Serikali ilitafutie dawa sahihi tatizo la mishahara
VIWANGO vipya vya mishahara ya wafanyakazi ambavyo vilitakiwa kuanza kutumika kuanzia mwezi uliopita (Januari) vimezua vurugu baina ya wafanyakazi na waajiri.
Sababu kubwa ya vurugu hizo ni kufuatia baadhi ya waajiri kutokuwa tayari kulipa viwango vipya vya mishahara, baada ya serikali kuridhia maombi yao (waajiri)yaliyokuwa yameambatana na sharti la kwamba kama wakilipa viwango vipya basi waruhusiwe kupunguza wafanyakazi.
Sekta iliyokumbwa zaidi na mkasa huo ni viwanda, ambayo wafanyakazi wake waligoma kupokea mishahara ya zamani ya Sh80,000 kwa kima cha chini wakidai kuwa lazima wapewe kiwango kipya cha Sh150, 000 kwa mwezi kilichowekwa na serikali.
Juzi ilikuwa siku ya kulipwa mishahara, wafanyakazi wa baadhi ya viwanda vikiwamo vya Sunflag cha Arusha, Urafiki na cha Mabomba vilivyoko eneo la Ubungo, jijini Dar es Salaam waligoma kupokea mishahara yao pamoja na kufanya kazi mpaka watakapolipwa kiwango halali kilichotangazwa na serikali.
Mbali na kugoma huko, baadhi ya wafanyakazi waliamua kwenda kumvamia na kumtoa ofisini Afisa Utumishi wa Kiwanda cha Urafiki kwa madai kwamba yeye ni chanzo cha wao kutolipwa mishahara mipya.
Mbaya zaidi wafanyakazi wa Kiwanda cha Sunflag walifikia hatua ya kumzomea Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidori Shirima aliyekuwa akiwasihi wakubali kulipwa kiasi hicho wakati suala lao likiendelea kushughulikiwa.
Kufuatia vurugu hizo zilizoambatana na kuimba nyimbo za kuwakejeli viongozi wa kiwanda na serikali pamoja na kukataa kutoka kwenye eneo la kiwanda hicho, Polisi wa Kikosi cha kutuliza Ghasia (FFU) waliitwa na kuwatawanya kwa kuwapiga mabomu ya machozi na virungu.
Hakuna anayefurahishwa na vitendo vya wafanyakazi kugoma, lakini nani wa kulaumiwa katika suala hili ambalo amri na agizo la utekelezaji wake unaonyesha kuwa ulichukuliwa bila kufanya utafiti wa kina?
Katika hili wafanyakazi wanaweza kuonekana na waajiri wao kuwa ni wakorofi na wakati huo huo waajiri kuonekana kuwa wadhalimu wakubwa wasiojali haki za watu wanaowatumikisha katika kazi zao.
Lakini kwa namna moja au nyingine serikali nayo inawajibika kwa tatizo hilo kwa kuwa ndiyo iliyotoa uamuzi kwamba lazima wafanyakazi wa sekta hiyo walipwe kiasi cha Sh150,000 kwa mwezi kama kima cha chini bila kuafikiana na waajiri wa sekta hiyo.
Serikali ilitakiwa kwanza kuwashirikisha waajiri juu ya marekebisho ya mishahara ili kuondoa utata kama uliojitokeza sasa kabla ya kutangaza viwango vipya. Tunasema hivyo kwa sababu mara baada ya kutangazwa viwango hivyo waajiri walisema hawawezi kulipa kiwango hicho na kupendekeza kuwa watakubali kufanya hivyo kwa sharti la kupunguza wafanyakazi kwa karibu nusu ya waliopo ili viwanda vyao visipate hasara.
Kibaya zaidi, baada ya kutangaza kiwango hicho na waajiri kutamka kuwa watapunguza idadi ya wafanyakazi, serikali iliwabembeleza na kuwakubalia kushusha kiwango hadi Sh80,000 kimya kimya na baadaye kutangaza kupitia kwenye vyombo vya habari juu ya mabadiliko hayo ambayo hayakuwa wazi kwa wafanyakazi.
Hilo linaonyesha kuwa serikali haikuwashirikisha kikamilifu wadau wote, kwani ingefanya hivyo ingetangaza viwango ambavyo sasa vinaathiri uzalishaji viwandani na maslahi ya wafanyakazi pia.
Jana Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligati akizungumza na Waandishi wa habari mjini Dodoma alirudia kuonya kuwa migomo kazini ni makosa na kwamba mtu yeyote atakayefanya hivyo anaweza kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
Hata hivyo, hilo siyo jawabu la matatizo hayo, tunaomba serikali itafute ufumbuzi wa kudumu ili kuumaliza mtafaruku huo unaowaathiri waajiri na wafanyakazi.