Serikali yasema imeanza kutathmini kuhusu Mahabusu, Wafungwa Kupiga Kura

Serikali yasema imeanza kutathmini kuhusu Mahabusu, Wafungwa Kupiga Kura

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826
Siku chache baada ya Mahakama Kuu kutoa hukumu kuwa mahabusu na wafungwa wa vifungo vya kawaida wana haki ya kupiga kura kuwachagua viongozi, Serikali imesema inaifanya tathmini kuona kama kuna hatua zaidi inazoweza kuzichukua kuhusiana na hukumu hiyo.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi, alipozungumza na Mwananchi kuhusiana na mtizamo wa Serikali juu ya hukumu hiyo.

Feleshi alisema kwa kuwa Tanzania ni nchi inayofuata utaraibu wa sheria, itazifuata katika kushughulikia hukumu hiyo, ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini kuona kama kuna masuala yanayohitaji kuchukua hatua.

“Taratibu ni kwamba judgement (hukumu) inapotolewa kinachofuata baada ya kuipokea ni tathmini kuona kama kuna hatua za kirufaa zitachukuliwa.

Mahakama Kuu nchini ilitangaza haki hiyo kwa mahabusu na wafungwa baada ya kubatilisha kifungu cha 11(1)(c) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (NEA), Sura 434, marejeo ya mwaka 2015 kinachozuia wanaotumikia kifungo cha kawaida kuanzia miezi, kupiga kura.

Mahakama ilifikia uamuzi huo katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Elinaza Luvanda kwenye shauri la kikatiba lililofunguliwa na raia wawili, Tito Magoti na John Tulla waliokosa haki hiyo kwenye Uchaguzi Mkuu 2020 wakipinga kifungu hicho kuwa kinakinzana na Katiba.

Magoti aliyekuwa mahabusu na Tulla aliyekuwa mfungwa wakati huo walifungua shauri hilo namba 3/2022 Mahakama Masjala Kuu dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Jeshi la Magereza.

Ingawa kifungu hicho hakiweki zuio la utekelezaji haki hiyo kwa mahabusu wanaosubiri usikilizwaji wa kesi zao, lakini Jeshi la Magereza halijaweka utaratibu unaowawezeaha mahabusu kutekeleza haki hiyo, jambo linalowafanya mahabusu wasipate haki hiyo.

Katika kiapo chake, Magoti alidai kuwa mwaka 2020 alinyimwa haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu kutokana na kuwa mahabusu katika Gereza la Segerea akisubiri usikilizwaji wa kesi yake ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili.

Kwa upande wake, Tulla alidai kuwa alinyimwa haki hiyo katika uchaguzi huo kutokana na kutumika adhabu ya kifungo cha takribani mwaka mmoja katika Gereza la Segerea.

Katika hukumu hiyo, Jaji Luvanda alisema haki ya mahabusu kupiga kura ni haki ya kikatiba inayohifadhiwa na kudumishwa na Ibara ya 5(1) ya Katiba.

Alisema hakuna sheria wala kanuni inayozuia mahabusu kusajiliwa au kushiriki katika uchaguzi kwa kupiga kura wala sheria au kanuni inayosema kuwa ni lazima uwekwe utaratibu wa kuwawezesha mahabusu kutekeleza haki hiyo.

Pia Jaji Luvanda alirejea Ibara ya 5(2), inayosema kuwa Bunge linaweza kutunga sheria kuweka sharti la kuzuia raia wa Tanzania kutekeleza haki hiyo wakiwemo wanaotiwa hatiani kwa makosa fulani ya jinai.

Alisema kuwa Bunge kwa kuweka sharti la zuio kuzingatia kifungo limekwenda nje ya muktadha wa Ibara hiyo ya Katiba kuwa Katiba haikumaanisha kuwa mtu yeyote anayehukumiwa kifungo cha muda fulani gerezani kwa kosa la aina yoyote ile anapoteza haki yake ya kupiga kura.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom