SoC04 Serikali ilegeze kamba maeneo yafuatayo kuchochea kasi ya ukuaji uchumi nchini na kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi

SoC04 Serikali ilegeze kamba maeneo yafuatayo kuchochea kasi ya ukuaji uchumi nchini na kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi

Tanzania Tuitakayo competition threads

Xpertz

Member
Joined
May 3, 2024
Posts
13
Reaction score
10
UTANGULIZI
Toka Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) kupata uhuru bado matatizo makuu ya nchi ni yale yale Ujinga, maradhi na umaskini, bado hakujawa na mikakati toshelevu yenye kuchochea mabadiliko chanya ya kasi kukabiliana na matatizo hayo na kulipeleka taifa mbele kiuchumi kwa kasi kama Mataifa mengine ambayo wakati tunapata uhuru miaka ya 60 yalikua na uchumi unaofanana na wetu ila kwa sasa yametuacha mbali mno. Sambamba na mipango mbalimbali ya maendeleo ila bado Serikali inabaki kama mwezeshaji mkuu au mkwamishaji mkuu wa adhima na mipango hiyo iwapo haitokuwa na mikakati bunifu mbadala ya kuisaidia wananchi kujikwamua. Mfano maeneo mengi ya nchi bado vilio kama ukosefu wa huduma bora za maji, ubovu wa barabara, ukosefu wa ajira, upungufu mkubwa wa madawati nk vinaendelea kurindima, NI AIBU.

Nini kifanyike kuivusha nchi kwa kasi kuelekea uchumi endelevu kwa kasi? Nashauri Serikali ILEGEZE kamba maeneo yafuatayo kufungua njia ya mabadiliko ya kasi ya kiuchumi nchini kama mwezeshaji mkuu ili kuifungua nchi:

1. Serikali itoe au kupunguza kabisa kodi kwenye pembejeo za kilimo, uvuvi na dhana za uchimbaji madini.
Tanzania kilimo kimeajiri zaidi ya asilimia 70 ya watanzania ila bado pembejeo bora za kilimo bei zipo juu hivyo wakulima wengi kushindwa kumudu gharama na kulima kienyeji kilimo kisicho na tija. Mfano vitendea kazi kama matrekta, mbolea, mabomba, pampu, majenereta, mabomba nk bei sio rafiki kwa wakulima. Maeneo mengi ya nchi kuna utitiri wa madini mengi yenye thamani kubwa kwenye soko la dunia ila wachimbaji wadowadogo wanalalamika zana za kisasa za uchimbaji madukani hazikamatiki bei ipo juu mno wanashindwa kumudu kuzinunua ili kuzitumia kurahisisha kazi zao za uchimbaji na kuongeza ufanisi na tija, wavuvi nao wanalia kilio hicho hicho mpaka wanalazimika kuvua kwa kutumia zana haramu ikiwemo mabomu. Serikali kama haiwezi kulegeza kamba kwenye vitendea kazi hivi ni bora iwape wananchi kwa mikopo ya riba nafuu itasaidia kupunguza ukubwa wa tatizo.

2. Serikali ipunguze kodi bandarini kwa vyombo vya moto hususani magari.
Magari yamekua nyenzo muhimu kwenye kuchochea kazi, biashara na uzalishaji hususan kwenye maeneo ya vijijini yaliyo mbali na miji kwa kuisaidia usafirishaji wa watu, malighafi, dhana za kiuchumi pamoja na huduma muhimu kwa jamii ila bado gharama za uagizaji magari nje ya nchi ni nafuu ila bandarini kwetu tunakamuliwa kodi kubwa mno zaidi ya nusu ya bei ya magari hayo kutoka nje. Hii sio sawa inakwamisha kwa makusudi kasi ya uchumi wetu. Serikali kuchota kodi kubwa hukwamisha watu wengi kushindwa kuagiza magari hivyo kukwamisha kasi ya matumizi ya vitendea kazi hivyo muhimu kwenye kuchochea kasi ya uchumi ambapo Serikali ingepata kodi nyingi zaidi na wananchi wangepata unafuu mkubwa katika shughuli zao. Kwa Upande mwingine ukosefu wa magari kwa bei nafuu huongeza ugumu wa maisha kwa wananchi usio na ulazima kwa kuwalazimu kulanguliwa mno na wamiliki wachache wa vyombo hivyo hususani kwenye usafirishaji wa malighafi mbalimbali na vifaa kazi kwenye shughuli zao za kiuchumi hivyo wakati mwingine kuwakwamisha kufikia malengo yao katika uzalishaji nk.

3. Serikali itoe au kupunguza utitiri wa leseni na vibali vya biashara kuchochea uwekezaji. Serikali ya Tanzania ni 1 ila kwenye vibali vya biashara na leseni nchini madukani vimejaa kama bidhaa, ni vurugu tupu sio manispaa, sio TRA, sio mamlaka mbalimbali yaani mfanyabiashara anafuatiliwa kama kibaka. Hakuna leseni 1 ya biashara iliyorafiki kwa mfanyabiashara, imefika hatua wafanyabiashara wengi kufilisika na wengine kuamua kufunga biashara na kufanya biashara kwa njia za siri kuepuka utitiri wa tozo. Kiujumla mazingira ya biashara sio rafiki kabisa nchini hata vijana wanaotaka kujaribu kujiajiri kwenye biashara wanakwama kabisa.

4. Serikali ipunguze kodi na tozo kwenye mafuta. Mafuta ni uti wa mgongo wa kazi za kiuchumi nchini na uzalishaji ila cha ajabu ndio Serikali imeyatwisha zigo la kodi na tozo zaidi ya 15,inamkomoa nani? Watumiaji wa mafuta hayo ndio wanafanya shughuli za uchumi na uzalishaji zinazosaidia kulipa kodi na kuchochea mapato ya nchi ila gharama kubwa za mafuta hupunguza kasi ya shughuli hizo za kiuchumi ambazo ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi.

5. Serikali ipunguze riba za mikopo kwenye mabenki nchini. Bado riba kwenye mabenki yetu nchini ni kandamizi sio rafiki, kwenye kausha damu ndio balaa kabisa, wananchi wanaumia mno. Bado mazingira ya mikopo kwa wananchi nchini sio mazuri hata kidogo wakithubutu kukopa wanaishia kuwatajirisha wakopeshaji sababu ya riba kuwa kubwa mno. Riba mabenki yanasema ni kuanzia asilimia 9 mpaka 17 ila cha kusikitisha mabenki mengi nchini yamejikita kwenye viwango vya mwisho yaani asilimia 16 na 17 ambavyo sio rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini hata kidogo. Nashauri angalau kuwe na kiwango kimoja cha riba ibaki asilimia 9 pekee.

6. Serikali ipunguze gharama za vifurushi na data. Matumizi ya mtandao nchini Tanzania kwa sasa ndio kimbilio la wananchi kutangaza biashara zao na kupeana fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii ila bado Serikali imekaza Upande wa vifurushi bei sio rafiki hata kidogo. Mfano kipindi cha hayati Rais John Pombe Magufuli shilingi 1000 ilikua inatosha kununua data kiashi cha MB 1,024 ila kwa sasa haitoshi kununua hata MB 500,nani ananufaika na ukandamizaji huu? Kupitia matumizi ya mitandao vijana wengi wamejiajiri huko kwanini Serikali inabana? Vijana wauza maudhui (content creators) wanakosa pesa nyingi mno kutokana na walaji wao kushindwa kumudu gharama za data.

Nawasilisha.
 
Upvote 1
. Hii sio sawa inakwamisha kwa makusudi kasi ya uchumi wetu. Serikali kuchota kodi kubwa hukwamisha watu wengi kushindwa kuagiza magari hivyo kukwamisha kasi ya matumizi ya vitendea kazi hivyo muhimu kwenye kuchochea kasi ya uchumi ambapo Serikali ingepata kodi nyingi zaidi na wananchi wangepata unafuu mkubwa katika shughuli zao. Kwa Upande mwingine ukosefu wa magari kwa bei nafuu huongeza ugumu wa maisha kwa wananchi usio na ulazima kwa kuwalazimu kulanguliwa mno na wamiliki wachache wa vyombo hivyo hususani kwenye usafirishaji wa malighafi mbalimbali na vifaa kazi kwenye shughuli zao za kiuchumi hivyo wakati mwingine kuwakwamisha kufikia malengo yao katika uzalishaji nk.
Yaani hili la magari. Na ukizingatia hatutengenezi magari nchini unabaki kushangaa. Yaani ilifaa kodi iwe ndoogo sana hasa kwa gari mpya na zenye faida kimazingira mfano hybrids.
 
Back
Top Bottom