WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesisitiza kwamba ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, unatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu. Pia, Profesa Mbarawa alisema hadi Desemba mwaka jana, jumla ya wananchi 2,183 sawa na asilimia 98.69 wamelipwa fidia ya Sh bilioni 45.65 ili kupisha ujenzi wa bandari hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Mbarawa alisema ifikapo Machi mwaka huu, majadiliano ya kiufundi na kibiashara, yatakuwa yamekamilika. Alisema Januari 8, mwaka huu kuna gazeti moja la kila siku (si HabariLeo), liliandika ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utasubiri, jambo ambalo si kweli.
“Napenda kuwataarifu kuwa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo hausubiri kukamilika kwa uongezaji wa kina cha maji katika bandari ya Dar es Salaam na uboreshaji wa bandari ya Mtwara, kama ilivyoandikwa katika gazeti hilo. Napenda kuwaarifu kwamba habari hiyo siyo sahihi na imepotosha umma,” alisema.
Jiwe la msingi Profesa Mbarawa alisema Serikali ya China, Serikali ya Oman na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilitia saini ya makubaliano ya ujenzi wa bandari ya Bagamoyo mbele ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete Oktoba 16, mwaka jana, siku ya uzinduzi wa ujenzi wa bandari hiyo.
Alisema mpaka sasa kikosi kazi maalumu cha nchi hizo tatu, kipo katika hatua mbalimbali za kuandaa mikataba ya kiufundi na kibiashara kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa bandari hiyo utagharimu Sh trilioni 21.5.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Kikwete alisema ujenzi huo utakapokamilika, utakuwa ni mradi mkubwa utakaoinua uchumi wa nchi na kuongeza uwekezaji kwenye sekta nyingine. Aliwataka watanzania kuwekeza katika viwanda na sekta za huduma.
Aidha, aliwataka Watanzania kujiendeleza kielimu na mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kupata ajira kupitia mradi huo. Alisisitiza kuwa hilo litawezekana ikiwa wananchi watadumisha amani na utulivu.
Aliwataka wananchi wa Bagamoyo kujenga ushirikiano na wawekezaji hao ili mradi huo ukamilike kwa wakati na ulete manufaa kwao na taifa. Mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo kutoa tani 600,000 za shehena ya makontena 1,000 na pia utatoa ajira kwa watu zaidi ya 1,000.