SIMULIZI: ELECTION SAGA (MONEY IN BLOOD)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
UKURASA WA HAMSINI NA SABA
“Mtu ambaye anayatafuta sana maisha yako”
“Nimekuuliza nahitaji jina lake na nataka uniambie kajuaje kwamba mimi ndiye ninacho hicho kirusi kwenye mkono wangu?”
“Kumbe hata wewe unaogopa eeh?”
“Unahisi namuogopa mbwa yoyote ndani ya nchi hii labda?”
“Anaitwa Tommy” mkurugenzi aliongea kwa masikitiko sana kwa sababu alikuwa amemchomea bwana mkubwa ili apate huruma ya familia yake kuweza kuachwa hai.
“Tommy yupi?”
“Mtoto wa Apson Limo”
“Una maanisha kwamba ndiye ambaye yupo nyuma ya haya mauaji ambayo yanaendelea?”
“Ndo huyo huyo”
“Hili linawezekanaje?”
“Na huyo ndiye ambaye anajua kwamba wewe una hicho kirusi kwenye mkono wako na hata ule mkutano wako na gaidi mwenzako ambaye mlipanga kukiuza kwa bei ghali sana huko uarabuni yeye ndiye ambaye amenipa hiyo taarifa ndiyo maana nilitokea lile eneo”
“Ooooh shiit! Amewezaje kujua haya mambo yote?” aliuliza kwa ukali akiwa anamsogelea mkurugenzi huyo kwa hasira.
“Hata mimi sijui amejuaje ila anajua kila hatua yako ambayo unaipiga hivyo jiandae muda wowote kuanzia sasa anaweza kukutafuta”
“Hawezi, hawezi, mimi ndiye mtu mkubwa zaidi ndani ya taifa hili, unahisi kuna binadamu anaweza kunigusa mimi? Nataka kujua kwamba umesemaje yeye ndiye emekitengeneza?”
“Yule alikitengeneza akiwa huko nchini Uingereza”
“Ebu nipe maelezo ya kutosha, yule gaidi aliniambia kwamba kiliibiwa kutoka kwenye mikono ya MI6 sasa unaniambiaje kwamba huyo mtoto ndiye ambaye alikitenegeneza?”
“Nikikwambia hili jambo naomba umuache mwanangu aliyebaki na mke wangu tafadhali”
“Yes, natafanya hivyo”
“Tommy ni moja kati ya majasusi kutoka ndani ya shirika hilo la MI6” Hilo ni jambo ambalo lilimfanya Boniphace Walawala abaki ameachana mdomo wake tu asiamini kwamba hicho kilichokuwa kinaongelewa kilikuwa ni cha kweli maana ni kama taarifa zilikuja kipindi ambacho hakuwa amezitegemea.
“No, no, haiwezekani kuhusu hili jambo”
“Hata mimi nilipigwa na mshangao zaidi yako lakini haikubadili ukweli kwamba inabakia kuwa hivyo”
“Wewe hizi taarifa ulizijulia wapi?”
“Kwake mwenyewe”
“Anawezaje kukupa taarifa zake kiwepesi sana namna hii?”
“Tulikuwa na makubaliano ya kazi hivyo tukaamua kuelezana uhalisia wa mambo ulivyo ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja”
“Huyo bwana mdogo amefanya kosa kubwa sana, naenda kuua familia yake yote kisha nitamaliza na yeye mwenyewe”
“Usifanye hilo kosa kwa sababu kama ukikurupuka kidogo tu ana ushahidi wako mwingi sana wa mambo ambayo unayafanya hivyo inaweza kukufanya ukajulikana na dunia nzima kwamba unataka kuiingiza dunia kwenye matatizo kwahiyo unahisi ni nchi gani itakubali hilo jambo litokee? Utaanza kusakwa sana na umoja wa mataifa, kama una shida ya kumaliziana naye mtafute yeye kama yeye na sio kugusa familia yake tena kwa sababu hata sasa anajua kwamba na wewe pia umehusika kwenye yale matatizo ambayo yameikumba familia yake hivyo anakuhesabia ni siku zako tu”
“Hawezi kunisogelea mimi kwa sababu huo utakuwa mwishio wake, naenda kumtafuta kila kona ya jiji hili, naenda kumsaka kila sehemu ambayo mwanadamu anaweza kujificha na kama nikimpata basi atajuta kuzaliwa kwenye dunia hii”
“Usihangaike sana hata kumtafuta kwa sababu muda ukifika atakujia yeye mwenyewe hata hivi kama sio mimi kumuomba muda kwanza huenda mpaka sasa angekuwa amesha wafikia. Najua unajiamini sana kwa sababu humjui wala hujawahi kumuona gizani na mambo ambayo anayafanya” aliongea kiongozi huyo wa usalama huku akimrushia mheshimiwa simu aweze kuangalia baadhi ya video za marejeo ambazo zilikuwa zinamuonyesha mwanaume huyo akiufanya mauaji, alikuwa anaua kikatili sana mpaka hata kiongozi huyo alijikuta anasisimka sana.
Alitoa ishara kwa walinzi wake ambao walimshambulia mtoto wa mkurugenzi aliyekuwa amebaki kwa risasi nyingi sana hata mkewe akiwa amezimia alipigwa risasi pale pale. Lingson alishikwa na uchungu sana kwani kama kumpa taarifa alizo zihitaji alikuwa amempatia lakini bado mtu huyo akaamua kuiua familia yake yote. Hali hiyo ilimfanya ashikwe na hasira sana kitu ambacho kilimfanya awasogelee watu hao akihitaji kuwavaa lakini kabla hata hajamfikia kiongozi huyo alipigwa risasi nyingi sana kichwani.
“Nooooooo” ni sauti ambayo ilisikika juu ya fensi ya jumba hilo ikiita kwa uchungu huku mtu huyo akiwa anarusha risasi kwa nguvu, risasi ambazo ziliondoka na walinzi wa raisi watatu baada ya kupigwa kweye vichwa. Mwanaume ambaye alikuwa anapiga makelele alikuwa ni Nick, wakati anafika ndani ya eneo hilo ndio wakati ambao kiongozi wake huyo alikuwa anapigwa risasi huku akishuhudia hivyo hakuweza kuvumilia, alipiga makelele huku naye akiwa anashambulia.
Kelele zile ndizo ziliwashtua watu hao lakini walikuwa wamechelewa kwani wenzao watatu walikuwa wamepoteza misha tayari hivyo wengi walimzingira mheshimiwa huku wengine wakiendelea kumrushia risasi kwa wingi sana Nick ambazo zilimfanya arukie upande wa pili na kutoweka hilo eneo.
“Amekimbia mheshimiwa ila haweza kufanikiwa kutoka nje ya jiji hili tutamtafuta kila kona” aliongea mlinzi ambaye alikuwa ametoka mpaka nje kwenda kumsaka mwanaume huyo.
‘Ni nani huyo?”
“Ni jasusi kutoka ndani ya idara ya usalama anaitwa Matiasi ndugu. Huyu ndiye ambaye mr Lingson alikuwa akimwamini sana ndiyo maana baada ya kufika tu hapa na kuona kiongozi wake anapigwa risasi ameanza kushambulia na huyu ndiye ambaye anazijua siri nyingi sana za huyu mzee kwani ni kama mkono wake wa kulia”
“Nahitaji atafutwe kila sehemu, atafutwe kwenye kila kichochoro ndani ya jiji hili na namtaka akiwa hai huyu anaweza kunisaidia kwenye mambo mengi sana”
“Sawa mheshimiwa”
“Na kwenye hii nyumba safisheni kila kitu kiasi kwamba pabakie kama hakuna ambacho kimetokea hapa na hii nyumba kuanzia kesho awekwe mtu hapa aanze kukaa ili mtu yeyote asije akahisi jambo lolote lile”
“Nimekuelewa bosi” mheshimiwa alimaliza kazi ambayo ilikuwa imempeleka huko huku akiwa amefanikiwa kuzijua na siri kadhaa ambazo zingeenda kuwa msaada mkubwa sana kwake.
Yalikuwa ni mazoea sasa ndani ya jiji la Dar es salaam kwamba usiku hauwezi kuisha bila mauaji kuweza kufanyika. Hata siku hiyo ndani ya jiji la Dar asubuhi na mapema sana wakati wavuvi wanaelekea baharini kuweza kuifanya kazi yao, waliukuta mwili wa kiongozi mkuu ambaye alikuwa anadili na makosa ya jinai nchini ukiwa umetupwa huko na mtu huyo amepigwa risasi za kutosha. Hawakuwa na namna zaidi ya kuliripoti jambo hilo polisi na habari hizo zikaanza kusambazwa kila sehemu na kila kona ya jiji.
Kuna watu ambao walijiita kwamba wao ni wajuvi wa mambo na walikuwa na habari nyingi za nchi pia walithibitisha kwamba hata mkurugenzi wa usalama wa taifa alikuwa ameuliwa usiku huo huo. Hizo ni habari ambazo zilibakia kuwa kama tetesi tu kwenye masikio ya watu wengi kwani hakuna mtu hata mmoja ambaye alikuwa anaweza kuzithibitisha moja kwa moja mbele za watu wengi. Jiji lilikuwa linaendelea kutisha kila siku ilivyokuwa inazidi kupungua na kuwafanya hata wananchi waache kabisa kujiamini huku wale waoga sana wakianza kulikimbia taratibu maana ilionekana kuwa sehemu ya watu ambao walikuwa na mabavu na uwezo mkubwa wa kuyafanya makubwa ambayo wengi hawakuwa na uwezo wa kuyafanya.
“Hivi kwa haya ambayo yanatokea nchini alaumiwe nani?”
“Ni ngumu sana kumpata mtu sahihi wa kuweza kumlaumu moja kwa moja nadhani labda ulaumiwe mfumo”
“Unahisi ni kwanini labda?”
“Kwa sababu kuna sehemu unataka kumlaumu raisi lakini unagundua kwamba hata viongozi wa huku chini wameamua kujigeuza vibaraka. Ngoja nikupe mfano, mimi niliwahi kubahatika siku moja kupata mwaliko bungeni kwenda kusikiliza, mategemeo yangu niliwahi kufikiria kwamba wale jamaa ile nafasi wanaitumia kueleza matatizo ambayo majimbo yao yanapitia, nilijua wabunge wapo pale kwa ajili ya kutoa kero za wananchi, niliamini kwamba wapo pale ili kuzipigania sehemu ambazo wanaziendesha lakini pia kutoa hoja zenye mashiko kuhusu mwelekeo wa taifa kwa ujumla ila nilichokishuhudia mle ndani ndicho kilinimaliza nguvu sana nikaamini kwamba kwenye taifa hili ili tuje kufanikiwa basi huenda kuna miaka hata mia tano mbele huko kama miaka ya hapa katikati tutakuwa tunapata viongozi wa aina hii hii”
“Kitu gani hicho ulikishuhudia huko bungeni?”
“Wabunge ni watumwa kifikra, wabunge ni watu wasio jiamini, wabunge ni vibaraka wa viongozi wakubwa lakini wabunge wengi wana uwezo mdogo sana kichwani kiasi kwamba ukimpa maiki azungumze, kwenye dakika tatu mpaka tano ambazo atatumia, dakika mbili na nusu mpaka nne na nusu anazitumia kumsifia raisi wa nchi jambo ambalo lilinishangaza mno zaidi ya sana. Kila mbunge lazima aanze kwanza namshukuru mheshimiwa raisi mara ikawa hivi ikawa vile kitu ambacho kinafanya hata hizo kero za wananchi wao zisizungumzwe tena na zinakuwa kama zinafukiwa jumla na wananchi wanasahaulika. Hapo ndipo nikataka kujua kwamba ni kwanini watu hao wanachagua kuwa watumwa kwa raisi?”
“Enhe uligundua kitu gani hapo”
“Kumbe wengi wanakuwa wanafanya hivyo ili waweze kupata nafasi mbali mbali kama uwaziri na maeneo mengine ya muhimu”
“Hilo ni jambo la hatari sana”
“Yeah ni jambo la hatari sana kwa sababu hata raisi mwenyewe anakuwa hawezi kusikia kero za wananchi kwani watu ambao wamepewa dhamana ya kuwawakilisha wananchi hao wanaitumia kumsifia yeye huku wananchi wakiwa hawana hata umeme wa uhakika, hawana huduma za maji ya uhakika, hawana huduma za barabara lakini hata mahospitali hakuna na ndio hao watu wao wanatumia muda mwingi kumsifia raisi bungeni hapo unategemea nini ndugu yangu?”
“Hapo kweli tunaingia pabaya sana”
“Hapawezi kuwa pazuri, mimi kama ningepewa nafasi ya kuishauri serikali moja kati ya jambo ambalo ningewashauri ni kwamba watoe kigezo cha mtu akitaka kuwa waziri lazima awe mbunge kwanza kwa sababu inawafanya wabunge waishie kuwasifia tu wakubwa hususani raisi ili tu awateue wale ambao anahisi kwamba wanamfaa yeye kwa sababu wanamsifia kila wakati kwahiyo anaamini kwamba wale wanao msifia watamlindia maslahi yake na atawatumikisha kadri anavyo hitaji yeye kwa sababu wanakuwa hawana kauli mbele yake”
57 niseme basi.
Wasalaam,
Febiani Babuya.