Shairi la leo; Na Mussa Bwakila

Shairi la leo; Na Mussa Bwakila

Mphamvu

JF-Expert Member
Joined
Jan 28, 2011
Posts
10,702
Reaction score
3,319
WIZARA ZIMEWASHINDA…!
Waziri Mkuu Pinda, metuacha na kololo!
Aonesha bado ‘kinda’, bado ‘amelala dolo’!
Kuongoza amepinda, liko wapi atendalo?
Wizara zimewashinda…

Ninakuomba “Mkubwa”, naomba unisikie
Umuondoe Kawambwa, Elimu simpangie
Umempa kazi kubwa, ameshindwa nikwambie
Wizara zimewashinda…

Nako wizara ya Maji, tunachokunywa matope!
Matope hawayachuji, tupate maji meupe!
Na huko kwenye vijiji, Maghembe kawa mapepe!
Wizara zimewashinda…

Kilimo ndiyo kabisa, kwa kweli wamekiviza
Mawaziri watutusa, wakulima wawaliza!
Si kilimo cha kisasa, akifanyacho Chiiza!
Wizara zimewashinda…

Nayo wizara ya Fedha, uchumi watelekeza!
Mgimwa ‘kakosa radha’, haongozi anacheza!
Nchi ‘inataka kadha’, ‘kadha wa kadha’ ni giza!
Wizara zimewashinda…

Rejea kwenye Nishati, wafanyalo hatuoni!
“Si hayati si mamati”, wanatuweka kizani!
Na TANESCO ‘maiti’, itajafufuka lini?
Wizara zimewashinda…

Nako huko TAMISEMI, miji mekuwa mizigo?
Kutwa ‘kuchonga ulimi’, ufanisi ni mdogo!
Hawa Ghasia hasemi, wizara kwenda upogo!
Wizara zimewashinda…

Turudi kwenye Michezo, Habari – Utamaduni
Huku nako ni uwozo, maendeleo sioni!
Tunaomba muongozo, kinachokwamisha nini?
Wizara zimewashinda…

Na wizara ya watoto, ‘Simba sasa kawa Swala’?
Mpambana na mazito, leo mtu wa kulala!
Kama niko kwenye ndoto, sijaamini Bwakila!
Wizara zimewashinda…

Hizo nyingine wizara, “Mkubwa” unazijuwa!
Ni chache zenye ubora, zingine zasuwasuwa!
Fanya kukurukakara, mambo uyaweke sawa
Wizara zimewashinda…

‘Wanakwenda msagunda’, “Mkubwa” unawalinda?
Ndege mpasua sanda, analia tutashinda?
Nchi iko njia panda, hatujajua pa kwenda!
Wizara zimewashinda…

Mussa Ally Salum Bwakila,
Mussa_ally@ymail.com


https://www.facebook.com/mussa.allybwakila?hc_location=stream
 
Back
Top Bottom