Kumekuwa na mwelekeo usio na afya katika mfumo wetu wa elimu, hususan baada ya mitihani ya darasa la saba. Punde tu mitihani inapomalizika, matangazo ya tuition za Pre Form 1 huibuka kwa kasi, yakichochea hofu na presha kwa wazazi. Wengi hujihisi wanalazimika kupeleka watoto wao, si kwa sababu ni muhimu kielimu, bali kwa sababu “wengine wanafanya hivyo.” Huu ni mkakati wa kibiashara unaolenga faida zaidi ya mahitaji halisi ya wanafunzi.
Serikali inapaswa kuingilia kati kwa kuweka miongozo ya wazi. Hii ni kwa sababu kuna kundi kubwa la wazazi ambalo lipo tayari kufanya maamuzi yasiyoangalia ustawi wa mtoto kama kuwapeleka watoto wadogo boarding, kuwaamsha saa tisa usiku kwenda shule, au kuwabana na tuition kila likizo. Hawa ndio wazazi wanaoongoza kuwasukuma watoto kwenye Pre Form 1 tuition mara tu mtihani unapoisha
Wanafunzi wa darasa la saba wanakamilisha safari ya miaka saba kwa kufanya mtihani wa kitaifa Septemba 11 na 12. Baada ya juhudi hizo, wanastahili kupumzika, kuwa na familia, kusaidia nyumbani, na kutulia kisaikolojia kabla ya kuanza hatua mpya.
Ni vyema tuition hizi zianze rasmi Jumatatu, Novemba 3. Serikali isaidie kuweka utaratibu huu, ili watoto wapate muda wa kupumzika na kujijenga kwa mwelekeo mpya wa sekondari.