Na Padri Privatus Karugendo -MwanaHalisi
NINAANDIKA makala hii kwa uangalifu mkubwa. Kama itakuwa na harufu ya ubaguzi, basi itakuwa ni bahati mbaya na kusema ukweli itakuwa nje ya uwezo wangu.
Mimi ninaamini kwamba binadamu wote ni sawa. Na nimekuwa nikitetea haki za binadamu na kuwatetea Watanzania ambao wamekuwa wakinyoshewa kidole na kuitwa wahamiaji haramu.
Sipendi ubaguzi. Hivyo, ikitokea nikateleza kwenye makala hii, natanguliza kuomba msamaha!
Ninajua baadhi ya watu watashangaa kwa swali ninaloliuliza, maana Rostam Aziz anafahamika sana. Huyu ni tajiri mkubwa, ana makampuni mengi, hata New Habari Corporation ni mali yake.
Ni mfanyabiashara maarufu wa ngozi, ni mwana CCM mkereketwa wa hali ya juu. Ni mtu mwenye ndoa safi asiyefahamika kwa kufukuzana na vimwana (ni wachache sana wa namna yake, hivyo ni lazima ajulikane).
Ni Mbunge wa Igunga, ni rafiki wa karibu sana wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edwrad Lowassa. Ni rafiki wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa; na ni swahiba wa karibu mno wa Rais Jakaya Kikwete, na ana uhusiano mkubwa na watu wengi maarufu nchini.
Kwa umaarufu huo, anafahamika Ngara hadi Mtwara, Bagamoyo hadi Kigoma. Ndiyo maana nimeanza kuwa kusema labda wapo watu watakaoshangaa swali langu.
Hata hivyo, swali langu hilo limechochewa na tamko lake mwenyewe alilotoa wakati anazungumza na waandishi wa habari kujitetea kwa mwaliko wake katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Kinondoni, Dar es Salaam, wiki chache zilizopita.
Kuna baadhi ya matamshi yake ambayo yamenifanya nijiulize, huyu ni nani? Nitayanukuu machache na kuyajadili hapa: Katika kikundi hicho, wamo ambao hawaridhiki na nafasi za uongozi walizo nazo na ambao wamejenga chuki kwa kudhani na kujiaminisha kuwa labda mimi nilihusika kuwazuilia kujichukulia fursa za ufahari na hadhi wasizostahiki kwa vyeo vyao.
Yeye ni nani kiasi afikiri watu wanawaza hivyo juu yake? Kwamba yeye anashiriki kupanga ni nafasi gani mtu achukue katika serikali? Yeye ni mshauri wa rais? Au urafiki wake unampatia nafasi ya kuingilia maamuzi mbalimbali katika serkali?
Katika kauli nyingine, anasema: Nataka niweke jambo moja wazi, kwamba kama (Mchungaji Christopher) Mtikila angekuwa amenituhumu mimi tu, nisingeitisha mkutano huu. Nisingefanya hivyo kwa sababu hastahiki heshima ya kujibiwa na mimi.
Matamshi kama haya yalinishutua na kunifanya nijiulize, huyu ni mtu gani anayejitukuza kiasi hiki? Ni mfalme wa nchi gani?
Huyu Rostam Aziz, ni nani ambaye watu wengine hawastahiki kujibiwa na yeye? Ni mtu gani huyu mwenye ubaguzi wa kupindukia? Ni mtu gani huyu mwenye dharau inayozidi mipaka?
Kama anabaguliwa Mchungaji Mtikila, ambaye ni kiongozi wa kanisa na chama cha siasa, watu wa kawaida watabaguliwa kiasi gani? Rostam anatoa wapi kiburi hiki? Ni kwa sababu ya utajiri wake? Ni kwa sababu ya ubunge wake?
Inashangaza sana jinsi Watanzania wanavyofumbia macho matukio kama haya. Huu ni wakati wa kusimama na kutetea heshima ya kila Mtanzania. Ni wakati wa kusimama na kusema: Hapana!
Tulidhalilishwa enzi zile za wakoloni na biashara ya utumwa, kwa nini tudhalilishwe leo ndani ya Tanzania huru? Huu ni wakati wa kuwakemea watu wa aina ya Rostam Azizi, wanaofikiri ni watu wa pekee kiasi cha kujikweza na kuwabagua baadhi ya watu.
Anatamba na kujigamba kwamba yeye ni mtu safi. Inawezekana mtu mwenye ubaguzi kama huu akawa safi? Mtu mwenye ubaguzi anakiuka haki za binadamu; na mtu yeyote anayekwenda kinyume cha haki za binadamu, hawezi kuwa mtu safi chini ya mbingu.
Hata akiwa na fedha nyingi kiasi cha kuweza kumgawia kila mtu, kama ni mbaguzi, hawezi kuwa safi. Hawezi!
Jambo jingine lililonishangaza sana kwenye tamko lake ni pale aliposema hivi: Mimi si miongoni mwa wale walioshindwa kutunza ndoa zao, na kutamani kuishi na wasichana wadogo ambao ni wa umri wa mabinti zao na wajukuu zao.
Ujumbe huu ulimlenga nani? Na ujumbe huu unahusiana vipi na kitendo chake cha kwenda kujisafisha kule kanisani? Sitarajii kwamba alimlenga Mchungaji Mtikila. Tunamfahamu Mchungaji na mkewe. Si familia yenye kustahili kurushiwa maneno hayo.
Wale wanaomfahamu vizuri Rostam wanafikiri ujumbe kama huu angewapelekea rafiki zake wa karibu sana, anaowafahamu fika, na anaowatetea. Tunawafahamu.
Kwenye tamko lake, anatoa historia yenye uchungu, ambayo sifikiri kama kuna mtu anapenda kuikumbuka:- Fedha zangu ni pato halali linalotokana na jasho langu kupitia biashara ambayo imekuwa ikiendeshwa na familia yangu tokea mwaka 1852 huko Tabora ilipoanzishwa na babu zangu.
Wengi tunaifahamu vizuri historia. Ni biashara gani ya mwaka 1852 katika ardhi yetu ilikuwa halali? Tunaifahamu Tabora na historia ya watumwa na biashara ya pembe za ndovu. Ilikuwa biashara chafu kiasi kwamba mtu mchafu pekee ndiye anaweza kujivunia historia ya biashara hiyo.
Haiwezi kuwa tofauti na mikataba ya kidanganyifu ya Karl Peters na wenzake. Haiwezi kuwa tofauti na kile kilichotokea mwaka 1884-1885, kuigawa Afrika vipande vipande na kuitawala.
Ni biashara kama ile iliyoendeshwa na Wahindi, kununua mazao ya babu zetu kwa udanganyifu. Kwetu Kagera, kulikuwa na bakuli kubwa za Wahindi ya kununulia kahawa, ambazo zilipewa jina la Balimanyaila.
Maana yake ni kwamba, itawachukua miaka mingi kugundua hila zetu. Mabakuli haya yalibondwa bondwa kwenye pembe na kupanuliwa kiasi cha kumeza mabakuli ya kawaida kama mawili au matatu ya kahawa. Hivyo babu zetu waliuza matatu yaliyohesabika kuwa moja! Waliibiwa!
Anajigamba kwenye tamko lake, akisema: Ili kutendeana haki basi, na kujua ukweli wa mambo natoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa madai ya ufisadi dhidi yangu awasilishe ushahidi huo katika vyombo vya sheria.
Vinginevyo, ni afadhali wafunge midomo yao Ni wazi kuwa Rostam Aziz anajua jinsi anavyofanya mambo yake kiujanja akishirikiana na Watanzania aliowaweka mfukoni.
Anasema ana watoto watatu anaowapenda na anapenda kuwalea kwa maadili mazuri. Je, watoto hao wanasomea kwenye Sekondari za Igunga, ambazo ameshiriki kuzijenga? Watoto hao wanashiriki maisha, na kuonja adha wanayoipata watoto wetu wa Kitanzania? Wanaishi wapi watoto hawa?
Je, kwa uzalendo alionao, anawasomesha watoto wake nje ya nchi?
Anasema:- Kwa kumalizia, napenda Watanzania na waumini wa KKKT, waelewe kuwa nilikwenda katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Usharika wa Kinondoni, kwa mwaliko
Mbona inafahamika kwamba aliyekuwa amealikwa rasmi kwenye hafla hiyo ni Lowassa, ambaye baada ya kukataa mwaliko akawapendekezea mtu mwingine (Rostam) kwa vile aliaamini atawachangia fedha nyingi?
Kama, Rostam Aziz anataka tumwamini, mbona hasemi ukweli wote? Inasikitisha sana kwamba tamko la Rostam Azizi limejaa dharau na majigambo kama yale ya rafiki yake, Lowassa.
Inawezekana (hata hivyo, watu wanasema) kwamba tamko hilo liliandaliwa kwa kushauriana. Kila mtu ana namna yake ya kuandika. Hata akijificha namna gani, ni lazima atajifichua kwa kutumia baadhi ya maneno kama vile: Ili kutendeana haki.., Hastahiki heshima.., Upande wa pili wa sarafu.. Nataka niweke jambo moja wazi, Hii hali inayoshamiri hivi sasa ya kuviziana, kutungiana uongo na kutakiana mabaya.... maneno ambayo mara nyingi yamekuwa yakitumiwa na Lowassa, kwenye hotuba zake. Au Rostam aliibia staili hiyo?
Kimsingi, KKKT hawakuwa na kosa kumwalika Rostam Azizi, wala yeye hakuwa na kosa kwenda kule. Kosa alilisababisha mwenyewe alipoanza kujisifu mbele ya waumini, na kuzungumzia usafi wake, huku akiwarushia wengine makombora akiwa kanisani; na kulishukuru kanisa kwa kutambua usafi wake. Hapo ndipo mgogoro ulipoanzia.