Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
View: https://www.youtube.com/live/ofrr-5ZXSAM
[Hotuba ya Kiongozi wa Chama Ndugu Dorothy Jonas Semu kwenye Maadhimisho ya Miaka 11 ya Kuzaliwa kwa ACT Wazalendo yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hakainde Hichilema, Makao Makuu ya Chama, Dar es Salaam]
Ndugu viongozi na wanachama wote mliohudhuria kwenye tukio hili,
Ndugu wanachama na wananchi wote mnaofuatilia kongamano hili la maadhimisho ya miaka 11 ya ACT Wazalendo kupitia vyombo vya habari;
Ninawasalimu kwa salamu ya Chama chetu, ACT Wazalendo; Taifa Kwanza Leo na kesho!
Ingawa takribani miaka yote ACT Wazalendo imejiwekea utamaduni huu wa kuadhimisha kuzaliwa kwake, maadhimisho ya mwaka huu ni ya kipekee kwa Chama chetu. Maadhimisho haya yanafanyika kwenye mwaka wa uchaguzi mkuu ambao, kama nitakavyofafanua baadaye, nao ni wa kipekee kwa mustakabali wa demokrasia nchini.
TUJIPONGEZE KWA MIAKA 11 YA MAFANIKIO!
Ndugu wanachama na viongozi napenda kutumia fursa hii kama Kiongozi wenu wa Chama kuwapongeza wote kwa Chama chetu kutimiza miaka 11 tangu kipate usajili wa kudumu. Kwa hakika, safari hii iliyoanza rasmi tarehe 5 Mei 2014 haikuwa rahisi. Ilikuwa ni safari nzito yenye kila aina ya changamoto ambazo kwa pamoja tumekabiliana nazo na kuzishinda. Imekuwa ni safari ya miaka 11 ya mafanikio makubwa!Hivi sasa, wachambuzi wote makini wanakubaliana kuwa licha ya uchanga wake kiumri, ACT Wazalendo ndio Chama kinachokua kwa kasi zaidi kuliko vyama vyote nchini.
Mafanikio ya ACT Wazalendo hayajifichi, yapo bayana. Tukisheherekea miaka 11 ya kuzaliwa kwetu naomba wanachama na viongozi wote tutembee kifua mbele kwa kazi kubwa tuliyofanya kukijenga Chama chetu hadi kikawa chombo kinachotumainiwa na Watanzania wa Zanzibar na Tanzania Bara kuleta ukombozi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa!
Ninaomba kwa leo tusheherekee maeneo 10 ambayo kwa hakika kila mwenye macho atakubaliana nami kuwa ACT Wazalendo tumepiga hatua kubwa zaidi ya vyama vyote vya siasa nchini;
Tumeongoza katika siasa za hoja dhidi ya siasa za vioja, vituko na "uchawa" ambazo ndizo zimetawala katika Chama cha Mapinduzi. Daima, ACT Wazalendo tumetanguliza mbele kuzisemea changamoto za Watanzania na kupendekeza majawabu yake kupitia sera zetu makini.
Tumejenga jukwaa mbadala ambalo ni kimbilio kwa wanasiasa wanaopenda siasa safi na ambao hawaridhishwi na ukandamizwaji wa demokrasia kwenye vyama vyao. Kielelezo cha mafanikio haya ni kumpokea Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake mwaka 2019. Kuaminika na jabali la siasa za Afrika Mashariki, Afrika na Dunia Maalim Seif Sharif Hamad (Mungu amlaze mahala pema) ni ishara ya ukomavu wa siasa za ACT Wazalendo.
Tumejenga jukwaa la kuaminika na vijana. Mara zote, kupitia chaguzi na teuzi zetu, tumetuma salamu kwa vijana wa Tanzania kuwa hiki ni Chama kinachowaamini na kuwapa nafasi vijana kuonesha vipaji vyao vya kiuongozi. Kuchaguliwa kwa Katibu Mkuu mwaka 2020 akiwa na miaka 34 ilikuwa ni alama ya wazi kwa vijana wote kuwa ACT Wazalendo ni jukwaa lao.
Tumejenga jukwaa la ukombozi wa wanawake. Tumevunja minyororo ya kukandamiza demokrasia kwa kuongoza kwa vitendo dhana ya usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia kwenye vyombo vyote vya maamuzi. ACT Wazalendo ndio chama pekee kilichoweka sharti la wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu wa kuchaguliwa kuwa 50/50! Haya ni mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya siasa. Kusimama kwangu mbele yenu kama kiongozi namba moja wa Chama ni ishara nyingine kuwa Chama hiki kinawaamini wanawake!
Tumejenga jukwaa la kuaminika la ukombozi wa Wazanzibari ili kujenga Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja na yenye mamlaka kamili. ACT Wazalendo inaenda kuwaongoza Wazanzibari kuikomboa nchi yao kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Kwa hakika, 2025 kwetu ni mwaka wa maamuzi!
Tumefanikiwa kujenga jukwaa la kupigania Taifa la wote kwa Maslahi ya wote hasa katika kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kuwakomboa wananchi
kiuchumi na kijamii. Tumesimama na makundi yote kwenye jamii; wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, vijana, wanawake, wazee n.k Hawa wote wanaitazama ACT Wazalendo kama sauti ya matumaini.
Tumejenga chombo madhubuti cha kupigania haki za binadamu ndani na nje ya mipaka ya nchi.
Tumeonesha kwa vitendo demokrasia ya ndani ya Chama. Uamuzi wa Chama kuzingatia ukomo wa madaraka wa miaka 10 kwenye Uchaguzi wa ndani ya Chama wa Mwaka 2024 ni mfano wa wazi uliowashinda wengi.
- Tumejenga Chama kinachoongozwa kwa uwazi na uwajibikaji.
Tumejenga Chama kinachokua kwa kasi zaidi nchini kwa vipimo vya kupokea wanachama, kutanuka kimtandao na ushawishi wake kisiasa ndani na nje ya mipaka ya nchi.
2025 NI MWAKA WETU, TUJIPANGE, TUSIMAME IMARA
Kama nilivyotangulia kusema kwenye salamu zangu, huu sio mwaka wa kawaida kwetu, ni mwaka wa kipekee. Ni mwaka ambao mbali na wajibu wetu wa kawaida wa kupambania malengo yetu kupitia uchaguzi, tuna wajibu mkubwa katika kutoa uongozi katika mapambano ya kuitetea na kuilinda demokrasia nchini.Ninaomba niwakumbushe azimio la Halmashauri Kuu kuwa kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, Chama chetu cha ACT Wazalendo KITAPAMBANA KIKISHIRIKI NA KITASHIRIKI KIKIPAMBANA!
Uamuzi wetu wa kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu haukuja kwa bahati nasibu. Ni zao la tafakuri na uchambuzi wa kina. Kama tulivyosema awali, sababu zetu ni tatu; Mosi, tumejiridhisha tunashiriki kulinda thamani ya kura. Pili, tunashiriki kwa sababu tumejiridhisha kuwa kususia uchaguzi kunaimarisha udikteta. ACT Wazalendo tukisusia, CCM itafurahia uamuzi huo. Tatu, CCM imeshindwa kuendesha nchi, ikae pembeni, tutaishinda.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, ACT Wazalendo ina majukumu makuu matatu ambayo kila mwanachama na kiongozi atapaswa kuyapigania kwa nguvu zote.
- Tusimame Imara Kupigania Malengo ya Chama
Kwa Zanzibar, huu ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar, mwaka wa maamuzi. Ni mwaka wa kukata kiu ya muda mrefu ya Wazanzibari ya kupata Zanzibar mpya, Zanzibar moja na yenye Mamlaka kamili.
Wazanzibari, kuliko kipindi chochote, bila kujali tofauti za kiitikadi, wameonesha kuuchoka utawala wa Rais Mwinyi kutokana na kukithiri kwa ufisadi na kuvunjwa kwa misingi ya utawala bora. 2025 ni mwaka wa kuwaunganisha Wazanzibari kwa ajili ya ukombozi wa Zanzibar.
Mwenyekiti wa Chama Ndugu Othman Masoud ameniomba niwafikishie ujumbe kuwa yeye yupo tayari kuongoza Wazanzibari bila hofu ili mwaka 2025 waipate Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja na yenye mamlaka kamili.
- Tupiganie Maboresho ya Mfumo wa Uchaguzi
Chama chetu kimetangaza kuwa kitapigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi hadi dakika ya mwisho. Tumeutangaza mwaka 2025 kuwa mwaka wa kuihami na kuitetea demokrasia.
Chaguzi tatu zilizopita zimetuonesha sura halisi ya adui yetu. Tumebaini kuwa adui yetu tunayepambana naye sio CCM bali vyombo vya dola. CCM imetangulizwa mbele lakini mipango haswa ya kuvuruga demokrasia na kuhujumu inapangwa na dola. Tunajua sio kazi nyepesi kupambana na adui yetu lakini tumejipanga na tupo tayari kumkabili.
Ujumbe wangu kwa wanachama na viongozi wa ACT Wazalendo ni kuwa zawadi ya kipekee tunayoweza kuwapatia Watanzania tukiadhimisha miaka 11 ni kuongoza mapambano ya kulinda thamani ya kura na kuihami demokrasia.
Tupaze sauti zetu hadi Uchaguzi Mkuu 2025 uwe huru, wa haki na wa kuaminika. Madai yetu sita yawe ndio wimbo wetu kuanzia saa hadi mwezi Oktoba. Tuieleze Serikali na wadau wote wa demokrasia kuwa sisi ACT Wazalendo;
Mosi, hatutaki wakurugenzi wa Halmashauri wasimamie uchaguzi; Pili, tunataka wajumbe wapya wa Tume ya Uchaguzi wateuliwe; Tatu, tunataka kura haramu zidhibitiwe;
Nne, tunataka wagombea wasienguliwe ovyo; Tano, tunataka mawakala wawe huru; na
Sita, tunataka vyombo vya dola visishiriki hujuma kwenye uchaguzi.
Kama walivyosema viongozi wa dini na wadau wengine wa demokrasia, madai haya yanawezekana hata sasa, yatekelezwe!
- Tuunganishe Taifa letu Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Watawala hawapaswi kuipuuza sauti hii. Sauti ya wanaolilia maboresho ya mfumo wa uchaguzi haipaswi kupuuzwa. Sauti ya wanaotaka vitendo vya utekaji na ukandamizwaji wa haki za binadamu viondoke haiwezi kupuuzwa!
Rai yetu kwa Rais Samia, asikilize sauti ya viongozi wa dini, asikilize kilio cha haki! Sauti hiyo, ikisikilizwa italiponya taifa letu kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025. Kinyume chake, sauti hiyo ikipuuzwa, italiweka rehani taifa letu.
ACT Wazalendo tunasimama na viongozi wa dini wanaopaza sauti kutaka maboresho ya mfumo wa uchaguzi na kutaka haki itawale ili amani ya kweli ipatikane!
HITIMISHO
Katika kuhitimisha, naomba niwaombe Watanzania waendelee kutuunga mkono. Tunawashukuru kwa kutuunga mkono kwenye safari yetu katika miaka 11 iliyopita. Ahadi yetu ni kuwa tutaendelea kulijenga jukwaa la ACT Wazalendo ili kuwakomboa Watanzania kwa kupigania ujenzi wa Taifa la Wote kwa Maslahi ya Wote na kwa upande wa Zanzibar, kuijenga Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Yenye Mamlaka kamili.Ahsanteni Sana!
ACT Wazalendo, Taifa kwanza, leo na kesho.
Dorothy Jonas Semu Kiongozi wa Chama ACT Wazalendo
05 Mei, 2025.
Dar Es Salaam.