MBILI
MSHTUKO!
Uso umekumbwa na fadhaa iliyoshindwa kujisitiri. fikrani mwake kuna mengi yaliyokorogeka, tibutibu! Akiwa mtaani kwao, nafsi ilimsuta, kujishtukia kukawa kwingi kana kwamba kuna mtu aliona kilichomkuta huko alikotoka.
Alitembea akiwa na wasiwasi huku akiangalia kila pande akiwa na hofu kuwa huenda kukawa na watu walikuwa wakimtazama kwa kila mwendo wake. Akiwa anakaribia na kwao, akakutana na shogaye. Akakunja mdomo na kubirua macho mithili ya mtu anayekata roho.
"Shoga, vipi?" Aliuliza shogaye Sijali. Sijali akamnyali shogaye. Akajikuta baridi linamwingia kwa hofu.
"Una tabia mbaya, Avijawa. Kilichokufanya unikimbie nini?" Alisema Sijali kwa hasira huku akitoa lawama.
"Shoga, nilivyosikia mtu anaagiza chupa zima la
alkasusu nikajua huko leo kuna kazi, na huenda akaomba msaada wa kuchimba madini. Nikaona aaaka!Cha kukobokea uke nini? Kwa hizo ginesi na nyama choma pekee?" Alisema Avijawa.
Sijali akamtazama bila kummaliza.
"Sasa kilichokuwa kina kukimbiza nini—kunifuata nyumanyuma na shughuli huiwezi! Loh, mwanamke m'baya wewe!" Alisema Sijali. Avijawa hakuwa na habari. Alijitingisha na kujishaua kana kwamba anayosema shogaye hayana maana. Yeye kakubuhu udangaji. Mwanafunzi wake kakutana na changamoto siku ya kwanza kazini.
"Em tuachane na hayo, jamaa yamemtoka maganda mangapi? Maana yule bwana tolu halafu
alkasusu chupa zima sijui kama gereji ina usalama!" Alisema Avijawa. Akakenua na macho yake yaliyo na mng’aro wa paka jizi yakachezacheza kinafiki.
"Si bora ingekuwa hivyo!" Alijibu Sijali!
"He! Imekuwaje tena?" Alihoji kishankupe Avijawa. Akajiweka sawa ili aupate ubuyu vizuri. Mate yalikuwa yakimtoka kwa hamu ya kujua kilichojiri baina ya Sijali na Mzeta,
danga la kwanza la Sijali.
"Em njoo hapa tukae," alisema Sijali. Wakasogea kibarazani kwa nyumba ya jirani na akina Sijali. Wakaketi kisha Avijawa mwenye pupa likamtoka.
"Enhee, ilikuwaje? Maana sipati picha!" Alisema Avijawa. Wakati huo akiwa hana utulivu akiona kabisa mdomo wa shogaye unachelewa kumfikishia habari aliyokuwa na kiu nayo.
"Subiri basi, mbona ‘ivyo!" Alisema kwa hamaki Sijali. Akameza funda la mate kisha akaendelea, "shoga yule bwana tulishindwana. Baada ya kuliona chupa la
alkasusu juu ya meza ikabidi niongope n'na blidi!" Alisema Sijali kisha akaweka tuo.
"Heheheeeee! Haloooooo! Shuuutuuu!" Alisema Avijawa huku akidokoa vidole vyake hewani.
"Eh, usichekelee kwanza!" Alidakia Sijali.
"Enhe, ikawaje tena baada ya kuambiwa ngoma haichezwi?" Alisema Avijawa.
"Mwenzangu si akanigeuka, akainuka na kumlipa yule ustadh kasusu, kisha akamwambia muhudumu pesa ninayo miye nitalipa huduma tulokula. Jinsi mwanaume alivyo hana haya, aliondoka bila wasiwasi dada, kiwewe kilinishika kumkimbiza siwezi, wala kuinuka siwezi. Sijui kama sio mwanga yule bwana! Loh! Kilanga chote kimeniisha!" Alisema Sijali.
"Mungu wangu!" Alishtuka Avijawa huku akiziba mdomo kwa viganja vya mkono wake.
"Sasa ikawaje?" Sijali aliongeza.
"Iweje tena na hela za watu zinatakiwa, shosti! Mhh, sina hamu. Aibu ya mwaka kwa kweli," alisema Sijali.
"Aibu gani tena? ‘Embu sema haraka basi mbona unaongea kwa pozi na wewe! Aah, vipi ‘ivyo?" Avijawa alisema kwa kuudhika.
"Weeh, koma! Tena unikome kabisa. Sitaki unipelekeshe. Umes’kia? Kama ulitaka kujua mwisho wake, ungekaa palepale na sio kukimbia. ‘Em niwache kwanza!" Alisema kwa hasira Sijali. Jazba ikawa inamnyemelea hata mishipa ya kichwa ikachezacheza pasipo hiari yake.
"Basi shoga'ngu ‘mekutania tu! Aaai, hutaniwi na wewe eh, ‘aya malizia basi ikawaje?" Alisema Avijawa kwa kuomba, tena kinyenyekevu mno. Kaba limekaba kwa umbeya, asipoujua hakika hawezi kulala wala kuanzisha mazungumzo mengine ya ubuyu.
Sijali akashusha pumzi ndefu kisha akaendelea, "…muhudumu akaja kudai pesa yake, nikamweleza hakuelewa. Mwenzangu, si akaitwa meneja! Nikasuutwa huku nikitiwa masingi kwa tamaa. Uamuzi uliotoka nikapelekwa jikoni kuosha vyombo. Tangu ile saa saba hadi saa kumi na mbili jioni nimeosha mijombo juu ya mijombo. Nikafua mashuka yao ya gesti, kudeki chooni na kuteseka kote nilikoteseka, lakini ikawa haijatosha!" Alisema Sijali kwa masikitiko.
"Nini tena? Meneja kataka ujira wa kukaa mtupu ama namna gani?" Aliuliza tena kishambenga Avijawa.
"Bora ingekuwa hivyo kwa sababu nisingehitaji pesa kufanikisha alilotaka!" Alijibu kwa unyonge Sijali.
"Kumbe je!" Aliuliza tena Avijawa.
"We’ na we’ mpana kutaka kujua ya watu. Yakiwafika unakimbia. Uwe unabaki upate kuandika habari, maana maswali meengi kama mwandishi vile," alijibu kimaudhi Sijali.
"Aaaah, shoga! Mi' na wewe tena! Vibaya ‘ivyooo!" Alisema Avijawa. Sijali akacheka, wakapigishia makofi ya mchapo. Akawa anampigapiga mgongoni shogaye. Avijawa bwana!
"Malizia basi!" Alisema Avijawa.
"Hawajaridhika na huduma yangu, wamechukua na simujanja yangu. Wamesema hadi nikalipe elfu thelathini na tano zao nd’o n’tachukua simu yangu," alisema Sijali.
"Khaa! Shoga pole!" Alisema Avijawa.
"Pole yako hairudishi simu yangu!" Alijibu Sijali. Wakacheka wote kwa pamoja. Wakagongeana!
Sijali akaendelea kucheka peke yake. "Vipi shoga tena?" Avijawa aliuliza.
Sijali akaguna "mmmh, dunia hii!" Avijawa akazubaika.
"Dunia imefanyaje?" Alisema Avijawa.
"Sasa kilichokufanya utoke upesiupesi pale
dangani ni kitu gani?" Sijali aliuliza kisha akaendelea kucheka.
"Mwenzangu lile baba lenyewe uliliona. Refuuu halafu likaagiza alkasusu chupa nzima, cha kutobolewa kizazi nini? Nikaona maadamu umelitaka, basi umelipata!" Alijibu Avijawa.
"Nimelitaka miye tena? Mwalimu kweli unasema ‘ivyo? Tuache ‘ayo, ‘aya sasa wewe yule mgeni wako hadi hicho kizazi chako kitobolewe?" Alihoji Sijali.
"Weeee! Hujapata kusikia habari za
threesome eh? Maana kama kula nimekula, kilichokuwa kinafuata?" Alijibu Avijawa.
Sijali alibaki anamtazama tu Avijawa na asimpatie picha itakayomfaa. Moyoni kabaki kuning’inia na kufikiria yalompata shogaye.
TATU
KISA MKASA!
Baada ya siku tatu za matukio ya kukomolewa na kukomoana, akiwa mtaani kwao, Kona ya Maduka Mawili, Tandika—jina maarufu kwa Mwarabu, maskani,Mwamba Mzeta alilifurahisha baraza la wahuni wenzake.
Aliwachotea kisa na mkasa wote wa Sijali na mwenzake. Akaanika yote kama unga juu ya mwamba. Akaanza na namna alivyonusurika kama si kujinasua mikononi mwa popo watu, walawatu (vempaya).
Wahuni walifurahi sana kuipokea habari ile kutoka kwa mhuni mwenzao. Vicheko vikubwakubwa vikapasua anga yao. Kama ujuavyo tena, wahuni ukiwaambia mtoto wa kike kadhalilika wanaona fahari kwao! Tena huwa wanachangamka kama wameona kontena la kileo likianguka bila mwenyewe kuwepo.
"Kwa hiyo mwanangu walikuona Mzeta zezeta, kumbe konki faya!" Alisema mshikaji wake Mzeta.
"Yaani, we' acha tu. Nafikiri walivyosikia Mzeta wlifikiri ni lile zezeta kubwa lisilojua hata kwao, kumbe kichaa nambari chafu, haisafishiki hata kwa asidi manjano Mtaliano!" Alijibu kibabe Mzeta huku akijipiga kifua kwa kujimwambafai.
Wahuni wakalipuka kwa vicheko. Wakapiga mbinja za nguvu kuunga mkono ukomozi. Tabasamu ya wahuni ikaalika swali miongoni mwao.
"Je, mwamba hujapata habari kuwa yule demu nini kilimtokea baada ya kumwachia msala wake?" Mwamba mmoja alihoji. Akamtazama Mzeta akimiminika ili kujua kilichotokea.
"HAPANA—kwa kweli! Hakunipigia wala kunitafuta," alisema Mzeta.
"Daah! Mwamba una roho ngumu kinyama!" Mwingine alidakia.
"Lakini wao nd'o walianza sasa..." Kabla hajamalizia kauli yake, simu ikaita. Akahangaika kuzamisha mkono mfukoni mwake. Alivalia jinzi la kubana. Aina ya vimodo
Akaipata. Kutazama jina hakuna.
"Nani huyu?" Alisema kwa sauti Mzeta.
"Nd’o upokee umjue," alijibu mwamba wa pembeni.
Kwa upole, akaipokea.
"Halo!" Mzeta aliitikia.
"Halo!" Sauti mororo kutoka upande wa pili iliitikia pia.
"Nani mwenzangu?" Mzeta alihoji huku akitoa macho.
"Mi' Sijali!"
"Mbona namba haikuja na jina?"
"Mwenzangu we’! Huo mkasa mrefu!"
"Haunihusu, sema shida yako!" Mzeta alisema kwa kumkatisha Sijali.
"Mbona hivyo jamani!" Sijali alisema kwa masikitiko.
"Ndiyo, hainihusu…. sema shida yako mama! Maneno mengi ya nini?" Mzeta aliendeleza majibu ya hasira.
"Sasa!"
"Enhee!"
"Lini tutakutana?"
"Ili iweje!"
"Aah Mzeta ka' mtoto na wewe! Ka’ hujafundwa jando!"
"Nakuuliza tena, ili iweje? Uliona sisi watu wa mjini hapa tukienda jando wapi? Mambo hizo za warugaruga wa porini huko!"
"Haya achana na ya jando. Unauliza iweje nini na wewe wakati mambo hadharani!"
"Hao simba washamaliza kucheza uwanjani?"
"Si wamefungwa juzi na Yanga—hivyo uwanja mweupe! Ushindwe wewe tu!"
"Nije huko halafu unijazie nzi?"
"Sikujazii bwana. Nakuja peke yangu safari hii!"
"N'taamini vipi?"
"Nakuja kwenu badala ya wewe kuja kwetu!"
"Hapo sawa!" Mzeta akakenua meno kama mamba.
Wakakubaliana. Sijali amethibitisha kwamba hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Lakini je, ni kweli?
"Oya wana! Huyu n'lokuwa naongea naye nd'o yule gashi tuliyekuwa tukimzungumzia!" Alisema Mzeta. Wahuni wakashtuka huku wakiachia midomo wazi.
"Anataka nini?" Mwamba mmoja alihoji.
"Anataka nini… tena hilo nalo swali?" Alijibu Mzeta—wahuni wakapiga
hee-haa wakagongesheana kuonesha wanaunga mkono maangamizi.
"Tena uzuri zaidi anakuja yeye Tandika kutandikwa! Shenzi!" Alisema Mzeta. Wahuni wakaruka tena. Wahuni bwana, hawana maana kabisa.
Baadaye sana, majira ya saa kumi na moja jioni, simu ya Mzeta ikaita. Kutazama, ilikuwa namba ileile aliyotumia Sijali asubuhi.
Akaipokea.
"Haloooooo!" Aliivuta sauti yake kutia madoido. Wahuni sio watu wa mchezo-mchezo wakiwa na uhakika.
"Mambo!" Sauti kutoka upande wa pili ililonga.
"Fureshi tu, niambie mtoto mzuri!" Alijibu Mzeta.
"Poa tu... Sasa nimechelewa nachukua bodaboda, utamlipa ili niwahi!" Alisema Sijali.
Mzeta akaitikia kisimanzi na mwisho akasindikiza na sonyo refu baada ya kukata simu.
"Mademu wa BUZA bwana!" Alisema Mzeta.
Kidogo simu ikaita tena.
"Eh, niambie!" Alisema Mzeta.
"Hujanambia nikufuate wapi?" Ilisema sauti ya upande wa pili—Sijali.
"Njoo Davis Corner utanikuta sheli pale!" Alijibu Mzeta huku akionesha kukereka.
"Ayaa!" Sijali aliitikia.
Dakika kumi baadaye bodaboda si ikafunga breki.
"Mambo!" Sijali alimsalimia Mzeta aliyekuwa wima akimsubiria yeye.
"Fureshi tu!" Alijibu Mzeta.
"Aya, mpe basi pesa yake huyu bodaboda!" Sijali alisema kwa wasiwasi kana kwamba Mzeta kagoma kulipa.
"Fureshi tu, bei gani pesa yako, mwana?" Mzeta alihoji.
"Buku tatu mwamba!" Alijibu bodaboda. Mzeta akaruka utadhani kaelezwa anao ujauzito angali mwanaumeme, "buku tatu? Unaniona mi' kolo sana au? Sijapangika kizembe ‘ivyo bado wewe!" Alisema kwa hasira Mzeta.
"Bwana Mzeta, mpee!" Sijali alisisitiza. Lakini Mzeta alibaki na msimamo wake. "We' unataka kutoa shin'ngapi?" Sijali alihoji.
Mzeta akamkata jicho. "Sitoi zaidi ya buku bee 'apa!" Mzeta aliongea kisela.
"Funika kombe mwanaharamu apite, chukua buku hii hapa, aya Mzeta mpe buku mbili huyu bwana ende zake!" Alisema kwa hekima Sijali.
Wakati haya yakiendelea, Sijali alikuwa katika dunia mbili: moja ya mawazo kwamba kajiingiza wapi hapa, na nyingine ya potelea pote.
"
Kudanga nako kazi si n'takoma miye leo?" Alijisemea nafsini. "
Kama majuto ni mjukuu, mbona miye hata mtoto wake sina?" Aliendelea kujipa moyo.
"Bwana we! Itafahamika tu hukohuko kama ndo mwisho wangu ndo mwisho wangu n'tafanyaje????" Aliendelea kujiwazia nafsini.
Mawazo yasivyo na siri, Mzeta alishtukia ishu. "Vipi mbona kama hauko sawa?" Mzeta alihoji kinafiki.
"Kawaida tu, kuna mambo yangu hayako sawa!" Alijibu Sijali.
Waliendelea kuongea hadi walipofika nyumba ya ahadi!
Wakajitoma ndani, wakamkuta dada wa mapokezi, maswali ya unatoka na unakwenda wapi yakaulizwa. Walikotoka Dar na wanakoenda Dar vilevile.
Itifaki ilivyotimizwa, wakajitoma ndani.
NNE
MTU CHAKE!
Wakiwa mlangoni, wakihangaika kufungua mlango wa chumba cha gesti, Sijali akaanza kumbabaisha na kauli za kimahaba Mzeta.
"Hili lango nalo sijui bovu. Mambo ya kifala haya!" Mzeta alisema kwa hasira huku
akifosi mlango ufunguke.
"Oya, oya sista embu njoo kidogo lango lako limegoma kufunguka huku," alisema Mzeta kwa kelele.
"Aaaai, polepole basi, utakera wengine!" Alisema Sijali kwa upole.
Punde muhudumu akafika eneo la shida, akamtoa Mzeta. Akaushika mlango na kutekenya kidogo, kitu na boksi, mlango ukafunguka.
"Mtu chake bwana!" Alisema yule muhudumu.
"Ahsante eh," alisema Sijali. Muhudumu akaondoka, huku nyuma Mzeta akigezea sauti ya muhudumu 'mtu chake, aringe, ye' atabaki kuwa muhudumu tu," alisema Mzeta kwa sauti ya dhihaka iliyotoka puani.
Sijali akacheka.
"Enhe, ulikuwa unasemaje pale nje? Maana nilikuwa bize na kuufungua mlango," Mzeta alisema.
"Kwamba, nina shida na..." Kabla hajamaliza kusema, simu ya Mzeta ikaita. Akaitazama kwa makini, ilikuwa namba ya rafiki yake pale maskani, akaikata kisha akaizima simu yenyewe.
"Enhe, ulikuwa na shida gani?" Mzeta aliendelea kuuliza swali lake.
Sijali akataka kusita kusema. Akainua jicho lake la huba. Mzeta hakuingia geji na deko hilo. "Sema basi!" Mzeta alimaka.
"Nilikuwa n'na shida ya elfu arobaini!" Sijali alisema kwa maringo. Mzeta akamkata jicho kali sana.
"Ya nini hiyo yote?" Mzeta aliuliza kwa kumakinika.
"Nikagombolee simu yangu pale baa. We' si ulikimbia siku ile," Sijali alijibu. Mzeta akatulia. Akaanza kukuna kichwa utadhani alitafunwa na chawa. Akainuka, mara akakaa. Akaanza kuvua viatu vyake kana kwamba majibu yapo ndani ya viatu.
Akajibweteka kitandani puu!
"Anhaa! Sawa! Nitakupa!" Alijibu kirahisi sana Mzeta.
"Lakini...." kabla hajamalizia Mzeta, Sijali akadakia, "lakini nini tena jamani 'akati ushasema utanipa!" Sijali aliongea kwa madeko.
"N'takupa kwa awamu mbili tofauti!" Alisema Mzeta kisha akatulia kusikilizia upepo. "Aya, n'tafanyaje sasa na ushasema!" Sijali alisema kwa unyonge.
Sijali akatoka, akaingia chemba moja ya kutakasa mwili. Mzeta akawasha sigara yake, akapiga pafu kama tatu mfululizo—kabla ya sigara kwisha akaizima kwa kukata kile kipande kilichoungua na kukitupia kwenye jaa dogo la plastiki ndani ya chumba hicho.
Kile kipande aliuchobakiza akakiweka juu ya meza iliyokuwamo ndani mle chumbani.
Sijali anarudi, akamkuta Mzeta yupo kama alivyozaliwa. Hamadi! Kuona, akaguna, 'mmh, leo kazi ipo! Aya, ngoja tuone," Sijali alijisema nafsini. Anasema moyoni, machoni nako kunasema huku moyo ukimshinda kwa kishindo cha mapigo yake.
"Vipi?" Mzeta aliuliza.
"Wala hamna kitu, tuendelee" Sijali alisema kinyonge huku akimeza mate. Akajitupa kitandani. Mzeta katulia tu mithili ya Mandingo au Lexington Steel kama si Mr. Marcus (usiniulize akina nani hao).
Sijali akajitia ujuzi wee, mara kaimba, mara kasimama, mara eh, mara hii. Joka shimoni ukelele mithili ya mwanamwali kwa mara ya kwanza.
Mzeta hana masihara maana kelele kwake kwanza ndiyo zinamwamshia maruhani kichwani.
Mzeta alitaka kuhakikisha maudhi ya nafsi aliyosabisha Sijali yote yanaisha. Akatwanga kinu kama hataki tena kukitwangia siku nyingine.
Masaa mawili ya raha, yakageuka karaha kwa Sijali.
"Haya mateso tena na si starehe. Shida hizi jamani!" Alijisemea nafsini. Wametoka ndani wala hawakusemeshana. Kila mmoja alimchunia mwenzake. Sura angavu aliyoingia nayo chumbani Sijali sasa ilikuwa giza, nyeusi iliyojaa chuki na jasho!
"Kwa hiyo sasa hiyo nyingine utanitumia lini?" Sijali alimwuliza Mzeta wakiwa mbalimbali.
"Wewe tu, kama uko fresh kurudia gemu hata kesho au keshokutwa, fureshi tu," Mzeta alijibu.
"Nimechoka kusikia na hiyo 'fureshi yako kila wakati," Sijali alisema.
"Unayumba wewe!" Mzeta alisema.
"Kwanini?" Sijali alihoji.
"Si hivyo, nakwambia raundi ya pili we unaongea mengine," Mzeta alijibu.
"Kwa maana hiyo huwezi kunipa chochote hadi nikuvulie chupi, sio?" Sijali alisema huku akimwangalia kwa utata Mzeta.
"Kila mtu anaringia chake!" Mzeta alijibu.
"Haya ahsante kwa kunifahamisha!" Sijali alijibu.
Sijali alisonga hadi eneo la kituo cha daladala, mwendo
mdogomdogo anasikiliza maumivu ya tumbo. Nyonga mara zinakakamaa mara zinashikana! Koo mara limkauke na mara atamani kuficha donge la barafu huko sirini. Maana huko alikotoka kulikuwa matesoni.
Polepole alidandia gari ya kwao Buza. Kilanga komo! Ndani ya daladala usingizi ukampitia, badala ya kushuka kituo cha Buza kwa Lulenge, akaenda kushushwa Lumo Mwanzo.
Kosa kubwa kupanda gari la Gongo la Mboto. Akashuka, akadandia gari lingine la kurudi tena Buza. "Eh, Mungu wangu, kile kiasi chenyewe nilichokipata kwa ajili ya kukombolea simu, kinatumika katika nauli. Balaa gani hili," Sijali alijisemea nafsini.
Alivyoingia garini, hakuketi. Alisimama wima japo viti vilikuwapo. "Oya, sista kaa basi kitini unanichoreshea watu wataona gari imejaa kumbe bado," konda alilalama.
"Naogopa kupitiwa na usingizi. Nimechoka sana," Sijali alijibu kwa upole.
“Kwani unashuka wapi?” Konda alimwuliza Sijali.
“Buza kwa Lulenge,” Sijali alijibu kwa unyenyekevu huku uso wake ukionesha kama kachoka hasa.
"We lala tu n'takuamsha tukifika. Kaa naomba sisteri!" Konda alisisitiza. Sijali akaketi kwa heshima ya konda. Mawazo yakamchukua, akaenda mbali kuitazama dunia kwa urefu na mapana. Kichwani si jingine linampitikia kwa kujirudiarudia. Lile sura la Mzeta akiwa jinsi alivyozaliwa na namna alikuwa akimsulubu utadhani alikuwa katika punda akichana mbao. "Laiti kama ningelikuwa na kazi, haya yote yasingelitokea," alijisemea Sijali. Akaguna kisha akaegemeza kichwa chake katika kioo cha gari alichokifunga ili apate japo lepe la usingizi. Mkono akauweka sambamba na kichwa chenye nywele ambazo sasa ni timutimu lisilochanwa! Hakukumbuka hata kuchana nywele akiona heri tu angelipata muda wa kulala japo kidogo.
Akapitiwa usingizi palepale, tena na ndoto za kukimbizwa akiwa uchi, lakini dakika kadhaa mbele, akagutushwa, "oya, sista, sista!" Sijali alisikia sauti kwa mbali konda akimwita. "Tushafika kwa Lulenge shuka ukapumzike mida ya kubeti hii!" Alisema konda.
Sijali akashuka akatoa noti ya elfu kumi na kumkabidhi konda, konda akaikataa, "Nimekusaidia tu dada'ngu, unaonekana umechoka kinyama!" Konda alisema kisha akagonga gari liondoke.
Kwa mchechemo, alifika nyumbani. Alimkuta shoga’ke Avijawa yupo akipiga soga na mdogo wake.
"Heee! Shoga umerudi!" Avijawa alisema kipashukuna.
"Em niache kwanza, nimechoka kama nini mwenzako!" Sijali alisema huku akikunja uso.
"Mmmh we na we mbwembwe..." Avijawa aliendeleza utani wake.
"Enhee, niambie shoga mtoko vipi, mlikula chips kuku? Soda au bia ngapi mwenzangu!" Avijawa aliendelea kuuchota umbeya.
"Embu tulia basi... janaume bahili lile likatoe vitu vyote hivyo karogwa..." Sijali alijibu huku akijinyoosha. "Loh, mwili wote unauma... maana alivyonitinginya kama punda dada!" Sijali aliongeza.
"Amina naomba niletee INDOSIDI yangu ipo pale juu ya droo la kitanda," Sijali alisema.
Avijawa akatoa macho. "Indosidi tena shoga, imekuwaje?" Avijawa alihoji. Akajiweka vizuri kusikia majibu ya Sijali.
"Mwenzangu, yule bwana ana futi. Fuuutii dada na nilichopata hakuna!" Sijali alijibu.
"Mmmh, niambie koma we!" Avijawa alichochea.
"Koma mwenzangu, KOOOMAAA! Usithubutu kupatwa na bwana Mzeta," Sijali alisema.
"Lakini linaonekana lile jitu..." Avijawa alisema.
"Yaani, wenzie wanavuta bangi wawe na nguvu ya kulima na kufanya kazi, yeye anaivutia bangi papuchi, jamani! Sina hata hamu!" Sijali alisema.
"Kwani kaondoka na ngapi?" Avijawa alihoji, kisha akamtazama usoni Sijali.
"Miguu ya bajaji?" Avijawa aliongeza.
"Heeeee, polepole basi. Mbona una
kimuhemuhe hivyo cha kutaka kujua kwani vipi mwenzangu? Unataka kufungua gazeti la udaku au?" Sijali aliongea kwa hasira.
Avijawa akatulia. Akaikusanya mikono yake na kuiweka pamoja mapajani kwake. "Kaondoka na miguu ya gari," Sijali alijibu.
"Mtumee! Miguu ya gari hiyo kakulipa bei gani?" Avijawa alisema.
"Hapo nd’o kichefuchefu chenyewe kilipo..." Sijali alisema kisha akaweka tuo. "Kanipa pauni, halafu kila Pawasa bango moja, maana yake Nteze mbili kwa nne. Kijasho kilitoka. Kama haitoshi, hilo bango moja kufikia, utafute feni lilipo, vinginevyo utapiga kelele kama kichaa. Dunia ina watu hii? Si ajabu yule mshenzi anakunywa chupa zima la alkasusu," Sijali alisema.
Avijawa kucheka anataka, kulia anataka. “Sijaelewa hapo Pawasa na Nteze… Nd’o umemaanisha nini?” Avijawa alihoji. Sijali akamtazama bila kummaliza shogaye.
“Pawasa ni sawa na elfu tano, wakati Nteze ni sawa na elfu kumi. Kwani umezaliwa lini wewe hadi usijue misemo hiyo?” Sijali alisema huku akimsaili Avijawa.
"Enhee, ikawaje?” Avijawa aliendelea upekuzi wake
"Kiasi cha pesa nilichomuomba kanipa nusu, akasema nusu iliyobaki niende siku nyingine, nikakimbizane tena na matairi ya gari," Sijali alisema.
"Mmmh, mwenzangu atakuua!" Avijawa alisema.
"Aaka, cha kujifia kitu gani!" Sijali alisema.
Kidogo, Amina akawa keshafika, akamkabidhi kidonge dada'ke. "Sasa mbona maji hujaleta, n'tanywea mkojo wako au?" Sijali alisema kwa kufoka.
"Bwana we, n'tajua huko mbeleni kama mbivu ama mbichi..." Alisema Sijali huku akidumbukiza kidonge cha indosidi kinywani kwake.
TANO
RAHA KARAHA!
Usiku ulipita, japo kwa mikiki hatimaye asubuhi iliwasili na vishindo vyake. Ufahamu ulimrejea Sijali, lakini hakuwa na hali. Mwili wote ulikuwa umedoda, viungo havitamaniki,
nyakanyaka.
Kila akijivuta kulia, kagosheka, akijivuta kushoto kagosheka. Umechacha jumla na si rejareja tena.
Mzeta huyo!
"Jamani, shida hizi! ‘Aya sasa si mateso ya kujitakia. Hata sijui niseme nimetoka kutafuta penzi au panzi? Maana sio kwa gwaride lile. Mtu mgumu kama kitu gani!" Sijali alijisemea nafsini huku akiyasikilizia magumu aliyopitia.
Akajitoa kitandani pale, akaanza kutoka nje ya ua wao. Mwanga ulishatanda, kulikuwa kweupe kabisa.
"Amina, hivi saa ngapi sa' hizi?" Sijali alisema.
Amina akatazama saa ya simu yake, kisha akainuka kichwa na kumtazama dadaye, "Saa sita na nusu mchana!"
"Saa sita?" Sijali alimaka utadhani kakarahishwa.
"Ndiyo, saa sita!"
"Mbona hukuniamsha sasa?" Sijali alisema kwa kusikitika.
"Tangu lini hadi leo iwe ya pili ukataka uamshwe pindi ukiwa umelala? Si kila siku unasemaga tusikuamshe hadi uamke mwenyewe? Nd’o tumekuacha tena!" Alisema Amina kinongwa.
Sijali akainamisha kichwa chini. Akatulia tuli mithili ya maji ya mtungi. "
Utaratibu nimeuweka mwenyewe. Nisimtafute mchawi," Sijali alijisemea nafsini.
Bila kumwambia chochote mdogo wake, akatafuta maji yalipo na kuupoza mwili.
Huko chooni hata kuinua mkono tabu kwake, viungo vyote havina ushirikiano. Akiinama anahisi kama anavunjika. Anausikia mwili wote zinauma nyama zake.
Kila akigeuka koo, akirudi koo. "
Mwenzangu kama nimepandwa na tairi ya gari kumbe mtu," Sijali alijisemea peke yake. Akatoa matusi yote ya nguoni kwa Mzeta ili kukonga mtima wake. Huyo Mzeta mwenyewe hata amporomoshee matusi gani, hayasikii na keshazoea lakini kwake hewala! Tusi kwa mhuni kama Mzeta ni sawa na pambio tu!
Alimvua nguo mamaye Mzeta, mjombaye, shangaziye, babaye na ukoo mzima. Alihisi familia yao ina laana, inakuwaje wawe na jitu kama Mzeta anayeivutia bangi sehemu za siri za mwanadamu mwenzake.
Kwa kujikongoja, alitoka chooni huku akiusikilizia mwili wake. "Dada vipi?" Amina alihoji baada ya kumuona dadaye akijivuta huku wajihi wote ukiwa umesimanzika.
"We acha tu. Ukikua utayaona!" Sijali alijibu. Amina hakujali majibu ya dadaye. Alimsogelea na kumkokota chumbani. Akaenda jikoni kumchukulia chai na mkate, akamfosi anywe walau apate nguvu ya kupambana na siku mpya.
"Hivi Avijawa alikuja?" Sijali aliuliza.
"Ndiyo alikuja, lakini nikamwambia umelala," alijibu Amina.
"Dah, nakusumbua kweli mdogo wangu..." Alisema kwa masikitiko Sijali.
"Walaaa! Kawaida tu," alisema Amina kisha akaendelea kumhimiza Sijali anywe chai. Akapiga funda kadhaa—akasindikizia na selesi ya mkate huku sura yake ikiwa imetawaliwa na maumivu makali.
*****
Huko mtaani, Mzetahakuwa na habari. Wakati Sijali hana hali, Mzeta kwa hakika hakujali kabisa. Laitani angelifahamu yaliyokuwa yanamsibu Sijali, wala asingethubutu kujitoa ufahamu. Mzeta aliketi na marafiki zake wakijisifu kwa ushindi wake mnono.
"Yaani, mwanangu ushaunga sana, ushapakua choo cha Mzee Mshamu unanuka mavi, umeshiba harufu halafu kibwege tu mtu anataka pauni?" Alisema rafiki mmoja aliyekuwa akichochea mambo kwa Mzeta.
"Wao kwani wanalijua hilo?" Mzeta alisema huku akipiga pafu zake kadhaa za sigara. "Wanadhani kuna mti unaenda kuchuma tu pesa!" Mzeta alijibu.
"Yeah, mtipesa upo Davis Corner, kuchuma tundapesa sharti uwe kama ulivyozaliwa!" Wahuni walisemezana maneno ya kukomoa jinsia tofauti.
“Wahuni wote peponi! Hatunaga unafiki—hiyo pekee pepo itatuhusu!” Mzeta alisema. Wenzake wakafurahi.
"Lakini babu ungempigia yule demu kumuuliza kaamkaje. Ili kutengeneza mazingira ya raundi ya pili," alisema yule rafikiye wa kwanza.
"Kweli bwana!" Mzeta alijibu upesiupesi.
Akainuka pale alipokaa na kuifikia simu yake, akatafuta namba ya mwisho kuongea na Sijali.
Simu inaita....
"Halo!" Sauti ya Amina iliitikia.
"Hujambo?" Mzeta alisalimia... "Sijambo, we’ nani?" Amina alihoji. "Naomba kuongea na Sijali," Mzeta alisema.
Amina akanyoosha mkono, "mh, simu yako hiyo. Sijui nani hilo?" Alisema Amina.
Sijali akaipokea!
"Halo!" Sijali alisema.
"Niambie honey!" Mzeta alisema.
Sijali likamtoka sonyo refu hata kama ungekuwa mita mia ungelisikia. Sonyo m’buruto.
"Vipi tena jamani, mbona masonyo?" Mzeta alihoji kiuhuruma.
"Mi' honey wako au mbuzi wako?" Sijali alisema.
Mzeta akatulia kwanza. Akavuta funda la mate kisha, akamfikiriaSijali.Mzetaakawa kama anataka kucheka kumbe siyo, akaendelea, "Mbuzi? Haitokuja kutokea kukuona wewe kama mbuzi!" Mzeta alijitetea.
"Alaa, kumbe!" Sijali alisema.
"Ndiyo, haitokuja kutokea!"
"Basi mwenzako naumwa. Ile mikito ya jana kama vile unavuna kokoto, imenitoa kifigo. Nataka hela ya hospitali!" Alisema Sijali.
Mzeta akakata simu baada ya kusikia habari za pesa.
"Nyooo! Kusikia pesa tu kakata simu. Malaya mkubwa!" Sijali alisema kisha akasonya tena na simu kuitupa juu ya meza.
"Watu wengine wanatuonaje sijui sisi wanawake, kwamba punda wao wa kubeba mizigo yao ya hamu ama kitu gani? Jitu halina utu hata chembe?" Sijali alisema kwa hasira huku akimwangalia Amina.
Amina asiseme kitu. Kidogo simu ikaita tena, Amina akaichukua. "Mmh, yeye huyo jama’ko!" Amina alisema.
"Lete hapa nimkomeshe mbwa huyu!"
"Shidaaa?" Sijali alisema kwa hasira.
"Polepole basi, pupa ya nini?" Mzeta alijifanya kumtuliza Sijali.
"Unakumbuka jana tuliongea nini?" Mzeta alihoji.
"Tuliongea nini?" Sijali alihoji.
"Kwamba kama uko fureshi hata leo turudie raundi ya pili," alisema Mzeta. Sijali akauchuna. Kimya kikapita baina yao. "Sema basi Sijali mbona huongei kitu?" Mzeta aliongeza.
"Halo!" Mzeta aliita bila Sijali kujibu.
"Halo!"
"Unasemaje?"
"Mbona asa 'uongei?"
"Niongee nini?"
"Kuhusu kubanduka raundi ya pili!"
"Hivi wewe una akili kweli?"
"Ndiyo, ninazo!"
"Huna!"
“Ninazo"
"Kama unazo ni za kuvukia barabara na pengine za kupandia bodaboda!"
"Si kweli hayo usemayo!"
"Ni ukweli mtupu!"
“Nimekwambia naumwa, wewe akili yako inawaza shimo kila wakati!"
"
Sasa urafiki wa mwanaume na mwanamke ni shimo na chepe la kuchimbia hilo shimo!"
"Mwanaume huna haya wewe!"
"Kasema nani?"
"Unavyoonekana tu!"
"S’o kweli"
"Tena nina hakika we’ kwa akili zako hata maiti unaweza kuingiza dudu lako!"
"Huko umefika mbali sana!"
"Haya, yaishe hayo. Tuma pesa basi niende hospitali," Sijali alisema. Kusikia tena habari ya pesa, Mzeta akakata simu.
Sijali akasonya tena na kuporomosha mitusi mizito kwa mamaye Mzeta. Akajiuliza sana na kumuonea huruma mama yake Mzeta aliyeshikwa uchungu na kwenda hospitali kujifungua toto kama Mzeta, leo hii linaleta mtinginyiko mtaani.
"Sasa nishajua njia ya kukata maongezi na huyu mbwa," Sijali alisema kwa hasira huku akijapiza kufanya jambo baya. Akatuna kwelikweli. Kifua kimejaa na kisirani kipo mlangoni. Kimejitundika vyema usoni mwake.
"Kwani huyo bwana yupoje maana toka jana mnamzungumzia tu!" Amina alisema.
"Em nitokee ‘apa na wewe! Umbeya tu!" Sijali alisema kwa hasira kisha akainuka pale alipokuwa ameketi ukumbini na kutoka nje kabisa ya ua.
Aliwaza sana maisha haya ya kutegemea mwanaume kama mkombozi wako wa maisha. Akataka kumlaumu shogaye Avijawa aliyemshawishi kujiingiza udangani, lakini roho ikamsuta. Akaendelea kusafiri kimawazo hadi nchi ya mbali.
"Wanawake tunakwama wapi?" Alijisemea Sijali.
Lindi la mawazo lilimkumba Sijali kwelikweli. Akifikiria machungu ya jana na maudhi ya nafsi anayopata mchana huu baada ya kupokea simu kutoka kwa Mzeta, hana hamu. Yu njiapanda.
SITA
SIJALI!
Visa na mikasa ya Sijali yamejawa na mengi ya kiza.
Kama mwenyewe alivyosimulia hapo chini.
Jina langu ninaitwa Sijali Salum Kunyoma. Najua unachofikiria kichwani mwako, kwamba maisha haya nimeyachagua mwenyewe, hivyo yote yanayonifika ni sawa tu.
Ndiyo, ‘kweli ni chungu kwa msemwaji, lakini ni tiba kwa msemaji.’ Tapika nyongo ukonge mtima, usibebe vitu kifuani havifai kwa afya.
Nina hakika kabisa mioyoni mwenu watu wa jinsia tofauti na mimi munafurahia mateso ninayopitia na kujisemea nafsini kwamba mimi nimeyataka. Sasa ninakuhakikishia sikuyataka maisha haya, ila maisha yamenitaka mimi niwe hivyo.
Ngoja kwanza nikusimulie nilipotoka; Sijali mimi ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu katika familia yetu. Wa kwanza kaka, wa pili mimi na wa tatu Amina. Huyuhuyu kiziwanda unayemuona ninatumia simu yake kwa matumizi yangu.
Sijali mimi, nilikuwa na maisha yangu, kwa mume wangu kabisa wa ndoa—pika, pakua. Ndoa yenye nyingi rutuba ya huba. Mume nilimpenda akanipenda, kifupi tulipendana. Husda dada. Husda za walimwengu zikaingia ndoani. Kuna nini tena?
Si unajua tena mambo ya wanaume na wanawake, mume akaingia mkenge wa mwanamke aliyekuwa akiishi jirani nasi, dada la Kimanyema hilo. Tako tako, miye dera tu linapepea, akataka minyama mtu.
Hakuridhika kunichukulia mume wangu, akafanya ulozi akawa mke wa pili. Zamu ikapangwa, siku tatu kwake, siku tatu kwangu, ikifika zamu yangu dada mume hali, halali, wala hanioni, ndani kunamshinda, anarudi kwa Bi. mdogo.
Mmanyema kapindua meza, badala ya mimi kuwa mkubwa, nikawa mdogo. Polepole ahadi zikawa hewa, zamu zikafa, akawa kila siku huko kwa toto la Kimanyema, Mmakonde n’na maajabu gani?
Kwa vile yule alikuwa mume wangu mwanzo—kabla ya kuwa mume wetu, nikaenda huko kwa lidada la Kimanyema. Sikugonga mlango niliingia tu mpaka ndani. Nilisubiria muda ambao ninajua fika mume wangu atakuwa nyumbani.
Kufika nyumbani kwake, maana tulikuwa tukiishi Mbagala Zakiem, lakini huyu mshenzi alipangiwa Kijichi. Nikajitoma ndani, nikawakuta katika huba zito. Mguu wa Mmanyema juu ya paja la mume wangu, wakilishana tufaha kwa mahaba yote.
Moyo ulipasuka, nikachomoka mbio hadi mwilini kwa Mmanyema, sikuongea sana, nikamzaba vibao vitatu madhubuti, mume akanishika mikono ili nisiendelee kulipiga pendo lake jipya. Kosa kubwa alilofanya kunifunga mikono yangu, Mmanyema akaitumia fursa hiyo kunitandika konde moja madhubuti—jicho likaanza kutoa maji palepale.
Nikajichomoa mikononi mwa mume wangu, nikainama chini kupambana na maumivu ya konde hilo, “Ulivyo mshenzi, huchagui pa kupiga,” nilisema kwa hasira sana.
“Vita haina macho,” alijibu Mmanyema. Nikajikaza, nikainuka na kutaka kumvamia tena, lakini mume wangu alikuwa zaidi upande wa mke mpya. Akanizaba kibao kimoja matata sana, “em tulia, unaleta fujo nyumbani kwangu,” alisema mume wangu.
Kauli hiyo iliniumiza sana, inakuwaje mumeo anasema unaleta fujo nyumbani kwake, ina maana kwangu si kwake?
“Kwa hiyo mi’ mgeni hapa, wala sina haki ya kulilia mume wangu nikiona umepotea moja kwa moja?” Nilisema huku machozi yakinitoka. Mume asijali nililosema, akasonya. Akarusha mikono yake mithili ya mtu aliyechanganyikiwa. Nikiwa bado nimeweka mkono shavuni, mume akatoka pale alipokuwa na kwenda kumuinua Mmanyema na kumfunga na mikono yake kimahaba.
Dhahiri nikajua sina changu. Mbona sikuinuliwa?
“We’ fanya tu wende, sihitaji kukuona, na kuanzia leo sio mke wangu,” alinitamkia mume wangu. Maneno ‘
na kuanzia leo sio mke wangu’ yalikuwa kama ngoma iliyokuwa ikijipiga masikioni mwangu kila baada ya sekunde.
Kichwa kikaanza kuzunguka, mawenge yakanishika, dunia ikawa nzito kwangu, nikajishika kichwa kuitafakari, kelele za ‘
sio mke wangu’ ziliendelea kujirudia kwa wingi kiasi nikajikuta naenda chini tii.
Nilikuja kuamka siku ya pili mchana wake, nikiwa hospitalini kwetu, Buza. Hata sijui vipi nilifika nyumbani lakini nilikuta maelezo mengi kutoka kwa ndugu na jamaa.
“Sijali mwanangu, mumeo kakurudisha hapa na gari lake akiwa na mke mdogo. Hakuongea maneno mengi, alisema umeanguka baada ya kwenda kufanya fujo nyumbani kwa mke mdogo. Hivyo kasema kakuvumilia sana kwa tabia zako za kumchukia mke mdogo bila sababu.Talaka yako hii hapa. Rasmi amekurudisha nyumbani!” Alisema mama kisha kama aliyetaka kuendelea kusema jambo, nikamsimamisha.
“Kama linahusu mume wangu naomba achana nalo,” nilimjibu mama. Akawa kimya, akanitazama usoni huku akimeza funda la mate.
“Sasa unafanyaje?” Mama alihoji. Sikumpa jibu la haraka.
“Je, kakwambiaje kuhusu kugawana mali tulizochuma wote?” Nilimwuliza mama.
“Hakusema chochote kuhusu mali wala nguo zako. Kakurudisha wewe kama wewe tu!” Alisema mama. Nikaingiwa tena na hasira. Moyoni kwangu kulikuwa kama kunapita kiwembe kikali sana kinachonikata bila huruma.
“Kwani nimemkosea kitu gani?” Nilijiongelea nafsini mwenyewe.
“Wapi nilipokwama?” Nikaona kuliacha hili jambo mikononi kwa Mungu, itakuwa kosa kubwa. Mungu kamuumba Mmanyema na Mungu hajamtuma aingie maishani mwangu isipokuwa shida na hashuo zake.
“Sitokubali” Lilinitoka mbele ya mama. Mama akanisihi sana nisitumie hasira katika kutafuta haki yangu bali busara itawale. Sikuwa na hali ya busara tena. Busara humwendea mwenye busara, walo-washenzi huendewa kishenzi vivyo-hivyo.
Siku ya tatu tangu nianze kuhisi nina afadhali kiasi kwamba ninaweza hata kutembea, nikajikusanya na kurudi hadi Kijichi, huko anakoishi na malkia wake. Nikapiga hodi safari hii kuondoa shida zisizo na lazima. Akaja Mmanyema, nywele zilikuwa kazichanua tayari kwa msuko mpya. Mwenzangu anasuka nywele, mi’ nasuka kinyongo. Kaenea mlangoni, ule mkao usiingie humu.
“Huyo bwana yupo humo ndani!” Nilimwuliza. Akaendelea kunisaili mithili ya kinyago kimesimama kumbe ninaongea na nina utashi kama yeye. Kupata kuna mambo jamani! Mhh sina hata la kusema.
“Sema shida yako n’taifikisha kwake,” alinijibu kidharau.
“Siwezi kukwambia wewe shida zangu,” nilimjibu. Zogo likaanza tena. Mabishano yakawa mengi hatimaye mume akatoka.
Usoni kwake, alikuwa hana nuru kabisa. Inaonekana hili jambo limemkwaza. Huenda hakufurahia kuniacha. Nilihisi.
“Kuna nini hapa?” Aliongea kwa hamaki kidogo.
Si mimi wala Mmanyema aliyeweza kujibu swali la mume,
“Nijibuni basi kuna nini hapa
?” Mume aliongeza. Sikujibu kitu, badala yake, nikaingiza mkono pochini na kutoa barua ya wito kwa serikali ya mtaa.
“Barua hiyo wito kuja mazungumzoni serikali ya mitaa,” nimlijibu. Akanitazama kuanzia juu mpaka chini utadhani anakagua mti wa mwembe uliohujumiwa na wezi, kisha akainua ile bahasha juu kabisa huku akiichungulia juani. Akashusha mikono yake, akashika upenuni mwa bahasha halafu akaichana. Akatoa barua nakuanza kupitisha macho polepole huku akichezesha midomo yake—baada ya kumaliza akainua kichwa na kunitazama.
“Mpuuzi wewe mwanamke,” alisema kisha akanisindikiza na sonyo.
“Siendi na siji popote pale!” Alisema kwa hasira mume wangu. Akawa anaongea maneno mengi ya kuudhi nafsi huku akichezesha ile barua kama kitu kisicho na maana, hatimaye akaichanachana.
“Nenda kawaambie hao mabwana zako kuwa, sina muda wa kuja huko serikali za mitaa,” aliongeza mume wangu. Tukio hilo lilimkosha sanaMmanyema. Akawa ananicheka kwa shida zilizokuwa zikinipata. Tabasamu fupi alilitoa kinywani mwake wakati mume alivyokuwa akiniwakia kama mtoto mdogo. Nikataka kusema jambo, lakini nafsi ikanistopisha.
“Sawa, hakuna shida!” Nilimjibu. Kwa hasira, namimi nikaichanachana ile barua aliyoiacha kwa mama kama talaka mbele yake. Uso mkavu. Alinikata jicho hilo sio mchezo. Sikujali.
Nikarudi nyumbani, nikamuhadithia mama yote yaliyonisibu kwa mume wangu.Akanitaka niwe na subira. Subira ukawa msamiati niliouchukia kuusikia linapokuja suala la kumwachia mume wangu achukuliwe na mwanamke mwingine kizembe.
Nikajikaza, japo fundo lilinikaba lakini bado nilikuwa imara. Saa, siku, wiki ikapita. Nilikuwa mtu wa kujifungia ndani tu, kwi-kwi ilinikaba sipati-kukwambia. Nikajiuliza, hata nikilia, mume atarudi? Hapana!
Hatorudi na vilio havitamrejesha. Nikaanza kujipanga, hili jambo liwe kisheria zaidi badala ya lawama na chuki. Niko nyumbani, sina kivazi cha maana zaidi, karibia nguo zangu zote niliziacha kwa mume huko Mbagala.
Nikaamua kufunga safari hadi Mbagala kwa minajili ya kufuata nguo zangu ili ziweze kunisaidia katika safari zangu. Isitoshe, nilikuwa na kiji—akiba changu nilikiacha kitanisaidia katika safari ya hapa na pale.
Safari ni hatua kwa wasonia, wenye nia ni kama bamia tu. Nilifika katika mji wangu, nikaanza kupekua funguo zilipo ili nifungue mkuu wa mbele.
Chakura, chakura, hatimaye nikazipata, nikachomeka katika tundu lake. Lakini mwonekano wake ulikuwa hauendani kabisa na kishimo cha funguo za-geti. Nikalazimisha—bila mafanikio. Nikiwa katika harakati, kidogo nikahisi geti linafunguliwa.
Nikatulia kuona matokeo ya mfunguaji wa mlango. Sura iliyotokea mlangoni ilisababisha nianze kupata mkorogo toka tumboni, ngurumo na hasira zilizokuwa zikipita maungoni mwangu hazielezeki. Nikajikuta pumzi zinaenda mbio bila mpangilio. Hamaki na chaguzi nyingi zikatawala akili mwangu.
“We’ mbwa unafanya nini nyumbani kwangu?” Lilin’toka neno bila kutegemea. Hakujali wala kushituka mpuuzi wa Kimanyema—nd’o kwanza akanianzia juu mpaka chini. “Nikuulize wewe kiroboto mtia watu upupu,” alijibu Mmanyema.
“Hapa ni kwangu, nini kimekuleta?” Niliongeza. Kabla sijafikiria kujitoma ndani, akabamiza mlango nikabaki nje bila kutegemea kama angefanya kitendo hicho. Kumbe hata zile hangaika zangu za kufungua mlango hazikufanikiwa kwa sababu tu, nyumba walibadili vitasa.
Hasira zikazidi kunipanda baada ya kugundua nyumba yangu imevamiwa na shetani-mtu.
Ngo-ngo-ngo!
Nilibamiza lango kwa nguvu ili aje afungue. “Fungua mlango we’kengemaji,” nilisema kwa hasira huku machozi yakianza kunilenga. Hasira ikawa mali ya akili yangu kwa muda wote niliosimama. Kadiri alivyokuwa hajibu ndivyo nilivyozidi kufura.
Makelele niliyopiga yaliamsha hisia za majirani wengine na kuamua kusogea eneo la kisanga cha mama mwenye nyumba aliyegeuzwa kuwa mpangaji.
“Sijali vipi tena mbona hivyo?” Dada mmoja jirani yangu wa zamani aliyejulikana kwa jina la Mama Brian. “Si huyu mbwa kavamia nyumbani kwangu wakati mwenyewe niko katika matatizo,” nilimjibu Mama Brian.
“Tulia basi utavunja huo mlango!” Alisema Mama Brian. Nikatulia kidogo kuvuta pumzi ili nilianzishe tena. “Huyu mshenzi amefanya maisha yangu yamekuwa magumu sana,” nilimjibu Mama Brian. Ma’ Brian akajaribu kunituliza, “basi fanya mambo polepole ili upate mwafaka,” Ma’ Brian alisema.
“Mwafaka gani mwingine mbali na mimi kuingia humu ndani,” nilimjibu Ma’ Brian. Kutokana na bwato nililokuwa nikilitoa tangu kugundua mji wangu umevamiwa, kijasho na uchovu wa nafsi ulianza kunivizia konani. Baada ya makelele kuwa mengi, mume akatoka nje akanikuta miye tena ndiyo naelekea chini kwa presha na hasira.
Yakawa yaleyale, nilijikuta nimeamkia hospitali ya Temeke, chumba maalumu cha watu mahututi. Zaidi ya nesi, hakukuwa na mtu mwingine upande wa ndugu zangu wala mume.
************
“Nimefikaje hapa?” Nilimwuliza nesi aliyekuwa akipitapita kando yangu huku kijasho kikinitoka. Nesi akasimama, akanisogelea mahali nilipo, “Unaendeleaje?” Nesi aliniuliza badala ya kujibu swali langu.
“Sijambo, haya, niambie nimegundulika n’na nini safari hii? Ndugu na jamaa zangu wako wapi? Mume je?” Nilimfungashia rundo la maswali nesi wa watu na asiweze kujibu hata moja.
“Nakuja dada sasa hivi, ngoja nikuitie daktari aliyekuwa akikuchunguza huenda akawa ana majibu,” nesi alijibu huku akiondoka eneo langu na kuelekea nje alipo daktari. Hasira, hasira mtindo mmoja.
Ninatamani kuelewa ilikuwaje, na hii tabia ya kuzima wakati wa mambo yanataka kuwa matamu itaisha lini. Nilisubiri kwa dakika kadhaa bila kutokea mtu, nikaanza kubawabu kwa kina.
Haiwezekani.
Haiwezekani mimi kuendelea kubaki hapa ilhali ninafahamu fika kuwa nimedhulumiwa haki yangu. Nimedhulumiwa mume na nipo njiani kudhulumiwa na nyumba. Nikiwa katika lindi zito la mawazo, akili ikanirudia, kujitazama, nilikuwa nimechomekewa dripu, vimajimaji bado viliendelea kushuka. Nikajitia kuinuka, jaribio la kushusha mguu chinilikashindikana. Mguu ulikuwa mzito kuinuka, nikajiinua angalau nilalie lichuma la kitanda upande wa kichwani, lakini bado nalo lilishindikana.
Nikaanza kugaagaa kitandani. Nikiwa katika juhudi za kujikwamua na mkwamo wa hospitali, kidogo nikamuona daktari na nesi aliyeniahidi kwenda kumwita wanakuja wanguwangu.
“Pole, Sijali!Naona huelewi kitu. Vipi unaendeleaje?” Daktari alihoji. Nikabaki namtumbulia macho tu nisijue cha kumjibu. Lilikuwa fumanizi la nguvu la kutaka kujinasua kitandani pale.
“Sijambo! Nashukuru.Haya, nimefikaje hapa?”
“Uliletwa na kijana mmoja aliyesema ulikuwa mumewe zamani!”
“Mumewe zamani?”
“Ndiyo!”
“Kasemaje neno lingine?”
“Kwamba nikuhudumie mpaka upone na gharama ni juu yake, ila tu, ameniachia kikaratasi hiki hapa!” Dokta alisema kisha akanikabidhi.
Mkono ulikuwa mzito kupokea karatasi ile. Sikujua ni nini kilichomo, lakini dhahiri niliona jicho la shari likinitizama kutoka kwa nesi na daktari wake.
Sekunde kadhaa baadaye, nikabadilika kabisa baada ya kuisoma ile karatasi.
“Mjinga sana huyu!Mpuuzi wa kutupwa!Kenge kasoro mkia… sasa nitamwonyesha mi’ ni nani… maana ameanza kunipanda kichwani!” Nilisema kwa hasira huku nikiifinyangafinyanga ile karatasi,nikaitupa chini.Baada ya sekunde chache, nikamwomba nesi anirudishie karatasi yangu. Nesi akaikota na kunikabidhi.
“Pole dada,” alisema nesi baada ya kunikabidhi karatasi yangu. Nikashusha pumzi, nikainua uso wangu kumtazama daktari aliyesimama mbele yangu bila kusema chochote pamoja na povu kilo tano nilililolimwaga bila kulizoa. Pembezoni kulikuwa na wagonjwa wengine walinitazama tu bila kusema chochote kwa hakika walifahamu nimekwazika. Nyuso zao zilionekana kunishangaa sana.
“Lini natoka humu ndani? Halafu naumwa kitu gani” Nilimwuliza kwa ukali daktari. Daktari akashika jalada lake vyema, akaanza kupitia. “Ni presha tu ilikuja kwa kasi. Si jambo kubwa sana!” Alisema daktari.
Akaweka ukimya kwa nukta chache kisha akasema.
“Subiri baada ya saa zima utakuwa sawa, kisha tutakuruhusu uende zako!” Alisema daktari. “Lakini nisingeshauri uende peke yako mahali kokote pale bila ndugu zako waje maana hata itifaki zinanifunga kumruhusu mgonjwa kutoka peke yake,” daktari aliongeza. Nikatulia kwanza, nikashusha pumzi ndefu.
Nikaitazama dunia kwa marefu na mapana, nikajiwazia shida hizi nimeumbiwa miye tu au hata wenzangu nao wanazipata? Punde tu nikatopea tena ulimwengu wa mawazo. Daktari akahisi hiyo hali, “unazo namba za nduguzo kichwani, ninaweza kukusaidia simu yangu,” daktari alisema. Sikufikiria mara mbili kama simu yangu ina pesa au la. Nikaitumia fursa ya bure.
“Ndiyo ninayo!” Nilijibu upesiupesi—maana ilikuwa hakuna namna tofauti. Nikamtajia namba za Amina, akampigia.
Simu ikaita.
Ikaita tena na tena.
Amina hakupokea.
Akapiga tena.
Ikaita. Akiwa anakaribia kukata tamaa ndipo akasikia ilipokelewa na kuitikiwa.
“Halo!” Amina aliitika.
“We’ kwani vipi na hiyo simu yako jamani?” Nilibwata kwelikweli kwa Amina. Amina hata asijibu kitu. “Si nimekuuliza, inakuwaje na hilo simu lako?” Niliongeza.
“Nilienda kisimani, n’taendaje na simu?” Amina alijibu kwa hasira. “Lakini hiyo simu ya mkononi na si ya mezani!” Nilimjibu tena kwa kufoka.
“Babu eh sema shida yako, achana na mambo ya simu ya mkononi,” Amina alijibu tena kwa hasira kisha akanirushia na sonyo. Nikatulia sasa kuona namna bora ya kumfikishia ujumbe.
“Basi yaishe mama… yaishe mdogo wangu kipenzi. Nina jambo nataka kukuambia,” nilisema kisha nikaweka tuo.
“Jambo gani?” Amina alihoji. Kimya kikapita baina yetu.
“Mje mnichukue hapa hospitali ya Temeke!” Nilisema huku nikiwa nimehamanika.
“Hospitali?” Amina alishtuka, akawa kama kachanganyikiwa kwa habari ile.
“Ndiyo, kwani hupajui?”
“Sio sipajui!”
“Kumbe je?”
“Siye tukajua umelala kwa mumeo, mambo yameisha—maana dada kama wewe hukurudi jana!” Amina alijibu kwa kejeli.
“Mwenzangu, ni stori ndefu. Mje tu kunifata hapa tutaongea tukiwa njiani!”
“Mmmh, makubwa. Dunia hii!” Amina alisema kisha akakata simu.
“Ahsante daktari kwa msaada wako,” nilimshukuru daktari.
“Haina shida… ila tu, punguza hasira. Naona kuna siku itakuja kuwa mbaya zaidi ukiendelea na hasira za namna hii,” daktari aliongeza.
“Ahsante, nitaufanyia kazi ushauri wako!” Nilijibu tu, lakini kifuani nilikuwa na fundo limenifunga. Lilinitafuna kwelikweli hata pumzi zangu zilikuwa hazitoki vizuri.
Hasira, hasira, hasira. Nikawaza, nikimkamata yule mshenzi nitamtafuna akiwa hai na kumnywea na bia. Hali iliyokuwa ikipita maungoni mwangu, meno kukaza hadi nikachusha. Hasira mtetemo, uga ambao sikuwahipo kushiriki lakini sasa nina kadi ya uanachama wa chuki.
*****
Saa zima likapita, kwa mbali nikawa nasikia sauti la
konvoi la watu kutoka Buza likifika eneo la hospitali. Enhee! Si kwamba walikuwa wakipiga kelele, la hasha. Manukato bibi, manukatooo! Watoto wa Buza tunajuana manukato yetu hata kama ni gizani pua tu zitamtambua mtu wa Buza.
Dakika kumi baadaye, chomwaaa! Wamekuja vivuruge wa Buza: Amina, Avijawa, Chausiku na Sikudhani. Wakajaribu kudhibiti furaha zao ili wasilete taharuki mule hospitali. Wengine wakaambiwa wasubirie nje kidogo ili utaratibu wa kumruhusu mgonjwa ufanyike.
Wakafanya yao kisha tukaruhusiwa. Mume alikuwa keshalipa kila kitu. Dokta hakuniambia kikubwa sana kinachonisumbua, lakini zaidi alisema nipumzike na nisifanye kazi ngumu. Kama haitoshi, alinitaka nisiwe mtu wa kupandisha hasira kila wakati.
Mashoga moto umewashika, wanataka kujua kilichonisibu. Kama nimepigwa kitu cha kichwa ieleweke, lakini pupa zao nikazizima ki
-starring.
“Haya, bibi kama wewe, nd’o vipi hivi tena kuamkia hospitali badala ya nyumbani?” Avijawa alilianzisha huku akirusha vidole vyake hewani.
Nikatulia kwanza nikiyasikilizia yaliyokuwa yakiendelea kusawili mwilini mwangu. Maana kizigo si kizigo, basi tafrani tupu.
“Mwenzangu hata kuuliza hali yangu kwanza eh?” Nilimjibu kwa masikitiko Avijawa.
“Hali gani tena na ushatoka hospitali?” Avijawa alisema.
“Hata kama!”
“Hata kama hiyo veepee?”
“Eeeh, ilikuwaje?”
“Em niwache… sina la kujieleza kwako. Si wewe tu, hata nyie wengine!” Nilijibu huku tukiwa tunakaribia kituo cha daladala kwa mchechemo. Avijawa akatulia. Ananijua vizuri akili zangu.
Amina akaita Bajaji moja ili ituchukue.
“Kutupeleka Buza bei gani?” Amina aliuliza.
“Buku saba!” Dereva wa Bajaj alijibu.
“Mmmh, kakaaa!” Amina alisikitikia bei.
“Nd’o bei hiyo, sista!”
“Mi’ n’na elfu tano, kaka!” Amina alijibu huku akimrembulia jicho yule dereva wa Bajaji. Akaingia mzima mzima katika himaya ya Amina.
“Sawa, twendeni!” Alisema dereva wa Bajaji. Tukapanda mimi, Amina na Avijawa. Akina Sikudhani wakachukua nyingine kwa bei moja. Njiani vimacho vyao kutwa kuvitua machoni mwangu. Nikajifanya kama siwaoni vile, wajaa-laana wakubwa. Umbeya tu ulowajaa.
Amina hakutulia kabisa. Alikuwa mithili ya mtu mwenye jipu matakoni. Mara kakaa kushoto, mara kakaa kulia. Mara anichungulie, basi shida tupu. Kuondoa kiu yake, nikamkabidhi ile barua aliyoicha mume wangu.
Amina akaidaka upesi, akaisoma muda mrefu kuliko hata mimi mwenyewe.
“Sasa huyu nd’o kaandika nini? Mzima kweli huyu?” Amina alihoji.
“Em kwanza na mie nione”, Avijawa alidakia, lakini Amina karatasi aliishika imara. “Eeeh, eeh, msinichanie barua yangu. Polepole!” Nilifoka kidogo baada ya kuona mwelekeo sio mzuri. Wakatulia, nikatulia. Tukawa sasa twaangalia usoni.
Mithili ya askari vitani waliopigana kwa muda mrefu halafu uchovu ukawashika kwa mapambano. Wakatulia kutazamana huku kila mmoja akimvizia mwenzake aanze.
“Amina mpe barua Avijawa aisome!” Amina akanitupia jicho. “Mpe bwana!” Niliongeza. Amina akanyoosha mkono wake kinongwanongwa na kumpatia barua Avijawa. Hivyo siri hii ikawa wanaijua watu watatu kama si wa nne maana aliyeandika naye anajua.
“Mmmh maisha haya kuna watu wana…” Alisema Avijawa lakini kabla hajamaliza nikamdaka njiani, “Aya bwata tena! Bwata umati ujue kinachoendelea,” Avijawa akatulia kidogo. “Basi mama shika karatasi yako!” Avijawa alisema kwa nongwa mkononi.
Muda ukasafiri kama ilivyoada, tukafika nyumbani kwetu, ukumbini nikajitua huku nikitafakari kwa kina kinachoendelea kunitokea. Kwamba mi’ nd’o nimebandikwa shida pekee katika dunia hii au naitazama kwa woga tu?
Majibu hakuna!
Nikatopea usingizini kwa uchovu wa masindano yao tiba. Niliamka baadaye sana, hakukuwa na mtu yeyote sebuleni, lakini nilisikia maongezi kwa nje—uani kwetu. Nikajinyoosha polepole kisha nikajitahidi walau nitoke hapo uani.
Nilifanikiwa.
“Sijali vipi, unaendeleaje?” Amina aliuliza. Kwa uchovu, nikaitikia.
“Niko salama sasa tafauti na jana!” Amina akameza funda la mate, akataka kutia neno jingine. “Niwache, siko katika
mood ya kuongea sasa,” nilimkatisha jaribio lake la kutaka kuniongezea mzigo wa maswali.
Nikajisogeza hadi eneo la kizingiti cha mlango wa jikoni, nikajiketisha pale puu mithili ya mzigo uliotuliwa kwa uzito wa kubebwa.
Nikashusha pumzi kuubwa kabisa.
“Kichwa kizito mno—ninatamani kukitua!” Nilisema huku nikishika paji la uso.
“Pole!” Amina alijibu.
******
“Hivi n’tampata wapi Oswadi?” Nilimwuliza Amina.
“Nafikiri namba yake ninayo!” Amina alijibu.
“Em mpigie kwanza nina shida nae!”
“Shida gani tena, dada?”
“We’ mpigie, maswali mengi ya nini?” Nilimjibu Amina kwa kufoka.
Simu ikapigwa.
Haikuita milio mingi, Oswadi, akapokea simu.
“Halo!”
“Eh, Oswadi, Sijali hapa naongea!”
“Oooh, Sijali, mzima wewe?”
“Sijambo, unaendeleaje huko?”
“Sijambo, namshukuru Mungu, kwa kweli!”
“Nami pia, sijambo!” Nikaweka tuo kidogo kuruhusu mapishano ya maongezi.
“Nikusaidie nini, Sijali!”
“Bwana, nina shida, ukitoka kazini unipitie hapa nyumbani nina mazungumzo nyeti na wewe!”
“Sawa, nitapita hapo jioni nikitoka mihangaikoni kwangu!”
“Nitashukuru sana, Oswadi.”
Masaa matano baadaye, Oswadi alikuwa mlangoni nyumbani kwetu. Nikampa mkanda wote kisha nikamkabidhi barua aliyoicha mume wangu aisome.
“Naona wanakwambia huna chako tena. Mali zote zimeenda kwa mke mdogo na wewe hahusiki na chochote tena. Duh! Ina maana mumeo anataka kukudhulumu kila kitu chako mpaka nguo zilizobaki katika nyumba yenu ya Mbagala?” Alisema Oswadi kisha akaweka tuo. Kimya kikapita tena. Akashika kichwa chake huku akizubaisha nywele zake kwa mbele, mara nyuma. Akasisimama na kuanza kuumba hatua za karibu. Kenda kulia, kenda kushoto.
“Unataka tufanyaje sasa, Sijali,” alisema Oswadi aliyeketi chini baada ya kubawabu kwa muda.
“Mi’ nataka haki yangu tu, sitaki kingine.”
“Haki yako kivipi, yaani, kwamba upewe mgao wako au unataka kurudi kwa mumeo?”
“Kurudi nataka, lakini hilo haliko mikononi mwangu. Naona sio riziki tena, hivyo nipewe ninachostahili kisha kila mtu afe na hamsini zake!” Nilisema kisha nikashusha pumzi kidogo maana niliongea harakaharaka sana.
“Kama haitoshi, basi twende mahakamani ili mgao uwe wa kihalali, maana nikisema tugawane wenyewe haitowezekana. Wewe sasa mwanasheria ndo utaniambia nifanyaje,” nilihitimisha.
Oswadi akawa anajijadili peke yake.
“S’kia, Sijali. Tumwandikie barua ya kumtaka mazungumzo na mwanasheria wako yaende kidiplomasia kwanza kabla ya kufungua shauri mahakamani,” alisema Oswadi.
“Nani wa kuandika hiyo barua?”
“Nitaindika mimi. Nitaipiga na muhuri wangu ili kuonesha kuna u-
serious kiasi gani katika suala hili,” alisema Oswadi. Nikahisi moyo wangu unaanza kupata uhueini kiasi.
“Sawa! Andika. We’ nd’o unajua nini cha kuandika…” Nilimjibu.
“Sawa… nipe siku mbili hizi,” alijibu Oswadi. “Lakini…” Nikasita.
“Lakini nini tena, Sijali?”
“Nani atampelekea mume wangu hiyo barua?”
Oswadi akanitazama, kisha akatia neno. “Ni mi’ mwenyewe nitaipeleka kwa mjumbe wake halafu mjumbe ataifikisha kwa muhusika. Hata hivyo, tuanze kwanza mazungumzo naye mwenyewe, tukishindwa, twende baraza la kata kwa usuluhishi zaidi—na kama itatokea, elewa hapo kama itatokea imeshindikana kote huku, itabidi sasa tusonge mbele zaidi ili kupata haki yako stahiki,” alisema Oswadi.
Nikashusha pumzi ya nguvu, maana huo mlolongo haukuwa wa kitoto.
“Sawa, nitafuata ushauri wako,” nilimjibu Oswadi.
“Nipe namba yake,” Oswadi aliongeza. Nikamtajia, akaindika katika simu yake kisha akaondoka zake. Nikabaki na dhiki zangu zikiwa kichwani.
******
Siku zikapita, tukimsubiria Oswadi afanye kile kinachohitajika kufanywa ili tusilete magomvi na mikingamo baina yetu na mume. Katika hali ya kushangaza, Amina akapokea simu kutoka namba ngeni isiyokuwamo katika simu yake.
“Huyu nani tena?” Amina alisema kwa jazba. Nikamwambaia anipe, hakusita.
“Haloo! Nani mwenzangu?” Niliuliza baada ya kupokea simu.
Kimya! Hakuna sauti iliyoitika. Nikawa nasikia mihemo mithili ya mtu anayekimbizwa.
“Haloo! We’ nani mwenzangu?” Niliongeza swali la pili. Nikasikia sauti ya kumeza funda la mate, kwa makisio ya pumzi nilihisi kabisa huyu mtu kakwazika. Nikakata.
“Mtu mwenyewe haongei kitu,” nilimjibu Amina. “Basi kazi, mmmh!” Alijibu Amina. “Tena kazi kubwa si kitoto,” niliongeza. Kabla hatujakaa sawa, simu ikata tena. Namba ileile. Nikapokea.
“Halooooooooo—weeee’ nani?” Nilipokea kwa hasira na kelele sana ili kumkera. Sauti ikawa kimya tena..
“Kuna jambo kubwa litakutokea…
unless uwache kumfuatilia mume wangu—we’ ushaachika pambana na hali yako, kwaheri!” Sauti iliongea maneno hayo kisha akakata simu. Maneno yake yalinichoma kama msumari wa moto. Nilishikwa na uchungu ambao hauelezeki. Nilihisi kabisa kukabwa koo, mithili ya mtu anayetaka kusema jambo lakini sauti haitoki.
“Huyu mbwa nikimshika atajutraaa kuzaliwa!” Nilisema kwa hasira kisha nikatoa matusi mengi ya nguoni mfululizo. Nikamgeukia Amina, alishikwa na butwaa baada ya kuniona jicho limenitoka kama ndula huku mvurugo wa pumzi ukiwa mkubwa pasipo kifani.
“Vipi, dada, kwema?” Amina alisema. Nikarudi kwanza kuketi chini kabla ya kumjibu. Amina akanisogelea. Akaweka kiganja cha mkono wake juu ya kiganja changu. Akaanza kunipetipeti angalau nipunguze hasira.
“Hebu niambie, dada. Nini mbaya?” Amina alisema kwa upole huku akinipigapiga kimahaba mgongoni. Nikainua kichwa na kumtazama. Nikameza funda la mate angalau kilichonikaba kiniachie.
“Mmanyema huyo ndiye aliyepiga simu na kunitishia maisha,” nilimjibu Amina. Amina akamaka.
“Namba yangu kaipata wapi?”
“Atakuwa kaichukua katika simu ya mume.”
“Haiwezekani…”
“Inawezekana, kwa asilimia zote usipinge, Amina.”
“Sasa utafnayaje?”
“Sina cha kufanya, ninamsubiria Oswadi kwanza afanye yake kisha nd’o nijue ninaanzaje—anzaje.”
“Utamsubiria Oswadi mpaka lini?”
“Siku mbili hizihizi,” baada ya kumjibu hivyo Amina. Kichwa kikaanza kuuma sana eneo la paji la uso. Nikaanza kupiga kelele. Uvumilivu ukanishinda. Yalikuwa maumivu yasiyomithilika. Nimekuwa mtu wa misukosuko kila mara. Kichwa kilivyozidi, nikadondoka chini puu.
ITAENDELEA...