacho hakitakuja kufutika kamwe maishani mwako ila ndio hivyo Patrick ni kaka yako tena wa damu moja"
Pamela alikuwa analia sana, bi.Rehema akamsogelea kumbembeleza.
Adamu alihisi kuchanganyikiwa kabisa kuwa Tusa ameolewa na kaka yake kwani hakufikiria kabisa kama Patrick mwanae, alihisi Patrick ni mtoto wa Fausta na Maiko, kwakweli alijihisi kulaanika kabisa.
Tusa alikuwa akilia tu na yeye, huku wakibembelezana na Tina ambaye naye alibakwa na baba yake mzazi.
TUSA: Huu ukoo kweli una laana tena umelaanika toka kwenye kilele chake.
Patrick alikaa kimya kabisa akitafakari bila hata kuelewa kuwa kwanini imekuwa vile ambavyo imekuwa, hakuna aliyetarajia kuwa vile.
Marium naye aliwawaza tu watoto wake wawili Yuda na Sele ambao nao wanahitaji kuingia kwenye ukoo huo, alitamani warudi utotoni ili akawafungie ndani.
Anna alikuwa anamuwaza mwanae Mwita ambaye ni mmoja wa watu kwenye ukoo huo ambaye naye tayari alikwisha mbaka dadaye Tusa.
Ukoo ulijaa laana na ulinuka laana ambayo kiini chake hakikujulikana kwa wakati, hadi pale Mwita alipotoa barua ambayo iliachwa na Maiko kuhusu Mashaka. Barua ambayo bi.Rehema aliichukua na kuiangalia.
MWITA: Nadhani maelezo ya humu yanaweza kutupatia hata taswira ya nini kilitokea hadi kupelekea kuwa hivi, haya ni makosa yaliyofanyika tangu awali na hayakupatiwa ufumbuzi mapema ndomana ukoo umeweza kutoa magaidi ya kutosha.
Mwita aliongea hivyo kwani hata yeye mwenyewe hakuwa na tofauti sana na magaidi yaliyotangulia na ndiomana aliweza kumbaka hata dada yake bila ya kujua.
Tusa alimwangalia sana Mwita kwa kujiongelesha kuwa ukoo wao umejawa na magaidi ya kutosha.
Akajisemea moyoni,
"Ingekuwa amri yangu haya magaidi ya ukoo huu yote ningeyafyekelea mbali kasoro Patrick"
Tusa alijikuta akijawa na imani sana juu ya Patrick ingawa alishamfanyia mambo mengi mabaya.
Kila mmoja alikuwa akiwaza yake kwa muda huo kwani hakuna aliyeongea akaeleweka kwa mwingine moja kwa moja, mara gafla bi.Rehema akaanza kulia.
 
SEHEMU YA 99


Gafla bi.Rehema akaanza kulia.
Wote wakamtazama kwa mshangao na kumuuliza kwanini analia,
REHEMA: Hii barua ya Mashaka imeniumiza sana na kunikumbusha vitu vingi vilivyopita.
ADAMU: Vitu gani mama?
REHEMA: Yani Tusa anaposema kuwa ukoo huu umelaaniwa hata hajakosea, tatizo limekuwa ndani ya chimbuko la ukoo wenyewe.
FAUSTA: Tueleze tupate kujua maana tushachanganyikiwa tayari.
REHEMA: Nitawaeleza kile ninachokifahamu na maelezo mengine mtayapata kwenye hii barua ya Mashaka.
Wote wakatulia ili kumsikiliza bi.Rehema maana hali ya ukoo huo tayari ishakuwa tete na inatakiwa wairekebishe kabla ya vizazi vyao vitakavyokuja mbele.
Bi.Rehema akaanza kuelezea,
"Baba yangu kwao walizaliwa mapacha yani yeye na bamdogo ambaye ni baba yake na Neema ambaye ndio mama wa Fausta na Pamela.
Baba alimuoa mama yangu na bamdogo alimuoa mama yake na Neema, kuzaliwa kwangu na Neema hakukutofautiana sana yani tulifatana sana kuzaliwa na wakatuweka kama mapacha ndomana mimi nikaitwa Rehema na yeye Neema.
Familia zetu tulipendana sana na tulikuwa tukitembeleana kila mara, haikuwa kitu cha ajabu mimi kulala kwa bamdogo au Neema kulala kwetu.
Siku zikapita taratibu na mapendo kati yetu yakaendelea kukua hadi alipokuja huyu mwanamke kwenye maisha yetu, mwanamke ambaye mimi namfananisha na shetani kwani alisambaratisha familia yetu yote na upendo wote kati yetu ukafa sababu ya huyu mwanamke.
Na hapa nikapata kujua mengi, si kila anayekuja kwenye familia ni mtu mwema wengine ni waharibifu na haitakiwi kumuamini kila mtu katika maisha wengine hawaaminiki na hawatakiwi kuaminiwa.
Kwa kipindi hiko nilikuwa mtoto wa pekee kwa baba yangu na mama alikuwa na ujauzito ambao nilitarajia kupata mdogo wangu.
Siku moja nilimsikia baba akizozana na mama, inaonyesha kuwa baba alikuwa akimwambia mama kuwa amepata mwanamke mwingine na anataka kumuoa. Mama akapinga swala la baba kuoa mke mwingine kwani mama yangu hakutaka uke wenza ila baba akaoa kwa lazima huyo mwanamke ambaye mimi namfananisha na shetani.
Mama hakukubali kumkaribisha huyo mwanamke kwenye nyumba yake, ni hapo kwa mara ya kwanza nilishuhudia baba akimpiga sana mama na alimpiga kweli bila ya kujali ujauzito aliokuwa nao. Roho iliniuma sana ila kwa utoto ule sikuwa na la kufanya.
Kesho yake mama aliamka vidonda mwili mzima, yule mwanamke alimwangalia mama na kumcheka huku akimkejeli.
Mama hakuweza kuvumilia, baba aliporudi akamdai taraka ili arudi kwao kwani hawezi kuishi na mtu ambaye hawaelewani ila baba alikataa kumpa mama taraka.
Kwa hali isiyotegemewa, siku hiyo nilimuona yule mwanamke akiingia chumbani kwa mama wakati mama amelala na baada ya muda akatoka, mimi nikakimbia kuona kuna nini maana yule mwanamke hakupatana na mama, ni hapo nilipokuta mama akiwa chini kabisa hajitambui, nikajaribu kumuamsha lakini hakuamka nikapiga yowe na watu wakafika badae nikaambiwa kuwa mama yangu amefariki nililia sana yule mwanamke akaniambia nisijari yeye atanilea ila bado nililia kwani upendo wa mama hakuna wa kufananisha nacho.
Baada ya msiba nilimueleza baba kuwa kabla ya kifo cha mama yule mwanamke aliingia mule ndani, nikamwambia kuwa nahisi amemuua mama ila baba alinikataza na kuniambia kuwa sitakiwi kuhisi watu vibaya.
Maisha yakaendelea na huyu mama mpya aliyejaa vitimbwi vya kila siku.
Akapata ujauzito, ni hapo ambapo baba akaanza kunichukia mimi na nikaamua kukimbilia kwa bibi, naye bibi akaniambia kuwa nisijari ni hali ya muda mfupi tu.
Nikiwa kwa bibi tukapata taarifa kuwa mama yake na Neema amefariki tena kifo cha gafla kabisa kwakweli nilisononeshwa sana kwani na yeye nilimuona kama mama yangu.
Kwahiyo Neema hakuwa na mama na mimi sikuwa na mama zaidi ya yule mwanamke wa baba.
Siku moja nikiwa kwa bibi na Neema, Neema akaniambia kuwa amekutana na yule mwanamke na amempa pole ya kufiwa na kumwambia kuwa asijari atamlea.
Tukafikiri kuwa labda yule mwanamke ana moyo wa upendo ila haikuwa vile tulivyodhani.
Laiti baba angejua kama yule mwanamke anafata mali basi hata asingelazimisha kumuoa.
Yule mwanamke ilikuwa kama una mali basi utampata.
Akajifungua mtoto wa kiume ambaye baba alimuita Mashaka, kwakweli baba alimpenda sana Mashaka kuliko mimi kwavile Mashaka alikuwa mtoto wa kiume na siku zote baba alitaka mtoto wa kiume atakayeongoza familia na kurithi mali zake.
Mashaka alipofikisha miaka miwili tabia ya mama yake ilibadilika zaidi, mara nyingi hakuonekana nyumbani wala wapi.
Kuna kipindi akapotea kwa miezi miwili, baba akamtafuta sana kuja kugundua kumbe anaishi kwa bamdogo huko anapika na kupakua.
Kwakweli sijui huyu mwanamke aliwapa nini baba zangu hawa.
Kikawekwa kikao cha familia na yule mwanamke alikiri kuwa ana ujauzito aliopewa na bamdogo.
Ikabidi bamdogo na baba waamue moja kuwa nani abaki na yule mwanamke, wote waligoma kwani baba alitaka kurudi na yule mwanamke nyumbani kwakuwa ni mke wake na wana mtoto mdogo na bamdogo nae akataka aende na yule mwanamke kwake kwakuwa ana ujauzito wake, wote wawili walimng'ang'ania ndipo wazee walipomtaka yule mwanamke achague na hawakuweza kumpa adhabu sababu ya ule ujauzito.
Yule mwanamke akachagua kwenda kwa bamdogo.
Yule mwanamke misingi yake ilikuwa ni kwa mwanaume mwenye mali na kwavile bamdogo alikuwa na mali nyingi kushinda baba ndio akachagua huko.
Ilimuuma sana baba yangu tena sana ukizingatia yule mwanamke amemtafuta mwenyewe.
Ndipo baba alipotamka kauli kuwa yeye na bamdogo wasijuane tena na undugu wao ufe, na bamdogo nae akaafiki, sijui huyu mwanamke alikuwa na mimi hadi kuweza kuua undugu wa mapacha wale.
Wazee walijitahidi sana kusuruhisha lakini ilishindikana, vikao vingi vikawekwa kwaajili ya baba na bamdogo ila bado hawakupatana.
Undugu ulikufa kabisa, si mimi wala Neema tulioruhusiwa kuonana.
Roho iliniuma sana kutenganishwa na Neema ila sikuwa na la kufanya kwani yalikuwa ni maswala ya familia.
Mara moja moja nilionana na Neema kwa bibi na alikuwa akinieleza jinsi vile mwanamke yule alivyomchoyo, Neema alikonda sana utafikiri baba yake hakuwa mtu mwenye mali nyingi.
Baada ya bibi kufariki ukawa ni mwisho wa mimi na Neema kuonana hadi ambapo nimekutana na watoto wake wawili Fausta na Pamela ambao wameingia kwenye majanga na watoto wangu.
Kwenye kukua kwangu nilikuwa na mdogo wangu Mashaka ambaye badae tabia yake ilibadilika sana.
Kwani mimi nilipoanzisha mahusiano na mzee Ayubu hadi kupata ujauzito, nyumbani walikataa nisiolewe nae kwakuwa tumetofautiana kabila.
Kwetu hawakutaka mtu aolewe na kabila tofauti, hivyo basi nilipojifungua wale mapacha na kukua kua kidogo tukaamua kugawana watoto. Wazee hawakutaka kabisa mimi nionane tena na mzee Ayubu na akafukuzwa pale kwenye kijiji chetu ndipo alipoondoka na mwanangu Jumanne na mimi kubakiwa na Juma, sikupata kumuona tena mzee Ayubu hadi pale kwenye mazishi yake.
Nilibahatika kuolewa kule kijijini na kupata mtoto wa kike, ila Mashaka aliniulia mwanangu na kufanya niachike nilipoolewa na hapo wakagundua kuwa akili ya Mashaka si nzuri, akakamatwa na kupelekwa Mirembe.
Mara ya mwisho kurudi nyumbani akadai amepona, nilimpokea kwakuwa ni mdogo wangu ila akaja kutoroka na mwanangu Juma ambaye ndio huyo nimemjua ukubwani akiwa gaidi wa kutupwa huku akitumia jina Maiko.
Kwakweli mdogo wangu Mashaka ameniumiza sana tena sana"
Bi.Rehema alimaliza huku akijifuta machozi, Deborah akauliza.
DEBORAH: Inamaana huyo mwanamke aliwapa dawa mama zenu za kuwaua au aliwapa dawa baba zenu za kumpenda?
FAUSTA: Labda aliwapa limbwata, ndiomana familia hii haieleweki. Ilitakiwa pale mwanzoni kumtokomeza huyu shetani ambaye alijivaa kwa mwanamke huyo ila kwa kipindi hiko hayakuonekana madhara makubwa kama haya.
REHEMA: Barua aliyoandika Mashaka ndiyo iliyoniliza sana, Mashaka hakuwa mtu mzuri kabisa.
Ikabidi Patrick aichukue ile barua na kuanza kuisoma,
"Mimi Mashaka, natumaini kama mmeipata barua hii na kuisoma basi sipo tena duniani ila maandishi yangu tu ndio yaliyobaki.
Najua kwa yeyote atakayesoma barua hii hatokuwa na maswali zaidi kwangu kwani hata kama akiwa nayo hayo maswali sitaweza kumjibu kwavile sipo tena duniani ila nadhani mtanielewa kwa kile nilichoandika na mtaelewa kwanini nipo kama nilivyokuwa.
Katika kukua kwangu sikufurahia kabisa maisha ya kukua bila mama tena huku nikiambiwa kuwa mama yupo kwenye familia nyingine ya bamdogo.
Kuna wakati nilikuwa nakutana na mama kinyemela akiniambia vitu vingi kuwa bado anampenda baba sema bamdogo kambana, nilitamani nikue upesi ili niweze kupapambana na bamdogo. Kwani nilidhani kuwa bamdogo ndio mtu mbaya kwa kumuiba mama toka kwa baba. Lakini bamdogo hakuwahi kulihisi hilo na hakuwahi kunifukuza nyumbani kwake ila nilimchukia sana.
Katika kukua kwangu niliwaza jambo moja tu kupapambana na bamdogo ambaye sikuwahi hata kuishi naye.
Mama hakuruhusiwa kufika nyumbani ndiomana nilikuwa naonana nae kinyemela.
Ila nilipokua nilianza kwenda mwenyewe kwa bamdogo kumsalimia mama ambaye alikuwa na mtoto wa kike, bamdogo hakuwa mtu mbaya ila mama alisisitiza kuwa bamdogo ni mtu mbaya na anamtesa sana, anatamani kurudi kwa baba ila anashindwa kwasababu ya kubanwa nae. Nilimuahidi mama kuwa nitamsaidia kwahiyo asijari kitu. Upande wa baba sikuwa na shaka nao kwani najua kuwa baba alimpenda mama na bado aliendelea kumpenda ingawa kwa kipindi hiko alikuwa ameweka mke mwingine nyumbani kwaajili ya kujiliwaza tu.
Kwa mara ya kwanza nikaamua kufanya kitu cha ajabu pale kwa bamdogo ili kumfurahisha mama.
Ila ilikuwa kinyume kwani kitu nilichofanya ndio kilichofanya niwe kama nilivyokuwa.
 
SEHEMU YA 100 ............ MWISHO


kitu nilichofanya ndio kilichofanya niwe kama nilivyokuwa.
Ila niliomba ushauri kwanza, kipindi hiko nilikuwa na mpenzi wa kuitwa Maria.
Nadhani Maria hakuwa mshauri mzuri kwangu kwani yeye alitakiwa kunikataza kitu hiki cha hatari ila yeye aliniruhusu na kunielekeza njia ya kufanya.
Siku hiyo nilikuwa na Maria nikamweleza kila kitu kuhusu familia yangu na kumwambia kuwa nataka kummaliza bamdogo yani kumuua kwani nilijua kwa kufanya hivyo kutampa nafasi mama ya kurudi tena kwa baba, Maria akaniambia kuwa kama nimeamua hivyo basi ni sawa na nikamuuliza nifanyeje akaniambia nitumie sumu, nimuwekee yule baba kwenye chakula anachopenda sana.
Sikuwa mtaalamu sana na maswala ya simu ila Maria alizijua sumu porini.
Sikutaka kumshirikisha mama kwa hili kwani angeniona mtoto wake ni muuaji. Wala sikutaka kumshirikisha mdogo wangu mzuri wa kike aliyezaliwa na mama kwa kupitia bamdogo, mdogo wangu mzuri Chaurembo aliyekuwa mrembo kweli kama jina lake.
Nilipokuwa tayari kwa zoezi hilo, Maria akanipeleka porini na kunichumia majani hayo ya sumu.
Akaenda kuyaponda kisha kuyachanganya na maji na kuyachuja halafu akaweka kwenye kichupa na kunikabidhi, aliniambia kuwa ile ni sumu inayoua mara moja na kweli kwa hilo hakuongopa kabisa.
Siku hiyo nikaenda kwa bamdogo kwa lengo moja la kummaliza tu.
Nilipofika nikakuta mama ameandaa chakula mezani, nikamwambia mama kuwa nina njaa ila mama akaniambia nisile kile chakula ni cha baba. Ningoje ataniandalia changu, kwakweli niliposikia hivyo nilifurahi sana, nikavizia mama ametoka nje nami nikafunua kichupa changu cha dawa na kutia kwenye bakuli la mboga ambayo ilikuwa ni nyama ya kuku iliyoungwa vizuri sana.
Baada ya kutia ile dawa, mama akaniita nje akaniambia nimuendee kwa fundi nguo kumchukulia nguo yake halafu nikirudi nitakuta chakula changu kiukweli nilichukia kwani nilitaka kumshuhudia yule baba akila kile chakula nikamuuliza kuwa kwanini asingewatuma wakina Neema na Chaurembo? Mama akaniambia kuwa nao wametoka kidogo, wamepeleka maziwa kwa wateja wao ikabidi nisibishe sana. Niliamua kwenda aliponituma mama huku nikiamini kuwa nitakaporudi lazima nitapata habari ya msiba tu.
Nilipotoka kwa fundi na nguo ya mama kwenye mfuko, nilimkuta Neema akiwa nje amekaa huku akisononeka nikajua lazima mambo yameharibika tayari nikamuuliza mbona yupo nje akaniambia kuwa njaa inamuuma, nikamshangaa wakati chakula kipo ndani nikajiuliza labda anangoja baba yake ale kwanza.
Nikamuuliza kwanini asile, alinijibu
"Mama kaniambia nisile hadi niende kuchukua mahindi kule bondeni wakati baba amekataa kula kile chakula alichoandaliwa nae amesema ameshiba, baada ya kuniachia mimi na Chaurembo tule kile chakula eti yeye ndio kaamua kula na Chaurembo sijui kwavile mimi sio mwanae wa......"
Kabla hajamalizia ile sentensi nilihisi kama moyo wangu umeripuka, niliangusha ule mfuko pale pale na kukimbilia ndani.
Nilimkuta mama akiwa chini huku akitapatapa, mdogo wangu Chaurembo ndio hakutamanika kabisa pale chini. Nilimuita Neema kwa nguvu na kumwambia alete maziwa ili tujaribu kuwanusuru ila ilisemekana kuwa maziwa yote yaliuzwa na yaliyobaki mama aliyaficha, hali ilikuwa mbaya sana ila Neema alienda kuomba maziwa kwa majirani huku tukijaribu kutafuta uwezekano wa kuwawahisha hospitali. Kwakweli ilikuwa kazi ngumu kwani hata maziwa aliyoleta Neema nayo hayakusaidia na kufika nao hospitali walikuwa tayari marehemu.
Hili lilikuwa ni pigo kubwa sana kwangu hata pale msiba ulipoisha bado nilikuwa na pigo kubwa sana.
Nilijikuta nikimchukia Maria kupita maelezo kamavile yeye ndiye aliyeshauri kuwa niue.
Ila sikuachana nae kwavile bado nilikuwa nampenda.
Ila moyoni nilikuwa namuwazia mawazo mabaya sana Maria bila ya yeye kujua laiti kama angejua basi angejiepusha na mimi mapema sana.
Nilikuwa mtu wa mawazo tu na kumuona kwangu bamdogo nikaona kama akinizidishia maumivu tu ya kuendelea kumkumbuka mama yangu.
Nikafanya mpango wa kummaliza bamdogo ila bado ilishindikana.
Kipindi hicho nyumbani kulikuwa na mgogoro wa dada yangu Rehema na mwanaume ambaye amezaa nae, wakati tukirumbana hadi kufikia kugawana wala watoto na yule mwanaume kufukuzwa pale kijijini kumbe Maria nae alikuwa amejifungua mtoto wangu ila alikaa kimya bila hata ya kuniambia.
Bado nilikuwa na uchungu juu ya bamdogo na kipindi hicho baba na bamdogo walianza kupatana patana tena, na mimi nikaitumia nafasi hiyo kummaliza bamdogo.
Nikaweka mtego shambani kwa bamdogo kwa bahati mbaya baba na bamdogo walienda pamoja kwenye lile shamba na ule mtego ukamvaa baba yangu na kummaliza papo hapo.
Ukoo mzima ukamchukia bamdogo na kumwambia kuwa ndio chanzo, bamdogo akafukuzwa pale kijijini na akaondoka na binti yake Neema kwenda kuanza maisha mengine kabisa.
Roho iliniuma kwa kusababisha kifo cha baba na mama na mdogo wangu ila yote ni katika harakati za kummaliza bamdogo.
Nikawa kama vile mtu aliyechanganyikiwa, nikapotea nyumbani na kuzamia Mombasa, nilikaa huko kwa miaka mitano huku nikipanga namna ya kummaliza bamdogo.
Niliporudi bado sikuwa na amani ya moyo, nilimkuta dada ameolewa ila akiwa mjamzito tena na katoto kake ka kwanza kakiwa kamekua kua vya kutosha.
Nikapata wazo la kumtembelea Maria, nikamkuta nae akiwa na mtoto halafu ni mjamzito.
Nilichukia sana, nilipomuuliza alidai kuwa yule mtoto ni wangu ila hakuniambia kwavile nilipotea ila ule ujauzito kuna mwanaume amempata, kuja kufatilia nikagundua kuwa huyo mwanaume ndio yule aliyezaa na dada yangu mtoto wa kwanza, roho ikaniuma sana kuona yule mwanaume kaona haitoshi kuniharibia dada yangu na sasa amehamia kwa mchumba wangu.
Nikaapa kuwa lazima nije kulipa kisasi.
Ila labla ya kuanza mapinduzi ya kisasi niliamua kwanza kuondoka na wale watoto wa kiume ili nikawafunze kazi huko Mombasa.
Dada nikamdanganya kuwa natoka na mwanae mara moja, kisha nikaenda nae hadi kijiji cha kina Maria na kumchukua mwanangu huku nikidai kuwa naenda kutembea nae tu.
Kwakweli watoto hawa wawili niliweza kuwatofautisha kwa majina tu ukizingatia sijaishi nao.
Niliondoka na watoto wale hadi Mombasa, nikakaa huko kwa siku chache kisha nikawakabidhi kwa rafiki yangu na mimi kurudi tena kijijini, lengo lilikuwa ni kumshawishi dada yangu ili niende nae Mombasa ila ile kurudi tu kijijini dada yangu akaanza kunishambulia kwa maneno na kunidai mtoto wake ila alikuwa ameshajifungua na ana mtoto mchanga, nikaachana nae pale na kuelekea kwa Maria kwani nilijua kuwa na yeye lazima atakuwa amejifungua, moyoni nikajisemea kuwa lazima nikammalize huyo mwanaume.
Nilipofika kwa Maria naye alianza kunidai mtoto wake na yule mwanaume sikumuona, nikaona Maria ananiletea longolongo tu hivyo hata sikumchelewesha, nilichukua kisu na kumchoma nacho tumboni yani sikuwa na huruma kabisa kisha nikaondoka.
Kurudi tena kwa dada naye akawa anadai mtoto wake namwambia yuko Mombasa hataki kunielewa anamtaka mwanae halafu akaniitia polisi.
Nilikuwa kama mtu niliyechanganyikiwa, nilijikuta nikimnyanyua yule mtoto mchanga wa dada na kumuinua juu kisha kumbamiza chini kama mzigo, na alilia mlio mmoja tu kisha ikawa kimya.
Wale mapolisi wakaona wanikamate kinguvu ili kuepusha majanga mengine.
Nikapelekwa jela ila mambo ambayo nilikuwa nafanya humo ikaonekana kama vile sina akili nzuri, hivyo wakanipeleka jela ya vichaa na kwakweli nilikuwa kichaa kwa kipindi hiko kwani nilifanya mambo ya ajabu hadi ya kujishtukia.
Nilikaa jela kwa miaka mitano kasoro, badae nikaanza kutafuta namna ya kutoroka pale gerezani.
Nilipopata nafasi sikuangalia nyuma nilitoroka moja kwa moja na kukimbilia kwa bamdogo kule ambako alikuwa amehamia tangia kifo cha baba, ni mimi tu niliyepajua kwa bamdogo kwakuwa ndugu zake na ukoo mzima walimtenga nami nikaona kuwa kule nitakuwa salama zaidi.
Nilimkuta Neema akiwa na mabinti wawili kwa kuwakadilia miaka huyu mkubwa alikuwa na miaka nane na mdogo miaka minne.
Pale kwa bamdogo hapakuwa na tatizo kwani Neema alinihudumia vizuri sana tatizo lilikuwa kwa huyu binti yake mkubwa huyu wa kuitwa Fausta alikuwa na nyodo sana halafu alikuwa ananidharau sana mara nikiwekewa chakula aseme kuwa mimi nakula sana, nikimtuma kitu anakataa kwakweli huyu binti alikuwa ananikera sana na kama ingekuwa amri yangu basi ningekimaliza muda mrefu sana.
Roho iliniuma kwa kusodolewa na binti mdogo kama Fausta ila nikawa navumilia tu, kitu kibaya ni kuwa Neema hakuweza kumgombeza mtoto wake huyo ingawa alikuwa anaona mambo ya ajabu aliyokuwa ananifanyia, ukimwambia anajibu ni utoto tu huo msamehe bure dah huyu mtoto nilimchukia sana.
Nilikaa kwa bamdogo miaka miwili kasoro hadi pale Fausta ambaye anatetewa na mama yake kuwa ni utoto alipokwenda kunishtaki polisi kuwa mimi ni muharifu, nilishangaa mapolisi kuja na kunikamata.
Nilichukia sana na kuapa kuwa laziama nimmalize yule mtoto nikitoka jela.
Safari hii nilikaa tena jela kwa miaka mitatu hadi pale nilipopata nafasi ya kutoroka ila niliwapa mapolisi wawili sumu na nilipotoka jela safari yangu ilikuwa ni kwa bamdogo kwa lengo la kummaliza Fausta.
Kufika pale nilimkuta mama yao ndani, nilipomuuliza alikataa kunitajia Fausta alipo hata nilipojaribu kumtishia bado hakutaja, nikaona ananiwekea usiku tu nikachukua kisu na kumchoma nacho habari yake ikaisha.
Wakati natoka nikakutana na bamdogo mlangoni.
Bila kuchelewesha muda nilimchoma na kisu ili kupoteza ushahidi kisha nikaingia chumbani na kusomba pesa zote milizozikuta na kuondoka nazo, zikaniwezesha kusafiri na kwenda tena Mombasa.
Kufika kule niliwakuta watoto wamekua kweli ila bado waliwataka mama zao nikawaambia kuwa mama zao wamekufa ila hawakutaka kukubali, Maiko alipoona nimebadilika akatulia ila Juma alijifanya mbishi na kuendelea kunisumbua sana, sikutaka kero hivyobasi nikamfyekelea mbali huku nikijua nimemfyeka mtoto wa dada yangu kumbe nimemfyeka mwanangu na kumuacha mtoto wa dada yangu dah Maiko ni mshenzi sana.
Nikawa nafanya biashara za magendo na watu wa kule ila kila leo biashara za magendo zinatanuka hadi kufikia kuuza viungo vya watu, nikasafiri nchi nyingi kupeleka viungo hivyo na nikawa na pesa nyingi pia ni hapo nilipoamua kulipa kisasi kwa yeyote niliyejisikia kummaliza, hata oda ya kummaliza mzee Ayubu niliitoa mimi kwani alitembea na mpenzi wangu.
Katika kisasi changu nimesumbuliwa na kiumbe mmoja tu huyu wa kuitwa Fausta. Mungu akupe maisha marefu ila ukweli ni kwamba nakuchukia sana na ningekumaliza siku nyingi sana wewe.
Najua mpo mtakaoumizwa na hii barua ila ndio hivyo yalishatokea ya kutokea.
Na katika watu walioniharibia mpango wangu wa kuwa bilionea kwasasa ni huyu wa kuitwa Patrick, nakuchukia sana wewe kijana. Umeharibu maisha yangu sana.
Ila samahanini kwa yote niliyowakosea, ni mimi MASHAKA"
Kila mmoja alijikuta akipumua kwa nguvu baada ya ile barua.
Kila mmoja alikuwa kimya kabisa, Deborah akauvunja ukimya ule.
DEBORAH: Jamani kila mmoja nadhani amesikia maelezo ya hiyo barua.
REHEMA: Yani nimeumizwa sana kuona mdogo wangu alifanya vitendo vya makusudi kiasi hiko. Ameharibu ukoo mzima.
DEBORAH: Ni kweli ila kinachotakiwa ni kuvunja hiyo laana kwenye ukoo wenu.
REHEMA: Kitu kingine ni ndoa ya Pamela na Adamu, nyie wawili mlikosea sana kuoana ndugu sasa watoto wenu mtawaweka wapi?
Amina alikuwa ameinama na kutoa machozi ukizingatia kifo cha mtoto wake Tulo halafu na barua iliyosomwa ilimuumiza sana, naye akaamua kusema.
AMINA: Jamani huyo Maria ndio mama yangu mzazi ambaye nilipewa habari kuwa aliuliwa kikatili kumbe aliyemuua ni huyu jamaa!!
Amina alisikitika sana na wakaamua kumbembeleza.
DEBORAH: Mmh!! Na huyo mzee Ayubu nae ilikuwaje kuzaa na huyu na huyu na huyu?
REHEMA: Ngoja nimtetee kwa hilo, kwanza kabisa alizaa na mimi ila kwetu wakamkataa na tukagawana watoto, pili akazaa na Neema nadhani bamdogo pia alimkataa kwakuwa bado anasheria za kule, tatu akaenda kuzaa na huyo Maria ambaye aliuliwa na Mashaka kwakweli hakuwa na la kufanya hapo jamani. Ila ninachomlaumu ni kuwa alipoona kijiji hakimtaki angehama kabisa na asingethubutu kuzaa na mwanamke mwingine yeyote wa karibu ila nadhani kifo cha Maria ndio kilichomkimbiza Morogoro, pole sana mzee Ayubu.
Ikabidi wajadili hatma ya Tusa na Patrick, safari hii Patrick bila kinyongo akaamua kuachana na Tusa kwa amani tu ili kuepusha mabalaa mengine katika ukoo.
PATRICK: Kwa hiyari yangu na kwa amani kabisa naamua kuachana na Tusa ila Deborah ataendelea kuwa mama yangu siku zote za maisha yangu.
Kauli ile ilimfurahisha sana Deborah kwani aliona swala la Patrick kuachana na Tusa ni swala zuri sana na pia ilikuwa furaha kwa Sele aliyempenda Tusa kupitiliza hata Tusa nae alifurahi ila kilichomuuma ni kuwa kwanini Patrick atokee kuwa kaka yake.
Adamu na Pamela waliumia kitu kimoja kikubwa nacho ni kukataliwa na Patrick.
Marium bado alikuwa na swali kwa mwanae kuwa kwanini hawezi kuachana na Tusa.
MARIUM: Hivi mwanangu Sele huyu mwanamke alikupa nini hadi hutaki kumuacha?
SELE: Mama, mimi na Tusa tulikula kiapo cha milele najua Tusa hawezi kuishi na mwanaume yeyote ila mimi. Nampenda sana naye ananipenda sana.
PATRICK: Ni kweli kabisa asemavyo Sele, Tusa hawezi kuishi na mwanaume yeyote yule. Kwa jinsi ambavyo nimeishi na Tusa na mambo mengi niliyomfanyia ni wazi kuwa Tusa hawezi kuishi na mwanaume yeyote zaidi ya huyo Sele.
DEBORAH: Kama ndio hivyo tuwaache waoane tu maana wanapendana, ingekuwa mwanaume mwingine angemuacha Tusa kitambo kwa mapito aliyopitia ila kwakuwa Sele ana mapenzi ya dhati basi na amuoe Tusa.
PATRICK: Sele anapaswa kuigwa kwenye jamii, na nitasimamia harusi yao yote.
Tusa alimshangaa sana Patrick kwani hakuwazia kuwa ipo siku Patrick atakuwa ni mwanaume wa kutamka maneno mazuri kiasi kile.
Mwita nae aliungana na ndugu zake na kuamua kuvunja laana zote ambazo zimeikumba hiyo familia.
Harusi ikapangwa kisha Sele na Tusa wakafunga ndoa.
Kila mmoja aliwatakia maisha marefu Sele na Tusa, kisha Deborah akamwambia Sele.
DEBORAH: Natumaini utakuwa mume mwema, nawatakia maisha marefu na usithubutu kuwa kama MUME GAIDI, pesa tafuta kwa njia halali na Mungu atakuwezesha.
Waliyafurahia yale mahusia na kupiga makofi.
Baada ya hapo kikafanyika kikao cha mwisho cha familia na hapo ndipo Yuda nae akatangaza kumuoa Tina na hukuna aliyepinga.
Deborah aliamua kuwaaga na ndugu zake kuwa wanataka kurudi kwao Mwanza ila kabla ya kuondoka Patrick aliweka sherehe ya kuagana na familia ya kina Tusa.
Katika sherehe hiyo alimsimamisha Deborah na kuongea maneno haya,
"Huyu mwanamke mnayemuona mbele yenu, ndiye mama yangu, chakula changu, furaha yangu, amani yangu na kila kitu katika maisha yangu. Nampenda sana huyu mama, sitamtupa wala kumtenga hadi naingia kaburini"
Kisha akamuangalia kwa karibu Deborah na kumwambia,
"Nakupenda sana mama"
Akamkumbatia kwa furaha na kesho yake wakasafiri kurudi Mwanza wakiwa na furaha iliyopitiliza.
Pamela aliumia sana na kujiona kuwa na mkosi mkubwa sana maishani mwake. Kitendo cha kumtupa mtoto kilimuumiza sana.
Walipokuwa Mwanza, siku hiyo Patrick alilala usiku na kutokewa na mzimu wa mzee Ayubu kisha ukampungia mkono kama ishara ya kumuaga tena huku akitabasamu.
❤
❤
❤
MWISHO
❤
❤
❤
 
Maoni yenu na mawazo yenu wadau ni ya muhimu sana.
Asanteni kwa ushirikiano wenu mwanzo hadi mwisho.

Imeletwa kwenu na BURE SERIES
 
Back
Top Bottom