funzadume
JF-Expert Member
- Jan 28, 2010
- 13,624
- 21,362
Sambusa ni tamu bwana,
Nyingine hakuna tena,
Wa kijiji ninanena,
Vingine sijaviona! - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Ukishaonja sambusa,
Vitumbua utasusa
Na utatumia mapesa,
Uje upate sambusa! - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Na zile zenye mafuta
Ulimini zinanata,
Na ladha ukishapata
Waweza tangaza vita - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Zipo zenye nyamanyama
Zaliwa Kijitonyama
Hata ukenda Dodoma
Sambusa hutojinyima - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Zipo zile zenye mboga
Zilochumwa kama boga
Wale wasio waoga
Wazila hata Msoga! - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Zipo zenye vitunguu
Zilotiwa karafuu
Ukila mluzi huu
Waimba "mikono juu" - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Na sambusa za Kihindi,
Utazikuta Malindi
Hata Mtwara na Lindi
Zinapikwa na mafundi! - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Uonje 'zopikwa Tanga
Ngonjera utazitunga
Ukipata za Iringa
Na baridi la Mafinga - sambusa ni tamu bwana, hasa zisizofanana!
Beti zangu nazifunga
Tungo nimeshazipanga,
Sambusa sitojivunga
Nayeya ninapuyanga
SAMBUSA NI TAMU BWANA, HASA ZISIZOFANANA!
Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
funza ninasimama, sambusa kuzitizama
macho yanipima, kwa kudunda kwa mtima
mate yaniwama, mdomoni yamekwama
Napata hamu nasema, sambusa nikitizama