WAKALA WA SIRI 07
Mtunzi; Robert Ng'apos Heriel
0693322300
ILIPOISHIA
Baada ya masaa matatu, Stanslaus alizinduka. Alijikuta yupo kwenye kichumba kidogo kisicho
na dirisha chenye giza. Alikumbuka mara ya mwisho alikuwa akipigana na Fernanda, sasa
akajiuliza yupo wapi, na nani aliyemleta. Kabla hajafika mbali katika kujiuliza, mlango
ukafunguliwa na Fernanda akatokea.
INAENDELEA
“ Habari yako, Stanslaus Mahige, muuaji mahiri. Unajionaje?” Fernanda alimsalimia Stanslaus huku akitabasamu kwa dharau.
“ Nimekaa na wewe zaidi ya masaa matatu ukiwa huna fahamu, kama ningeamua kukuua ningekuwa nimeshakuua, sasa hivi ungekuwa ni maiti, tena maiti iliyokosa maziko. Lakini nimekuacha hai kwa sababu ya jambo moja tuu. Hilo ndilo litakuwa dhamana yako. Usiponambia nakuhakikishia utakufa kwa uchungu mwingi sana” Fernanda alisema, kisha akamburuta Stanslaus mpaka kwenye chumba kingine kikubwa kilichokuwa na madirisha mawili. Alafu akambandua ile gundi aliyompachika mdomoni ili asiongee. Kisha akatoka akamuacha pale chumbani, kitambo kidogo alirejea akiwa na chupa ya wine na glass mbili. Akaiweka ile chupa kwenye stuli iliyokuwa pale chumbani, akamimina ile wine kwenye zile glass mbili. Kisha akaenda kumnyanyua Stanslaus na kumuegemeza kwenye ukuta.
“ Karibu Rafiki yangu, kunywa tufurahi, sisi ni marafiki kwa sasa, tusahau vita vyetu, fungua mdomo basi rafiki” Fernanda aliongea akiwa anajaribu kumnywesha Stanslaus wine. usisahau Stanslaus alikuwa amefungwa mikono na miguu.
“ Nambie nani amekutuma, unajua lolote kwenye jambo hili? Nambie rafiki muuaji usiye na huruma, nambie kisha nitakuruhusu uifyonze roho yangu itoke kwenye mwili wangu. Hautafurahi? Si ulisema wewe ni muuaji mahiri, sasa nataka unambie ukweli kisha uniue. Je hapo sitatenda haki kwako?” Fernanda aliongea akiwa anazunguka zunguka ndani ya kile chumba huku akiwa ameshika glass iliyojaa Wine.
“ Unataka nikuambie nini, mimi namtafuta Sajenti, adui wa nchi, huyo ndiye namtafuta, na sipaswi kurudi bila kuwa naye. Mimi ni muuaji mahiri, lakini leo nimenaswa na mshale laini wa mabua” Stanslaus alisema, macho yake yalikuwa yamejeruhika kwa kucha alizoshambuliwa na Fernanda wakati ule wakiwa wanapigana.
“ Mshale wa mabua! Haloo! Unamaneno sana rafiki muuaji. Haya tusipoteze muda, nambie unachojua kuhusu jambo hili” Fernanda alicheka kishambenga kisha kwa ghafla akabadilika uso wake ukawa wa mwanamke katili.
“ Kila usemalo wanalisikia, unajiingiza kwenye matatizo makubwa, ingefaa ungenambia alipo Sajenti huenda hiyo ndio ingekuwa ponapona yako” Stanslaus aliongea, maneno hayo Fernanda aliyaelewa. Akajua huenda Stanslaus amefungwa vifaa vya kurekodi sauti na wasiwasi uliongezeka pale alipohisi kuwa huenda hata muda ule kulikuwa na watu wanaomfuatilia na hawapo mbali.
“ Kelele nguruwe wewe! Utasema au husemi, eehe! Unadhani mimi natishwa na maneno yako ya kipuuzi, sasa utasema kwa mateso, wewe si hautaki kusema” Fernanda alisema huku akimshika Stanslaus sehemu nyeti. Stanslaus alipiga yowe kwa maumivu makali aliyoyasikia.
“ Nasema! Tafadhali niachie nitasema sasa, uuwhi!” Stanslaus alisema akijaribu kujitingisha mikono yake iliyofungwa na kubana mapaja ili kumzuia Fernanda asibinye nyeti zake. Maumivu ya kubinywa nyeti hayalinganishwi na maumivu yoyote yale, kubinywa nyeti ni adhabu kubwa na inayokaribia adhabu ya mwisho kwa mwanaume. Ilikuwa ni afadhali Fernanda amchinje lakini sio kumbinya makende yake.
“ Sema sasa, usifikiri nipo hapa kukuchekesha. Nambie nani kakutuma?” Fernanda alisema, akiwa kamuachia Stanslaus Nyeti zake.
“ Watu wabaya, wenye nia ovu na wasiolitakia mema taifa letu. Hao ndio wamenituma” Stanslaus alisema jasho likiwa linamtoka.
“Watu gani hao, sitaki maelezo mengi, wataje..” Fernanda alisema.
Ajabu ni kuwa kabla hajasema chochote Stanslaus alianza kulegea mwisho akapoteza maisha, Fernanda alishangazwa na hali hiyo, awali hakutaka kuamini kuwa Stanslaus amekufa, alidhani anamfanyia maigizo lakini ni kweli kabisa Stanslaus alikuwa ameaga dunia. Kilichomshangaza zaidi ni kuwa, stanslaus alianza kubadilika uso wake, macho yake yalibadilika na kuwa meusi tii. Hapo Fernanda akajua kuwa kilichomua Stanslaus kilikuwa ni sumu. Fernanda alienda kuchukua Gloves za mikononi akazivaa, kisha akarudi, ndipo akamkagua Stanslaus ili apate kujua kilichomuua ni kitu gani japo alishahisi ni sumu lakini alitaka kuhakikisha, akamgeuza kwa nyuma, looh! Alishtuka kuona chini ya kichwa karibu na shingo kwa nyuma ilikuwepo chipu ya kurekodia sauti. Akaigusa na mkono wake, alishangaa kuona kwa pembeni damu ilikuwa ikivuja kidogo kama kaupele kaliko tumbuka, aliposhika kale kaupele aligundua ndani kuna pini, hapo hapo Fernanda akaelewa ni kwa nini Stanslaus amekufa. Kilichomuua ilikuwa ni ile pini, ambayo iliwekwa makusudi nyuma ya kichwa karibu ya kisogo pamoja na ile chipu ya kurekodia. Pini ile huwekwa sumu maalumu ambayo endapo jasusi au mpelelezi akikamatwa na adui basi hujigongesha kwa nyuma kisha pini humchoma, na mara moja mtu hupoteza maisha. Basi Fernanda alihuzunika sana kwa kitendo cha Stanslaus kujiua kabla hajamwambia siri ya nani aliyemtuma na nani yupo nyuma ya uovu wote ule. Kwa upesi akamtoa stanslaus ndani ya nyumba na kumuingiza kwenye gari, nyuma ya buti. Kisha alirudi ndani, akasafisha nyumba kusudi kuondoa ushahidi wa aina yoyote ile. Ile meza ya kioo iliyopasuka kutokana na wao kupigana aliokota vipande vya vioo na kwenda kuvitupa kwenye shimo la taka lililokuwa nyuma ya mabanda ya kuku ya nyumba hiyo.
Jioni ilifika, Fernanda alitoka akiwa na gari alilobeba maiti ya Stanslaus. Alikuwa anaenda kuitupa katika mapori ya Bagamoyo. Aliendesha gari kwa uangalifu mpaka alipouacha mji wa Dar es salaam na sasa alikuwa ameingia katika mapori makubwa ya Bagamoyo. Njiani alipishana na magari machache na hii ndio sababu ya kuchagua mapori ya Bagamoyo ambayo magari yanayotumia njia hiyo kwa mida ya jioni yalikuwa ni machache ukilinganisha na Morogoro Road. Hivyo ingekuwa vigumu kushtukiwa.
Aliona barabara ya vumbi ikikata kulia akaamua kuifuata, akaangalia huku na huku kuona kama kuna gari inamfuata lakini hali ilikuwa shwari. Akaendesha umbali wa kilometa mbili kutoka Bagamoyo Road, hapo akaona sehemu nzuri ambayo ingemfaa kutupa ile maiti ya Stanslaus. Alisimamisha gari, kisha akaangalia huku na huku kwa Mbele hakuona mtu, alafu akachungulia kwa nyuma Kupitia vioo vya pembeni ya gari, pia hakuona mtu. Akashuka akiwa kavaa suruali nyeusi, raba nyeusi zenye soli nyeupe, juu akiwa kavalia blauzi ya rangi ya damu ya mzee na uso wake ukiwa nyuma ya miwani ya rangi ya hudhurungi.
Upepo mwanana ulimpuliza, tayari jua lilikuwa limezama, mwanga wa jua uliokuwepo ni ule wa buriani. Fernanda alisimama kama mlingoti kisha akatulia tuli kusikiliza kama kuna uwepo wa mtu eneo lile, hali ilikuwa shwari, eneo lilikuwa kimya ndege wakiimba nyimbo za kuiaga siku ile. Alienda kwenye buti la gari akafungua, kisha akaitoa ile maiti kwa kuivuta, ikatoka ikaanguka chini. Fernanda hakuweza kuibeba, hivyo aliiburuza kwa kuivuta mpaka nje kidogo ya barabara, kisha akaiburuza tena umbali wa mita thelasini, muda wote alikuwa kavaa Gloves mikononi. Alijua kuwa ile maiti muda mchache ujao itaonekana na uchunguzi utaanza. Baadaye alirejea ndani ya gari, akachukua kikopo kidogo kwenye mkoba wake. Akatoka nacho na kwenda kule kwenye ile maiti ya Stanslaus. Alipofika akaimwagia ile maiti kemikali iliyokuwa ndani ya kile kikopo. Kazi ya kemikali ile ni kupoteza fingerprint zilizogusa mwili wa marehemu, hivyo Fernanda hakutaka alama zake za vidole zibaki kwenye maiti ya Stanslaus ili kupoteza ushahidi kuwa yeye anahusika kwenye kifo cha Stanslaus.
Hatimaye alimaliza, na safari ya kurudi nyumbani kwake ikaanza. Akiwa njiani Fernanda alijaribu kumpigia simu Sajenti Warioba lakini namba ikawa haipatikani. Huzuni ilimkumba, simanzi ikamkumbatia. Alikumbuka mambo yote mema aliyokwisha kufanya akiwa na Sajenti. Hakuona mwanaume afananaye na Sajenti. Alimpenda Sajenti kuliko kitu chochote kile, alitamani muda wote awe naye, lakini leo alikuwa pekeyake bila kujua ni wapi Sajenti alipo. Punde si punde alikumbuka jambo muhimu lililomfanya asimamishe gari kwa ghafla. Wakati huo alikuwa keshakaribia Bunju, alipata wazo, akageuza gari kurudi Bagamoyo. Muda huu aliendesha kwa kasi kidogo akiwa kawasha taa za gari kutokana na giza lilikuwa limeingia. Ndani ya lisaa limoja na dakika chache alikuwa kaingia Bagamoyo, ilikuwa mida ya saa mbili na nusu. Bado maduka yalikuwa hayajafungwa, alienda kwenye vibanda vya kutolea pesa. Hapo akataka kutoa pesa kutoka kwenye simu yake. Alishangaa kuona kila akitaka kutoa pesa inakataa, alipewa ujumbe kuwa akaunti yake ilikuwa imefungwa hivyo afike ofisini kwa ajili ya kushughulikia jambo hilo. Akili ya Fernanda ikakosa utulivu, tayari alijiingiza kwenye mkondo wa balaa. Alijua kuwa akaunti zake zimefungwa makusudi ili asiweze kutoa pesa zitakazo msaidia kutoroka.
Lakini hiyo isingeweza mzuia hata kidogo, Fernanda alikuwa jasusi mbobezi wa kimataifa, tayari ameshafanya kazi nchi nyingi hivyo anauzoefu wa matata na hekaheka za namna ile. Alisonya, kisha akatoa zile laini na kuzivunja vunja, alitoa simu nyingine ambayo aliisajili kwa majina NADIA BANDA. Alijua ni muhimu kuwa na laini za simu tofauti tofauti na majina yasiyofanana ili ikitokea siku ya matatizo aweze kujinasua. Alijua ni rahisi kudhibitiwa ikiwa utakuwa na laini za simu zenye jina moja tuu, lakini ukiwa na laini zenye majina tofauti sio rahisi kudhibitiwa. Hivyo kwenye laini ya kawaida aliweka pesa lakini hakuweka pesa nyingi tofauti na laini aliyojisajilia kwa majina mengine asiyotambulika nayo.
Alitoa milioni moja na nusu kisha akaziweka kwenye mkoba, huyo akatoka na kuingia ndani ya gari lake. Akiwa njiani kutafuta Lodge ya kupumzika alitupa zile simu zilizokuwa na laini zenye majina ya Fernanda kwa kuhofia kuwa wapo watu wanamfuatilia, Moja kwa moja alichukua chumba kwenye moja ya Lodge nzuri zilizokuwa pale Bagamoyo. Aliandikisha jina Nadia Banda kisha akapewa chumba.
Aliingia kuoga alafu akatoka akakaa kitandani akazikausha nywele zake ndefu za kibrazil. Baadaye akapumzika. Akili yake ilimrejesha asubuhi alipovamiwa na jitu jeusi, ndilo Stanslaus. Kisha akakumbuka habari za Sajenti Warioba, alikumbuka penzi zito alilopewa na Sajenti mwezi mmoja uliopita. Alitamani raha zile. Alijikuta akitabasamu, alafu akasema; Nakupenda sana Otieno.
Usingizi ulimpitia akalala.
ITAENDELEA
Usisahua ku-like na kushare.
Jipatie Riwaya ya MLIO WA RISASI HARUSINI" Ambayo ipo sokoni. Hutojutia.
Kitabu Tsh 15,000
0693322300
Airtelmoney
Robert Heriel.
0758216209
M-PESA
Robert Heriel