Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
Serikali Imeahidi Kufanya Jitihada za Kuhakikisha Mtandao wa Google Unakuwa na Tafsiri Sahihi na Sanifu kwa Lugha ya Kiswahili
"Lugha ya Kiswahili kwa sasa ni Lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU). Kila tarehe 07 Julai ya kila Mwaka inaadhimishwa kama siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Lugha ya Kiswahili ni nyenzo muhimu katika kuwezesha mawasiliano Duniani hususani katika shughuli za kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni, kitafiti na kisayansi" - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk
"Hali hii inachangia moja kwa moja katika Diplomasia ya Uchumi kupitia ajira za Wataalam wa ufundishaji wa Lugha ya Kiswahili. huduma za ukalimani na tafsiri katika mataifa na mikutano mbalimbali na kutumika kama vyenzo wezeshi katika biashara " - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk
"Lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika katika maelezo ya bidhaa mbalimbali na ushawishi wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, machapisho ya vitabu na tafiti mbalimbali za kisayansi ambayo yamekuwa yakiuzwa na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na kuchangia pato la Taifa" - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk
"Mtandao wa Google umekuwa ukitusaidia sana kutoa tafsiri ya Lugha mbalimbali Duniani kuja katika Lugha ya Kiswahili lakini bado tafsiri haikidhi viwango na vigezo vya tafsiri sanifu ya Kiswahili. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kufanya jitihada zozote ili kukiwezesha Kiswahili kuwa na sura ya Kimataifa" - Mhe. Ameir Abdallah Ameir, Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe
Je, kuna ithibati yoyote ya uwepo wa vituo vya Utamaduni (Cultural Centres) katika Balozi zetu mbalimbali Duniani na zinatoa mchango gani hizi Cultural Centres katika kukuza, kutangaza Utalii wetu hususani katika kuueleza Utamaduni wa Mswahili, Waswahili, Uswahilini na hata asili ya neno Mswahili" - Mhe. Ameir Abdallah Ameir, Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe
"Serikali inatambua mchango mkubwa wa tafsiri ya mtandao wa Google katika kukuza na kukiendeleza Lugha ya Kiswahili. Lakini ni kweli baadhi ya wakati Google haitoi Lugha fasaha na sanifu. Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha tafsiri inayokuwa Google inakuwa sanifu na fasaha zaidi" - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk
"Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa ni mdau mkubwa katika utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa kukibidhaisha Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi. Sasa hivi kuna Balozi 16 za Tanzania ambazo zimefungua vituo vya Utamaduni na kufundisha Lugha ya Kiswahili nchi za nje. Vituo vyote tayari vina ithibati kutoka Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA)" - Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk