SIMULIZI: ELECTION SAGA (MONEY IN BLOOD)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
UKURASA WA ISHIRINI NA MOJA
“Una maanisha nani na kwa sababu ipi?” swali lake liliashiria kwamba alikuwa anaulizia mtu ambaye alitakiwa kuishi kwenye sura yake na kwa sababu ipi mpaka awe huyo mtu.
“Mr Oscar” baada ya jina hilo kutajwa raisi alihema na kutikisa kichwa akiwa anasikitika, mzee huyo alikuwa mbele ya muda kwenye suala zima la kufikiria, alijiona mwamba sana kuwa na mtu mwenye akili kama huyo kwenye mkono wake hivyo alitaka kuelewa sababu ya msingi hasa ilikuwa ni ipi?
“Haujanipa sababu”
“Kosa ambalo Mr Oscar amelifanya kwa miaka yake ya uongozi na hata sasa ni kuamini kwamba yeye ni mtu mwenye nguvu kubwa sana na anaweza kufanya lolote ndiyo maana hata siku ile ulisema kwamba anaanza kukutishia kwa sababu aliamini kwamba anaweza kukuendesha hata wewe bila kukujua kiundani. Lakini ni kwamba vijana wake wengi ni vijana wetu hivyo ni suala la muda tu tukihitaji kumdondosha chini pale uingie wewe”
“Hiyo inahusiana vipi na mimi kuachia madaraka”
“Nadhani unakumbuka kwamba Mafupa siku kadhaa nyuma alikutana na mr Oscar na kuomba msaada wa kusaidiwa kwenye uchaguzi?”
“Hilo nalijua ndiyo”
“Sasa kwenye hayo makubaliano alimpa sharti Mafupa kwamba akiingia madarakani anatakiwa kufanya kazi chini yake hivyo yule atakuwa kama raisi kivuli tu ila nchi itakuwa inaendeshwa na mr Oscar. Sasa vipi kama wewe ukiwa mr Oscar ukawa unamuendesha mtu ambaye yupo madarakani kama unavyotaka mwenyewe na akafanya yale ambayo wewe unayahitaji kwa muda ambao unautaka wewe?”
“Hahahaahah hahaha” raisi alicheka sana huku akiwa anapiga makofi kwa furaha, ni michezo ya akili ambayo ilikuwa inatakiwa hapo. Maana raisi huyo kwa mambo ambayo alikuwa ameyafanya kwenye uongozi wake, viongozi wengi hususani wa vyombo vya usalama hawakuwa wakimkubali sana na huenda siku moja wangekuja kumuanika mabaya yake hivyo huo ushauri ulikuwa unamuweka nje ya mchezo mazima na angeendelea kula mema ya nchi kwa utulivu pasipo kuumiza kichwa huku misala yote akimuuzia mwenzake ambaye alitakiwa kuingia madarakani wakati huo.
“Itakuwa hivyo mheshimiwa, halafu kwenye hiyo frash kuna mazungumzo yao yote juu ya waliyo kubaliana lakini pia kuna historia nzima ya maisha ya mr Oscar na Mafupa mwenyewe”
“Maana yake mr Oscar anatakiwa kufa haraka sio?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Hahahahahaha hahahha nabaki na yule mwanamke wake pamoja na binti yake ambaye kamficha kwa muda mrefu sana”
“Kitu cha kusikitisha ni kwamba yule sio binti yake”
“Whaaaat?”
“Yule ni binti wa mwanamke ambaye yeye aliwahi kumpenda sana lakini baada ya kujichimbia kwenye siasa alikuja kupotea muda fulani alipo enda kwenye majukumu ya nje ya nchi wakati anarudi alimkuta mwanamke yule amezaa na mtu mwingine na wakati ule mtoto alikuwa ni mchanga na kwa bahati mbaya sana tangu mwanamke yule aweze kujifungua alisumbuliwa na magonjwa ambayo yaliuchukua uhai wake hivyo kwa sababu alikuwa na mapenzi mazito sana na mwanamke yule aliamua kumlea yule mtoto kama wake na anampenda kuliko kitu chochote kile huenda ni kwa sababu hana uwezo wa kuzaa”
“Kuna mwingine anaye lijua hili jambo?”
“Hapana mheshimiwa”
“Fanya kama hakuna kilichowahi kutokea na lisije likatoka kwa mtu yeyote yule. Nitakapokuwa tayari nitakupa taarifa hivyo jiandae maana wewe unatakiwa kubaki Ikulu hapa kwa namna yoyote ile ili yule mpuuzi kama akiingia hapa afanye kile ambacho nataka mimi” mheshimiwa alionekana moja kwa moja kuridhia ushuri huo wa mshauri wake kwani aliona ni ushauri mzuri sana na unao faa, angekaa sehemu akiwa anayafaidi mema ya nchi huku akimuuzia misala mwenzake ambaye yeye alikuwa anafikiria pesa tu huku wenzake wakiwa wanafikiria pesa kwa kuitawala akili ya mtu ambaye anaweza kuziwezesha hizo pesa kwanza.
“Sawa mkuu hilo nitalifanyia kazi mapema sana”
“Unaweza kwenda” Raisi alimruhusu mzee huyo aweze kutoweka ndani ya hilo eneo.
Tommy baada ya kutoka ndani ya kituo kikubwa cha polisi aliweze kurudi tena hospitali kuweza kujua hali ya baba yake kwani mara ya mwisho baada ya kumfikisha tu mzee huyo haspitali alikamatwa na kupelekwa kituoni ambako aliishia kuua polisi wawili ambao walikuwa wakimtesa tena mbele ya IGP. Kurudi kwake ndani ya hospitali ni kwa sababu alikuwa anahitaji kuweza kupata majibu ya ile oparesheni ambayo baba yake aliweza kufanyiwa.
Alikuta madaktari hao wamemaliza kazi na huenda walikuwa wanamsubiri ni yeye tu, majibu ambayo walimpatia yalimkatisha tamaa sana. Baba yake alikuwa ametolewa risasi kwenye mwili wake na kuondolewa kwenye hali ya hatari ambayo huenda ingeyachukua maisha yake ila kitu cha kusikitisha ni kwamba mzee Apson alikuwa amepata koma na angekaa kitandani huenda kwa miaka yake yote ambayo angekuwa hai labda kama ungetokea muujiza wa Mungu ndipo angeweza kupona na kurudi kwenye hali yake ya kawaida tena.
Tommy aliingia ndani ya hiyo wodi kumuangalia baba yake, mzee huyo alikuwa amelazwa kwenye kitanda huku akiwa anapumulia mipira, alisikitika kwa sababu kulikuwa na uwezekano baba yake kuyatumia maisha yake yaliyokuwa yamebakia akiwa juu ya hicho kitanda. Alikuwa anakumbuka mbali sana namna baba yake alivyokuwa mtu bora na baba bora sana kwa familia yake, alikuwa anaukumbuka ule ucheshi na utani wa baba yake, alikaa kwenye kiti akiwa anamwangalia kwa uchungu sana mwanaume.
Alikuwa anawaza mambo mengi sana kwenye kichwa chake lakini baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanamuwazisha kichwa ni kwamba mpaka wakati huo hakuwa amempata dada yake je angeanza vipi kutoa taarifa zingine hizo za baba yake kuwa kwenye hiyo hali kwa mama yake mzazi? Kilikuwa ni kitu ambacho kisingewezekana kabisa hivyo alitakiwa kwanza kumtafuta dada yake na kama angefanikiwa kumpata basi ndipo angetakiwa kumtaarifu mama yake kuhusu suala la baba yake huku akiwa amemrudisha Patrina nyumbani.
Hilo ndilo lilimkumbusha kwamba hakuwa na muda wa kulala wala kupoteza kwani usiku huo huo alitakiwa kumtafuta dada yake haraka sana hivyo akaitoa simu yake na kuwapigia walinzi ambao walikuwa wanashughulika na hiyo kesi ya dada yake tangu mchana wa siku hiyo. Baada ya kupewa maelekezo yote kuhusu mtu ambaye walimhisi lakini na hatua zote ambazo walikuwa wamezichukua, mwanaume aliamua kwanza kwenda kwenye kampuni ya urembo ya dada yake ambapo alikagua kila kitu mpaka zile cctv kamera za mle ndani kisha akatoka na kuelekea Upanga nyumbani kwa akina Noelia mwanamke ambaye alikuwa ndie rafiki mkubwa wa Linda au Patrina.
Baada ya kufika ndani ya hilo eneo mwanaume alishuka na kugonga geti ambapo ilichukua muda sana mpaka mlinzi kuweza kufungua geti hilo, baada ya kujitambulisha alikaribishwa mpaka ndani ambapo alikutana na bibi pamoja na mjukuu wake wote wakiwa sebuleni na mambo yao ila iliwalazimu kuweza kumsikiliza. Kwa Noelia ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kabisa kuweza kumuona mwanaume huyo kwenye maskio yake ambaye sifa zake nyingi alikuwa akizisikia tu kwa dada yake, na alikuwa akivutiwa sana na mwanaume huyo kwa sababu alikuwa na mwonekano mzuri sana isivyokuwa kawaida.
“Shikamoo bibi” alimsalimia bibi huyo huku akiwa anampa mkono Noelia na binti alibakia ameushikilia tu huo mkono kana kwamba hakuwa akihitaji kuuachia kabisa.
“Marahaba mjukuu wangu karibu sana”
“Nadhani utakuwa haunifahamu ila mimi ni mtoto wa Apson Limo” alijitambulisha mbele ya mwanamke huyo mzee ambaye aliishia kutabasamu.
“Kwa mtu ambaye yupo makini na macho yake basi hauna haja ya kujitambulisha mbele yake kwani unafanana sana na baba yako, jisikie upo nyumbani”
“Samahani sana bibi kwa kuwasumbua na usiku wote huu ila sina namna kwani jambo hili ni mhimu sana kwa upande wangu na familia, mimi kidogo sikuwepo nchini na baada ya kurudi ndo nakutana na hali kama hii ambayo inaendelea, imenifanya nisiwe na namna zaidi ya kufanya hivi”
“Usijali mjukuu wangu naelewa nini maana ya maumivu ya familia hivyo unacho kifanya upo sahihi kabisa” bibi huyo baada ya kumjibu hivyo ni kama alikuwa nampa ruhusa ya kumhoji mtu wake na hicho ndicho ambacho alikifanya
“Nina imani utakuwa na taarifa zozote kuhusu kupotea kwa dada yangu. Nimesikia mchana umefanikiwa kuwaeleza walinzi baadhi ya taarifa ambazo kwa namna moja ama nyingine zimesaidia sana lakini una uhakika kwamba hakuna kitu hata kimoja ambacho ulikisahau?” sauti hiyo ni kama ilimshtua Noelia maana muda wote alikuwa akimkadiria sana mwanaume huyo.
“Hapana mimi nina muda mrefu sana sijawasiliana naye kwa sababu nilitakiwa kusafiri hivyo sijakutana naye wala kuwasiliana naye kwa muda na kile ambacho nimewaeleza ndicho ambacho nilikuwa nakifahamu tu”
“Ushawahi kumuona labda anagombana na mtu au kujibishana na mtu vibaya?”
“Hapana hajawahi kuwa mtu wa hivyo hata siku moja”
“Wewe ni kipi ambacho unakijua kuhusu kupotea kwake?”
“Hakuna ninacho kijua”
“Unaweza ukaniazima simu yako?” swali la Tommy lilimfanya mwanamke huyo kuonyesha mashtuko wa wazi kwani hata Tommy aliuona kwenye macho yake, alifanya hivyo makusudi kwa sababu aliambiwa kwamba mwanamke huyo ilionekana kabisa kwamba kuna mambo alikuwa anayaficha na huenda anajua ukweli au kuna taarifa anazo ambazo hakuhitaji watu hao waweze kuzipata”
“Simu yangu nilikuwa nachezea imeisha chaji kwa sasa labda mpaka niichaji” jibu lake ndilo ambalo lilionyesha moja kwa moja kwamba ni kweli kuna mambo ambayo alikuwa anayajua mwanamke huyo. Tommy hakuongea kitu zaidi ya kubaki amemkazia macho tu kwa muda kisha akayarudisha tena kwa bibi na kuweza kumuaga.
“Bibi asante sana kwa kunikaribisha nyumbani, nina imani ipo siku nyingine tutaonana tena, nawatakieni usiku mwema” mwanaume aliaga ghafla sana kitu ambacho hata bibi huyo na Noelia mwenyewe kiliwashtua maana walihisi huenda anaweza kuendelea kuuliza maswali mengine hata bibi huyo alianza kuhisi kwamba labda huenda mjukuu wake anajua kitu maana alikuwa anatoa majibu ambayo ni wazi yalionyesha hakutaka kabisa kutoa ushirikiano wakati huyo alikuwa ni rafiki yake kabisa wa karibu.
Mwanaume baada ya kuaga alitoka mpaka nje ya geti kisha mlinzi akafunga geti hilo, Tommy aliiangalia saa yake, ulikuwa unasoma mshale was aa nane ya usiku, alitikisa kichwa chake kama kukubali jambo. Alisimama nje ya hilo geti kwa dakika tano kisha akaanza kuondoka huku akiwa ameiacha gari yake hilo eneo na haikujulikana kama ilikuwa ni kwa bahati mbaya au kwa makusudi. Alikuwa anatembea taratibu sana kama mtu mwenye mawazo ila ni kama vile kuna mtu ambaye alikuwa akimsubiri hilo eneo huenda ndiyo sababu aliamua kuiacha gari yake ambayo alikuja nayo. Mwendo wake ulikuwa unazidi kumsogeza mpaka alipofika mita kama miatatu kutoka nyumbani kwa akina Noelia ndipo aliposimama baada ya umeme kukatika ghafla.
Ishirini na moja naweka nukta hapa.
Wasalaamu,
Febiani Babuya.