Ferruccio Lamborghini
JF-Expert Member
- Apr 15, 2020
- 1,667
- 2,633
Hili ni uhakika, haiwezekani kueleza siasa za Zanzibar na mabadiliko ya kizazi kwa kizazi pasipo kuwa na kurasa nyingi za kufafanua na kuchambua uhusika wa Seif Sharif Hamad. Na huwezi kuitaja historia ya Zanzibar na nyakati zake bila jina la Seif.
Kwa miongo minne, Seif aliweza kujitengeneza kama mhusika mkuu wa siasa za Zanzibar. Alifanya hivyo enzi za chama kimoja, akavuka akiwa imara kabisa baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Ni kwa sababu hiyo, kuna watu walimtambulisha Seif kama ndiye siasa za Zanzibar na humuweka daraja moja na magwiji wa siasa visiwani, kuanzia Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Aman Karume, Aboud Jumbe Mwinyi (Rais wa Pili), Profesa Abdulrahman Babu, Mohamed Shamte na wengine wa mzani huo.
Sababu ni moja; Kwa miaka 36, Seif alikuwa sawa na kionjo mithili ya chumvi kwenye mboga katika siasa za Zanzibar. Mwaka 1984, katika masaibu yaliyomkuta Aboud Jumbe, kufukuzwa uanachama CCM, kuvuliwa urais wa Zanzibar na vyeo vingine vyote kwenye chama na serikali, Seif alitajwa kuwa ndiye alimhujumu.
Kwamba Seif, alivujisha kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mipango wa Jumbe ya kuiondoa Zanzibar kwenye Tanzania. Na ikaelezwa kuwa taarifa za Seif ndizo ziliwezesha kumtia hatiani Jumbe, kisha akavuliwa vyeo vyote alivyokuwa navyo.
Katika uchaguzi wa Rais Zanzibar mwaka 1985, yaani kwenye mchakato wa kupata jina la mgombea urais wa CCM, mchuano ulikuwa mkali mno baina ya Seif na Rais wa Nne wa visiwa hivyo, Idris Abdul Wakil. Kwamba Wazazibari wengi walitaka Seif ndiye awe Rais wa Zanzibar baada ya Rais Ali Hassan Mwinyi kupitishwa na Halmashauri Kuu CCM kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata kitendo cha Abdul Wakili kupigiwa kura nyingi za hapana, sababu ilitajwa ni Seif. Hicho ni kipimo kuwa Seif ni maudhui kwenye matukio makubwa ya kisiasa Zanzibar. Baada ya Abdul Wakil kuwa Rais, akamteua Seif kuendelea kuwa Waziri Kiongozi. Seif alianza kuwa Waziri Kiongozi tangu kipindi cha urais wa Mwinyi Zanzibar.
Uchaguzi wa urais wa Zanzibar mwaka 1990, ulifanyika kipindi Seif akiwa jela. Mwaka 1995, alitikisa kwa mara nyingine. Alitoka wa pili nyuma ya Rais wa Tano wa Zanzibar, Dk Salmin Amour Juma, katika mchuano uliokuwa mkali, ingawa yeye alidai alishinda lakini aliibiwa kura.
Seif akaendelea kuwa mada kila uchaguzi, kutoka mwaka 2000 mpaka 2005, akalazimisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar mwaka 2010, halafu mwaka 2015, akaitikisa dunia baada ya kujitangaza mshindi wa kiti cha urais Zanzibar, lakini matokeo yakafutwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Mvutano huo wa kisiasa Zanzibar ukasababisha matamko mengi kutoka jumuiya ya kimataifa dhidi ya Tanzania. Kutoka azimio la Umoja wa Ulaya mwaka 2008 hadi uamuzi wa Mfuko wa Malengo ya Milenia wa Marekani kupunguza misaada. Ni kuonesha jinsi ambavyo Seif alivyo na athari kubwa.
Katika Uchaguzi Mkuu 2020, Seif akawa kishindo kingine cha kisiasa. Aliingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa mara nyingine, yeye ni Makamu wa Kwanza wa Rais. Cheo hicho alikishika pia kati ya mwaka 2010 mpaka 2015.
Kwa kupima muktadha huo wa uhusika wa Seif kisiasa, hupotezi muda kujaribu kumpinga anayesema kuwa Seif ni siasa na historia ya Zanzibar. Ni kweli, kwa tafsiri kuwa kizazi kimoja hadi kingine hupishana miako 10, basi kwa vizazi vinne, Seif alikuwa kichwa cha habari chenye kusisimua katika siasa za Visiwa vya Karafuu.
NI SEIF WA MTAMBWE
Seif alizaliwa Oktoba 22, 1943, Kijiji cha Nyali, Mtambwe, Chakechake, Mkoa wa Kaskazini, Pemba. Hicho ni kipindi cha utawala wa Kisultan, Zanzibar. Seif, alisoma Shule ya Msingi Uondwe na Wete Boys, Pemba kati ya mwaka 1950 mpaka 1957.
Mwaka 1958 alianza elimu ya sekondari Shule ya Kumbukumbu ya Mfalme George VI na kuhitimu mwaka 1961. Mwaka 1962 mpaka 1963, Seif alisoma kidato cha tano na sita, shule hiyohiyo ya Mfalme George.
Kati ya mwaka 1964 na 1972, Seif alizuiwa kuendelea na masomo ya chuo kikuu ili kujaza nafasi za kazi za utumishi wa umma, zilizoachwa wazi baada ya Waingereza kuondoka, kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, 1964. Hivyo, kati ya mwaka 1964 mpaka 1972, Seif alifanya kazi ya ualimu wa sekondari.
Mwaka 1972, Seif alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikosomea Shahada ya Sayansi ya Siasa, aliyohitimu mwaka 1975. Mwaka 1977, aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu Zanzibar. Mwaka 1980, Seif alikuwa mmoja wajumbe waasisi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Vilevile kati ya mwaka 1977 na 1980, Seif alikuwa mbunge, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kati ya mwaka 1980 mpaka 1988, Seif alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CCM) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM. Alipata kuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango CCM. Kuanzia Februari 1982 mpaka Januari 22,1988, Seif alikuwa Waziri Kiongozi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, akifanya kazi chini ya marais wawili; Rais wa Tatu wa Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Nne Zanzibar, Idris Abdul Wakil.
Baada ya kufukuzwa uwaziri kiongozi Zanzibar, Seif alifukuzwa uanachama wa CCM, hivyo kupoteza ujumbe wake wa Baraza la Wawakilishi, kisha alifunguliwa mashitaka ya kukutwa na nyaraka za Serikali. Alikaa mahabusu kuanzia Mei 1989 mpaka Novemba 1991. Alipata kueleza kuwa mateso aliyopata yalikuwa makubwa sana gerezani. Zaidi aliteswa kisaikolojia kwa kufungiwa chumba kimoja na watoto.
Alipotoka mahabusu, Seif alijiunga na vuguvugu la harakati za kupigania uhuru wa kisiasa Zanzibar, zilizoitwa Kamahuru. Ni Kamahuru iliyoungana na Chama cha Wananchi (CW), kilichokuwa kinaongozwa na hayati James Mpalala. Kwa muungano huo wa Kamahuru na Chama cha Wananchi, kikazaliwa chama cha Civic United Front (Cuf), ambacho pia huitwa Chama cha Wananchi.
Cuf ilipoanzishwa, Seif alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti, aliishika nafasi hiyo kuanzia mwaka 1992 mpaka 1999, alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu, yaani mtendaji mkuu wa chama. Seif alitetea ukatibu mkuu Cuf kila uchaguzi uliopofanyika ndani ya chama, hadi Machi 2019, alipoachia ngazi baada ya mgogoro mkubwa wa uongozi.
Mwaka 2015, mgogoro wa uongozi ulianza Cuf. Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba, alijiuzulu uongozi kwa hoja kuwa alitofautiana msimamo na wenzake. Baadaye, alirejea akitaka atambuliwe kuwa ni mwenyekiti halali kwa sababu barua yake ya kujiuzulu haikupelekwa kwenye mkutano wa Baraza Kuu ili kuthibitishwa, hivyo kisheria yeye alikuwa bado Mwenyekiti.
Seif na wenzake walipinga Lipumba kurejea kwenye uongozi. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, aliunga mkono mkono hoja ya Lipumba kwamba alikuwa bado bado Mwenyekiti halali wa Cuf. Seif na wenzake walipokwenda mahakamani, mahakama ilipiga msumari kuwa Lipumba alikuwa mwenyekiti halali. Na kwa uamuzi huo, Seif na wenzake waliondoka Cuf na kujiunga na ACT-Wazalendo.
Kuondoka kwa Seif Cuf, kumekuwa sababu ya chama hicho kuwa dhoofu. Kwa mara nyingine, Seif alionesha yeye ni maudhui yasiyopaswa kubezwa kwa namna alivyoifilisi Cuf mtaji mkubwa wa watu na kuifanya ACT-Wazalendo kuwa chama kikubwa ghafla.
Seif alipojiunga na ACT-Wazalendo, aliteuliwa na Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe kuwa Mshauri Mkuu. Katika uchaguzi wa viongozi uliofanyika mwaka 2020, Seif alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama. Nafasi hiyo anayo mpaka sasa.
SEIF NA FAMILIA
Seif katika maisha yake alioa mara ya mbili. Mke wake wa kwanza ni Fourtuna Saleh Mbamba, aliyezaa naye mtoto mmoja. Ndoa ya pili, Seif alifunga na Aweina Sinani Masoud mwaka 1977 na kufanikiwa kuzaa naye watoto watatu ambao ni wa kike.
Baba wa Seif jina lake ni Sharif Hamad, mama yake ni Time Seif Haji. Ni ufafanuzi tu kwamba “Seif”, jina hilo alipewa kurithi jina la babu yake mzaa mama, Seif Haji. Nyongeza ni kuwa Seif ni mtoto wa pekee kwa mama yake.
©Luqman MALOTO