NewChapter
JF-Expert Member
- May 17, 2024
- 306
- 196
DKT. SAMIA AMEWAIBISHA WALIOMBEZA, AITHIBITISHA TANZANIA INAWEZA - DC SHAKA
Asema Uongozi Wake Umeleta Matokeo Makubwa na Kuifanya Tanzania Kung'ara Kimataifa
DodomaMkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewanyamazisha na kuwaibisha wale waliokuwa na mashaka kuhusu uwezo wake wa kuendeleza na kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati ya Taifa baada ya kuingia madarakani.
Akitoa maoni yake katika hafla ya uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Shaka alisema kuwa licha ya changamoto mbalimbali zilizolikabili Taifa na dunia kwa ujumla, ikiwemo janga la UVIKO-19, ukame na misukosuko ya uchumi wa kimataifa, Rais Samia amefanikiwa kuhakikisha kuwa hakuna mradi wa kimkakati uliosimama au kukwama.
Alisema miradi yote mikubwa ya maendeleo imeendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa, huku matokeo yake yakionekana wazi katika sekta mbalimbali na kugusa maisha ya Watanzania.
Alieleza kuwa katika kujenga Taifa lenye umoja, mshikamano na amani, Rais Samia ameendelea kusimamia utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo vinavyozingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo, mipango ya ukuaji wa uchumi pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)."Wapo waliodhani kuwa miradi mikubwa ya Taifa ingekwama, lakini leo ukweli umeonekana. Miradi imeendelea, mingine imekamilika, na mingine imefikia hatua kubwa za utekelezaji. Haya ni mafanikio yanayodhihirisha uongozi madhubuti wa Mhe. Rais Samia," alisema Shaka.
Kwa mujibu wa Shaka, Rais Samia ameonyesha kwa vitendo kuwa ni kiongozi jasiri, mchapakazi na mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi, jambo ambalo limeifanya Tanzania kuendelea kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Shaka alisema mafanikio ya ujenzi na uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba ni ushahidi wa wazi wa namna Rais Samia anavyoweka mbele maendeleo badala ya siasa zisizo na tija."Dkt. Samia ameithibitishia Afrika na dunia kuwa Tanzania ina viongozi wenye uwezo wa kusimamia maendeleo makubwa. Ameonyesha ukomavu wa kisiasa, uzalendo na dhamira ya dhati ya kulitumikia Taifa," alisisitiza.
Alifafanua kuwa Mji huo wa Serikali si mkusanyiko wa majengo pekee, bali ni alama ya hadhi, heshima na utambulisho mpya wa Taifa la Tanzania.
Aidha, Shaka alisema Watanzania wana kila sababu ya kumuunga mkono Rais Samia kutokana na namna alivyodhihirisha uongozi wa vitendo kwa kuendeleza maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, sambamba na kutimiza ndoto ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ya kuifanya Dodoma kuwa kitovu kamili cha utawala wa Serikali."Huu si ujenzi wa majengo tu. Huu ni ujenzi wa historia, heshima na taswira mpya ya Taifa letu. Ni ushahidi kwamba Tanzania inaweza kutekeleza miradi mikubwa kwa viwango vya kimataifa," alisema.
Aliongeza kuwa uwekezaji uliofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba utafungua fursa nyingi za ajira kwa vijana, kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuifanya Dodoma kustawi zaidi kama mji mkuu wa kisasa na wa kidiplomasia.
Akihitimisha, Shaka alisema kuwa maendeleo yanayoendelea kushuhudiwa Dodoma yanathibitisha kuwa mji huo sasa ni Makao Makuu ya nchi kwa vitendo na si kwa jina pekee."Mafanikio haya yametokana na uthubutu, maamuzi sahihi na uzalendo wa kweli wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ameonyesha kuwa hakuna kinachoshindikana pale Taifa linapokuwa na uongozi wenye maono na dhamira ya maendeleo," alisema.
"Kwa mafanikio haya, Mhe. Rais Dkt. Samia ameipa Tanzania heshima kubwa na kuithibitishia dunia kuwa Watanzania tukiamua, tunaweza kufanya makubwa zaidi kwa kasi, ubora na mafanikio makubwa. Mji wa Serikali Mtumba ni alama ya uwezo wetu wa kujijengea mustakabali wetu wenyewe," alihitimisha Shaka.