Follow along with the video below to see how to install our site as a web app on your home screen.
Note: This feature may not be available in some browsers.
WellSIMULIZI: ELECTION SAGA (MONEY IN BLOOD)
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
UKURASA WA PILI
Mr Apson baada ya safari yake ya muda mfupi ambao aliutumia kuendesha gari yake kwa kasi isiyo ya kawaida alifanikiwa kufika nyumbani akiwa anahema kwa nguvu mno, walinzi wake walibaki wanamshangaa kiongozi huyo maana hakuwahi kuwa kwenye hali kama hiyo siku zote za maisha yake hata ule msafara wake ambao ulikuwa unamlinda ulikuwa unamshangaa kiongozi huyo kwani hakuwa akiendesha gari bali alikuwa akiendeshwa siku zote lakini siku hiyo alitoka ofisini na kuingia kwenye gari akaitoa kwa kasi bila taarifa hali ambayo ilipelekea walinzi wake kumfuata nyuma na magari mengine.
Alikuwa anaishi maisha ya kifahari sana mheshimiwa Apson kwani hata jumba lake tu lilielezea namna alivyokuwa na maisha mazuri. Aliwapita walinzi wake kama vile hakuwa akiwaona huku gari akiwa ameiacha nje. Alikimbilia mpaka ndani lakini hakukuta mtu ila alisikia kelele upende wa pili ambako aliwaona watoto wake wakiwa wanacheza na mkewe, alijikuta anatabasamu na kukaa kwenye korido ya kushukia eneo hilo ambalo lilikuwa na bustani nzuri na bwana la kuogelea akiwa anaiangalia familia yake.
Kwake familia ilikuwa kila kitu, hakuwa na kitu ambacho angeweza kukiweka sawa na hiyo familia akakilinganisha kwenye mzani mmoja. Mkewe alikuwa ni rafiki mkubwa sana kwa wanae hususani yule mtoto wa mwisho ambaye ndiye alionekana kupendwa kuliko wengine wote. Baada ya kuona watu hao hawana muda naye kabisa ikabidi ajikohoze kidogo ili kuwashtua na ndipo hapo walipo tulia kwanza na kugeukia upande ambao yeye alikuwepo.
Mtu wa kwanza kumkimbilia alikuwa ni mwanae wa mwisho wa kike ambaye ndiye alikuwa kipenzi chake, alimkumbatia baba yake huku akidai zawadi zake lakini tajiri huyo hakuwa na zawadi kwa muda huo kwani aliondoka kwa kasi tu kuweza kuwahi nyumbani hakuwa hata na muda wa kubeba zawadi yoyote ile hivyo akamuahidi mwanae kwamba angemletea baadae maana ameagiza tayari.
Watoto wote walimkumbatia kwa mapenzi mazito mno kuonyesha ni familia ambayo ilikuwa na raha mstarehe isivyo kawaida, mtu wa mwisho kabisa alikuwa mkewe ambaye alimkumbatia baada ya watoto kuondoka na kwenda ndani. Akiwa kwenye kifua cha mmewe aliinua uso wake na kumtazama mwanaume huyo kwenye uso wake
“Una hofu sana, nini shida baba?” kitu ambacho hakuwa na uwezo wa kukificha ni uhalisia wake kwa mwanamke huyo ambaye alikuwa anamjua vizuri sana, kumkumbatia tu kidogo aligundua kwamba mumewe alikuwa na wasiwasi isiyo ya kawaida.
“Nawaza sana kuhusu mustakabali wa maisha yangu kuhusu siasa, siasa naiona kabisa kama sio sehemu salama kwangu, nadhani ile siku ambayo nilikubali kuwa mwanasiasa ndiyo siku ambayo niliamua kuitoa sadaka familia yangu. Naomba unisamehe mke wangu, naogopa sana” aliongea huku akiwa anaketi chini kwenye hizo korido lakini mkewe alimkumbatia na kukilaza kichwa cha mumewe kwenye mapaja yake.
“Hili unalo lifanya ndilo limeifanya familia hii kuwa yenye furaha kubwa sana, watoto huwa wanajivunia sana kuwa na baba kama wewe hususani unapokuwa mbele ya vyombo vya habari ukiwa unaongea, namna unavyo tengeneza hoja fikirishi, namna ulivyokuwa mtu wa kuwaza mambo makubwa na mambo ambayo yanajenga fikra za mtu yeyote hivyo hauna haja ya kutuomba sisi msamaha bali unatufanya tujivunie kuwa na wewe. Najua siasa ina mambo mengi sana na sio hapa tu bali duniani kote kwani unakuwa na maadui wengi sana na ndiyo maana wewe hapo una mke ili pale unapokuwa kwenye hali kama hii mimi nipo kukuweka sawa. Kitu ambacho unatakiwa kukifanya popote ulipo kifanye kwa ukubwa hata kama utakutana na changamoto gani kwa sababu unatakiwa kujua kwamba mkeo ndiyo mshabiki wako namba moja ambaye anakupenda sana kama kiongozi wake lakini pia anakupenda na kukuheshimu kama mumewe” alitabasamu mr Apson na hiyo ndiyo sababu ambayo mara nyingi sana ilikuwa ikimfanya amuwaze mkewe kila anapokuwa mbali naye. Huyo mwanamke alikuwa chanzo kikubwa sana cha furaha kwake, ambapo angehisi kuchanganyikiwa basi akiwa mbele ya mwanamke huyo alikuwa anakuwa sawa. Mawazo yake yote yaliisha ndani ya dakika moja wakajikuta wote wanacheka sana huku wakitaniana na mkewe alimtaka mwanaume huyo akaoge kisha wakapate chakula pamoja.
“Dady nataka kumuona kaka, nimemmiss” ilikuwa ni sauti ya Latifa ambaye alikuwa ndiye mtoto wa mwisho kabisa wa mr Apson, aliongea wakati wakiwa wanaendelea kupata chakula. Kauli yake aliiongea kwa masikitiko sana, alikuwa ni mtoto wa mwisho ambaye alipendwa sana hivyo wazazi walikuwa tayari kufanya lolote kwa ajili yake yeye. Ndani ya familia hiyo kulikuwa na mtoto wa kiume mmoja tu ambaye alikuwa anaelewana sana na Latifa na ndiyo sababu alikuwa akimkumbuka sana kaka yake kwani ndiye aliyekuwa akimpenda sana kuliko ndugu zake wengine wote.
Mr Apson aligeukia upande wa ukutani akiwa kwenye tabasamu zito, ukutani palikuwa na picha kubwa sana ya wanaume wawili wakiwa ndani ya suti za blue ambazo zilikuwa zinafanana kwa kila kitu. Wanaume hao walikuwa wanafanana mno ila kilichokuwa kinawatofautisha ni umri, upara na kitambi. Mr Apson kwenye hiyo picha ndiye alikuwa na umri mkubwa zaidi, na ndiye ambaye alikuwa na kitambi pamoja na upara ila ilikuwa ni tofauti kwa huyo mwanaume mwingine ambaye bila shaka alikuwa ni mwanae wa damu kwani alikuwa anafanana naye utadhani alijitoa kopi yake.
Huyo ndiye alikuwa mwanae pekee wa kiume ambaye ndiye alikuwa mrithi wake kwa kila kitu hivyo mwanae huyo wa kike kudai anataka kumuona kaka yake, alitabasamu sana baada ya kuiona ile picha kisha akatamka
“That’s my boy” aliongea akiwa na cheko la furaha kisha akaitoa simu yake na kupiga video call kwa mtu huyo ambaye alionekana kuwa nje ya nchi ili mdogo wake huyo aweze kumuona. Kweli simu iliita kwa muda mfupi kisha ikapokelea na mtu ambaye ungehisi ni yeye mwenyewe kwa namna walivyokuwa wanafanana. Hawakuongea lolote zaidi ya kumpa simu kwanza Latifa maana angeanza kusalimiana na wengine hapo ingekuwa kesi nyingine hiyo. Alifurahi sana kumuona kaka yake ambaye alimpenda mno kisha kijana huyo akawasalimia na wengine kisha akakata simu yake huku akiahidi kwamba muda mfupi ambao ulikuwa unakuja angeweza kurudi nchini maana amemaliza masomo na kwa wakati huo alikuwa anatalii kabla ya kuianza safari.
“Mwanangu arudi tu nimemkumbuka sana, ni muda sana sijampikia chakula change, watakuwa wanamlisha mavyakula ya hovyo ya dukani huko maana naona amepungua sana” aliongea mama yake akiwa amemkazia macho mumewe kama kumwambia hakikisha mtoto anarudi haraka namtaka nyumbani hapa. Mzee Apson ilibidi ajikohoze maana mkewe alimpiga jicho kali mpaka yeye mwenyewe ikabidi azuge kwa kubadilisha maada ya hapo.
“Linda yuko wapi?” aliuliza swali kuhusu uwepo wa binti yake mkubwa ambaye ndiye alikuwa mtoto wa kwanza kuzaliwa kwenye familia.
“Atakuwa kwenye biashara zake huko maana alisema kwamba amepata watu wa nje wa kufanya nao kazi nadhani atakuwa anamalizana nao kwenye masuala mazima ya mikataba” mkewe alimjibu kwa ufupi ili kumridhisha maana mzee huyo kwa namna alivyokuwa anawapenda wanae kama asingepewa taarifa ya maana angeacha hata kula hapo akamtafute mwanae.
“Hahahaha my princess, anapambana sana ndiyo maana najivunia yeye kuwa wa kwanza kuzaliwa kwani anakuwa mfano kwa wenzake kila inapo itwa leo. Nataka nimfungulie kampuni kubwa zaidi ya mitindo maana ile aliyo nayo kwa sasa ana uwezo wa kuisimamia vizuri hahahaha nataka mwanangu awe malkia wa mitindo kwenye hili bara zima la Afrika” aliongea kwa kutamba mzee huyo akiwa ananyanyuka na kucheza kidogo kitu kilicho pelekea wote kulipuka kwa kicheko maana mzee huyo alikuwa mwenye furaha sana na alipenda wakati wote familia yake iwe ina furaha.
“Na mimi sasa unitafutie biashara kubwa nyingine sio unawawaza wanao tu unamsahau mkeo aliyekuletea hao watoto, yaani nyie wanaume mkiwa na watoto tu hata mke unamsahau sijui mlirogwa na nani” mkewe aliongea huku akiwa anacheka kitu kilichofanya watoto wote wamzunguke kumcheka.
“Mama unawaonea wivu hadi wanao hahahahaha” wanae walikuwa wanamcheka huku wakiwa wanamtekenya, walianza kukimbizana humo ndani huku mumewe akikimbilia bwawani kuogelea. Ilikuwa ni moja ya familia ambazo zilikuwa kwenye furaha kubwa sana.
Ndani ya jengo lingine kubwa la kifahari majira ya usiku, alionekana mr Mafupa akiwa anavuta sigara yake ya bei ghali akiwa ametulia sehemu ambayo bila shaka ilikuwa ni mapokezi akiwa anasubiria kukutana na mwenyeji wake. Baada ya dakika tano za kusubiri akiwa anaivuta sigara yake, alikuja mwanaume mmoja ambaye alikuwa amejaa sana kwenye mwili wake na kumtaka asimame. Hakuwa na usumbufu wowote kwani alisimama na kuikabidhi sigara hiyo kwa kijana wake ambaye alikuwa amemshikia mkoba wake kisha akasimama na kuanza kusachiwa kama ana silaha yoyote kwenye mwili wake na baada ya kuonekana kwamba hana shida, mwanaume huyo alimpa ishara ya kumfuata ili akakutane na mtu ambaye alikuja kumuona huku mlinzi wake akibakia nje sehemu ya mapokezi.
Baada ya kuingia ndani alikutana na mtu mmoja ambaye alikuwa amesimama kageukia ukutani akiwa anaangalia picha kubwa nzuri za gharama ambazo zilikuwa zimepambwa ukutani mwili wake ukiwa ndani ya kanzu ndefu sana nyeupa na kichwa chake kikiwa wazi kabisa.
“Samahani sana kwa kukuingilia kiongozi, naona unajikumbushia mbali sana kwa kuangalia picha nzuri za kihistoria” Mr Mafupa aliongea huku akiwa anautua mkoba wake chini na kubaki amesimama kama alivyo ingia maana hakuona kama ni sahihi kukaa kabla ya kukaribishwa ingali mwenyeji wake naye bado amesimama.
“Unajua watu wengi mpaka leo bado hawajui kwamba hii ni moja ya nchi zilizo barikiwa kila kitu. Huwezi kuamini kwamba haya mazingira yapo hapa hapa Tanzania na hata mchoraji ni mtanzania, hizi ni miongoni mwa picha adimu sana kupatikana duniani hata nikiamua kusema nazipeleka kwenye minada huko kwa wenzetu naweza kutengeneza pesa ambayo nitakula mpaka nakufa na bado nitaiacha”
“Mhhhhh sasa kwanini hauziuzi?”
“Kuna muda kwenye maisha yako hakikisha kwenye mkono wako una vitu vya thamani ambavyo ni adimu kupatikana hiyo itakufanya upate heshima kubwa sana kwenye maisha yako yote na ndiyo maana hizi huwezi kuzikuta popote pale zaidi ya kwangu tu kwani hata mchoraji alikufa miaka mingi sana iliyo pita. Wamekuja wachoraji wengi sana wamejitahidi ila bado hakuna ambaye anaweza kuingia ligi moja na aliye zichora picha hizi na ndiyo maana zinabaki kuwa picha bora sana kuwahi kuchorwa ndani ya nchi ya Tanzania” mzee huyo aliongea akiwa anampa ishara mgeni wake aweze kuketi chini, haikuwa sawa kufanya mazungumzo wakiwa wamesimama wakati walitakiwa kupata vinywaji kidogo.
“Mr Oscar, kila nikiyaona matendo yako, nikisikia maneno yako kama hayo lakini pia nikitulia na kuisoma akili yako pamoja na misimamoyako basi naishia kumkumbuka sana wajina wako na nawaza sana kwamba kwanini uliishia tu kuwa waziri mkuu wakati kwa uwezo wako ulikuwa unaweza kuingia mpaka Ikulu kabisa?”
“Mhhhh usiniambie kwamba unamzungumzia Oscar ambaye ni miongoni mwa waasisi wa TANU?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Maisha hayakupi unacho kitaka wewe na kuna muda akili ikizidi sana matatizo makubwa yanaweza kutokea na ndiyo sababu hakuwa na mwisho mzuri sana. Tuachane na hayo unaweza ukaniambia sababu ya msingi ya mimi kukutana na wewe?”
“Nahitaji kuingia Ikulu”
“Sasa mimi nahusikaje hapo wakati ni suala la wewe kuwa na ushawishi mkubwa tu ili uchaguliwe na kuungwa mkono na wananchi pamoja na watu wa chama chako?”
“Mpaka nakuja kwako nina uhakika unaelewa vyema namna siasa ilivyo, unaelewa vizuri kwamba ninashindana na raisi wangu lakini pia nina uhakika wewe unaelewa namna siasa inavyo fanya kazi, kuna muda Ikulu sio wananchi wanao kuweka bali watu kama wewe hapo ndio ambao wana uwezo wa kumuweka mtu Ikulu au kumtoa Ikulu kwani hii nchi nyie mnaijua kuliko mtu mwingine yeyote yule”
“Mhhhhh unahisi ni sababu gani labda ambayo itanishawishi mimi kukusaidia wewe uingie Ikulu kama unavyo hitaji?”
Naam ukurasa wa pili nafika mwisho, ungana na mimi kwenye ukurasa wa tatu ambao unafuatia.
Wasalaam,
Febiani Babuya.
Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
[emoji119][emoji119][emoji119][emoji119]
[emoji91]Ahsante sana
[emoji1666]Kazi nzuri[mention]FEBIANI BABUYA [/mention]