BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Dk Slaa asema serikali inamuogopa Dk Hosea
Mwandishi Wetu
Mwananchi
Mwandishi Wetu
Mwananchi
NAIBU kiongozi wa upinzani bungeni, Dk Willibrod Slaa amesema serikali inachelea kuchukua hatua dhidi ya mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kwa sababu inamwogopa na inamlinda kwa maslahi binafsi.
Kauli hiyo imetolewa wakati serikali bado haijatangaza hatua dhidi ya Dk. Hosea pamoja na mwanasheria mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika ambao wametajwa kwenye kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji wa umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development LLC na serikali kushauriwa kuwachukulia hatua.
Katika taarifa ya utekelezwaji wa mapendekezo ya Bunge, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema wawili hao wameshaandikiwa barua za kutakiwa kujieleza, lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa na mamlaka husika dhidi yao.
Akizungumza na Mwananchi jana, Dk Slaa alisema ukimya wa serikali kuhusu hatua dhidi ya Dk Hosea, ambaye taasisi yake ilieleza kuwa hakukuwepo na rushwa katika utoaji wa zabuni hiyo kabla ya kamati teule ya Bunge kubaini kuwepo kwa mchezo mchafu, ni ishara ya kumwogopa na kumlinda kwa maslahi binafsi.
"Kutokana na nyaraka za bunge kupitia kamati ya (mbunge wa Kyela, Dk Harrison) Mwakyembe, huyu Dk Hosea anahusika. Kitendo cha kuisafisha Richmond tu kinastahili awajibishwe kwa kuchukuliwa hatua. Nashangaa kwa nini Kikwete hachukui hatua," alisema.
"Serikali hii ni ya ajabu. Ina macho na masikio makubwa, lakini haisikii. Inasema inamchunguza, inachunguza kwa miaka mingapi."
"Hii inaonyesha jinsi serikali ilivyokosa utawala bora.
"Utendaji wa Rais Kikwete na serikali yake una mtia shaka kutokana na kufumbia macho na kutochukua hatua katika masuala mengi yaliyo wazi na yenye maslahi kwa taifa na hivyo kuacha maswali kwa wananchi.
"Ni wazi hakuna utawala bora bali ni kulindana kwa maslahi binafsi, nimeshasema mara nyingi hilo lipo wazi.
"Naamini Kikwete alielezwa kuhusu Richmond, cha kushangaza ni kigugumizi alichonacho kumchukulia hatua Dk Hosea.
"Haikuwa rahisi zabuni kubwa kama ile kutolewa kwa Richmond, wala mitambo mikubwa ya kuzalisha umeme kuingia nchini bila yeye (Kikwete) kufahamu, najua anafahamu sasa kigugumizi cha kuchukua hatua kwa Hosea anayestahili kuwajibika kwa kuisafisha Richmond."
Kuhusu Mwanyika, ambaye pia serikali ilisema inamchunguza, Dk. Slaa alisema alishatoa kauli yake na kumtaja aliyehusika.
Katika taarifa yake kwa Bunge kuhusu kampuni ya Richmond, Takukuru ilieleza kuwa uchunguzi wao ulibaini hapakuwa na rushwa katika utoaji zabuni kwa kampuni hiyo, jambo ambalo ni tofauti na taarifa ya kamati teule ya bunge iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Dk Mwakyembe.
Kamati ya Dk Mwakyembe, pamoja na mambo mengine ilibaini kuwepo kwa mazingira ya rushwa katika utoaji zabuni hiyo na ripoti ya kamati hiyo ilisababisha Edward Lowasa kujiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu kutokana na kutajwa kwenye kashfa hiyo.
Kuhusu kauli ya Dk. Hosea kuwanyooshea kidole wabunge kuwa wanachukua posho zaidi kuliko uhalisia wa kazi wanayoifanya kwa wananchi, Dk.Slaa alisema mkurugenzi huyo wa Takukuru asitumie nafasi hiyo kisiasa kulipa kisasi na kuwashambulia wabunge.
Alisema kimsingi hana ugomvi na Dk. Hosea na kwamba ni jambo baya kwa mkurugenzi huyo iwapo amefanya hivyo kwa lengo la kuwaumbua na kuwanyamazisha wabunge kwa malengo yake binafsi.
"Asitumie nafasi yake kulipa kisasi... kuwanyamazisha wabunge. Asitumie nafasi hiyo kisiasa kutaka kuwashambulia na hata kuwaumbua wabunge," alisema Dk Slaa.