Riwaya ya Kijasusi; Mtoto wa Rais

Oh my God poti sina neno imebaki mwili tu ndo unatetemeka asante sana wanyumbani
 
Duh, hii kali, moto, hatari.
Safi sana mtunze na wewe unayepost.

Sent from my SM-A207F using JamiiForums mobile app
 
Kali sana, Tengo anashikwa mchana kweupe
 
[emoji16][emoji16][emoji16][emoji16][emoji16]
 
RIWAYA; MTOTO WA RAIS
Imeandikwa na Halfani Sudy
Simu 0652 212391

Sehemu ya Kumi na Mbili

"Karibuni sana wajumbe. Samahani kwa kuwaita tena kwa ghafla namna hii. Mkiona wito wa haraka namna hii najua nyote mnajua kwamba kuna dharura. Na ni kweli leo kuna dharura.." Donald Tengo alitulia kidogo kuongea ili kila mmoja yamwingie vizuri maneno yake.

"Tangu mwanzo kwa'kweli tumejitahidi sana kufanya kila tuwezalo ili kuhakikisha mipango yetu inakwenda sawa, lakini bado kuna kidudumtu kinatusumbua sana. Kuna adui mpya ameingia katikati ya mipango yetu. Adui huyo mpya ndiye aliyemteka Alexander, pia amewateka watoto wangu wawili wakiwa wanatoka shule. Leo hii alivamia nyumbani kwangu na kufanya uhalifu mkubwa sana na kwa bahati mbaya sana kaondoka na Kasiki yangu yenye siri zetu. Ndani ya hiyo Kasiki kuna siri kubwa sana za huu mtandao wetu, hivyo kwa weledi wa adui yetu ninaamini mambo yetu yatakuwa hadharani, katika mikono yake. La msingi ni kuhakikisha siri hiyo haisogei katika mikono mengine.." Donald Tengo alinyamaza tena na kuwaangalia wajumbe.

"Ni nani huyo adui anayekitafuta kifo kwa nguvu kiasi hicho?" Mjumbe mmoja akauliza.

"Adui yetu anaitwa Daniel Mwaseba. Ni mpelelezi kutoka kitengo maalum ndani ya idara ya usalama wa Taifa. Huyu kijana ni msumbufu sana. Amekuwa akitufatilia kwa siri mimi na Balozi Rwekaza. Na katika ufatiliaji wake amefanikiwa kufika hadi nyumbani kwangu na kuiiba Kasiki yangu yenye taarifa mbalimbali za siri" Donald Tengo alisema.

"Mh. Donald samahani kwa kusema hili. Kwa'kweli umetuangusha sana. Ni wewe pekee ndiye unayestahili lawama zote katika hili. Ulinzi hafifu umemfanya Alexander Helb akamatwe. Ulinzi hafifu umesababisha watoto wako watekwe. Na sasa limezuka hili jipya kabisa. Kasiki ya siri yenye siri zetu inaibiwa? Hiyo ni sawa na kutuvua nguo sisi wote. Unawekaje Kasiki muhimu mahali ambapo pameweza kufikiwa na huyo kijana?" Mjumbe mwengine aliuliza kwa jazba.

"Kasiki niliiweka sio sehemu rahisi kufikiwa, ilikuwa sehemu ya maficho sana. Hadi sasa sijaelewa kwa namna gani Daniel ameweza kupagundua mahali ilipokuwa Kasiki. Lakini wajumbe huu sio muda wa kulaumiana, ni wakati wa kujadiliana kwa kina na kuhakikisha mpango wetu unakamilika. Pia ni lazima tuhakikishe tunaitoa roho ya huyu kijana mfukunyuku" Donald Tengo alisema kwa kirefu.

"Ni kweli kabisa, huu sio muda wa kulaumiana. Huu ni wakati wa kupanga mikakati thabiti. Mimi ninaona kitu muhimu cha kufanya ni kumuua huyo kijana na kuhakikisha taarifa zote zilizopo katika Kasiki tunazipata. Pia ni lazima tuwatumie vijana wetu wa Bahari nyekundu kuhakikisha tunampata Alexander, tunawaokoa watoto wa Donald na kuipata Kasiki yake. Kisha mipango yetu iendelee kama kawaida" Balozi Rwekaza alisema.

"Upo sahihi Balozi Rwekaza ingawa hatujui zitachukua siku ngapi hayo mambo kukamilika. Kumbukeni muda hautusubiri sisi, na jukumu letu kuu ni kuhakikisha mpango wetu unakamilika haraka iwezekanavyo. Hivyo mimi nashauri tuyafanye kazi yote hayo kwa wakati mmoja. Yaani vijana wa Bahari nyekundu wamsake Daniel Mwaseba huku tukitafuta namna ya kumuua Rais Mark!" Mjumbe mwengine alisema

"Uko sahihi mjumbe, lakini, Je kuna mtu mwenye namna yoyote ya kumuua Rais Mark tofauti na ya kumtumia Alexander?" Donald Tengo aliuliza.

Mjumbe mmoja alinyoosha mkono na kuruhusiwa kuongea "Mimi nashauri tutafute muuaji mwengine aje kutekeleza hiyo kazi, kama alivyosema mjumbe kumsubiri Alexander ni kujichelewesha wenyewe, huku mipango yetu ikiendelea kuchelewa" Mjumbe mwengine alisema.

Kikao kiliendelea zaidi ya saa mbili, walikubaliana jinsi ya kutekeleza mipango yao. Baadaye, wajumbe wote walitawanyika kwa njia wanazozijua wao.

***

Daniel Mwaseba na Martin Hisia walikuwa sebuleni. Dakika saba zilizopita walikuwa wamerejea kutoka katika nyumba ya Donald Tengo. Walikuwa wametoka kutekeleza mpango wa hatari sana uliopangwa na Daniel mwenyewe. Mpango wa kujikamatisha ili aingie katika ngome ya Donald Tengo, akisubiri wakina Donald Tengo wafanye kosa lolote lile ili awaadhibu.

Na kweli, walifanya kosa..

"Kuna lolote jipya lililotokea hapa nyumbani?" Daniel aliuliza huku akimwangalia Hannan usoni.

"Nilikuwa nina wasiwasi sana baada ya kuzimika ile kamera. Sikuubariki mpango wako wa kujikamatisha mikononi mwa Donald Tengo. Usithubutu tena kufanya kitu kama hiko. Daniel, wewe ni wa thamani sana kwangu. Kuhusu hapa nyumbani kuna kitu nilikuwa sijakueleza ambacho nimekigundua katika mitandao ya siri ya kijasusi"

"Ni kitu gani hicho ulichogundua?" Daniel aliuliza kwa hamu.

"Katika kutafuta zaidi taarifa za Donald Tengo nimegundua kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na Mke wa Rais!...." Hannan alianza kuelezea.

"Madam Magdalena Lema!" Daniel alidakia kabla Hannan hajamaliza kuelezea.

"Ndio," Hannan alisema huku akibonyaza tarakilishi yake.

"Haiwezekani Bwana!" Daniel alikataa.

"Taarifa hizi hata mimi na Martin zilitustua sana tulipoziona awali. Hivyo tulianza kumchimba zaidi Mke wa Rais. Katika uchunguzi wetu tukagundua kuwa rafiki yake mkubwa ni mwanamke mmoja anayeitwa Salma Lungu. Tumejaribu kumchunguza huyo Salma Lungu lakini hatujapata taarifa yoyote kutoka kwake. Hakuna taarifa yoyote katika mtandao juu ya Salma Lungu" Hannan alisema.

"Naona mmekua sasa vijana. Kwa'sasa ninaamini hata siku nisipokuwepo nitakuwa nimeacha watu makini sana wa kufanya uchunguzi. Yaani mmechimba hadi mmegundua kuhusu Salma Lungu?" Daniel alishangaa.

"Daniel, unataka kuniambia unamjua Salma Lungu?" Martin alishangaa.

Daniel alikaa kimya akiwaza.

"Daniel!" Hannan aliita.

"Namfaham Salma Lungu, ni mimi mwenyewe ndiye niliyempandikiza katika nyumba ya Donald Tengo. Alienda pale kama mfanyakazi wa ndani lakini Donald Tengo alimlazimisha hadi wakawa wapenzi. Na huo ndio ulikuwa mpango wangu, kumchunguza Donald Tengo kupitia kwa mtu wake wa karibu, Salma Lungu." Daniel alisema.

"Kumbe huu mpango unaonesha ni wa siku nyingi sana na ulikuwa unaufahamu hata kabla hajagundua kuhusu simu ya Balozi Rwekaza. Ulikuwa unachunguza nini kwa Donald Tengo hapo kabla?" Hannan aliuliza maswali mfululizo.

"Ni kweli, huu mpango wa siku nyingi kidogo. Kulikuwa na taarifa mezani kwetu kwamba Donald Tengo alikuwa anajihusisha kwa siri na mtandao wa madawa ya kulevya, ndio maana nikafanya mpango wa kumpenyeza Salma Lungu katika maisha yake ili kumchunguza" Daniel alisema.

"Nini aligundua Salma Lungu katika upelelezi wake?" Martin akauliza.

"Salma aligundua mambo mengi sana ya siri yanayomhusu Donald Tengo, lakini mambo mawili makubwa ni kweli Donald alikuwa mshiriki katika mtandao wa siri wa Madawa ya Kulevya hapa nchini unaoshirikisha vigogo wakubwa sana. Na kingine aligundua Donald ana uhusiano wa siri wa kimapenzi na Mke wa Rais."

"Kumbe unajua Daniel. Kwanini sasa hajakamatwa kwa kujihusisha na mtandao huo wa Madawa hayo haramu?" Martin aliuliza tena.

"Bado tunakusanya taarifa za kina za kuweza kumtia hatiani Donald Tengo. Na pia tunataka kuhakikisha tunawakamata washirika wake wote katika mtandao huo haramu" Daniel alieleza.

"Kwanini hukutueleza hayo mambo kabla Daniel? na wakati tupo katika misheni moja?" Hannan aliuliza.

"Samahanini sana jamaa zangu. Sikujua kama uchunguzi wetu ungetufikisha huku, pia nilidhani kwamba hapa tupo katika misheni nyingine tofauti na ile niliyoifanya na Salma Lungu!" Daniel alisema.

"Ni nani hasa Salma Lungu? Kwanini hakuna taarifa zake sehemu yoyote ile katika mtandao?" Hannan aliuliza tena.

"Salma Lungu ni Elizabeth Neville! Nilimwingiza Elizabeth katika maisha ya Donald Tengo kwa jina la Salma Lungu. Donald Tengo hakujua kama Salma ni Mpelelezi kutoka kitengo maalum katika idara ya Usalama wa Taifa" Daniel alisema.

"Aisee!" Martin na Hannan walisema kwa pamoja.

"Ndio hivyo ndugu zangu, eeh tuendelee na haya tuliyoyapata kwa Donald Tengo, ilinipasa kwenda katika nyumba ile, maana nilivyoongea na Elizabeth aliniambia kwamba mpango wa kuwatumia watoto wake usingefanikiwa kumfungua Donald Tengo. Donald Tengo ana roho mbaya sana, asingewajari sana watoto wake. Yeye alishauri kwa namna yoyote ile niingie nyumbani kwake na akanielekeza mahali Kasiki ya siri ilipo na jinsi ya kuipata. Na sasa Kasiki tunayo mbele yetu, tuifungue tuone tutapata nini ndani yake?" Daniel alisema.

Martin Hisia aliisogeza ile Kasiki mbele na kuanza kuifungua..

Itaendelea..

Ofa ya leo wanagroup..
Soma msimu huu wa kwanza na wapi wa Mtoto wa Rais kwa sh 3000 tu.
Ni whatsapp 0652 212391

Na Red butterfly inapatikana kwa sh 5000.
Ni Whatsapp 0652 212391
 
RIWAYA; MTOTO WA RAIS
imeandikwa na Halfani Sudy
Simu 0652 212391

Sehemu ya Kumi na Tatu

Martin Hisia aliisogeza ile Kasiki mbele na kuanza kuifungua.

Dakika kumi na tano zilitosha kuiacha wazi Kasiki ya siri ya Donald Tengo. Ilikuwa Kasiki ya chuma ambayo kuifungua kwake ilihitaji ufundi wa kimakinikia na teknolojia. Daniel na Martin walihusika kila palipohitaji makenika wakati Hannan alitumia ujuzi wake wa teknolojia. Kuna muda walitumia moto wa gesi, kuna wakati walitumia risasi ya moto, mwisho Hannan alifanikiwa kuifungia nywila ngumu sana kwa kutumia ujuzi wa teknolojia.

Baada ya Kasiki kuwa wazi, Daniel alianza kutoa vitu vilivyokuwepo ndani ya kasiki ile. Juu kabisa ya Kasiki kulikuwa na pesa nyingi sana za Kimarekani. Walitoa mabunda kumi yaliyokuwa yamewekwa kwa juu na kuyaweka juu ya meza. Yalikuwa ni mabunda ya dola mia moja yaliyofungwa kwa pamoja. Baada ya mabunda kutolewa kwa chini, walikuta mafaili matatu na tiketi ya ndege.

"Kila mmoja ashike faili lake na kulisoma tuone kuna nini ndani ya mafaili haya" Daniel alisema wakati akiyagawa yale mafaili matatu kwa kila mmoja. Kukawa kimya kila mmoja akisoma faili lake, wote majasho yaliwatoka wakati wakisoma mafaili yale.

Nusu saa baadaye walikuwa wamemaliza, walibadilishana yale mafaili na kuanza kusoma tena. Baada ya kumaliza kwa mara ya pili, wakabadilishana tena, wakasoma kwa mara ya mwisho na kumaliza. Wote sasa wakawa wameyasoma mafaili yote matatu kwa wakati mmoja. Daniel akaiangalia ile tiketi, ilikuwa ni tiketi ya ndege ya shirika la ndege la kimataifa la Qatar ikionesha ujio wa mtu aliyeandikwa kwa majina ya mawili, Zayiid bin Khalifa. Kwa mujibu wa tarehe iliyoandikwa katika ile tiketi, ilionesha kwamba huyo Zayiid aliwasili siku tano zilizopita kutoka nchini Iran.

"Hannan, hebu jaribu kutafuta taarifa za huyu Zayiid bin Khalifa, ni nani haswa?" Daniel alisema akimwangalia Hannan.

Harakaharaka Hannan alianza kubofya tarakilishi yake, wakati Daniel na Martin wakisubiri kwa hamu kubwa sana taarifa za Zayiid bin Khalifa. Hawakuwa na wasiwasi wowote ule kwani Hannan alikuwa ni mchawi wa kike wa Kompyuta. Mtu mwenye kuweza kuvunja uzio wowote ule kwenye Kompyuta na kuweza kupata taarifa anayoitaka.

"Zayiid bin Ally bin Khalifa" Hannan alianza kusoma huku uso wake ukiitazama tarakilishi yake " Kwa mujibu wa mtandao wa Magaidi wanaotafutwa kwa siri na Serikali ya Marekani, Zayiid ni mmoja wa watu wanaosakwa sana na nchi hiyo. Zayiid amehusika katika matukio mengi sana ya kigaidi. Lakini tukio aliolifanya hivi karibuni ni kutengeneza kemikali ambazo zimetumika kuuwa wanafunzi hamsini na tatu katika chuo kikuu cha Harvard huko Marekani. Zayiid bin Khalifa ni kijana wa Kiiran mwenye umri wa miaka thelathini na tisa. Anahusishwa pia na mahusiano na kikundi cha kigaidi cha Alqaeda" Hayo ndio yaliyopo katika mtandao wa magaidi wanaotafutwa kwa siri na Marekani.

"Kwanini kuna orodha ya magaidi wanaotafutwa kwa siri? Vita ya magaidi ni ya kimataifa, siyo vita ya nchi mojamoja. Sasa kwa nini nchi ya Marekani wawe na orodha ya magaidi wanaotafutwa kwa siri? Huoni kwamba wangewaweka hadharani ingekuwa rahisi kuwakamata? Mimi ninaamini hata huyu Zayiid zingewekwa taarifa zake hadharani asingeweza kuingia nchini kwetu" Martin alisema huku akimwangalia Hannan.

"Upo sahihi Martin kwa kila ulichosema. Lakini njia hii hufanywa kwa malengo maalum. Marekani wana orodha yao ya magaidi wanaowatafuta kwa siri, lengo lao kuu ni kuondoa taharuki hapa Duniani. Hawapendi Dunia iwe na hofu sana juu ya Magaidi. Lakini pia kuwatafuta kwa siri inawapa uwanja mpana sana wa kuwakamata. Magaidi wanakuwa hawajui nguvu namna gani inatumika kuwasaka, hivyo ni faida kubwa sana kwa Mtafutaji." Hannan alimwelezea Martin.

"Umeelezea vizuri sana Hannan. Sasa turudi kuchakata taarifa za huyo Zayiid bin Khalifa. Donald Tengo ana tiketi ya mtu huyu hatari sana, kwanini tiketi hii iwepo katika kasiki yake ya siri? Ni kwa bahati mbaya? Zayiid ana rekodi mbaya sana za kigaidi, sasa kwanini huyu Zayiid aje hapa Tanzania? Kwa lengo gani? Na kwa'sasa yupo wapi?" Daniel aliuliza maswali mfululizo.

"Daniel umeuliza maswali mazuri sana. Lakini majibu ya maswali hayo yote yapo kwa Donald Tengo pekee. Ni yeye pekee ndiye anajua alipo Zayiid bin Khalifa na yeye pia anajua sababu iliyomleta hapa nchini" Martin alisema.

"Lazima tumsake Donald Tengo haraka iwezekanavyo na kumleta hapa. Tutaitumia siri yake ya kutoka na Mke wa Rais ili kumfungua kila kitu" Daniel alisema.

"Na haya mafaili?" Hannan aliuliza.

"Kama tulivyoona. Hiyo ni mipango ambayo imeshatekelezwa. Inavyoonesha hawa watu wanaweka mafaili ya mipango yao iliyotekelezwa kwa Donald Tengo, sasa tuna kazi ya kusaka mafaili ya mipango yao isiyotekelezwa bado. Lazima tujue mafaili hayo yanakaa kwa nani? Hapa tumepata ushahidi tu kupitia mafaili haya kuwa wao ndio walioiangusha ndege ya abiria ya Coastal na kuuwa abiria wote 356, pia wanahusika na mpango wa wizi mkubwa wa dhahabu huko Geita, na katika hilo faili la tatu tumeona ni wao ndio waliofanikisha mauaji ya Makamu wa Rais, Marehemu Jamal Mlimi. Kazi yetu sasa ni kuchunguza sababu za kufanyika matukio yote hayo matatu, bila shaka, Balozi Rwekaza na Donald Tengo watakuwa na majibu!" Daniel akasema.

Hannan na Martin wakaitikia kwa kutikisa kichwa.

"Sasa Hannan hebu iwashe simu ya Robin tuone kama tutapata chochote?" Daniel alisema.

Hannan akaiunganisha simu ya Robin na tarakilishi yake, akaiweka katika mfumo ambao hata mtu akiitafuta haitaonesha kama ipo mahali pale. Mara zikaanza kuingia jumbe mbalimbali. Hannan alisoma jumbe zote, jumbe ya sita kuingia ndio ilimstua sana.

"Daniel njoo uisome hii meseji" Hannan alisema huku uso wake ukiwa katika tarakilishi.

Daniel alisogea hadi katika meza iliyokuwepo tarakilishi ya Hannan, na kuanza kusoma ujumbe. Ujumbe ulisomeka hivi..

'Robin, vipi umejua mahali mzigo wa ZAK ulipo?'

"Nini kinachokupa shaka juu ya ujumbe huu Hannan?" Daniel aliuliza baada ya kuusoma na kutouelewa.

"Bila shaka huu ujumbe ni fumbo, na kilichonifanya niutilie wasiwasi hivyo ni anuani ulipotoka ujumbe huu"

"Umetokea wapi?" Daniel aliuliza.

"Ujumbe umetoka katika kompyuta iliyopo katika makao makuu ya ujasusi Marekani!"

"C.I.A?" Daniel alishangaa.

"Ndio. Na umetumwa nusu saa iliyopita. Nimeshangaa maana Robin alisema ameacha kazi C.I.A, kwanini ujumbe huu utokee hukohuko C I.A, Bila shaka Robin alitudanganya" Hannan alisema.

"Inavyoonesha Robin aliingia hapa nchini kuusaka mzigo wa ZAK na ndio maana C.I.A wanauliza kama amefanikisha kuupata. Swali la kujiuliza ni mzigo gani huo wa ZAK? Na upo wapi? Cha kukatisha tamaa mtu pekee wa kujibu swali hii amejiua.."Martin alisema kwa kukata tamaa.

"Kwakuwa Robin aliletwa na kina Donald Tengo bila shaka watakuwa wanajua juu ya mzigo wa ZAK. Sasa jukumu letu kuu ni kumsaka Donald Tengo popote pale alipo. Ni yeye pekee ndio tumaini letu" Daniel alisema.

"Kwa tulichomfanyia Donald Tengo lazima sasa atakuwa amejipanga zaidi kiulinzi. Tunahitaji silaha za kutosha katika mapambano haya. Mimi na Martin tutaenda nyumbani kwangu kuchukua silaha kisha tutarudi tena hapa. Hannan hakikisha usalama wa watoto wa Donald. Tunaweza kuwatumia baadae itakapobidi"

"Sawa Daniel, watakuwa salama"

Daniel na Martin wakachukua gari kuelekea nyumbani kwa Daniel Mwaseba.

Itaendelea...
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…