SIMULIZI: ELECTION SAGA (MONEY IN BLOOD)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
UKURASA WA TATU
“Wakati ukiwa kiongozi, ulikuwa ni moja ya watu wa mfano kwangu hali ambayo ilinifanya mimi nikufuatilie wewe kwa ukaribu sana, kwenye kukufuatilia kwa umakini nilijifunza vitu vingi sana kwako lakini sikuishia hapo tu bali niliyajua mengi sana ambayo yalikuwa kwako na yalikuwa yakikuzunguka” mr Mafupa alijikohoza kidogo kisha akaendelea tena.
“Huko Kahama kuna migodi yako ambayo ilikuwa inakuingizia pesa nyingi sana ila kwa bahati mbaya ikaja kubinafsishwa na serikali ikakutishia kukupatia kesi ya uhujumu uchumi kama utakuja kuifuatilia tena kitu ambacho kilikupelekea wewe kuingia hasara kubwa sana mpaka mwisho wa siku ukawa kama umeikatia tamaa kabisa. Sasa nahitaji hivyo vitu nivirudishe kwenye mikono yako lakini pia utakuwa mtu wangu wa karibu sana hali ambayo itapelekea wewe kuweza kufanya biashara yoyote ile ambayo utajisikia ndani ya nchi hii na hakuna mtu yeyote yule ambaye atakugusa. Hayo yote hayawezi kufanyika mimi nikiwa nje huku na ndiyo sababu ni lazima uhakikishe naingia Ikulu ili haya yote yaweze kutimia kwa urahisi zaidi” Mr Mafupa baada ya kumaliza maelezo yake alitulia kwanza na kuhema akiwa anamsikilizia kigogo huyo aweze kuongea lolote.
Mr Oscar alimwangalia sana mwanaume huyo ambaye alionekana kuwa na moto usio wa kawaida kuweza kuingia Ikulu, aliinyanyua pombe kwenye chupa na kuinywa yote, akatikisa kichwa chake na kuuinua uso wake kumwangalia tena Mr Mafupa kwa umakini akiwa kama anapima jambo kwenye macho yake.
“Wakati unaingizwa kwenye baraza la mawaziri nilijua kabisa nchi imepata kirusi kipya ambacho kitakuwa ni hatari sana kwa taifa hili. Ni hatari sana kama nchi inaanza kuwa na viongozi wenye tamaa kubwa sana namna hiyo kushika madaraka kwani kinachokuwa kinawapeleka pale ni maslahi yao tu na sio kuipigania nchi, hali hii inanifanya niwaonee sana huruma watu maskini japo sio biashara yangu hivyo inabidi tu wapambane na hali zao maana mimi hayanihusu. Mimi nitakusaidia wewe kukichukua hicho kiti lakini kama ukija kwenda nje na maneno yako au ukanisaliti basi wewe na familia yako ambayo huwa unaificha na kuwadanganya watu kwamba hauna, nitawafanyia kitu kibaya sana. Nina imani kama ulinichunguza basi utakuwa unajua mimi ni mtu wa namna gani hususani pale anapo tokea mtu na kunisaliti” aliongea kwa msisitizo sana maneno ambayo aliamini kwamba Mr Mafupa alikuwa akiyasikia vyema kabisa kwenye ngoma za maskio yake.
“Nakuelewa mheshimiwa, mpaka nakuja hapa nakuamini sana hivyo siwezi kupoteza imani kwa mtu anaye niamini kwa sababu siku nyingine yakinikuta nitakuwa sina pa kukimbilia, hivyo nakupa maneno yangu siwezi kwenda nje na makubaliano yetu”
“Mimi nakusaidia lakini kwa sharti kubwa moja”
“Nakusikiliza mheshimiwa”
“Mimi nataka kuwa nje kabisa ya haya mambo”
“Unamaanisha hautaki kujulikana kama umenisaidia wala kuwa na mimi upande mmoja?”
“Safi, kumbe umekomaa kisiasa na tunaongea lugha moja. Mimi sitaki kabisa kujulikana kwamba nipo kwenye hii michezo, mimi sitaki kutajwa tajwa kwenye vyombo vya habari, mimi sitaki kabisa hata wewe ujulikane kwamba huwa tunakutana au kuwasiliana. Mimi nitakuwa kama kivuli tu kwako na hili jambo hatakiwi kulijua mtu yeyote yule kwamba mimi nilikuwa nyuma yako maana inaweza kuwa na athari baadae hata ukikichukua kiti wananchi watakuwa hawakuamini kabisa kwa kujua kwamba una uwezo mdogo sana ndiyo maana uliwategemea watu wengine ili kupata nafasi. Kama nikija kujua kwamba maongezi yangu mimi na wewe yapo kwa mtu mwingine au kukutana kwetu kuna mtu mwingine anajua nadhani unajua ni kipi ambacho nitakifanya kwako na kwa watu wako wanao kuzunguka”
“Nimekuelewa vizuri mheshimiwa”
“Una mpango gani kwa sasa?”
“Nataka kwanza niipate imani ya wananchi”
“Unaipataje”
“Nadhani nitumie pesa nyingi sana kwa sasa kuweza kuziridhisha nafsi zao”
“Huwa unafikiria kweli kabla ya kufanya maamuzi? Mbona unakurupuka sana? Una miaka mingapi kwenye siasa?”
“Ni zaidi ya miaka ishirini”
“Haukutakiwa kuwepo huku, bado una akili za darasa la saba. Kwa miaka yote hiyo ambayo ulikuwa kwenye siasa kuna jambo gani la maana ambalo umewafanyia wananchi kiasi kwamba wakukumbuke wewe au kukupa imani?”
“Sina imani sana kama lipo”
“Usiwe na mawazo kama mtoto mdogo. Wananchi huwezi kuzishinda imani zao kwa kuwapa pesa japo haimaanishi kwamba watazikataa pesa zako, dunia hii hakuna mtu anazikataa pesa ila unahisi hata baada ya kupata pesa hizo ndo watakupigia kura? Hapana hata wao wanajua wewe ni mtu mjinga tu ambaye hauna huo uwezo wa kuiendesha nchi hii hivyo kwa kutupia pesa tu pekee hakuna utakacho kipata zaidi ya kupoteza tu, akili inatakiwa kuanza kwanza ndipo pesa inafuata na hivyo ndivyo jinsi siasa inavyofanya kazi”
“Unaweza ukanipa maelezo zaidi kiongozi?”
“Kitu pekee ambacho unatakiwa kukifanya wewe ni kuhakikisha kwamba wananchi hawana chaguo lingine zaidi ya kukuchagua wewe, ndiyo njia ambayo utaitumia kuweza kuingia Ikulu kirahisi sana”
“Unamaanisha kwamba niwaue wapinzani wangu ili mwenye nguvu nibaki mwenyewe?” Mr Mafupa aliuliza akiwa ana hamu kubwa sana ya kuweza kujua kwani alikuwa mbele ya mtu ambaye alikuwa ni mkongwe mkubwa sana wa siasa na alikuwa na uzoefu kuliko yeye hivyo hata nchi yeye ndiye alikuwa anaijua zaidi yake hata namna siasa ilivyokuwa inafanya kazi kwa sababu aliwahi kuwa waziri mkuu wa nchi. Mr Oscar alitabasamu na kunywa pombe nyingine ili kuendelea kukiweka kichwa sawa kuweza kutengeneza hoja kwenye hilo eneo ambalo aliona moja kwa moja lina maslahi makubwa sana kwake.
“Moja kati ya njia nzuri zaidi ya kumshinda adui yako sio kuwa na mipango hatari zaidi bali ni kuidhoofisha mipango yake yeye, ndiyo sababu kubwa huwa unaona kwenye masoko kampuni zinazo fanikiwa sana ni zile ambazo zinawekeza sana kumsoma mpinzani wake, wanakuwa wanajua huyu mjinga atatoka hapa ataenda pale hivyo sisi tunageuza kete tu kuiweka pale ushindi tunachukulia mezani kirahisi sana. Hata kwenye siasa ipo hivyo ukiujua udhaifu mkubwa wa mpinzani wako hata ukikurupuka saa tisa usiku basi mchezo utakao ucheza unashinda ndani ya dakika kumi tu za mwanzo na sio tisini” Mr Oscar alimtazama Mr Mafupa ambaye alikuwa makini sana kuisikiliza kila sentensi ambayo ilikuwa inatamkwa pale. Baada ya utulivu huo wa muda mfupi kupita Mr Oscar aliendelea;
“Kumfanya mtu asiwe na chaguo, ina maana atafanya lile lililo mbele yake hata kama halipendi au halihitaji. Ni sawa na mtu mwenye njaa kali na hapendi aina fulani ya chakula, kama chakula ambacho kipo ndicho pekee kinachoweza kuituliza njaa yake hata kama atakula kwa manung’uniko ila bado atakuwa amekula tu. Kwa maana hiyo inatakiwa ucheze na udhaifu wa wenzako. Tafuta udhaifu wao mkubwa kisha utumie kuwateketeza maana siasa haitaki huruma, siasa inataka wanaume ambao huwa tunasema kwamba wanakuwa wameaga kwao”
“Jambo la pili ukisha ujua udhaifu wao na kuutumia ili kuwafanya wananchi wasiwe na namna hakikisha una watu wa kukulinda endapo kuna mambo mabaya yataanza kujitokeza kwa baadae. Najua utapata kiburi kwa sababu upo na mimi ila hapa nazungumzia kwamba unatakiwa kuishinda mioyo wa wale viongozi wa ngazi za juu zaidi kwenye jeshi la polisi, jeshi la nchi pamoja na wale watu wa usalama. Hawa watu ukiingia Ikulu watakuwa chini yako ndiyo na wewe ndiye unaye wateua na kuwatoa pale unapo jisikia mwenyewe lakini kuwa chini yako haimaanishi kwamba watakuwa waaminifu kwako au watakuwa wanakusikiliza, ili wakusikilize inatakiwa uishinde mioyo yao na kuwafanya wawe waaminifu sana kwako kwa kila jambo na kila hatua. Sasa wanakuwaje waaminifu kwako?” mheshimiwa alitulia tena na kutoa bunda la noti kisha akaliweka mezani. Akaendelea;
“Hawa inatakiwa ule nao vizuri tu, yaani wape wanacho kihitaji na kwa sababu moyo wa mwanadamu umeumbwa na matamanio basi pesa itakuwa ndiyo njia nzuri zaidi ya kuwashawishi wao kuwa upande wako yaani unakuwa kama mfuga mbwa na namna mbwa ambavyo anakuwa anakutii kwa sababu wewe ndiye unamlisha. Ukifanya hivyo hawa watakusikiliza sana na ndio ambao watakuwa wanakuletea habari zote na kukufanyia kazi zote chafu ambazo wewe hutataka kuhusika moja kwa moja wala kutaka kujulikana kama ulikuwa unahusika nazo. Lakini ukiishi na hawa vibaya wanaweza hata kukutoa kwenye hicho kiti na usiwe na la kufanya hususani wakiamua kuungana pamoja hivyo hawatakiwi kuwa karibu sana hawa watu wao kwa wao kwa gharama yoyote ile”
“Kitu ambacho unatakiwa kukikumbuka sana ni namna unavyo itumia akili yako kuwaweka hawa watu kwenye mikono yako, sio kila sehemu itatumika pesa na sio kila sehemu yatahitajika mabavu ila kuna sehemu itahitajika zaidi akili. Hawa watu kabla ya kuwapa hiyo ofa ya maisha mazuri hakikisha kwanza umewatafiti na kujua kila mmoja anavutiwa sana na nini na hicho ndicho utakacho kitumia kumkamatia, kirahisi sana atakuwa kwenye mkono wako”
“Kama ukiona kuna mmoja wapo anaanza kwenda tofauti na unavyo hitaji wewe basi hakikisha anakuwa wa kwanza kumezwa na udongo yaani umuue haraka sana kwa sababu ukichelewa tu itakugeukia wewe mwenyewe, ila hiyo hali ya kumuua inatakiwa kuwa ya mwisho kabisa pale ambapo njia zingine zinakuwa zimeshindikana kabisa kutumika na hakuna namna nyingine zaidi ya hiyo. Hapo nadhani umejifunza jambo kwamba ni mhimu hizo nafasi nyeti uwape watu wako ambao unawaamini kana kwamba likitokea tatizo watakulinda maana sio kila kiongozi ana tamaa ya pesa, kuna watu ni wazalendo isivyo kawaida yaani kwao pesa sio chochote sasa ukijichanganya kumpa mtu kama huyo nafasi wakati unajijua wewe sio mzalendo ndipo utakapo anza kuona hicho kiti ni kichungu sana.” Mr Oscar aliendelea kumpa somo Mr Mafupa kama alivyokuwa anahitaji kisha akaendela;
“Unamjua mshindani wako mkubwa?”
“Ndiyo, ndiyo namjua, ni Mr Apson Limo”
“Kwanini unahisi hivyo?”
“Kwa sababu anapendwa sana na wananchi na ndiye kipenzi cha wananchi ambaye wananchi ndio walimuomba aweze kuingia Ikulu”
“Umeona namna wenzako wanavyokuwa wanazipata imani za wananchi eeh”
“Mhhhhh sijui aliwezaje kufanya hivi”
“Ni namna unavyokuwa unajiweka, ukiwa na malengo ya mbali na ndivyo unavyokuja kuwa. Hauwezi ukawa kibaka mtaani halafu unajua kabisa baadae unataka kuwa kiongozi, unadhani nani atakupa nchi? Lakini ukijiweka kwa namna inayo takiwa basi wananchi wenyewe watakuomba uwe mtu fulani na ndicho kinacho tokea kwa Apson, tangu zamani amekuwa mtu wa kusaidia sana jamii, mtu safi hata kwenye wizara akili yake imebadilisha sana mambo mengi ya nchi, sasa unahisi mtu kama yule unaweza kushindana naye wewe?”
“Hapana hapana”
“Ndiyo maana nimekwambia unatakiwa kuwafanya wananchi wasiwe na chaguo lingine”
“Kwahiyo unataka nimuue Apson Limo”
“Mimi siwezi kukupangia cha kufanya ila kitu cha kwanza unatakiwa kuutafuta udhaifu wake mkubwa ulipo. Mara nyingi mtu anakuwa sawa pale ambapo vitu anavyo vipenda vipo sawa ila visipokuwa sawa hata ile nguvu ya kupambana huwezi ukaiona tena kwake hiyo inakuwa ni nafasi yako kubwa ya wewe kushinda huku ukiwa na hao watu wa mamlaka na nafasi kubwa za ulinzi na usalama basi unakuwa unafanya unacho kitaka”
“Mr Limo udhaifu wake mkubwa sana ni familia yake, kwake familia ni kila kitu na ndiyo ambayo inampa nguvu kubwa sana ya mapambano hivyo kama ukiiyumbisha familia yake basi atakuwa kwenye hali mbaya sana kitu ambacho kitamfanya awe anafanya maamuzi ya kukurupuka na kila kitu hakikisha wananchi wanakijua. Itafika wakati wataona kwamba mtu ambaye wanampenda hayupo sawa kutokana na matatizo ambayo yanampata na wakisema wampe Ikulu huenda itakuwa hatari kubwa sana hivyo wataamua kumpatia mtu wa pili ambaye utakuwa ni wewe hapo. Ila kama ikishindikana basi muue” maelezo hayo ya Mr Oscar yalilichanua tabasamu kwa mr Mafupa na ndiyo maana alimfuata mzee huyo kwani hakukosea kabisa.
“Hahahaha hahahaa sikufanya kabisa makosa kukuchagua wewe kuwa role model wangu maana ni mtu mwenye mawazo mapana na unaona mbali sana. Hili ni jambo ambalo nilikuwa naliwaza tangu muda sana kwamba huenda mambo yatakuwa hivi, hivyo kuna jambo ambalo nililifanya mapema kama kujilinda tu sasa naanza kuuona umuhimu wake” Mr Mfupa aliongea kwa furaha sana
“Lipi hilo?”
“Nilisha ingia tayari kwenye familia yake”
“Una maanisha nini?”
“Unajua kwenye ujana wangu nilikuwa na mambo mengi sana hivyo kuna mtoto ambaye nilimpata kwa siri na huwa sipendi sana ajulikane kwamba ni wangu ila namtunza kwa kila kitu na ndiye ambaye anafanya kazi zangu nyingi sana kwa siri na ndiye ambaye nilimtumia kumuingiza kwenye ile familia”
“Usiniambie kwamba ndiye mpenzi wa yule binti mkubwa wa mr Apson?”
“Ndiyo mheshimiwa” jibu la Mr Mafupa lilimfanya mr Oscar kucheka sana
“Hahahah hahahah wewe mjinga kumbe kuna muda huwa una akili kidogo, hilo ni moja kati ya jambo bora sana kuwahi kulifanya kwenye maisha yako, enhe ni mpango upi ambao unafuata kwenye akili yako”
“Kama ulivyo nipa ushauri nataka nimdhoofishe kupitia familia yake huku nikijiweka mbali sana na masuala ya ugomvi ili yakitokea nisije nikaonekana nahusika kwa lolote. Nataka nimuue binti yake wa mwisho ambaye ndiye kipenzi cha familia kwa sababu ndiye ambaye anapendwa sana, kufa kwake litakuwa pengo kubwa sana kwao hivyo lazima familia itayumba pakubwa sana lakini wakati hilo likifanyika basi nitampoteza na binti yake mkubwa kupitia mwanangu hivyo hakuna ambaye atajua yupo wapi sasa hapo ndipo nitaamua kutokana na hali atakayo kuwa nayo Mr Apson kama nimuue au nifanyaje”
Unayaamini maneno ya Mr Mafupa? Mimi sijui ila ukurasa wa tatu naishia hapa.
Wasalaam,
Febiani Babuya.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app