Simulizi ya nane
VITA YA MOGADISHU 1993
(Marekani haitokuja kuisahau Somalia)
Duniani kuna waasi wengi sana ila waasi wa Afrika ndiyo mwisho, hata shetani huwa anawashangaa wamepata wapi hizi roho. Shida ya waasi wa Afrika hawatosheki kunywa damu wanaweza wakapigana mpaka nchi ikawa majivu yote, na yote hii kwasababu ya ubinafsi. Usiombe nchi ya Afrika iangukie kwenye vikundi vya waasi.
Vita ya Mogadishu ilitokea Somalia na yalikuwa mapigano makali kati ya jeshi la Marekani Delta Force na Rangers wakisaidiwa na jeshi la umoja wa mataifa (UNOSOM) dhidi ya Somali National Alliance (SNA) na vikundi vingine vya waasi,3-4 Oktoba, 1993. Vita iliyomgharimu Marekani na kuamua kukimbia.
Marekani alipeleka wanajeshi wake Somalia mwaka 1992 kutokana na vita za wenyewe kwa wenyewe lakini kubwa zaidi ni changamoto iliyotokea. Baada ya vikundi vya waasi hasa vya ukoo wa Habr Gidr wa jenerali Mohammed Farah Aidid kumpindua rais dikteta aliyekuwa madarakani Siad Barre wakaanza kutawala mji wa Moghadishu kusini.
Sasa kutokana na vita za muda mrefu na ukame baa la njaa likaingia Somalia karibia watu 300,000 walikufa.
UN na Marekani walichukua jukumu la kwenda kutoa misaada ya chakula na kulinda amani, jambo la ajabu ni kuwa wanamgambo wa SNA walioongozwa na Mohammed Farah Aidid walikuwa wakiteka misafara ya gari za chakula za UN na kupora chakula, wao njaa ilikuwa ni moja ya kete muhimu kuidhoofisha serikali na vikundi vingine hasimu.
Mohammed Farah Aidid akavuka mipaka ikafikia kipindi wanangambo wake wakaua wanajeshi 24 wa UN ambao ni raia wa Pakistan. Hapa sasa Mmarekani akaona huyu kijana anachezea sharubu za simba. Waka unda mkakati wa wakusambaratisha uongozi wa SNA, ikaanzishwa operation maalum iliyojulikana kama
Operation Michigan au
Abdi House Raid ambayo ilifanyika 12 Julai,1993 kwenye wilaya ya Hodan pale Mogadishu. Ambako jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi ya anga na kupelekea mauji ya watu 54 na majeruhi 215. Sasa haya mauaji yaliua raia wengi wasio na hatia na kupanda mbegu ya chuki dhidi ya jeshi la Marekani. Waandishi wahabari walioenda kuripoti hili tukio ambao ni wazungu waliuliwa na wengine walifanikiwa kukimbia.
Uhasama ukawa wazi kati ya SNA na jeshi la Marekani, wakawa wanamtafuta jerali Mohammed Farah Aidid. Rais wa Marekani Bill Clinton akaanzisha Operation Gothic Serpent kwa lengo la kumkamata jenerali Aidid. Mshauri wa masuala ya ulinzi Jonathan Howe akatangaza dau la $25,000 (Tzs 61,249,000) kwa atakayefanikishwa kukamatwa kwake.
Jeshi la UN likaanza kuvamia baadhi ya maeneo kwa matumaini ya kumshika Aidid, kunakipindi watu waliandamana kupinga uvamizi wa UN ila jeshi la UN likawamiminia risasi na karibia watu 20 walipoteza maisha hii ikapelekea uhasama na chuki kuongezeka kati ya raia na waasi dhidi ya jeshi la Marekani na UN.
CIA asset(mtu aliyeajiriwa kwa usiri mkubwa kutoa intelijensia) ambaye alikuwa ni raia wa Somalia akawashitua na kuwaambia anataarifa za uhakika sehemu ambayo Jenerali Aidid atakuwepo. Akawaambia atakuwa na maongezi na baadhi ya viongozi wa SNA na wa ukoo wa Habr Gidr ambao ndiyo wanatawala Mogadishu ya kusini.
Akawaambia atakuwa jirani na jengo la Olympic Hotel na jasusi huyu akatumia paa la gari yake kuchora muelekeo wa nyumba husika ili ndege ikiwa angani iweze kuona.
Eneo hili ilikuwa ni moja ya ngome ya Aidid kuanzia Olympic Hotel mpaka soko la Bakara.
Jeshi la Marekani kwa haraka wakachangamkia fursa na kujipanga kwenda kumkamata Aidid, wakaandaa jeshi la Delta Force na Rangers chini ya Captain Michael Steele. Walipanga safu ya mashambulio ya anga na ardhini hasa kuwachukua mateka.
Plan kulizunguka eneo na kuwakamata viongozi wa SNA. Wao walipiga hesabu kuwa ni tukio la dakika 30 tu limezidi sana saa 1. Waswahili wanasema usilolijua ni sawa na usiku wa giza, kumbe kazi ilikuwa kubwa kama wako Vietnam.
SNA na wao hawakukaa kizembe kwasababu walikuwa wanajua washachokoza nyuki kwahiyo muda wowote mitaa itawaka. Jenerali Mohammed Farah Aidid sio mwepesi alisomea masuala ya kijeshi Urusi. SNA waliigawa Mogadishu ya kusini katika sekta 18 za kijeshi na zina field officer ambaye anaripoti taarifa, pia walikuwa wenyeji yaan walikuwa wanazijua chochoro zote za mitaani, pia walijifunza kwenye mashambulio ya nyuma ya kuwa moja ya mbinu wanayotumia jeshi la Marekani ni speed kwahiyo kikitokea chochote inabidi wawe na speed. Col. Sharif wa SNA aliwaambia faida nyingine ni kuwa jeshi la Marekani linaamini wao wanaakili na bora zaidi hivyobasi watatudharau na kutuchukulia kwa wepesi kitu ambacho ni hatari kwasababu SNA walikuwa ni kama wanapigana vita na mahasimu wao kila siku hapo mjini.
Kwenye uvamizi jeshi la Marekani walirusha kwanza helicopter(ndege) 16 ilikuwazuga SNA wakapitiliza kwanza target yao ila kuna jambo walilishuhudia ila hawakuona kama tatizo, Wasomali walikuwa wameanza kuchoma matairi barabarani kitu ambacho kinaonesha ishara ya machafuko. Kufikia saa 9:42 helicopter 2 zikawashusha wanajeshi wa Delta eneo mahususi kwaajili ya operation japo kuwa vumbi lilikuwa jingi, ghafla wakaanza kusikia milio ya bunduki. Col. Sharif akaanza kukusaja jeshi la SNA lifike eneo la wanja wa vita.
Ndani ya dakika 10 barabara zote zinazoingia eneo la Olympic Hotel zikawa zimefungwa na wanamgambo. Baada ya hapo Col. Sharif akawa hawasiliani tena na radio wakawa wanatumia karatasi tu na mdomo kwa kuhofia Marekani watadukua mawasiliano yao.
Kipindi ndege inawashusha Private Todd Blackburn alikosea kushika kamba akaanguka kutoka juu ya ndege mpaka chini urefu wa mita 21 na alipata majeraha makubwa, ikabidi Humvee(Hummer za jeshi) tatu zimrudishe kambini kwaajili ya matibabu na wakiwa njiani mwanajeshi wa kwanza wa Marekani anapigwa risasi na kufa. Sasa mpaka kufikia hapa shughuli ishaanza kuwa ya moto, milio ya risasi ilikuwa inalindima kila sehemu.
Kipindi wanaendelea na operation ndege ya kwanza ya Mmarekani inatunguliwa na Wasomali kwa RPG-7,ndege ya Black Hawk.
Ndege ilivyoanguka marubani walikufa palepale na waliopona wakaanza kujilinda. Wanamgambo wa SNA wakaanza kuwaambia watu “tokeni njee na muilinde nchi yenu”, nilisema awali ya kuwa raia walikuwa wameshawachukia Wamarekani kutokana na mauaji ya nyuma.
Kufikia hapa tayari mitaa ya Mogadishu inanuka risasi na damu, unajua Marekani anachanganyikiwa kwenye vita kuona adui yake anatumia AK 47 vitani, Ak 47 ni silaha bora sana na ni rahisi kupatikana na kutumika ila wao huwa hawazitumii kwasababu zilitengenezwa Urusi. Afrika hii ndiyo silaha ya waasi wakishika hii silaha kuwa makini.
Saa 10:40 ndege ya pili ya Mmarekani inatunguliwa na SNA kwa RPG na hawajamaa walikuwa wanapiga ule upanga wa nyuma baada ya hapo ndege chini. Hapa sasa wanasema maji yamezidi unga na vita haikuwa ya SNA peke yao sasa ni kama wa Somali wote, watoto, wanawake mpaka wazee walioweza walipewa silaha mitaa ya Mogadishu ilikuwa imechafuka kweli matundu ya risasi yamejaa kwenye nyumba.
Ndege nyingine ikaenda kuokoa sehemu ambayo ndege ya pili ilianguka na hii pia ikatunguliwa kwenye injini lakini haikuathirika sana ikawalazimu kukimbia ilo eneo na kwenda kutua mbali kidogo. Wadunguaji(sniper) wengi wa Kimarekani waliumizwa sana, sehemu ambazo ndege zilianguka zikawa kama machinjioni.
Saa 12:40 jioni Aidid akamtumia ujumbe Col. Sharif ahakikishe hakuna mwanajeshi wa Marekani anatoroka. Wanajeshi wa Marekani ilibidi waanze kujilinda huku wakiwa wanarudi walikotokea mdogomdogo ila mitaa haikuwa rafiki.
Ya Mungu mengi sana, hii siku Saida Omar Mohamud alikuwa amejifungua mtoto wa kike na furaha yao ilikatishwa baada ya ndege ya Black Hawk kuanguka karibu na nyumbani kwao na ghafla wanajeshi kama 10 Wamarekani wakavunja mlango kwenda kujificha na wakageuza sebule kuwa hospitali ya dharura na meza zikawa vitanda vya wagonjwa. Na akaamua kumuita mtoto wake Amina Rangers. Shida nyingine ni nyumba nyingi za Somalia zimejengwa kwa udogo hivyobasi hazikuwa salama sana kutumia kujificha maana risasi zinaweza kupenya.
Zoezi walilodhani ni dakika 30 likawakuta mpaka usiku wa manane wanatupiana risasi mitaani, shida nyingine walifanya siri hata makamanda wa UN walikuwa hawajui chochote mpaka mambo yalivyoharibika ilibidi jeshi la UN liende kusaidia kuokoa wanajeshi wa Marekani shida kwenye wanja wa vita gari zilikuwa zikisindikizwa na kukaribishwa kwa mvua za risasi. Aidid akaona sio vizuri wa Somalia kuendelea kufa ila pia aliogopa nguvu kuongezwa zaidi kutoka Marekani akaruhusu corridor moja ya kutokea iwe wazi kuwawezesha kutoka lakini bado haikuwa rahisi mapigano yaliendelea.
Baada ya msaada kutoka UN na nguvu kuongezwa wakaweza kutoka ila wanajeshi wengine wakakosa nafasi ndani ya gari ikawabidi wakimbize gari nyuma nyuma na kutumia magari kujificha dhidi ya risasi, hii safari ya maili tatu ilijulikana kama Mogadishu Mile inasemekana kipindi wanakimbia kwa miguu wanajeshi wawili waliuliwa njiani.
Mapigano yaliisha saa 12:30 asubuhi ya Jumatatu 4 Oktoba,1993. Baada ya vita baadhi ya miili ya wanajeshi wa Marekani ilianza kuburuzwa mitaani na rubani wa Marekani alishikiliwa mateka. Tukio hili liliwaudhi na kuwauzunisha sana Wamarekani.
Wanajeshi wa Marekani 18 walipoteza maisha na wakiwamajeruhi 73, vifo hivi mara ya mwisho kushuhudiwa ni kwenye vita ya Vietnam na upande wa Somalia zaidi ya watu 200 walipoteza maisha na zaidi 700 walikuwa majeruhi. Mmarekani akaamua kuliondoa jeshi lake kwa kuhofia mgogoro kuendelea. Mmarekani mara zote anashinda vita kwenye nchi ambazo zinamigogoro mikubwa ya ndani hivyo inakuwa rahisi kupandikiza wasaliti. Marekani alijifunza kutokudharau jeshi lolote.
Jenerali Mohammed Farah Aidid alikufa mwaka 1996 kutokana na mshituko wa moyo.