Sehemu ya kwanza: Nafasi ya wanalindi kwenye mradi wa gesi

Sehemu ya kwanza: Nafasi ya wanalindi kwenye mradi wa gesi

Membe S K

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
1,389
Reaction score
1,253
PART I: NAFASI YA WANALINDI KWENYE MRADI WA GESI LINDI.

Mradi wa kuchimba na kuchakata gesi asilia (LNG) Lindi mjini ni mradi ambao wakazi wengi wa Lindi wanautegemea uje ubadirishe maisha yao. Hata hivyo Wanalindi wengi hawajui mradi huu unahusu nini haswa na utaanza lini au kwanini haujaanza. Muhimu zaidi wanalindi hawajawekwa wazi watafaidika vipi na mradi huu.

Leo tena najipa jukumu la kuwaelimisha Wanalindi wenzangu juu ya mradi huu kwa kadri ninavyoujua. Kisha sehemu ya pili nitaandika tena juu ya kinachoendelea kwenye meza ya mazungumzo kati ya wawekezaji na serikali. Lengo ni kuwekana wazi wanalindi ili tujipange.

KWANI LNG NI KITU GANI CHENYEWE HIKI?
Vuta kiti. Uozo wa mimea na wanyama uliopo kwenye miamba aridhini unapokumbana na joto kali la dunia na msukumo kutoka kwenye miamba kwa miaka mingi sana (yawezekana milioni na zaidi) unageuzwa kuwa gesi asilia au mafuta au mkaa wa mawe. Chukulia gesi asilia kama hewa na kingereza chake ni Natura gas, kifupi NG. Tupo pamoja?

Sasa NG (yaani gesi asilia) ni nishati inayoweza kuendesha mitambo kama vile magari na mashine za viwanda lakini pia kupikia. Sasa yawezekana baadhi ya watu wanaonisoma hawajui NISHATI na uhusiano wake na NG. Kwa faida ya wengi KUNI, MAFUTA, JUA, UMEME, MKAA ni aina za nishati. Nishati inatengeneza nguvu ya mashine kujiendesha pasipo nguvu za mwanadamu. Mfano kuni zinawaka pasipo binadamu na kuchemsha maji, mafuta yanachomwa na kufanya mashine ya gari izunguke pasipo binadamu. Kadhalika NG ikichomwa inatembeza mashine mbalimbali, na hivyo ni NISHATI.

Mradi wa Lindi sio wa NG bali LNG, inakuaje sasa mbona kuna L mbele ya NG? Ni hivi NG ni mzito sana, ni hatari sana kwa afya ya binadamu na ina harufu mbaya. Haya yote yanafanya usafirishaji wa NG kuwa mgumu na wa hatari. Sasa tunafanyaje? Tunaichakata kwa kuipoza hadi ifikie nyuzi joto -162. Maji tunayooga ni nyuzi joto sifuri, sasa NG inabidi tuipoze hadi nyuzi joto HASI 162. Ikipoa kiwango hicho inakuwa maji, inakosa pressure na harufu. Pia mchakato unaondoa rangi. MUHIMU ZAIDI ikipozwa inakuwa nyepesi sawa na nusu tu ya uzito wa maji na jambo nzuri kabisa ni kwamba ujazo wake mpya unakuwa sawa na ujazo wa mwanzo ukigawa kwa 600. Yaani lita moja yenye milliliters 1000 kabla ya mchakato ni sawa na chini ya milliliters 2 tu. Hivyo mchakato huu unafanya NG kuwa salama na rahisi kusafirisha. Mchakato huu unaitwa LIQUEFACTION kwa kingereza na hivyo kufanya hili neno tulilolizoea la LNG (liquefied natural gas).

Tanzania Mungu ametuzawadia NG na Lindi ndiko mtambo wa kuchakata (LNG) utajengwa. Tanzania tunakadiriwa kuwa na trillion 57 foot za ujazo za NG na kati ya hizo trillion 49 zimo ndani ya maji yetu ya bahari ya India. Maana yake Lindi na Mtwara hatupaswi tena kuwa masikini kama tuna watu na uongozi makini unaojali wananchi wake. Kwanini? Jibu linafuata.

Matumizi na vyanzo vya NISHATI duniani vimeitumbukiza dunia kwenye kitu wenye lugha na usomi wao wanaita TRILEMMA. Yaani mkanganyiko wa mambo matatu (ule wa mambo mawili wanaita DILEMMA). Kwanza ni chanzo cha uhakika na cha kutegemewa, pili ni Nishati isiyosambaza hewa ya ukaa angani pale inapotumika, na tatu ni Nishati ya gharama nafuu. Sasa Mungu ametutunuku watanzania na haswa mikoa ya kusini kwa kutujazia LNG inayowianisha mambo haya matatu kadri ya mapendekezo ya Dunia.

Dunia inatuonea wivu kwasababu tuna Nishati bora kuliko aina nyingine zote za Nishati. LNG ikilinganishwa na mkaa wa mawe inashinda kwa kupunguza viwango vya hewa ya ukaa (carbon dioxide) kwa asilimia 40 na ikilinganishwa na mafuta inashinda tena kwa 30%. Sio hivyo tu LNG haitoi moshi na inatoa viwango vya chini sana vya kemikali zinazoharibu mazingira kama vile Sulphur na dioxide mercury (kama majina hayo magumu kuyasema kunywa maji yapotezee hahaha). Zaidi ya hayo LNG haitoi vumbi wala chengachenga zinazoweza kuathiri afya.


SASA NI AKINA NANI HAO WANAVIZIA KUWEKEZA KWENYE GESI YETU LINDI?
Watakusikia!! Kampuni tano kutoka kwa wababe wa dunia ndio yanapanga kutoa "posa" kwa bint wa Lindi huko kwenye bahari ya Hindi. Haya ni Equinor ya Norway, British Shell na Ophir Energy za Uingereza, ExxonMobil ya Marekani, na Pavillion Energy ya Singapore. Mshenga mkuu wa posa hapa nchini ni TPDC (Tanzania Petroleum Development Corporation). Vile vile wamo TANESCO na EWURA. Mradi huu unategemea kugharimu dola za marekani Milioni 30, hizo ni gharama za ujenzi tu.

ZIPI FAIDA ZA KIUCHUMI ZA MRADI HUU?
Mara nyingi faida za kiuchumi za miradi mikubwa ni kujitokeza kwa biashara mpya, ajira, kodi, gawio la faida ya mradi, na uhakika wa huduma au bidhaa inayotokana na mradi.

Hadi sasa hakuna upembuzi yakinifu juu ya faida za kiuchumi za mradi wa LNG. Kilichowekwa hadharani ni makadirio ya ajira 6000 wakati wa ujenzi na 500 tu wakati wa mradi kufanyakazi. Ajira hizi haijulikani ni za wasifu wa juu, wakati au wa chini.

Makadirio ya benki ya Stanbic ya mwaka 2022 yanasema ajira zitategemea bei ya gesi kwenye soko la kimataifa. Bei ikiwa ya chini mradi utatoa ajira laki 3 kasoro na ikiwa bei ya juu utatoa laki 6 na nusu. Hata hivyo makadirio haya hayaleti maana halisi kiuchumi kwasababu madaraja ya kazi kulingana na ujuzi na wasifu havijawekwa wazi. Faida nyingine zote za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo hazijulikani au hazijawekwa wazi.


MKOA WA LINDI UNA NAFASI GANI KWENYE MRADI HUU?
SINA jibu kwenye swali hili muhimu. Jibu la swali hili linahitaji utafiti unaoitwa kwa kingereza SOCIO-ECONOMIC IMPACT ASSESSMENT (SEIA). Yaani utafiti unaotathmini faida au hasara zitokanazo na mradi kwa jamii inayozunguka au iliyokaribu na eneo la mradi. Sijaona utafiti wa aina hii na sina taarifa ya uwepo wake.

Mara nyingi kama sio zote tafiti ya SEIA na pacha wake Environmental and Health Impact Assessment (EHIA) zinatakiwa kisheria ziwe zimefanywa kabla ya mradi kuanza. EHIA ni tafiti inayotathmini athari chanya au hasi za mazingira na afya za watu zinazotokana na ujenzi na uendeshaji wa mradi. Tafiti ya EHIA ikibaini uharibifu wa mazingira na magonjwa basi kampuni husika na serikali watakubaliana njia za kuzuia au kukabiliana nazo kwa kupunguza athari hizo. Tafiti ya SEIA inalenga kujuwa faida halisi kiuchumi na kijamii za mradi kwa jamii za karibu na mradi.

Sasa ni vigumu kuanza kuibana serikali ionyeshe tafiti za SEIA na EHIA kwasababu mradi haujaanza na kwamba yawezekana sababu za kutoanza kwa mradi ni pamoja na kusubiri kukamilika kwa tafiti hizi. Vilevile serikali kwa sasa serikali ipo kwenye hatua za mwanzo kabisa za mazungumzo na wawekezaji. Makubaliano yakishafanyika ndipo tafiti hizi Itafanyika.

Umuhimu wa tafiti hizi ni mdogo kwa wawekezaji na serikali kwasababu wao kimsingi wamekubaliana mradi utekelezwe. Kwa wanalindi tafiti hizi ni MUHIMU SANA kwasababu (a) wanalindi wanahitaji kujuwa fursa za kiuchumi za mradi huu kabla haujaanza; (b) tafiti hizi zitatoa picha za mahitaji ya mradi kabla na wakati unapofanyakazi na hivyo wanalindi watajiweka tayari kuhudumia mahitaji ya mradi na (c) taasisi kama benki, hospitali, bandari na mamlaka ya kodi ya mkoa zitatumia tafiti hizi kupanua uwezo wake na (d) mchakato na matokeo ya tafiti hizi yanalenga kujenga ushirikiano wa faida kati ya wanalindi na wawekezaji ili kupata njia za pamoja za kukabiliana na athari hasi za mradi. Pasipo tafiti hizi zitakazoshirikisha wanalindi uhusiano kati ya serikali, wanalindi na wawekezaji unaweza kuwa hatarini na hivyo kuhatarisha ufanisi wa mradi.


HITIMISHO NA USHAURI WA BURE KWA MAMLAKA HUSIKA.
Mradi wa LNG ni mradi unaoweza kubadirisha Lindi kiuchumi na kimaendeleo. Faida tarajiwa za mradi huu kwa wanalindi zifanyiwe tafiti na kuwekwa wazi kama kuna dhati ya kuiendeleza Lindi. Wanalindi wana haki ya kujuwa kwa mfano ajira ngapi za kudumu na za muda mfupi zitatolewa kwa wanalindi. Wanahaki pia ya kujuwa elimu au ujuzi tarajiwa wa ajira zitakazokuwapo. Kadhalika faida tarajiwa kwa nchi na mikoa ya kusini zinahitaji utafiti huru wa kina.

Ushauri: Kabla ya mradi kuanza serikali ianze rasmi kuelimisha na kuwatayarisha wanalindi kuelekea mradi huu. Ufanisi wa mradi huu utategemea ushirikiano kati ya wanalindi na wawekezaji. Wanalindi wakiachwa gizani kama ilivyo sasa nao wanaweza kudai kwamba GESI HAITOKI HATA KWA MRIJA WA PENI.

Pia Wanalindi wana haki ya kuwa sehemu ya umiliki wa mradi huu. TPDC na TANESCO wanajukumu la kuhakikisha wanalindi wanakuwa sehemu ya mradi na wanufaika wa moja kwa moja. Hili litawezekana tu kwa kuwashirikisha kikamilifu wanalindi katika maamuzi yote muhimu katika maisha yao. Maamuzi yatakayo athiri wanalindi yafanywe Lindi na wanalindi, Sio Dodoma na sio Dar.

Soma sehemu ya pili ujuwe mradi huu hadi sasa umefikia wapi.

SEMA NIMESEMA

Membe S K
Mtama, Rondo Chiponda Lindi
Tel: +255689463664
email: Smembe426@gmail.com

April 01 2014
 
Back
Top Bottom