JamiiCheck imefuatilia na kujirirdhisha kuwa video hio si ya mwaka 2026 na haiendani na vita inayoendelea ya Marekani, Iran na Israel.
Video hiyo ni ya tukio lilitokea mwaka 1991 ambapo wanajeshi wa Marekani walikamatwa nchini Iraq wakati wa vita ya Ghuba iliyoanza mwaka 1990.
Aprili 5, 2026 Video hiyo ilichapishwa katika
chaneli ya Youtube ya APT News kama kumbukizi na kuambatanisha ujumbe unaosharia kuwa video hiyo ni tukio la mwaka 1991 baada ya Kanali David William Eberly kukamatwa punde baada ya ndege yake kushambuliwa.
APT waliandika:
Video hii ya kumbukumbu (throwback) inarejea tukio la Vita vya Ghuba vya mwaka 1991, ambapo Kanali wa Jeshi la Anga la Marekani, David William Eberly, rubani wa ndege aina ya F-15E Strike Eagle, alipigwa na kuangushwa nchini Iraq wakati wa Operesheni Desert Storm.
Kanali David William Eberly
alikuwa Mkurugenzi wa Operesheni katika Kikosi cha 4 cha Ndege za Kivita wakati wa Operesheni Desert Shield na Desert Storm. Alilazimika kujirusha (eject) kutoka kwenye ndege yake akiwa juu ya anga la Iraq katika usiku wa nne wa vita.
Alilikwepa jeshi la Iraq kwa siku tatu kabla ya kukamatwa na kuchukuliwa kama mfungwa wa vita (POW) tarehe 25 Januari 1991. Kanali Eberly alikuwa afisa mwenye cheo cha juu zaidi katika Kikosi cha 5 cha wafungwa wa vita wa Muungano (Allied POW Wing), na aliachiliwa huru tarehe 5 Machi 1991.
Kanali David
alikusanya zaidi ya saa 3,400 za kuruka akitumia ndege aina ya T-38 Talon, F-4E na F-4G Phantom II, pamoja na F-15E Strike Eagle, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika misheni za kivita wakati wa Vita vya Ghuba ya Uajemi.
Baada ya kustaafu kutoka Jeshi la Anga la Marekani, David William Eberly alichapisha kitabu kiitwacho Faith Beyond Belief mwaka 2002, kinachoelezea uzoefu wake katika Vita vya Ghuba.
Vita vya Ghuba vilikuwa mzozo wa kijeshi kati ya Iraq na muungano wa nchi 42 ulioongozwa na Marekani. Juhudi za muungano huo zilifanyika katika hatua mbili: Operesheni Desert Shield, ambayo ilihusisha kujenga nguvu za kijeshi kuanzia Agosti 1990 hadi Januari 1991; na Operesheni Desert Storm, iliyoanza na mashambulizi ya anga dhidi ya Iraq tarehe 17 Januari hadi ukombozi wa Kuwait ulioongozwa na Marekani tarehe 28 Februari.