Pia unapoongelea uungu katika wakristo wa kweli Utatu Mtakatifu ni jambo la kuzingatia na linalofanya uungu wa Yesu kutokuwa wa kutilia shaka wala wa kuquestion.Hii ni moja ya jambo la msingi sana katika Ukristo.Mwisho kama mwana wa binadamu ni binadamu kamili na mwana wa Mungu ni Mungu kamili.
Ndugu yangu usiimbe mafundisho ya kanisa au maneno ya mchungaj/padr wako, sikiliza Yesu mwenyewe anasema nini hapa chini:
Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
Yohana 12.49-50
Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.
Yohana 5.30
Fakhari kubwa ya Yesu ilikuwa kwamba kila alisemalo na alitendalo ni kufuata mapenzi ya Mungu na kutii maamrisho yake.
Katika hadithi ya muujiza wa kufufuliwa Lazaro tunasoma kama ilivyo katika Injili ya Yohana:
Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake. Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.
Yohana 11.38-42
Kutokana na kisa hichi tunajifunza nini? Mambo matatu hapa yanatudhihirikia wazi:
1. Yesu anamwambia Martha, dada wa maiti, kuwa "ataona utukufu wa Mungu" si utukufu wa Yesu, kwani muujiza ni wa Mwenyezi Mungu, si wa Yesu, Mwana wa Adamu. Mfufuaji ni Mwenyezi Mungu, mwenye uwezo wa kila kitu. Yesu "hawezi kufanya neno mwenyewe".
2. Yesu anamwomba Mungu na anamshukuru Mungu kwa kumwitikia na kuyasikia maombi yake.
3. Yeye Yesu anajua kuwa Mungu siku zote anamwitikia maombi yake, lakini alifanya yale hadharani ili athibitishe kwa wale waliohudhuria kuwa kweli yeye Yesu ametumwa na Mungu, yaani yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kamaalivyosema mwenyewe:"ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma." Yesu pia anathibitisha kuwa ayatendayo ni mapenzi na amri ya Mungu.
Hayo ndiyo, lakini yeye mwenyewe Yesu kafufuka kutoka wafu. Huo si muujiza wa kuonyesha kuwa yeye ni Mungu? Hebu tuitazame Biblia inasema nini juu ya tukio hili. Kila tusomapo kitabu hichi kitakatifu tunaona kuwa ni Mungu ndiye aliyemfufua Yesu.
Hatuoni kuwa Yesu kajifufua mwenyewe. Vile vile tunasoma humo humo kuwa si yeye peke yake aliyesimuliwa na kuaminiwa kuwa kafufuliwa kutoka wafu. Twasoma katika 2 Wafalme:4.32-37 vipi Nabii Elisha (Al Yasaa) alivyomfufua mtoto aliyekwisha kufa. Kisa kingine kama hicho kinasimuliwa katika 1 Wafalme 17.22. Biblia pia inawataja watu wengine wasiokuwa Yesu waliopaa wakenda mbinguni. Katika 2 Wafalme tunasoma:
Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili (Elisha na Eliya, yaani Al Yasaa na Ilyas); naye Eliya (Ilyas) akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli.
2 Wafalme 2.11
"Kisulisuli" ni upepo wa chamchera au kimbunga. Hadithi kama hizo za watu watukufu kupaa mbinguni na kufufuka zilikuwa zimeenea sana katika zama za Yesu.
Josefas akiandika katika kitabu Antiquities (Ya Kale) anasimulia khabari ya Musa: "Kwa ghafla kiwingu kilisimama mbele yake, naye akapotea katika bonde fulani, ijapokuwa ameandika katika vitabu vitakatifu ya kuwa alikufa. Hayo yalifanywa kwa kuogopa wasije kusema kuwa kwa sababu ya uchamngu wake uliopita kiasi, alikwenda kwa Mwenyezi Mungu." Josefas pia ametaja kuwa baadhi ya watu walifikiri kuwa "Musa ameingizwa katika ungu."
Na J. Jeremias katika Moyses amesema:
"Watatu wamepaa mbinguni nao wahai: Enoko, Musa na Eliya".
Almuradi tunaona kwa uthibitisho wa maandiko matakatifu ya Kikristo kwamba si Yesu peke yake aliyeitwa "Mwana wa Mungu, au Mungu", wala si yeye peke yake aliyefufua wafu, wala si yeye peke yake aliyefufuka na kupaa mbinguni.