SEHEMU YA TISA
Kwenye maktaba ya jiji kulikuwa na taarifa nzuri na mbaya. Kwenye kitabu cha namba za simu watu walioitwa Jacob walikuwa wengi. Wengine kutoka Manhattan, Bronx, Brooklyn, Queens na kila sehemu. Hiyo ilikuwa taarifa nzuri.
Taarifa mbaya ni kwamba hakukuwa na namba wala jina la mpelelezi wa kujitegemea anayeitwa Costello. Reacher aliguna, lakini hakushangaa. Ingeshangaza sana kama angekuta Costello Investigation: Tunashughulika na kutafuta watu waliopotea.
Namba nyingi za wapelelezi zilikuwa na majina yanayofanana huku wengi wao wakishindania herufi A ili wakae juu zaidi kwenye kitabu. Reacher alikivuta kitabu karibu na kuanza kunakili namba kumi na tano za askari wa idara ya polisi New York. Alikaa muda kidogo kutafakari kama ndiyo uamuzi sahihi. Aliporidhika alianza safari kutafuta sanduku la kupiga simu. Alitoa pesa na kidaftari kilichokuwa na namba na kuanza kupiga simu moja baada ya nyingine.
Bahati yake ilikuwa kwa mtu wa nne. Watu watatu wa mwanzo hawakuwa watu wake. Simu ya nne ilianza kama simu zingine zote. Mlio wa kuita halafu sauti za mtu kuishikashika na kupokelewa.
"Namtafuta mtu anaitwa Costello," Reacher alisema. "Amestaafu na sasa anafanya kazi ya upelelezi. Umri wake ni kati ya miaka 60."
"Sawa, Wewe ni nani?" Sauti ya upande wa pili ilihoji. Ilikuwa inafanana sana na sauti ya Costello. Reacher alihisi ni Costello mwenyewe.
"Naitwa Carter," Reacher alidanganya. "Kama jina la Rais tu."
"Unataka nini kwa Costello, bwana Carter.?"
"Nina kazi nataka tufanye, lakini nimetafuta namba yake bila mafanikio."
"Hiyo ni kwasababu namba zake hazipo kwenye hivyo vitabu."
"Kwahivyo unamfahamu?"
"Namfahamu? Mimi ninamjua."
"Ofisi yake ipo wapi kwani?"
"Ipo Greenwich avenue kama nakumbuka vizuri."
"Namba ya mtaa?"
"Sina."
"Namba ya simu?"
"Sina."
Reacher alishangaa kwanini watu wanasema wanawajua watu ilihali hawamjui. Lakini hakutia neno.
"Kuna mwanamke anaitwa Jacob, unamjua?"
"Hapana, sijawahi kusikia hilo jina."
"OK, Ahsante kwa msaada wako." Reacher alisema.
"Poa."
Reacher alikata simu na kurudi tena maktaba ambako alichukua kitabu kumtafuta mtu wa jina la Costello kwenye orodha ya namba za watu wa Greenwich Avenue. Hilo jina halikuwepo. Aliingia mtaani tena.
Greenwich Avenue ni mtaa mdogo uliopo kusini mashariki mwa Fourteenth street. Unazungukwa na ofisi ndogondogo nyingi. Reacher alifika barabara kuu na kuanzia ofisi za kaskazini. Hakupata kitu. Aliporudi majengo ya kusini aliona alichokuwa anakitafuta. Ulikuwa ni mlango wenye kibao kilichoandikwa Costello kwa juu. Mlango ulikuwa umepakwa rangi nyeusi na ulikuwa wazi.
Ndani kulikuwa na korido ndefu ambayo ukuta wake ulikuwa umeandikwa kila jina la ofisi na kazi yake. Reacher alisoma na chumba namba tano ndicho kilikuwa ofisi ya Costello.
Reacher alianza kupanda ngazi kuelekea kilipokuwa chumba. Mlango ulikuwa umepakwa rangi ya kung'aa na ulikuwa wazi. Haukuwa umefunguka sana, ila ulikuwa wazi. Reacher aliusukuma kwa mguu wake na wenyewe ukafunguka. Kilichokuwa mbele yake kilikuwa chumba cha mapokezi. Kilikuwa kimepakwa rangi ya kijivu mpauko. Meza ya katibu muhtasi ilikuwa hapo ikiwa na simu pamoja na kompyuta juu yake.
Chumba hiki hakikuwa na mtu. Lakini pia kilikuwa na ukimya usio wa kawaida. Reacher aliingia ndani na kuufunga mlango nyuma yake kwa kutumia mguu wake tena. Aliingia na kuufuata mlango wa kuingia ofisi ya ndani. Hapo akalivuta shati lake na kufunika kiganja cha mkono wake ndipo akashika kitasa kufungua. Kama askari watatafuta alama za vidole!
Kilikuwa chumba cha Costello. Hilo lilithibitishwa na picha zilizokuwa zimening'inizwa ukutani. Zilimuonesha Costello akiwa mwembamba alipokuwa mdogo na kadri alivyokuwa ndivyo alivyozidi kunenepa. Mpangilio wa zile picha ilikuwa kama tangazo la mtu aliyeenda Gym kupunguza mwili likiwa limegeuzwa - Kutoka wembamba kwenda unene.
Reacher alitoka nje kurudi chumba cha mapokezi. Kulikuwa na harufu ya utuli iliyoning'inia angani. Alienda hadi kwenye meza na kukuta mkoba ukiwa umefunguliwa zipu. Alichukua penseli yake na kupekenyua. Kulikuwa na mkusanyiko wa vitu ambavyo wanawake hubeba kwenye pochi zao.
Kioo cha kompyta kilikuwa kinawaka. Reacher alibonyeza kielekezi kwa penseli yake. Hapo kioo kikafunguka na kuonesha maneno yakiwa hayajamaliza kuandikwa - kama mtu alikuwa anaandika halafu akapata dharura akaachia njiani. Ghafla picha ya mwili wa Costello kule Key West ikamuijia Reacher kichwani, halafu mkoba wa mwanamke ukiwa wazi ilihali wanawake huwa hawaachi mikoba yao wazi, milango iliyokuwa wazi hapo ofisini na zaidi maneno ambayo hayakuwa yamemaliza kuandikwa. Mwili ukamtetemeka.
Aliitumia penseli yake kukata faili lililokuwa linaandikwa. Kompyuta ikamuuliza kama anataka kulihifadhi au la. Alibonyeza 'no'. Alifungua file manager kutafuta taarifa za malipo. Alijua Costello ni mtu makini aliyeendesha biashara kwa umakini hivyo lazima angekuwa na taarifa za malipo humu. Alianza kukadiria ingekuwa zimepita siku ngapi kabla ya Costello kujua yupo West Key. Jibu lilikuwa rahisi - Siku ya kwanza ya kupigiwa simu na kupewa maelekezo na kulipwa hela ya kuanzia. Siku ya pili kufikiria. Siku tatu baadae kutafuta taarifa. Taarifa za mwanajeshi mstaafu zingechukua muda hadi kupatikana na benki lazima zingemsubirisha Costello kwa siku kadhaa kabla ya kumpatia taarifa za mteja wao. Hivyo ingekuwa ni kati ya siku kumi zilizopita. Hivyo mtu wake alikuwa kwenye orodha ya watu wa siku kumi zilizopita, aliwaza.
Alifungua faili na kuanza kuanza kutafuta jina la Jacob kwanza. Halikuwepo. Majina mengi ya Costello yalikuwa yanaandikwa kwa ufupisho tu. Akaamua kuangalia tarehe. Aliona taarifa moja ya siku tisa zilizopita. Ilikuwa imeandikwa Sgr&t-09.
Hii ilimaanisha Costello alikuwa anafanya mambo kwa kasi kuliko Reacher alivyomchukulia au ni katibu muhtasi wake alikuwa mzembe. Aliibonyeza hiyo taarifa ya malipo likafunguka jedwali dogo linaloonesha dola elfu moja zimelipwa kwaajili ya kutafuta mtu anayeaminika amepotea. Anuani iliyotuma pesa ilikuwepo, lakini hakukuwa na namba za simu.
Reacher alilifunga hilo faili akafungua databezi. Akaandika Sgr&t halafu akabofya enter. Hapo likafunguka jedwali lingine. Hili lilionesha anuani ya mlipaji, namba za simu, faksi na barua pepe.
Alilizungusha tena shati lake kuziba viganja vyake na kunyanyua simu ya mezani iliyokuwepo hapo. Simu ilianza kuita halafu ikapokelewa.
"Spencer Gutman," Sauti ya upande wa pili wa simu ilisema. "Sijui nikusaidie nini?"
"Naomba kuongea na Mrs. Jacob tafadhali." Reacher alijibu.
"Nipe dakika moja," Yule mtu alijibu.
Ukaja mziki kwenye spika za simu halafu ghafla sauti ya yule mtu ikarudi tena.
"Mrs. Jacob, tafadhali." Reacher alisema.
"Ametoka kuelekea Garrison na sifahamu atarudi saa ngapi."
"Mwanamke inaonekana anatoka asubuhi sana nyumbani kwake, sio?"
"Mwanamke?" Yule mtu aliuliza na kuongeza, "Ni mwanaume sio mwanamke."
Reacher alitulia kidogo na ili asishtukiwe alikuwa hamjui Mrs. Jacob aliendelea kuongea, "Namaanisha huyo mwanaume. Nimechanganya tu kuo...."
"Usijali," Ile sauti ilisema. "Mimi ndiye nililichapa jina hivyo kwa maksudi."
Alipomaliza alimsomea anuani ya kumpata Mrs. Jacob huko Garrison.
"Ningekushauri uwahi," Yule mwanaume alisema.
"Sawa! Nitawahi." Reacher alijibu na kuishusha simu chini.
Alinyanyuka kutoka kwenye kiti na kufunga lile jedwali lililokuwa kwenye kioo cha kompyuta. Alitoka nje kuingia mtaani kumfuata Mrs. Jacob ambaye hakuwa mwanamke bali mwanaume!
SEHEMU YA KUMI