Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Utiaji saini mikataba miwili kati ya Wakala ya Barabara (TANROADS) na Mkandarasi wa Ujenzi pamoja na Mhandisi Mshauri umefanyika leo Septemba 21, 2024 katika Uwanja wa Samora Mkoani Iringa na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile pamoja na viongozi wa CCM, Serikali na Wananchi wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua barabara hii ikijengwa itafungua fursa za Kiuchumi na Kitalii kwa wana Iringa na ametoa fedha maalum kiasi cha shilingi Bilioni 142.56 ambayo itawezesha barabara kuanza kujengwa mpaka kukamilika fedha inatiririka tu“, amesema Bashungwa.
Vilevile, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuunganisha Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa barabara za lami ili kuboresha miundombinu ya usafiri, kurahisisha biashara, na kukuza uchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera na Uratibu William Lukuvi, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Iringa - Msembe ukikamilika kwa kiwango cha lami utafungua uchumi wa wananchi wa Iringa kwa kuwa tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli na hivyo wananchi watashuhudia makampuni mengi ya kitalii yakiongezeka.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa kukamilika kujengwa kwa barabara ya Iringa - Msembe utasaidia kukuza utalii wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hasa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kurahisisha ufikaji wa watalii katika hifadhi hiyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba ameiomba Serikali kushughulikia mapema suala la fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya Iringa - Msembe (km 104) kwa kiwango cha lami ili isiwe kikwazo katika mradi huo.
Akitoa taarifa, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta amezitaja Kampuni zilizoshinda zabuni za ujenzi ambazo ni China Henan International Corperation (CHICO) pamoja na Mhandisi Mshauri Conseil Ingenierie Et Recherche Appliquee (CIRA SAS) ya Mali kwa kushirikiana na NIMETA Consult ya Tanzania ambapo utekelezaji wake ni miezi 24.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe (km 104) ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuharakishamaendeleo ya kiuchumi na kijamii Mkoani Iringa hususani katika Wilaya za Iringa mjini na Iringa vijijini kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya Usafiri na Utalii.