Mwanamwana
Platinum Member
- Aug 1, 2011
- 9,604
- 22,722
----
Hakukuwa na maneno ya kutosha kuyaelezea. “Hii si hali ya kawaida,” ndicho kilichorudiwa angalau mara tatu na padre aliyeongoza ibada ya mazishi ya Dainess Raphael Sisa. Dainess, aliyefikisha umri wa miaka 28 tarehe 20 Oktoba 2025, alipoteza maisha tarehe 29 Oktoba 2025. Mashahidi kadhaa wanasema alipigwa risasi kifuani katika maeneo ya Tabata Shule.
Tofauti na mazishi mengi, hapakuwa na mwili. Mnamo Novemba 14, 2025, watu wapatao 100 walikusanyika katika Parokia ya Yohana 23 huko Kibo, Dar es Salaam. Picha yake ikiwa ndani ya fremu ilitumika kuchukua nafasi ya mwili wake.
Kabla ibada haijaanza, ilikuwa wazi kwamba hakuna aliyekuwa akijua jinsi ya kuendana na hali hiyo isiyo ya kawaida. Mwanzoni, picha yake iliwekwa kwenye kiti cha plastiki kilichofunikwa kwa kitambaa. Kisha mwanafamilia aliweka kiti kingine juu ili kuongeza uonekano. Padre alipoingia, alijadiliana tena na wasaidizi wa kanisa, na hatimaye picha ikawekwa mbele ya altare, na ikabaki hapo mpaka mwisho wa ibada.
Dainess, fundi cherehani stadi ambaye wakati wa kifo chake alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya maji inayopatikana Kigamboni, alikuwa akiishi na rafiki yake Cecilia Pius huko Tabata, Dar es Salaam. Tarehe 29 Oktoba, alimwambia rafiki yake kwamba anakwenda kumtembelea dada yake na atalala huko.
“Asubuhi ya tarehe 29 Oktoba, alipoamka, alilegeza nywele zake, akajiandaa, na kusema anaondoka kuelekea Ubungo kumwona dada yake. Alisema anakwenda kusuka nywele na angeendelea kulala huko, kwamba asingerejea,” alieleza Cecilia Pius, akikumbuka siku za mwisho anazozijua kuhusu rafiki yake.
Akaongeza: “Alikuwa anabeba nguo alizozipakia kwenye mkoba. Kwa sababu hakuwa na simu—alikuwa ameipoteza siku za nyuma—jioni nilipopiga simu alipokuwa anakwenda, waliambia hajafika. Niliwaambia aliondoka asubuhi akisema anakuja huko, lakini walisisitiza hajawahi kufika.”
Kutafuta Dainess
Kwa kuwa kulikuwa na amri ya kutotoka nje (curfew), Cecilia na dada yake Dainess waliamua kusubiri kuona kama wangepata taarifa zozote.
“Asubuhi iliyofuata, nilipokea simu kutoka kwa bosi wake. Tangu apoteze simu yake, alikuwa akitumia simu yangu kuwasiliana na wenzake kazini. Bosi wake akauliza kama nilikuwa na taarifa zozote kumhusu Dainess. Nikamwambia sina. Kisha akasema kuwa wamepokea simu kutoka kwa mtu mwema (Good Samaritan) aliyeripoti kwamba Dainess alipigwa risasi siku ya tukio la maandamano katika eneo la Tabata Shule. Alikimbizwa katika hospitali moja jirani Tabata,” Cecilia aliendelea kueleza.
Baada ya amri ya kutotoka nje kuondolewa, baba na kaka zake Dainess walitembelea hifadhi za maiti na hospitali mbalimbali Dar es Salaam, kuanzia zile zilizo karibu na Tabata. Walitafuta kwa wiki nzima bila mafanikio. Kisha waliwaomba baadhi ya watu maarufu waliokuwa wakisaidia familia kutafuta ndugu waliopotea, washirikishe taarifa zake kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya taarifa kusambaa, mashahidi waliomwona akipigwa risasi waliwasiliana na familia. Mwanamke mmoja aliyebeba mwili wake pia alipiga simu, akieleza kwa kina mavazi na sura yake.
“Miongoni mwa watu waliombeba Dainess, mmoja wao alipiga simu kujibu tangazo la kutafutwa. Alieleza kwamba anamkumbuka vizuri kwa sababu wao ndio waliombeba, kwamba alipigwa risasi kifuani na alifariki njiani wakimkimbiza hospitali,” alisema dada yake Dainess, Anuarite Hussein.
“Alisema walipofika hospitalini na Dainess, tayari alikuwa ameshafariki. Walijaribu kukabidhi mwili hospitalini Tabata, lakini ikawa ngumu kwa sababu muda huo polisi tayari walikuwa wamefika hospitalini. Hivyo wakaacha mwili nje.”
Aina mpya ya maombolezo
Akiwa mzaliwa wa Turiani, Morogoro, kabla ya kuhamia Dar es Salaam kwa mafunzo ya ufundi na ajira, familia ya Dainess iliamua kuwa ibada hiyo ndiyo itakuwa shughuli ya mwisho ya mazishi ya mpendwa wao.
Wakati wa ibada, padre alifanya sala maalumu kwa ajili ya picha ya Dainess, na mshumaa uliwashwa kwa ajili ya kumbukumbu yake. Familia ilikabidhiwa picha hiyo iliyobarikiwa kama ukumbusho. Wakati wa kifo chake, Dainess hakuwa na mtoto wala hakuwa ameolewa.
Mwisho wa ibada ulileta majonzi makubwa. Wanawake wengi waliangua kilio, wengine wakilia hadharani huku wakiuliza mwili wake uko wapi. Waombolezaji walipiga picha wakiwa na picha hiyo iliyobarikiwa, jambo lililoonyesha jinsi tukio hilo lilivyokuwa lisilo la kawaida.
Familia ya Dainess ni miongoni mwa nyingi zilizolazimika kufanya mazishi bila miili ya wapendwa wao kufuatia vifo vilivyotokea wakati wa maandamano ya siku ya uchaguzi na operesheni za kiusalama zilizofuatia.
Kwa mfano, mwili wa David Julius, mkazi wa Igoma, ulionekana umelala chini katika video iliyosambaa, lakini haukupatikana—familia yake ilifanya maziko Novemba 19, 2025. Vilevile, familia ya Michael Antony Mnakai, mkazi wa Kigogo Dar es Salaam, aliripotiwa kupigwa risasi tumboni na kupelekwa hospitalini, lakini mwili wake haukuonekana tena.
Katika matukio mengi, familia zimefanya mazishi kwa uthibitisho wa video, ushuhuda wa mashahidi, au vitu binafsi—kama ilivyokuwa kwa Allen Humphrey Isanja, kijana kutoka Arusha aliyepotea Oktoba 30. Viatu vyake vilipatikana mochwari, hatua iliyowafanya familia kuendelea na maziko baada ya kushindwa kuupata mwili wake.
Chanzo: The Chanzo