ROMAN ABRAMOVICH: UTAJIRI WA DAMU, RISASI NA UMAFIA
SEHEMU YA NNE
Baada ya kikao hicho muhimu kati ya Berezovsky na Abramovich kufanyika na mambo ya siri kukubaliana… hatimaye ukasubiriwa utekelezaji.
Hapa nieleze kidogo,
Sehemu kubwa ya Urusi (kwa maana ya ardhi) ni jimbo kubwa linaloitwa Siberia. Siberia inajulikana kutokana na hali yake ya hewa ya baridi kali kupitiliza pamoja na barafu kwa muda mwingi wa mwaka. Lakini pia Siberia ina kitu kingine adhimu zaidi duniani… “dhahabu nyeusi”… mafuta. Jimbo la Siberia lina utajiri mkubwa mno wa mafuta na sehemu kubwa ya utajiri huu wa mafuta unamilikiwa na kampuni yenye kuitwa Sibneft ambayo wanamiliki eneo la visima vya mafuta lenye eneo kubwa zaidi ambalo linaweza kulingana kabisa na ardhi yote ya nchi ya Wales kama tukilinganisha kwa ukubwa wa ardhi.
Hapa ndiko hasa ambako Abramovich alikuwa amepalenga.
Baada ya uchaguzi kuisha na serikali kuanza kufanyakazi, Abramovich akamfuata Rais Boris Yeltsin na kumkumbusha kwamba wakati wa ‘kuwakumbuka’ ma-oligarch waliowasaidia kwenye uchaguzi umewadia. Kama ambavyo yeye Abramovich hakutaka kupewa cheo chochote kile serikalini ndivyo vivyo hivyo pia alipendekeza kwamba ma-oligarch wengine ‘wakumbukwe’ kwa namna nyingine badala ya kufikiria tu kuwapa vyeo vya kiserikali.
Ukawekwa utaratibu wa kubinafsisha makampuni mengine ya umma ambayo bado yalikuwa chini ya serikali. Makampuni yakabinafsishwa kwa ma-oligarch. Abaramovich hakuzuzuka na kutaka kudandia hisa kwenye kampuni nyingine hizi, kichwani alikuwa na lengo moja tu… target moja tu ambayo alitaka kuifikia.
Visima vya mafuta ni rasilimali adhimu kwa nchi yeyote ile. Kwa hiyo japokuwa Russia ilikuwa kwenye uwendawazimu wa ubinafsishaji kiholela lakini ilipofika kwenye visima vya mafuta ilikuwa ni suala lilifanyika kwa tahadhari kubwa zaidi. Naam, viko visima vya mafuta ambavyo vilibinafsishwa lakini visima vya mafuta vya kumilikiwa na kumpuni ya Sibneft viliwekewa utaratibu maalumu na ikulu.
Uzuri au ubaya ni kwamba katika kipindi hiki ulikuwa ukiongelea ikulu ya Russia unaongelea ‘Utatu Mtakatifu’, Abramovich, Tatyana na Yumachev.
Watatu hawa wakaandaa utaratibu maalumu wa namna ya kuibinafsisha kampuni ya Sibneft. Nisisitize tena, Sibneft wanamiliki ‘oil fields’ kubwa kuzidi ardhi yote ya nchi kama Wales. Na katika miaka hii kampuni ya Sibneft ilikuwa na thamani ya zaidi ya dola Bilioni 50 za kimarekani (zaidi ya trilioni 120 za Kitanzania).
Utaratibu ukaandaliwa. Roman Abramovich akahakikisha anaweka vigezo na masharti kadhaa ya mtego mtego ili kukwamisha wengine. Hatimaye mnada wa kuiza Sibneft ukafanyika lakini ajabu ni kwamba katika mnada alijitokeza ‘bidder’ mmoja tu. Ni nani huyu? Nitaeleza…
Bidder huyu alitoa ofa ya kuinunua Sibneft kwa kiasi cha dola milioni 150.!! N
Nisisitize na kukumbusha tena, Sibneft walikuwa na ‘oil fields’ ukubwa zaidi ya nchi ya wales na ‘valuation’ yake ilikuwa ni zaidi ya dola bilioni 50. Auction ikafanyika… Sibneft ikauzwa kwa mwekezaji huyu.
Naamini tayari tunaweza kubashiri kwamba ‘bidder’ alikuwa ni Roman Abramovich. Lakini swali ni kwa namna gani Abramovich anaweza kuwa na dola milioni 150 kwa kipindi kile kuinunua Sibneft??
Nilieleza awali kuhusu kikao cha Abramovich na Berezovsky wiki kadhaa baada ya uchaguzi mkuu. Katika kikao kile Abramovich alimpa ‘ofa’ mentor wake huyo kwamba kwa ushawishi alionao sasa kwa Rais Yeltsin anaweza kutengeneza mazingira wao wawili wauziwe visima vyote vya mafuta na mali za kampuni ya Sibneft lakini akamweleza kuwa anahitaji kitu kimoja tu kutoka kwake… fedha. Makubaliano yao ni kwamba Berezovsky atatoa rasilimali fedha na Abramovich atahakikisha anatengeneza mazingira Ikulu na kuhakikisha kwamba kampuni hiyo inatua kwenye mikono yao.
Ndio kusema kwamba Sibneft kampuni yenye kumiliki visima vya mafuta kwenye eneo kubwa sawa na chi ya Wales, kampuni ambayo ‘valuation’ yake inanesa kwenye dola bilioni 50 ikauzwa kwa Abramovich na Berezovsky kwa dola milioni 150 tu… hela ya ugoro kama asemavyo mzee Rugelamarila. Yaani kitendo cha wao kukabidhiwa tu kampuni siku hiyo hiyo uwekezaji wao uliwalipa faida karibia 400%. Miaka miwili baadae uwekazaji wao huu ulikuja kuwalipa karibia mara 1000 ya fedha waliyonunulia kampuni?
Lakini kama ambavyo nilieleza awali kwamba Abramovich alikuwa mahiri wa mifumo ya kibepari inavyofanya kazi kuwazidi watu wengi nchini Russia kipindi kile na hata serikali yenyewe ambayo bado ilikuwa na tongotongo za ujamaa machoni. Kwa hiyo hata kwenye ununuzi wao wa Sibneft hawakununua tu kichwa kichwa kwa kuweka majina yao kwenye makaratasi ya umiliki bali aliweka mfumo complex wa umiliki kuhakikisha kwamba ni ngumu kufahamu hasa nani anamiliki hisa kiasi gani kwenye kampuni,na nani anapokea dividends kiasi gani na bila kusahahu kuhakikisha wanalipa kodi ndogo iwezekanavyo kwenye mapato.
Nitoe mfano kidogo kabla ya kwenda mbali zaidi… sijui ni wangapi wanakumbuka mwaka 2013 mwishoni ndugu Rostam Aziz alipouza nusu ya hisa zake za kampuni ya Vodacom kwa karibia bilioni 400 za Kitanzania. Jambo la kufurahisha ni kwamba tulipata kodi kiduchu mno, yani kiduchu haswa kutoka kwenye uuzaji huo wa hisa tofauti na ambavyo tulitegemea. Tukabaki tumeduwaa tu wengine wakimnyooshea kidole Rostam kuwa pengine ‘amecheza rafu’ na watu wa system. Yes, hatukupata kodi lakini Rostam hakuvunja sheria na wala hakucheza rafu kwenye ile deal. Alitumia umahiri tu wa kibiashara… hisa zake alikuwa anazihold kupitia ‘private Trust’ ambayo imesajiliwa nchini Mauritus kama nakumbuka vyema. Tunafahamu namna ambavyo sheria za kodi za nchi ya Mauritus zilivyo ‘loose’. Kutoka hapo mtoto wa mjini Rostam akacheza na loopholes za sheria za kimatafa na hata za nchi yetu wenyewe na deal ikafanyika huku vibunda vikibaki mfukoni mwake na vingine kwenda serikali ya Mauritus na kiduchu tukapata sie akina yakhe. Maarifa… maarifa… maarifa.
Hii ndio sababu huwa naamini kwamba Idara ya Usalama wa Taifa wanapaswa kufanya mageuzi ya kusudi kabisa kuhakikisha wanaenda na kasi ya ulimwengu. Kwa mfano maafisa kwenye ‘directorate’ ya Collection wengi ni watu wazima. Mindset zao bado zimejiseti kana kwamba tunakabiliana na adui aliyebeba AK47. Zama zimebadilika mno, adui sasa habebi guruneti… adui sasa hivi anaweza kuwa amejificha tu mahala fulani chumbani na laptop mkononi kama silaha yake na akaitikisa nchi. Adui sasa hivi hawazi tena kupindua nchi bali anafanya hila kuhujumu mfumo wa uchumi… adui sasa hivi hataki madaraka bali anataka kumiliki njia na nyenzo za uchumi wa nchi. Tuko kwenye zama ambazo maafisa wetu wa Idara ya usalama wa Taifa wanapaswa kujua namna ya kunyumbulika na kizazi hiki cha sasa na changamoto zake.
Idara yetu kwa sehemu kubwa inafanya kazi kwa kutegemea ‘Humint’ kama waitavyo wenyewe na ‘open source intelligence’ kitu ambacho sio kibaya sana kutokana na uhalisia wa nchi yetu na uwezo wetu kama nchi na rasilimali tulizonazo. Kwa hiyo ni muhimu sana sana, kuwa na maafisa ambao wanaweza kunyumbuka na uhalisia wa nyakati tulizonazo pamoja na kuwa na mindset sahihi. Unapokuwa na maafisa wenye mindset ya enzi zile za kupambana na adui amebeba AK47 akitaka kushika dola ni ngumu kwake kung’amua vipaumbele anavyotakiwa kujishughulisha navyo na mwisho wake tutahoji juu ya ubora wa intelligence tunayoipata na mwisho wa siku itaathiri hata ufanyaji kazi wa watu wa ‘directorate’ inayosimamia processing. Kinachokuja kutokea ni kwamba pale kitengoni, idara inayohusika na Tasking inajikuta ina-allocate resources nyingi (kwa maana ya maafisa, muda, wataalamu mahususi ) kwenye masuala ambayo pengine hayakupaswa kuwa vipaumbele. Lakini mzizi unaanzia wapi? Idara inayohusika na Collection… tupunguze maafisa watu wazima au kwa usahihi zaidi niseme tuhakikishe tuna maafisa ambao wanaendana na kizazi cha sasa na mnyumbuliko wake… sioni faida au ufanisi unaopatikana kwa kuweka watu wazima wengi kwenye idara hii. Sio kwamba wasiwepo, la hasha… mtu mzima dawa bhana… lakini tupunguze. Lazima watu walioko kwenye kitengo mahususi kwa ajili ya idara hiyo waweze kunyumbulika na zama tulizonazo… nature ya adui imebadilika mno… na sisi tunapaswa kujiboresha.
Kuna mtu atasema “…wewe The Bold unajifanya unajua kuliko Usalama wenyewe…?” tabia na swali kama hili ndio kwa umombo tunasema kuwa ni “Obnoxious”.
Hivi EPA, Richmond, Escrow n.k. hizi ‘abracadabra’ zilivyotokea tulikuwa wapi? Hatukujua kabla ya kutokea? Tulijua. Tulikuwa na nia ya kuzuia. Yes tulikuwa na nia… kwa nini hatukufanikiwa?? Ndio maana tunashauri, kwenye hili suala la Collection ya intelijensia hebu tufanye mageuzi makini pale… nature ya adui imebadilika lazima tujue namna ya kunyumbulika na zama hizi.
Tuache hayo, nahisi naanzisha mada ndani ya mada…
Lakini nimetoa mfano huu ili kuelewa namna ambavyo Abramovich aliweza kucheza na nyakati… wananchi, serikali na hata Idara zake bado walikuwa na ‘hangover’ ya ujamaa wakati ambao Abramovich alikuwa tayari ana umahiri wa namna ubepari unafanyakazi.
Nimeeleza kwamba ili kuhakikisha yeye Abramovich na mentor wake Berezovsky wanaficha kiwango chao cha umiliki wa Sibneft, lakini pia kuhakikisha wanalipa kodi kiduchu iwezekanavyo na ‘kucheza’ za mfumo wa mgawanyo wa dividends (kiasi kidogo kilikuwa kinapaswa kwenda serikalini) Abramovich na mwenzake hawakuweka majina yao moja kwa moja kwenye nyaraka za umiliki. Je, nyaraka zilionyesha nani wamiliki wa Sinbeft.
Kipindi hicho ilikuwa ukichimba kwenye nyaraka za ulipaji wa dividends wa Sibneft unakutana na majina matano tu… CarbonRow ltd, Craven Investments, Gemini Co., MarteChelo Plc na White Pearl ltd. Makampuni manne kati ya haya matano yalikuwa yamesajiliwa nje ya Russia nchini Cyprus, moja ya nchi inayojulikana ulimwenguni kwa kuwa na sheria loose mno za masuala ya kodi na benki. Swali ni akina nani hasa wanamiliki makampuni haya? Tuchukue kwa mfano CarbonRow ukiitazama kwenye nyaraka za kumbukumbu inaonyesha kwamba CarbonRow inamilikiwa na ‘private trust’ inayoitwa MERITSERVUS (TRUSTEES) LIMITED. Nani anamiliki Meritservus Ltd? Dimitris Yunidis…ni nani huyu? Ukichimba ndani zaidi ni kwamba Dimitris ni Accountant ammbaye anamiliki kampuni inaofanya ‘flagging’ ya ‘shell companies’. Kwa kifupi tu ni kwamba kadiri unavyochimba ndio unazidi kuchanganyikiwa na huwezi kuliona jina la Abramovich au Berezovsky na hata ukifanikiwa kuliona huwezi kuona kiwango cha dividends anacholipwa yeye binafsi au kiwango cha umiliki wake wa Sibneft.
Lakini inakadiriwa kwamba Abramovich alikuwa anamiliki 51% ya Sibneft na asilimia zilizobaki walimiliki Berezovsky na serikali ya Russia. Kisheria kwa sababu yeye ndiye alikuwa anamiliki hisa nyingi zaidi, kwa maneno mengine yeye ndiye alikuwa mwenye kauli ya mwisho ndani ya Sibneft , na kwa maneno mengine Sibneft ilikuwa ni kampuni yake.
Ndani ya mwaka mmoja tu baada ya yeye na Berezovsky kununua Sibneft, Roman Abramovich, kijana yatima aliyekulia kwenye umasikini wa kutupwa ambaye miaka mitatu tu nyuma alikuwa anauza wanasesele na matairi chakavu, mara moja alipanda chati na kufikia status ya ubilionea ambapo kwa kipindi kile utajiri wake ulikuwa unafikia dola 3.4 bilioni za kimarekani (kama trilioni 7 za kitanzania) na hii ikamfanya kuwa oligarch kijana zaidi kipindi hicho nchini Russia akiwa na miaka 31 tu.
Lakini wanasema penye riziki hapakosi fitina… Naam, kitendo hiki cha Abramovich kutumia ushawishi alionao Ikulu kujilimbikizia utajiri wa kutupwa kiliwaudhi baadhi ya watu wa ‘system’. Kuna watu waliumia pia mtoto mdogo wa miaka 31 hata harufu ya maziwa haijamuisha ati leo anakuwa oligarch. Ikaanza minong’ono na vuguvugu la chini kwa chini kuwapiga vita Abramovich na Berezovsky.
Vuguvugu hili likaenda mbali zaidi ambapo mwendesha mashtaka mkuu wa serikali kipindi hicho Bw. Yuri Skuratov alifanya mkutano na wanahabari na kusema kwamba anakusanya ushahidi ili afungue mashtaka dhidi ya baadhi ya ma-oligarch. Japo hakuwataja majina lakini kila mtu alijua anamlenga nani.
Lakini Abramovich alikuwa mboni ya Rais Yeltsin. Rais akamuita Mwendesha Mashtaka mkuu wa serikali na kumtaka aachane na jambo hilo… Yuri Skuratov akakataa.
Yeltsin akajaribu kumfukuza kazi, lakini bunge likapinga uamuzi huo wa Rais na kumrejesha kazini Bw. Yuri Skuratov. Wabunge walikuwa na vihoro… roho ziliwauma kijana mdogo kama Abramovich kuwa na ushawishi mkubwa hivyo kwenye nchi ambayo miaka si mingi ilikuwa ndiyo ‘superpower’ ya ulimwengu.
Yuri Skuratov aliporejeshwa kazini na bunge kiburi kikamjaa zaidi… akaitisha mkutano mwingine na wanahabari na kuwaeleza kuwa ana ushahidi wa kutosha dhidi ya Roman Abramovich na Berezovsky na anakusudia kuwafungulia mashtaka ya kuhujumu uchumi. Watu wa system walifurahi kweli kweli wakijua huo ndio mwisho wa Abramovich… kama wangelijua kipindi kile Abramovich ni mtu wa namna gani wasingelithubutu kumtikisa. Walikuwa wanapima kina cha bahari kwa goti la mguu…
Ma-oligarch wenzangu, tuonane kesho kwa ajili ya sehemu ya tano…
Stay here…
The Bold – 0718 096 811
To Infinity and Beyond