SEHEMU YA KUMI NA MBILI
"Mambo, Reacher." Alisema kwa sauti ya chini.
Reacher alimtazama. Alikuwa anamfahamu ni nani. Na yeye alikuwa anamfahamu Reacher ni nani. Ilimwijia kama filamu fupi kuelezea kumbukumbu za miaka kumi na tano iliyokuwa imepita. Msichana mdogo aliyemfahamu sasa alikuwa amekuwa mwanamke mkubwa wa kuvutia ndani ya muda wa sekunde chache tu. Garber, ndilo lilikuwa jina kwenye sanduku la barua. Leon Garber kwa muda mrefu ndiye alikuwa Kamanda wa Reacher. Aliyakumbuka mahusiano waliyokuwa nayo kuanzia mara ya kwanza walipokutana kwenye jioni moja walipokuwa wakichoma mishkaki huko Ufilipino. Kwa mbali kulikuwa na msichana mdogo akiwa anachezacheza. Jodie, Binti yake Garber. Mtoto wake pekee. Nuru ya maisha yake. Huyo ndiye alikuwa Jodie Garber, Miaka kumi na tano sasa ilikuwa imepita. Alikuwa amekuwa msichana mkubwa na tafsiri ya neno mrembo. Na sasa alikuwa amesimama kwenye ngazi akisema alikuwa anamsubiria Reacher.
Reacher aliinua macho kuitazama ile kadamnasi ya wa waombolezaji.
"Habari, Reacher?" Jodie alisema tena.
Sauti yake ilikuwa ya chini na iliyopooza. Alikuwa ni mwenye huzuni kama tukio lililokuwapo hapo.
"Nzuri tu, Jodie." Reacher alisema.
Halafu akataka kuuliza aliyefariki alikuwa ni nani. Lakini hakupata namna ambayo ataliweka swali lake bila kuonekana ni la kipuuzi, au la kijinga. Jodie alimuona na kama aliyesoma mawazo ya Reacher alisema, "Baba."
"Lini?" Reacher aliuliza.
"Siku tano zilizopita," Jodie alijibu. "Alikuwa ameugua kwa muda mrefu, lakini ilitokea ghafla sana mwisho wa siku."
Reacher alitikisa kichwa taratibu. "Pole sana," Alisema.
Reacher aliinua uso na kuutazama mto ambao ulikuwa mbele yao na nyuma ya migongo ya wale waombolezaji. Karibu nyuso za wote aliowaona ziligeuka kuwa nyuso za Garber. Mwanaume mfupi na mkakamavu. Uso wake ulipambwa na tabasamu muda wote hivyo iliwafanya watu washindwe kujua kama anafuraha au amekasirika. Kiongozi hodari. Aliyekuwa shupavu kimwili na kiakili. Mtu ambaye ndiye alikuwa mshauri wa Reacher. Mlinzi wake. Alikuwa amefanya mambo ambayo hata yangeweza kuhatarisha uhai wake ili kumuokoa Reacher.
"Pole sana, Jodie." Reacher alisema tena.
Jodie alitikisa kichwa kukubali pole ya Reacher bila kusema neno neno lolote.
"Inaniwia vigumu sana kuamini," Reacher alisema. "Nilionana naye mwaka jana na afya yake ilionekana ni njema. Ilikuwaje akaumwa?"
Jodie hakusema kitu.
"Lakini alikuwa mtu shupavu." Reacher aliongeza.
Jodie alitikisa kichwa kukubali. "Ni kweli. Alikuwa shupavu na mbishi hata kwa maradhi."
"Na sio kwamba alikuwa mzee sana." Reacher alisema.
"Miaka sitini na nne tu."
"Nini haswaa kilichotokoea?"
"Maradhi ya moyo," Jodie alisema. "Yalimpata na kumtafuna mwisho wa siku. Unakumbuka namna alivyokuwa akisema hana shida yeyote ya moyo."
"Ninakumbuka. Alikuwa na moyo mweupe ndiyo."
"Nililigundua hilo mama alipofariki," Jodie alisema. "Mimi na baba tulikuwa marafiki kwa zaidi ya miaka kumi na nilimpenda kuliko kitu chochote."
"Nilimpenda pia kama vile alikuwa ni baba yangu kuliko alivyokuwa baba yako." Reacher alisema.
Jodie alitikisa kichwa, "Yeye pia alikuwa akikuongelea kila siku."
Reacher alitazama pembeni. Alikuwa kageuka bubu ghafla. Lakini ukweli mmoja ulikuwa wazi kichwani mwake. Alikuwa amefikia hatua ya umri ambayo watu wake wa karibu wengi aliokuwa anawafahamu walikuwa wanakufa. Mama yake alikuwa amekufa. Baba yake alikuwa hayupo hai. Kaka yake pia. Na mtu ambaye angeweza kuchukua nafasi zao kama ndugu wa karibu alikuwa amefariki siku tano zilizopita.
"Alipata mshtuko wa moyo miezi sita iliyopita," Jodie alieleza. "Halafu kama muujiza akawa amepona na afya yake ikaleta matumaini. Lakini kumbe alikuwa anatafunwa polepole ndani kwa ndani."
"Pole sana, Jodie." Reacher alisema kwa mara ya tatu.
Jodie alimgeukia na kuushika mkono wake.
"Isikuhuzunishe sana. Naamini baba huku aliko ana faraja zaidi kuliko ambavyo angeendelea kuwa hai."
Reacher alitikisa kichwa kwa huzuni.
"Njoo uungane na waombolezaji wengine. Naamini kunao baadhi unaoweza kuwa unawafahamu." Jodie alisema.
"Sidhani kama mavazi yangu yananiruhusu," Reacher alisema. "Kiukweli najisikia vibaya na aibu. Naomba niondoke tu."
"Haijalishi," Jodie alimwambia. "Unadhani baba angejali kuhusu mavazi yako?"
Picha ya Garber akiwa amevaa nguo zake za kujikunjakunja na kofia kubwa ilimjia Reacher kichwani. Ladha ya mavazi ya Garber ilikuwa kichekesho cha aina yake. Miaka yote kumi na tatu ambayo Reacher alifanya naye kazi hakuwahi kuona mtu asiyejali kuhusu mavazi kama Garber. Alitabasamu kidogo.
"Nadhani asingejali," Reacher alisema.
Jodie alimuongoza hadi umati wa wale waombolezaji ulipokuwepo. Kulikuwa na watu sita tu aliowafahamu kati ya mamia waliokuwepo hapo. Lakini nyuma ya ubongo wake alikuwa na hakika katika wakati mmoja au mwingine wote alikuwa ameshiriki nao kwenye kazi ya hapa na pale. Jeshi ni kama timu! Unaweza kufanya kazi na mtu bila kumfahamu. Alibadilishana mikono ya salamu hapa na pale huku akijaribu kukariri majina aliyokuwa akiambiwa bila mafanikio. Mengi yalikuwa yanaingilia sikio moja na kutokea sikio la pili. Halafu ule mshangao aliouwa ameutengeneza alipotokeza mara ya kwanza ukaisha. Watu wakasahau nguo zake chafu na kuendelea na hamsini zao. Jodie alikuwa bado ameushika mkono wa Reacher. Ulikuwa mlaini kama wa mtoto mdogo kwenye ngozi ya Reacher.
"Kuna mtu ninamtafuta," Reacher alisema. "Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyofanya nifike hapa."
"Ninafahamu," Jodie alijibu. "Unamtafuta Mrs. Jacob, sio?"
Reacher alitikisa kichwa kukubali. "Yupo hapa?"
"Mimi ndiye Mrs. Jacob," Jodie alijibu.
Wale wanaume wawili waliokuwa kwenye Tahoe waliitoa gari lao kutoka kwenye maegesho. Walitelezea nje kidogo ya eneo hilo. Walipofika mahali salama, Dereva alitoa simu na kuandika namba f'lani kabla ya kubonyeza kitufe cha kupiga. Gari likatawaliwa na ukimya. Halafu ile simu ikapokelewa na mtu aliyekuwa takribani maili sitini kusini akiwa kwenye ghorofa namba themanini na nane.
"Kuna tatizo, boss," Dereva alisema. "Kuna shughuli inaendelea hapa, inaweza ikawa msiba au kitu cha namna hiyo. Kuna zaidi ya watu miamoja wanaozungukazunguka. Hakuna nafasi wa kumkamata huyu Mrs. Jacob. Mbaya zaidi tunashindwa hata kumtambua ni yupi. Kuna wanawake lukuki hapa, anaweza kuwa yeyote kati yao."
Sauti ya Hobie ilisikika kwenye spika ya simu. "Na?"
"Yule mlinzi wa bar wa kule keys amefika hapa kwa Taxi dakika kumi baada ya sisi na ameungana na watu wa msiba."
Spika ya simu ikaunguruma. Hakukuwa na jibu.
"Kwahivyo tunafanyaje?"
"Endeleeni na mpango," Sauti ya Hobie ilisema. "Mnaweza kuliegesha gari na kutafuta sehemu ya kujificha kwa muda. Subirini hapo hadi kila aliyepo aondoke. Hiyo nyumba ni ya Mrs. Jacob kwa taarifa nilizonazo. Kwahivyo kila mtu ataondoka, lakini yeye ndiye atakayebaki. Msirudi bila Mrs. Jacob!"
"Na huyu jamaa wa Keys?"
"Kama ataondoka, mwacheni aende zake. Asipoondoka mfuteni. Lakini hakikisha huyo Mrs. Jacob mnamleta hadi kwangu."
SEHEMU YA KUMI NA TATU