SHAABAN ROBERT!
MIMI sichelei kufa, kudura yake Manani,
Kufa budi nitakufa, mchana ama jioni,
Hufa visivyo na ufa, sembuse aliye duni!
Nakata shingo nusufa, na mkia kiungoni.
Kama kufa ni maafa, naona bwana huponi,
Kiumbe hana sarifa, mauti yamo milini,
Nikifa hupati mafa, furaha yako nini?
Nakata shingo nusufa, na mkia kiungoni.
Ikiwa kufa kashifa, si peke yangu ufuni,
Ikiwa neno la dhifa, sina mfundo moyoni,
Iwapo kufa sharafa, sifi ninangoja nini?
Nakata shingo nusufa, na mkia kiungoni.
Hufa watu wenye sifa, na mafao duniani,
Wapenzi wake latifa, kama Mitume wa dini,
Hufa walaji wa mofa, na walao biriani,
Nakata shingo nusufa, na mkia kiungoni