RPC Maigwa: Silaha zisizomilikiwa kisheria zisalimishwe kabla ya Oktoba 31,2026

RPC Maigwa: Silaha zisizomilikiwa kisheria zisalimishwe kabla ya Oktoba 31,2026

Ndagullachrles

JF-Expert Member
Joined
Jun 20, 2023
Posts
256
Reaction score
259

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (SACP )Simon Maigwa, amewakumbusha wananchi na kampuni za ulinzi binafsi wenye silaha zinazomilikiwa kinyume cha utaratibu wa kisheria kuzisalimisha kwa hiari kabla ya kukamilika kwa muda uliowekwa, Oktoba 31, 2026.

Maigwa ametoa msisitizo huo alipokuwa akizungumza mubashara katika kipindi cha Darasa Mseto kinachorushwa na kituo Cha Radio Cha Moshi FM, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni ya Ongea na Kamanda, inayolenga kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya usalama na kuimarisha ushirikiano kati ya Polisi na wananchi.

Amesema kampeni ya usalimishaji wa silaha kwa hiari ilizinduliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani mwezi Septemba mwaka huu, ikiwa na lengo la kuhakikisha silaha zinazomilikiwa nje ya utaratibu wa sheria zinakabidhiwa kwa mamlaka husika.

Akizungumzia kampuni za ulinzi binafsi, Maigwa amesisitiza umuhimu wa kampuni hizo kuhakikisha silaha zinazotumika katika shughuli zao zinamilikiwa na kutumika kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Ametoa mfano wa kampuni inayoendelea kutumia silaha iliyokuwa ikimilikiwa na mlinzi ambaye ameacha kazi, amefariki au hastahili tena kuimiliki, akieleza kuwa hali hiyo inapaswa kushughulikiwa kwa kuzingatia masharti ya kisheria kuhusu umiliki na matumizi ya silaha.

Aidha, amewataka wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha masharti ya kisheria kutumia muda uliobaki kuzisalimisha kwa hiari. Ametoa mfano wa watu waliofikia umri wa miaka 70, ambao kwa mujibu wa maelezo yake hawatakiwi kuendelea kumiliki silaha.

Kamanda huyo amesisitiza kuwa baada ya muda wa usalimishaji kumalizika, Jeshi la Polisi litafanya operesheni kuwafikia wale watakaobainika kuendelea kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Amewataka wananchi na kampuni za ulinzi binafsi kuchukulia suala hilo kwa uzito, kufuata taratibu za usalimishaji na kushirikiana na mamlaka husika ili kuimarisha usalama wa jamii.

Kampeni ya Ongea na Kamanda inaendelea kutumika kama jukwaa la utoaji elimu na mawasiliano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, likiwapa fursa ya kuuliza maswali, kuwasilisha changamoto na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbali mbali ya kiusalama.
 

Attachments

  • VID-20261024-WA0219.mp4
    65.3 MB
  • IMG-20261024-WA0209.jpg
    IMG-20261024-WA0209.jpg
    235.6 KB · Views: 8
Back
Top Bottom