Tulipokuwa watoto wadogo wakubwa zetu walikuwa wakitumia mbinu mbalimbali kutuhadaa. Kitu ambacho hatukujua ni kuwa tulikuwa tunadhulumiwa kitu fulani kwa kutumia ulaghai wa maneno matamu, na vichekesho visivyo na kichwa wala miguu. Mojawapo ya janja ya wakubwa hao ni ile ya kupukuchua mahindi.
Katika ulaghai huu kaka mkubwa au dada mkubwa alikuwa anachukua hindi lililochomwa ambalo mdogo wake ameshikilia na anamuahidi "kumtengenezea njia". Basi, katika kufanya hivyo atapuchukua mistari michache na kutengeneza njia ya kwenda "Dodoma" na hata ya kwenda "Iringa".
Zile punje za mahindi walizopukuchua hata hivyo walizibugia mdomoni kwa mbwembwe zote. Sisi wadogo zao tulifurahia kukabidhiwa mahindi yaliyotengenezwa njia kadhaa!
Ndugu zangu, kile ambacho Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini Bw. Edward Hosea alikifanya wiki iliyopita kina fanana kabisa na hadaa ya kupukuchua mahindi. Na alichofanya kamanda huyo kinazidi mazingaombwe ya Profesa Ndumba Nangae! Niwakumbushe kidogo kuhusu mazingaombwe. Katika mazingaombwe yoyote mwanamazingaombwe mahiri ni yule anayeweza kutumia "vipoteza lengo" ili kuficha vitu kwenye vidole au viganja vyake na hatimaye kufanya viini macho.
Bw. Hosea na wenzake wametumia suala la Waheshimiwa Zitto na Amina kutuletea taarifa muhimu na nyeti wakijua kwa hakika watanzania hawana muda wa kufuatilia na kuulizia kwa makini kwani wamenogewa na utamu wa kachumbari ya masuala ya mapenzi Bungeni!
Hata hivyo, kwa mzee wenu hapa kijijini hakuna jambo ambalo linahusu Tanzania litakaloachwa kupita bila kuangaliwa kwa karibu kama kupekua kwa kurunzi chini ya uvungu. Tulilizungumzia suala la Richmond tangu mwanzo wake na tukaweka wazi kuwa hicho kikampuni hakikuwa na uwezo wala ubavu wa kuleta majenereta na kuzalisha umeme!
Tukazua maswali ambayo maelezo ya Bw. Hosea hayakujaribu hata kidogo kujibu. Ni makusudio yangu kuyazua tena maswali haya ili kila Mtanzania aweze kuelewa ni jinsi gani Bw. Hosea na wenzake wamejaribu kutufunga kamba mbichi mchana kweupe.
Lengo langu ni kuonesha kuwa TAKURU ni chombo ambacho hakina ubavu wa kupambana na rushwa kubwa, na hakina uhuru wa kukabiliana na vigogo (na familia zao) katika vita za kutokomeza uovu huu. Miaka nenda rudi Takuru imekuwa ikikamata na kuwakaanga dagaa, ikiwachemsha kambare, wakati papa na nyangumi wakiendelea kuogelea bila hofu ya kukamatwa na nyavu hizo za TAKURU.
Takuru imebakia kuwa ni kama simba wa kwenye picha ambaye ametoa kucha na anaonekana kuunguruma huku meno yake yaliyochongoka yamekenuliwa! Wote tunajua simba huyo wa karatasi haumi ila anaweza kuwatisha watoto wadogo tu na watu wasio na akili timamu.
Kwa vile TAKURU wamesema kuwa kwenye suala la mkataba wa Richmond hakukuwa na vitendo vyovyote vya rushwa, tunaomba basi Bw. Hosea na wenzake wawajibu Watanzania wenzao maswali haya yafuatayo ambayo yamejengengeka tangu mkataba huu kuingiwa.
Kama ushahidi wa majibu yake anao wauweke hadharani au iundwe tumu huru yenye uwezo wa kuita mashahidi na wale wote waliohusika waweze kuitwa hadharani na kuhojiwa kuhusu kuhusika kwao. Maswali haya yana lengo la kutaka serikali iwe wazi na kutoa hadharani vidhibiti vyote ambavyo vimewafanya wafikie mahali pa kusema katika "mchakato mzima, hakuna rushwa"! Bw. Hosea, ya kweli hayo?
Kwanza, ilikuwaje kampuni ya hiyo ya Richmond Richmond Development (RDC) ipewe tenda hii? Majibu aliyoyatoa Bw. Hosea ni majibu ya kitoto na ya shule ya msingi. Iweje kampuni ya kupiga chapa na kuchapisha vijitabu na vielelezo ipewe tenda ya nishati? Tangu mwanzo wa suala hili kampuni hii imejivika majina ya ajabu ajabu na kutangaza uwezo wake.
Kinachoshangaza ni kuwa hakuna mtu katika serikali yetu aliyethubutu kuangalia kama kampuni hii ya RDC ina rekodi yoyote ya kushughulika na masuala ya nishati ukiondoa maelezo ya kwenye tovuti yao. Je, watendaji wetu walipitia ushahidi gani wa kazi za RDC na kuridhishwa nayo hadi kuamua kuwapa tenda ya mabilioni ya shilingi? Katika kuwapatia tenda hiyo, sheria ya manunuzi ya serikali ilizingatiwa kwa kiasi gani?
Pili, Wakati Balozi Andrew Daraja alipokwenda kutembelea Houston na kukaribishwa na viongozi wa kampuni ya Richmond Printing alioneshwa kitu gani hadi kukubali kuwa kampuni hiyo ina uwezo wa kushughulikia masuala ya nishati? Je aliona orodha gani ya nchi zilizoridhishwa na utendaji kazi wa RDC hadi kuipigia debe serikalini? Kama siyo yeye ni nani basi aliyesema kampuni hiyo ina uwezo wa kutuletea majenereta?
Tatu, kabla ya kampuni ya RDC kupewa tenda ya Nishati, ilipewa tenda nyingine ya kujenga bomba la mafuta toka Mwanza hadi Dar, bomba ambalo mradi wake ulibuniwa na kampuni ya Africommerce. RDC ilipopewa tenda hiyo kiulaini, watu wa Africommerce walilalamika kupokonywa mradi huo lakini viongozi wetu hawakujali hilo wakawapa RDC.
Miezi kumi na nane baadaye RDC walishindwa kufanya lolote na badala yake mradi huo ukapewa kampuni nyingine toka Uarabuni. Ilikuwaje kwa kampuni iliyoshindwa kuanza kutekeleza mkataba wa bomba la mafuta kwa miezi 18 kupewa mradi wa kuleta majenereta ndani ya wiki 14?
Jambo moja ni dhahiri. Mtu yule yule aliyeipigia debe kampuni hii hadi ikapewa mradi wa bomba la mafuta ndiye yule yule aliyeipigia debe na ikapewa mradi wa majenereta. Bw. Hosea yuko tayari kuwaambia na kuwathibitishia Watanzaina wenzake kuwa watu wale wale waliohusika na bomba la mafuta siyo waliohusika na mradi wa majenereta?
Nne, Kutokana na rekodi zilizoko kwenye ofisi ya Tarafa ya Harris (Harris County) kwenye jimbo la Texas, kampuni ya RDC imeorodheshwa kuanzia mwaka 2003 ikiwa ni sehemu ya kampuni mama ya Richmond Printing. Cha kushangaza ni kuwa chini ya mwaka mmoja baadaye kampuni hiyo ikapewa tenda ya bomba la mafuta nililotaja kwenye swali la tatu, na hivyo kina Elisante Muro kunyang'anywa mradi wao.
Je, Bw. Hosea na wakubwa wa Wizara ya Nishati na Madini wanaweza kuwaeleza Watanzania ilikuwaje kampuni changa namna hiyo kupewa mradi mkubwa wa nishati wakati haina historia ya biashara ya sekta husika? Je tukiwaambia kuwa hiyo ndiyo sababu ya mabenki ya Marekani kuikatalia mkopo wa fedha za awali kampuni hiyo kwa vile hawana historia ya mikopo kama kampuni ya nishati kina Hosea watakataa?
Kama Wamarekani wameona kuwa kampuni hiyo haina uwezo wa kustahili mkopo mkubwa wa fedha kiasi hicho ilikuwaje wasomi wetu na maafisa waliotajwa na Bw. Hosea wakakubali kuipa tenda? Ni nani huyo aliyeipigia debe kampuni hiyo na mtu huyo ana maslahi gani?
Tano, wakati Rais Kikwete anazungumza na wananchi mapema mwaka huu alielezea kusita kwake kukubali kampuni hiyo kupewa malipo ya aina yoyote na akawahakikishia wananchi kuwa RDC haikulipwa kwani alikuwa na mashaka nayo.
Je, TAKURU walimhoji Rais Kikwete awaelewe kwanini alisita na ni nani aliyemshawishi hadi akaacha mkataba huo kuendelea? Tukiwaambia kuwa yule aliyeipigia debe kampuni hii kwa Rais Kikwete na yule aliyehakikisha kampuni changa namna hii ilipewa tenda kuwa aidha ni mtu mmoja au wana udugu wa damu, Bw. Hosea anaweza kutuonesha kinyume chake?
Sita, inawezekana ni kweli kuwa hakukuwa na rushwa iliyolipwa moja kwa moja na ikapewa jina "rushwa" kwenye mchakato wa mkataba wa RDC. Hata hivyo hatuna budi kumuuliza Bw. Hosea kama alianza kuangalia mchakato huu kabla ya mkataba kuingiwa na umbali gani wa historia ya nyuma alienda.
Sijui kama Bw. Hosea anafahamu uhusiano wa karibu wa Bw. Msabaha na familia ya kina Gire uliodumu kwa miaka kadhaa sasa (kabla ya mikataba hii). Inapotokea kuwa rafiki wa familia anapewa mikataba miwili inayohusu sekta moja ambayo rafiki yao ndiye Waziri wa wizara hiyo hatuna budi kuhoji na kuchunguza mikataba hiyo.
Je, Bw. Hosea ameweza kumhoji Bw. Msabaha chini ya kiapo na kuhakikishiwa hakupokea yeye (au ndugu zake) kitu chochote ambacho kinakatazwa katika sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 na sheria nyingine?
Ni kwa kiasi gani urafiki wa Msabaha na kina Mohammed Gire,Naeem Gire, Zahor Gire, Abdul Gire, Imaduddin Gire, Mumtaz Gire, Adam Gire, Sharrifa Gire na ndugu zao walioko Ulaya na waliopo nyumbani ulichangia kwa wao kupewa tenda hizo?
Saba, katika maelezo yake kwa wananchi Bw. Hosea alisema wazi kuwa kutokana na dharura iliyotokea ya nishati Waziri Mkuu aliingilia kati na kuunda kamati ya watu watatu kuharakisha utatuzi wa tatizo la nishati. Swali langu kwa Bw. Hosea, je ni sheria gani inayompa madaraka Waziri Mkuu kusimamisha sheria ya ununuzi wa serikali ya 2004 na kuweza kuingilia utaratibu wa utoaji tenda?
Waziri Mkuu alipoingilia utaratibu uliowekwa wa kutoa tenda alifanya hivyo kwa mamlaka gani? Kusema kuwa ulikuwa ni "wakati wa dharura" ndio mwanzo wa kuleta maamuzi ya kiimla.
Kwa vile mtanzania mwenzetu ni Waziri Mkuu isiwe ni kisingizio cha mti huyo kupinda/kuvunja sheria kwani, ni wakati wa dharura ndipo tunataka kuona viongozi wetu wazisimamie sheria kwa umakini zaidi.
Kama kamati aliyounda Waziri Mkuu haina mamlaka ya kisheria, maamuzi yake basi pia ni batili hata kama yamefanywa kwa nia nzuri! Kwa maneno mengine, mkataba wa RDC uliingiwa kinyume na sheria na hivyo hauna nguvu ya kisheria, isipokuwa pale Bw. Hosea na wenzake watakapotuonesha utaratibu uliotumika kutoa tenda hiyo usiopingana na sheria ya Manunuzi ya Serikali ya mwaka 2004.
Nane, Bw. Mohammed Gire Afisa Mkuu Mtendaji wa RDC amekuwa akitoa michango wakati wa kampeni na bila ya shaka ndugu zake nao hufanya hivyo. Inafahamika kuwa kina Gire waliichangia CCM na kampeni yake ya uchaguzi ya mwaka 2005 (mwaka mmoja baada ya kampuni kuundwa).
Je, Bw. Hosea anaweza kuwaambia Watanzania ni kiasi gani kilipokewa toka kwa kina Gire kusaidia kampeni ya Rais Kikwete, ya Lowassa, na ya Msabaha? Tukimwambia kuwa kina Gire walichangia ya kutosha kampeni hizo wakiwa na matarajio ya kupewa mkataba wa Bomba la mafuta na kupewa mkataba mwingine wa nishati atatukatilia?
Je, michango ya namna hiyo haiwezi kuonekana kama ni rushwa? Kama CCM watapinga kuwa hawakupokea michango toka kina Gire, wako tayari kutoa orodha ya wachangiaji wao wakubwa wa ndani na nje ya nchi? Bw. Hosea anaweza kutaka orodha hiyo akapewa?
Tisa, katika suala hili zima, jina moja limekuwa likihusishwa na kupatikana kwa mkataba huu na kupewa tenda kwa RDC. Jina hilo ni la Waziri Mkuu Mhe. Edward Lowassa (Monduli - CCM). Wakati huo huo kumekuwa na tuhuma kuwa mmojawapo wa watu waliohusika katika kuipigia debe kampuni hii ni kijana mmoja mwenye mahusiano ya damu na Waziri Mkuu.
Ni kweli kuwa kijana huyo hayupo sasa kwenye orodha ya viongozi wa kampuni hiyo (kama alivyodai mmoja wa viongozi).
Swali kwa Bw. Hosea, je wakati wowote katika mchakato wa tenda hii kuna ndugu wa kiongozi aliyekuwa na nafasi ya uongozi na baadaye akajiondoa/kuondolewa kwa sababu ya kuonekana mgongano wa maslahi? Mtu huyo ni nani na nafasi yake ni ipi? Je serikali ilipata nafasi ya kumhoji?
Kumi, tumeambiwa kuwa RDC hawakulipwa na serikali kwa sababu ya kushindwa kutimiza mkataba, hilo linawezekana kuwa ni kweli lakini ni kweli kuwa fedha za serikali hazikufikia mifuko ya kampuni hiyo? Ni nani aliuza mkataba wa RDC kwa Dowans?
Kama Richmond waliuza mkataba huo kwa kipengele walichoweka kwenye mkataba, na serikali ikailipa Dowans dola milioni zaidi ya mia moja, je RDC hawakulipwa na Dowans? Bw. Hosea anaweza kuuhakikishia umma wa Watanzania kuwa hilo la kuuza mkataba halikuwa "janja ya nyani" kwa RDC kulipwa bila ya kufanya kazi!
Naweza kuendelea kuuliza maswali mengi, lakini kwa leo wacha niishie hapa ili niwape muda wa TAKURU kutafuta majibu. Wakisha jibu hayo nitaangalia kama nina maswali mengine ya ziada (na uzee huu maswali yanajileta yenyewe tu). Nafahamu ugumu wa Bw. Hosea na waliohusika kujibu maswali haya kwa undani na kwa ukweli kwani wameshafikia uamuzi wa kusema "hakukuwa na rushwa".
Kilichotokea ndugu zangu ni kile ambacho kilishuhudiwa kwenye fainali ya kombe la dunia mwaka 1986 kule Mexico wakati timu ya Argentina ikiongozwa na mchawi wa soka Diego Armando Maradona ilipoweza kuifunga timu ngumu ya Uingereza kwa lile goli ambalo limebakia likijulikana kama "goli la mkono wa Mungu".
Maradona alifunga goli hilo kwa kunyanyua mkono wake juu ya kichwa chake na mwamuzi alidhania ameona goli la kichwa. Wakati wachezaji wa Uingereza wanalalamika mwamuzi alielekeza mkono katikati ya uwanja. Watanzania tumefungwa goli la Maradona, hakuna pa kulalamika isipokuwa kuendelea kuuliza maswali.
Hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa ili kuionesha RDC kwa ukweli wake na jinsi mkataba huu ulivyokuwa na maswali mengi. Mwamuzi (Bw. Hosea) keshahesabu goli, na kapiga kipenga mkono ukielekezwa kwenye mduara wa uwanja, mpira kati! Tushangilie au tulie?