Limeshakuwa suala la kitaifa sasa kumpongeza Majaliwa, ni sawa kwa vile ameonyesha ujasiri ambao hata baadhi ya askari hawanao.
Lakini pongezi kwake zisiondoe ukweli wa mapungufu ya vyombo vyetu katika uokozi. Nimekuwa najiuliza swali moja, hivi kwa mfano Ile crane iliyotumika leo kuitoa ndege ziwani ingetumika japo kuisogeza ndege ikiwa bado na wahanga ndani vifo vingekuwa 19 kweli.
Hivi kitengo cha maafa ambacho kiko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu kazi yake kuu ni ipi, kungojea janga litokee wakatoe misaada ya mablangeti, vyakula n.k. Hivi vitengo husika vimejipanga vipi zinapotokea dharura kama hizi au ndio zinategemea uwepo wa wavuvi wenye zana duni kama kina Majaliwa?
Huko alikopelekwa Majaliwa kusomeshwa masuala ya uokozi hivi watajisikiaje kumfundisha mtu ambae bila mafunzo ameweza kusababisha uokozi wa watu 24 kitu ambacho wakufunzi wenyewe kwao ni ndoto, unamfundishaje ujasiri mtu wa hivyo.
Wakati tukiwa na majonzi ya kuwapoteza ndugu zetu 19 katika ajali hii, nadhani ni vema kama taifa, ajali hii iwe imetupa funzo la namna bora ya kujipanga ili majanga ya aina hii yakijitokeza tujue tunayakabili vipi. Hata kama hatunyosheani vidole basi na tujifunze kutokana na makosa.