Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Japo Jenerali Ulimwengu anasema hakuwa na urafiki wa karibu na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, wawili hao wana historia ya kufanya kazi pamoja, tangu wakiwa gazeti la Daily News miaka ya 1973- 74 na baadaye walipokutana kwenye siasa.
Hata hivyo, ilifika mahali wawili hao wakatofautiana na hapa Jenerali Ulimwengu ameeleza kwa kina sababu za kutofautiana kwao, katika mahojiano haya.
Endelea....
Swali: Kumekuwa na simulizi nyingi kuhusu uhusiano wako na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, nini kiliwafarakanisha wakati mlikuwa marafiki?
Jibu: Hapana. Mkapa hatujawahi kuwa marafiki hata kidogo. Alikuwa kama bosi wangu. Watu wanasema hivyo, lakini ukweli ni kwamba hajawahi kuwa rafiki yangu.
Mkapa alikuwa ni mtu anayejitenga sana na watu. Wewe fikiria mwaka 1995 anagombea urais, mimi ni kampeni meneja katika makampeni zake, nilikuwa chini ya Abdulrahman Kinana. Tatizo tulilopata kutoka kundi lolote lile kubwa ni waandishi na vyombo vya habari.
Sasa watu wakawa wanauliza, huyu si alikuwa mwandishi wa habari mbona anakuwa hivi?"
Nikawaambia hapana Mkapa hajawahi kuwa mwandishi wa habari Mkapa alikuwa ni mdhibiti wa habari aliyetumwa na Ikulu kudhibiti habari huko alikokwenda. Mimi nilikuwa namuita ni chief resident cencor (mdhibiti mkuu mkazi).
Maana yake mwandishi wa habari kwangu mimi ni mtu ambaye huko alikotoka aliwahi kusimama mbele ya mnyama mkali anayetisha anaitwa news editor ana stori yake kwenye mfuko wa suruali, halafu anaangalia sura ya yule mhariri wa habari anajishauri nimpe sasa hivi au niondoke nirudi nikiakiwa na smaili, huyu ndio mwanahabari.
Kwa sababu angekuwa mwanahabari asingepata taabu sana na waandishi wa habari huko walikuwa ni komredi wanazungumza kirahisi, hakuna itifaki nini wanagonga tano na nini, lakini Mkapa alikuwa ana uhusiano mbaya sana na waandishi wa habari.
Na kila alipoongea na waandishi wa habari alikuwa ni kukemea.
Mimi wakati ni mkuu wa kampuni ya Habari Corporation, alikuwa ananiuliza wakati mwingine hadharani, 'hivi bwana Jenaral hivi huwa mnafundisha kweli waandishi wa habari? Nilimwambia hapana mheshimiwa, hatujafunza waandishi wa habari si leo wala si miaka wewe ulipokuwa kwenye vyombo vya habari.
Swali: Wakati mnakutana Daily News mwaka 1973, uhusiano wenu ulikuwaje?
Jibu: Wakati naingia Daily News mwaka 1973 hakuwepo. Alikuwa kwenye nadhani idara ya Maelezo au vipi. Lakini alinikuta baadaye.
Nadhani mwaka mmoja baada ya mimi kuingia Daily News alikuja Mkapa akawa mhariri mtendaji mpaka nilipoondoka mwaka 1974.
Swali: Kuna wakati ulisafiri kwenda Msumbiji ukiambatanana aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Samora Marchel na inasemekana Mkapa ndiye aliyekupendekeza?
Jibu: Sijawahi kusema hivyo, ila kilichotokea ni kwamba yeye, alikuwa bosi wangu na ndiye aliyeniruhusu nisafiri.
Ilikuwa hivi, kuna siku tulikuwa katika hoteli ya Kilimanjaro, kulikuwa na mikutano ya ukombozi wa Afrika na sisi tumeketi pale mahala kulikuwa na baa inaitwa Zebra.
Tunapiga soga waandishi wa habari, mimi nilikuwa naeleza habari za ukombozi, maana wakati huo nimetoka chuo kikuu bado nina ari ya kuzungumza masuala haya na vijana wenzangu.
Basi akapita Samora Machel pale akasikia tunazungumza, hanijui, lakini kwa kuwa alikuwa anaelewa Kiswahili, akavutiwa na mjadala, akasogea.
Akaniambia, 'wewe unazungumza kama nani?'. Tukasimama kumsalimia na nini nikamwambia mimi nazungumza nawaambia vijana wenzangu kuhusu vita vya ukombozi vinavyokwenda.
Akasema, 'wewe unazungumzaje juu ya ukombozi kabla hujafika University of Mozambique, Universidade de Moçambique'. Nikamwambia, 'mnayo nyinyi basi? Si mpaka mpate uhuru wenu ndio mtengeneze hiyo university nitakuja mimi kusoma hapo'.
Akasema 'ipo'. Nikasema 'iko wapi?' akasema kama uko tayari kuja nitakuruhusu uje'. Nikamwambia niko tayari kama unayo niambie iko wapi. It was a joke.
Miezi miwili baadaye ndio ninaletewa meseji na Hashim Mbita sasa hiyo ndio ilipita kwa Mkapa kwamba kuna mtu wako anaitwa hivi na hivi, mwambie atoke ofisini aje na hatakwenda mahala pengine popote tukitoka hapa tunakwenda uwanja wa ndege. Na hivyo hiyo siku hiyo nikajikuta niko Newala. Na usiku ndio tukavuka kuelekea Msumbiji.
Swali: Alipokuwa Rais mwaka 1995, unasema ulikuwa ukienda kumwona Ikulu, ulikuwa na mambo gani kama hamkuwa marafiki?
Jibu: Nilikwenda kumuona kwa sababu nilikuwa na masuala muhimu. Eh, tuiweke hivi ni kwamba mimi sijawahi kuwa na uhusiano na Mkapa ambao ni wa kinabfsi).
Ila nimefanya kampeni yake mwaka 1995. Na kuna mambo ambayo tulikuwa tukirudia kuyazungumza mara kwa mara.
Swali: Mlikuwa mnazungumza nini?
Jibu: Kwanza kabisa nilikuwa nikimwambia wakati tuko kwenye kampeni na hata baada ya kumaliza kampeni, kwamba ingekuwa vyema kama Ikulu labda hata nyumbani kwake akawa na ubao wa mafanikio ya utawala wake kwa mambo ambayo amewaahidi Watanzania wakati wa kampeni.
Ili aweze kuyarejea mara kwa mara kwa kuangalia ni nini amefanya, kama ni program za kisheria, kama ni hatua za kiutendaji, au kama kama ni mahitaji ya watendaji.
Aweke vitu kwa sababu nilimwambia kabisa mimi sijawahi kuwa rais, ila nimewasoma marais wengi, hasa marais wa nje, wakuu wa nchi wa nje hasa Marekani, na mawaziri wakuu wa Uingereza, hivi mawaziri wakuu wa India na kadhalika.
Kuna tatizo la kuwa kulewa madaraka ya urais ukapanda kiasi cha kwamba ukapata kizunguzungu.
Ili kujikinga na hilo, nilikuwa namwambia Benjamin Mkapa, unahitaji uwe na timu ya rais ambayo ina watu unaowaamini, ili hayo uliyowaahidi Watanzania kwamba yanatekelezwa na waweze kukuambia ni wapi ulipo hivi sasa.
Kwa sababu yatakuja mambo mengi sana, utakuwa unakimbizana na vitu vilivyoibuka jana au leo asubuhi, kiasi cha kwamba hutaweza kuona nini kinatakiwa kifanyike kutokana na strategic vision uliyokuwa nayo.
Swali: Baada ya kampeni za uchaguzi mliendelea kukutana?
Jibu: Baada ya uchaguzi kwisha, tukawa tunapongezana kwamba kampeni imekwenda vizuri, akaenda kuapa.
Tukamwambia sasa tunakutakia kila la heri na tunajua kwamba utazingatia hayo ambayo tumeyazungumza.
Akataka kutupa namba yake, akasema 'eh na namba zangu kama mnaona kuna kitu chochote ambacho kinahitaji attention yangu, namba zangu hizi'.
Mimi nikamwambia 'hapana, hatuhitaji... mimi sihitaji kuwa na namba ya rais mkononi mwangu, inaweza kuwa ni hatari kwangu mimi'.
Akanicheka, akaniuliza 'mbona wewe eti hutaki?' nikamwambia anachoweza kufanya ni kutupa namba ya msaidizi wake ili tukitaka kumwona tutampigia. Akatupa namba mbili za msaidi wake anayeitwa Mombo.
Nilikwenda kuonana na Mkapa mara nane alipokuwa rais na nikuambie tu kwamba, kila nilipompigia Mombo simu na kumuomba anifanyie mpango nimuone rais, haikuchukua saa 24 nilimuona.
Swali: Ilikuwaje?
Jibu: Nilikwenda mara ya kwanza kabisa hiyo naikumbuka, Mkapa amekwenda Zanzibar, amekwenda mahala panaitwa Kibandamaiti. Mwanzoni kabisa 1996.
Akahutubia watu akasema yeye anamuunga mkono Salmin Amour (aliyekuwa rais wa Zanzibar) na akamuita Komandoo kwa mambo yote anayofanya kwa sababu ametumwa na CCM na anafanya kazi ya CCM na nini, na wapinzani 'wanikome'.
Hivyo hivyo, 'wanikome'. Mipasho. Kwa sababu hiyo kazi anafanya komandoo ni kazi aliyotumwa na CCM."
Siku hiyo hiyo nikampigia simu Mombo. Naomba kuonana na Rais Mkapa,
Nilipokwenda sasa Ikulu mara ya kwanza kabisa, nikamwambia 'nimesikia hotuba yako ya Kibandamaiti, imenishtusha sana'.
Nikamkumbusha niliyokuwa nimekwambia kila siku 'sijawahi kuwa rais wala sitarajii kuwa rais huko mbeleni, lakini hili linanihusu mimi'.
Kwa sababu kwanza umekuwa ukifuatilia taarifa za watu mbalimbali, hakuna mwenye uhakika Salmin alishinda uchaguzi.
Kwa maana hiyo Salmin anakuhitaji wewe kuliko wewe unavyomhitaji Salmin. Sasa sababu gani unakwenda kumpa kadi zako zote kwamba 'wanikome', uko nyuma yake Salmin, unaamini anachofanya ni kwa ajili ya CCM na nini? Nikamwambia 'huyu mtu anakuhitaji wewe ili apate authority hapo alipo, kwa nini unampa nguvu yote hii?
Nikamwambia mimi nina hofu kwamba Salmin hivi karibuni atakudharau, atakosa sababu ya kukuheshimu kwa sababu kadi zote umeshampabidhi yeye.
Akasema mambo mengi, kwamba hata mabalozi wamekuja wamesema hivi na vile, nikamwambia hapana, utaharibu heshima ya CCM.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza.
Swali: Mara nyingine mlizungumza nini?
Jibu: Mara ya pili ni pale alipokwenda Kimara (Dar es Salaam) na kuwaambia wananchi wanaobomolewa nyumba zao kwa sababu zimejengwa ndani ya hifadhi ya barabara.
Hayati John Magufuli akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi wakati huo, akasema hakuna fidia na ndiyo hizo amekuja kuendeleza ubomoaji alipokuwa rais. Lakini Mahakama sasa imemuru hao watu walipwe.
Nilichomwambia Rais Mkapa wakati ule ni kwamba, aliyezungumza kaba yako ni Magufuli ambaye ni Naibu Waziri, kati ya Naibu Waziri na Rais kuna umbali na kuna watu wengi, mkuu wa mkoa yuko wapi, Waziri yuko wapi, makamu wa rais yuko wapi?
Halafu kuna watu wamebomolew aisivyo haki, wengine wametapeliwa sawa, lakini hawana kosa, kwa nini usitumie vyombo vyako na unavyo vingi kuchunguza nani yuko sahihi na yupo hayuko sahihi?
Mara ya tatu ilikuwa ni pale nilikwenda kumtambulisha Profesa Issa Shivji. Mara ya nne ilikuwa ni kuhusu Shirika la Ndege la ATCL, nilimwambia kuna utapeli unafanywa na wakubwa wa Serikali kuiza kwa Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) kwa beri ya bure kabisa.
Kwa hiyo ilikuwa mara nane na mara zote hizo sikwenda kuomba fedha hata mara moja. Wakati wote kama tulivyokuwa Daily News, sijawahi kuhudhuria hata birthday moja za watoto wake, wala yeye hatjafika birthday hata moja ya mtoto wangu.
Kwa hiyo sio rafiki yangu kabisa.
Swali: Kwa nini kiliwafarakanisha?
Jibu: Kulikuwa na matatizo mengi, lakini mojawapo ni uandishi wa habari. Alikuwa anapata taabu sana kwamba mimi naweza kufanya uandishi wa habari unaomkosoa yeye wakati nimemfanyia kampeni awe rahisi, kitu ambacho hakiingii akilini.
Mimi nilimfanyia kampeni nikiamini atatekeleza yale tuliyotangaza, lakini ninavyoona sivyo unavyofanya.
Kwa mfano, suala la kuuza nyumba za Serikali, nani alifanya kampeni kwamba atauza nyumba za Serikali kwa bei za kutupa kabisa Sh8 milioni, milioni 15, wapi ulituambia utauza nyumba kwa marafiki zako kwa mahara zako? Nilikuwa namkumbusha.
Suala la kuuza shirika la Ndege (ATCL) kwa makaburu wakati ul, tulimpelekea kuonyesha kuwa wamesaini makubaliano ya kibiashara yanayoonyesha saini za watu wengi waliokuwa wakihusika na mawaziri wa Uganda, Afrika Kusini na wengine, lakini karatasi ya mkataba haipo.
Nilimpeleka mwenyekiti wa bodi yetu, wakati ule Balozi Abbas Sykes sasa ni marehemu.
Lingine ni uuzwaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa makaburu vilevile. Mimi nilimweleza kwamba ni makossa kuwauzia kwa sababu moja mbili tatu, kwamba mnaweza kuruhusu watu wafungue benki zao, lakini na Serikali iwe na benki yake ambayo itakuwa nauwezo wa uokozi, matatizo yakitokea huko mbele.
Mnawauzia kwa bei ya bure kabisa, mkataba wenyewe mnawapa na mali ambazo hazihusiani na benki kama mkataba unavyoonyesha majumba nchi nzima, mmewapa. Kwa kuchukua hizo nyumba tu, ABSA wanaweza kulipa hilo deni.
Sasa waziri wake ambaye sasa ni marehemu Dk Hassy Kitine, tulipata nyaraka zilizoonyesha kuwa ameiba.
Uandishi wa habari huwa unaanzia kwenye tips, inaweza kuwa ni tetesi, wewe kazi yako ni kuifuatilia kuona kama ni kweli. Usidharau hata siku moja, kama ni kweli ina masilahi na nchi? Kama ina masilahi, nani anahusika na amesaidiana na nani?
Ukishapata taarifa zako zote, mwendee huyo anahusika, muulize, mwambie chifu hii ni stori ndiyo tunaifuatulioa, je unakiri umehusika au unakanusha?
Tumempelekea waziri, wale vijana wangu wamekwenda, wamempelekea Waziri, majibu yake, mmetumwa na Ulimwengu? Basi mwambieni miminitamshughulikia, nikishamaliza kumshughulikia atakuja ka magoti hapa kuomba radhi.
Wakaja wale vijana, wakasema wakasema amekasirika sana, nikawauliza hakuwafungulia mbwa? Wakasema hakufungulia, maana wakati ule niliwaambia hata akiwafungulia mbwa kwa sababu umemwambia stori uliyonayo, hiyo kuwafungulia mbwa nayo ni sehemu ya story.
Nikasema kama amewaambia hivyo, chapisha. Ndiyo tukachapisha hiyo habari.
Baada ya habari kutoka kukawa na shinikizo la waziri kujiuzulu na Mkapa alimkingia kifua, lakini baadaye akajiuzulu.
Mkapa akaonyesha kusikitika, kana kwamba sisi ni wapiga majungu, basi tukamwacha.
Basi tukamwacha hivyo hivyo lakini nikajua kwamba hapa hakuna nia njema hata kidogo, na mambo yote tulikuwa tukifanya.
Tukaanza kusikia tetesi sasa watu wanatuambia kwamba tunajifanya sisi ni watu wa Nyerere sana. Wakati huo Mkapa ashaonyesha kwamba hamtaki kabisa Nyerere kwa sababu alikuwa anamwingilia mambo yake.
Swali: Je, huu ndio wakati ulionyang’anywa uraia wako?
Jibu: Ndiyo
Swali: Ilikuwaje?
Jibu: Kwanza kabisa serikali kusema mimi sio raia, sijawahi kuichukulia kama tatizo kubwa. Kwa sababu watu wote waliotoka mipakani, ukiwaangalia vizuri utakuta kuna kipengele kimoja cha sheria walishindwa kukitekeleza.
Hiyo shughuli ilisubiri miaka miwili wakitafuta watu watatu wengine wa kuwaweka pamoja na mimi ili isije ikaonekana ni mimi niwe nimebanwa.
Ikaonekana kwamba ni mimi kwa sababu hawa wote wanne walikubaliana kwamba wataomba uraia, na tukaomba sote, wakakubaliwa wote hao watatu walioingizwa dakika za mwisho, mimi nikakataliwa.
Ikawa ni uthibitisho wa hiyo niliyokuwa nimeambiwa. Hiyo nadhani ilikuwa mwaka 2001 au 2002.
Swali: Wewe ulijuaje kama ni njama?
Jibu: Haiwezekani ukawa na hali ambapo kuna njama ndani ya serikali dhidi yako halafu akakosa mtu ndani ya serikali wa kuja kukuambia.
Haiwezekani. Atakuja mtu mmoja... mimi nilikuwa na mtu ndani ya serikali, mtu very high up, na ananiambia kila kinachoendelea.
Mpaka nakuja kuuliza nini huyu mtu ana maslahi gani na mimi, kumbe ni mtu alikuwa na watoto wanasoma Oysterbay Primary School ambapo dada yangu naye ana watoto wake na alikuwa mwalimu pale.
Jibu: Na katika kuwashughulikia na kuwasaidia watoto wao wakawa marafiki wa familia ya dada yangu na huyu huyu mtu. Mimi sina habari. Lakini kila siku ananitafuta ananiambia 'wamefikia hapa, wamefikia hapa, mpaka kesho watatangaza hiki'. Kwa hiyo nilikuwa na onyo kila wakati la nini kitatokea.
Nilikuwa najua. Hata hiyo ya kusema kwamba sasa wamemaliza kukushughulikia wewe wanawatafuta wengine wenye hadhi."
Swali: Kwa hiyo ikachukua muda gani tena mpaka ukakubaliwa?"
Jibu: Ah ilichukua karibu miaka mpaka Mkapa anakaribia kumaliza. Eh, na kwa sasa kama hivyo ina maana nilikuwa sasa naishi kama nakwenda kuongeza muda wa uraia.
Tena wakati huo nikapata mialiko mingi sana mabalozi kwenda kutembelea nchi zao. Nawaambia mimi sina passport waniambia 'tafuta hata driver's license' halafu unavukaje hapo airport, 'tafuta karatasi yoyote tu'. Nikapewa sijui emergency travel document, temporary, vitu gani..."
Kwa hiyo, nilikuwa nasafiri, kipindi hicho nimesafiri sana kwa hizo travel documents kwa mabalozi kuniandikia mapendekezo kwamba ninapofika nchi nakokwenda nisipate taabu.
Kwa kweli hata kampeni nyingi, nilikuwa kampeni hapa nchini nyingi na watu kutoka nje wakawa wanamtukana Mkapa. Mimi nikawaambia 'jamani msiwe mnamtukana Mkapa maanake mtamfanya akasirike.
Hata hivyo, niliendelea kufanya kazi kwa kipindi chote hicho nimefanya kazi. Uhamiaji hawajui wanifanye nini sasa, nikawauliza sasa mimi mnanipeleka nchi gani? Wakasema 'hatukupeleki kokote bwana wewe ni mwananchi wetu bwana, si mtu wa hapa bwana' nawaambia 'sasa mbona mmeninyang'anya passport yangu?'
Wakaniambia 'ah no tutakuhakikisha kwamba wewe utatembea tu usiwe na wasiwasi'.
Swali: Mbali na Mkapa, unalinganishaje utawala wame na marais wengine tangu wakati wa Mwalimu Julius Nyerere, Mwinyi na hao wengine waliofuata?
Jibu: Kwa uaminifu, hadi kufikia kwa Rais Ali Hassan Mwinyi, sina matumaini makubwa kwa waliokuja baada yake.
Tunaenda tu, kama upepo unavyotupeleka.
Mwinyi alijua hawezi kujua kila kitu.
Wengine wanajifanya wanajua kila kitu. Hilo haliwezekani. Urais ni taasisi, unahitaji washauri.