SEHEMU YA KUMI NA TISA
Hook Hobie alikuwa amekaa peke yake ofisini kwake ghorofa namba themanini na nane akisikiliza ukimya uliokuwamo kwenye chumba hicho. Alikuwa akitafakari sana huku akibadilisha mawazo. Yeye mwenyewe alikuwa ni mtu anayeweza kubadilikabadilika kama kinyonga kutokana na mazingira na alijivunia hilo. Alikuwa amejifunza kusikiliza na kuelewa na kubadilika.
Alienda Veitnam bila uhakika wa uwezo wake katika uwanja wa vita. Zaidi ya yote hakuwa na uhakika kama atarudi tena Marekani akiwa hai kwa sababu kipindi hicho alikuwa mdogo sana. Lakini pia alikuwa ametokea mtaa ambao haukuwa na mbele wala nyuma katika kumpa mtu msingi wa maisha ya kujiamini.
Veitnam ikambadilisha. Ingeweza kumvunjavunja . Ilikuwa imewavunja watu wengi na kuharibu maisha yao. Watu ambao alikuwa akiwaona kwa macho yake, sio kusimuliwa. Na hawakuwa vijana. Walikuwa ni watu wakubwa wenye uzoefu kwenye uwanja wa vita kwa miaka mingi. 'Nam iliwaangukia kama mzigo mzito na kuwavunjavunja vipandevipande baadhi na wengine kuwakomaza.
Yeye hakuvunjika. Aliangalia na akabadilika na akazoea. Alisikiliza na kuelewa. Ilikuwa rahisi. Alikuwa aina ya mtu ambaye hakuwa amewahi kushuhudia kitu kikiwa kimekufa mbele yake isipokuwa mende na sungura waliogongwa na gari barabarani karibu na nyumbani kwao. Lakini siku ya kwanza tu alipotua nchi ya 'Nam aliona miili ya maiti nane za raia wa marekani wakiwa wamekatwakatwa vipande na kuwa vipisi vya viuongo vya binadamu ishirini na tisa. Huku mkono, pale kichwa na kule miguu. Wenzake alioripoti nao siku moja walikuwa wanatapika hovyo na kuguna kwa uoga. Lakini yeye alikuwa anatazama zile maiti tu.
Akaanza kufanya biashara. Kila mtu alikuwa anahitaji kitu. Kila mtu alikuwa anapiga kelele kuhusu vitu alivyokuwa anahitaji. Na ilikuwa kazi rahisi sana. Mtaji pekee uliohitajika ni kusikiliza tu. Hapa kulikuwa na bwana asiyevuta sigara lakini anakunywa bia, kule kulikuwa na bwana mwingine anayevuta sigara, lakini hatumii bia. Chukua sigara kutoka kwa mnywaji mpeleke mvutaji na chukua bia kutoka kwa mvutaji mpelekee mnywaji. Ukiwa kama dalali kuna asilimia f'lani ya mzigo utabaki nayo kama mshahara wa kazi yako na ndivyo utakavyopata faida na vitu unavyohitaji. Ilikuwa ni rahisi sana kiasi kwamba ilimuwia vigumu kuamini namna biashara yake hiyo ilivyofanikiwa haraka. Na ndiyo maana hakuwa akiitilia maanani kwa sababu alikuwa anajua isingedumu kwa muda mrefu - Wale wanajeshi wengine wangegundua mchezo wake na wangeanza kufanya wao.
Hawakuwahi kugundua. Hilo lilikuwa kama somo lake la kwanza - Aligundua alikuwa na uwezo wa kufanya vitu ambavyo watu wengine walikuwa hawawezi. Alikuwa na uwezo wa kubuni vitu ambavyo watu wengine walikuwa hawawezi. Kwahivyo akawa makini kwenye kusikiliza tena. Walikuwa wanahitaji nini tena? Vitu vingi: Wanawake, Chakula, Dawa za maumivu, Rekodi na taarifa mbalimbali, Dawa za kuulia kunguni na mbu, Bangi, Penicilin, Heroin, Sindano zilizo safi za kujidunga na mambo mengine. Alisikiliza na kuelewa na kutafuta na kutekeleza.
Halafu jitihada zake zikazaa matunda. Ilikuwa ni kama njia ya kumuongoza kufikia mafanikio yake mengine aliyoyapata baadae. Ilikuwa kama mwitikio wa tatizo lililokuwa mbele yake. Tatizo la kwanza ilikuwa kazi ngumu ya kutafuta vitu husika - Hii ilikuwa changamoto sana. Kupata wanawake ambao hawana maradhi ilikuwa kazi ngumu, lakini kupata wanawake wenye bikra ilikuwa kazi ngumu zaidi. Kutunza kiwango cha kutosha cha madawa ya kulevya isingewezekana na ilikuwa ni kazi hatari.
Tatizo la pili lilikuwa ushindani. Ilimjia kama radi kwamba hakuwa wa kipekee. Alikuwa na bidhaa adimu lakini sio za kipekee. Vijana wengine pia walikuwa wanakuja kwa kasi ya ajabu kwenye mchezo wake. Soko huria na ushindani vilikuwa vimeanza kuzaliwa. Watu walianza kukataa kubadilishana bidhaa zake kwa madai kuna sehemu ambako wangepata kwa gharama nafuu. Ilimshangaza.
Badilika uendane na mazingira; Akapata ufumbuzi wa tatizo lake. Alikuwa amekaa jioni moja akitafakari peke yake - Yeye alikuwa tayari anajulikana, sasa kwanini alikuwa anahangaika kutafuta bidhaa ambazo ni ngumu kupatikana na zingezidi kuwa adimu? Kwanini asianze biashara mpya ya bidhaa iliyo tele na ya kipekee?
Bidhaa gani? Dola ya kiMarekani. Akawa mkopeshaji.
Pesa ndiyo ilikuwa suluhisho la matatizo yote. Kama mtu angehitaji viatu, au heroine au wanawake wazuri na mabikra angeweza kuvipata hivyo vitu kwa hela aliyokuwa amekopa kwa Hobie. Angemaliza haja zake leo, halafu wiki ijayo angetakiwa kuirudisha na riba kidogo juu. Hobie angekaa tu kama malkia wa nyuki. Alifikiria zaidi. Akagundua sikolojia iliyokuwa imejificha kwenye namba. Namba ndogo kama tisa ilionekana ni ndogo na ya upendeleo sana. Kwahivyo alianza kutoza riba ya asilimia tisa. Ilionekana sio chochote kwa wakopaji wake. Tarakimu moja kwenye karatasi tena iliyo chini ya kumi.! Lakini kwa Hobie tisa ilikuwa kubwa. Asilimia tisa kwa wiki ni sawa na asilimia 468 kwa mwaka. Watu wangechelewesha deni zao kwa wiki nyingi tu halafu 468 ingegeuka kuwa asilimia 1000 kwa kasi sana. Lakini hakuna aliyegundua hilo. Hakuna mtu aliyejali isipokuwa Hobie. Wengine wote waliiona tarakimu tisa ni ndogo na ya upendeleo.
Mcheleweshaji wa kwanza kulipa alikuwa ni bwana mmoja mwenye mwili mkubwaa wa kutisha na roho mbaya. Alikuwa akiogopeka na watu wengi. Hobie alipoongea naye alitabasamu akamwambia nimekusamehe. Yule bwana akajihisi ana deni kwa Hobie hivyo akaomba awe "mgambo" wa Hobie. Kuanzia hapo hakukuwa na watu waliogoma kulipa au kuchelewesha mikopo yao. Hata hivyo, namna ya kuwadhibiti ilichukuwa muda kidogo. Hobie alitaka yule bwana aishie kiwango cha kutisha tu lakini yule bwana alienda mbali hadi kuwajeruhi na kuwavunja miguu baadhi ya wanajeshi. Yote kwa yote walilipa pesa zake kwa wakati na kama inavyotakiwa.
Mpaka siku ambayo aliungua uso wake na kupoteza mkono , Hobie alikuwa amekusanya pesa nyingi sana kiasi aliingia daraja la matajiri. Mpango wake mwingine ukawa ni kuhakikisha anarudi nyumbani na mali yake yote aliyokusanya. Watu wengi walikuwa wamejaribu kutoroka jeshini hasa Vietnam na kushindwa, achilia mbali mazingira ambayo Hobie aliyapitia hadi kutoroka. Hii ilikuwa kama uthibitisho mwingine yeye hakuwa mtu wa kawaida. Baada ya kutoroka historia ilikuwa fupi tena, Alipofika New York sura yake ikiwa haieleweki na bila mkono wake wa kulia alijihisi amefika nyumbani. Huko kwao Manhattan kulikuwa kijijini. Hakuna sababu ya kurudi huko. Na pia hakuna haja ya kuahirisha biashara yake ambayo alikuwa amekwishaianza na kwa muda huo alikuwa na mtaji wa kutosha.
Akaanza tena kujaribu bahati yake kwenye kukopesha. Alikuwa na mwonekano na mtaji. Akapata msaada wa kuingia kwenye mchezo. Akapambana na wa iTalia. Akahonga polisi hapa na pale ili abaki kwenye kivuli asionekane.
Halafu bahati ikatabasamu mbele yake. Haikutofautiana sana na ile ya mara ya kwanza. Ilikuwa ni mwitikio tu wa tatizo na tatizo lenyewe lilikuwa ni dogo tu. Alikuwa na mamilioni ya pesa yaliyo mikononi mwa watu. Kuna huyu alikuwa anamdai asilimia kumi, yule asilimia tisa kwa wiki na kule asilimia miatano kwa mwaka. Hela nyingi sana ilikuwa mikononi mwa watu wengine. Halafu akawaza akagundua kidogo kinaweza kuwa kikubwa. Ilimwijia ghafla. Asilimia tano ya riba kwa baadhi ya makampuni ni kubwa kuliko asilimia miatano za mtaani tu. Akawataifisha wote aliokuwa akiwadai na kuuza na kurudisha hela zake na faida. Akanunua suti za gharama, na kukodi chumba cha ofisi kwenye jengo la WTC. Kama muujiza akawa anakopesha makampuni makubwa.
Lilikuwa ni wazo la kipekee. Alikuwa ametoka hatua ya chini na kuingia uwanja wenye fursa. Akaanza kupata wakopaji wengi wenye taasisi kubwa ambao benki ziliwaona kama "hawafai kukopeshwa tena." Wanaume waliosoma walikuwa wakipishana kuja kwake awasaidie huku wakiweka vitu vya thamani kama dhamana baadala ya dhamana za nyumba zenye mabanda ya mbwa. Kiwango cha riba yake akakishusha chini na akazidi kupata faida kubwa - Kidogo kinaweza kuwa kikubwa!
Unabii wake ukathibitika. Japo kulikuwa na matatizo ya hapa na pale lakini yalikuwa yanaweza kushughulikiwa. Akabadilisha mfumo wake wa kuwashughulikia wacheleweshaji. Hawa walikuwa ni wanaume wasomi waliozijali na kuzipenda familia zao kuliko kitu chochote - wake zao au watoto na mara nyingi tishio moja tu lingetosha kuwafanya walipe. Ni mara chache sana vitendo vilifanyika. Hata hivyo, ni jambo lililokuwa linampa faraja sana Hobie kuona watoto na wale wake wakimuomba msamaha. Biashara ilikuwa nzuri. Lakini kuna kitu kilikuwa kinamuambia alikuwa anahitaji kubadilika na kuendana na mazingira. Ndiyo maana leo alikuwa peke yake ofisini kwake akiwaza na kubadilisha mipango hii na ile
TAKRIBANI MAILI HAMSINI kaskazini, Marilyn Stone alikuwa akitafakari pia. Alikuwa na akili. Alikuwa anajua Chester ana matatizo ya kifedha kwa wakati huo. Halikuwa tatizo lingine. Hakuwa na mchepuko. Alikuwa na uhakika na hilo. Wanaume wakiwa na mahusiano ya pembeni kuna dalili ambazo huwa wanazionesha, na Chester hakuwa akionesha hizo dalili. Kwahivyo tatizo kubwa lilikuwa ni fedha. Mwanzo mpango wake ulikuwa ni kusubiri. Kukaa tu na kusubiri hadi siku ambayo Chester angeamua kufunguka kila kilicho kwenye kifua chake. Alikuwa amepanga kuisubiria hiyo siku ifike na kuanzia hapo angeweza kumshauri nini wafanye. Wanawake wapo vizuri sana linapokuja suala la kuhimili mambo mazito kuliko wanaume. Angeweza kushauri hatua zipi Chester achukue.
Lakini kwa sasa alikuwa amebadilisha mawazo yake. Asingeweza kuendelea kusubiria. Chester angeweza kufa kwa mawazo. Angetakiwa afanye jambo kuhusu hilo tatizo. Hakuna haja ya kuongea na Chester. Chester alikuwa ameamua kuficha matatizo yake. Hata kama angeongea nae bado Chester angeficha vitu. Kwahivyo ilikuwa ni lazima afanye jambo. Kwa faida ya Chester na faida yake.
Suluhisho namba moja kabisa lingekuwa kuiweka nyumba sokoni. Kwa vyovyote vile, kuuza nyumba kungeweza kutatua tatizo lolote ambalo walikuwa wanapitia.
Mwanamke wa kitajiri anayeishi Pound Ridge anakuwa na namba za watu wengi walio kwenye biashara ya nyumba. Sio kwa sababu ana kazi nao, lakini ni kwa sababu anajisikia fahari tu. Sanasana anazihifadhi namba za hao watu ili wamsaidie na kumshauri kuhusu mapambo ya nyumba, hakuna kitu kingine. Marilyn alipata namba nne za marafiki ambao angeweza kuwapigia mara moja. Alizichambua na hatimaye akaishia kumchagua mwanamke mmoja aliyemwandika kwa jina la Sheryl, ambaye hawakuwa wakifahamiana sana, lakini alimpigia.
"Marilyn," Sheryl alisema. "Nikusaidie nini?"
Marilyn alivuta pumzi kidogo.
"Tunafikiria kuuza nyumba yetu," Alisema alipoipata sauti yake.
"Na umeamua kunitafuta mimi? Marilyn, Nashukuru. Lakini kwanini umeamua kuiuza. Una mpango wa kuhama?"
Marilyn alivuta tena pumzi, "Nadhani Chester anafirisika. Siwezi kuliongelea hilo suala, lakini nafanya mipango ya dharura."
"Wewe ni mwanamke mwenye busara sana," Sheryl alisema. "Watu wengi huwa wanasubiri hadi mambo yakiharibika zaidi ndipo wanaamua kuuza kwa haraka na matokeo yake wanapata hasara."
"Watu wengi? Unamaanisha hili ni tatizo linalotokea kila wakati?"
"Sio masihara. Tunaliona hili tatizo kila leo. Ni bora kulitatua mapema kuliko kusubiri hadi mambo yakufike shingoni. Niamini mimi unafanya jambo sahihi kwa sababu sisi wanawake tunaweza kushughulikia mambo mazito kuliko wanaume."
Marilyn alihema na kutabasamu. Alijisikia kama alikuwa anafanya jambo sahihi, na mtu aliyemshirikisha ndiye alikuwa mtu sahihi.
"Nitaiweka sokoni," Sheryl alisema. "Ninashauri tuiweke kwa bei ya dola milioni mbili huku tukiwa tumelenga kupata dola milioni moja nukta tisa. Hiyo inaweza kupatikana haraka."
"Baada ya muda kiasi gani?"
"Kwa soko lilivyo muda huu," Sheryl alianza kueleza. " Na eneo ambalo nyumba yako ipo? Wiki sita. Baada ya wiki sita utakuwa umepata mteja. Ninakuhakikishia hilo."
SEHEMU YA ISHIRINI